Wapinzani tusijivunie kifo cha Nyerere -CUF

lBado tuna kazi ngumu kuing'oa CCM

Na Getruder Madembwe

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema licha ya mwasisi mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kufariki dunia, bado vyama vya upinzani vina kazi kubwa ili kuweza kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2000.

Katibu Mwenezi wa Chama Cha Wananchi (CUF) Bw. Ramadhani Mzee aliliambia gazeti hili ofisini kwake jana kuwa vyama vya upinzani bado vinayo kazi kubwa kuiondoa CCM madarakani ingawa Mwalimu Nyerere aliyekuwa mpigadebe mashuhuri na maarufu wa chama hicho amefariki. Alisema Mwalimu aliisaidia CCM kujijengea msingi imara ambao unahitaji kazi kubwa kuubomoa.

"Sio kwamba sasa Uchaguzi ujao utakuwa rahisi kwa wapinzani na hivyo tutaipiku CCM kirahisi kutokana na kifo cha Nyerere, labda tuwe na msimamo wa uhakika," alisema Katibu huyo Mwenezi wa chama upinzani kuongeza. "Wapinzani tusijivune eti sababu Mwalimu amefariki tutashinda uchaguzi ujao. Kwanza kutamani watu wafe ndipo usherehekee kwamba utashinda katika siasa, huo utakuwa sio upinzani ni unyama,"alisema Bw. Ramadhani.

Aliisifu CCM na kusema wanajitahidi kurekebisha baadhi ya mambo waliyoahidi wakati Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 1995 ambayo hakutaka kuyataja.

"Hilo sisi tumeligundua sababu wao CCM wamefahamu udhaifu wao upo wapi na ndiyo maana wameanza kujirekebisha" alisema Ramadhani Mzee.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 1995 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipanda jukwaani na kuisaidia CCM katika kampeni. Katika kampeni zake Mwalimu ambaye alikuwa na ushawishi (influence) mkubwa kwa Watanzania alibadili kabisa mwelekeo wa wananchi wengi ambao awali walipania kuiondoa CCM madarakani pengine tu kwa kuwa na msisimko wa kutaka mabadiliko.

Watu kadhaa wamekuwa wakinong'ona kwamba huenda Chama cha Mapinduzi kikadhoofu na kupoteza mshikamano wake baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere na hivyo kutoa nafasi kwa wapinzani kuingia Ikulu kirahisi.

Baadhi ya wachunguzi wa masuala ya kisiasa pia wamekuwa wakitabiri kwamba huenda Muungano wa Tanzania ukatetereka au kuvunjika kufuatia kifo hiki cha mwasisi wake, lakini Rais Benjamin Mkapa aliwahakikishia Watanzania wakati alipokuwa akitangaza kifo cha Baba wa Taifa, Oktoba 14, kuwa Tanzania itaendelea kuwa imara kwa misingi ile ile iliyojengwa na Baba wa Tiafa na hakuna kitu kama kuvunjika kwa Muungano.

 

Tanzania haitaporomoka kama nyumba ya karata - Mwinyi

Na Mwandishi Wetu

RAIS Mstaafu wa awamu ya pili Mheshomiwa Ali Hassani Mwinyi amesema pamoja na umuhimu mkubwa aliokuwa nao Mwalimu Julius Nyerere katika uhai wake kwa tifa hili, Tanzania haitaporomoka kirahisi kama alichokiita "nyumba ya karata"

Mheshimiwa Mwinyi alisema jana jioni kwamba pamoja na kwamba taifa limepata msiba mkubwa lakini msingi madhubuti wa Taifa aliyoujenga Mwalimu Nyerere katika Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chenye serikali ni kama "Mwamba usiotikisika"

Mwinyi ambaye alikuwa akiongea na shirika la habari la Uingereza kwa njia ya simu alisema hata viongozi wa vyama vya upinzani nchini hawatarajiwei kusababisha matatizo kwa vile wao pia walikuwa wanafunzi wa siasa wa Mwalimu Nyerere kama walivyo wenzao wa CCM.

