Wajibu wa wafungandoa kila mmoja kwa mwingine

Kila Mwanandoa ana wajibu na haki sawa katika mambo yote yanayohusu ushirika katika maisha ya ndoa (MSK, k 1135). Ukubali ndoa unaotolewa na kila mfungandoa kwa hiari, humfanya kila mmoja awe na wajibu msingi wa ndoa kwa mwanandoa mwenza.

Hii inahusisha pia haki msingi katika uwanja huo kwa sababu wajibu na haki katika maisha yoyote yawayo yale, ni vitu pacha kwa kuwa haiwezekani pakawepo na wajibu bila haki na kinyume chake.

Haki na wajibu msingi katika ndoa huwa na msingi katika Agano Ndoa lenyewe ambalo ni aina pekee ya maisha kwa wanadamu.

Katika makala yake juu ya ndoa katika kijalida cha Jimbo Katoliki la Moshi (News Bulletin of the Diocese of Moshi-Kilimanjaro),Mwanasheria Kanuni, Padre Augustine Mringi, alijadili mambo muhimu katika ndoa kama yanavyoelezwa.

Licha ya kukosekana usawa katika maisha ya ndoa miongoni mwa baadhi ya jamii na tamaduni mbalimbali za wanadamu, ndoa ya Kikristu imekuwa ikisisitiza wafungandoa na wanandoa kuwajibika katika haki sawa kwa kila mmoja kwa mwingine.

Wafungandoa na wanandoa wanapaswa kupeana haki zilizo sawa na kuwajibikiana bila kupunjana.

"Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha, rudianeni tena ili shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu’ (1Kor.7:5).

Katika kupeana denindoa(debitum), wanandoa wote ni sawa na kila mmoja, ana haki na hata wajibu wa kudai mwanandoa mwenza bila unyanyasaji wowote wa kijinsia.

"Mume atimize wajibu wake kwa mke, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe. Mke hana mamlaka juu ya mwili, bali mmewe anayo. Hali kadhalika naye mume hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo" (1Kor. 7:3-4).

"Basi, mtu yeyote(yaani mwanandoa) asimkosee au kumpunja mwanandoa mwenzake kuhusu hili" (1Tes 4:4). Ama kweli denindoa ndilo linaloonesha upeo wa mapendo ya kindoa; na likikosekana bila sababu msingi na kweli, huleta zahama, mtafaruku na kasheshe zisizoisha.

Haki na wajibu msingi za wanandoa ni nyingi. Wanasheria kanuni na wazoefu wa kutoa hukumu mbalimbali katika mahakama za kikanisa, husema kwamba miongoni mwa haki na wajibu msingi za wafungandoa na wanandoa, ni pamoja na kuheshimiana na kusaidiana, kuishi pamoja kama mtu na mke (au na mume) na kuwa na mahusiano yanayochangia na kuchangamana.

Wajibu na Haki za wazazi kwa Watoto

Wazazi wanao wajibu mzito na haki msingi ya kufanya kila wanaloweza kuona kwamba wanawalea wao kimwili, kijamii, kiutamaduni, kimaadili na kidini (MSK, k 1136).

Maumbile ya chombo ndoa na mapendo ndoa yenyewe huelekezwa kwenye kuzaa watoto na kuwalea. Huu ndio upeo na umaarufu wa ndoa (GS, na 48).

"Mungu akawabariki na kuwaambia (Wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva), "Zaeni mwongezeke, mkajaze nchi na kuimiliki...’ (Mwa 1:28). "Ni kawaida ya wazazi kuwaweka watoto wao akiba (urithi), na si watoto kuwaekea wazazi wao" (2Kor 12:14).

"Ninyi akinababa msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo" (Efe 6:4). Nanyi wazazi msiwachukize watoto wenu la sivyo, watakata tamaa" (Kol 3:21).

"Mzazi ampendaye mwanae, atamrudi mara kwa mara ili amwonee fahari jinsi atakavyokua. Amfunzaye mwanawe nidhamu, baadaye atafaidika naye. Atajivunia mwanawe mbele ya wanaofahamiana naye" (Sira 30:1-2).

Watu wawili wanapooana, hujitwalia majukumu ya kuwalea watoto wowote wale watakaotokana na ndoa yao bila kubagua wala kukatiza.

Kwa kweli, wanandoa hawawezi kwa ridhaa yao wenyewe kujiengua na wajibu huu.

Wazazi wakiishi vema ndoa yao, itakuwa na malezi bora na ya kuwanufaisha mno watoto.

Malezi dini kwa watoto ni muhimu sana! Malezi haya huanza hasa watoto wanapobatizwa; na malezi haya huendelezwa na wazazi wanapowaongoza watoto wao na kuwataka waishi imani hiyo kwa matendo.

Licha ya malezi wanayopewa watoto kutoka watu mbalimbali na tofauti katika maisha, malezi ya wazazi ni msingi na muhimu sana na hivi hayawezi yakatolewa na wengine wawao wale isipokuwa itokee dharura ambayo haikusababishwa na yeyote miongoni mwa wazazi husika.

Kulingana na mkusanyo Sheria Kanuni 1983, kutokana na ubatizo wao, watoto wanayo haki ya kupata malezi ya kikristu ambayo kwayo watalelewa kiutu inavyopaswa, na wakati huohuo watawezeshwa kuishi vema Fumbo la Wokovu. (MSK, K 217).

