Mapapa wawili kupewa Utakatifu Jumapili

lNi wenye historia na waanzilishi wa mitaguso tofauti

lMmoja alipendwa sana na watu kinyume na mwingine

lPius alilaumiwa kwa kumteka nyara mtoto, lakini angefanyaje amtoe utumwani?

lYohane aliliokoa Kanisa lisiwe kisiwa

Dalphina Rubyema na Josephs Sabinus

BABA Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, Jumapili hii anawatangaza mapapa wawili waliomtangulia kuwa Watakatifu huku wakiwa na historia tofauti za wema, utumishi na kupendwa. Hali hiyo imewashtua Wayahudi waliomchukia mmoja kati yao.

Mapapa wanaotangazwa Jumapili hii ni Pius wa Tisa aliyechukiwa na Wayahudi kwa kuwa kinyume na matendo yao mabaya wakati huo, na Yohana wa 23, anayeleezwa kuwa mwema na aliyeliunganisha Kanisa.

Akilifafanulia gazeti hili juu ya mapapa hao, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, alisema ofisini kwake mwishoni mwa juma kuwa viongozi hao walikuwa na historia tofauti ya kupendwa kutokana na muda na mazingira ya utumishi wao kwa Kanisa.

Papa Pius aliliongoza Kanisa kwa kipindi cha 1846 hadi 1878, wakati Papa Yohane aliongoza tangu 1958 hadi 1963.

Mhashamu Kilaini alisema kutokana na mazingira ya utumwa wa dhambi yaliyokuwapo wakati wa uongozi wa Papa Pius wa Tisa, Wayahudi walimchukia sana.

"Kwa jinsi walivyoishi, Wayahudi waliwafanya watu wamchukie Papa Pius kwa kuwa walikuwa watu watesi, wanyang’anyi, wenye pesa waliotawala mabenki na mikopo na hivyo, hawakujali lolote.

Suala la Papa kupinga maisha hayo, walimuona vibaya na kumchukia kweli kwa kuwa alikuwa kinyume nao," alisema.

Akizungumzia mtoto wa Kiyahudi, Edgardo Mortara(6) aliyechukuliwa na Jeshi la Papa Pius wa Tisa, ili kumtumikia Mungu huko Roma, Mhashamu Kilaini alisema, "Ingawa alibatizwa na mtu mwingine, Papa alimuona mtoto huyu kama kondoo wake na alichofanya ni kuimarisha imani yake kwa kuwa alimuona kama aliyetumwa na Mungu.

Papa aliona wazazi hawaelewi. Ni sawa na kumuona mtoto anateseka kwao, ukaamua kumchukua umsaidie, ni moyo wa huruma, hilo ndilo alilofanya Papa kumsaidia mtoto huyu na kumuokoa," alisema na kuongeza,

"kwa mtoto kilichokuwa kizuri ni mtoto kuwa Mkatoliki maana, Wayahudi walikuwa wameasi. Kumbe basi kwa kumfanyia hivyo, alikuwa amekombolewa toka utumwa wa dhambi.

Kwa mujibu wa Profesa wa Historia katika Chuo Kikuu cha Brown katika Kisiwa cha Rhode, Papa Pius wa Tisa aliwahi kumuandikia Edgardo akisema, "Wewe ni mpendwa wangu sana. Nimekupata kwa ajili ya Kristo kwa bei ya juu."

Akiwa na miaka 55, mwaka 1907, Mortara aliandika kumsifia Pius akisema, "...Nilikuwa mtoto wa machozi lakini, alinipenda kama mama anavyompenda mwanaye aliyempa mateso," Mortara mwenyewe kwa hiari alipokuwa mkubwa alikataa katakata kuutoka Ukatoliki.

Hata hivyo, Wayahudi waliomchukia sana Papa huyu kwa kuwa alikuwa kinyume na tabia na matendo yao mabaya.

Wameshtushwa na uamuzi huo wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kumtangaza Papa Pius wa Tisa kuwa mtakatifu pamoja na Papa Yohane wa 23 ambaye anasifika ulimwengu mzima kuwa alikuwa mwema na wengi wametega masikio wasikie maelezo yatakayotolewa na baba Mtakatifu wakati akiwatangaza mapapa hao kuwa watakatifu.

Katika kipindi cha utumishi bora wa Papa Pius, alitoa hati ya huruma kwa wafungwa wengi sana.

Hata hivyo, katika kipindi chake, Serikali mpya ya Italia, ilijionesha wazi kuwa adui mkubwa wa Kanisa.

Mwaka 1869, alifungua Mtaguso wa Ishirini katika Vatican (Mtaguso Mkuu wa Kwanza waVatican), ambapo ilitangazwa wazi kuwa Papa hawezi kukosea ukweli anapotangaza au kuelezea imani kama Papa.

Papa Yohane wa 23, aliishi muda mrefu bila kujulikana nje. Ingawa alikuwa Askofu wa Venesia, hakuna aliyejua kuwa atachaguliwa kuwa Papa. Kutokana na mafundisho yake yenye nia kubwa ya kuliunganisha na kulirekebisha kanisa yaliyowashangaza wengi, aliitisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baada ya kikao cha kwanza tu, alifariki dunia.

Anakumbukwa zaidi kutokana na wema wake usiokuwa na mipaka.

"Sijui kama kwa karne zilizopita, kuna Papa aliyependwa kama Papa Yohane wa 23... Alilikomboa Kanisa maana pengine hata lingeweza kuwa isolated (Kuwa pweke). Akalifungua ili liweze kuwasiliana na ulimwengu mzima badala ya kuwa kama kisiwa,"alisema.

