Kilio cha jamii ni matokeo ya kutowajibika - Kanisa Katoliki

lLashangaa wasiojiandikisha kupiga kura kulia matatizo

lLasema linataka kazi bora na si bora kazi

lRais asema moyo ukifeli, mwili umelala

lPadre asema baba mbaya hukimbiwa na wanae

Na Waandishi Wetu

KANISA Katoliki nchini, limesema kuwa kilio na mateso miongoni mwa jamii, ni matokeo ya jamii kutowajibika na kupuuza mambo muhimu ukiwamo uchaguzi ambao wasioushiriki, huwa wa kwanza kulalamikia hali mbaya inayojitokeza.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine NiweMugizi, aliyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati akihimiza umuhimu wa wananchi kwenda kupiga kura ili kuwachagua madiwani, wabunge na rais katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika nchini Oktoba 29, mwaka huu, katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi.

Mhashamu NiweMugizi alikuwa anazungumza na Wafanyakazi wote wa TEC katika ukumbi wa Mikutano wa Baraza hilo uliopo Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Aliwataka wafanyakazi hao na Wakristo wengine, kila mtu kwa nafasi yake, kujiuliza ni kwa kiasi gani anawajibika kwa uaminifu na kwa ufanisi kwa manufaa ya Baraza, Kanisa na taifa zima la Tanzania.

"Kila mmoja ajiulize amewajibika na kuwa muaminifu kwa kiasi gani, kwa kuwa Baraza na taifa, linamtegemea kila mtu," alisema.

Alisema kutokujali maisha yetu na kutowajibika vimekuwa ni vyanzo vya kilio katika jamii na akashangaa hata wasiowajibika kwa masuala muhimu kama upigaji kura, mambo yanapokwenda kombo, huwa mstari wa mbele kulia na kulalamikia uongozi uliopo madarakani wakati wao wenyewe ndio wamekuwa vyanzo vya matatizo hayo.

"Mtu anakuwa hakujali kujiandikisha wala kupiga kura, akichaguliwa kiongozi mbaya matatizo yakazidi ndiye wa kwanza kulia. Hata ambaye hakujiandikisha, atalia. Lazima kila mmoja wetu ajue kwamba kutowajibika ni dhambi ingawa kila siku husali tukisema....kwa kutotimiza wajibu, nimekosa mimi...

Hatujali ndiyo maana tunasema lakini bado tunaendelea na kosa hilo hilo. Tunahitaji kazi bora..." alisema.

Rais huyo wa TEC alisema kuwa, wafanyakazi wa TEC , ndio moyo wa Baraza na kwamba Baraza linategemea uwajibikaji, na uwakili wao ili Kanisa liweze kufanikiwa.

"Ninyi ndio moyo wa Baraza na Kanisa. Bila utendaji wenu bora, maaskofu wenyewe hawawezi kufanikisha kitu. Tujue kuwa sehemu moja ya moyo ikifeli, moyo mzima umezima, na mwili umelala," alisema Mhashamu NiweMugizi.

Alimtaka kila mmoja bila uoga, kujitambua na kujithamini kama kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli za Kanisa na akasisitiza ushirikiano baina yao ili kuboresha utendaji wao.

"Kila mmoja aondoe moyo wa uoga na badala yake, awe na ushujaa, upendo na ushirikiano,"

Akielezea dira ya Baraza hilo la Maaskofu, katika mkutano huo uliofanyika Septemba 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, alisema kwa kuwa baraza hilo linao wataalamu wa fani mbalimbali, hawana budi kutumia utaalamu wao kuboresha shughuli zao za uinjilishaji na kueneza Neno la Kristo.

Padre Rutechura alisema ni wajibu wa kila mmoja kuona kuwa mafanikio yaliyokwisha fikiwa na TEC tangu kuanzishwa kwake miaka 44 sasa yanaendelezwa badala ya kubweteka nayo hali inayoweza kusababisha kurudi nyuma.

"Kwa kuwa hapa kuna vyungu vizuri vyenye mbinu, lazima tupikiwe vizuri ili mafanikio hayo yasirudi nyuma bali yaendelezwe katika kazi ya Kristo," alisema Rais wa TEC kuunga kauli ya Padre Rutechura.

Padre alisema miongoni mwa njia sahihi za kuboresha utendaji, ni kila mmoja kujiangalia na kujipima ili ajue nguvu, bahati, madhaifu na matishio aliyonayo.

Aliitaka Idara ya Mawasiliano ya TEC, kusaidia kukusanya taarifa zilizopita na akahimiza idara zote kushirikiana na kutumia wataalamu wa ndani kabla hata ya kukimbilia wa nje.

Alionya dhidi ya tabia ya kuzoea kuomba na kuanzisha miradi kwa kutegemea misaada kwani inahatarisha mafanikio ya malengo.

"Katika miradi ya kuomba tujue tuko mbali na uwezekano wa kustarehe. Kwa hiyo ni vyema tutumie vizuri vile tulivyonavyo maana kukitunza vizuri ulichonacho, ni moja ya siri za mafanikio," alisisitiza.

