Magazeti Wiki Hii

Vijana Zanzibar washinda juu ya dari kukwepa Polisi

Nipashe Aprili 10:

BAADHI ya vijana wanalazimika kushinda juu ya dari za nyumba zao kuhofia mkong’oto wa polisi katika zoezi la kamata kamata linaloendelea.

Uchunguzi wa PST ulionyesha kwamba tangu juzi hadi jana, polisi walikuwa wakiendesha msako wa nyumba hadi nyumba katika mitaa mbalimbali ya mjini hapa.

Katika tukio moja, kijana mmoja Ali Kidishi, aliteremshwa na polisi kutoka juu ya dari la nyumba yake katika eneo la Mwanakwerekwe A..

Polisi walifika katika eneo hilo ili kupekua nyumba za wanachama wa chama cha upinzani cha CUF na ofisi za chama hicho.

Pia, katika eneo hilo, polisi walivamia kituo cha kufundishia mchezo wa Judo saa 11:00 jioni na kuwafurumusha watu waliokuwepo hapo.

Katibu wa CUF tawi la Mwanakwerekwe A, Bw. Shaibu Amabr Khamis, alisema askari hao wamekuwa wakiingia katika kila nyumba kuwakamata baadhi ya watu na kuwapiga.

Ongezeko la watu toka Bara lazorotesha huduma Z'bar - Waziri

Nipashe Aprili 10:

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Bw. Mohamed Hashim Ismail, amesema ongezeko la watu kutoka Tanzania Bara kuja Visiwani, limechangia kuzorotesha huduma za kijamii Zanzibar.

Aliseama hayo wakati akichangia mjadala wa Sera ya Ongezeko la Idadi Watu Zanzibar, uliokuwa umeandaliwa na Wizara ya Nchi na Vitega Uchumi katika hoteli ya Bwawani.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inashindwa kutoa huduma za kijamii kama vile maji, madawa na elimu, kutokana na kuwepo wahamiaji wengi kutoka Bara.

Waziri huyo ameshauri kuanzishwa kwa utaratibu wa hati za kusafiria yaani pasipoti kwa watu kutoka Tanzania Bara kuingia Visiwani kama ilivyokuwa awali.

Alisema bila kuchukuliwa hatua hiyo, huduma za kijamii Zanzibar haziwezi kuboreshwa, kwa sababu bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inaelemewa na mzigo wa watu.

Polisi wanafunzi 200 watimuliwa

Nipashe Aprili 12:

MKUU wa Chuo Cha Polisi Moshi (CCP) Samwel Masatu amewafukuza masomo askari wanafunzi (kuruta) ziidi ya 200 kutoka Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Habari kutoka CCP zinasema kuwa kufukuzwa kwa askari hao kutokana na kutokuwa kwao na sifa za kujiunga na jeshi hilo.

Habari zilizothibitishwa na maofisa wa CCP na Mkuu wa wilaya ya Moshi, Bw. Henry Clemence Orauya, zimesema kuwa waliofukuzwa ni pamoja na wale ambao hawakupitishwa na kamati za ulinzi na usalama katika ngazi za wilaya hadi Mkoa.

Wengine waliofukuzwa ni wale waliogundulika kuwa na michoro mwilini kama vile nge na tandu,vijana wafupi na ambao majina yao hayakuwepo katika orodha za makamanda wao wa mikoa. Kwa upande wa vijana wa Arusha imeelezwa kuwa vijana ambao hawakuwasiliana na Kamanda wa Mkoa huo, Bw. Juma Ng'wanang'waka. "Kwa kweli habari hizo za kufukuzwa wanafunzi hata sisi tumezisikia kama ulivyosikia wewe, kama unahitaji ukweli mwone kamanda wa chuo au mkuu wa chuo... lakini mimi kama mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama tuliendesha usaili barabara na kukabidhi kunakohusika" alisema Bw. Orauya.

Waziri asema Uongo

Alasiri Aprili 13

KAULI ya Naibu Waziri wa Kazi na maendeleo ya Vijama, Mheshimiwa Williamu Lukuvi kwamba Dar es Salaam hivi sasa haina ombaomba, leo imewafanya waheshimiwa wenzake wamgongee meza na kumpigia kelele za 'ahaaahaa' ambazo mara nyingi hutolewa wakati mtu anapoboronga ama kutoa maelezo ya uongo Bungeni.

Mheshimiwa Lukuvi ambaye alikuwa akijibu swali lililomtaka kuelezea mpango wa wizara kuhakikisha ombaomba hawarejei tena jijini akasema zoezi lililopita liliwafagia wote na hivi sasa Dar hakuna hata mmoja. Baada ya kauli hiyo wabunge wakagonga meza na kutoa sauti za 'aaahaahaa' kuonyesha kuwa analolieleza Bunge si la kweli. Hata Mheshimiwa Lukuvi akaendelea kujikanyaga na kusema ni kweli ombaomba wameondoka wote na hatarejea tena Dar es Salaam

Wabunge wa CCM, Upinzani wataka Chenge ajiuzulu

Mtanzania Aprili 13,

Mtanzania Aprili 13,

BAADHI ya wabunge wa CCM, wameungana na wale wa upinzani kumtaka Mwanasheria Mkuu Adrew Chenge ajiuzulu au awajibishwe kwa kubadilisha sheria bila kushirikisha bunge.

Wakichangia taarifa ya kamati ya Bunge ya mambo ya Katiba na Sheria juu ya masahihisho yasiyo halali ya sheria namba 23 ya 1997, bungeni jana wabunge hao walisema hatua hiyo ni kuingilia mamlaka ya Bunge na kuichezea Katiba.

Sheria namba 23 ya 1997 inahusu muundo mpya wa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara, mali na madeni yake (The National Bank of Commerce Reorganisation and Vesting of Assets and Liabilities) iliyotumika kuigawanya benki hiyo katika NBC (1997) Ltd. NMB na NBC Holding Corporation.

Akiwasilisha taarifa hiyo bungeni Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Katiba na Sheria, Arcado Ntagazwa alisema ya kuwa baada ya sheria kuwa baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge masahihisho ya kifungu cha 6 (1) (b) ya sheria hiyo yalifanywa na mwandishi mkuu wa sheria za Bunge akidai kuwa,amepewa maelezo kutoka serikali.

Ubadhilifu wazidi kukithiri serikalini - Cheyo

Majira Aprili 14:

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Bw. John Cheyo, amesema serikalli imeendelea kuvunja kanuni za matumizi ya fedha za umma ambapo sh. bilioni 45.828 katika Mwaka wa Fedha1997/98 zilitumiwa ama bila nyaraka au kwa nyaraka pungufu.

Akiwasilisha taarifa ya PAC kuhusu hesabu za Serikali Kuu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha unaishia Juni 30, 1998 bungeni jana, Bw. Cheyo alisema kiasi hicho kimeongezeka kutoka sh. bilioni 31.681 kilichoripotiwa mwaka wa fesha 1996/1997