Nyumba 20 zachomwa moto katika mapigano ya makabila

Na Amicuss Butunga, Tarime

JUMLA ya nyumba 20 zimechomwa moto katika Kijiji cha Korotambe kata ya Mwema Wilayani Tarime baada ya kuzuka mapigano ya makabila madogo ya Kikurya wilayani hapa.

Hali hii imefuatia vita iliyozuka baina ya vijiji vya Korotambe na viwili vya Remagwe na Ngerengere katika Kata ya Sirari, Tarafa ya Inchungu, Wilayani hapa kufuatia Wakila wanaoishi Remagwe na Ngerengere kufukuzwa eneo la kijiji cha Korotambe ambacho kinakaliwa na Wakurya wa kabila dogo la Wanchari.

Ugomvi huo unatokana na makabila hayo mawili kutofahamu vema mipaka ya vijiji na makabila yao na ipo haja kubwa zikatafutwa juhudi za makusudi kuiweka wazi.

Habari zilizopatikana mjini hapa zinasema kufuatia vita hiyo iliyoanza Agosti 28, watu watano walijeruhiwa kwa mikuki na mishale na kwamba wamelazwa katika Hospitali ya kibinafsi ya Dk. Winani ya mjini hapa.

Habari zimewataja watu hao kuwa ni Petro Sando, Mang’era Mwita, Sinsiga Sinsiga, Wesiko Mang’era na James Wambura, wote wakazi wa kijiji cha Korotambe wilayani Tarime.

Kufuatia ugomvi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Dk. Charles C. Magoti, amesema serikali wilayani hapa ina mpango wa kuangalia na kugawanya upya maeneo yenye utata.

Hata hivyo, gazeti hili lilipotaka kuwasiliana na Mkuu huyo wa Wilaya ya Tarime kwa njia ya simu kutoka Makao Makuu ya gazeti jijini Dar-Es-salaam, ili kupata ufafanuzi zaidi juu ya taarifa hiyo, Dk. Magoti alikataa kulizungumzia. na kusisitiza,

"Aliyewapa taarifa hizo aseme kila kitu kwa kuwa mimi ninaweza kusema hali hiyo ipo kumbe haipo au nikasema ipo kumbe haipo. Hivyo ni vema aliyewaambia mumuamini na kama sivyo, basi mje huku wenyewe."

Mkuu huyo wa wilaya alipoombwa kutoa ushirikiano zaidi juu ya suala hili kwa gazeti hili alisema, "hata kukujibu hivi ni ushirikiano mkubwa."

Hali kama hiyo isipodhibitiwa mapema, itaathiri jamii kwa kusababisha hasara hasa katika mashamba yaliyo mipakani mwa vijiji husika. Inapotokea, hali kama hii husababisha wengine kufyeka na kteketeza mazao na hivyo kusabisha jamii kuathirika kwa njaa.

Pia hali hii ni vema ikakemewa mapema na vyombo husika ili isilete madhara kwa Watanzania ambauo tayari walishazoea kuishi kwa amani, ushirikiano, umoja na upendo wa kidugu.

Mkuu wa Mkoa ahimiza viongozi wa dini kupigia debe upigaji kura

Na Steven Mchongi, Mwanza

MAASKOFU, Mapadre, Wachgungaji, Maimamu na Masheikh mkoani Mwanza, wametakiwa kuwahimiza waamini wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Mwito huo umetolewa hivi karibuni jijini Mwanza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw. Stephen Mashishanga, kufuatia viongozi hao wa madhehebu ya tofauti ya kidini kufanikisha kwa kiasi fulani, zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Katika zoezi la uandikishaji wapiga kura lililoanza Agosti 8, 2000 na kumalizika Agosti 28, mwaka huu, viongozi hao wa madhehebu ya dini waliwahimiza wananchi bila kujali tofauti za kiimani wala itikadi za kisiasa, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha hapa mkoani Mwanza.

Akitoa Mwito wake, Bw. Mashishanga amewaomba viongozi hao wa madhehebu ya Kikristo na Kiislamu kwa pamoja bila kujali tofauti zao, kuwahimiza wananchi makanisani na misikitini ili wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi watakaoliongoza taifa.

Alisema ni jukumu la kila mmoja bila kujali imani za dini au itikidi za siasa kuhimiza wananchi kujitokeza kupiga kura kuchagua madiwani, wabunge na rais katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaokuwa wa pili kufanyika nchini katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi.

Kufuatia mwito huo wa Mkuu wa Mkoa, tayari viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini jijini Mwaza, wamekuwa wakiwahimiza wananchi wakati wa ibada makanisani na misikitini, wajitokeze kuchagua viongozi itakapofika siku ya uchaguzi.

Akizungumzia miito hiyo hivi karibuni jijini hapa, Msimamizi wa Uchaguzi wilaya ya Mwanza, Asumpta Ndimbo alisema, wanatarajia itafanikisha kuhimiza wananchi kupiga kura Oktoba 29 kama vile ambavyo ilikuwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Anthony Mayala, alisema hakuna ubaya kwa viongozi wa dini kuwahimiza waamini kuwachagua viongozi wao wa kisiasa na hivyo, anaamini taifa litapata viongozi bora iwapo wananchi watajitokeza kwa wingi.

Awali sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Omari Balamwezi alisema viongozi wa dini wanao wajibu wa kuwahimiza waamini kujitokeza kuchagua viongozi na bila kuwashawishi wampigie kura na kwamba ni katika uchaguzi huo.

