Uchaguzi mkuu ujao

Utulivu,amani vitawale kumuenzi Mwalimu Nyerere

lWapiga kura tumieni busara zenu kuchagua viongozi bora

lUsipande mchungwa ukatarajia kuvuna ndizi,malimau

Na Ibrahim M. Kaduma

Kumuenzi Mwalimu J.K. Nyerere vita dhidi ya Ujinga, Umaskini, Maradhi na Dhuluma

Utangulizi:

KATIKA uchaguzi wa Oktoba mwaka huu,utakuwa ni uchaguzi wa kwanza ambao tutaufanya bila kuwa na Baba wa Taifa ambaye tulikuwa naye tangu wakati wa Uhuru na katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi uliofanyika miaka mia tano iliyopita.

Vile vile ikumbukwe kuwa wakati wa uchaguzi wa mwaka huu, tutakuwa katika kumbukumbu ya Baba yetu huyo kutimiza mwaka mmoja tangu achukuliwe na Mwenyezi Mungu hapo Oktoba 14 mwaka jana.

Hivyo sitakuwa nimekosea nikisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa pekee na wakihistoria.

Kwa bahati mbaya sana, ingawa historia inaweza ikajirudia kwa maana kwamba fundisho la kihistoria linaweza likaja tokea tena, lakini tukio la kihistoria halijirudii katika nchi ile mara mbili. Watanzania hatutampata mwasisi mwingine wa Taifa letu ambaye ataacha kumbukumbu kama aliyoiacha Mwalimu Nyerere.

Ndiyo maana tunawajibika kuukumbuka mwaka huu kipekee na hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa viongozi wanaotakiwa kuliongoza Taifa letu kwa miaka mitano ijayo ambapo hatutakuwa tena na mshauri wetu mkuu aliyekuwa amejaa hekima na ambaye kila siku mtu ulipenda ukae na umsikilize akitoa wosia wake.

Hivyo kwa heshima yake Mwalimu na kwa sababu miongoni mwetu bado tunao watu wengi waliofanya kazi naye na kunufaika na mafundisho yake ,itakuwa vema kama tutajikumbusha misingi aliyoisimamia Mwalimu Nyerere ili iwe kielelezo kwa wapiga kura kujua ni viongozi wa namna gani tunaowahitaji ili nchi yetu iendeleze heshima aliyotujengea Mwalimu.

Mimi ni miongoni mwa watu hao; na ninamshukuru Mungu sana kwa kuniwezesha kupata nafasi hii ya kuandika mawazo haya ili kuchokoza na kuchangia katika shughuli nzima ya kuteua wagombea na katika kuwapima hulka zao na kuwapigia kura. Ni matumaini yangu kwamba vyama vyetu vyote na wananchi kwa ujumla, watanufaika na mchango huu ambao lengo lake ni kudumisha Umoja, Amani na Haki katika nchi yetu.

Tukumbuke sana hekima za Mungu wetu ambaye ametuonyesha kwamba ukipanda mchungwa utavuna machungwa. Kama haja yako ni malimao au mapera au ndizi basi usitegemee kuvuna mazao hayo unayoyahitaji kwa kupanda mchungwa. Itabidi utafute miche ya malimao au mapera au migomba.

Halikadhalika katika uchaguzi huu.,vyama vikiwaruhusu watu walioshinda kura za maoni kwa kutoa rushwa kuwa wagombea kwa kisingizio cha kwamba ndio wanaopendwa na wananchi na hivyo, ili Chama kishinde sharti kiwatue watu hao, tujue tunapenda rushwa na hivyo tunamsaliti Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuteua watoa rushwa ati kwa sababu tunataka kushinda uchaguzi!.

Na zaidi tukumbuke kuwa kufanya hivyo tutakuwa chukizo kwa Mungu ambaye katika kitabu cha Mithali (17:23). amenena kwamba "Asiye na haki hutoa rushwa kifuani ili kuzipotosha njia za hukumu"

Haya ni maneno ya Mungu wala siyo ya mwanadamu. Wote tunajua kwamba Mungu wetu ni mwenye hukumu za haki naye atajua hata tunayoyawaza mioyoni mwetu. Mtu anayetoa rushwa ni dhahiri si mtu anayeitakia mema Tanzania na watu wake bali ni mtu anayejali nafsi yake tu kwa hiyo lengo lake ni kupotosha haki; na hivyo ‘MTU ANAYENUNUA KURA YAKO ATAUZA HAKI YAKO’.

