KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 29:

Kanisa lahimiza wanawake nao kuchaguliwa

l Lasema ni waadilifu na wachapakazi, latoa mfano wa WAWATA

Na Dalphina Rubyema, aliyerejea toka Iringa

KANISA Katoliki Jimbo la Iringa, limesema kuwa umefika wakati wa jamii kuachana na mawazo yasiyofaa kwamba mwanamke hawezi kuongoza na katika kuonesha kukomaa kimawazo, wananchi wametakiwa kuwapa kura wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Askofu wa jimbo hilo la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jimboni kwake.

Alisema kuwa wanawake ni viongozi wazuri wakipata uongozi na ushirikiano mzuri.

"Wanaijali jamii ipasavyo tofauti na mawazo ya watu walio wengi kwamba mwanamke hawezi kuongoza,".

Askofu Ngalalekumtwa alitoa mfano wa chama cha Kitume cha Wanawake Tanzania (WAWATA) kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa kwa kazi nzuri wanayoifanya.

"WAWATA ni mfano mzuri sana wa uongozi mzuri wa wanawake kama kuna shughuli yoyote kuanzia ngazi ya jumuiya hadi Taifa lazima WAWATA itume ujumbe hata kama shughuli hiyo inafanyika mbali kiasi gani na huo ujumbe wa WAWATA unakuwa na mchango mkubwa" alisema.

Alitoa mfano mwingine wa umuhimu wa WAWATA kuwa ni ule wa kukubali kwa roho nyeupe kuwa walezi wa Seminari Ndogo ya Visiga.

"WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam ndio walezi wa Seminari ndogo ya Visiga iliyopo jimboni humo, wanatoa vitu vya mamilioni mwaka hadi mwaka kwa ajili ya seminari hiyo" alisema.

Aliongeza, "Hata WAWATA wa jimbo langu ni kiungo muhimu sana, utendaji wao wa kazi ni wa kuridhisha hata kama nina sherehe yoyote wao hunisaidia kimawazo na kiutendaji."

Mhashamu Ngalalekumtwa alisema wanawake wana moyo wa upendo huruma na haki katika utendaji wao wa kazi na uongozaji wa ujumla.

Oktoba 29, mwaka huu, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Pili katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi.

Viongozi mbalimbali wakiwamo wa kiroho wamekuwa wakisistiza sana wananchi kujutokeza siku hiyo ili kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaofaa.

Mama mwenye UKIMWI aomba asaidiwe kutunza watoto

lAsema mmoja ana ugonjwa wa kifafa, mwingine ana ugonjwa wa akili

Na Mwandishi Wetu

BIBI Juli Dominic (52) mkazi wa Magomeni Kota jijini Dar-Es-Salaam, ameomba msaada wa hali na mali kutoka kwa wasamaria wema ndani na nje ya nchi, wa kuweza kumsadia kuendesha maisha yake na watoto wawili.

Bi. Dominic ambaye amekuwa akiishi na virusi vya UKIMWI kwa takribani miaka 16 sasa ana watoto wawili wa kiume wenye matatizo ambapo wa kwanza mwenye umri wa miaka 35 anakabiliwa na ugonjwa wa kifafa na yule wa pili (20) anakabiliwa na tatizo la ugonjwa wa akili.

Akizungumza na gazeti hili kwenye ofisi za kituo kimoja kilicho chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, kinachoshughulikia huduma za kimwili na kiroho kwa waathirika wa UKIMWI, cha UPENDANO maarufu kwa jina la PASADA, alisema yeye na familia yake wanaishi kwa taabu mno wakikabiliwa na tatizo la lishe duni hivyo wanaomba msaada kwa mtu au kikundi chochote chenye mapenzi mema ili kuwasaidia kukabiliana na tatizo hilo.

"Afya yangu ni kama unavyoniona. Wanangu wananitegemea kwa kila kitu na tatizo kubwa ni chakula. Kama unavyojua wenye ugonjwa huu(Ukimwi), tunatakiwa kupata lishe bora, sasa mimi ninayepata mlo mmoja kwa siku au siku nyingine nisiupate, si nitakufa!

Nikifa mimi, si hata wanangu watakufa vile vile! Nani atakuwa tayari kuwasaidia?" alihoji kwa uchungu Bi. Dominic huku akikataa kutaja majina ya watoto hao.

Akaongeza, "Naomba Mungu aendelee kunilinda maana nawaonea huruma sana watoto wangu. Japo wana matatizo yao, sijawachoka na sitathubutu kuwachoka ama kukata tamaa kuwatunza."

Mwanamke huyo ambaye anaishi kwenye kota za Tume ya Jiji nyumba namba 510 mkabala na Kanisa la Anglikana Magomeni, ameomba kujengewa walau kibanda cha kumsitiri na wanae pamoja na kupatiwa mtaji wa sh. 225,000/= ili auze walau mkaa na kujipatia matumizi ya siku.