Hivi karibuni katika zoezi la uandikishaji wapiga kura lililomalizika Agosti 28, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alitoa wito kama huo kupitia viongozi wa dini na taasisi mbalimbali ambapo aliwataka wawahimize wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura.

Mwito huo wa Bw. Mashishanga ulifuatia kuzorota kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura katika majimbo mbalimbali mkoani Mwanza ambapo ni watu wachache walikuwa wamejitokeza kujiandikisha.

Sungusungu Tarime wadaiwa kuchangia mauaji

lTLP wadai ni kukiuka agizo la Mkapa

lwadaiwa kuigeuza kuwa kitega uchumi

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Sambamba na kujipatia vipato kinyume, Walinzi wa Jadi (Sungusungu) katika tarafa ya Inchage wilayani Tarime mkoani Mara, wanadaiwa kuwanyanyasa kwa vipigo na kuchangia vifo kwa baadhi ya watuhumiwa wa ujambazi, wasio na vitambulisho na wasiolipa kodi.

Wananchi kadhaa waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wilayani hapa hivi karibuni, wamesema kwa kisingizio cha kuwasaka wahalifu hususani majambazi na wakwepa kodi, sungusungu hao wamekuwa wakilipiza visasi binafsi na kudai hongo toka kwa watu wasiolipa kodi na wasio na vitambulisho.

Walidai kuwa sungusungu wamekuwa wakiwapiga watuhumiwa na kuwajeruhi vibaya hali iliyosababisha baadhi ya watuhumiwa kufariki wakiwa hospitalini na wakaongeza kuwa sungusungu wamekuwa wakidai shilingi elfu mbili kwa mtu aliyekamatwa njiani bila kodi pesa wanayoiita "kiatu" ambaye ni kwa manufaa ya sungusungu binafsi.

Wananchi hao walidai kuwa anayekamatwa kwa kukosa kitambulisho au kodi hudaiwa pesa njiani na wanapokosa, hufunguliwa mashitaka mbalimbali zikiwamo tuhuma za ujambazi na uzururaji.

Kwa kawaida kodi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni shilingi 4000/=, baada ya muda kupita, adhabu ya asilimia 50 huongezwa na kufikia shilingi 6000/=. Lakini sungusungu hao wanapodai "kiatu" malipo yaliyogeuzwa kinyamela kuwa sheria, hulipwa shilingi 8000/=.

Wananchi hao walisema hata katika misako yao katika nyumba wanazoshuku, wamekuwa wakifika na kuanza kuwapiga wanafamilia wote katika nyumba bila kujali ni nani mkosefu hali waliyoisema ni unyanyasaji.

Akizungumzia ukatili wa sungusungu, mmoja wa ndugu wa marehemu, Chacha Mwita Nyasagaya (30), mkazi wa kijiji cha Kemakorere aliyefariki Agosti 3, mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kufuatia maumivu ya kichwa (kwa mujibu wa kibali cha mazishi cha hospitali hiyo.ambacho nakala yake tunayo), yaliyodaiwa kutokana na kipigo cha sungusungu hao kwa madai kuwa marehemu alikuwa na historia ya ujambazi, Bw. Bhoke Magasi wa kijiji cha Kemakorere, alisema,

"Sungusungu hawa hawafanyi kazi kwa haki kwa sababu hata watu wote wanajua kabisa wanafanya mambo kwa kuchukulia fitina tu.

Kila mtu pale kijijini anajua kulikuwa na fitina tangu zamani kati ya marehemu na ukoo wa Mwenyekiti wa kijiji."

Bw. Magasi alitahadharisha kuwa endapo sungusungu hawatafuata maadili, ipo hatari ya kuiangamiza jamii kwa chuki za kibinfasi.

Muuguzi mmoja wa wodi namba 7 hospitalini hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa madai kuwa sio msemaji hivyo anahofia kibarua na mahusiano yake kuharibika, alisema, "Lakini hivyo sungusungu hawafanyi vizuri. Si kuna mwingine tena alikuwa anaitwa Marwa Chacha (29) wa Nkongore, alipewa admition alilazwa tarehe 22/7 na amefariki juzi juzi tu kwa kupigwa. Sasa kama walinzi wa amani watakuwa mstari wa mbele kufanya hivyo, siyo vizuri," alisema.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha TLP mkoani Mara, Bw. Maganya Roman Nyangi, alisema, "... inashangaza hata Rais anasisitiza utawala wa kisheria, lakini hilo halitumiki.

Siku hizi kila kijana anataka awe sungusungu; hawafanyikazi wala kulima.

Wameona sungusungu ndiyo ajira pekee na wako radhi kuuza hata mifugo ili waingie sungusungu."

Kaimu Katibu Tarafa wa Inchage Bw. Kalebu Fanuel Kehogo, alikanusha madai hayo na kusema ni kawaida kwa familia ambazo ndugu zao wamechukuliwa hatua kulalamika.

"Ingawa anayeweza kusemea vifo hivyo ni daktari, lakini kuna madai kwamba huyu wa Kemakorere aliposikia anakuja kukamatwa, alipanda darini akaning’inia huko mpaka alipochoka na kuanguka chini. Sasa Can you imagine (unaweza kufikiria) kwa umbali ule alioanguka, aliathirika kwa kiasi gani."