Katika mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza tangu Rais huyo wa TEC Mhashamu Severine NiweMugizi, achaguliwe kushika wadhifa huo mwezi Juni, mwaka huu, Mkurugenzi wa Utume wa Walei ngazi ya Tafa, Padre Nicholaus Segeja na Mratibu wa Kitengo cha Kudhibiti Ukimwi George Kanga, walimshukuru Mhashamu kwa heshima ya pekee aliyowapa wafanya kazi wa TEC kwa kukutana nao na kuwataka wasimuogope bali washirikiane nae.

"Baba mwema anapoonekana, watoto humkimbilia lakini yule baba mbaya, watoto humkimbia na kuomba awahi kuondoka," alisema Padre Segeja.

Askofu wa Kianglikana ataka makanisa yasigeuzwe biashara ya kimachinga

lAsema, msiote tu, mkajiita maaskofu

Na Waandishi Wetu, Iringa

"WATU wasigeuze makanisa kama biashara ndogondogo ya vioski, watu wamefikia hatua ya kuyachezea makanisa. Wanalala na kuota ndoto zao wakiamka, wanajiita mapadre, wachungaji na maaskofu, msiligawanye kanisa."

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Iringa, Owdenburg Moses Mdegela, wakati akitoa salamu kwa waamini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, waliohudhuria ibada ya maadhimisho ya Miaka 2000 ya Ukristo jimboni humo.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika uwanja wa Samora mjini hapa Jumapili iliyopita.

Askofu huyo Muanglikana alisema kuwa, bila kujali maana halisi ya Kanisa, baadhi ya watu wamekuwa wakihama katika madhehebu yao ya asili na kuanzisha makanisa yao binafsi na kuanza kujiita mapadre, wachungaji na hata maaskofu.

Askofu Mdegela alisema hali hiyo inashangaza kwa muhimu wa kiroho, wameupataje.

Mbali na kutoa changamoto hiyo, Askofu Mdegela ambaye pia aliwakilisha Umoja wa Makanisa ya Kikristo nchini(CCT), ameyataka madhehebu mbalimbali nchini kuacha tabia ya kukashifiana.

"Tusitemeane mate, tusikashifiane kwa kuwa Mungu wetu ni mmoja. Wote tunakiri kwa imani moja kwamba tunamkataa shetani na kazi zake zote," alisema.

Alisema Kanisa katoliki kama Kanisa Mama, ni lazima liungane kwa pamoja na makanisa mengine kuudhihirishia ulimwengu kuwa ni Kanisa la kweli.

Katika kutekeleza hilo, Askofu Mdegela alisisitiza, "Adui wetu ni mmoja. Hivyo, Wakristo tusitemeane mate wala kudharauliana. Tuwe alama na mwanga kwa kuwa watu wa dini kweli na siyo kuwa watu wa karaha."

Alisisitiza umuhimu wa kuwaita zaidi walio nje kuingia katika Ufalme wa Mungu na kuendelea kuwaimarisha na kuwalinda walio ndani ya Ufalme huo.

"Sura halisi ya Kanisa, ni kuwa na umoja ndani ya Kristo. Kristo hana ubaguzi na imani yetu ni moja. Hivyo, izingatiwe kuwa Yesu Kristo si wa madhehebu fulani na tuko hapa sisi wote kuwaambia wakazi wa Iringa kwamba wale ambao hawajampokea Yesu, sasa ni wakati wa kutubu nao wokovu unakuja kwa njia ya Yesu Kristo’ alisema.

... Askofu wa Iringa alia na ukatili duniani

Dalphina Rubyema na Getrude Madembwe, Iringa

"Binadamu wa leo hayuko tofauti na yule wa Zama za Yesu Kristo lakini, tofauti kubwa iliyopo ni kwamba, binadamu wa leo, shetani amemfilisi kiroho. amelala katika matatizo ya dhambi, ukaidi, mauaji ya wasio na hatia ambao wengine wananyongwa wakiwa ndani ya matumbo ya mama zao kabla hata hawajaona jua".

Amesema Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa wakati wa ibada ya maadhimisho ya Miaka 2000 ya Ukristo jimboni humo na kuongeza,

Ulevi, ubakaji, uasherati na uzinzi, wizi mkubwa mkubwa, ujangili, ujambazi ukahaba na mambo mengine meengi mabaya yanayoweza kuingizwa katika mfuko wa uhalifu, ni njia zinazoweza kuingizwa katika mfuko wa madhambi ni njia inayoonesha namna binadamu alivyopumbazwa na kuwa kama taahira au mtu mwenye mtindio wa ubongo."

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Samora mjini hapa na kuwashirikisha maelfu ya waamini, Mhashamu Ngalalekumtwa alikemea vitendo hivyo viovu vinazvyozidi kushamiri siku hadi siku katika maeneo mbalimbali duniani.