"Nikipata shilingi 225,000 hata kama ni kuuza mkaa ili angalau nipate lishe, nitauza," alisema.

Ameomba pia msaada wa shilingi 200,000 kwa ajili ya kumfanyia operesheni mwanawe wa kwanza anayesumbuliwa na uvimbe tumboni kwani anadai madaktari wamekwisha tahadharisha kuwa uvimbe huo ukipasukia tumboni, mwanae huyo atafariki.

Akieleza kwa masikitiko jinsi alivyopata ugonjwa huo hatari wa Ukimwi, Bi Dominic anaanza kusimulia:_

"Nilikuwa muathirika wa ugonjwa huu tangu mwaka 1984, nilikuwa na tezi kwenye fuko la uzazi na daktari alinishauri nisifanye operesheni lakini kabla ya kufanya upasuaji huo, walitaka nilete ndugu wa kunitolea damu."

Alitulia kidogo kisha akaongeza, "Maskini ningejua kwamba nitapata maumivu na mateso zaidi ya yale ya mwanzo hata huyo ndugu yangu ambaye alijitolea kunipa damu nisingekubali.

Nisingekubali kabisa kuwekewa damu ya mtu mwingine."

"Mtoto wa dada yangu alijitolea kunipa damu lakini kumbe tayari alikuwa kaisha athirika na UKIMWI hivyo nami baada ya kuwekewa damu hiyo ndiyo nikawa nimeathirika. Nikaingia kwenye mtego usio wangu.

Hata hivyo naomba Mungu amlaze pema peponi huyo aliyenipa damu maana, najua hakutaka kuniua bali alitaka kunisaidia. Yeye aliaga dunia mwaka 1985. Nami nilikuja kubainika nina virusi mwaka 1987. Damu yenyewe niliwekewa mwaka 1984," alisema.

Hata hivyo Bi.Dominic alisema kuwa kinachomsaidia ni kufuata ushauri wa madaktari na alisema kama angekuwa na lishe nzuri hivi sasa angekuwa na afya ya kuridhisha.

Hivi sasa anaendelea kutumia madawa ya Wachina ambayo hupata bure toka kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Anaomba yeyote mwenye nia ya kumsaidia, aulizie kupitia maelezo hayo yaliyotolewa ili kumpata.

Padre atamani viongozi, wagombea wahojiwe kama kweli wanatii viapo

lAICT, Kanisa Katoliki yatamani Rais anayelijua Neno la Mungu

Steven Mchongi, Mwanza na Peter Dominic Dar es Salaam

WAKATI Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT, Dayosisi ya Mwanza, amewataka Watanzania kumchagua Rais Mcha-Mungu, anayetambua uhuru wa kuabudu na mwenye uchungu kwa anaowaongoza, Padre Mkatoliki amesema anatamani kuonana na viongozi waliopo madarakani na wagombea ili wakiri kama kweli wanatii viapo vyao.

Askofu huyo, Daniel Nung’wana, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akisimikwa rasmi kushika nafasi hiyo jijini Mwanza.

Alisema, utamaduni wa amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania, utaendelea kuwepo kama Watanzania waliojiandikisha kupiga kura, watamchagua mtu mwenye sifa za uchaji Mungu.

Alisema huyo ni yule kiongozi mwenye kulielewa vema na kulifanyia kazi Neno la Mungu, na yule anayetambua na kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa kila Mtanzania.

Akitoa mafundisho kwa waamini na wafanyakazi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzani(TEC), wakati wa sherehe za Kutukuka kwa Msalaba Alhamisi iliyopita, Padre Liberatus Mwenda alisema anatamani kuwaona waliowahi kugombea na kuchaguliwa kushika madaraka na waliochukua fomu za kugombea uongozi mbalimbali, ili awahoji kama kweli wameongoza na wataongoza kwa kadri walivyoapa.

"Ninashangaa sana hawa watu wanapochaguliwa kushika madaraka wanakula viapo kwamba watalitumikia taifa kwa uaminifu lakini, wanaposhika madaraka, wanatumia nafasi hizo kwa manufaa yao binafsi," alisema na kuongeza,

"kama ningekuwa na uwezo, ningependa kumuuliza kila mmoja aliyechukua fomu kugombea urais au nafasi yoyote kama kweli ana moyo wa kuwatumikia watu wote kwa uaminifu na kubeba misalaba yao," alisema na kuongeza kuwa hakuna kiongozi anayepaswa kujiona yuko juu kwa kuwa anayefanya hivyo kimadaraka, anawaumiza walio chini yake.

Kama Askofu wa AICT, Padre Mwenda naye alisema, rais anayewafaa Watanzania ni yule asiyependelea wala kubagua dini yoyote kwa manufaa yake binafsi, chama wala kikundi chochote.

Alisema kiongozi wa namna hiyo akiwa madarakani hatakubali na atajithaihidi zaidi kuona kuwa madhambi mbalimbali yakiwamo mauaji yanapungua kama sio kuondolewa kabisa ndani ya jamii.

Kauli hiyo ya Askofu Nungwana imekuja katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na ongezeko la mauaji ya wazee vikongwe na watu mbalimbali katika eneo la mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa imani za uchawi.

Askofu Nugwana ambaye pia ni Profesa katika chuo cha Theolojia cha Nasa, wilayani Magu, alichaguliwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanza wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Sinodi ya Uchaguzi wa kanisa hilo uliofanyika Juni 28, mnwaka huu hapa jijini Mwanza.

Alichaguliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Samwel Masingili aliyefariki Januari 9, mwaka huu.

Sherehe za kusimikwa Askofu Nungwana awali zilipangwa kufanyika Agosti 6, mwaka huu lakini, baadae zikasogezwa mbele na kufanyika Septemba 3, jijini hapa.

Katika sherehe hizo viongozi mbalimbali wa kidini walihudhuria akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT nchini, John Nkolla ambaye alimsimika Askofu Nungwana.

CUF wavamia Mkutano wa Injili Mwanza

lWawagawia waamini vipeperushi na kuwalilia Wapentekoste waichague CUF

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAFUASI wa Chama cha Wananchi (CUF), wamevamia mkutano wa Injili na kuendesha kampeni na kuwashawishi watu waliokuwa katika mkutano huo kusikiliza mahubiri ili wawapigie kura wagombea wao wa udiwani, ubunge na urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika viwanja vya Furahisha kata ya Kirumba jijini Mwanza, wakati wa kilele cha Mkutano wa Injili ulioandaliwa na Kanisa la Pentekoste Assemblies of God (PAG).

Mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya watu, ulikuwa ukihubiriwa na Mwinjilisti Egon Folk, ghafla uliingiliwa na genge la vijana, ‘wapiga debe’ wa CUF ambao walianza kugawa vipeperushi vyenye majina na picha za wagombea udiwani na ubunge wa chama chao wa Mwanza mjini na vijijini.

Pamoja na kugawa vipeperushi vyao, lakini vijana hao hawakufanya vurugu na walikuwa wakiwahimiza watu waliokuwa wakisikiliza mahubiri ya Mwinjilisti Folk, wakumbuke kuwapigia kura wagombea wa chama chao wakati wa uchaguzi.

Zoezi hilo la CUF kupenyeza kampeni zao katika mkutano wa Injili lilikwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni zao za nyumba kwa nyumba zilizoanza rasmi Agosti 27 hapa jijini Mwanza.

Kampeni za CUF za nyumba kwa nyumba zilianza katika kitongoji cha Kirumba ambapo vijana wa chama hicho waliokuwa wakitembea wawili wawili kila mtaa, walikuwa wakiwashawishi wananchi wakipigie kura chama chao.

Miongoni mwa vijana hao wengine ndio ambao walivamia mkutano wa Injili na kuendesha zoezi lao la kuwashawishi watu waliokuwepo kukikubali na kukichagua chama chao cha CUF ambacho kinadaiwa kuungwa mkono na Waislamu wengi.

Kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini kote hapa Mwanza zilianza rasmi Agosti 27, mwaka huu, kwa vyama mbalimbali kuwanadi wagombea wao wa udiwani na ubunge ambapo katika uzinduzi huo kumekuwa na vituko mbalimbali ndani ya kampeni hizo.

Maaskofu walaumiana kwa kuingiliana makanisa

Na Steven Mchongi, Mwanza

ASKOFU wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, John Changae amemshutumu vikali Askofu wa Dayosisi ya Kagera, Aron Kijanjali kwa madai kuwa ni miongoni mwa wanaowasaidia wachungaji wakorofi wa kanisa hilo ambao tayari walishafukuzwa kazi za kichungaji.

Shutuma hizo za Askofu Changae zinafuatia hatua ya hivi karibuni ya Askofu Kijanjali wa Dayosisi ya Kagera kukubali mwaliko batili wa wachungaji hao wa kwenda kuongoza ibada na kutoa Sakramenti za Ubatizo na Kipaimara katika Dayosisi ya Victoria Nyanza.

Akitoa taarifa yake hapa jijini Mwanza hivi karibuni, Askofu Chagae amesema kuwa Askofu Kijanjali aliingia ndani ya dayosisi yake kikazi bila idhini wala mwaliko wowote na kuendesha Ibada ya Ubatizo na Kipaimara Agosti 26 na 27, mwaka huu jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Kanisa hilo la Kianglikana nchini.