Akizungumzia madhara ya rushwa, Mwenyezi Mungu katika kitabu cha Taurati amenena"Kwa maana Bwana, Mungu wenu yeye ndiye Mungu wa miungu, na bwana wa mabwana, Mungu Mkuu mwenye kuogofya asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. Usipotoa maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa upofusha macho ya wenye akili, na kugeuza dawa ya wenye haki. Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana Mungu wako". (Kumb: 10:17; na 16: 19 -20).

Majumuisho ya wosia huu wa Mungu wetu ni kwamba:-

(a) Wanaotoa rushwa wanapotosha haki. Watoa rushwa ili wapatiwe heshima wasiostahili.

(b) Wanaotoa na kupokea rushwa hawamwogopi Mungu. Tukitambua kwamba shetani ni malaika wa Mungu ambaye aliasi, basi wanaotoa na kupokea rushwa watambue kwamba kwa kutomwogopa Mungu wanaasi mafundisho yake na hivyo wanaungana na shetani.

(c) Kwa vile Mungu ‘hakubali rushwa’ ni dhairi kwamba wanaotoa na kupokea rushwa wanapigana na utashi wa Mungu.

(d) Mungu pia amesema ‘ usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza dawa ya wenye haki’. Kwa kukubali kupokea rushwa, wapiga kura wanajinyima haki. Mwalimu Nyerere alitufundisha Watanzania tangu mwaka 1962 alipoandika kwamba Rushwa ni adui wa haki.

Alitaka kila mwanachama wa TANU na hatimaye CCM aape kwamba hatatoa wala kupokea rushwa’.

Mafundisho ya Mwalimu Nyerere

Katika uhai wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitufundisha mengi ya hekima itokayo kwa Mungu na ambayo yalijenga amani ambayo tunaisheherekea leo. Kwanza kabisa inafaa tujikumbushe zile ahadi kumi za TANU ambazo aliziandika katika kipindi cha karibu mwaka mmoja aliokaa nje ya serikali baada ya kujiuzulu kama Waziri Mkuu wa Tanganyika huru tarehe 22/1/62.

Miongoni mwa ahadi hizo ni ahadi muhimu zifuatazo:

1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.

2. Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote.

3. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa Umaskini, Ujinga; Magonjwa na dhuluma.

4. Rusha ni adui wa haki. Sitatoa wala kupokea rushwa.

5. Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

6. Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

7. Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.

8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

Ahadi hizi nane ambazo hakika zinastahili kuwa ni ahadi za Taifa zima badala ya kuwa ni ahadi za wana CCM peke yao; ndizo hasa chimbuko la umoja wa watanzania na amani na utulivu tunavyojivunia leo. Ahadi ya kwanza inatufundisha kuchukia ubaguzi wa aina yoyote uwe ni wa kabila dini rangi jinsia au taifa. Ahadi hii ndiyo ulikuwa msingi wa siasa yetu ya kupinga ubaguzi wa rangi kutetea umoja wa Afrika; siasa ya kutofungamana na upande wowote na kuunga mkono dhanaya umoja wa mataifa. Tulifundishwa kuwaenzi wanadamu kama binadamu wenzetu na hivyo kuimarisha uhusiano mwema baina ya mataifa.

Ahadi ya pili ilitufundisha kujali zaidi utaifa wetu kuliko nafsi zetu. Kwa hiyo hata tunapopanga safu za kazi tunawapanga watu kufuatana na uwezo wao wa kulitumikia taifa letu kwa faida ya sisi wote bila kujali mtu anakotoka, dini yake, rangi yake wala maumbile yake ndiyo maana Mwalimu Nyerere kila wakati aliwadharau sana watu wanaotukuza ukabila; udini; rangi za watu; nakadhalika akiwaita ni watu waliofilisika kisiasa. Tofauti za jinsi hii hazitofautiani sana na rushwa. Kwa hiyo, ukabila, udini; rangi ya mtu na tofauti za kijinsia - vyote ni adui wa haki kama iliyo rushwa. Chama chochote na wananchi kwa ujumla wakigundua uwepo wa upendeleo wa jinsia hii sharti wakatae kwani ni tofauti zinapotosha haki kama rushwa ilivyo.