Mkusanyo Sheria Kanuni huohuo unatoa miongozo mbalimbali kuhusu malezi ya watoto hasa yale ya Kikristu.

Wazazi wanao wajibu wa kuwalea watoto wao katika imani na kuwawezesha kuishi imani hiyo kimatendo (MSK, k 793), wanayo haki na wajibu wa kuwalea watoto wao na kuwachagulia kusoma katika shule au taasisi zinazofaa kwa elimu yao na malezi (MSK, k 797)

Wanao wajibu wa kuona kwamba watoto wao wanapewa Ubatizo majuma ya kwanza kabisa baada ya watoto hao kuzaliwa (MSK, k 867); wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wao wanapokea Sakramenti ya Kipaimara wakati unapowadia (MSK,k 890) na wanao wajibu wa kuona kwamba watoto wao wanatayarishwa inavyopasa ili waweze kupokea Komunyo ya Kwanza (MSK, k 914).

Wototo halali

Watoto waliotungwa mimba au wanaozaliwa kutokana na ndoa kweli au ndoa inayodhaniwa kuwa ndoa wakati yenyewe si ndoa, huitwa watoto halali (Fillii Legitimi); ama sivyo, watoto waliozaliwa nje ya ndoa huitwa watoto haramu (Fillii Illegitimi); MSK, K 1137).

Katika Sheria za Kanisa na Sheria za Kiserikali (yaani za Nchi), watoto halali huaminishwa kama watoto waliozaliwa kutokana na ndoa halali. Yafaa lakini ieleweke wazi kwamba msemo "mtoto halali" ni wa kisheria na hivi hauna uhusiano na masuala ya kimaadili au ya kiroho ya mtoto husika.

Watoto waliotungwa mimba au wanaozaliwa kutokana na ndoa kweli au na ndoa inayodhaniwa ni ndoa, huitwa watoto halali.

Ndoa inayodhaniwa kuwa ni ndoa lakini kikweli si ndoa (matrimonium putativum), ni ile inayodhaniwa kuwa ni kweli angalao na mmojawapo wa wanandoa wakati kikweli ndoa kama hiyo ni batili (yaani haipo) (MSK, k 1061, # 3).

Endapo ndoa hiyo inayodhaniwa kuwa ni kweli baadaye itatangazwa na mahakama ya kikanisa kuwa ni batili (invalid), basi watoto waliokuwa wametungwa mimba au waliokuwa wamezaliwa kutokana na ndoa hiyo, watachukuliwa kuwa ni halali.

Lakini endapo wanandoa wote wawili watakuwa wanajua kwa uhakika kwamba ndoa yao hiyo ni batili kutokana na kuwepo kizuizi batili ndoa au kutokuwepo utaratibu Kanuni na kadhalika, basi watoto watakaozaliwa na ndoa kama hiyo watachukuliwa kuwa ni haramu.

Baba mzazi ni yule ambaye anatokana na ndoa halali isipokuwa pawepo na mabishano yanayodhihirisha au yanathibitisha kikweli vingine.

Watoto huhisiwa kuwa ni halali endapo wamezaliwa angalao siku 180 baada ya ndoa kusheherekewa au katika siku 300 tokea siku ile uhusiano wa kindoa baina ya mume na mke ulipositishwa (MSK, k 1138).

Baba mzazi wa watoto waliozaliwa kutokana na ndoa kweli au ndoa inayodhaniwa kuwa ni ndoa, ni yule mtu ambaye anatajwa kuwa ni mume wa mama mzazi husika.

Hisia hii ya kisheria inatokana na Sheria za Waroma ambao baadaye ziliathiri sana sheria za nchi nyingi ukiwemo Mkusanyo Sheria Kanuni.

Hata hivyo hisia kama inaweza kufutwa pakiwepo na ushahidi mwingine mzito zaidi kuliko ule wa kwanza.

Inapaswa hata hivyo kuthibitisha kwamba kipindi chote ambacho mama alikuwa na uwezo wa kupata mimba, mama huyo hakuweza kupata mimba kwa sababu kipindi hicho uhusiano wa kimwili haukuwa unawezekana kwani hawa wawili walikuwa wametengana kimwili, au mwanaume alikuwa hanithi, au palikuwepo na sababu nyingine za kisheria ambazo ziliwazuia wasiweze kujamiiana.

Kukiri tu kwamba mama alikuwa amezini na hivi kukaibuka tuhuma kuwa mimba au mtoto aliyenaye mama mzazi huyo si ya baba mzazi husika bali ni mtu mwingine, hakutoshi kuhakikisha kuwa mtoto ni haramu.

Ukweli usio na utata ni lazima utolewe ili ushahidi uthibitishwe kuwa ni kweli.

Kuhalalika mtoto au watoto

Watoto haramu hufanywa kuwa halali kwa njia ya ndoa ya wazazi inayoshuhudiwa baadaye iwe kweli au inahisiwa kuwa ni kweli, au kwa njia ya barua, majibu (rescript) kutokana Jimbo Takatifu (MSK, k 1139).

Watoto wanaozaliwa kutokana na ndoa batili huwa watoto halali ndoa hiyo inapoponywa kwa njia za kawaida kwa mujibu wa sheria (sanatiio Simplex) (MSK, k 1156 -1160) au kwa njia ya kuponywa kutoka shinani (Sanatio in radice) (1161 - 1165).