"Kitendo hicho cha Askofu Kijanjali kinadhihirisha kuwa yeye ni miongonni mwa wanaowasaidia wachungaji wakorofi wa kanisa hilo la Kianglikana wa Dayosisi ya Victoria Nyanza ambao tayari walishafukuzwa kazi kwa kuwapa nguvu, kiburi na kuwatia moyo kwa kukubali mwaliko batili wa wachungaji hao," alisema sehemu ya taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa kitendo hicho cha Askofu Kijanjali kuendesha ibada katika kanisa la DVN lililoko katika shule ya Biblia Nyakato jijini hapa, ni utovu wa nidhamu kwani ni kinyume na katiba ya Dayosisi yao ya Victoria Nyanza utamaduni wa kanisa la Kianglikana.

Alipoulizwa baadae na KIONGOZI kwa nini ameamua kuchukua hatua hiyo Askofu Chang’are alisema kuwa haipendezi maaskofu wa dhehebu moja au jimbo moja kulumbana katika vyombo vya habari lakini ameamua kuliweka wazi suala hilo kwa kuwa limeshaendea kuwashitusha na kuwakera waamini.

Askofu Kijanjali wa Dayosisi ya Kagera aliingia Dayosisi ya Victoria Nyanza mnamo Agosti 26 hadi 27 ambapo aliendesha ibada ya Ubatizo na Kipaimara bila kuwa na mwaliko wala taarifa rasmi kutoka kwa Askofu Changae wa Dayosisi hiyo.

Dayosisi ya Victoria Nyanza ya Kanisa la Kianglikana imekumbwa na msuguano wa chinichini ambapo wachungaji kadhaa wa kanisa hilo walisimamishwa na kufukuzwa kazi za kichungaji kutokana na sababu mbalimbali.

Jamii yatakiwa kuwa karibu na yatima

Na Steven Mchongi, aliyekuwa Bukoba

JAMII imetakiwa kuwa karibu na watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kutokana na ugonjwa hatari wa Ukimwi badala ya kuwanyang’anya mali na kuwafukuza kwenye nyumba walizoachiwa na wazazi wao.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Sista Deborah Bryke wa shirika la Wadiakonia lenye makao yake makuu nchini Sweden ambaye amekuwa akisaidia watoto yatima na waathirika wa ukimwi mkoani Kagera.

Alisema kwa upande mmoja jamii imekuwa akiwachukulia watoto yatima kama mzigo fulani ama kama hawana haki yoyote ya kurithi mali za wazazi wao hivyo kufukuzwa na kunyanyaswa.

Akitoa mfano,Sista Bryke alisema katika mkoa wa Kagera ambako anafanya kazi,baadhi ya watoto yatima hunyang’anywa mali na kufukuzwa katika nyumba walizoachiawa na wazazi wao.

Alisema ujuzi alioanao unaonyesha kuwa ni jambo la kawaida mkoani humo kwa ndugu au jamaa kunyang’anya mali za yatima na kuwafukuza kwenye nyumba zao.

Hata hivyo alisema pamoja na kuwepo vitendo hivyo vya kikatili miongoni mwa watu lakini kwa upande mwingine wapo watu wema wanaochukua jukumu la kuwasaidia watoto hao waliofiwa na wazazi wao.

Aliongeza kusema kuwa bila shaka si mkoa wa Kagera tu wenye tabia hiyo bali hata mikoa mingine ya Tanzania hivyo kusisitiza kuacha tabia hiyo mara moja kwani yatima ana haki sawa na mtoto yoyote yule.

Asilimia 40 ya watoto mkoani Kagera,wamepoteza wazazi wote wawili na asilimia 30 wamepoteza mzazi mmojawapo kati ya baba au mama.

Sista Deborah katika mradi wake anawasaidia yatima kwa kuwalipia ada ya shule, sare, vitabu vya shule na pia huwasaidia chukula na matibabu.

UNICEF yalilia haki za watoto

Na Mwandishi Wetu

"KILA binadamu anahitaji hali ya amani na utulivu ili aweze kufanya kazi yake vizuri, hivyo ni lazima awe mbali na mateso ya namna yoyote kimawazo, kiroho na kimwili."

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Akinamama na Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bw. Bjorn Ljungqvist wakati akizungumza katika Tamasha la Amani na Mshikamano la Watoto la Afrika Mwaka 2000 lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana cha Parokia Katoliki ya Mtakatifu Maurus -Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Fredy Mhagama, mwakilishi huyo alisema umaskini, maradhi na ujinga, vimekuwa vyanzo vikubwa vya hatari za misingi ya maendeleo ya binadamu na kwamba ni wajibu wa kila mtu kupambana navyo.

Bw. Mhagama aliyekuwa akizungumza na gazeti hili parokiani kwake muda mfupi baada ya kurejea toka kwenye tamasha hilo na kikundi chake cha The Drums of Steel Band, alimnukuu Bw. Ljungqvist akilitaka tamasha hilo kuyapa kipaumbele masuala ya haki katika jamii inayopenda haki, ustahimilivu na upendo.