Alisema kila mtu hana budi kufuata nyayo za maisha ya Kristo kwa kuwa ndiye mganga pekee mwenye uwezo wa kutibu maradhi yote ya kimwili na kiroho.Katika ibada ya siku hiyo ya Septemba 3, mwaka huu ambayo pia Kanisa Katoliki lilikuwa linasherekea Siku ya Msamaria Mwema, sadaka iliyotolewa siku hiyo ilikuwa kwa ajili ya kuwasaidia wasio na uwezo ambapo Mhashamu Ngalalekumtwa alidokeza kuwa itawasilishwa katika ofisi za shirika la misaada la CARITAS Taifa.

"Tulikuwa na ukoma, tulikuwa na harufu mbaya na ya kunuka , lakini kwa mapendo yake makubwa miaka 2000 iliyopita, Mungu mwenyewe alimtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo aje kutukomboa wanadamu hivyo tunaposema Msamaria Mwema, tunamaanisha Mungu mwenyewe," alisema Askofu.

Alisema, "Tunahitaji kujinyima kwa ajili ya kuwasaidia wasio na uwezo hivyo sadaka yetu ya leo itapelekwa moja kwa moja bila mmego kwenye ofisi za CARITAS Taifa ili kuwasidia wale wasio na uwezo."Maelfu ya waamini jimboni wakiwemo mapadre, watawa na walei, walihudhuria sherehe hizo zilizojaa shamrashamra.

Askofu Ngalalekumtwa alikuwa kivutio tosha alipoanzisha nyimbo na kucheza jukwaani huku waamini wakiitikia kwa furaha na vigelegele.

Kisha, Askofu wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Iringa, Owdenburg Moses Mdegalla na Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, Mhashamu Magnus Mwalunyungu, walihudhuria ambapo Askofu huyo wa Kianglikana, alimuunga mkono Askofu Ngalalekumtwa.

Chagueni wanaoeleza sera, siyo dosari - Wito

Na Josephs Sabinus

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Mhashamu Damiani Dallu, amewataka wananchi kuwaepuka wagombea wanaokalia kueleza sifa na dosari za wengine na badala yake, wawachague wanaoonesha na kuelezea namna watakavyopambana na umaskini, ujinga na maradhi ili kuboresha maendeleo ya jamii.

Pia, Mhashamu Dallu amesema mtu hawezi kulaaniwa kwa kuwa amerubuniwa na kupokea rushwa toka kwa mgombea kisha akaacha kumpigia kura na badala yake, akampigia mwenye sifa zinazofaa kuwa kiongozi bora kwa kuwa, rushwa inakiuka maadili ya Kimungu na kijamiii.

Aliyasema hayo katikati ya juma katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, wakati mwandishi huyu alipotaka kujua kama ni dhambi kwa mtu kupokea rushwa halafu asitekeleze matakwa ya mtoa rushwa.

"Kwanza kile kitendo cha kutoa rushwa, ni kukiuka hata maadili ndani ya jamii na kwa Mungu. Sasa, kwa kuwa wanatoa rushwa wanajidai kuwa wanatoa zawadi, akikupa chukua lakini, ujue hicho si kigezo cha kukufanya umchague," alisema na kuongeza,

"Wewe akileta, chukua. Ndio maana hata siku hizi watu wanasema, unakula kwa fulani, lakini unalala kwa fulani. Hili ni "suala zito". Lazima mpiga kura ajue kuwa kweli kiongozi huyu atatufaa na kutujali.

Wengine wanaojijua wanahistoria na utendaji mzuri hawana wasiwasi wanapiga kampeni vizuri tu, bila rushwa. Lakini hao wenye matatizo..."

Aliwataka Watanzania kutokubali kurubuniwa kwa vijizawadi vidogo vikiwamo wali, chumvi na kanga ambavyo vitakuja kuwapa majuto ya milele baada ya kuwachagua waliotumia rushwa huku wakiipamba kwa lugha ya zawadi au takrima.

Amesema mtu huwezi kulaaniwa kwa kuwa umepewa rushwa kisha ukakataa kumchagua aliye kuhonga kwa kuwa huko ni kukiuka maadili ya Mungu na ya jamii yanayozuia rushwa.

Mhashamu Dallu aliyesimikwa hivi karibuni kuliongoza Jimbo la Geita, amesisitiza tabia ya kukithiri kwa rushwa na kuifanya waziwazi bila hofu kama ilivyofanyika katika kura za maoni za Chama Cha mapinduzi ambapo kulitokea vilio na malalamiko mengi juu ya vitendo vya rushwa vya waziwazi.

Hata hivyo, CCM iliwaengua waliothibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa kujipatia ushindi katika kura za maoni

Amewahimiza waliojiandikisha, kujitokeza kwa wingi na kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, utakaokuwa wa pili nchini katika mfumo wa kidemokrasia wa vyma vingi vya siasa nchini.

 

Mwinjilisti wa KKKT ashangazwa na wanaokula nyama, ubongo wa watu

Na Elizabeth Steven

"Siku hizi dunia imebadilika binadamu anadiriki kumchuna ngozi binadamu mwenzie! Songea watu 6 walifukua maiti na kula nyama, tazameni ubaya alionao mwanadamu siku hizi binadamu amegubikwa mnyama."