Ni wazi kwamba kabla ndoa hiyo batili haijaponywa kwa mujibu wa sheria, ni lazima ihakikishwe kwamba kizuizi batilindoa kilichohusika kimetoweka au kimeruhusiwa.

Vilevile, watoto wanaozaliwa nje ya ndoa huhalaika ndoa ya wazazi wao inapohalalika. Kwa vyovyote ndoa inapoponywa au ndoa inayofuata inapodhaniwa kuwa ndoa na kwa hiyo batili, watoto waliotokana na ndoa za aina hiyo bado wataitwa watoto halali.

Watoto haramu huweza pia kuhalalika kwa njia ya baruamajibu kutoka Jimbo Takatifu kuhusu hili yafaa ieleweke wazi kwamba ijapokuwa barua huwafanya watoto haramu kuhalalika; hata hivyo, baruamajibu hiyo haiponyi ndoa batili ya wazazi husika.

Mambo yanabaki yaleyale mpaka ndoa hiyo itakapofanywa kweli au itakapodhaniwa kuwa ndoa kwa mujibu wa sheria (MSK, k 1061, #3;1156 -1165).Watoto wa kuokotwa na wale waliofanywa wana kwa mujibu wa sheria, huhisiwa kuwa ni watoto halali mpaka hapo itakapo hakikishwa vingine.

Kwa mujibu wa mkusanyo sheria Kanuni, watoto waliohalalika hulinganishwa au huwekwa kuwa sawa na watoto halali kuhusu haki na wajibu kama watoto isipokuwa, sheria iagize vingine wazazi (MSK, k 1140).

Sababu ni kwamba mfumo wa kuita watoto wengine HALALI na wengine HARAMU, una msingi wake katika uwanja wa kisheria tu na hakuna la ziada.

Hatima

Wafungandoa na wanandoa huingia ushirika wa maisha yote (MSK, k 1055) unaokataa katakata talaka (Mat 19:6) "Na ndiyo maana mwanaume humwacha baba na mama yake, akaambatana na mkewe na wao wawili huwa mwili mmoja (Mwa 2:24). ‘na kwa hiyo wao si wawili tena bali mwili mmoja, basi alichounganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe’ (Marko 10:8 -9).

Kifungo ndoa hiki miongoni mwa wahusika huwaletea wafungandoa na wandoa haki na wajibu zilizo sawa kila mmoja kwa mwingine na huwapasa kuwalea watoto wowote wawao wale watakaopewa na Mungu.

Na Mwisho, tumeona kwamba kisheria, watoto wanaozaliwa katika ndoa huitwa watoto halali na wale wanaozaliwa nje ya ndoa huitwa watoto haramu.

Na tena watoto haramu huweza kuhalalika na kuwa watoto halali na kuwa na haki na wajibu zilizo sawa na watoto hawa endapo ndoa batili za wazazi husika zitaponywa kwa mujibu wa sheria (MSK, 1156-1165).

Leo hii wazazi wengi katika jamii na tamaduni mbalimbali na tofauti za wanadamu wakiwemo watoto, wamechanganyikiwa sana kwa sababu ndoa nyingi haziheshimiwi na malezi hayazingatiwi inavyopasa.

Baadhi ya wazazi huenda wamesahau kwa hasara yao wenyewe mafundisho ya Mtume Paulo kuhusu ndoa: "Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu (kwani Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi" (Ebr. 13:4).

Wazazi wengine huenda wamesahau malezi kwa watoto bila kutambua athari mbalimbali za kosa na usahaulifu kama huo. ‘Anayemharibu mwanawe atakuwa na kazi ya kufunga vidonda, na kwa kila kilio moyo wake utashituka.

Mfunze mwanao nidhamu na kuwa mvumilivu ili usije ukaaibishwa na aibu yake’ (Sira 30:7,13). Watoto nao huenda kutokana na kutokutaka kupewa malezi na wazazi, huingia hasara kubwa na kupata laana zisizokuwa na sababu.

"Maana watoto wasiomheshimu mama yao ni balaa... (kwani mtoto) anayemtupa baba yake anamkufuru Mungu na anayemkasirisha mama yake analaaniwa na Bwana" (Sira 3:11,16).

Ni matumaini yetu kwamba baada ya wazazi na watoto kuyasoma kwa makini na kina makala haya na kuona umuhimu wa wazazi wa kuwalea watoto wao ni umuhimu wa watoto wa kupokea malezi kutoka kwa wazazi wapate kuleleka ipasavyo, ndoa na familia ambazo ni msingi wa jamii zote za watu zitazidi kupamba moto na hivi kufutilia mbali matatizo na mahangaiko mengi yaliyomo katika jamii na tamaduni mbalimbali za watu leo hii.

Kwa kuzingatia mafundisho ya makala haya na mengineyo muhimu tutaachana na kule kuwasikia wazazi hapa na pale wakilalamika na kupiga kite huku wakisema "watoto wa siku hizi wametushinda" nao watoto wakijibu, "Mkitaka matatizo yenu yaishe, basi nendeni na wakati.

Ni kweli kabisa kwamba kazi ya kulea au ya kupokea malezi yanayotolewa mara kwa mara ni ngumu. Lakini, licha ya ukweli wote huu kwa kila upande, hatuna la kuogopa kwa sababu Kristu Bwana aliwaambia mitume na wafuasi wake wa kale na hata wa leo.

"watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa" (Mat. 10:22)

 

 

Mjue Mwenyeheri Bakhita (2)

Baadaye Mimina na Bakhita wakapelekwa kwa muda kwenye nyumba ya masista wa Kanossa huko Venice kwa sababu mama wa familia alikwenda safari. Huko Bakhita alipokelewa kama Mkatukumeni ambapo alifundishwa imani ya Kristu. Naye anahadithia katika vitabu vyake;

"Masista wale walinifundisha kwa uvumilivu mkubwa kumfahamu na kumjua Mungu, ambaye tangu utoto wangu sikumjua bali nilimsikia moyoni. Nakumbuka jinsi nilivyoangalia jua, mwezi, nyota anga na viumbe vingine na kujiuliza ni nani anaweza kuwa bwana wa vitu hivi vyote vizuri! Mara nyingi nilikuwa na shauku ya kumuona na kumtolea heshima na shukrani" (Ms 26).

UAMZI WA MAISHA

Baada ya kugundua uzuri wa Mungu na mema mengi aliyomtendea Bakhita aliamua kubaki Italia, ingawa moyo wake uliumia sana kuachana na mama yule aliyemtendea mema, kwa lengo la kutaka kukua zaidi katika imani ya Kikristu vile vile alikuwa bado hajabatizwa.

Tarehe Januari 9 mwaka 1896, ni tarehe isiyosahaulika katika maisha ya Bakhita kwani ni tarehe aliyobatizwa ,aliyopata komunio ya kwanza na Kipaimara. Alipobatizwa alipewa jina jipya la Yosefina Fotunata.

Alibaki hapo kwa miaka minne, na baadaye akajisikia moyoni wito wa kumtolea Mungu maisha yake, yaani kuwa Mtawa. Lakini alisita, kwani kule utumwani hakukuwa na mtu mweusi kama yeye, lakini mama mkuu wa Masista wa Kanossa akampokea kwa mikono miwili, hivyo kwa furaha kubwa Bakhita alifunga nadhiri katika shirika la Mabinti wa Upendo wa Kanossa, baada ya kumaliza mafunzo.

SHAHIDI WA UPENDO

Maisha yote ya Bakhita yalikuwa ushahidi wa mapendo makuu ya Kristu mwokozi.

Unyenyekevu wake, tabasamuu lake daima na unyoofu wa moyo uliwavutia wote waliopata kukutana naye.

Hakika tabia yake njema haikubadilika kamwe licha ya mateso mengi aliyoyapata maishani.

Kwa wepesi wa moyo na wajibu wa hiari alifanya kazi kuanzia jikoni, sakristia, mapokezi na popote alipoambiwa kwenda. Daima watu waliistaajabu jinsi utendaji wake ulivyokuwa kwani alifanya yote kwa uangalifu na kwa upendo mkubwa.

Wakati alipokuwa jikoni masista wenzake wanakumbuka jinsi wakati wa baridi alivyodiriki hata kupasha moto vikombe na sahani ili vyakula viwafikie walaji vingali bado vya moto. Wagonjwa aliwahudumia kwa namna ya pekee.

Kwa upendo aliwaandalia chakula maalum kutokana na afya zao na jinsi alivyowafikishia milo yao, walielewa kwamba kila mgonjwa alikuwa ni kielelezo cha upendo wake wa huruma.

Kwa vile alipitia mateso alielewa barabara mateso ya wengine na alijitahidi sana kuwatuliza.

Wakati mwingine mama Yosephine Bakhita aliwekwa kuwa mngoja mlango.

Watoto wa shule walipomwona walipenda kumsalimu, na kutafuta kila kisingizio ili kuongea na sista huyu mwema. Naye aliwawekea mikono yake kichwani mwao na kuwabariki.

Kwa moyo mkunjufu na kwa ukarimu alikaribisha watu wote waliofika kwenye nyumba yao. Daima alikuwa na neno au ujumbe wa kutia moyo na kufariji kwa kila aliyemkaribia na wote wanakiri kwamba hicho kidogo alichowamegea kiliwatosheleza na kuondoka wakiwa wametulizwa.

Kwa busara aliyokuwa nayo aliweza kupokea jambo na kulipatia ufumbuzi mzuri.

Pole pole watu waliiona karama hii ya mama Yosefina na watu wengi hasa watu wa ndoa, wanawake na vijana wanafika kwake kupata ushauri, hata inapombidi kuonya au kukemea maovu hakusita kufanya hivyo, hasa alipogundua uchungu wa mioyo na uhasama katika maongezi ya watu.

Baada ya miaka mingi ya kumtumikia Mungu, afya ya Yosefina Bakhita ilianza kuzorota. Alisumbuliwa na maumivu kwenye viungo hasa wakati wa baridi kali na hata ikampasa kutembelea mkongojo na baadaye gari la magurudumu.

Mtumishi wa Mungu ambaye alikuwa ametumikia Kristu katika maisha ya kitawa zaidi ya miaka 50 kwa unyenyekevu, upole, furaha kubwa alifariki Januari 8 mwaka 1947, saa 2 usiku na kuzikwa Januari 11 mwaka 1947.

Uso wake kama kawaida ulionekana mtulivu hata watoto hawakuona woga kumwangalia. Watu wote wa mji wa ‘Schio’ walifurika kwa wingi kumuaga mama huyu waliyezoea kumwita ‘mama Mweusi’.

