BAADA YA MWAKA TANGU KIFO CHA NYERERE

KKKT wagongana na Wakatoliki

lWasema mkapa hana tofauti na Nyerere

lWakatoliki wasema Nyerere angekuwapo, rushwa isingetawala kura za maoni CCM

Getrude Madembwe na Leocardia Moswery

WAKATI Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limesema halioni tofauti ya kabla na baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Wakatoliki wamemlilia Nyerere na kusema angekuwa hai, rushwa iliyotawala waziwazi wakati wa kura za maoni za CCM, angeikemea mapema.

Mawazo hayo ya makanisa yalitofautiana wakati Gazeti la KIONGOZI lilipozungumza na viongozi wa makanisa hayo kwa nyakati tofauti jijini Dar-Es-Salaam, ili kujua tofauti walizogundua tangu kifo cha hayati Nyerere Oktoba mwaka jana.

Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT, Mchungaji Adam Kombo, alisema kanisa lake halioni tofauti yoyote baina ya enzi za uhai wa baba wa Taifa, na Rais wa sasa, Benjamin Mkapa.

"Sisi hatuoni mabadiliko yoyote baina ya Rais wa Awamu ya Tatu, na yule wa Awamu ya Kwanza. Mkapa anaheshimu sana misingi aliyoiacha Baba wa Taifa. Haendi kinyume kama wengi walivyodhani," alisema.

Mchungaji Kombo alidai kuwa licha ya kuwa na vyama vingi hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, bado amani na utulivu vinadumu na serikali inaelekeza nguvu zake katika kuimarisha amani hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Padre Pius Rutechura, alisema kuwa hali ya kutanda kwa rushwa iliyoonekana wakati wa kura za maoni za Chama Tawala, ingekemewa mara moja kabla haijajitokeza kama Marehemu Baba wa Taifa angekuwa hai na hivyo isingeonekana hadharani namna hiyo kama kwamba ni kitu halali.

"Siyo kwamba enzi za Nyerere hapakuwa na rushwa ila, isingeweza kuonekana waziwazi kama ilivyo sasa," alisema Padre Rutechura.

Aliishauri serikali kuchimbua mizizi yote ya rushwa badala ya kung’ang’ania kukata matawi. "Rushwa kama rushwa ipo. Kinachotakiwa ni kuichimbua mizizi yake kwa kuwa huwezi kusema kuna wadudu bila kuchimbua chini kuhakikisha umemaliza vyanzo vyote," alisema.

Aidha, Padre Rutechura aliwaasa viongozi wa dini kuepukana na kampeni za kisiasa kwa kuwa ni hatari na zinaweza kuleta mgawanyiko endapo kiongozi aliyepigiwa kampeni atashinda na kufanya mambo kinyume na kiongozi huyo wa dini alivyowaaminisha waamini wake wakati akimpigia debe mgombea.

Alisema, kama viongozi wa dini, wana wajibu wa kukemea na mambo yanayokwenda kinyume katika jamii na akaitaka jamii isiwatenge viongozi wa dini katika kukemea maovu kwa kuwa na wenyewe ni watu ndani ya jamii.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alifariki Oktoba 14, mwaka jana katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko London, Uingereza. Jumamosi hii Watanzania wanaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo chake.

Wakati huo huo: KKKT dayosisi ya Mashariki na Pwani, inatarajia kueneza Injili katika maeneo ya Uzaramoni na Zanzibar ili wakati wa maeneo hayo wanufaike kiroho.

Katibu wa dayosisi hiyo, Bw. Eneza T. Abrahamu alizitaja sehemu hizo kuwa ni pamoja na Kisiwa cha Zanzibar, Kisarawe katika maeneo ya Mzenga, Gwata, Mtalayo, Maneromango na maeneo mengine yanayohitaji huduma hiyo ya kiroho.

Alisema KKKT itawatuma wainjilisti watakaotumia baiskeli kutoa huduma hiyo ya kiroho.

