Mpemba na Muunguja, nani Mzanzibar? (2)

Inatoka Toleo lililopita

HISTORIA ya Visiwa vya Unguja na Pemba imekuwa ni ya migogoro na migongano baina ya makundi yanayo tofautiana kwa asili, rangi ya ngozi, uchumi na kisiasa.

Katika makala hii Mwandishi Widimi Elinewiga wa DSJ, anajaribu kueleza juu ya migongano hiyo ya kihistoria visiwani humo.

Hayati Sheikh Amri Abed Amani Karume alipoulizwa kuhusu juu ya umwagaji damu na kuwekwa kizuizini kwa baada ya Mapinduzi, alijibu kwamba huo ni wakati wa kuwageuzia kibano Waarabu ili nao wapate maumivu kutokana na kuvaa kiatu kinacho bana .

Hayati Nyerere na Hayati Mzee Karume walihakikisha kundi la Waarabu halifurukuti visiwani humo.Kuundwa kwa muungano huo pia ni katika harakati za Mwalimu kutekeleza ndoto yake ya kuleta muungano wa Bara la Afrika .

Chuki na migongano baina ya makundi ya watu visiwani humo yaliendelea hadi kufikia kuuawa kwa Mzee Karume kwa kupigwa risasi na watu wenye asili ya Kiarabu.

Hata hivyo, baada ya mauji hayo, Nyerere aliviweka visiwa hivyo chini ya ulinzi mkali mpaka Mzee Abdu Jumbe alipokuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Tangu mapinduzi hayo, Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar liliendelea kudhibitiwa na ASP ambao wengi wao ni Waafrika Weusi wenye asili ya Bara.

Alhaji Aboud Jumbe alipogundua uwezekano wake wa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa umetoweka, aliuza hekaya za Zanzibar na kumezwa na bara, Waislamu kuonewa na suala la serikali ya tatu.

Lakini kwa ujanja wake, Nyerere aliingilia kati suala hilo na kumtolea mfano wa hesabu ya kujumlisha moja na moja ambayo jibu lake ni mbili na kamwe haiwezekani kuwa tatu. Alikuwa akimaanisha kwamba serikali mbilizikiungana zinaunda serikali mbili .

Kinyang’anyiro cha urais mwaka 1984 na 1985 kilithibitisha pia kwamba kambi ya waasisi wa ASP ndiyo inayokata shauri katika maasuala ya nani atawale nchini

Dk. Salmin Ahmed Salim alilazimika kutoa jina lake katika kinyang’anyiro hicho kutokana na hali ya hewa ilivyokuwa wakati huo. Ingawa suala la asili yake halikutajwa, Kamati Kuu ya CCM ilimteua Mzee Ali Hassan Mwinyi kuwa mgombea pekee wa kiti cha urais.Ifahamike kwamba ingawa februari 5, 1977, TANU na ASP ziliungana na kuzaa CCM, Hakikuleta mabadiliko ya msingi visiwani humo. Ukweli ni kwamba hata muungano wa 1964, haukuwa na mabadiliko yoyote ya kimuundo kwa upande wa Zanzibar.

Makubaliano kati ya Nyerere na Karume yalipitishwa na Bunge upande wa Tanganyika na Baraza la Mapinduzi, kwa upande wa Zanzibar, yalipitishwa kwa mizengwe.

Wakati ule Serikali ya Zanzibar ilibaki ilivyo na Tanganyika ilitoweka kabisa baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano.

Hayati Baba wa Taifa alitumia umaarufu wake kumpatia ushidi mgombea wa kiti cha urais 1985 Sheikh Abdul Wakil baada ya kunyimwa kura na Wazanzibar wengi.

Hata hivyo, Wakil alishindwa kuhimili migogoro iliyokuwepo visiwani humo mpaka akalazimika kuachia ngazi baada kumaliza kipindi kimoja tu.

Kutokana na historia ndefu ya visiwa hivyo uhasama baina ya makundi hayo mawili utaendelea kuwepo endapo Watanzania hao wa Visiwani hawatatumia busara zao kuondoa tofauti zao za kikabila na kujiona kwamba wao ni wamoja nchi mwao na hakuna mzalendo wa maana kuliko mwenzake .

Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa waziri kiongozi alihakikisha amewapa madaraka wafuasi wake na kubadili katiba ya ili kumweza mtu rangi yeyote kuitwa Mzanzibari.

Kimsingi hivi leo wanachama wa vyama hivi hawajali rangi ya mtu au asili yake , lakini ni kweli CCM inaungwa mkono zaidi na watu wenye asili ya bara, na CUF inaungwa na mkono na wale walioathirika na mapinduzi ya 1964.

Uchaguzi wa 1995 ulithibitisha tofauti kubwa ya kisiasa pale ambapo vyama vyote havikuwa tayari kukubali matokeo ya uchaguzi mmoja wao akishinda.

Awali mgombea wa CCM Dk. Salmin Amour alitangaza kkuwa kama mgombea wa CUF Maalim Seif angeshinda angekubali matokeo hayo. Baada ya CCM kushinda naye Maalim Seif alikataa kuyakubali matokeo haya mpaka sasa yeye anaendelea kudai kuwa alishinda.

Kama kweli CUF ilishinda basi zile mbinu walizotumia ZNP na ZPPP kuinyang’anya ASP ushindi, ndiyo nao waliotumia CCM

Ni dhahiri kwamba Rais Benjamin Mkapa anafahamu kiini cha mgogoro wa Zanzibar ndiyo maana anasema Kwamba CCM haitaruhusu Mapinduzi ya Zanzibar yabezwe na kudharauliwa, na alitoa mfano wa methali alisema, ni afadhali zimwi ulijualo kuliko usilolijua .

Maisha na Mikasa

Madaktari walitushauri tuvunje ndoa yetu

lKisa; kuzaa watoto wenye 'Sickle Cell'

lMimi, mke wangu tuliukataa ushauri huo

lMungu ni mkubwa! sasa tunao watoto saba kati yao watano ni wazima

KATIKA maisha tunayoishi kila siku tumekuwa tukisikia mara kwa mara kwamba ndoa ya watu fulani imevunjwa kutokana na sababu kadhaa.

Nyingine zimekuwa zikivunjika kutokana na ushauri wa ndugu ama jamaa wa upande mmoja wapo aidha wa mwanamke ama mwanaume ama madaktari.Hali hii ndiyo iliyompata Bw.Martin Luembo na Mkewe Bibi Spensioza Luembo wakazi wa Uvinza mkoani Kigoma.Wapendanao hawa walishauriwa na madaktari mbalimbali waachane na wavunje ndoa yao kutokana na kuzaa watoto wenye ugonjwa wa "Sickle Cell"lakini kutokana na upendo wao wa dhati waliokuwa nao walikataa kabisa ushauri huo na hadi hivi sasa wanao watoto nane kati yao wawili tu ndio wanaosumbuliwa na ugonjwa huo.Ungana na Mwandishi Dalphina Rubyema upate undani wa mkasa huu kama livyohojiana na wanandoa hawa alipokutana nao Kigoma hivi karibuni.

"MADAKTARI na ndugu zetu wa karibu walitushauri tutengane eti kwa vile tulikuwa tunazaa watoto wenye Sickle Cell.

Kwa vile mimi na mke wangu tulikuwa tukipendana sana na pendo letu lilikuwa ni la dhati ,tuliukataa kata kata ushauri huo,tukaamua kuendelea kuishi pamoja hadi hapo kifo kitakapotutenganisha"

".Nawashukuru sana wazazi wangu na hayati Marehemu James Sanga wa Jimbo Katoliki la Mbeya kwani nao waliunga mkono uamuzi wetu".

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyotoka kinywani mwa Bw.Martin Luembo ambaye ni hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Uvinza mkoani Kigoma maneno ambayo yaliungwa mkono na mkewe Bibi Spensioza.

Bw.Martin ambaye anaishi Kigoma kikazi akitokea katika eneo la Kinambo-Zimba mkoani Rukwa anasimulia kuwa Desemba 3 mwaka 1975 ndipo alipo funga pingu za maisha na Bibi Spensioza ambaye naye ni mwenyeji wa mkoa wa Rukwa eneo la Msia-Zimba ,ndoa ambayo ilifungwa katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Kigoma la Bikira Maria Mshindaji.