"Huu ndio wakati muafaka hasa kwa kuwa katika nchi jirani kuna vurugu hivyo inapendeza kuona watoto wakikusanyika pamoja na kusherehekea Ujumbe wa Amani," Bw. Mhagama aliyanukuu maneno ya Mwakilishi huyo katika tamasha hilo lililofunguliwa Agosti 29, mwaka huu jijini Dar-Es-Salaam.

Bw. Ljungqvist alisema ni wajibu wa kila taifa, na jamii kwa ujumla, kuona watoto wanaishi na kukua katika hali ya amani na utulivu. Pia, wanapata haki ya kutumia vipaji vyao kwa kuwa, nao ni sehemu ya jamii.

Katika tamasha hilo lililowahusisha watoto 400 toka nchi kadhaa za Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Habari na Utamaduni cha Vijana, (YCIC), walioandaa tamasha hilo, Bw.Geoffrey Mhagama, alisema inasikitisha kuwa watoto wengi wa Afrika wameathirika kutokana na vita na ugomvi ndani ya familia zao unaosababishwa na watu wazima.

Baya zaidi Mkurugenzi Mkuu huyo Bw. Mhagama alisema ni watoto kulazimishwa kujihusisha na vita na kwamba hali hii inawanyima haki ya amani. "Watu wazima wengi wanajifanya wanajua kutatua matatizo ya watoto lakini, badala yake wameshindwa kutatua matatizo ya msingi yanayowakabili watoto."

Bw. Mhagama ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa Linaloshughulikia Watoto, Sanaa za Maonesho na Nyimbo(ISCCPA), Kanda ya Afrika, alisema kwa kuwa sanaa za maonesho huwapa watoto fursa ya kueleza matatizo yao, watu wazima na jamii kwa ujumla, hawana budi kuyapa kipaumbele matatizo hayo na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu.

Alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa ISCCPA, Dk. Jack Kukuk, kutoka Arizona, Marekani kwa kuiwezesha Tanzania kuingia katika mtandao wa shughuli za ISCCPA tangu mwaka 1999.

Tamasha hilo lililodhaminiwa na UNICEF kwa ushirikiano wa namna tofauti na Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam, Concern Worldwide, Ultimate Security, CocaCola na wengine wakiwamo wazazi wa watoto, lilihudhuriwa na watoto toka nchi za Afrika Kusini, Eritrea, Burundi, Rwanda, Zambia, Kenya na watoto wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Somesheni watoto ili kuwaepusha na umachinga

Na Charless Hillila, Shinyanga

WAZAZI mkoani Shinyanga wamepewa changamoto kuwapeleka shule watoto wao badala ya kuwaacha wakizagaa mitaani wakifanya biashara ndogondogo na kuchunga mifugo ili kupanua upeo wa akili na kuwajengea mazingira bora ya maisha yao ya baadaye.

Changamoto hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Aloysius Balina wa jimbo Katoliki la Shinyanga, wakati wa sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi katika shule inayoendeshwa na parokia ya Shinyanga mjini ambayo inafundisha masomo yake yote kwa lugha ya kingereza iliyopo Ng’wasele mjini Shinyanga.

Aliwaambia wazazi walioshuhudia uwekaji wa jiwe hilo la msingi kuwa, sasa umefika wakati kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kukimbilia suala la elimu ili kuwasogelea wenzao wa mikoa mingine ambayo hivi sasa iko mbele sana kielimu.

Mwaka jana mkoa wa Shinyanga ulishika namba ya mwisho kwa matokeo ya shule za msingi.

Askofu Balina alizidi kuwasisitizia wazazi kuthamini elimu ya hapa nchini kuliko ya nje ya nchi kwa kuwa ni yenye maadili na inayoheshimu mila na tamaduni nzuri za Kifarika kinyume na elimu itolewayo nchi za nje.

Mhashamu Balina alisema watoto wengi ambao wamekuwa wakisoma nje ya nchi, badala ya kujifunza masomo, wamekuwa wakijifunza tabia na maadili ya nchi hizo ambayo alisema mengi ni mabovu yanayokwenda kinyume na utamaduni, mila na desturi za jamii ya Kiafrika.

Alisema kuwa kwa vile elimu ni paji mojawapo la Roho Mtakatifu, ni kosa la mzazi hasa Mkristo Mkatoliki kutompatia mtoto paji hilo pamoja na mahitaji mengine muhimu katika kukua kwa mtoto.