Juu ya pengo lololoachwa na Mwalimu Nyerere katika usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Mwinyi alisema anaamini kuwa mazungumzo ya mgogoro huo yatafika mwisho mwema kwa vile Mwalimu Nyerere alikwishafanya sehemu kubwa ya kazi hiyo.

Alisema mahali alipofika Mwalimu Nyerere ni sawa na mvuvi aliyekwisha sogeza mtumbwi wake hadi karibu na pwani ambapo mwingine anakuwa na kazi ndogo sana ya kutia nanga ufukweni.

Mwinyi pia alimsifu Mwalimu Nyerere kama mtu aliyejenga Umoja wa kitaifa na kuondoa ubaguzi wa kidini , rangi na kadhalika, jambo ambalo halitasahaulika kamwe.

 

... Mwalimu kuzikwa Jumamosi

MWILI wa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam Jumatatu Oktoba 18 na atazikwa Jumamosi ijayo nyumbani kwake Butiama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jana mwili huo utawasili ukitokea nchini Uingereza kwa ndege maalum iliyokodiwa na serikali ambapo utawekwa kwenye jukwaa na mizinga 21 kupigwa kwa heshima yake.

Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya hapo mwili wa marehemu utapelekwa moja kwa moja nyumbani kwake Msasani ukiwa umebebwa katika gari maalum la Jeshi ambalo litatoa nafasi kwa wananchi kuliona jeneza lake.

Jumanne Oktoba 19 mwili wa Mwalimu utapelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu jiji kwa ajili ya misa kisha atapelekwa katika Uwanja wa Taifa kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho.

Siku ya Alhamisi itakuwa maalum kwa ajili ya wakuu wa nchi kutoa heshima zao kabla ya mwili huo kusafirishwa kwa ndege kwenda Musoma ambako kutakuwa na siku mbili za wananchi wa huko kutoa heshima zao za mwisho. Mwili Mwalimu hatimaye utazikwa kijijini kwake Butiama Jumamosi ya Oktoba 23, 1999.

Taarifa ya Ikulu pia imetangaza kuundwa kwa Kamati itakayosimamia utaratibu wote wa mazishi ikiongozwa na Waziri Mkuu Bw.Frederick Sumaye. Wajumbe wengine katika kamati hiyo ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Bw.Pius Msekwa, Waziri Kiongozi wa Zanzibar Bw.Mohamed Billar, Waziri wa Ulinzi Bw. Edgar Maokola Majogo, Waziri wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa Bw.Kingunge Ngombale Mwiru, Jaji Mkuu Bw.Francis Nyalali, , ,Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bw.Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri wa Mambo ya Ndani Bw.Ali Ameir Mohamed.

Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi Bw. Martini Lumbanga, Jaji Joseph Warioba Kanali Mstaafu Bw. Abdalah Natepe Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Bw. Wilson Masilingi, Waziri wa Nchi wa Zanzibar Bw. Mohamedi Ramia, , Waziri wa Fedha Bw. Danieli Yona Waziri wa Ujenzi Bi.Anna Abdalah, , Mshauri wa Rais wa Mambo ya Siasa Kanali Moses Nauye

Mhesimiwa Mkapa pia ameteua Kamati ya Utendaji ya Kamati ya Matayarisho ya Mazishi itakayo ongozwa na Bw. Lumbanga katika utendaji wake.

Amewataja wajumbe wengine katika kamati hiyo ya watu 13 kuwa ni pamoja na makatibu wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, Wizara za Utumishi, Mambo ya Nje, Fedha, Ulinzi, Mambo ya Ndani, wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa Tume ya Jiji na Mwandishi wa Habari wa Rais.

Kamati hii inategemewa kuandaa utaratibu mzima ikiwa ni pamoja na kupanga na kuratibu mapokezi na tarehe ya mazishi ya mwili wa Mwalimu.

WAKATI HUO HUO:Kamati Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) imewaomba Watanzania kutumia muda huu wa majonzi kuimarisha mshikamano, upendo, udugu na Umoja wa Kitaifa, utulivu na amani.