MWINJILISTI Ajuaye Ubwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Tabata katika dayosisi ya mashariki na Pwani, aliyasema maneno hayo kwa masikitiko wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani kwake jijini Dar-Es-Salaam.

Hivi karibuni katika mikoa ya Kusini, watu wapatao sita, walikamatwa wakiwa wanafukuwa maiti na huku waengine wakiwa na mapande ya nyama za maitai za binadamu zinazosadikiwa kuzitumia kwa ajili ya kitoweo na kuna madai kuwa ubongo wa binadamu hao wafu ni maarufu katika maeneo hayo kwa kuweka katika mboga za majani.

Mchungaji Ubwe, amewataka waamini wa kanisa hilo kutojiingiza na pia kuvipiga vita vitendo vyote viovu vinavyotokea miongono mwa jamii ikiwa ni pamoja na mauaji ambacho ni kitendo kisichompendeza Mungu.

Alisema wakati sasa umefika kwa binadamu kutubu madhambi yake na kunuia kutoyarudia kabisa kumrudia muumba wake ili apate kuurithi Ufalme wa Mbingu.

Alisema kuwa haitoshi kwa binadamu kusema anampenda Bwana wakati matendo yake yako kinyume kabisa na mapenzi ya bwana.

"Haitoshi kusema kuwa unampenda Bwana, wakati unakwenda kinyume na mapenzi yake. Wewe na mimi tuwe watumishi wa kweli wa Bwana. Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwainua wanyenyekevu.

Makumbusho ya Kisukuma yazinduliwa

lMtemi avaa ngozi ya simba, mkewe avaa ya chui

Na Charles Hililla, Shinyanga

MKURUGENZI wa Makumbusho kutoka serikali ya Norway Bw. Torveig Dahl pamoja na Bi. Stein kutoka ofisi ya Makumbusho ya Mila na Utamaduni wa watu wa Norway wamezindua Makumbusho ya Mila na Utamaduni wa Kabila la Kisukuma katika mji mdogo wa Malampaka wilayani Maswa mkoani hapa.

Uzinduzi wa makumbusho hayo hivi karibuni uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo, ulitanguliwa na maonesho mbalimbali yakiwamo ya ngoma za asili za Kisukuma, michezo, vyakula vya jadi na kuwasha moto kwa kupekecha vijiti.

Maonesho mengine yalikuwa ya tiba za jadi ambapo waganga 18 wa jadi kutoka maeneo hayo walionesha zana zao za kazi kwa wageni hao na kuonesha wanavyofanya shughuli zao za tiba.

Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, wataalamu hao wa tiba za jadi walikubaliana kuanzisha upandaji miti.

Siku hiyo mgeni rasmi Bi. Stein alizindua vitalu vitatu kwa kupanda mbegu zaidi ya 90 ya aina mbalimbali hasa inayotumika mara nyingi katika tiba za waganga hao.

Upandaji huo ulishuhudiwa na viongozi waliozisifu juhudi za waganga hao na ikasisitizwa katika upandaji huo kuwa, waganga wa jadi hawana budi kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la utunzaji wa mazingira.

Ilielezwa kuwa hali hiyo itasaidia kuepuka jangwa na kutoweka kwa miti mbalimbali ikiwamo inayotumiwa na waganga hao kwa ajali ya tiba zao za jadi.

Uzinduzi huo ulihitimishwa na kutawazwa na kusimikwa rasmi kwa mtemi wa jadi, Malisha Mhangirwa, wa kabila la Wasukuma wa eneo la Bukigi katika kitongoji cha Segerema tarafa ya Malampaka.

Tukio hilo liliwasisismua wengi hasa ambao hawakuwahi kuona mavazi rasmi ya watemi wa kale.

Mtemi Malisha Mhangirwa(48) alivalishwa na wazee wa jadi nguo nyeusi ya kaniki. Mkononi, alikuwa ameshikilia mkuki na ngao alama ya ushujaa na mabegani alivalishwa ngozi ya simba dume ambayo ilishuka hadi chini.

Wakati anava ngozi hiyo, mgore wake (mkewe) alivaa nguo nyeusi sambamba na kunyoa nywele kwa wembe, alivalishwa pia ngozi ya chui mabegani.

Bi Stein alisema anafurahishwa na udumishaji wa mila na utamaduni wa Kisukuma na akaahidi kuwa pindi atakaporudi nchini, kwake ataomba kuondoka na baadhi ya watu wa maeneo hayo ili wakaoneshe mambo hayo nchini kwake.

Alisema huo utakuwa ni mwanzo wa ushirikiano wa mambo ya mila kwa nchi za Tanzania na Norway kwani hata Wanorway watapenda kuja hapa nchini kujifunza mila na tamaduni mbalimbali.