Mgombea ataka wanaokwenda bungeni kula chips, mishikaki wasichaguliwe

Na Peter Dominic

MGOMBEA ubunge kwa tikiti ya chama cha TLP Jimbo la la Temeke, Macmilian Lyimo, amewatahadharisha wananchi kutowachagua viongozi ili kujaza nafasi kwa kuwa hali hiyo ndiyo huwafanya baadhi ya viongozi kwenda kuzunguka bungeni wakitafuta kula mishikaki na chips.

Bw. Lyimo alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Wavuvi eneo la sabasaba katika manispaa ya Temeke hivi karibuni.

Alisema ili kupata mabadilko yatakayoleta ushindani wa kuleta maendeleo katika taifa, mabadiliko ya uongozi ni lazima kwani hata historia ya siasa duniani inaonesha kuwa maendeleo ya haraka huchochewa pia na ushindani na mabadiliko katika uongozi.

Alisema hata katika Maandiko Matakatifu imeelezwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye hutoa watawala na ndiye pia huwaondoa na hivyo wananchi hawana budi kushiriki kikamilifu kutekeleza wajibu wao wa kuwapigia kura wanaoona wanafaa kisha wamuachie Mungu awaamuriye mtawala bora.

Alisema kwa kawaida viongozi wanaochaguliwa kwa misingi ya ukabila, udini na lengo la kujaza nafasi, huwa hawawjibiki kwa wananchin abadala yake, hujineemesha wenyewe huku wakisahau wajibu wao kwa taifa.

‘Someni vitabu vitakatifu Mungu ndiye hutoa watawala na ndiye huwaondoa’ alisema Bw. Lyimo na kuwataka wananchi wasikumbatie viongozi wabovu kwa kusingizia hakuna viongozi wengine na kutawala badala yao.

Alisema siasa siyo ugomvi na kwamba watu wanapoigeuza kuwa ugomvi, ndipo mambo huenda mrama.

Aliwataka wapiga kura kuomba amani na kutumia busara zao kuhakikisha hawafanyi kosa katika zoezi la kupiga kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

Wapentekoste wawaacha Wamoraviani

lWasali Ibada moja ya mwisho

lViongozi watakiwa kuwa tayari kulaumiwa

lWasema Mungu ni tofauti na madiwani, wabunge

Na Josephs Sabinus

MWANGALIZI Mkuu wa Jimbo la Mashariki na Pwani wa Kanisa La Kipentekoste Tanzania(KLPT), Askofu Japhet Kyara, amesema viongozi yeyote sharti awe tayari kulaumiwa katika kuwatendea vema watu wake.

Pia amesema makanisa mengi, vikundi mbali mbali hata serikali na watu binafsi walianza vizuri lakini baada ya muda mfupi, vikundi vingi vilikufa, pesa zikaliwa na kutokea vurugu kwa kuwa watu wanashindwa kujinyenyekeza na kila mtu anataka kujiinua.

Aliyasema hayo wakati akiongoza ibada ya kuagana baina ya Kanisa La Pentekoste Tanzania, Parishi ya Kekomachungwa katika Jimbo la Mashariki na Pwani, na Kanisa la Moraviani Tanzania, usharika wa Keko Jimbo la Kusini Wilaya ya Mashariki, iliyofanyika katika kanisa hilo la Kipentekoste Jumapili iliyopita.

Alisema iwapo kila mmoja atakuwa mnyenyekevu kwa mwenzie, kutakuwa na ufanisi na amani katika utendaji wa kazi ya Mungu na kuongeza kuwa, kufanya hivyo kutaleta ushirikiano katika Kristo bila kujali majina wala madhehebu.

Alikwisha ahidi kukupokea ukimgeukia."

Katika ibada hiyo, Mchungaji Salatieli Mwakamyanda wa Moraviani Keko, alisema umoja katika Kristo ndio uliowatuma Wamoraviani kutokuomba hifadhi ya ibada katika maeneo mengine kama shule na badala yake, wakawaomba Wapentekoste wa Keko waliowapa hifadhi.

"Watu wengi Wakristo na wasio Wakristo, walipoona mumetukaribisha kufanya ibada zetu hapa, walijiuliza na kutuuliza; imekuwaje mmekubaliwa kufanya ibada katika kanisa la Wapentekoste?