Akihutubia wandishi wa habari mara baada ya kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Ikulu chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw.Philip Mangula amewataka Watanzania kuondoa hofu kuwa kufuatia kifo cha Mwalimu, huenda misingi ya amani,upendo na utulivu aliyoijenga vitaathirika.

Mwalimu Nyerere alifariki Oktoba 14, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London, Uingereza ambako alilazwa tangu Septemba 24, mwaka huu akisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya damu.

Zahanati ya parokia Bagamoyo kuwa Kituo cha Afya

Na Dalphina Rubyema

PAROKIA ya Bagamoyo iliyopo katika Jimbo la Morogoro inatarajia kubadilisha zahanati yake kuwa kituo kamili cha afya;imefahamika.

Daktari wa zahanati hiyo, Dk.Conrad Guandu, alisema hivi karibuni ofisini kwake kuwa hivi sasa parokia inatafuta usajili wa kituo hicho cha afya na kuongeza kuwa vifaa na mahitaji mengine ya kutolea huduma vimekwishapatikana.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vitanda vya kutosha kulaza wagonjwa 50, chumba na vifaa vyote vya maabara, chumba cha X-ray, chumba cha meno (dental room) pamoja na vifaa vingine muhimu kwa kituo chochote cha afya.

Alisema hivi sasa kinachokosekana ni chumba cha upasuaji (theatre) na vifaa vyake. Hata hivyo alisema tayari ujenzi wa chumba hicho umeanza na kwamba wapo wafadhili waliokwisha jitokeza kuleta vifaa.

Akizungumzia zahanati iliyopo parokiani hapo, Dk.Guandu alisema hivi sasa ina uwezo wa kutoa huduma zote za matibabu kama zilivyo hospitali nyingine ambazo zimekwisha pita ngazi ya zahanati.

"Zahanati yetu inavyo vifaa vya kutosha na inaweza kulaza hata wagonjwa lakini kwa vile serikali inakataza kufanya hivyo basi wagonjwa katika zahanati yetu wanapumzishwa tu. Kwa siku tunaweza tukapata kati ya wagonjwa 25-50"alisema Dk.Guandu.

Alisema zahanati hiyo inatoa nusu ya huduma za afya kwa wakazi wa Bagamoyo ambapo nusu iliyobaki hutolewa na hospitali nyingine ikiwemo ile ya wilaya ambayo mara nyingi inapoishiwa, huomba msaada katika hospitali hiyo ambayo mara nyingi huwa na madawa ya kutosha kwa muda mwingi.

Alifafanua kuwa hadi hivi sasa zahanati yake ina wateja wa kudumu kutoka mashirika na makampuni mbalimbali likiwemo Shirika la Umeme nchni (TANESCO), Kampuni ya Simu nchini (TCCL),Mamlaka ya Maji na Kampuni ya Paradise.

Alisema wateja binafsi wa siku nyingi na wa kudumu wanapewa kadi maalum ili waweze kupata matibabu pasipo usumbufu.

Zahanati hiyo pia ina wodi inayojulikana kama Mtakatifu Theresia ambapo akina mama wagonjwa na wajawazito hupumzishwa. Ina jumla ya wafanyakazi 12 akiwemo Dk. Guandu mwenyewe ,wasaidizi wa daktari watatu, wauguzi wawili, msaidi wa wauguzi mmoja na mhudumu wa maabara mmoja.

 

Wajawazito 400 hufa kila mwaka Kisarawe

Na Josephs Sabinus, Kisarawe

WAJAWAZITO 400 kati ya wanawake 100,000 ambayo ni sawa na asilimia 2 ya wanawake wazima hufa kila mwaka wilayani hapa kutokana na matatizo mbalimbali ya uzazi yanayosababishwa na mambo mbalimbali likiwemo kubwa la kuzalia nyumbani bila kufuata kanuni za kitaalamu; Kiongozi limegundua.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dk. Ahmed M.Mtambo alisema mjini hapa hivi karibuni wakati akifunga semina ya majuma matatu kwa wakunga wa jadi 30 na watumishi wa afya 16 iliyoandaliwa na hospitali yake na kudhaminiwa na shirika la kimataifa la PLAN INTERNATIONAL juu ya uzazi salama ili kupunguza vifo hivyo kuwa akina mama wajawazito hawana budi kuhudhuria kliniki mara tu wanapojitambua kuwa wajawazito ili wapimwe na kupewa ushauri na huduma za kitaalamu.