Bw. Kalebu ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Tarime mjini alikanusha madai ya sungusungu kupokea rushwa kwa madai kuwa huwa wanaambatana na maafisa watendaji wa kata na vijiji na akasema pia kuwa alikuwa hajayasikia. alisema atakayebainika kuhusika na vitendo vya rushwa na unyanyasaji wa raia, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kanisa Katoliki kupanua matawi Mwanza

Na Steven Mchongi, Mwanza

KANISA Katoliki Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Ilemela jijini Mwanza inatarajia kujenga na kufungua vigango vipya katika kata za Igombe, Kayenze, Kilinho, Kilabela na Mhonze.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Padre Richard Makungu wa Parokia hiyo iliyopo Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, imeeleza kuwa ujenzi na ufunguzi wa vigango hivyo unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akitoa taarifa hiyo kwa Askofu Mkuu Mayala mbele ya waamini, Padre Makungu alieleza kuwa ujenzi na ufunguzi wa vigango hivyo vitano unafuatia ongezeko la idadi ya waamini katika maeneo yanayoizunguka parokoa hiyo.

Parokia hiyo ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambayo Julai 17 mwaka huu ilitimiza mwaka mmoja, sasa ina idadi ya waamini 7,968 walioko katika vigango vya Ilemela, Lumala, Nyang’wilolelwa na Kabangaja.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kusimikwa rasmi waamini 1358 ambao ni watoto wachanga walipatiwa Sakramenti ya Ubatizo na waamini 134 walipatiwa Sakramenti ya Ndoa hadi sasa.

Aidha kufuatia ongezeko la waamini Padre Makungu alisema upanuzi wa kanisa la Kigango cha Kabangaja nao umekamilika ili kukidhi ongezeko hilo la waamini wanaofika kusali kanisani hapo.

Mhashamu Mayala alisomewa taarifa hiyo ya maendeleo ya Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu wakati wa sherehe za kumkaribisha Fratela Kizito Ng’wandu zilizofanyika parokiani hapo na kuhudhuriwa na waamini kutoka vigango mbalimbali.

Awali kabla ya sherehe hiyo kulifanyika ibada maalumu kanisani hapo ambayo iliongozwa na Mhashamu Mayala na aliwataka vijana wa Kikristo kuwaheshimu wazazi.

Akizungumza wakati wa mahubiri, Mhashamu Mayala alisema katika ulimwengu wa leo maadili yameshuka miongoni mwa jamii na hasa vijana ambao wamekuwa hawana heshima kwa wazazi wa na watu waliwaopita umri.

Kutokana na hali hiyo Askofu Mkuu huyo amewataka watu kusali na kufuata mafundisho ya kiroho na kuepuka mambo ya kiulimwengu ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha kuporomoka kwa maadili miongoni mwao.

Wachagueni watakaotunza uhuru wa kuabudu - TAG

Na Benjamin Mwakibinga

ASKOFU Mwangalizi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God(TAG)sehemu ya Kinondoni Mchungaji Nathaniel Sasali amewataka Wakristo kuwachagua viongozi watakaoendeleza kuwapo kwa uhuru wa kuabudu ili Watanzania wazidi kumjua Mungu.

Mchungaji Sasali aliyasema hayo katika ibada ya Donimika iliyopita alipokuwa akihubiri katika mkutano wa Injili uliofanyika katika uwanja wa kanisa la TAG Kijitonyama jijini Dar-Es-Salaam.

"Nendeni mkajiandikishe na siku ya kupiga kura muende kupiga" alisema na kuongeza kuwa wamachague mtu ambaye uongozi wake hautaweka vikwazo kwa Watanzania kuabudu.

"Mimi sisemi mkamchague nani lakini ninyi mnamjua mtu mwenye sifahizo".

Askofu huyo alisema kuwa Taifa lenye wacha Mungu siku zote huwa na amani na utulivu.

Katika mahubiri yake alisema Wakristo na Mungu ili wawe watenda kazi hapa duniani na kwamba matendo ya mtu ndiyo yatakayoamua ni wapi mtu huyo atakwenda mara baada ya kifo chake.

Askofu Sasali aliwataka Wakristo na wasio Wakristo kutoamini kuwa sala na dua kwa wafu zinaweza kumfikisha mtu kwa Mungu, bali ni matendo yake na uchaji mbele za Mungu ndio njia pekee kumfikisha huko mbinguni.

Awali katika mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Makanisa matatu ya TAG sehemu ya kinondoni ambayoni Kinondoni, Magomeni na wenyeji wa Kijitonyama palifanyika maombi maalumu kwa ajili ya kuliombea Taifa la Tanzania na viongozi wa Serikali akiwemo Rais Benjamin Mkapa.

Aidha katika maombi hayo yaliyoongozwa na Mchungaji Mulokozi aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo, walimuomba Mungu alisaidie Taifa hili kwa kipindi chote cha Kampeni na hata mara baada ya uchaguzi na kuwataka Wakristo wasijihusishe na vurugu za aina yoyote ili Taifa liendelee kuwa na amani pamoja na utulivu.

Toeni mikopo kulingana na mazingira ya walengwa

Na Dalphina Rubyema

MASHIRIKA na taasisi mbalimbali zinazohusika na utoaji mikopo nchini, zimetakiwa kutoa mikopo kulingana na hali halisi ya mazingiria wanakoishi wakopeshwaji, amesema Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya ya Kibaha Bi. Rahia Kupasa.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na KIONGOZI wilayani kwake katika mkoa wa Pwani juu ya mikopo mbalimbali inayotolewa kwa wananchi na vikundi mbalimbali.

Bi. Kupaza alisema kuwa umefika wakati ambao mashirika na taasisi husika kutoa mikopo kwa kuweka masharti kuwa ni lazima wakopeshaji waingize mikopo hiyo katika biashara na siyo shughuli nyingine.