Anasema Januari 30 mwaka 1977,miaka miwili baada ya ndoa yao walifanikiwa kupata mtoto wa kiume anayeitwa Renatus.

Anasema Renatus tangu kuzaliwa kwake alikuwa akisumbuliwa sana maumivu ya mara kwa mara na baada ya kupimwa hospitalini ilibainika kuwa alikuwa akikabiliwa na "Sickle Cell".

"Tuliendelea tu kumlea hivyo hivyo lakini kila kukicha ni sisi na hospitali"anasema Bibi Spensioza na kabla ajamaliza mmewe anaingilia kati "Hata sasa ukimwona huwezi ukaamini kama ni kijana mwenye umri wa miaka ishirini na tatu,anaumbo dogo sana kutokana na kusumbuliwa na huo ugonjwa".

Baba huyo anaendelea kuelezea kuwa miaka miwili baada ya kuzaliwa Renatus ambaye ni kifungua mimba wao,walifanikiwa kupata mtoto mwingine wa kike aliyepewa jina la Martina ambaye naye alikuwa na tatizo lile lile la Sickle Cell.

Anasema mwaka huo huo aliozaliwa mtoto wao wa pili na kukutwa na tatizo sawa na yule wa kwanza,ilibidi waende kutafuta ushauri wa kitaalamu kwa madaktari ambapo walienda katika hospitali ya mkoa wa Kigoma inayoitwa Mauweni na huko ndiko waliko kutana na ushauri ambao hawakutegemea.

"Madaktari walitwambia kuwa kila mtoto tutakayekuwa tukimzaa atakuwa anakufa na "solution" iliyopo ni mimi kutengana na mke wangu"anasema Bw.Luembo.

Anaongeza "Tulipofika nyumbani tuliangaliana na mke wangu kila mmoja alikuwa na hamu ya kusikia uamzi wa mwenzake lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kutamka neno lakini kwa vile mimi ni mwanaume nilijikaza kusema jambo".

"Nilimuuliza mke wangu,vipi si umesikia ushauri wa madaktari?Wamesema tuachane sasa lini utaondoka hapa nyumbani kurudi kwenu kuanza maisha mapya na huyo mwanamme mwingine utakaye mpata?Lilikuwa ni swali lililougusa sana moyo wangu lakini nilijikaza"anasema Bw.Martin.

Bibi Spensioza anaingilia kati "Kwakweli ulikuwa ni wakati mgumu sana hata sipendi kukumbukia!,mimi nilimwambia mme wangu aamue mwenyewe la kufanya ingawa sikupenda hata kidogo kutengana naye akini kama angesema tuachane mimi ningefanya nini?".

Wanasema baada ya kukaa wote na kutafakari kwa pamoja walifikia muhafaka kwamba hawawezi kuvunja ndoa yao kwa sababu kama hiyo.

"Tuliamua kwamba haiwezekani kuvunja ndoa yetu na katika maadili ya dini yetu ni kwamba kifo ndicho kitutenganishe,kwa hiyo tukakubaliana kwamba hata kama watoto tutakao wazaa watakufa wote tusikubali kuachana"anasimulia Bw.Martin.

Anaongeza "Hata wazazi wangu waliniunga mkono kwamba hakuna kuachana na mwingine aliyetuunga mkono ni hayati marehemu James Sangu wa Jimbo Katoliki la Mbeya ,huyu Askofu tulimshirikisha kwa vile ni mtu wa nyumbani hivyo tulimuomba ushauri".

Anasema hayati Askofu Sangu aliwambia kuwa ndoa ni msalaba kama alioubeba Yesu Kristo hivyo lazima na wao wakubali kuubeba.

Anasema baada ya hapo ndoa yao iliendelea kudumu katika pendo la hali ya juu na walifanikiwa kupata watoto wengine zaidi na waliendelea kuishi katika pendo na walifanikiwa kupata watoto wengine zaidi lakini mtoto wao wa pili Martina alipofikisha umri wa miaka mitano,bahati mbaya alifariki dunia!.