Ahadi ya tatu ndicho kipimo cha ukamilifu wa utu wa mtu. Umaskini na ujinga ndiyo hasa chimbuko la rushwa kwa ujinga wao wananchi wanafikiri wananufaika kwa kupokea rushwa; hawatambui kwamba kwa kukubali kugeuzwa mawazo yao kwa rushwa wanauza uhuru wao wa kuwahukumu wagombea kwa matendo yao. Hatima yake, ni kuuza uhuru wao na hivyo kuendeleza dhuluma.

Fedha kidogo wanayoipokea katika rushwa wala haiondoi umaskini wao. Rushwa wala haiondoi umaskini wao. Rushwa hiyo inawaongeza ufukara na hivyo kuwaletea maradhi pia; kwani chanzo cha maradhi mengi katika nchi zetu ni umaskini. Mwalimu Nyerere aliona hatari za hawa adui wanne - yaani Ujinga, Umaskini, Maradhi na Dhuluma - tangu mapema na akatuandaa kuyaepuka. Ndiyo maana tangu tumeacha misingi ya Azimio la Arusha, umaskini wetu unakua haraka sana na dhuluma zinazidi kushamiri.

Ahadi ya nne hadi ya nane zinasisitiza tu umuhimu wa ahadi tatu za kwanza. Rushwa ndio dhuluma yenye; wakati uongo ndio chimbuko lenyewe la dhuluma. Mtu anapotoa rushwa anataka apatiwe haki na njia ya udanganyifu. Kwa upande mwingine, ahadi ya sita ambayo inasisitiza umuhimu wa Elimu, ndio ufunguo wa kufuta ujinga ambao kama tulivyoona hapo juu ndicho chanzo cha upokeaji rushwa. Ahadi ya tano na ya Saba zinasisitiza ushirikiano wa wananchi wote kwa faida ya taifa zima badala ya kuweka mbele faida za binafsi. Aidha,Ahadi ya nane ndio msingi wa dhana ya ‘Ukweli na Uwazi’ ambayo anaisimamia Rais Mkapa.

Hitimisho

Kutokana na maainisho hayo hapo juu tungependa kumalizia makala haya na ushauri ufuatao:-

a). Kwa mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi kutumia rushwa kuwashawishi watu wampigie kura ni ishara ya wazi kwamba mtu huyo hafai kukabidhiwa madaraka ya kuliongoza taifa letu. Mtu wa namna hiyo ama ni mpumbavu au ni mtu mwenye tamaa ya mali na asiyethamini utu wa watu wengine.

Mtu wajinsi hiyo ni rahisi kununuliwa. Hivyo atauza uhuru wa nchi yetu na haki zetu. Ole wao wanaodiriki kumchagua mtu wa aina hiyo!.

b) Kutoa na kupokea rushwa na halafu kutii matakwa ya mtoa rushwa ni dhambi na chukizo kwa Mungu kwa sababu ni kitendo cha dhuluma. Ole wao wanaoshiriki katika matendo ya jinsi hii kwa maana katika kitabu cha Zaburi Mungu asema hivi:

"BWANA huwahifadhi wote wampendao na wote waso haki atawaangamiza" (Zab: 145:20)

Mungu hasemi ni lini atakapowaangamiza. Lakini uangamivu ni wa hakika kwani Mungu hasemi uongo. Ukitaka usidhulumiwe na wewe usidhulumu. Vinginevyo utavuna ulichopanda. Watu wanaodhulumu haki za wengine wawe na hakika kwamba watahukumiwa. Hii ni pamoja na kushindwa uchaguzi baada ya kupoteza mali nyingi.

c) Katika kutufundisha uwelevu katika kuamua au kupima mambo, Mungu katika Injili ya Mathayo Mtakatifu anatuasa hivi:

"Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali:Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba au tini katika mibaruti?. Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya." (Mt:7:15-17).