Mama Yosefina Bakhita aliacha sifa kubwa ya utakatifu wake, na sifa zake ziliendelea kuvuma siku hadi siku jambo ambalo lilimfanya Askofu wa Jimbo la Vicenza afanye utaratibu wa kuchunguza maisha yake baada ya uchaguzi ulichukua miaka mingi, Desemba Mosi mwaka 1978. Papa Yohane Paulo wa II aliamuru ichapwe hati juu ya ujasiri wa fadhili za mtumishi wa Mungu.

Juni 17 1992 alitangazwa mwenyeheri na mwaka huu wa Jubilei kuu atatangazwa Mtakatifu Oktoba Mosi mwaka huu wa 2000.

Riwaya

Roho ya Hausi gelo!

Na Josephs Sabinus

SIKU hiyo Joma nilisimama nikamtumbulia macho. Binti aliyekuwa wa kuvutia kwa sura, alikuwa ni mwenye uso ulojaa tabasamu na kicheko mdomoni.

Alikuwa amesimama katika kibanda kile akipunguza joto la Dar-Es-Salaam kwa soda aina ya Coca-Cola baridi.

Nilimtazama tena na tena huku nikirudisha nyuma kumbu kumbu ya akili yangu. Nikaamua kumtishia kicheko. Naye ni shujaa asiyeogopa kitu, Akanitishia pia. Wakati mimi nimerusha makombora matatu ya tabasamu, yeye tayari alikuwa amekwisha fikisha zaidi ya saba.

Siyo siri alikuwa akiniwahi kwa mengi hata nikaamini kuwa anauwezo wa kuhesabu mpaka "Z", wakati mimi sijahesabu hata "A" yenyewe.

Ndivyo tulivyo vijana tunaotoka vijijini tulivyo na papara ya kupenda. Joma nasema ndivyo tulivyo vijana wakuja, eti kila unayemuona umempenda tena siku hiyo hiyo, kweli!

Lakini ni kweli maana hata kule tulipo, tumezoea kuwaona wanawake wazalendo wenye rangi na ngozi ya asili, wenye kuchapa kazi kulijenga taifa, walioiva kimaadili ya kidini na kijamii na wanaokula kilichopo; kiwe cha gharama kubwa au hata cha thamani ya chini ili mradi, wanajua namna ya kuthamini chako.

Ndiyo, ni kweli. Tumezoea kuwaona namna anayeitwa mzuri na msafi ni yule asiye jua bei au hata aina moja ya kiungo cha mkorogo.

Kwanini mtoto wa Wajita nisichanganyikiwe kumuona Havijawa aliyekuwa katika mavazi yale yaliyoiruhusu sehemu kubwa mno ya mwili wake kuonekana ukiwamo uso uliokuwa na rangi nyororo mithili ya mtoto mchanga ingawa haikuwa na asili ya mvuto.

Hata hivyo anayependa, chongo hugeuza akaita kengeza, mimi sijui ni kwanini na wala usiniulize.

Hata hivyo, Joma nikaona huyu ni pekee anayestahili kudunda akimsindikiza kijana wa Wajita kuingia kijijini kwao kama "wife".

Sisemi wala kumtukana kuwa alikuwa "Maharage ya Mbeya", hapana si hivyo, hiyo ndiyo maana halisi ya penzi. Yaani nakupenda kwa dhati nawe unanipenda kwa dhati ili wote tuishi katika maadili ya kijamiii na hata ya ki-Mungu.

Nikaona kwa kuwa si mwingi wa maneno wala mbishi, Havijawa ana sababu gani kubwa ya kuacha kuitwa Mama-Joma?

Lazima awe kwa kuwa hata zile mila za kuoana kwa kujali ukabila na rangi zimekwisha pitwa na wakati. Bora tu, mmependana na mko tayari kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

Basi, tumekaa siku kadhaa kama marafiki waliozoeana na huku wakilenga kabisa kufunga pingu za maisha. Tayari Joma nilishapeleka nyumbani taarifa zote muhimu juu ya mtarajiwa wangu ili akapewe mkono wa heri na wazazi wangu baadaye, twende kwao nami nikainamishe kichwa kwa aibu ya kudeka ukweni huku nikiwa mgeni wa heshima nyumbani kwao.

Lakini, yote haya baadaye yahitimishwe na baraka za Mwenyezi Mungu pale kanisani.

Tumejadili kwa pamoja na kukubaliana. Tuanze kwa mume. Si huko ndiko kwao mume? Sasa kwanini tuanzie upande mwingine?

Kadri siku zilivyozidi kukaribia kwa ajili ya safari ya kwenda majita huko Musoma, ndivyo badala ya kuongezeka furaha moyoni, mapigo ya moyo wangu yalizidi kunienda mbio kwa hofu.

Kila nilipopiga hesabu zangu, zilikataa. Hakuna hata moja iliyonipa jibu sahihi kuwa ni tamuingiza wapi Havijawa.

Ninasema hivyo kwa kuwa Havijawa msichana wa kabila la Wachaga ambaye tangu siku ya mwanzo kuonekana katika mboni za macho yangu, niliamini ni mtu wa familia na ukoo bora. Familia ambayo niliamini ni yenye kila aina ya maisha ya starehe na ufahari ingawa simaanishi kwamba kwao ndio funga kazi. Kumbe ni kweli wanaposema ushukumu kitabu kwa muonekano wake wa nje.