Tangu lini Wapentekoste na Wamoravian wakashirikiana? Hata waandishi wa habari walituhoji sana juu ya ushirikiano huo."

Alisema Mchungaji Mwakamyanda na kuongeza, "sisi tuliwajibu kuwa, Wamoraviani na Wapentekoste; wote imani yao ina msingi katika Yesu Kristo... Kusudi letu ni kumuabudu Mungu na kumpinga ibilisi. Hivyo, hatuwezi kukwepa kushirikiana kwa kuwa wote tunafanya vita vya kiroho dhidi ya adui mmoja." Alisema.

Naye Mchungaji Luther Shumba wa KLPT, Keko alisema "Wakristo wote tupande kwenye chombo. Hakuna kusema mimi ni Yohane, Mathayo au Petro. Wote, kwenye chombo twende ng’ambo. Kusudi la Mungu si dini wala jina, ni kupanda chomboni kwenda ng’ambo. Hata pakitokea dhoruba chomboni, tujipe moyo."

Tangu Aprili 30, mwaka huu, Wapentekoste wa Parishi ya Kekomachungwa wamekuwa wakiwahifadhi Wamoraviani wa Keko kwa kutumia kanisa lao kufuatia ujenzi wa kanisa la Moraviani Keko unaooendelea.

Wamoraviani waliruhusiwa kutumia kanisa hilo kwa siku za Jumapili tangu saa 12:00 hadi saa 3:30 asubuhi ambapo Wapentekoste nao wanaanza ibada zao. Pia, Wamoraviani walipata nafasi ya kuendesha semina na fellowship mbalimbali katika jengo hilo la KLPT.

Ujenzi wa la kanisa la Moraviani Keko lenye ghorofa mbili linalotarajiwa pia kuwa na shule ya awali, hospitali na ofisi ya mchungaji, ulianza mwaka 1996 na umekwisha gharimu zaidi ya shilingi milioni 25 kati ya shilingi milioni mia moja zinazohitajika.

Ufanisi huo umetokana na nguvu za waamini katika michango na ushiriki wa kazi za mikono.

Askofu Kyara wa KLPT aliyahimiza makanisa hayo mawili kujenga utamaduni wa kualikana kushiriki kazi za mikono katika ujenzi na shughuli za makanisa hayo. Alitaka ushirikiano baina ya makanisa uimarishwe ili watu wengi wajiunge na Ukristo.

Waamini Tabata wajenga Kanisa

lLitachukuwa watu 1600 kwa wakati mmoja

Na. Peter Dominic

WAAMINI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Tabata katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Saalam wamefanikiwa kujenga kanisa litalokuwa likichukua waamni 1600 kwa wakati mmoja.

Akizungumza na Gazeti hili ofisini kwake Tabata hivi karibuni,Paroko wa Parokia hiyo Padre Albin Tesha alisema ujenzi huo unatokana na juhudi na ushirikiano wa karibu wa waamini hao. "Kwakweli ushirikiano uliofanywa na waamini wa parokia yangu unatia moyo na kufuta mawazo ya kuwategemea wafadhili kujenga nyumba za ibada"alisema padre Tesha.

Aliongeza " tunajivunia kuona tumeweza kujenga kanisa kubwa kwani sasa waamini watapata nafasi ya kutosha kukaa tofauti na kanisa tulilonalo kwa sasa kwani watu wanakaa nje wakati wa ibada na wale wanaokaa ndani wanajibana sana".

Akifafanua zaidi juu ya ujenzi huo Padre Tesha alisema ubunifu wa mikakati ya kuchangia ujenzi huo ulisaidia zaidi.

Alisema watu mbalimbali wakiwemo waandisi na mafundi wa ujenzi walisaidia kutoa nguvu kazi zao na ushauri.

‘Kila aliyetoa wazo ama ushauri alisikilizwa na ushauri wake ulifanyiwa kazi"alisema.