Akinamama wa WDS ‘kuwabeba’ vijana wa YDS

Na Leocardia Moswery

KIKUNDI cha akina Mama cha Mbagala Kizinga Bugdadi kijulikanacho kama Women Development Soceity(WDS), kimeamua kuwapiga jeki vijana wa Kikundi cha Maendeleo ya Vijana cha (YDS) kilichpo Mbagala jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni ofisini kwake jijini, Mwenyekiti wa akina mama hao wa WDS, Bi. Christina Rwebangiha, alisema kuwa "Tumeamua kuwasaidia kwa kuwatafutia mashamba, bustani na masomo kwa sababu wapo ambao hawakwenda shule", alisema Bi. Christina.

Alisema vijana wengi wa Kitanzania hawana ajira lakini watakapopatiwa mwelekeo na shughuli ya kufanya, watafanya na hali hiyo itawasaidia kuondokana na hisia zenye muelekeo wa kutenda uhalifu ukiwamo ubakaji, uvutaji bangi, madawa ya kulevya pamoja na anasa.

Aliendelea kusema kuwa tayari wameshawapatia vijana hao eneo la nusu heka ambalo wapo mbioni kupanda miti pamoja na mboga za majani.

Alisema Bi. Christina kuwa Jumapili hii wanategemea kupata wageni kutoka Wizara ya Afya ambao watoa semina kwa vijana juu ya malezi.

Naye Mwenyekiti wa vijana wa kikundi hicho Bw. Mohamed Mshamu, alisema kuwa juhudi za akina mama zimewakomboa na kuwawezesha kuachana na vitendo viovu ukiwamo uzururaji.

Alisema hadi sasa tayari vijana 76 wamejitolea kufanya kazi za mikono kikiwemo kilimo na akawataka wenye moyo wa kukisaidia kikundi hicho, wajitokeze kwani wao wako tayari kuonesha nia kwa uwajibikaji wao wenye lengo la ufanisi.

Walimu wambiwa wajitazame kimaadili

Na Peter Dominic

WALIMU katika taasisi mbalimba za elimu nchini, wametakiwa kulivalia njuga suala la kuwafundisha wanafunzi wao umuhimu wa maadili bora ya jamii bila kujali vyeo vya wazazi wa wanafunzi hao.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa walimu Wakatoliki wa Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-Salaam, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Jumamosi iliyopita.

Walimu hao walikuwa katika mafungo ya siku moja kwa lengo la kujiandaa kwa ajili ya Jubilei ya Walimu inayofanyika katika kituo cha hija cha Pugu Jumapili hii.

"Pamoja na elimu kushuka, hivi sasa kuna kilio cha ulimwengu juu ya maadili kwa vijana. Jamii imekabidhi vijana kwa walimu wawafundishe. Japokuwa vijana wanalaumiwa kwa kukosa maadili, lawama hizo zinawarudia nyinyi walimu kwa mzunguko endapo hamtakuwa imara kuwaadilisha, alisema Kardinali Pengo.

Alisema ili kuepukana na lawama hizo, walimu wanatakiwa kuwafundisha vijana ukweli juu ya maadili na akaongeza kuwa chimbuko la shida hizo zote ni kutokuwaambia ukweli.

Kardinali aliongeza kutahadharisha kuwa taaluma ya ualimu isiwe ni kufundisha masomo ya Kemia na Fizikia ambayo kutokana na kutomshirikisha Mwenyezi Mungu tayari yameubadilisha ulimwengu, bali ihusike na ufundishaji wa maadili kwa vijana na jamii nzima.

Alisema ujuzi usiokuwa na utaalamu wa Mungu ndani yake, hufanya mambo yaende kinyume na matarajio ya wanadamu.

"Tusipofundisha maadili hatutakuwa na ulimwengu bora tusijenge hofu kuwafundisha vijana juu ya maadili’, alisema

Kardinali Pengo aliendelea kusema kuwa hivi sasa vijana wanakosa misingi mizuri kimaadili kwa vile wanaowategemea wengi wao nao hawana tegemeo ndiyo maana wanajiingiza katika maisha ya ovyo.

Aliwataka walimu kuacha mawazo mabaya kwa kukosa tumaini bali wamuombe Mwenyezi awatangulie katika kuwalea watoto kimaadili ili kulinusuru taifa.

Awali akifungua mkutano huo, Katibu wa Idara ya Elimu wa baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Padre Elias Msemwa, aliwataka walimu wasifundishe kwa kupania mishahara huku wakisahau kazi yao. "Mnaweza kujenga kiburi kwa kuyaweza masomo mkadharauliana wenyewe kwa wenyewe na kuwaweka wanafunzi katika matatizo," alisema.

Pia walimu wakatoliki walitakiwa wajiulize wanahusika vipi katika kuvunja maadili ya mwanafunzi kutokana na mahusiano ya mapenzi ambayo hujitokeza biana yao.

Ilielezwa kwamba uhusiano wa kimapenzi unachangia kwa kiasi kikubwa wizi wa mitihani sambamba na watoto wa kike wenye akili nzuri kuangushwa kwa mbinu za makusudi wanapowakatalia walimu kimapenzi.

Walei waombwa kuchangia ujenzi wa Bakanja

Na Dalphina Rubyema

WAAMINI wa Kanisa Katoliki nchini wameombwa kutoa michango yao ya hali na mali katika kukamilisha ujenzi wa kituo cha Utume wa Walei Taifa cha Bakanja.