"Mfano mzuri kule vijijini kama Rufiji mtu anayeishi huko unampa mkopo na kumuwekea masharti kwamba lazima afanye biashara huko Rufiji aitafanya biashara gani?" alihoji.

Aliongeza, "Mtu wa eneo kama hilo inafaa umpe mkopo na autumie katika masuala ya kilimo, mpe auweke kwenye kilimo cha mpunga, nyanya, matango na mazao mengine ya aina hiyo na utafurahi ukifika msimu wa mavuno, kwani kila mkulima uliye mkopesha atakurudishia mkopo wako na riba juu bila matatizo".

Afisa huyo wa maendeleo ya jamii alisisitiza kuwa mkopo siyo lazima uwe wa fedha taslimu, bali unaweza kuwa hata wa vitendea kazi kama trekta au hata majembe ya kukokotwa na ng’ombe.

Alisema mkopo kama huu utasaidia hata kupunguza mitaji ya shughuli zao zikiwemo za uchomaji wa mkaa.

Hata hivyo Bi. Kupasa aliwashukuru wanawake wa wilaya yake kwa kutumia kwa uaminifu mikopo na sasa kwa kiasi kikubwa, wameweza kujikwamua kimaisha.

TEC yahimiza WID kuwa waangalifu, waaminifu

Na Getrude Madembwe

KATIBU Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Padre Pius Rutechura, amewataka waratibu wa Kitengo cha Maendeleo cha Wanawake(WID)cha shirika la Caritas kuwa na moyo wa kujitolea na kuwa waaminifu katika kazi zao.

Aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua semina ya wiki moja iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Semina hiyo iliwashirikisha waratibu wa kitengo hicho kutoka katika majimbo 29 ya Kanisa Katoliki. Lengo la semina hiyo lilikuwa kutathimini maendeleo ya kitengo kwa miaka mitatu tangu kianze shughuli.

Aliwataka kuwa waangalifu, kutunza kumbukumbu na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka.

"Kutoa kwenu taarifa sahihi kutasaidia au kuhimiza kitu gani kifanyike pale ambapo hapajaweza kufanyika na wala sio kutoa taarifa za uongo kuwa jimbo langu limewafanya akinamama wawe wa maendeleo na vitu vingine kama hivyo,"" alisema Padre Rutechura

Alisisitiza mpangilio na mgawanyo wa kazi ili kuleta ufanisi katika malengo yaliyowekwa kimaendeleo.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Katibu mtendaji wa Shirika la Misaada la CARITAS Tanzania Bw. Peter Maduki alisema kuwa ofisi ya Taifa inategemea sana matokeo wanayoyatoa majimbo kwao.

"Ni vizuri mkafanya tathimini yenu ya miaka 3 kikamilifu kwani ofisi ya Taifa inategemea sana matokeo yenu," alisema Bw. Maduki.

Kwa mujibu wa Mratibu wa kitengo cha maendeleo ya wanawake (WID) taifa kilichopo chini ya CARITAS, Bi. Oliver Kinabo, alisema semina hiyo imeandaliwa na ofisi ya WID Taifa.

Semina hiyo ilijadili yaliyofanywa na WID kwa kipindi cha miaka 3 tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 1997.

Alisema kuwa kitengo hicho kinajulikana kama (WID and Children) yaani Maendeleo ya Wanawake na Watoto ingawa bado hawajaanza kazi kwa upande wa watoto ambao kitaanza kuwashughulikia baada ya tathmini ya Julai 2000 na Juni 2001.

Tangu kitengo hicho kianzishwe kimefanikiwa kuendesha semina katika majimbo mbalimbali ya kanisa pamoja na kuwainua wanawake kiuchumi kwa mahitaji yao muhimu.

Tunzeni Biblia kumheshimu Mungu-Wito

Na Elizabeth Steven

Pamoja na kusisitizwa kuepuka kuweka Biblia katika mazingira machafu kwa kuwa ni kumdharau Mwenyezi Mungu, Waamini wa Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Anuarite, Parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wametakiwa kujenga Jumuiya Ndogo Ndogo na kuziweka katika hali ya amani na familia zao na

Wito huo ulitolewa na Paroko wa Kanisa hilo Padre Gerard Derksen, alipokuwa akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita ambapo alisimika Biblia parokiani.

"Wakristo wanapaswa kuziweka Jumuiya Ndogo Ndogo pamoja na familia katika hali ya usafi na kuzijenga. Pia, wanapaswa pia kuziheshimu Biblia na kuzihifadhi katika mazingira safi kwani kwa kufanya hivyo, ni kumtukuza Mungu na kumheshimu,"

Alisema kuwa ni wajibu kwa wana jamii na hawana budi kulipenda, kulitumikia, na kulitangaza Jina la Bwana kwani limeingizwa kanisani ili lifanyiwe kazi.

Padre Derksen alisema kuwa Biblia imewekwa ili watu wapate kujua kuwa Neno la Mungu ni mwanga, nuru na anayelishika, ataishi milele.

"Neno la Mungu ni kama mbegu, lazima lipandwe na listawi pia Neno la Mungu ni kama mvua imeleta uzima na uhai."

Maandamano hayo ya kusimika Biblia parokiani hapo, yalihudhuriwa na waamini wa parokia hiyo wakiwemo vijana, watoto, wazee, akina mama na akina baba.

