Magazeti Wiki Hii

Wadaiwa kugawana sanda ya marehemu

Uhuru Aprili 5:

SANDA aliyovishwa maiti iliyoporwa baada ya gari lililokuwa likisafirisha maiti hiyo kupinduka katika eneo la Isongole mkoani Mbeya inadaiwa waligawana watu waliopora na wengine kuuziwa ili kutengeneza vizimba.

Habari zilizopatika hapa zinasema kuwa mali zote ziliporwa katika ajali hiyo ambapo mjukuu wa marehemu aliyekuwa akisafirishwa. Nehemia Mwakatobe na utingo wa gari lililopata ajali walikufa papo hapo na wasindikizaji 24 kujeruhiwa zilikuwa zimerejeshwa hadi jana.

Habari zilizopatikana pia zinasema kuwa kati ya vitu hivyo sanda ambayo ilivuliwa toka kwa maiti haikuweza kupatikana kwa kuwa ilichanwa vipande vipande kugawanywa miongoni mwa watu waliopora na kuipeleka kwa mganga wa jadi ili kutengeneza vizimba vya kuwasaidia kutokamatwa wanapofanya uhalifu hasa wa uporaji na mauaji.

Moto wawaka Zanzibar

Majira Aprili 4:

HALI ya kisiasa visiwani hapa inazidi kuzorota ambapo Polisi watatu wamejeruhiwa katika mapambano na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Wakati Polisi hao wamelazwa Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini hapa Katibu Mkuu wa CUF Bwana Seif Shariff Hamad jana alikamatwa na polisi na kuachiwa kufuatia vurugu hizo.

Bw. Hamad alikamatwa pamoja na wanachama watatu wa CUF, Katibu Msaidizi wake Bw. Jusa Ladhu na walinzi wa Bwana Hamad wawili Bw. Rashid Dadi na Bwana Hamisi Haji.

Bw. Hamad alikamatwa saa 11:40 mara baada ya kuahirishwa kwa kesi ya uhaini iliyowakabili wanachama 18 wa CUF iliyokuwa itolewe uamuzi wa ama kutoa dhamana au la kwa wanachama hao ambao wamekuwa ndani kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Wote walikamatwa na polisi wakishirikiana na Maofisa wa Usalama wa Taifa na kuwapakia kwenye gari la polisi namba STJ 6443, aina ya Land Rover.

Kiongozi huyo ambaye kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 aliwania kiti cha Urais wa Zanzibar na kushindwa na Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour kwa asilimilia 0.4 ya kura zote, inadaiwa kuwa leo atafikishwa kizimbani kujibu shitaka la kujeruhi na kupora silaha.

‘Ningekuwa CCM ningedundana na Mangula’

Majira Aprili 6

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha kutetea Haki za binadamu nchi (LHRC), Bi. Hellen Kijo - Bisimba amesema angekuwa mwanachama wa CCM angeshikana mashati na Katibu Mkuu wa Chama hicho Bwana Philip Mangula kwa kuwadhalilisha wanawake.

Bibi Kijo- Bisimba alitoa kauli hiyo juzi jijini wakati akitoa mada katika Semina ya Haki za Binadamu kwa mahakimu wa mahakama za mwanzo ambapo alisema kauli ya Bwana Mangula kuwa CCM haitaki kuwa na mgombea urais mwanamke inakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu kwamba kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Alisema vitu vingine vilivyomkera kwenye kauli hiyo ni ubaguzi dhidi ya wanawake na kwamba kauli hiyo inawadhalilisha wanawake.

Mbunge afariki dunia

Majira Aprili 6

MBUNGE wa Liwale (CCM) Bw. Salum Hemed Ngajulage (53) amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo katika nyumba ya kulala wageni ya Kilamia mjini hapa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Dk. Zainabu Chaula alisema kuwa marehemu amethibitika kufa kwa ungonjwa wa moyo baada ya maiti yake kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Mkoa.