Padre Tesha aliendelea kutaja mikakati mingine iliyowekwa kufanikisha ujenzi huo kuwa ni pamoja na kuhamasisha waamini walioko kwenye jumuiya ambapo zoezi hilo limefanikisha upatikanji wa pesa na kufanya kazi kwa kujitolea na mpango wa kutoa fungu la asilimia 20 katika mchango unaotolewa kila sikukuu ya Pasaka na pesa yote huingizwa katika ujenzi.

Alisema Parokia yake pia iliweka mpango wa kutembelea waumini majumbani kwao.

Hata hivyo Padre Tesha alisema ujenzi wa kanisa hilo ulioanza miaka miwili unahitaji nguvu za ziada kuweza kukamilika hivyo awaomba wakristo na watu wengine wajitolee kutoa michango yao katika kufanikisha ukamilishaji wa jengo hilo ambalo linatazamiwa kuanza kutumika Novemba 26 katika sherehe ya sikukuu ya Kristo Mfalme.

Padre Tesha alisema hadi sasa ujenzi umekwishagharimu milioni 16.

Wanawake sita kati ya kumi hupigwa na waume zao, rafiki zao- Utafiti

Na. Dalphina Rubyema

PAMOJA na Tanzania kukemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa wanawake, lakini bado wanawake sita kati ya kumi hupigwa na waume zao ama rafiki zao wa kiume.

Taarifa ya utafiti iliyotolewa na Chama cha Mtandao Afrika cha kutetea haki ya wanawake kwa kutumia sheria (Women Law and Development in Africa - WILDAF), inasema takwimu hizo zimepatikana baada ya chama hicho kufanya mahojiano na wanawake mbalimbali nchini.

Mratibu wa Chama hicho Bi, Judith Odunga ambaye alihojiana na gazeti hili jijini Dar es Salaam katikati ya wiki alisema kuwa vitendo hivyo havipo Tanzania tu bali nchi nyingi Ulimwenguni.

Alizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Canada ambapo asilimia 62 ya wanawake walifariki kutokana na kunyanyaswa na waume zao ikiwa ni pamoja na kupigwa na tukio hilo lilitokea mwaka 1987.

Alisema nchini Kenya katika wilaya ya Kisii asilimia 42 ya wanawake hupigwa na waume zao wakati mjini Kampala - Uganda asilimia 73 ya wanawake walihojiwa na kukiri kupigwa na waume zao.

Kwa upande wa ubakaji. Bi Odunga alisema kuwa kulingana na ripoti ya vifo vya wanawake, ubakaji unachangia asilimia 10 ya vifo hivyo.

‘Ubakaji umezidi kuimarisha mizizi yake katika bara zote za ulimwengu mzima, kati ya mwanamke mmoja au wanne wamewahi au watabakwa katika maisha yao’. Anasema Bi. Odunga.

Katika kuondoa yote hayo, Mratibu huyo wa WILDAF alisema kuwa chama chake kinasisitiza kuwa taratibu zilizowekwa kimataifa za kuwatetea na kuwalinda wanawake ziwekwe sahihi na muhimu zaidi vyombo vya kimataifa vitumike kikweli kweli.

Sheikh adokeza siri ya kuushinda UKIMWI

lAsema ni jamii kufuata maadili ya Mwenyezi Mungu

Na Seraph Kuandika, Morogoro

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA wilaya ya Morogoro Mjini Sheikh Mohamed Kairo, amesema mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI yanaweza kupata mafanikio iwapo jamii ya wanadamu itabadili tabia na kufuata misingi ya maisha yaliyowekwa na Mwenyezi Mungu.

Sheikh Kairo aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mjadala katika semina ya mafunzo ya mbinu mpya za kupambana na UKIMWI uliyofanyika katika chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) cha mjini hapa.

Alisema kushamiri kwa ugonjwa wa UKIMWI ni matokeo ya watu kwenda kinyume na katiba ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya kuishi maisha yenye kufuata maadili ya Kimungu na kibinadamu kama yanavyoelezwa katika vitabu vitakatifu.

Sheikh Kairo alisema kuwa, tofauti na wanyama, binadamu wamepewa mpangilio wa maisha ya kila siku hasa katika ndoa, lakini kwa sasa, hali imebadilika ambapo maisha yanaendeshwa kwa mtindo ambao ni dhahiri hamfurahishi Mwenyezi Mungu.