Wafanyabiashara wakimbia soko

Na Peter Dominic

BAADHI ya Wafanyabiashara katika Soko la Temeke Sterio katika Manisapaa ya Temeke mkoani Dar-Es-Salaam,wameyakimbia mabanda yao baada ya kukosa wateja, KIONGOZI limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili sokoni hapo, umebaini kwamba wafanyabiashara sokoni hapo wamekuwa wakipata ugumu wa kuuza biashara zao hali inayowasababishia hasara.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya mabanda sokoni hapo yamefungwa na taarifa ya kuamini kutoka kwa wafanyabiashara waliobaki sokoni hapo, inasema waliofunga mabanda yao, wamehamia katika soko la Tandika lililopo jirani na Soko la Temeke Stereo.

Vyanzo vya habari sokoni hapo vimedai kuwa, pamoja na kushindwa kuuza bidhaa zao, wafanyabiashara wa sokoni hapo wamekuwa wakilazimika kulipa kodi ya pango.

Wafanyabiashara wa soko hilo waliozungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti, wameilaumu Manispaa ya Temeke ambayo zamani ilikuwa ikifanya kazi chini ya Tume ya Jiji kwa kwa kuwa imekuwa ikiwaahidi kushughulikia tatizo lao bila kutimiza.

Walisema manispaa mekuwa ikiahidi mara kwa mara kuvunja soko la Tandika ili wafanyabiashara wote wahamie Temeke Stereo lakini haifanya hivyo.

"Wameondosha bidhaa zao wameona hawapati faida, wameamua kutafuta sehemu zingine. Huwezi kukaa unapiga miayo wakati hakuna mteja anayekuja kuuliza angalau bei halafu, mwisho wa mwezi unadaiwa kodi sijui utalipa nini"

alisema mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Paul Shayo.

Mbali na wafanyabiashara hao kuelekeza shtuma zao kwa uongozi wa Manispaa, pia waliulaumu uongozi wa soko hilo kwa madai kuwa ulichangia wafanyabiashara wengi kulikimbia soko hilo kutokana na kuweka viwango vya juu vya kodi na hivyo, kuwafanya wengine kurudi sokoni Tandika.

"Walianza na viwango vya juu vya kodi lakini baada ya kuona watu wanakimbia ndipo walipoamua kupunguza, walitanguliza tamaa," alidai Bw. Richard Mkulya.

Meneja Msaidizi wa soko hilo Bw. John Fue, alikiri kukimbia kwa baadhi ya wafanyabiashara na akasema suluhisho litapatikana pale Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bw. Idd Nyundo, atakapotekeleza mpango wa kulivunja soko la zamani la Tandika.

"Ni kweli wafanyabiashara wengine wameondoka kwa vile wateja ni wachache mno, hata sisi tumepunguza kodi kuwapa nafuu wapangaji lakini tumelazimika kuwapunguzia pia wafanyakazi wetu na tayari tunashindwa kuendesha huduma za soko kutokana na tatizo hilo la wateja," alisema Bw.Fue bila kutaja kodi halisi inayolipwa kwa sasa.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari wamekwisha andika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kukumbushia wazo la kuvunja kwa soko la Tandika ili kuboresha soko hilo jipya.

PSRC yazindua gazeti

Na Dalphina Rubyema

TUME ya Taifa ya Kurekebisha Mfumo wa Mashirika ya Umma(PSRC), imezindua rasmi gazeti lake la ndani ambalo litakuwa likitolewa mara mbili kwa mwezi, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Tume hiyo iliyolifkia gazeti hili ikiwaimesainiwa na Mwenyekiti wa PSRC Bw. John Rubambe, gazeti hilo litatolewa bure kwa watu mbalimbali wakiwamo maafisa wa serikali, wabunge, waajiriwa wa mashirika na vyombo vya habari.

Taarifa imesema gazeti hilo litakuwa linaelezea kwa uwazi namna zoezi zima la ubinafsishaji linavyoendelea nchini.

Imesema kuwa gazeti hilo la rangi, tayari limeisha tolewa katika matoleo yake ya mwezi Mei na Juni mwaka huu ambapo habari kubwa katika matoleo hayo ilikuwa juu ya kubinafsishwa kwa Container Terminal iliyo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania(THA).

Matoleo hayo pia yalikuwa na taarifa ya ubinafshaji wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), hitimisho la makubaliano ya ubinafshaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC -1997) Ltd, Usafirishaji wa Mizigo kwa Njia ya Ndege (DAHACO), kiwanda cha karatasi ya Mfindi.

Taarifa inasema lengo la kuanzishwa kwa gazeti hilo ni kuelimisha na kutoa taarifa kwa umma kwa upana juu ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma.

Baadhi ya wananchi waliozungumzia suala la gazeti hilo, wameipongeza PSRC kwa hatua hiyo na kusema sasa imeongeza imani kwa wananchi kwa kuwa wataweza kujua habari mbalimbali zinazohusu ubinafsishaji nchini.

SHDEPHA+ yashauri kuepuka mambukizo ya ukimwi kwa makusudi

Na Neema Dawson

MWENYEKITI wa chama cha Afya na Maendeleo kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (SHDEPHA+), Bw. Joseph Katto, amewashauri vijana walioathirika na ugonjwa wa ukimwi kuwa wazi kwa wenzao ambao hawajaathirika ili kuepuka maambukizo ya makusudi.

Bw. Katto aliyasema hayo wakati akizungumza na vijana walio katika kikundi kinachohusika na masuala ya kupiga vita ugonjwa wa Ukimwi nchini TAYOTA katika tamasha lililofanyika katika ukumbi wa Don Bosco jijini Dar-Es-Salaam, lilowashirikisha vijana kutoka katika shule mbalimbali, mashirika na taasisi za kidini.

