Make your own free website on Tripod.com

Magazetini Wiki Hii

He! Watu wanywa gongo uchi Dar!

Mwananchi Mei,29

ENEO la bonde la Dambweni lililopo Yombo Vituka wilayani Temeke mkoa wa Dar es Salaam, limegeuzwa kuwa eneo la kufanyia ufuska na uzalishaji wa maelfu ya lita za pombe haramu ya gongo ambapo wanywaji hunywa wakiwa uchi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa pombe hiyo haramu imekuwa ikiazisha kwa kutumia mitambo zaidi 20 iliyopo katika eneo hilo kwa muda mrefu bila vyombo vya dola kuchukua hatua.

Wanywaji hao pamoja na watengenezaji wa pombe mara nyingi wanalazimika kuvua nguo zao na kubaki na nguo za ndani kutokana na joto kali la moto unaotumika kuendesha mitambo hiyo ya gongo lililotanda katika eneo lote.

Mmoja wa wanywaji katika eneo hilo (jina tunalihifadhi) aliliiambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa wapika gongo wa eneo hilo wameweka ulinzi madhubuti kuhakikisha kuwa hawakamatwi na vyombo vya dola.

CUF sasa yadai Mahita muuaji

Mwananchi Mei 31,

MAMBO yanaweza kumgeuka Inspekta Jenerali wa Polisi, Omar Mahita, baada ya Chama cha Wananchi CUF kuanza kukusanya saini za hiari za askari polisi waliotumika kuwapiga raia huko Zanzibar na ambao wako tayari kueleza kwamba walilazimishwa kufanya hivyo na makamanda wao.

Aidha, Chama hicho kimesema Inspekta Jenerali wa Polisi Omar Mahita amehusika moja kwa moja na kifo cha Suleiman Said Khalfan na kama anataka kupambana, apambane na familia ya marehemu wala siyo chama hicho.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Mohamed Ally Yusuph, alisema jana kuwa chama hicho kimesambaza kwa mashirika ya haki za binadamu ripoti ya miezi mitatu inayoonyesha hali ya vipigo ilivyokuwa Zanzibar.

Kiongozi huyo alisema hata mara moja CUF haijawahi kusema kwamba inamshitaki Mahita, isipokuwa chama hicho kilisema kwamba kinazisaidia familia za ndugu walioathirika. "Sisi tumesema wapi kwamba tutamshitaki?Tulieleza wazi kuzisaidia familia zilizoathirika na vipigo vya askari polisi baada ya kuhimizwa na Mahita kupiga watu na hasa wafuasi wa CUF" alisema Ally Yusuph.

Maalim Seif amkalisha 'kitimoto' Mzee Ruska

Majira Mei 30

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedai kuwa kauli iliyotolewa naRais Mstaafu Alahaji Ali Hassani Mwinyi kuwa kutatokea mgawanyiko katika Muungano iwapo chama hicho kitashinda uchaguzi Zanzibar ni ya kujikomboa na kuonesha kupuuza sheria ya vyama vya siasa nchini.

Aidha CUF imedai kuwa kauli hiyo ya Alhaji Mwinyi inaonesha kukiuka maadili ya uongozi na kuelekeza mawazo yake kama kiongozi aliyeamua kupitisha sheria hiyo ili kulinda maslahi ya CCM.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Makao Makuu ya chama hicho Bunguruni jijini Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa CUF ilikuwa ikidhani kuwa Alhaji Mwinyi anaweza kutetea sheria hiyo kwa kusisitiza uchaguzi huru na wa haki.

Alisema CUF inadhani kuwa heshima aliyoipata katika kipindi chote kirefu kama kiongozi mwadilifu nchini inaonekana kutaka kufikia mwisho hivyo kumtaka aache kujifanya hakimu katika masuala yanayowahusu watu wengi nchini.

Mahita kushitakiwa na familia 50

Tanzania Leo Mei 31

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kwamba mashitaka dhidi ya Inspekta Jenerali wa polisi, Omari Mahita yako pale pale na yatafunguliwa na familia 50 za wana CCM na CUF walioathirika na operesheni ya polisi visiwani.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Mohammed Ali Yussuf alisema mjini hapa jana kwamba kinachofanyika sasa ni kukusanya vielelezo na ushahidi ili kuwezesha kumshitaki Mahita.

Watu Kumi wafa ajalini

Mtanzania Juni 2

WATU kumi walikufa jana asubuhi na wengine 38 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka katika eneo la Ruanda Mkoani humu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Laurian Sanya alisema jana kwamba ajali hiyo ilihusisha basi la Air Shengena lenye namba za usajili TZL 5164, lililokuwa likisafiri kutoka Mbeya kwenda Sumbawanga mkoani Rukwa.

Alisema ajali hiyo iliyotokea jana asubuhi, ilitokana na mwendo wa kasi, Miongoni mwa maiti hao sita walikufa papo hapo.

Maiti nne za watu za watu waliokufa katika ajali hiyo ikiwamo ya Mmarekani mmoja zilikuwa zimetambuliwa hadi ilipofika jana jioni.

Wananchi wamechoshwa na CCM - Lipumba

Majira Juni 1

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema wananchi wamechoshwa na utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Profesa Lipumba alidai kuwa kwa miaka 40 ya utawala wa CCM, imeshindwa kushughulikia kero za wananchi.

Profesa Lipumba alisema Watanzania wengi hasa vijijini wameendelea kuwa maskini wajinga na wenye kuandamwa na maradhi ambapo kipato chao ni kidogo kuweza kumudu maisha bora.

alikuwa anazungumzia mambo waliyoyagundua wakati wa ziara yao katika mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro ambapo alisema walikuwa wakiwahimiza wananchi kuachana na CCM na kuchagua chama kingine ambacho kitaweza kutatua matatizo sugu waliyonayo.

"Kuendelea kukumbatia CCM ni kuendelea kukumbatia Umaskini, maradhi na Ujinga," alisema Profesa Lipumba kuwa ndiyo msimamo wa CUF.

Mganga Kortini kwa kubaka na kunajisi

Majira Juni 2

MGANGA wa Zahanati ya Nyamakula iliyo kwenye kijiji cha Nyamkula Kata ya Nyakisasa Tarafa ya Rulenge wilayani Ngara Richard Kaunua anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kubaka na kumnajisi mtoto mdogo msichana mwenye umri wa miaka 2.

Kamanda polisi Mkoa wa Kagera Bw. Elihuko elihaki alsema juzi kuwa mganga huyo anatuhumiwa kutenda kitendo hicho mei 29 mwaka huu saa 12 jioni.

Bw. Elihaki aliongeza kuwa mtuhumiwa alimnajisi mtoto huyo akiwa nyumbani kwake na kufafanua kuwa mtoto alikuwa anacheza karibu na nyumba yake ndipo alipomwingiza ndani ya chumba chake na kumfanyia kitendo hicho.

Kamanda alifafanua kuwa mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika