Make your own free website on Tripod.com

Magazetini Wiki Hii

Nitajiuzulu - Jaji Makame

Mwananchi Juni 8

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Lewis Makame amesema ikithibitika kwamba anakipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) katika utendaji wake ndani ya Tume hiyo, yuko tayari kujiuzulu uenyekiti na ujaji wake.

Jaji Makame pia amesema baadhi ya wananchi wana mawazo kwamba Rais anaweza kumfukuza kazi saa yoyote, kumbe hawajui kwamba hana uwezo huo kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mkutano kati ya tume hiyo na wafadhili uliofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro jijini jana, jaji Makame alisema hapendelei chama chochote cha siasa katika utendaji wake.

"Kukiwa na ushahidi kwamba napendelea CCM, nitajiuzulu si uenyekiti pekee, bali hata ujaji" alisema jaji Makame na kuongeza kuwa wananchi wanadhani kwamba anaipendelea CCM kwa sababu chama hicho hakilalamiki kupitia vyombo vya habari.

"Wanadhani sisi ni marafiki sana wa Serikali, lakini ukweli ni kwamba serikali haifurahishwi na utendaji wetu," alisema mwenyekiti huyo na kuwataka watu wenye mawazo kwamba NEC inakipendelea chama tawala na serikali yake wakasome ripoti ya Tume hiyo baada ya uchaguzi mwaka 1995.

Leo ndio leo Dodoma

Mtanzania Juni9

MGOMBEA wa Kiti cha Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia CCM anatarajiwa kufahamika leo baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri Kuu NEC ya Chama hicho mjini hapa.

Kutangazwa kwa jina la mwanachama atakayewakilisha chama hicho kunahitimisha pilikapilika za wagombea wanne wa nafasi hiyo.

Mapema wiki hii Kamti Kuu ya CCM (CC) katika kikao chake mjini Dar es Salaam ilipitisha majina yote manne ya wanachama wanaowania nafasi hiyo.

Hao ni wanawake pekee Waziri wa Fedha wa SMZ Amina Salaum Ali, Waziri Kiongozi wa SMZ Dk. Mohamed Gharib Bial, Waziri wa uchukuzi na Mawasiliano Amana Abeid Karume na Naibu Waziri wa Fedha wa Jamuhuri ya Muungano Abdisalam Issa Khatib.

Bodi ya Bima ya Afya yazinduliwa

Mtanzania Juni 9

WAZIRI wa Afya Dk. Aron Chiduo amewataka wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa Watumishi wa Serikali, kutotumia tofauti zao kuzusha mivutano na migogoro ya utendaji ndani ya Bodi.

Dk. Chiduo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizindua bodi hiyo inayojumuisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali kwenye sherehe zilizofanyika katika ukumi wa Hoteli Karibu Dar es Salaam.

"Tofauti zinazowakilishwa na wajumbe wa Bodi hii zisiwe chanzo cha mivutano na migogoro ya utendaji ndani ya bodi" alionya Chiduo na kuongeza kwamba tofauti hizo zitumike katika kuanzisha mijadala yenye kutoa mapendekezo ya manufaa kwa taasisi zote zinazowakilishwa katika Bodi hiyo.

Bodi hiyo inawajumuisha wajumbe kutoka vyama vya wafanyakazi taasisi ya Bima wanasheria wenye hospitali binafsi na watumishi wa Wizara ya Afya.