Ombi hilo limetolewa na Katibu wa Idara ya Utume wa Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Padre Nicholaus Segeja wakati alipokuwa akizungumza na Kiongozi ofisini kwake katikati ya wiki ambapo alisema kuwa kukamilisha ujenzi huo kutakuwa kumeweka kumbukumbu muhimu na ya kukumbukwa katika mwaka huu Mtakatifu.

Katibu alifafanua kuwa kutakuwa na makundi matatu ya kutoa michango hiyo ambapo alilitaja kundi la kwanza kuwa ni lile la michango ya waamini wote na kila mtu mzima anaombwa kutoa walau sh.500 na watoto pamoja na wanafunzi wa shule sh.100.(Fomu WW)

Alisema kuwa vile vile kuna michango ya hiari ya makundi vikiwemo vyama vya kitume parokiani,kwaya,mashirika ya kitawa ,vikundi vya kitume na vile vya maendeleo,madhehebu mbalimbali katika maeneo maalum ambapo makundi haya yanaomba kutao walao kuanzia sh.10,000.(Fomu VW)

Alilitaja kundi la mwisho kuwa ni lile la watu maalum na wahisani ambao wamepangwa katika vipengele viwili kipengele cha kwanza kikiombwa kutoa kuanzia sh.25,000 (Fomu WMA) na kipengele cha pili ni kuanzia sh.100,000.(Fomu WMB)

Wakati huo huo,Septemba 16 mwaka huu kutakuwepo na ufunguzi wa kongamano la Bikira Maria na siku hiyo pia itakuwa ni Jubilei ya chama cha kitume cha Legio Maria Taifa ,shughuli itakayofanyika Bakanja ,eneo la Ukonga Sitakishari ,Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Akizungumza na Gazeti hili hivi karibuni,Makamu Mwenyekiti wa Legio Maria Taifa na Meneja wa kituo cha bakanja,bw.Conrad Kuyawaga alisema kuwa hiyo ni moja ya maandalizi ya awali ya Jubilei ya Walei Taifa itakayo anza Novemba19 hadi Novemba 26 mwaka huu.

Padre Segeja alisema fomu hizo zinapitishwa kwenye jumuiya ndogo ndogo na Makapuchini.

SACHITA kutoa chanjo, tiba bure kwa watoto na wajawazito vijijini

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Shirika lisilo la kiserikali la SACHITA, linakusudia kutoa bure huduma za chanjo kwa watoto wadogo na mama wajawazito dhidi ya magonjwa ya polio, kifua kikuuu na tetenasi katika vijiji visivyo na hospitali wala zahanati wilayani hapa.

Shirila hilo la Save Children of Tarime limekuwa kwa muda mrefu likitoa huduma za afya katika vijiji vilivyo mbali na huduma za hospitali na zahanati kwa kutumia gari lake (Mobile Clinic).

Katika mazungumzo na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa hivi karibuni, Rais wa shirika hilo, Bw. Peter Mwera, alisema lengo la mpango huo ni kupunguza vifo vya watoto na wajawazito vinavyotokana na ukosefu wa huduma za afya katika vijiji vilivyo mbali na hospitali na zahanati.

Alisema sababu za vifo hivyo zimekuwa ni kutokana na umbali wa upatikanaji wa huduma hiyo na uwezo duni wa jamii husika kumudu gharama na hivyo akasema ni jukumu la shirika lake kutumia uwezo mdogo alilonalo kuokoa maisha ya wanadamu hao yasiangamie ovyo.

Bw. Mwera alisema kwa mujibu wa matarajio ya mipango waliyonayo, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu, vijiji vya Kyoruba, Kimusi na Kobori vitafaidika na chanjo hizo kwa awamu tatu tofauti.

Alivitaja vijiji vingine vilivyo katika mpango huo kuwa ni pamoja na Kenyamanyori,Borega na Kyongera.

"Baada ya wakazi wa maeneo hayo kuomba huduma hiyo kwa kuwa hawana hospitali kwa karibu na serikali kukiri kuwa vijiji hivyo viko mbali na zahanati, tumeamua kuwasaidia kwa njia hiyo," alisema Bw. Mwera.

Alisema tangu Aprili mwaka huu, watoto yatima zaidi ya 16 wa vijiji vya Nyabisaga,kitagutiti, Sang’ana na Katakasembe katika tarafa ya Inchugu, wamesaidiwa na SACHITA kwa kununuliwa nguo za shule, madaftari, vitabu na kalamu katika shule mbalimabli.

Hata hivyo Bw. Mwera alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1997, watoto zaidi ya 3012 wilayani hapa, wanahitaji msaada wa jamii na mashirika mbalimbali ili kupata huduma muhimu za kijamii zikiwamo afya, elimu, chakula na malazi.

Alisema katika tarafa ya Inchage pekee, watoto mayatima zaidi ya 500 wa shule za msingi za sabasaba, turwa, Nyamisangura, Buhemba na Rebu, wanahitaji misaada ya namna hiyo na akatoa wito kwa jamii na mashirika mengine kuunga mkono juhudi za kuwasaidia kwa kuwa ni taifa la kesho.

