Magazetini Wiki Hii

First Adili yafungwa

Mtanzania Mei 16

BENKI Kuu ya Tanzania imeifunga kwa muda usiojulikana Benki ya First Adili kuanzia jana kutokana na benki hiyo kuwa kwenye hali mbaya ya fedha.

Kwa mujibu wa taarifa ya BoT ambayo ilibandikwa kwenye kuta za jengo la benki hiyo jana benki hiyo ya kwanza kumilikiwa na wazawa wa nchini itakuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa Benki Kuu kuanzia jana.

'Benki Kuu ya Tanzania imechukua usimamizi wa Benki ya First Adili Ltd. kutokana na wenye hisa katika benki hiyo kuonyesha uwezo mdogo wa kuiendesha na kuwa kwenye hali mbaya ya kifedha" ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema kwamba BoT imechukua uamuzi huo chini ya sheria za benki na Taasisi ya Fedha ya mwaka 1991 kifungu cha 42 kinachoipa mamlaka Benki Kuu kuingili ana kusimamisha kazi za benki yoyote pale inapoonekana kudodora kiutendaji.

Moto wateketeza Hospitali ya Temeke

Tanzania Leo Mei 17

WATU wawili wamefariki na wagonjwa kadhaa hawakujulikana walipo kufuatia purukushani zilizojitokeza wakati wa harakati za kuuzima moto mkubwa uliozuka na kuteketeza jengo la utawala na uhasibu katika Hospitali ya Manispaa ya Temeke mjini Dar es Salaam jana jioni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa DCP Alfred Gewe aliyekuwapo kwenye eneo la tukio alisema kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa au kufa kutokana na kuuguzwa na moto huo ambao chanzo chake hakikuweza kujulikana mara moja.

Moto huo ulianza majira ya saa 10:45 jioni, ingawa chanzo chake hakikuweza kufahamika.

Gari la Mbunge laporwa Arusha

Mtanzania Mei 17

GARI la Mbunge wa Viti Maalum, wanawake kwa chama cha CUF, Elizabeth Kasembe ni mojawapo ya magari matatu yaliyoporwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika matukio ya ujambazi yaliyotokea kati ya Mei 4 hadi 14 mwaka huu mjini Arusha.

Katika matukio hayo yaliyotokea katika eneo la Njiro, lililopo nje kidogo ya Manispaa ya Arusha majambazi hao kwa nyakati tofauti walivamia nyumba za wakazi mbalimbali wa eneo hilo na kupora mali ambazo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Wenceslaus Magoha alisema katika taarifa yake juzi kuwa katika moja ya matukio hayo, majambazi hayo yalivamia nyima ya Mbunge huyo usiku wa Mei 4 mwaka huu.

Sihusiki na madawa ya Kulevya - Diria

Rai Mei 18,

MWANASIASA mkongwe nchini, Ahmed Hassan Diria, anayewania Urais wa Zanzibar, amesema kuwa kamwe hajapata kushiriki biashara ya madawa ya kulevya.

Ameiambia RAI kwamba habari na uvumi kwamba yeye alipata kuhusika na biashara hiyo haramu ya mihadarati ni uongo mtupu.

"Sitaki kujibu tuhuma hizo, kwa sababu ni mambo ambayo hayana msingi, lakini kama kuna mtu mwenye ushahidi juu ya tuhuma hizo aseme.Laiti kama ningekuwa na dosari, viongozi wangu, marehemu Mwalimu Nyerere na baadaye mzee Ali Hassan Mwinyi, wasingeniacha kwenye madaraka kwa muda wote huo wa zaidi ya miaka 20," anasema Diria.

Jeshi la Polisi lanunulia askari wake nyumba

Uhuru Mei 17

JESHI la Polisi nchini limewanunulia nyumba kadhaa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kuliendeleza jeshi hilo kwa kuboresha maisha ya askari wake. Hayo yalisemwa na baadhi ya askari polisi mkoani Dar Es Salaam jana na kumpongeza Mkuu wa Jeshi hilo Inspekta Jenerali Omar Mahita kwa jitihada za kuliboresha jeshi hilo.

Mwalimu afa kwa hofu ya wakaguzi

Tanzania Leo Mei 19

MWALIMU wa kike wa shule ya Msingi Vingunguti 'B' mjini Dar es Salaam amefariki hivi karibuni katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana wiki hii mjini Dar es Salaam zilieleza kwamba mwalimu huyo alifariki wakati wakaguzi wa idara ya elimu mkoani Dar es Salaam walipokuwa wakiendelea na ukaguzi shuleni hapo.

Mwalimu huyo alitajwa kwa jina la Anumiye Kilaga ambaye alikuwa mwenyeji wa Njombe Mkoani Iringa.

Habari zilizopatikana kutoka shuleni hapo zilieleza kwamba Mwalimu huyo alifariki dunia Aprili 30, mwaka huu saa 3.00 usiku nyumbani kwake huko Vingunguti.

Habari hizo zilisema kwamba Aprili 28 mwaka huu wakaguzi wa Shule za msingi kutoka makao makuu ya Mkoa wa Dar es Salaam walifika shuleni hapo ili kukagua utendaji kazi wa walimu hao.

Ajiua kwa kukumbushwa deni na Dada yake

MKAZI mmoja wa Manzese kwa Mfugwa Mbwa, Abdallaha Nyiho (18) amedaiwa kujiua kwa sumu baada ya dada yake kumkumbusha deni lake la sh 100,000. akithibitisha tukio hilo jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Alfred Gewe alisema Nyiho alikuwa anadaiwa na dada yake Mwanjaa Raphael ambaye inasemekana alimkopesha fedha hizo ili afanyie biashara.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 7:40 mchana wakati akipelekwa hospitali ya rufani ya Muhimbili kutibiwa kutokana na hali yake kuwa mbaya baada ya kunywa sumu ambayo haijafahamika.

Gewe alisema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na polisi bado wanalifanyia upelelezi zaidi.