Ni dhahiri kwamba wanaotoa rushwa wanatenda dhambi na ni watu waovu. Hivyo haiwezekani tutegemee matunda mazuri au mema kutoka kwao. Aidha na sisi tukipokea rushwa, tutakuwa tunatenda dhambi pia kwa kuushangilia uovu. Tujiepushe na balaa hii.

d) Ili kuhakikisha kwamba tunashindana katika uchaguzi huu ambao watatuondolea balaa ya rushwa, tusikubali vyama vyetu kupitisha majina ya watu ambao ama wamebainika au wanatuhumiwa kuwa wametumia rushwa kununua kura za watu. Tutabarikiwa sana kama tutatoa hukumu za haki kuwakataa watoa rushwa na kuwateua wanyonge kugombea katika uchaguzi huu. Mungu ametuahidi kwamba tukitenda haki ya Mungu kwa maana kwamba tunafanya lile tunaloamini na hakika ya mioyo yetu, yeye anatusikiliza na kutimiza haja zetu. Kwa sababu Mungu anaahidi hivi:-

"Bwana ni mwenye haki katika njia zote, na Mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.

Bwana yu karibu na wote wamwitao,wote wamwitao kwa uaminifu. Atawafanyia wamchao matakwa yao,naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.

Bwana huwahifadhi wote wampendao, na wote wasiohaki atawaangamiza. (Zab: 145:17-20).

Watu wa Mungu tuziamini ahadi hizi za Mungu kwa sababu ni ahadi za kweli.

Mungu anachotaka ni sisi kuwa wakamilifu na kutenda haki; kusema kweli kwa mioyo yetu; kutokana na fedha ili tupate faida tusizostahili na kutochukua rushwa na kuwaangamiza wasio na hatia.

Mungu ana ahidi kwamba ‘mtu atendaye mambo hayo, hataondoshwa milele" (Zab:15:5(b))

Ni matumaini yangu kwamba vyama vyetu vya siasa vitazingatia ushauri huu;na tukifanya hivyo tutakuwa tunamtii Mungu na kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alizitii kwa ukamilifu ahadi ambazo yeye ndiye aliyeziasisi.

Aidha ahadi hizi ni hekima itokanayo kwa Mungu. Mungu awabariki wagombea wote wanaoenenda kwa haki washinde uchaguzi huu. Mungu aibariki Tanzania ili iendelee kudumisha amani

Tukumbuke kwamba umaarufu hauji kwa rushwa bali umaarufu unaletwa na matendo mema yakukumbukwa.

Mjue Mwenyeheri Bakhita

lAlikuwa ni mtumwa aliyeuzwa kwa mabwana watano kwa awamu tofauti

lKwa heshima ya bwana wake aliyemnunua,alichorwa alama sita kifuani,sitini tumboni,48 mabegani

lAlifungwa minyororo mwezi mzima

lOktoba Mosi mwaka huu atatangazwa Mtakatifu

OKTOBA Mosi mwaka huu ni siku inayosubiriwa kwa furaha sana kwani siku hiyo ndiyo Mwenyeheri Bakhita ‘jina la ubatizoYosefina Fotunata’atakapo tangazwa Mtakatifu.Katika Maisha yake Bakhita amepitia raha na mateso mengi.Mama huyu ambaye alifariki dunia Januari 8 mwaka 1947 na kutangazwa Mwenyeheri Juni 17 mwaka 1992 ni mfano wa kuigwa na watu.Kupata undani wa Mama huyu ungana na Mwandishi Wetu Dalphina Rubyema.

 

KATIKA Mwaka huu wa Jubilei Kuu Wakristu wote wa Bara la Afrika na Ulimwengu mzima tunafurahia na kushangilia, pamoja na kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya Mtakatifu Yosefina Bakhita, binti wa Afrika na ua la Sudan.