Aliongeza kuwa, tofauti na matakwa ya Mungu, badala ya kuzuia UKIMWI kwa kuendesha maisha yanayofuata maadili mema, watu wanafanya mambo yanayozidisha kasi ya kuenea kwa UKIMWI.

Semina hiyo ya siku moja iliyofunguliwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dk Godfrey Mtei na kufungwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro Dk. Diwani Mrutu ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka vyombo vya habari, madhehebu ya dini, elimu, taasisi zisizo za kiserikali na wawakilishi kutoka serikalini.

MICHANGO YA KONGAMANO LA UTUME WA WALEI TAIFA

Jimbo Katoliki la Bukoba lawasilisha Sh. 1/m

lMajimbo mengine yawa kimya

Na Dalphina Rubyema

JIMBO Katoliki la Bukoba limewasilisha zaidi ya shilingi milioni moja kwenye ofisi za Utume wa Walei Taifa kama mchango wa kufanikisha Kongamano la Utume wa Walaei Taifa litakalofanyika Novemba 19 hadi Novemba 19 mwaka huu.

Akizungumza na Gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni,Katibu wa Idara ya Baraza la Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Padre Nicholaus Segeja alisema kuwa baadhi ya Majimbo bado hayajawasilisha mchango huo likiwemo Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam ambalo ndiyo wenyeji wa Kongamano hilo.

"Kwa kweli hali ya michango ya kifedha bado siyo nzuri,ofisi ya Utume wa Walei Taifa bado haijapokea michango ya majimbo mbalimbali likiwemo Jimbo la Dar-Es-Salaam ambalo litakuwa wenyeji,Jimbo la Bukoba hadi sasa ndilo linaloongoza kwani limekwisha wasilisha zaidi ya shilingi milioni moja"alisema Padre Segeja.

Kutokana na hali hiyo,Padre Segeja ameyakumbusha Majimbo yote ambayo hayajawasilisha michango yao,kufanya hivyo kwani mafanikio ya Kongamano hilo yanategemea na michango hiyo.

Hata hivyo Katibu huyo wa Baraza la Walei TEC alisema kuwa mbali na Majimbo kuchelewa kuwasilisha michango yake, dalili za kufanikisha Kongamano hilo tayari yamenza kujitokeza kwani tayari watoa mada mbalimbali wameisha andaa mada watakazotoa.

Alisema mada zitakazotolewa katika Kongamano hilo litawashirikisha zaidi ya watu 300,000 ambao ni Wakurugenzi wa Majimbo,Kamati Tendaji ya Halmshauri ya Walei na vyama vyote vya kitume pamoja na washauri wa vyama hivyo,zitalenga kuandaa mwelekeo na dira ya utendaji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa kama matunda ya Jubilei Kuu.

Alisema Kongamano hilo pia litakuwa na hija itakayowashirikisha pia Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa itakayofanyika Novemba 24 TEC.

"Hija hii ya Kitaifa ni tukio pekee kwani itawashirikisha Walei na Maaskofu wote, pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na litafanyikia TEC kwani hapa ndiko kwenye Msalaba wa Kitaifa wa Jubilei Kuu"alisema Padre Segeja.

Alisema Kongamano hilo litafanyakika katika vituo vitatu ambavyo ni Msimbazi,TEC na kituo cha Baraza la Walei Taifa cha Bakanja Laity Centre.

Akifafanua zaidi,Padre Segeja alisema mada zote za Kongamano hilo zitafanyika Msimbazi na Hija TEC wakati tathmini ya kila siku itafanyika Bakanja.

Hata hivyo Padre Segeja alisema kuwa kutakuwepo na vituo vingine vidogo vidogo kwaajili ya mahitaji maalumu. Vitenge na fulana maalumu vimetolewa kwaajili ya Kongamano hilo la kipekee.