Alisema wakunga wa jadi hawapaswi kubeba majukumu ya kuzalisha wajawazito majumbani na badala yake wanapaswa kuwa changamoto kwa akinamama hao kuhudhuria kliniki na kwamba lengo la semina hiyo sio kuwachochea kufanya hivyo bali ni kuwapa elimu ili inapolazimu kuwasaidia wajawazito kabla ya kufika hospitali, wawe na ujuzi kidogo wa kusaidia kitaalamu ili kupunguza vifo.

"Hatuwazuii wakunga wa jadi kutoa msaada pale inapobidi na pia hatuwasisitizi kubeba jukumu la kuzalisha huko majumbani bali tunawapa ujuzi ili inapotokea dharura, waweze kusaidia kitaalamu na hivyo kupunguza uwezekano wa vifo, na maambukizo kwa wajawazito, watoto na wakunga wenyewe", alisema Dk.Mtambo.

Alisema semina hiyo iliyowashirikisha wakunga wa jadi toka vijiji vya Msimbu, Homboza, Gumba na Kisanga ililenga pia kuwaepusha watoto kutokana na maambukizo ya magonjwa mbalimbali kama tetenas.

"Endapo mjamzito ana ukimwi na mkunga hana mipira ya kuvaa mikononi, kama ana michubuko mikononi anaweza kuambukizwa; au mtoto kama hakuhudumiwa kitaalamu wakati wa kuzaliwa ipo hatari ya kuambukizwa tetenus. Ndiyo maana baada ya semina, wakunga hupewa baadhi ya vifaa muhimu vya uzazi," alisema.

Alitoa wito kwa wajawazito kuhudhuria hospitali bila kuhofu gharama kwani huduma zote za wajawazito na watoto wadogo zinatolewa bure zinatolewa bure na akabainisha kuwa lengo la hospitali yake ni kupunguza vifo hivyo kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kwa 50% ifikapo mwaka 2001.

Wakati huo huo, Mganga huyo wa Wilaya amesema ukosefu wa huduma ya chakula kwa wagonjwa unawakwaza wagonjwa kufika hospitalini kwani baadhi yao huogopa gharama za chakula wanapolazwa na hivyo kulazimika kuugulia nyumbani na wengine kutoroka hospitalini kukwepa gharama wawapo hospitalini.

Katika tukio jingine: utafiti uliofanywa na hospitali hiyo katika shule 12 za msingi katika tarafa za Chole na Mzenga kwa kutumia michezo ya sanaa za maonesho yakiwezo maigizo, hivi karibuni umebain kuwa zaidi ya 70% ya wanafunzi hao wapato 450 wameanza kutambua athari, njia za maambukizo na namna ya kujikinga na ukimwi.

 

Ndoa 91 zafungwa kwa mpigo kanisani

Na Peter Dominic

JUMLA ya ndoa 91 zimefungwa katika Parokia ya Msimbazi iliyopo Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kwa kipindi cha majuma mawili ikiwa ni kutimiza lengo la parokia hiyo la kuwapa unafuu waamini wake kupata sakramenti hiyo ili kujiandaa vema kusherekea Jubilei Kuu ifikapo mwaka 2000.

Akiogea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Paroko wa parokia hiyo Padre Sergi Tarimo alisema parokia yake imeamua kuondoa vizuizi vinavyowabana Wakristo wanaotaka kufunga ndoa ili kuwapa mwanya kuzibariki ndoa zao ili kuingia Jubilei Kuu bila vizuizi vya sakramenti vinavyowafanya hata baadhi ya watoto kunyimwa sakramenti za msingi.