Tunamsheherekea binti huyu mpendwa wa Mungu dada wa wote ambaye licha ya mahangaiko na mateso makali aliyoyapataa maishani mwake ameweza kuishi kishujaa na kwa ukamilifu fadhili za kikristu na anawekwa mbele yetu kama mfano wa kuigwa. Msichana huyu aliyekuwa mtumwa na asiyejulikana leo anarudi kwetu kama Mtakatifu! Maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristu yanapata maana kubwa katika maisha yake:

"Nakushuru Baba, Bwana wa Mbingu na nchi kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga" (Mt. 11:25-26).

Katika maisha yake ya kusisimua na kushangaza tunaona jinsi Mungu alivyotenda makuu kwa wale wanaomtumaini, vilevile yanatupa changamoto ya kuishi ukristu wetu kwa uaminifu katika mambo makubwa na madogo ya kila siku.

Bakhita sio jina alilopewa na wazazi wake, bali ni jina alilopewa na watu waliomteka na lina maana ya ‘Bahati’.

Watu waliompa jina hili hawakujua kuwa wanatabiri ukweli juu ya binti huyu, kwani licha ya mahangaiko mengi aliyopitia, Bakhita amekuwa kweli mtu mwenye bahati.

Maisha ya mwanzo ya Bakhita na jinsi alivyochukuliwa utumwani

Alizaliwa mwaka 1869, katika kijiji kidogo cha Darfur kiitwacho Olgosa nchini Sudan.

Familia yake iliundwa na baba na mama, wavulana watatu, wasichana watatu. Maisha yake ya mwanzo pale kijijini yalijaa furaha na amani, hakuja mateso maana yake ni nini.

Lakini tukio lililotokea asubuhi moja lilibadilisha kabisa maisha yake. Katika vitabu kadhaa vinavyomuhusu,Bakhita mwenyewe anasimulia:

"Ilikuwa ni asubuhi tulivu na jua lilikuwa limekwisha chomoza. Wenyeji walikuwa wanakwenda mashambani, na watoto walibaki nyumbani wakifanya kazi ndogondogo na wengine kucheza.

Mimi na rafiki yangu tulikuwa porini tunacheza.

Ghafla wakatokea watu wawili wageni, wakanituma niwachukulie mzigo waliouacha nyuma yao na wakamuamuru mwenzagnu arudi kijijini. Kwa vile nilikuwa nimezoea kutii wakubwa wangu, nilikwenda mara moja watu wale wakanikamata kwa nguvu, wakanibeba na kukimbia nami".

Huo ndio ukawa mwisho wa Bakhita kuiona familia yake na kijiji chake. Tunaweza kuhisi uchungu mkubwa alioupata kwa kutenganishwa na ndugu zake wapendwa. Amekuwa sasa mtumwa, mali ya mabwana wale wa kiarabu.

Kuanzia sasa Bakhita ni kama bidhaa sokoni, kwani katika maisha yake kama mtumwa aliuzwa mara tano kwa mabwana mbalimbali ambao walimtesa sana. Ni kwa uwezo wa Mungu ambapo dada huyu aliendelea kuishi na hivi leo tunamsheherekea kama Mtakatifu kwani watumwa wenzake wengi walifariki kwa kupigwa, kwa magonjwa, njaa, kazi nzito na mateso mengine makali.

Alipotekwa kwenye kijiji chake aliuzwa kwenye msafara wa watumwa uliokuwa unaelekea kwenye soko la watumwa. Huko sokoni, alinunuliwa na bwana wa kiarabu ambaye alimfanyisha kazi za nyumbani na shambani. Siku moja yeye na mtumwa mwingine mdogo walifanikiwa kutoroka, lakini katika kuzunguka zunguka wakajikuta wamerudi mikononi mwa bwana mwingine wa Kiarabu.

Uchungu wa Bakhita hauwezi kuelezeka kwani alifikiri kuwa punde ataungana tena na familia yake, lakini amerudi kuwa mtumwa tena.

Bwana huyu akamuuza tena kwa bwana mwingine ambaye mwanzo alimtendea wema kidogo, lakini siku moja alifanya kosa lililosababishwa apigwe mijeledi wa kuendeshea farasi mpaka akazimia.

