Make your own free website on Tripod.com

Magazeti Wiki Hii

Watu watano wa familia moja wafa ajalini

Majira Mei 8

WATU watano wa familia moja wamekufa papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali ya barabarani.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Handeni kuja wilayani hapa, kugonga treni ya mizigo katika kivuko cha barabara na reli.

Habari za Polisi zilizopatikana jana zilisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa moja usiku eneo la Majengo baada ya gari hilo aina ya Land Rover namba TZD 8699 kusindwa kusimama na kuligonga treni hilo.

Waliokufa wametambuliwa kuwa ni Shahid Mohamed (13) Naseem Karim, Abdulatif Noormohamed (48) aliyekuwa dereva wa gari hilo, Mariam Isaac na Naseem Mohamed wote wana asili ya Kiasia.

Afa baada ya kukatwa kimeo

Majira Mei 8

MKAZI wa Mbiji, Kinondoni aliyetambuliwa kwa jina moja la Omary, amefariki dunia kutokana na maumivu makali yaliyotokana na kukatwa kimeo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Alferd Gewe, aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa iliyopita kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 25, alifariki akiwa kazini katika machimbo ya mchanga.

Alisema kabla ya kukumbwa na mauti Omary aliwaambia wafanyakazi wenzake kuwa alikuwa na maumivu makali kwa kuwa alikuwa amekata kimeo.

Bw. Gewe alisema Bw. Omary akiendelea na shughuli zake alianguka ghafla na kutokwa damu puani, hatimaye kufariki dunia, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Muhumbili.

Komoni yaua wanne Dar

UHURU MEI 9

WATU wanane wamekufa na wengine 17 wamelazwa katika hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam wakiwa mahututi baada ya kunywa pombe ya kienyeji ya komoni inayosadikiwa ilikuwa na sumu,Mwanamke anayedaiwa kuuza pombe hiyo anashikiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo Macdonald Mwaijande watu hao wanadaiwa walikunywa pombe hiyo jana asubuhi eneo la Kimara King'ong'o nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Mwandishi wa habari hii, ambaye alikuwa katika maeneo ya mapokezi hospitalini hapo alishuhudia miili ya Marehemu hao pamoja na walionusurika wakishushwa kutoka kwenye magari mbalimbali kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza huku umati wa watu ukishuhudia tukio hilo.

Watu waliosindikiza marehemu hao pamoja na walioathiriwa na pombe hiyo waidai kuwa watu hao walikuwa wakiokotwa kutoka sehemu mbalimbali huko Kimara wakiwa katika hali mbaya mara baada ya kunywa pombe hiyo.

Rushwa Tanzania yakatisha tamaa wawekezaji

Uhuru Mei 9

WAWEKEZAJI wengi kutoka nje wanashindwa kuwekeza nchini kutokana na tatizo la rushwa kushamiri katika sekta mbalimbali.

Hayo yalisemwa jana na Balozi wa Marekani nchini Charles Stith wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ubalozi huo mjini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na nchi kuwa na uoto wa asili na vivutio vingi vinavyoweza kuwapendeza wawekezaji lakini tatizo la rushwa limechangia kwa kiasi kikubwa kuwakatisha tamaa.

Stith alikiri kwamba tatizo la rushwa halipo Tanzania peke yake bali karibu nchi zote duniani zinakabiliwa na tatizo hilo ingawa serikali husika zinajitahidi kupiga vita.

Aliyataja matatizo mengine kuwa ni sheria ngumu za upatikanaji wa leseni na urasimu ulipo kwenye sekta mbalimbali za serikali.

Dawa za Ukimwi kuuzwa nafuu

Mtanzania Mei 12

RAIS Bill Clinton wa Marekani amesaini waraka utakaowezesha dawa za kupambana na Ukimwi zipatikane kwa bei rahisi katika nchi za Afrika.

Kwa mujibu wa waraka huo ambao ulitiwa saini juzi, Marekani itayawekea masharti nafuu, makampuni yatakayotengeneza dawa za kupambana na Ukimwi ambazo zitatumika Afrika.

Mwakilishi wa Marekani kuhusu masuala ya biashara, Cjarence Barshfsky alisema katika siku za nyuma Marekani ilikuwa ikiweka masharti magumu kwa ajili ya makampuni yanayosambaza dawa nje ya nchi hiyo.

Majambazi wavamia Ikulu ndogo Shinyanga na kupora

Mtanzania Mei 9

MAJAMBAZI wasiofahamika idadi yao, usiku wa kuamkia jana walivamia Ikulu ndogo mjini Shinyanga na kupora bunduki na risasi za walinzi.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Emson Mmari zinasema ya kuwa watu hao waliingia katika Ikulu ndogo hiyo inayotumiwa kama makazi ya Rais awapo mjini humo, kati ya saa sita na saa saba usiku.

Majambazi hao waliovamia Ikulu ndogo baada ya umeme kukatika katika eneo hilo la uzunguni, waliwajeruhi polisi wawili waliokuwa lindoni na kuwapora bunduki mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG) zikiwa na risasi 20 kila moja.

Majambazi hao ambao walikuwa na jiwe kubwa la Fatuma linaloaminika pengine lingetumika kuvunja nyumba hiyo hawakuchukua kituo chochote zaidi ya bunduki hizo na risasi

Majambazi hao kwa mujibu wa habari hizo waliingia baada ya kukata seng'enge zilizopo nyuma ya Ikulu hiyo inayopakana na nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga walipowashambulia kwa mawe polisi hao wawili waliokuwa katika lindo na kisha kupora bunduki hizo.