"Mzazi anayeshindwa kumlea mtoto wake katika malezi hayo hana sifa ya kuitwa binadamu kwa vile kazi mojawapo ya binadamu akishazaa, ni kumlea huyo aliyemzaa kufuatana na mpango wa Mungu," alisema na kuongeza,

"Anayeshindwa kulea lakini ameweza kuzaa ni sawa na wanyama, mimea, ndege na viumbe wengine ambao kwao kazi ni kuzaa tu, na wala siyo kulea."

Uwekaji wa jiwe la msingi ulienda sambamba na kupewa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana wapatao 522 wa parokia ya Shinyanga Mjini katika Kituo cha Old Shinyanga na Shinyanga Mjini.

Kwenye mahubiri yake wakati wa misa na ibada ya Sakramenti ya Kipaimara siku hiyo, Askofu Balina aliwaasa vijana hao kuishi maisha ya Sakramenti na sala siku zote za maisha yao.

Aliwasisitizia sana kupokea Sakramenti ya Kitubio mara kwa mara wanapotenda makosa na maji yanavyohitajika kwa mwenye kiu.

Askofu huyo alizawadiwa mifuko 189 ya saruji na waamini wa parokia hiyo ili imsaidie katika shughuli mbalimbali za ujenzi jimboni humo.

Mwenge kuzindua madarasa mawili ya m. 6/=

Na Getrude Madembwe

MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kufika katika shule ya msingi Mabibo iliyopo jijini Dar-Es-Salaam na kuzindua madarasa 2 ya shule hiyo yenye thamani ya sh. Milioni 6.

Akizungumza na gazeti hili katikati ya juma kwa njia ya simu, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Bw. Shedrack Mkodo, alisema Mwenge huo utafika shuleni kwake Septemba 20 mwaka huu.

"Mwenge utafika shuleni hapa siku ya Jumatano tarehe 20, saa 4 asubuhi na madarasa 2 yenye thamani ya shilingi milioni 6 yatazinduliwa rasm," alisema Mwalimu Mkodo.

Alisema Mwenge huo utapokelewa na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bi. Hawa Ngurume kwenye mpaka wa wilaya ya Kinondoni na Ilala uliopo Tabata relini.

Alisema madawati 60 yenye thamani ya shilingi 180,000 yatakabidhiwa katika sherehe hizo za kuupokea mwenge.

"Madawati 60 ya shilingu 180,000 ni michango ya wazazi wa wanafunzi wa shule hii ikiwa pamoja na ujenzi wa madarasa hayo," alisema Mwalimu Mkondo na kuongeza kuwa.

"Madarasa hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 240 kwa awamu mbili za asubuhi na mchana. Kila moja watoto 120,"alisema.

Wakati huo huo: Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya WIDA, Bw. Mahui Ijumaa ijayo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuwaaga wanafunzi wa Darasa la Saba wa shule hiyo.

Wataalamu waambiwa: Tafuteni sababu ya kuongezeka UKIMWI

Na Mwandishi Wetu

WATAALAMU wa afya nchini, wameshauriwa kufanya utafiti zaidi ili kujua sababu za kasi ya ongezeko la waathirika wa UKIMWI na pia, kupata mbinu sahihi na rahisi za kukabiliana na tatizo hilo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Elimu ya jamii wa kituo kimoja cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, kinachojishughulisha na utoaji wa huduma za kimwili na kiroho kwa waathirika wa UKIMWI cha UPENDANO, kilichopo Chang’ombe jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Adolf Mrema, katika sherehe za ufunguzi wa majengo mapya ya kituo hicho maarufu kwa jina la PASADA.

Kwa mujibu wa taarifa ya kituo ya PASADA (Pastoral Activities Services for People with AIDS Dar-Es-Salaam, Archdiocese), takwimu kadhaa za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wa UKIMWI, huongezeka nchini licha ya elimu ya ugonjwa huu kutolewa hadi mashuleni.

"Idadi ya waathirika na ugonjwa wa UKIMWI ni kubwa sana huko mitaani. Wengi wao hawajielewi, na wale wanaojielewa, huficha na kukataa kujulikana hata kwa wapenzi wao, au kujitokeza katika vituo vinavyotoa huduma ushauri nasaha... Waathirika hawa wasiojielewa, ndio chimbuko kubwa la usamabazaji wa VIRUS," inasema sehemu ya taarifa hiyo.

PASADA imeshauri serikali na jamii kwa ujumla, kuboresha hali ya uchumi inayosababisha vijana hasa wa kike kujihusisha na biashara ya ukahaba.

Alisema hii inatokana na vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta kazi na kuamua kujiingiza katika shughuli hizo hatari kiafya wanapokosa ajira.

Alisema vijana makahaba, watumiaji wa bangi na madawa ya kulevya, na waathirika wa UKIMWI, wanaweza kuepushwa na hatari hiyo endapo wataelimishwa na kusaidiwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kuboresha maisha yao kiuchumi.

