Make your own free website on Tripod.com

Magazetini Wiki Hii

Lamwai arejea CCM

Majira Mei 22

KIONGOZI wa zamani wa Chama cha NCCR - Mageuzi , Dk. Masumbuko Lamwai, jana alirejea katika chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkutano maalum wa chama hicho jijini wa kumpongeza Rais Benjamin Mkapa kwa kurudisha fomu za kugombea urais.

Katika mkutano huo uliofanyika uwanja wa ndani wa Taifa.Dk. Lamwai alimwomba Rais Mkapa amsamehe kwa kitendo chake cha kuihama CCM na kujiunga na upinzani.

"Lengo langu la kujiunga na upinzani lilikuwa kuunda hoja ili kuleta upinzani na Chama cha Mapinduzi miaka yangu minne na nusu niliyokaa upinzani nimegundua kuwa Mkapa ni kiongozi madhubuti" alisema Dk.Lamwai

CUF itashinda Zanzibar - Seif

Majira Mei 22

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bw.Seif Sharif Hamad ameapa kwamba iwe isiwe Serikali ya Zanzibar itaongozwa na CUF baaa ya uchaguzi Mkuu ujao.

Bw. Seif alisema hayo wakati akihutubia maelfu ya wana CUF katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa pia na polisi wengi baadhi wakiwa na silaha.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Malindi Bw. Seif aliwaambia wana CUF kwamba hakuna kitakachozuia CUF kuchukua ungozi wa nchi, kwani njama zinazopangwa na CCM zinajulikana.

Wanaowania Ubunge ruska 'kijipitisha pitisha'- CCM

Nipashe Mei 25

KATIBU Mkuu wa CCM Bw. Phillip Mangula, ametangaza kwamba ni ruksa kwa wana CCM wanaowania Ubunge kujitambulisha kwa wapiga kura lakini ni mwiko kabisa kufanya kampeni na tafrija.

Hali kadhalika amewakumbusha wale wenye shauku ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM kwamba muda wa kuchukua na kurejesha fomo umekwisha.Bw. Mangula alisema hayo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo ya makao makuu Lumumba jijini jana.

"Muda wa kuchukua na kurejesha fomu za urais umekwisha". alisema Bw. Mangula ikiwa ni siku moja tu baada ya mwana CCM mmoja Nassoro Abdallah Mtime, kudai atachukua fomu kupambana na Rais Benjamin Mkapa kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Bob Makani adai, mimi pia CCM wamenifuata lakini sijiungi nao

Mtanzania Mei 23

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bob, Makani, amedai kwamba amekuwa akifuatwa na kushawishiwa kujiunga na CCM kwa ahadi kwamba atapewa wadhifa na chama hicho.

Makani aliyasema hayo jana, makao makuu ya chama hicho, Kinondoni Dar es Salaam mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Medard Mutungi.

"Mkapa anaogopa uchaguzi wa huru na haki kwa kuwa anafahamu kwamba atashindwa... hivi sasa wameanza kuwaendea viongozi na kuwapa ahadi lukuki wahamie CCM.

"Mimi mwenyewe wamenijia na kunishawishi nijiunge na CCM na kuniahidi kwamba nitapewa wadhifa" alidai Makani hali akikataa kumtaja aliyemfuata na kumshawishi.

Viongozi wa upinzani wamponda Dk. Lamwai

Mtanzania, Mei 23

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bob Makani amesema Dk. Lamwai ambaye juzi amerejea CCM si mwanasiasa mzito kama ilivyoelezwa na chama hicho bali CCM inapokea makapi na watu walichoka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, makao makuu ya CHADEMA Kinondoni Dar es Salaam, baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho Makani alisema Dk. Lamwai si ngome ya siasa nchini na wananchi katika jimbo lake walimkataa.

Dk. Lamwai ambaye hivi karibuni alitangaza kujiuzulu kutoka chama cha NNCR-Mageuzi juzi alijiunga na CCM. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 Dk. Lamwai kupitia NCCR-Mageuzi alishinda na kuwa Mbunge wa jimbo la Ubungo, hata hivyo ushindi huo ulitenguliwa na mahakama.

Wafadhili wamkalisha Mkapa Kiti moto

WAFADHILI katika hali isiyotegemewa, jana walimkalisha kiti moto Rais Benjamin Mkapa na kumtaka ashughulikie mgogoro wa Zanzibar kabla ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

"Kwa nguvu ulizonazo kama Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inakulazimu kushughulikia mgogoro wa zanzibar ili kurejesha amani visiwani humo" hiyo ilikuwa ni kauli ya Mshauri wa Norway katika masuala ya Afrika Bw. Kjell Harald Dalen.

Bw. Dalen alitoa kauli hiyo wakati wajumbe wa nchi wahisani wakichangia mjadala kwenye mkutano wa Mashauriano baina ya serikali na wafadhili (CG) katika hoteli ya Sheratoni jijini jana.

...Licha ya kujigamba kugharamia uchaguzi, awaangukia wafadhili

Majira Mei 25

BAADA ya Rais Benjamin Mkapa kujipiga kifua kuwa serikali yake mwaka huu itagharamia uchaguzi mkuu, ili kutondokana na shinikizo la wafadhili wa kimataifa, jana alitafuna maneno yake na kuwasilisha rasmi ombi la kusaidiwa kwa wafadhili hao.

Rais aliyasema hayo jana katika Hoteli ya Sheraton jijini wakati akifungua mkutano na wafadhili uliofanyika jijini ambao pamoja na mamabo mengine unaangalia jinsi Tanzania inavyoshughulikia masuala ya uchumi na kujikwamua na umaskini.

"Mpaka sasa ni wafadhili wanane wamonesha nia ya kuisaida kama dola za Marekani milioni nane kwa ajili ya uchanguzi, lakini bado kapu tupu. Kwa hiyo nawaomba wengine wajitokeze kusaidia" alisema Rais Mkapa.Alisema kuwa gharama kwa ajili ya uchaguzi huo ni zaidi ya sh.billioni 32 (dola za kimarekani milioni 40)

Wakurugenzi watatu wasimamishwa kazi PPF

Mtanzania Mei 26

WAKURUGENZI watatu wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), wamesimamishwa kazi kuanzia juzi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa sababu za kikazi.

Wakurugenzi ambao wamesimamishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, Freeman Malya Mkurugenzi wa Fedha juma Muhimbi na Mkurugenzi wa Mipango, Edward Chiombola.

Viongozi wote hao waliosimamishwa walikuwa wakichunguzwa na Tasisi ya kuzuia Rushwa (PCB) kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinawakabili maofisa wa mfuko huo.

Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala aliyejitambulisha kwa jina la D.Magwiza alithibitisha kusimamishwa kazi kwa maofisa hao jana, ingawa alikataa kuingia kwa undani juu ya suala hilo kwa madai kwamba yeye si msemaji wa shirika.