Alipopata ahueni Bakhita akauzwa kwa mwanajeshi Mturuki, na huko aliteseka sana, kama mwenyewe alivyohadithia:

"Kwa miaka mitatu niliyowatumikia, sikupitisha siku hata moja bila kupigwa, nilijaa madonda mwili mzima. Siku moja nilisikika nikieleza jinsi nilivyowahi kutoroka, hivyo nilifungwa minyororo mwezi mzima, lakini kibaya zaidi ni kuwa ilikuwa desturi kwa watumwa kupigwa chapa mwilini kwa heshima ya bwana wao.

Hivyo nilichorwa alama sita kifuani, sitini tumboni na mabegani arobaini na nane, kishwa nikachanjwa kwa wembe sehemu zote hizo na kupakwa chumvi.

Nilizama katika ziwa la damu! Jinsi maumivu yalivyokuwa makali, ilikuwa ni miujiza yake Mungu kuwa sikufa wakati ule, kweli alikuwa amenitayarishia mambo bora zaidi maishani. Zaidi ya mwezi nililala chini bila kujigueza.

MWISHO WA UTUMWA

Hatimaye Jenerali yule Mturuki aliamua kuuza watumwa wake, na hapo Bakhita alinunuliwa na Bwana Kalisto Legnani (Muitaliano). Hii ilikuwa ni mara ya tano na ya mwisho kwa Bakhita kununuliwa. Kwa njia ya bwana huyu, Mungu alimfungulia Bakhita mlango wa uhuru.

Historia ndefu iliyojaa hofu, vitisho na udhaifu inafikia mwisho. Bwana huyu mpya alikuwa mwema na mwenye huruma, na kipindi hiki Bakhita alikuwa kweli ni mwenye bahati.

Wakati fulani ilimpasa bwana Kalisto kwenda Italia, Bakhita alikuwa amekwisha pata upendo kama wa mzazi kutoka kwa baba huyu, akapenda kwenda naye. Huko Italia akachukuliwa na rafiki wa yule bwana ili awe yaya wa mtoto wake aliyeitwa Mimina.

Maisha na Mikasa

Mwanamke aliyefiwa na mumewe apata chungu ya maisha

lNi Kutoka kwa ndugu wa marehemu

lAsema 'Kama matatizo yangekuwa yanaua, basi na mimi ningekuwa nimesha kufa'

PAMOJA na serikali na Mashirika mbalimbali kuweka nguvu zake nyingi katika kupiga vita vitendo vya unyanyasaji wa wanawake hususan wajane,juhudi hizi zinaonekana kugonga mwamba kwani wajane wengi wamekuwa wakinyanyaswa na ndugu wa upande wa marehemu.

Mara kwa mara tumekuwa tukisikia kuwa fulani baada ya kufiwa na mme wake kafukuzwa na ndugu wa marehemu bila kujali kama mali iliyoachwa ni nguvu za wote wawili yaani mume na mke na hata kama wamezaa watoto, ndugu nao wako tayari kubaki na watoto wao lakini kumwamuru mama yao afunge virago, kama sivyo basi baadhi ya mali za marehemu zitagawiwa hata kwa watu wasiohusika.

Hali hii ndiyo iliyo mkuta Sarah Koja. Kupata undani wa kisa hiki cha kusikitisha ungana na Mwandishi Jenifer Aloyce wa DSJ.

"KATIKA kipindi cha miaka 15 nilichokaa na marehemu mme wangu,sikutarajia kwamba itakuja itokee siku niwe katika hali ya majuto namna hii,tuliishi raha mstarehe pasipo matatizo ya aina yoyote".

"Loh!siku chache baada ya kufariki kwa marehemu mme wangu ndipo nilipoanza kusikia chungu ya maisha,ndugu wa marehemu walinigeuka kama hawanijui,ndugu yangu, kabla hujafa,hujaumbika" hayo ni maneno yaliyotoka kinywani mwa mwanamama ,Sarah Koja.

Akieleza kwa undani mkasa huo,Mama Koja ambaye ni mjane anasema kuwa ilikuwa ni Oktoba 24 mwaka 1979 siku ambayo alifunga pingu za maisha na Bw.Stephen Millanzi.