Bw. Mrema alisema ingawa serikali imekuwa ikipata misaada mbalimbali kwa ajili ya kupambana na UKIMWI, bado tatizo hilo ni sugu na linaongezeka licha ya elimu iliyokwisha tolewa.

"Kila Mtanzania hapendi kufa, hasa kufa kwa UKIMWI; lakini, kwanini wagonjwa wa ukimwi wanaongezeka?" Alihoji Bw. Mrema katika taarifa yake.

Ameitaka tabia ya baadhi ya wanajamii kuamini kuwa njia pekee ya kukabili matatizo ya kiuchumi ni ukahaba, kukomeshwa mara moja ili kuinusuru jamii isizidi kuangamia.

Alisema ingawa kila Mtanzania anawajibu wa kujikwamua dhidi ya hali duni ya kimaisha kwa kufanya kazi kwa bidii, serikali inawajibu mkubwa kuwasaidia. Alisisitiza kuwa katika suala hili, vikundi na vyama visivyo vya kiserikali, vinaweza kusaidia kutoa misaada.

Mkurugenzi huyo wa elimu ya jamii alisema kwa kuwa hivi sasa maabara nyingi zilizopo nchini, zinatumia teknolojia duni na akashauri serikali na wafadhili kuona kuwa, maabara nchini zinakuwa zenye teknolojia ya hali ya juu ili kuchunguza na kufanya tafiti mbalimbali juu ya UKIMWI.

Alisema jamii haina budi kuhamasishwa zaidi kuwa na mazoea ya kupima damu mara kwa mara, na akasema hili litawezekana endapo maabara za kupimwa HIV, zitaongezeka, gharama za upimaji zitapunguzwa au kuwa bure pamoja na muda wa kupata majibu kuwa mfupi.

Warioba ashauri wagombea wa CCM wachunguzwe, kuchaguliwa

Na Christopher Gamaina, Tarime

WANANCHI wa jimbo la Tarime wameshauriwa kuwachunguza wote wanaogombea nafasi za uongozi kupitia CCM ili wachaguliwe walio safi kwa kuwa CCM ndicho chama chenye sera nzuri kwani vyama vya upinzani vina sera za jukwaani papo kwa hapo.

Ushauri huo wa Jaji Joseph Warioba aliutoa wakati akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Uchaguzi la Tarime.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa shule ya msingi Gamasara, kata ya Nyandoto Septemba 11, mwaka huu na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wa wilaya hii, Jaji Warioba alisema wananchi hawana budi kufahamu kuwa kuna vyama 13 vinavyoshindania uongozi nchini na hivyo wanatakiwa kuipatia CCM ushindi na sio vyama vya upinzani ambavyo wagombea wake hutunga sera mara tu, wanapopanda jukwaani.

"Mpinzani akifika sehemu akaelezwa kuwa tatizo la sehemu hiyo ni maji basi atakapopanda jukwaani kuomba kura atasema, mkinichagua nitamaliza tatizo la maji. Tayari ametunga sera hapo hapo jukwani." alisema.

Aliongeza kuwa Watanzania hawapaswi kumchagua kiongozi kwa misingi ya ukabila kwa kuwa hali hiyo ina hatari ya kuwapata viongozi wabovu.

"CCM ni chama cha Kitaifa sio cha ukoo. Tusibaguane kwa kuchagua kiongozi wa ukoo. Tunachagua kiongozi kama Mtanzania ili ashirikiane na wananchi kuleta maendeleo nchini, sio kwa kuangalia huyu ni Mwiregi au huyu ni Mnyabasi," alisema.

Katika mkutano huo, Jaji Warioba alikuwa anampigia debe, Rais Benjamin Mkapa kutetea kiti chake, Kisieri Chambili, mgombea ubunge waJimbo la Tarime na Bw. Masiaga kuwa diwani wa kata ya Nyandoto,wote kupitia tiketi ya CCM.

Aliongeza kuwa sera ya msingi ya CCM ni umoja ambao ndio unaoleta amani na utulivu.

Wakati huo huo: Bw. Makongoro Nyerere, katika mkutano huo, aliwaponda wapinzani kuwa ni watu wanaotafuta ajira na kwamba wakishapata, hula na wake zao.

Bw. Makongoro aliwahi kujiunga na chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi hadi lipojiengua baada ya kifo cha baba yake Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa madai kuwa amefanya hivyo ili kumuenzi baba yake.

Mashirika ya dini yatakiwa yaendeshwe kwa wito

Na Dalphina Rubyema

WAAMINI waliopo kwenye mashirika mbalimbali ya kidini ndani na nje ya nchi, wametakiwa kutowalazimisha wala kuwabembeleza watu kuingia kwenye mashirika yao kwani kufanya hivyo kunaweza kupoteza maana halisi ya mashirika husika.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa juma na Mshauri wa shirika la Fransisko Wasekulari(SFS) Taifa, Padre Artur Hausser wakati wa mkutano wa Halmashauri na washauri wa Wasekulari wa SFS Taifa, unaoendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar-Es-Salaam.