"Tumegundua kuwa Wakristo wengi wanashindwa kubariki ndoa zao kwa kukosa shilingi 21,500 hivyo tumefuta gharama nyingine na kubakiza sh.5500/= kwa ajili ya kulipia cheti cha ndoa", alisema na kuongeza kuwa hali hiyo ndiyo iliyowafanya waamini wajitokeze kwa wingi ili kubariki ndoa zao baada ya kutangaziwa kiwango hicho."

Toka Parokia hiyo ilipotangaza utaratibu wa kufungisha ndoa hizo maarufu kama "Ndoa Poa" waamini wamekuwa wakimiminika katika parokiani hiyo wakitaka kujiandikisha kwa ajili ya kubariki ndoa zao.

Hata hivyo paroko huyo alifafanua kuwa utaratibu wa kufungisha ndoa kwa pamoja sio wa kudumu kwa vile hufanyika mara moja kwa mwaka na akasisitiza kuwa kwa wale ambao hawakupata nafasi hiyo watalazimika kulipia gharama zote kama ilivyo kawaida.

Akifafanua gharama za kulipia sakramenti ya ndoa kama ilivyo kwa utaratibu uliowekwa na parokia hiyo Fr,Tarimo Sergi alisema ili kupata sakramenti ya ndoa muumini atatakiwa kulipa gharama hizo kama alivyofafanua kwa viwango, shilingi 5500 kwa ajili ya cheti cha ndoa,5000 kwa ajili ya kwaya itakayoimba katika ibada hiyo ,4000 kwa ajili ya semina ya ndoa,1000 kulipia misa ya ndoa na shilingi 5000 ada ya ndoa.

Aliwaonya wenye tabia ya kuwa na "nyumba ndogo" waache na kuogeza kuwa jambo hilo limekuwa likikwamisha juhudi za Kanisa kupata mafanikio kwa vile watu hao ni wagumu kuitika mwito wa ndoa kwa vile wanajua kufanya hivyo ni kuweka nadhiri za kudumu na aliyefanya hivyo haruhusiwi kumuacha mke wala kuwa na mke mwingine labda kutokana na kifo cha mmoja wao.

Tujenge mazingira mazuri kujitegemea - Walemavu

Na Mwandishi Wetu

Jamii imeshauri kuwajengea walemavu mazingira yatakayotambua na kuzingatia kikamilifu mahitaji yao ili wawe changamoto katika kuboresha maisha kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar es Salaam hivi karibuni na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Bw. Hosea Kalumuna alipokuwa akizungimza na gazet hili ofisini kwake.

Alisema kimsingi walemavu ni watu wenye upungufu wa viungo vya mwili na hivyo wanastahili kusaidiwa lakini akasema kuwapa fedha na chakula tu kwa muda sio ufumbuzi wa kudumu wa matatizo yao bali jamii iwaendeleze kielimu na huduma nyingine muhimu ili watumie vipawa vyao kupata mwanga na hivyo kukabiliana na maisha kulingana na hali zao.

"Kumpa sh.100/=, kipande cha muhogo au kanga sio kumsaidia mlemavu na wala sio suluhisho la kumuondolea adha.Sio kwamba mlemavu hawezi kufanya kazi ya maendeleo;anaweza ila tatizo ni kwamba jamii imejenga kasumba mbaya kudhani kuwa tangu anapozaliwa, mlemavu ni mtu wa kusaidiwa tu.

Mtazamo huo umechangia kurudisha nyuma maendeleo ya jamii na pia umepitwa na wakati. Mbona mimi ni mlemavu lakini nimesoma hadi chuo kikuu na sasa nimeajiriwa serikalini ninawatumikia Watanzania."alihoji mwenyekiti huyo ambaye ni mlemavu wa macho asiyeona.

Ameitaka jamii kuwahusisha walemavu katika mabaraza na nyadhifa mbalimbali ili waeleze matatizo yao na kujifunza mbinu za kukubiliana na maisha kulingana na aina zao za ulemavu.