Ninasema hivyo kwa kuwa hata mavazi anayovaa, rangi ya ngozi yake, inaonesha ni maelfu ya fedha yanayotumika kuikarabati hata aonekana kama robo tatu ya Mzungu.

Nilijua ni msichana wa gharama kubwa tena ambaye kila mtoto katika familia yao, anachumba cha pekee chenye huduma muhimu zote ndani. Hakuna cha kutokatoka eti kwenda chooni wala bafuni, kila kitu ni huko huko ndani kwa ndani.

Iweje sasa ninampeleka Havijawa kule nyumbani kwetu kijijini ambako unapokuwa ndani, mnaweza kusalimia na yule aliyeko nje kutokana na ubovu na matundu ya nyumba yenyewe tunayojidanganya kuiita nyumba?

Ni vipi nimpeleke kule ambako hata mlango tunaotumia ni ule ambao umeegeshwa kwa msaada wa ile miti ya michongoma iliyokwisha liwa na mchwa, inayozibwa na maboksi? Milango ambayo hata teke la kuku aliyechoka baada ya kufukuzwa na kunusurika toka mikononi mwa kicheche mwenye njaa, linaweza kuubomoa?

Ni vipi nimpeleke katika nyumba ambayo hata choo chake, ni kile kilichofunikwa kwa magunia machakavu na makaratasi ya nailoni? Ambacho nacho ili ujisaidie, inabidi uwaambie walioko jirani watoke au basi uwaombe radhi wasigeuke maana haitapendeza.

Ninampeleka Havijawa katika familia ambayo tofauti na ninavyomuona ni mtoto wa familia inayotumia mboga nane, pale ni ambapo hata uji wa muhogo usio na sukari wala chachu ya limau? Wala pilipili mtama haipatikani mpaka siku maalumu pengine kama kuna Pasaka, Krismasi au Ubatizo.

Joma mtoto wa Wajita, nikazidi kuchanganyikiwa na kuamua kuchagua usafi wa andazi kujikirimu juu ya mafuta huku linaungua. Nikajikaanga kwa mafuta yangu mwenyewe kama sangara wa ziwa Victoria. Nikaona heri niuze kila kidogo nilichonacho, ili aone kuwa nina maisha mazuri hapa nilipo, je kule kwetu kwenyewe, masikini mpiga ngumi ukuta...

Na mimi nikaanza kujitambia namna kwetu sasa palivyo na ufahari wa kinadharia na kumbe sio kimatendo.

Kwanza sioni ubaya kwanini nisimwambie kuwa kwetu kuna magari matatu ya kifahari likiwamo lile PRADO la bluu na yale mengine mawili.

Hayawi hayawi, yamekuwa. Sasa ni siku ya siku. Siwezi kufanya ninalotaka kufanya. Haitapendeza kwa kuwa lazima hata mwenyewe Havijawa apaone na kupajua nyumbani. Asalimiane na ndugu zangu na hata kushikana mikono. Wamjue kwa sura na hata yeye awatambue walau kwa sauti.

Tuko njiani kuelekea Musoma sasa. Lakini njia nzuri na iliyo salama na ya mkato, mara nyingi watu hupendelea kupita nchi jirani ya Kenya.

Tuko njiani. Tumevuka mji unaoitwa Kisii. Tumekuja mpaka Migori nchini Kenya na basi la TAKRIM lililkuwa linaendelea kutambaa juu ya barabara ile ya lami.

Nikaona hapa, nimelikoroga, lazima nilinywe mwenyewe. Ninaanza kujuta ni kwanini nilikuwa ninajikaanga kwa mafuta yangu mwenyewe maana hatima ya uongo wangu sasa, inakuja kubainika maana yale yote niliyojisifia kwa Havijawa, sasa yanakwenda kuonekana kinyume maana hata nyumba yetu yenyewe ni ile inayomithilishwa na mbavu za mbwa yule wa kijiji kilichokumbwa na baa la njaa. Hii ni kweli na wala siungi chumvi kwa kuwa hiyo ni kazi ya wapishi kule jikoni.

Hapo nyumbani hata uwayo mmoja wa kuku wa jirani, haupatikani kwa kuwa hata wao kuku wenyewe wanajua hakuna watakachoambulia maana hata panya wamekwisha hama kwa kukosa chochote cha kuhemea sasa kuku wakija watapata nini cha kudonoa.

Waje kutafuta nini wakati pale haidondoki chembe hata moja walau ya ulezi? Itoke wapi katika familia yenye taabu namna ile?

Basi, nikaamua tu, ngoja tuteremke pale Migori kwa mjomba ili hata nipate kuwajulia hali.

Si hilo tu, maana sasa ipo haja kubwa ya kuenda pale ili wakati mkewe mjomba anaendelea na mapishi wakisaidiana na mke wangu mtarajiwa, Havijawa huku wakiongea mambo yao ya kike, sisi tubaki na mjomba huku sebuleni.

Nitumie nafasi hiyo kumueleza mjomba ukweli mambo na kumuomba ufunguo wa ile nyumba yake mpya anayoijenga pale Mkendo maana Mkendo, ni katikati ya mji ule wa Musoma.