Anasema wakati anafunga ndoa hiyo ya Kiislamu iliyofungwa mkoani Tanga,alikuwa bado ni kijana mbichi kwani alikuwa na umri wa miaka 18 tu wakati mmewe ambaye sasa ni marehemu,alikuwa na umri wa miaka 35.

Anasema baada ya ndoa yao walikuja kukaa Jijini Dar-Es-Salaam na huyo mmewe ambaye hadi anafariki alikuwa ni Meneja wa Walaka wa Shirika la Meli nchini (NASACO) Kanda ya Mbeya.

Anasema katika kipindi cha ndoa yao waliweza kununua viwanja viwili katika eneo la Mbagala Jijijini,ambapo kiwanja kimoja wapo ambacho kilionekana kikubwa kilinunuliwa na mmewe pamoja na kujenga nyumba kwenye kiwanja hicho.

Anasema kutokana na yeye kujishughulisha na biashara ndogo ndogo aliweza kununua kiwanja kidogo ambacho kilipakana na kile alicho nunua mumewe na kujenga nyumba .

"Kwa vile mme wangu alishanunua kiwanja kikubwa na kujenga nyumba,tuliona kwamba hakuna haja ya kujenga nyumba kubwa kwenye hicho kiwanja nilichonunua mimi, tulishauriana na mme wangu ambapo nilijenga banda la vyumba vinne na kuanza kufuga kuku"anasema Mama huyo.

Anaongeza kuwa wakati huo,marehemu alikuwa na mke mwingine ambaye alimjengea nyumba katika eneo la Tandika Wilayani Temeke Jijini Dar-Es-Salaama aliyemtaja kwa jina la Anastazia James ambaye naye kwa hivi sasa ni marehemu.

Anasema pamoja na ndoa hiyo kuwa niya uke wenza lakini haikuwa na migongano yoyote kwani mmewe alimtosheleza kwa kila jambo.

Mjane huyo anaendelea kusema kuwa katika kipindi cha ndoa yao na marehemu mmewe aliyefariki dunia Mei 12 mwaka 1994,walifanikiwa kupata watoto wanne wakiwemo wavulana wawili na wasichana wawili.

Anawataja watoto hao kuwa ni Millanzi S.Millanzi (20),Neema Milanzi (18),Danile Millanzi (13) na Bahati Millanzi (10).

Alisema kama zilivyo mila na taratibu za makabila mengi hapa nchini,baada ya kufariki marehemu, wana ndugu upande wa marehemu walikaa kikao na kumchagua msimamizi wa mirathi ambapo mtoto mkubwa wa marehemu anayeitwa David S.Millanzi alichaguliwa kusimamia mirathi hiyo.

Anasema David ambaye ni mtoto wa mke mwenzake alikabidhiwa vitabu vya benki vilivyo achwa na marehemu mmewe pamoja na nakala mbambali za mkataba wa Bima na NPF.

"Tangu kufariki mme wangu nimepokea hela mara mbili tu ambazo niliambiwa ni kutoka Bima na NPF ya marehemu,tangia hapo sijawahi kupewa kitu chochote na wala sijui hiyo pesa iliyokuwa benki imepelekwa wapi!"anasema bila kutaja kiasi cha pesa alicho pokea.

Anasema kinacho msikitisha zaidi ni kwamba Desemba 12 mwaka jana wanandugu pamoja na watoto wa mke mwenzake walikaa kikao bila kumshirikisha yeye ama watoto wake.

Katika kikao hicho wanandugu hao walifanya maamuzi ya kugawa mali za marehemu ambapo mke mwenzake pamoja na watoto wake walipewa nyumba ya Tandika na yeye (Sarah) na watoto wake walipewa nyumba ya Mbagala na bila kujali kwamba banda la Mbagala nalo ni lake alilijenga kwa nguvu zake mwenyewe,banda hilo alipewa mtoto mwingine aliyedhaniwa kuwa mtoto wa marehemu aliye mtaja kwa jina la Issa Millanzi ambaye hata hivyo anasema marehemu mmewe kwenye orodha ya watoto aliowaacha jina hilo halipo.