Dk. Chaula alisema matatizo hayo yalianza kumpata Marehemu tangu Aprili mwaka jana.

Kaimu Mganga Mkuu huyo alisema kuwa uchunguzi umeonesha marehemu alikuwa na tatizo katika mishipa inayopelekea damu kwenye moyo ambayo ilikuwa midogo kuliko kawaida.

Wahudumu wa nyumba aliyofikia walisema kuwa Marehemu Ngajulage hakuwa na matatizo hadi kufikia saa 6:00 usiku wa kuamkia jana alipokwenda kwenye chumba chake kulala.

Hata hivyo gari linalowapeleka wabunge bungeni lilipopita kwenye nyumba hiyo Saa 2:30 asubuhi jana, hakukuwa na dalili kuwa alikuwa akijiandaa kuhudhuria kikao hicho, jambo lililosababisha hisia kuwa alikuwa bado amelala. Wahudumu wa nyumba hiyo walimweleza dereva anayewaendesha wabunge kuwa huenda Bwana Ngajulage alikuwa amelala.

Kakobe amtishia Nchimbi

Mtanzania Aprili 5:

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Zakaria Kakobe amemtisha Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, Emanuel Nchimbi na kumpa muda wa wiki moja ili ‘atubu dhambi’ ya kumfananisha na kiongozi wa kikundi cha kidini ambacho mamia ya wafuasi wake walikufa kwa moto nchini Uganda Joseph Kibwetere.

Alisema katika kipindi hicho kama Nchimbi hataomba toba yake Mungu atamwonyesha tofauti kati yake na Kibwetere na kumfanya awe fundisho kwa watu wengine.

Kakobe alisema kuwa kwa kuitwa Kibwetere hakukashifiwa yeye, bali Mungu aliyemchagua na kumweka katika utumishi wake.

"Kwa taarifa hii ninampa Emmanuel Nchimbi siku saba za kutubu dhambi hii. Kama toba haitanifikia kitika muda huo kuanzia leo (jana) Mungu wangu atamwonyesha tofauti yangu na Kibwetere", ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kibwetere ni kiongozi wa kanisa la kurejesha amri kumi za Mungu nchini Uganda ambaye anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya waumini wa kanisa lake zaidi ya 1,000 machi 17 mwaka huu.

Hatua hiyo ya Kakobe ya kumtaka Nchimbi kutubu inafuatia kauli aliyoitoa juzi kwenye vyombo vya habari kuwa Kakobe anakoelekea anaweza kufikia hatua ya kuwachoma moto waumini wake.

Wiki iliyopita Kakobe alinukuliwa katika gazeti la RAI toleo la Machi 30-Aprili 5 akikiri kuvunja ndoa za Waislamu, hasa wanaume ambao walikuwa dini ya Kiislamu, lakini wakaamua kujiunga kanisa lake.

Alisema kuwa matamshi hayo ya Kakobe yanaweza kuhatarisha amani iwapo Waislamu wataamua kuchukua hatua dhidi ya vitendo vinavyofanywa na askofu huyo

Polisi wasaka wafuasi wa kanisa la Uganda nchini

Tanzania Leo Aprili 7:

Jeshi la Polisi nchini linafanya uchunguzi wa kina ili kuwanasa na kuwachukulia hatua za kisheria watu walioanzisha nchini tawi la Kanisa lililoua mamia ya waumini wake huko Kanungu Uganda.

Sambamba na hatua hiyo, Polisi nchini pia wanatafuta idadi kamili ya Watanzania waliokufa kwa kuungaua moto katika madhehebu ya Kanisa la Kurejesha Amri Kumi za Mungu huko Kanungu, Magharibi mwa Uganda hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Adadi Rajabu aliliambia Tanzania Leo wiki hii kuwa serikali imeamua kulivalia njuga suala la kuwasaka na kuwanasa viongozi walioanzisha tawi la Kanisa hilo hapa nchini.