"Wengi wenu yazungumzwayo kuhusu ukimwi yanawafikia, mnayapata lakini, mnayapuuza. Ni kwa sababu ya ufinyu wa kutambua mtu aliyeathirika na virusi vya ukimwi," alisema Bw. Katto.

Alisema vijana hawana budi kuachana na vitendo vya uasherati na kujishirikisha na tendo la ndoa kabla au nje ya ndoa zao ili kuwajibika, kujithamini, kujiheshimu kwa kufuata maadili mema yatakayo zinusuru afya na maisha kwa kufuata misingi ya malezi ya kidini, wazazi na taifa kwa ujumla.

Bw. Katto aliwashauri kuwa inawabidi vijana kusimama wenyewe kudai na kushiriki kuboresha mazingira wanayoishi ili weze huru na kujipatia haki juu ya maisha yao.

Alitoa mfano wa mambo wanayopaswa kuwa huru nayo kuwa ni pamoja na kulazimishwa kuoa, kuolewa na kurithishwa wajane, tohara kwa vijana (wa kike)na uhuru wa kutoa na kutosikilizwa maoni yao.

Tamasha hilo pia lilihudhuriwa na viongozi wa dini ambapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) liliwakilishwa na katibu mtendaji wa Idara ya Elimu padre Elias Msemwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania liliwakilishwa na Sheikh Hassan Chizenga.

Tumieni elimu, nguvu kulinda maadili- Wito

Na Charles Hililla, Shinyanga

VIJANA wametakiwa kutumia elimu na nguvu zao kwa ajili ya kulinda maadili ya taifa na kutetea haki za raia badala ya kukalia kuiga tamaduni za kigeni zinazopotosha mila na utamaduni njema za mababu.

Wito huo ulitolewa na Askofu Aloysius Balina, wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, wakati akihubiri katika ibada ya Jubilei Kuu ya Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) iliyofanyika kijimbo katika Kanisa Kuu la Jimbo la Shinyanga.

Ibada hiyo ya hivi karibuni ilitanguliwa na mfungo ya siku moja kwa VIWAWA wa jimbo hilo siku ya kilele vijana hao walitembea kwa maandamano umbali wa kilometa sita kutoka parokia za Buhangija, Shinyanga Mjini na Ngokolo ilikofanyika ibada.

Askofu Balina aliwaambia vijana kufuata mafundisho mbalimbali yanayotolewa na wazazi wao, walezi walimu na viongozi wao ili kujiwekea hazina ya kuwa walimu wa maadili mema kwa vizazi vingine.

Askofu aliilaani tabia ya baadhi ya wazazi kutotimiza wajibu kwa watoto wao kwa kuwa mzazi ana wajibu wa moja kwa moja kumpa mtoto malezi bora ikiwa ni pamoja na kumpa mahitaji muhimu ya kijamii kama elimu, chakula, malazi, mavazi, afya na maadili mema.

Askofu Balina alisema kuwa mzazi asiyefanya hayo kwa mtoto wake, anakuwa hatimizi wajibu wake kwa Mungu kwa kuwa hawatunzi wala kuwalea watoto kama sheria ya Mungu inavyosema na hivyo, wao wenyewe kuwa vyanzo vya kuharibikiwa kwa watoto hao.

Alisema mzazi anayemuacha mtoto wake bila kumtimizia wajibu huo, anakuwa hana tofauti na ndege na wanyama ambao wakisha zaa, huwa wanaona wamemaliza kazi. Alisisitiza kuwa maisha ya ndoa si kuzaa kuzaa tu bila kutoa malezi bora kwa watoto.

Kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka huu aliwaambia vijana hao kutumia haki yao kikatiba kujiandikisha na kisha kuchagua viongozi wanaofaa kuwaongoza na kamwe wasithubutu kuchagua viongozi wanaotumia rushwa kuwarubuni watu ili wawapigie kura.

Misa hiyo ya Jubilei ya vijana ilihudhuriwa na vijana wapatao 200 kutoka parokia mbalimbali za jimbo la Shinyanga.

Vijana walisema wamefurahishwa na mafundisho ya kiroho waliyopewa siku moja kabla ya ibada hiyo ya Agosti 20 mwaka huu,yalitolewa na Padre Charles Bundu na wakaahidi kufanya mafungo ya namna hiyo mara kwa mara.

Semina hiyo ilifadhiliwa na nchi za Ulaya ambazo ni Finland, Norway, Netherland, Ireland, Dernmark na Uingereza kwa lengo la kuhamasisha Watanzania umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika suala zima la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.

Kanisa laitahadharisha Serikali juu ya njaa Kanda ya Ziwa

Na Steven Mchongi, Mwanza

KANISA la African Inland Church Tanzania (AICT), limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa ukame na njaa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na baa hilo.

Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Sinodi wa Kanisa hilo mjini Shinyanga, na nakala yake kupatikana hapa jijini Mwanza, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, John Nkolla alisema janga hilo ni tatizo linalohitaji juhudi za haraka za kitaifa.

"Tatizo hilo la ukame na njaa liko nje ya uwezo wa Askofu na linahitaji juhudi za kitaifa’, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi sasa inakabiliwa na njaa kali kufuatia kutonyesha mvua za masika kwa muda mrefu jambo ambalo limesababisha kunyauka kwa mazao ya chakula.

Aidha, kanisa hilo la AICT limepokea msaada wa shilingi 100,226,504 kutoka kwa wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii hasa kilimo.

Hivi karibuni chini ya ufadhili wa shirika la DWHH na serikali ya Ujerumani kanisa hilo liliweza kutoa msaada wa chakula kwa vijiji vya Mihama, Baledi, Lagama na Mwanadhulu mkoani Shinyanga.