Ingawa roho inaniuma kwa kuikana familia yetu, ingawa pia nijajua kuwa cha kuazima hakisitiri matako, inabidi nifanye hivyo maana vinginevyo, Havijawa akianza kuniulizia vile nilivyotambia kuwa navyo nyumbani kwetu na hata nyumba yetu akiiona, sijui.

Lakini, nifanye nini wakati nimelikoroga mwenyewe na sina budi kulinywa.

Tumeteremka pale kituoni Migori, tumevuta hatua kuelekea ilipo familia ya mjomba.

Havijawa hajui lolote yeye ni mgeni, yake ni macho na namna ya kuyatumia.

Tunafika kwa mjomba, ni saa za kazi ambazo zinaelekea kuisha ili hata wakubwa wa familia, warejee toka makazini na ndio maana muda huo, tulipokelewa na watoto wadogo.

Sikuwa ninafahamu ni kwanini ghafla baada ya kuingia tu pale sebuleni tulipokuwa tumeketi na Havijawa, Nafsa, binti mkubwa wa mjomba, alipoingia ndani na kutukuta tu, uso wake ulibadilika ghafla na hata Havijawa mwenyewe hakuwa na hali niliyoitarajia inayoashiria kuwa pale alikuwa ni "kuku" mgeni ambaye asingekosa kuwa na "kamba mguuni."

Alionekana kuhaha na kuchanganyikiwa. Macho yake yalibadilika rangi na kumtoka kwa hofu. Kilikuwa ni kitendawili kwangu. Hata hivyo, sikuhofu chochote maana Havijawa ni mgeni katika nchi hiyo jirani sasa hofu ya nini tena kwa mtoto mdogo huyo wakati hata "pass port" anayo.

Mara masikio yetu yaliyokuwa yametekwa na sauti ya redio ya nchi hiyo (KBC), yakaporwa na kuwa katika mawimbi ya sauti iliyosababisha mlango ule kufunguka kwa utaratibu. Tulipoelekeza macho yetu, yaligongana na yale ya Uncle Martini akiwa ametangulizana na mkewe wakitoka kazini kwao.

Tulikumbatiana nao huku Havijawa akiwa ameketi pale kitini kwake jirani na kona ya chumba kile. Akitweta kwelikweli huku kijasho cha mbali kikionekana usoni kwake licha ya baridi ya Kenya.

Kisha walielekea kuweka mafaili yao mezani ili tuendelee na mazungumzo ya awali.

"Aaah! Mai ni wewe!" Mke wa mjomba akamaka akifupisha jina la Maimuna. Nikashangaa kimya kimya. Kwanini nisishangae kimya kimya wakati katika siku zangu zote za kumjua Havijawa hakuna siku aliyoniambia wala kumjua kuwa kama anaitwa Maimuna?

Akakaa kimya tu, asijibu lolote wala kusalimia. Nikamuangalia macho yanayoashiria kumtaka atoe salamu kwa wenyeji hao ambao ni watu muhimu ili baadaye nifanye kazi ya utambulisho.

Kimya cha dakika tatu hivi kikatawala huku mimi nikijisikia aibu kwa kuwa ninashangaa mke wangu hasalimii wakwe!

"Hivi lile tangazo uliliona? " "Lipi mjomba?" "Hivi kwani imekuwaje, huyu umempataje?" Sikujua asili ya swali lile ila mimi nilizidi kuchangamka ili kufuta aibu ambazo zilikuwa zinanikabiri.

Nikasema, "Huyu ni mke wangu mtarajiwa hivi sasa ninampeleka akapaone nyumbani." "Unasema kweli Joma?" Mkewe mjomba akadakiza nami nikajibu kuwa ni kweli ndivyo ilivyo.

Safari hii nilijibu kishujaa huku nikijiamini nikidhani kuwa labda ana mwelekeo wa kunipongeza kwa chaguo langu la mwanamke mzuri.

"Ama kweli milima haikutani isipokuwa ni binadamu ndio wanaokutana."

"Ni kweli," nikasema kumuunga mkono mke wa mjomba. Mwanangu ngoja nikuambie," "Eehe!" nikamuitikia nae akaanza kuelezea kwa huzuni ambayo kadri muda ulivyozidi kusogea, ndivyo alivyozidi kupandisha hasira na kutoa sauti kali ya kufokayenye lundo la jazba.

Hata mimi nikajikuta kwanini nimekwenda pale. Kukimbia nilishindwa na hata kunyamazisha nilishindwa. Nikabaki nimetumbua macho kwa kuwa hata kitendo cha kupita pale nyumbani, ulikuwa ni umbea ambao ni sawa na kulikoroga tope na hivyo sina budi kulinywa.

"Joma. Mwanangu nakulaumu lakini ninakushukuru kwa kuwa umeniletea "mwana mpotevu". Aliye nifanya hadi hapa nilipo sina mtoto wa kiume.

Ngoja nikuambie. Mtoto huyu Maimuna alikuwa mfanyakazi wangu wa ndani wakati tunafanya kazi kule Tanzania , kule Arusha.

Siku moja tumekwenda kazini. Mungu wangu! Sijui Mai; hivi Maimuna kweli nilikukosea nini mpaka ukanifanyia hivyo Mai?. Kweli maimuna ukamchukua mtoto wangu mchanga na kumfanyia vile? Kwanini hukunifanyia mimia au baba yake kuliko..." mama huyo akasema huku akimtazama Mamuna (havijawa ) kwa macho ya kumsuta.

