Magazeti Wiki Hii

'Kususia Muungano ni kuwasaliti Watanzania'

BAADHI ya Viongozi wa vyama vya upinzani Jumatano, walihudhuria sherehe za kutimiza miaka 36 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na wakasema kwamba kususia sherehe hizo ni kuwasaliti Watanzania.

Akizungumza jana mara baada ya sherehe hizo, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi, James Mbatia alisema kususia sherehe hizo siyo busara kwa kuwa hiyo ni sehemu pekee ambayo inawakutanisha viongozi na wananachi wa vyama mbalimbali vya siasa.

"Hizi ni sherehe za kutujengea umoja, mtu au Kiongozi anayezisusia haitakii mema jamii ya Watanzania," alisema kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo.

Mbatia alisema kwamba kwa kiongozi wa chama cha upinzani kususia sherehe hizo ni jambo lisiloeleweka kwa vile kiongozi ndiye anatakiwa kuwa mfano kwa wafuasi wake katika kuujenga na kuutetea Muungano.

Kiongozi mwingine aliyehudhuria sherehe hizo ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), profesa Ibrahimu Lipumba ambaye yeye alisema kwamba chama chake kinautambua na kuuthamini Muungano na ndiyo maana yeye alihudhuria kama Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).

Amuua mume wakati akinyemelea mke wake

MTU mmoja Bakari Mohamed (40) anatuhumiwa kumpiga hadi kumuua mume wa mwanamke aliyekuwa anafanya naye mapenzi kwa wizi mjini hapa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, maeneo ya Zavilla alisema tukio hilo lilitokea saa tisa usiku wakati mtuhumiwa alipokuwa amekwenda kumtembelea mwanamke huyo. Fatuma Yassin (32), nyumbani kwake.

Alisema Fatuma ambaye ni mke wa pili wa marehemu, siku hiyo alikuwa na mumuwe, Hashimu Mapunda, na mtuhumiwa bila kujua alikwenda kumtembelea mpenzi wake kama kawaida na alipofika akagonga mlango.

Kamanda Zavalla alisema Mapunda alikwenda kufungua mlango kuona kuna tatizo gani lakini ghafla alishambuliwa na kupigwa hadi kuzimia. ilielezwa kuwa mtuhumiwa alimvuta marehemu na kumtumbukiza katika korongo la mto Mateka ambako alifariki baadaye.

Mtoto mwenye umbo la ajabu

Uhuru Aprili 27

MTOTO wa kiume aliyezaliwa na umbo la ajabu, jumamosi iliyopita ameruhusiwa kuondoka katika hospitali ya Kitete mjini hapa.

Kwa sharti kwamba arejeshwe katika hospitali hiyo mapema Julai mwaka huu, kwa uchunguzi zaidi.

Mtoto huyo aliyezaliwa na mwanamke mmoja aitwaye Marwa Mohamed, akiwa na sura inayoonekana kama ni ya mtu mzima huku mashavu yake yakiwa yamevimba na chini ya kidevu chake kukiwa na uvimbe mkubwa unaomfanya aonekane na umbo la ajabu, alilazwa katika hospitali hiyo Jumatatu wiki hii.

Mjamzito afanyiwa tohara akiwa kwenye uchungu

Mtanzania Aprili 26

MWANAMKE mmoja mjamzito amefanyiwa tohara wakati akijifungua, imeelezwa.

Ofisa Ustawi wa Jamii ya Sekretarieti ya Mkoa wa Singinda Zuhura Karya aliyasema hayo hivi karibuni kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika kwenye kituo cha walimu, mjini hapa.

Zuhura alisema hata akina mama ambao hawajatahiriwa mkoani Singida pia wako kwenye hatari ya kutahiriwa bila ridhaa yao. Alisema kuwa mjamzito huyo aliyekuwa anajifungua alidhani ana uchungu wa kujifungua kumbe wakati huo huo alikuwa anatahiriwa Mwanamke huyo hakutajwa jina.

"Tohara inayofanywa mkoani hapa ni mbaya sana, kwani inafanywa hata kwa watoto wachanga, tofauti na mikoa mingine ambako ni wanawake wenye umri mkubwa ndio wanaotahiriwa," alisema Zuhura na kuongeza kuwa sasa wakati umefika kwa jamii kuelimisha ili kulichukia tendo hilo na kuliacha kabisa.

Kwa mujibu wa Zuhura kuanzia mwaka 1997 hadi Juni 1999, akinamama 41,627 waliofika katika hospitali na zahanati mbalimbali moani hapa kujifungua, 16,866 walikuwa wametahiriwa. Vyombo vinavyotumika kutahiria mkoani hapa ni kucha, vipande vya glasi, nyembe na visu.

Mtu mmoja afa maji baharini

Majira Aprili 27

MKAZI wa Majengo Wilayani Muheza Salim Barabara (16) amekufa katika bahari ya Hindi wilayani Pangani wakati alipokuwa akiogelea.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Bw. Abdallaha Zombe aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 24 mwak ahuu saa 12 jioni wilayani Pangani.

Alisema baada ya kijana huyo kuzama mwili wake haukuweza kupatikana siku ya tukio hadi kesho yake Saa 1 asubuhi ulipoonekana katika eneo la Pangadeko wilayani Pangani.

CUF watofautiana

Uhuru Aprili 27

KUMEJITOKEZA mikanganyiko miongoni mwa viongozi wa kitaifa wa Chama cha CUF ambapo Katibu Mkuu Seif Shariff Hamad alisusia sherehe za Muungano, lakini mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim :Lipumba alihudhuria gwaride rasmi na kueleza kwamba anauheshimu muungano.

Alipoulizwa na Mwandishi wa habari hizo kwa nini amehudhuria sherehe hizo huku Katibu Mkuu wake Hamad alitangaza kutohudhuria alisema "Hii ni sherehe ya kitaifa... CUF inatambua Muungano"

Lipumba alifafanua kwamba suala linalozungumziwa na CUF juu ya Muungano ni mfumo wake na si vinginevyo, na kwamba alikuwa na kila sababu ya kuhudhuria sherehe hizo na kuitikia mwaliko aliopewa.

Mapema juzi Hamad alitangaza kususia maadhimisho ya sherehe za miaka 36 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika jana.

Katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam, Hamad alisema amesusia kushiriki katika maadhimisho hayo kutokana na kupinga unyanyasaji wa polisi dhidi ya raia visiwani.