Katika msaada huo, wakulima waligawiwa tani tisa za mbegu ya mtama na majembe 700 ya mkono ambapo kutokana na msaada huo ekari 235 za mtama zililimwa wilayani Shinyanga.

Nalo shirika la Tear Fund lililotoa tani 75 za mahindi aina ya "kilima", tani sita za maharage na 30 za mtama kwa vijiji vya Mwakipoya, Ilula, Ngema na Kishapu.

Misaada mingine ya kijamii iliyotolewa kupitia ka kanisa hilo la AICT ni kutoka kwa mashirika ya Arther Foundation, Presbyterian World Service and Development na Kurugenzi ya Maafa na Wakimbizi ya CCT.

Hongera Padre Beda Pavel, Hongera wakatekista na hongera parokia ya Kilimahewa

Na Pd. Raphael Kilumanga

Mheshimiwa Padre Beda Pavel, mwanashirika Mbenediktini na paroko wa Kilimahewa, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Agosti 27, mwaka huu, aliadhimisha Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre.

Sambamba na sherehe za paroko huyo muasisi, Kilimahewa ilisheherekea pia mwaka mmoja tangu ifunguliwe Septemba 3, mwaka jana na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Aidha, siku hiyo ilikuwa pia ni sherehe za Wakatekista wa parokia hiyo.

Akizungumza wakati wa ibada ya misa iliyoongozwa na Pd. Beda, Monsinyori Deogratias Mbiku, ambaye ni paroko wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam, aliwataka waamini wa Kilimahewa washirikiane na Padre Beda katika kazi ya Wokovu.

"Padre Beda ametumwa kuhubiri Habari Njema na siyo kuja kustarehe. Ameteuliwa ili azae matunda ya kudumu kama umoja, amani, utulivu, upendo, haki na upatanisho," alisema Monsinyori Mbiku na kuwataka waamini washirikiane naye kwa kuiishi imani ya Kikristo.

Aliwataka watu waidhihirishe imani inayoambatana na matendo ili kuonesha kuwa Wakristo wamekubali Wokovu.

Aidha, Monsinyori Mbiku aliwataka waamini wawe chumvi ya dunia kwa kuwavuta walegevu.

Vilevile Monsinyori huyo aliwaomba Wakristo wamuombee Padre Beda na kuwakumbusha kuwa padre huyo aliletwa Tanzania kama chombo chake kwa ajili ya watu na wamshukuru Mungu kwa ajili ya karama za Padre Beda zinazowanufaisha siyo kanisa la Kilimahewa tu, bali pia kanisa la ulimwengu mzima.

Kiongozi huyo pia alimshukuru Padre Beda kwa kukubali uteuzi wa Mungu kwa ajili ya watu.

Katika risala ya wanaparokia, Padre Beda alielezwa kuwa ni mtu wa upendo, msikivu, huruma kwa wanyonge na hivyo anajulikana parokiani hapo kwa jina la "Mzee au Bwana Chochote" kutokana na moyo wake wa ukarimu.

Padre Beda ameelezwa kuwa ni mtu anayependa maendeleo ya watu kielimu, kiafya na kiuchumi licha ya kidini.

Alizaliwa Juni 7, 1935 Budweis, Ujerumani; alipadrishwa Juni 29, 1960 na aliyekuwa Askofu Abate wa Abasia ya Ndanda.

Miaka 1961-1963 alikuwa Uingereza kwa masomo ya ualimu na Oktoba 1963, alitumwa Tanganyika na kuanza Umisionari akiwa mwalimu kwa miaka miwili katika Seminari ya Likonde, Mbinga.

Baadaye kati ya 1968 hadi 1976, alifundisha katika Seminari ya Namupa Jimbo la Lindi.

Kisha, mwaka 1976 - 1985 alikuwa Seminari ya Soni katika Jimbo Katoliki la Tanga akiwa muasisi wa seminari hiyo.

Miaka ya 1985 - 1998, alikuwa makao ya Wabenediktini, Kurasini Dar-Es-Salaam, akiwa Mkuu wa nyumba ya Watawa na wakati huo huo kuanzia mwaka 1987, alikuwa anakwenda Kilimahewa ambacho kilikuwa ni Kigango cha Mbagala.

Mwaka 1999, aliwekwa kuwa paroko wa Kilimahewa yenye msimamizi wake Bikira Maria Malkia wa Mbingu.

Akiwashukuru waamini waliofurika kumpongeza ambao baadhi yao walitoka Jimbo katoliki la Tanga na baadhi yao wakiwa ni wanafunzi wake wa zamani, padre beda alitaka pia pamoja naye, wapongezwe wale wote waliofanya jubilei mwaka 2000.

Miongoni mwa mwao walikuwa ni padre Stephen Nyirawi, paroko wa Pugu, aliyeadhimisha miaka 25 yaupadre na Brigedia msataafu mbena aliyeadhimisha miaka 45 ya ndoa.

Kilimahewa ipo katika kata ya Kimanzichana Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Ina wakazi kati ya 50-60,000 wengi wao ni Wandengereko na wachache ni Wamakonde. Katika hao Wakatoliki ni 3,000; wapo wakatekista kamili sita na wasaidizi wao wanaofanya kazi katika vigango tisa.

Zipo Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kati ya 18-20.

Pamoja na upya wa Parokia hiyo, Ukristo unapamba moto na mmoja wa Wakatekista ameeleza kuwa msalaba wa Jubilei Kuu umefanyakazi kubwa ya kuvuta watu kupokea Sakramenti.