Kauli hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wajumbe katika mkutano huo kusema kuwa utaratibu wa utabilishaji na uwekaji Nadhiri za Muda na za Maisha kwa Wasekulari wa shirika hilo la Fransisko unapaswa kuangaliwa kwa makini zaidi ili kuboresha mashirika hayo.

"Tusitumie nguvu, watu ambao wameguswa na Ufransisko watajitokeza wenyewe, Ufransisko ni wito siyo kulazimishana," alisema na kuongeza,

"Hili ni shirika siyo chama. Kulazimishana au kubembelezana siyo maana halisi ya Ufransisko. Tukikumbatiana eti tusikatishane tamaa, tutapoteza maana ya Ufransisko."

Kauli hiyo ya wajumbe ya kutaka ubatilishaji wa nadhiri uangaliwe ilikuja baada ya mhudumu wa SFS, Kanda ya Morogoro, Bw. Mathayo Mlegera, kutoa taarifa za jamaa zilizopo ndani ya kanda hiyo.

Jamaa ni sehemu au ngazi zinazounda kanda katika shirika hilo.

Katika taarifa yake, Bw. Mulengera alisema baadhi ya Wasekulari katika kanda hiyo, walikuwa wameweka ahadi za nadhiri za maisha lakini, ahadi hizo zilikuja kubatanishwa baada ya kubainika kuwa zilizotumika si sahihi.

Katika taarifa hiyo pia Bw. Mulengera alitaja jamaa mbalimbali zinazounda kanda yake ingawa hakuitaja jamaa ya ambazo siku za nyuma ilikuwa ni moja ya jamaa za kanda hiyo.

Mkutano huo unaoendelea pia utafanya uchaguzi wa Halmashuri ya SFS Taifa ambapo uongozi utakaochaguliwa utakaa madarakani miaka mitatu.

Uchaguzi huo utasimamiwa na Mkuu wa wasekulari, kimataifa Bi. Emanuela Denusio ambaye kwa niaba yake amemtuma mwakilishi Padre Selasio Njugi kutokana na mshauri wa Kanda ya Morogoro, Padre Edwin Hug wakishirikiana na Padre Hausser.

Kukosekana kwa ajira, Paroko awatetea vijana

Na Elizabeth Steven

KANISA Katoliki parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, limeilalamikia Serikali kuwa imeshindwa kutimiza azma yake ya kuwapatia ajira vijana na hali hiyo imewapelekea vijana wengi kujiingiza katika vitendo viovu vinavyo hatarisha maisha yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mwanzoni mwa juma lililopita, Paroko wa Parokia hiyo, Padre Gelard Derksen, alisema kuwa vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya vijana si tu kwamba vinasababishwa na vijana peke yao, bali kwa kiasi kikubwa pia huchangiwa na serikali ambayo imeshindwa kuwapa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ukosefu wa ajira.

"Siwezi nikawalaumu sana vijana kuwa labda hawapendi kujishughulisha na kazi au biashara ndogondogo kama vile mama ntilie, kufagia, na mambo mengine kwa kuwa yanachangiwa na serikali.

iwapo serikali ingetoa ajira, sidhani kama vitendo viovu kama unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji na uhuni uhuni vingezidi kuongezeka kama ilivyo sasa," alisema Padre Derksen.

Akitoa mfano Paroko huyo alisema, asilimia kubwa ya wafanyakazi wa mabaa hulipwa mishahara wao kidogo ukiangalia na kazi wanazozifanya hivyo kwa upande wa wasichana hushawishika kujiingiza katika biashara ya uuzaji miili yao.

Alisema hali hiyo ya ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana, inachangia kwa kiasi kikubwa ueneaji wa magonjwa ya zinaa ukiwamo huu hatari wa UKIMWI na mengine.

Alisema kuwa, "Iwapo Serikali ingewalipa wafanyakazi wake wa kima cha chini mshahara mzuri, sidhani kama hawa waajiriwa kama mahouse girl (Wafanyakazi wa ndani) au wauzabaa wangeachiwa kulipwa ujira mdogo namna hiyo."

Paroko huyo amewataka vijana wote, wake kwa wanaume kutopenda kuchagua kazi na kusubiri ajira toka serikalini, bali watafute njia muafaka zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe.

Amewataka pia kuacha mara moja vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wenzao kama kutumia madawa ya kulevya, unyang’anyi, ubakaji ambayo alisema vinaweza kuhatarisha maisha yao na kuharibu afya zao wakidhani ndio ufumbuzi wa matatizo yao.

Amewaasa pia kumkumbuka Muumba wao kwa sala na maombi siku zote na sio kusubiri mpaka wanapofikwa na masaibu.