Magazeti Wiki Hii

Hakuna nyongeza ya mishahara

Majira Mei 2

RAIS Benjamin Mkapa jana alishindwa kukata kiu ya wafanyakazi nchini walitarajia angetangaza kupanda kwa mishahara.

Hali hiyo ilitokana na Rais Mkapa kuzungumzia hali ya uchumi zaidi kwa kipindi cha uongozi wake miaka minne iliyopita na kuwataka wafanyakazi kivumilia hadi uchumi utakapoimarika.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yaliyofanyika kitaifa mjini Dodoma jana Rais Mkapa alisema utashi wa Rais yeyote na serikali yake kulipa mishahara minono hautoshi bila kuambatana na uwezo wa kulipa.

Hotuba hiyo ilitangazwa moja kwa moja na Redio Tanzania.

"Mzazi yeyote angependa kumpa mwanawe fedha za kutosha za matumizi ya shule. Anampa sh 500, haina maana kuwa zinatosha au asingelipenda ampe Sh. 1,000 kwani amejenga uwezo." alisema

Alisema kama ilivyo kwa mzazi, ndivyo ilivyo kwa Serikali na kwamba yuko radhi asipendwe kwa kusema ukweli, kuliko kupendwa kwa kulaghaoi wananchi.

Aliwataka wafanyakazi kushirikiana kufufua uchumi kuongeza uzalishaji na tija na hivyo kujenga uchumi endelevu unaokua na utakaowapa wafanyakazi haki ya kudai mishahara bora zaidi na marupurupu mengine.

Lipumba amponda Mkapa kwa kutoongeza mishahara

Majira Mei 2

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Bw. Ibrahimu Lipumba ameiponda hotuba ya Rais Benjamin Mkapa ya sikukuu ya Mei Mosi akidai haiwasaidii wafanyakazi kwani haikuzungumzia kuongeza mishahara.

Bw. Lipumba alisema hayo jijini jana katika ukumbi wa Jumba la sinema la Starlight jijini wakati akihutubia wanachama wa CUF waliokuwa wakisherekea Mei mosi kwa mkutano ukumbini hapo.

Alisema badala ya Rais Mkapa kuelezea sera za CCM kuhusu uboreshaji wa ajira, aligeuka mbogo akiwalaumu wafanyakazi wanaolalamikia mshahara mdogo na hali ngumu ya uchumi.

Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa kuna tatizo la ajira ambapo watu wanaotafuta kazi ni 700,000 lakini wanaopata kazi ni 20,000 tu na Rais Mkapa hajatumia mbinu zozote kuondoa tatizo hilo.

Pia Bw. Lipumba alisema Tanzania ina watu milioni 17 wenye uwezo wa kufanya kazi lakini walioajiriwa ni watu 137,000 tu, ambao ni chini ya asilimia moja.

"kama anazungumzia (Mkapa) watu wajiajiri, mtu anapomaliza darasa la saba hawezi kujiajiri. Ni lazima aajiriwe ili apate mtaji utakaomsaidia kujiajiri. Kwa hiyo suala la kuajiriwa bado ni muhimu katika mfumo wa serikali ya CCM"

Mwenyekiti CCM ataka anayempinga Mbunge atemewe mate

Majira Mei 2

MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Temeke, Abraham Ole Lukumay amewaonya wanachama na mabalozi wa chama hicho kuacha majungu dhidi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Bw. John Kibaso yanayolenga kukigawa chama.

Alitoa onyo hilo juzi katika hafla ya kutoa mikopo kwa akina mama na vijana wa kata ya Kurasini iliyodaiwa iliyoandaliwa na Mbunge huyo.

Bw. Lukumay aliwataka viongozi hao kuwaelimisha wanachama badala ya kuwagawa kwa kueneza majungu kuwa Mbunge huyo hajafanya kitu chochote.

"Kama mtu anataka kujinadi aeleze atawafanyia nini wananchi na siyo kueleza mwenzake kufanya nini na ameshindwa kufanya kitu gani" alisema.

"Mtu akikwambia Mbunge amenunua benzi (gari la Kibaso) kwa pesa za mikopo mtemee mate usoni kama anakutazama"

Alisema katika chama hicho kuna watu wamevaa ngozi ya kondoo huku ndani wakiwa ni chui.

Komeni kuisakama Serikali yangu - Mkapa

Tanzania Leo: Mei 2

Kinyume na matarajio ya wafanyakazi wengi nchini kwamba serikali ingetangaza angalau ongezeko la mishahara, Rais Benjamin Mkapa alitumia maadhimisho ya Mei Mosi kuwajia juu viongozi wa vyama vya upinzani nchini kutokana na kauli zao kwamba yeye pamoja na serikali yake wameshindwa kuleta maendeleo nchini.

Akihutubia taifa jana kutoka Dodoma katika maadhimisho hayo ambako hakugusia suala la mishahara au nafuu ya maisha, Rais Mkapa alisema kwamba kutokana na ufinyu wa mawazo, akili ndogo na wengine na wengine kutokuwa na mtazamo sahihi, viongozi hao wamekuwa mstari a mbele kupinga kila inalofanya serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Bila kuwataja majina yao, Rais Mkapa aliwashutumu baadhi yaViongozi wa upinzani ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitoa madai mbalimbali katika kupinga juhudi zinazochukuliwa na serikali iliyopo madarakani katika kufufua uchumu wa nchi.

Wafanyakazi wataka migomo irihusiwe

Uhuru: Mei 2

Wafanyakazi wa mkoa wa Dar Es Salaam, wametaka migomo iruhusiwe kazini kwa sababu sheria ya kuzuia migomo imepitwa na w akati ambapo sasa hivi sehemu nyingi za kazi zimebinafsishwa.

Katika risala yao jana kwenye Uwanja wa Taifa kwa mgeni rasmi katika sherehe za Mei Mosi, Waziri Mkuu Fredrick Sumaye, wafanyakazi hao walisema,

"Kifungu cha 11-14, sehemu ya lll ya Sheria ya Mahakama ya Kazi Tanzania namba 41 ya 1967 kinachozuia migomo kinahitaji marekebisho, kwa sababu kilipowekwa kilikuwa sahihi kwa sababu viwanda vilikuwa vyetu tusing eweza kujigomea wenyewe. Sasa hivi sehemu za kazi zimebinafsishwa na zingine zimeanziahwa upya na waajiri. Kwa hali hiyo upo umuhimu wa sheria hii ikaangaliwa upya ili iendane na hali halisi ya wakati tulionao na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii iliyoanza kuinhgia nchini

Wafanyakazi hao pia wameiomba serikali iwaondolee baadhi ya kodi kwa vile zimekuwa mzigo mkubwa ikilinganishwa na kipato wanachokipata.

"Kero nyingine ni tatizo la kodi mbalimbali anazolipa mfanyakazi na kipato kidogo anachopata ambapo kodi peke yake zinachukua robo ya nzima ya mshahara wa mfanyakazi," walisema wafanyakazi hao.