SHIVYAWATA ni shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu ambavyo ni Chama Cha Maalbino (CCMT),Chama cha Wasiona (T.L.B) na Chama cha wenye Ulemavu wa Akili (TAMH).Lengo la shirikisho hili ni kuleta na kuimarisha mshikamano wa pamoja wa vyama hivyo.

 

Wizara ya Elimu yasitisha sherehe Bara

Na Dalphina Rubyema

KUFUATIA kifo cha Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, shughuli zote za mahafali kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya mafunzo ya ualimu Tanzania Bara zimesitishwa hadi baada ya kipindi cha maombolezo kumalizika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Utamaduni kupitia Idara ya Habari (MAELEZO) jijini, wakuu wote wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu Tanzania Bara wametakiwa kufanya sherehe zote na kukabidhi vyeti vya kwa wahitimu baada ya muda wa maombolezo.

Hata hivyo taarifa hiyo haikufafanua kwanini wanafunzi wa taasisi husika huko Tanzania Visiwani hawakutajwa kuhusika katika agizo hilo.

Kufuatia kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, serikali imetangaza siku 30 tangu kifo hicho kilichotokea Oktoba 14 kwa ajili ya maombolezo na kwa kipindi hicho bendera zote nchini zitapepea nusu mlingoti.

WAKATI HUO HUO: Rais ya Jamuhuri ya Nchi ya Burundi Meja Pierre Buyoya amemtumia salaam za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamini Mkapa na Watanzania wote kwa ujumla kufuatia kifo cha Muasisi wa Chama cha Mapinduzi.

Katika taarifa yake iliyotolewa jijini, Meja Burundi imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwalimu na kumuelezea kama mtu aliyekuwa kiungo muhimu si kwa Wanzania tu, bali hata kwa Afrika na Ulimwengu mzima kwa ujumla.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia siku ya Alhamisi saa 4.30 asubuhi katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas Mjini London alipokuwa amelazwa kufuatia kuugua ugonjwa wa kansa ya damu..

CCBRT yawatibu bure watoto wenye matatizo ya macho

Na Neema Dawson

SHIRIKA moja la kuhudumia Walemavu Tanzania (CCBRT) lililopo Mwananyamala jijini linaendelea kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu kwa wadogo wenye matatizo ya macho ili waweze kuona na kwenda shuleni kusoma.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Bi. Mary Dunstan; mmoja wa wanao wahudumia wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo alisema kuwa shirika hilo linatoa huduma za macho bure kwa watoto wote walio na umri chini ya miaka 14 bila gharama zozote na kuwafanyia uchunguzi na tiba ukiwemoupasuaji.

Alisema huduma hizo zinatolewa pia katika mikoa mingine hapa nchini.Alifafanua kuwa kwa watoto huduma za kumuona daktari na kupatiwa dawa ni bure. Isipokuwa kwa yule anayetakiwa kufanyiwa upasuaji atakayetakiwa kuchangia nusu ya gharama ili apatiwe miwani.

‘’Kama miwani inagharimu sh. 8,000 mgonjwa, atatakiwa kuchangia sh.4,000 gharama nyingine mgonjwa ataongezewa na CCBRT ."alisema.

Aliongeza kuwa endapo wazazi wa mtoto hawawezi kabisa kumudu gharama hizo, CCBRT watajitahidi kumsaidia mtoto huyo ili asizidi kuathirika.

Aliongeza kuwa wagonjwa miaka zaidi ya 14 watachangia gharama zote ikiwa ni pamoja na kumuona daktari, matibabu na miwani bila kusaidiwa na CCBRT.

BI. Mary aliongeza kuwa huduma hizo zinatolewa katika vituo mbalimbali ( mobile Clinic) na jijini Dar Es Salaam huduma hizo zinatolewa Mwananyamala . Huduma kamili zitolewazo na CCBRT ni upimaji wa macho, utaji dawa, miwani na upasuaji mdogo. Wagonjwa wenye matatizo makubwa yanayohitaji upasuaji wa mtoto wa jicho.

Mtoto wa jicho (CATARACT) ,Glaucoma , Trachoma ni magonjwa ya macho ambayo yasipotibiwa mapema yanaweza kusababisha upofu.