Alisema licha ya juhudi zao, bado shirika lake linakumbwa na tatizo la usafiri linalotokana na ubovu wa barabara kwenda maeneo yaliyolengwa, na ukosefu wa gari.

Hata hivyo iliishukuru hospitali ya wilaya ya Tarime kwa kuwa imekuwa ikisaidia kwa kutoa gari pindi SACHITA inapokwama.

Wahubiri wa Kilokole wawatia kiwewe Waanglikana

Na Leocardia Moswery

PADRE wa Kanisa la Anglikana Watakatifu Wote katika Dinari ya Temeke, amesema kanisa lao limevamiwa na wenzao maarufu kwa jina la Walokole wanaohubiri kwa kasi mno na kuwashawishi waamini wengi kulihama kanisa hilo.

Akiongoza ibada katika kanisani hapo juma lililopita Padre Nathael C. Kipalamoto alisema kuwa uvamizi wa Walokole hao wanaowashawishi kwa maneno na Injili kulihama kanisa hilo, huna budi kuwa kichocheo cha kuimarisha imani yao.

"Tumevamiwa na Walokole, unajua Mungu anaweza kutuamsha usingizini ili tusilale kwa kutumia njia yoyote anayojua yeye mwenyewe," alisema Padre Kipalamoto.

Padre Kipalamoto aliyerejea kutoka likizo huko Mbeya alisema Wakristo walioko Mbeya walikuwa wakilalama juu ya Walokole wanaowashawishi ili waokoke na kuhama madhehebu yao.

Alisema Walokole hao walikuwa wakitoa huduma ya kiroho ambayo ilikuwa ikiwataka waamini hao kuacha pombe, uvutaji sigara pamoja na mambo mengine ambayo hayampendezi Mungu.

Alidai kuwa, wasipobadilika wao kama viongozi wa dini na kutoa mahubiri ambayo yatamgusa kila mtu, basi waamini hawana budi kuhama na kwenda makanisa na madhehebu mengine.

"Ili kubadilika lazima viongozi wa kanisa tuanze, ndiyo waamini wafuatie siyo padre ufanye kinyume halafu muumini abaki anasema sioni matendo mema ya kiongozi wangu kwa hiyo ...Dini ni imani yako wenyewe," alisema.

Alitolea mfano akisema Sulemani hakuomba kitu kingine kwa Mungu zaidi ya hekima. Aliacha mali na vitu vingine na kumwambia Mungu ampe uwezo wa kuongoza taifa lake kubwa. "Nasi tunapaswa kufanya hivyo hivyo," alisema na kuongeza kuwa wao kama wakuu wa dini, hawana chama cha kushawishi muumini ahamie chama kingine kama vilivyo vyama vya siasa ambavyo kila kimoja kinatoa sera zake bali, wao ni watoaji wa huduma ya kiroho na kimwili kwa kila kiumbe kilichopo ulimwenguni bila kubagua rangi, kabila wala dini.

Papa amtunuku Mtanzania nishani ya Utumishi

Na Waandishi Wetu

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amemtunuku nishani ya utumishi bora na wa muda mrefu, Mtanzania mmoja Bw. Clement Rwelamila, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya CARITAS katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) tangu mwaka 1973.

Akimvisha nishani hiyo kwa niaba ya Baba Mtakatifu, Rais wa TEC, Askofu Severine NiweMugizi, alisema katika ukumbi wa mikutano wa baraza hilo eneo la Kurasini jijini Dar-Es-Salaam, Alhamisi iliyopita kuwa utumishi bora wa Bw. Rwelamila hauna budi kuwa mfano bora wa kuigwa na kila mtumishi ndani ya Kanisa.

Alisema nishani kama hiyo kutolewa na Baba Mtakatifu kwa mtumishi wa kanisa, ni heshima kwa kanisa na taifa kwa ujumla na akampongeza Bw. Rwelamila kwa utumishi wake wa uaminifu ndani ya CARITAS.

Alimtakia kila la heri Bw. Rwelamila ili azidi kuitumikia CARITAS kuanzia familia na ngazi nyingine kwa utekelezaji wa vitendo baada ya kustaafu utumishi wake katika wadhifa huo mapema mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyowajumuisha wafanyakazi wote wa TEC, Bw. Rwelamila, aliwapongeza maaskofu wote wakiwamo waliomuongoza kama wenyeviti wa idara hiyo kwa vipindi tofauti na makatibu wakuu wa TEC kwa kuwa walimpa ushirikiano na malezi bora yaliyomuwezesha kutunukiwa tuzo hiyo na Baba Mtakatifu.

Aliwataja baadhi ya maaskofu walioshirikiana kwa ukaribu na muda mwingi kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa sasa wa CARITAS, Mhashamu Agapit Ndorobo ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge, Askofu Mkuu, Mario Mgulunde wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora na Mhashamu Aloycius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.