Yeye Maimuna, alikuwa amefunika uso kwa viganja vya mikono yake.

Mama akaendelea, "Nilivyokuwa ninakupenda kama mwanangu wa kuzaa ukanifanya siku hiyo ninatoka kazini tu kufika mtaa wa pili tu, nikasikia harufu ya mifupa na nyama ya kuchoma ikiungua, kumbe Maimuna ulikuwa..."

Mama yule akatoa machozi na baada ya muda akapenga kamasi na kujifutia kwenye upande wa kanga.

Akaendelea, "Na hiyo haikuwa mara ya kwanza. Siku nyingine ingawa alikataa, lakini watoto wa jirani wakaja wanakimbia, wanasema eti mfanyakazi wenu (Maimuna), amepenga kamasi na kukojoa kwenye maji.

Akayaleta tulipombana mbele ya watoto wale, akakiri na kuomba radhi. Tukamsamehe, yakaisha kabisa bila kinyongo."

"Siku nyingine, ilikuwa imepita miezi kama minane hivi, maskini sisi na mjomba wako tunajua tunaishi na mwenzetu ambaye kwa sasa ni kama au zaidi ya mzazi wetu kwa kuwa ndiye anayejua tutakula nini, tutakunywa nini na wala hakuna jambo litakalotoka jikoni asilolifahamu.

Sasa kwanini tusimuone kama mzazi wetu wa pili?

Jamani dunia hii! Siku hiyo ameandaa chakula sawa sawa. Akaja kutuita. Tulikuwa chumbani. Mungu ni mkubwa na alilopanga, haliharibiki kwani kazi yake haina makosa.

Na hata basi hata kama ingekuwa nayo, hairekebishwi na binadamu yeyote.

Ninasema hivyo kwa kuwa hatujui ilikuwaje hata ile tunanawa mikono baada ya kusali, huyu binti huyuhuyu mwenyewe, akarudi nyuma na kugonga meza.

Mboga ikamwagika pale sakafuni.

Ghafla, tunashangaa mchuzi unakuwa wa kijani kabisa. Tukashangaa hata kushindwa kujua ni vipi leo mchuzi huo uwe hivyo. Hisia zetu zikaenda mbali na hata aliye uona hakuwa na imani na matokeo hayo.

Tukasema hiki nini, lazima tupime hiyo hali. Tukaenda kwa wakemia. Maimuma huyu unayemuona, kumbe alikuwa ametuwekea sumu. Tufe wote eti. Familia nzima. Kweli Maimuna!?" akalia tena kwa kwikwi.

"Haya sasa acha hayo, siku hiyo mpaka tunaingia ndani toka kazini, tunasikia nyumba na eneo zima limetawaliwa na harufu hiyo ya mifupa inayoungua au hata nyama ya kuchoma. Tukaingia na kuzidi kuangaza angaza ndani huku Maimuma huyu haonekani wala mtoto wangu marehemu Derick, haonekani.

Mungu wangu! Niliposogea kwenye oveni, ninamkuta kweli mwanangu.... Maimuna kweli ukamuua mwanangu Derick kwa kifo cha kinyama namna hiyo? Ukambanika mwanangu kwenye moto wa oven kama samaki?" akaangua kilio na alipopunguza sauti huku akinyanyuka na hatujui alitaka kufanya nini, Maimuma(Havijawa) akadakiza,

"Kweli nimefanya kosa kwa kuongozwa na shetani, na kwanza naomba Mungu anisamehe na hata wanadamu wenzangu nisameheni.

Nilifanya hivyo kutokana na uchungu. Kweli mama wakati ule ulikuwa unanitesa sana, tena mno. Labda kwa kuwa ulijua umenitoa katika familia masikini. Hata mshahara ule wa shilingi 700/= kwa mwezi, uliokuwa unanifanyia makato mpaka najikuta ninafanya kazi huku ninadaiwa kazi ya miezi sita mbele.

Mama ingawa adhabu yangu haikuwa ya busara, ilitokana na hasira na hata mimi mwenyewe ninaijutia sana na naomba radhi na pia liwe fundisho kwa wengine wasiwe na hausigelo wakamgeuza kama mnyama hata hivyo ninamlaumu Joma kwa kuwa amenileta katika ‘mdomo wa mamba’ bila kujua."

"Havijawa kumbe hayo ni ya kweli, hivi na nyie maisha yenu ni kama yetu mpaka ukawa hausigelo, mbona mimi ulikuwa unaniendesha na kunipa kazi ngumu ya kukulea kifahari na wala hukuwahi kuniambia hilo?

Kumbe nilikuwa ninaoa muuaji? Aliyemuua mtoto wa mjomba kifo cha kikatili namna hiyo! Hivi huko ninakokupeleka , ndugu zangu watabaki?! Umelikoroga na wewe utalinywa mwenyewe na tangu leo..."

Nikakatizwa na ujio wa askari wale watatu walioingia ndani huku wameongozwa na mjomba.

Askari wale walipoingia machoni pa Havijawa, naye akazimia kama mama yule ambaye alitangulia kupoteza fahamu pale sakafuni baada ya kumsemea maneno hayo mbaya wake. Ama kweli Joma nikajisemea kimoyomoyo, "ROHO YA HAUSIGELO!"

 

MWISHO