JAPOKUWA NI WATU WANAISHI NA VIRUS VYA UKIMWI

Hatutachoka kuielimisha umma juu ya ugonjwa huu-SHDEPHA+

Na Dalphina Rubyema

Chama cha Afya ya Mandeleo kwa Watu Wanaoishi na Virus vya UKIMWI, SHDEPHA+, kimesema kinazidi kuongeza nguvu zake katika kupambana na ugonjwa huo bila kificho.

Mwenyekiti wa SHDEPHA+, Bw.Joseph Katto alitoa kauli hiyo ofisini kwake jijini Dar-Es-salaam hivi karibuni wakati akiozungumza na gazeti la KIONGOZI juu ya juhudi zao katika kupambana na ugonjwa huu.

alisema kuwa ni wajibu wa jamii nzima wakiwamo waathirika wa moja kwa moja wa UKIMWI, kuona kuwa wanatumia nguvu zao kuielimisha jamii juu ya athari za UKIMWI ili ugonjwa huo usizidi kuenea.

"Sisi hatutachoka,tutaendelea kuuelimisha umma juu ya ugonjwa huu pamoja na kwamba tumeathirika," alisema

Wakati huo huo,Mikoa ya Shinyanga na Kagera imekipatia ofisi za kufanyia kazi Chama hicha SHDEPHA +.

Bw. Katto alisema kuwa hali inayoashiria kuwa sasa serikali imenza kuelewa umuhimu wa chama chake.

Alisema kwa upande wa Mkoa wa Shinyanga,Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkao huo,imetoa ofisi ya tawi la SHDEPHA+ ambayo itakuwa inatoa ushauri na waotoa ushauri huo ni wauguzi wa hapo ambao pia ni waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Alisema tawi hilo litakuwa chini ya ofisi ya SHDEPHA+ mkoa ambayo pia ipo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa huo na ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa inashirikiana kwa karibu na SHDEPHA+ ikiwa ni pamoja na kuwapa vitendea kazi kama magari wanayotumia wakati wa kwenda nje ya kutoa ushauri.

"Kwakweli wa Shinyanga umeonyesha sana ukaribu kwani imeishirikisha SHDEPHA+ kwenye mbio za Mwenge,kwaniaba ya wanaSHDEPHA+ natoa shurani kwa mkoa huo,nilivyokwenda huko Mwezi uliopita nilifurahishwa sana nilipoambia kuwa hata ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa imetoa ofisi kwaajili ya kufungua tawi ,nimecha nimenunua samani zote za ofisi hiyo mpya"alisema.

Kwaupande wa Mkoa wa Kagera,Bw.Katto alisema kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mjini imetoa ofisi mbayo SHDEPHA+ mkoani humo itafungua tawi.

Taasisi zatakiwa kutoa elimu juu ya makazi

Na Anthony Ngonyani

SHIRIKA lisilo la kiserikali na Udhamini wa Maendeleo kwa Wanawake (WAT) limezitaka taasisi za dini kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu kuendeleza makazi yao.

Hayo yalisemwa na washiriki wa mkutano wa siku mbili uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa British Council uliopo jijini Dar es Salaam.

Washiriki hao kutoka serikalini na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) walisema jamii itaishi katika makazi mazuri endapo taasisi za dini zitaona umuhimu wa kuendeleza miji kwani wao watakuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii.

Wamesema rushwa iliyokithiri inachangia kutokuwa na makazi mazuri kwani walio wengi hutumia fedha katika kujipatia viwanja mijini na kwamba hali hiyo imechangia kuharibu ramani za miji.

Wamezitaja sababu nyingine kuwa ni ongezeko la watu mijini, utaratibu mgumu wa kupata mikopo ya kuendeleza ardhi, kukosekana taarifa muhimu kuhusu ardhi na pia, umaskini uliokithiri pamoja na mila na desturi.

Wamesema serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari wakishirikiana na wafadhili wanatakiwa kushirikiana na taasisi za dini ili kuhakikisha kuwa watu wana makazi mazuri yanayokwenda na wakati.

Mkutano huo uliandaliwa na shirika hilo lisilo la kiserikali(WAT) likishirikiana na Wizara ya Maendeleo ya jamii, Wanawake na Watoto pamoja na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa(UNDP)