"Hata watumishi wengine wa idara mbalimbali tulisaidiana sana wengine wakitoa huduma za kiroho na wengine tukitoa za kimwili," alisema Rwelamila na kuongeza,

"Kwa kuwa msingi wa CARITAS ni upendo kwa kuzingatia kuwa kila binadamu ni ndugu, kazi za CARITAS zinahitaji wito na sio kujali mishahara. Ndiyo maana hata mimi sasa ninakwenda kuwa mtekelezaji wa wa vitendo wa CARITAS kuanzia ngazi ya familia, jumuiya ndogo ndogo na hata kitaifa."

Akitoa mfano wa utumishi bora wa CARITAS nchini, Bw. Rwelamila alisema hata Hayati Mwalimu Nyerere, mara kadhaa katika enzi za uhai wake, alikuwa akiiomba CARITAS kuwasaidia wenye shida na maafa mbalimbali.

"Mwalimu kwa kujua umuhimu na utendaji wa CARITAS tofauti na hizi NGOs, aliwahi kuniita miaka ya 86 hivi, akaomba CARITAS iwasaidie walemavu baiskeli na hata wakati vibanda vimeungua moto huko Arusha miaka ya nyuma kidogo, alituita CARITAS tusaidie," alisema na kuongeza,

"Kufanya kazi CARITAS kunahitaji wito, uaminifu, na bila kuona aibu wala kujali cheo cha anayekwenda kinyume."

KIONGOZI lilipotaka kujua hisia zake baada ya kutunukiwa nishani hiyo na waraka maalumu toka kwa Baba Mtakatifu, Bw. Rwelamila alikuwa na haya ya kusema,

"Nilipofanya kazi, sikuwa ninajua kuwa ni muhimu kiasi cha kupewa tuzo kama hii ya kipekee. Kumbe kazi niliyofanya ilikuwa nzuri na inayotambuliwa kiasi hiki! Nimefurahi sana na siamini macho yangu."

CARITAS Tanzania ni Kitengo cha Kanisa Katoliki nchini kinachojishughulisha na utoaji wa misaada kwa watu mbalimbali wenye matatizo na maafa bila kujali tofauti za kikabila, itikadi za kisiasa, dini wala rangi.

Waamini Moshi wamuunga mkono padre mjubilei

Na Mwandishi Wetu

MAMIA ya Waamini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi wakiwemo mapadre,watawa na walei ,walijumuika kwa pamoja kusherekea Jubilei ya dhahabu ya Padre Ludovick Emil sherehe zilizofanyika hivi karibuni.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Jimbo hilo la Kristo Mfalme,yaliwashirikisha mapadre zaidi ya 90.

Katika ibada ya Misa hiyo Takatifu,Askofu wa Jimbo la Moshi,Mhashamu Amedeus Msarikie aliwataka waamini kutafakari kwa makini juu ya wito katika kanisa.

Aliwataka waamini pia kuwa na shukurani za kushukuru kwa kila jambo jema wanalofanyiwa na Mungu na kuzidi kumuomba kuwaepusha na mabaya yote.

"Kumbuka ni neno kuu katika agano la Kale, watu wakumbuke yale waliofanyiwa, kwa wema na huruma ya Mungu, wawe waaminifu na wamkumbuke Mungu daima"alisema Mhashamu Msarikie.

Aliongeza kusema "mwanadamu amejaliwa ukumbusho hivyo yampasa kutumia kipawa hicho kukumbuka yaliyopita na kuyatafakari".

Maadhimisho ya Jubilei hiyo yaliambatana na siku ya kuzaliwa kwa mujubilei huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80.

Waamini wa Kurasini waenda hija

Na Josephs Sabinus

WAAMINI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maurus, Kurasini katika Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, Jumamosi hii wanafanya hija katika kituo cha Pugu jimboni humo na wamekuwa wakichangia kwa hiari yao wenyewe kufanikisha shughuli hiyo.

Gazeti hili liliwashuhudia waamini mbalimbali kwa nyakati tofauti, wakipishana kwa kuingia na kutoka katika ofisi za parokia hiyo ili kuwasiliasha michango yao mbalimbali kwa lengo la kufanikisha safari hiyo ya hija.

Katibu wa Kamati ya Jubilei, Bw. Cleatus Majani, aliliambia KIONGOZI parokiani hapo mwanzoni mwa juma kuwa, hija hiyo inafuatia utaratibu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ambao kila parokia imepangiwa siku ya kwenda kuhiji hasa katika mwaka huu ambao Kanisa kote duniani linasherehekea Jubilei ya Miaka 2000, tangu kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo.

Majani ambaye pia ni Katibu wa Parokia hiyo, amewataka waamini kushiriki kikamilifu hija hiyo na akasema kwamba kila mmoja kwa nafasi yake, hana budi kujitokeza na kuungana pamoja na wenzake.

Kitendo cha waamini wa parokia hiyo kujitolea bila kusukumwa ili kutoa michango yao, ni ishara tosha kuwa uongozi wa parokia hiyo unashirikiana vema na waamini wake na umewafanya kuiva kweli kiimani.