Wanasema hilo halikuwa pigo la pekee,walipata pigo lingine kwani wiki moja baada ya marehemu martina kufariki walifiwa tena na mtoto wao mwingine aliyeitwa Yusta ambaye naye alikuwa akiugua ugonjwa huo wa Sickle Cell na ni mtoto wa nne kuzaliwa.

"Hawa hawakuwa ridhiki yetu kwani Mungu alimchukuwa"anasema kwa masikitiko Bw.Luembo ambapo mkewe anaongeza "Bwana alitoa na akatwaa" wote wawili kana kwamba walipanga ,wanatamka kwa pamoja "Jina la Bwana libarikiwe".

"Kwakuwa hakuna kitu chochote kinachoshindikana mbele ya Mwenyezi Mungu katika uzao wetu wa watoto tisa ni watoto wawili tu waliofariki na hawa saba waliobaki wawili kati yao ndio wenye Sickle Cell"anasema Bw.Luembo.

Anawataja watoto ambao hawasumbuliwi na ugonjwa huu kuwa ni Apolonia (18) anaye soma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Chumvi iliyopo mkoani humo,Imelda (17) anayesoma kidato cha kwanza Chumvi Sekondari,Odetha (12) anayesoma darasa la sita Shule ya Msingi. Uvinza,Aloyce(10) ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Uvinza na kitinda mimba Aditrude (5).

Anawataja watoto ambao ni wagonjwa kuwa ni kifungua mimba wao Renatus (23) na Libelatha (8) ambaye anasoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Uvinza.

Watoto waliofariki ni Martina aliyefarikia akiwa na umri wa miaka mitano na mtoto wa nne kuzaliwa aliyekuwa akiitwa Yusta ambaye alifariki akiwa na umri wa miezi saba.

"Renatus yeye aliishia darasa la saba,hakuendelea na masomo ya sekondari.Hivi sasa ni mfanyabishara na mpiga picha,pale tunapoishi ndiye mpiga picha mashuhuri hata kiwandani (Uvinza) wakiwa na sherehe zao huwa wanampa tenda "anasema Bibi Spensioza.

Anaongeza "Sikutegemea kama Renatus angeweza kupona maana kila siku alikuwa yeye na vidonge vidonge na yeye".

Wanandoa hao ambao Juni 20 mwaka huu waliadhimisha jubilei ya miaka 25 ya ndoa yao wanasema kuwa wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwani kile kilicho shindikana kwa wataalam kimewezekana kwa Mungu.

"Katika ndoa hakuna kitu kizuri kama uvumilivu,sisi tumevumiliana sana maana tunavyoishi hadi hivi leo tumepata vishawishi vingi toka kwa majirani na jamaa zetu ,kama tungevisikiliza vishawishi vya kututenganisha sijui sasa hivi tungekuwa wapi,tuliziba na tunaendelea kuziba masikio yetu,hatusikilizi la mtu labda kama ni zuri"anasema Bw.Martin.

"Mwaka huu tumesherekea Jubilei ya miaka 25 ya ndoa yetu tunamuomba Mwenyezi Mungu atufikishe mbele ili tuweze kusherekea hata miaka 50 ya ndoa yetu"anaongeza mkewe Bibi Spensioza.

"Masikini! Madaktari walipotaka tuvunje ndoa yetu tulikuwa tumeishi wote miaka minne,ndoa yetu ilikuwa bado changa ,tungekubali ushauri wao hii suala la kusherekea na kufurahi Jubilei ya miaka 25 kwetu ingekuwa ndoto"anaongeza Bw.Luembo.

Hata hivyo wanandoa hawa ambao sasa wanaanza kuelekea uzeeni wanasema kuwa kama suala la Sickle Cell halikuweza kuvunja ndoa yao,basi hakuna kitu chochote duniani kitakacho watenganisha ila Mwenyezi Mungu.

"Mungu tu ndiye atakaye tutenganisha lakini mwanadamu hawezi kitu,tumepata misukosuko mingi maishani ambayo hatutaweza kuisahau,Mungu azidi kutusaidia tulee watoto wetu hata hawa wanaoumwa Mungu aendelee kuwalinda"alisema Bibi Spensioza.