"Katika orodha yake,marehemu aliacha watoto wa nane,wanne wakiwa niliowazaa mimi na wanne wakiwa ni wa mke mwezangu. Sasa nashangaa huyo Issa Milanzi katoka wapi!"anasema kwa mshangao mama huyo.

Anawataja watoto wanaozaliwa na mke mwenzake kuwa ni David Millanzi,Marry Millanzi,James Millanzi na Dola Milaanzi.

"Baada ya kusikia taarifa hizi, nilijaribu kuwaeleza hao wanandugu juu ya kibanda hiki cha Mbagala ambacho kwa hivi sasa kina wapangaji wangu. lakini cha ajabu hakuna mtu aliye nisikiliza, kiwanja hicho nilichojenga,nilikinunua Machi 9 mwaka 1980" anasema.

"Hilo banda mimi nililijenga kwa nguvu zangu mwenyewe,iweje arithishwe mtu mwingine, kinacho nisikitisha zaidi nasikia banda langu hilo mpaka sasa limeuzwa kwa Bw. Lomwod Godifrey Kishura na makubaliano ya kuuziana banda hilo yalifanyika mahakamani japokuwa mimi sikutaarifiwa na wala sikuwepo"anasema.

Mama huyo alipoulizwa kuwa amejuaje kama mauziano hayo yalifanyika Mahakamani, alisema huwa anaona watu wanakuja kwenye eneo lile lilipo banda hilo na kuonyeshana mipaka wenyewe kwa wenyewe bila kumhusisha.

Anasema alipoona suala hili linazidi kumpa kero,alikata shauri la kwenda kwa mjumbe ambapo baada ya kumpa taarifa ,mjumbe huyo alimkabidhi makaratasi (nakala) na alipoyasoma ndipo alipoona jina la mtu huyo aliyerithishwa banda hilo na jinsi lilivyouzwa pamoja na mgawanyo wa nyumba za marehemu.

"Ndipo hapo nilipo gundua siri za hao wana ndugu wa marehemu mme wangu na makaratasi hayo yalionesha kuwa mauziano hayo yalifanyika kwenye Mahakama ya Mwanzo Mbagala"anasema

Anasema baada ya kuona hivyo alienda Mahakama ya Mwanzo Mbagala na huko alieleza matatizo yake ambapo yeye na hao wanandugu waliogawa mali hizo waliandikiwa siku ya kwenda kusikiliza kesi hiyo ya mirathi.

"Chakushangaza ni kwamba ilipofika hiyo tarehe nikaenda ,cha ajabu na kilichonisikitisha ndugu mwandishi ni hiki, nilipofika tu mahakamani Hakimu ambaye ni Mfawidhi wa Mahakama hiyo alianza kunisema eti kwanini nimekuja leo wakati wenzangu wamekuja jana, nilimuuliza hakimu kwanini wamekuja jana wakati tarehe tuliyopangiwa ni leo akaendelea kwa kunisema"anasema

Anaongeza "nilichofanya ndugu Mwandishi ni kuwatupia makaratisi yao pale mezani na kuondoka zangu kwa sababu kila tarehe tunayopangiwa wenzangu wanakuja tarehe tofauti".

Anasema baada ya kuona amezungushwa sana aliamua kwenda kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na huko walimpa ushauri kuwa kesi hiyo inabidi ihamie wilayani ndio waweze kunisaidia.

"Niliporudi Mahakama ya Mwanzo Mbagala kuwaelezea suala hilo, wao waliniambia kuwa kesi hiyo hawausiki nayo wamekwisha ipeleka wilayani na huko nimepata uhakika kuwa tayari imefika "anasema.

"Kama matatizo yangelikuwa yanauwa basi na mimi ningelikwisha kufa zamani kwa matatizo yanayonisonga mpaka inafikia kipindi nalia mpaka nachoka"anasema huku akifuta machozi.

Anaongeza "naomba kama kuna anayeweza kunisaidia ajitokeza ili haki iweze kutendeka katika hiyo mirathi ya mume wangu kwani ni uonevu mtupu ninaotendewa na hiyo kesi imekwisha hamishiwa wilayani Temeke.