Makaburi ya wakristo yageuzwa uwanja wa FFU, Wanangangari

lWaruka misalaba na kuangukia makaburi hovyo

Na Waandishi Wetu

MAKABURI ya Wakristo yaliyopo eneo la Wailesi katika Manispaa ya Temeke, yamegeuzwa kuwa uwanja wa mapambano baina ya Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU), na wafuasi wa Chama cha wananchi (CUF) na hali hiyo imewatia wengi simanzi.

Tukio hilo la Jumanne majira ya saa 7:00 mchana, lilishuhudiwa na waandishi wa gazeti hili ambapo wafuasi wa CUF walikuwa wanaandamana kuelekea Uwanja wa Taifa wakitokea Temeke zilipo ofisi za wilaya za chama hicho eneo la Sudan, wakitaka kuwawekea shinikizo maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili watangaze matokeo ya ubunge jimbo la Temeke.

Wakiwa safarini kuelekea Uwanaja wa taifa huku mara wakikimbia na wakati mwingine kukimbia, walizuka polisi waliokuwa ndani ya LandRover 110 nyeupe yenye namba za usajili STJ 650 na kuwataka watawanyike lakini, Wanangangari hao walianza kuwarushia mawe ndipo zoezi la kurushiana mawe baina ya polisi na Wanangangari, likaanza.

Hata hivyo, kwa msaada wa mabumo ya machozi waliyotumia polisi hao wa kutuliza ghasia wakishirikiana na polisi wa kawaida, walifanikiwa kuwatawanya waandamanaji hao wa CUF.

Zoezi la kurushiana mawe na mabomu ya machozi lilifanyika kuanzia kwenye makutano ya barabara ya Boko na Mandela yalipo makaburi ya Wakristo.

Hali hiyo, ilifanya mashambulizi hayo baina ya polisi na Wana CUF, kuendelea hadi kwenye makaburi hayo huku wengine wakiruka misalaba na kuangukia makaburi hayo ovyo

Kufuatia purukushani hizo, kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alilazimika kuruka ukuta wa shule ya Msingi Kibasila na kudondoka chini kwa ndani hali iliyosababisha wanafunzi kutaka kumshambulia kama mwizi hadi walimu na mlinzi wa shule hiyo walipowazuia na kumruhusu kuondoka eneo hilo.

Vijana kadhaa waliokuwa wakikimbia na kutawanyika kufuatia vurumai hiyo ambao pia walikuwa katika maandamano hayo, walitiwa nguvuni kwa kuwa walikuwa wakimbia na kurusha mawe huku wakijitupa kwenye mikono ya askari kanzu walikuwa wamezunguka eneo hilo.

Hata hivyo, katika hali iliyolaaniwa na wakazi wengi wa eneo la Temeke, wafuasi hao waliokuwa katika ofisi za CUF, walikuwa wakifanya majaribio ya kuwasakama watu kadhaa waliokuwa wakipita maeneo jirani na hayo kwa kuwadhania kuwa ni askari kanzu.

Wakati wafuasi wa CUF na CCM wakiwa katika ofisi zao kusubiri kutangazwa rasmi kwa matokeo, magari ya polisi wa kuzuia ghasia yalionekana yakipita huku maaskari wakiwa wamejiandaa.

Magari yaliyoonekana katika msafara huo ni STH 6381, STJ 3297, STH 6385, STJ 3300, STJ 3296 na STJ 3298.

KINYANG’ANYIRO CHA UCHAGUZI MKUU:

Siamini kama nimenyimwa kura - Cheyo

lAdai labda kulikuwa na majinamizi vituoni

lKigoma ana wafuasi 6000, lakini alipata kura 50

Na Dalphina Rubyema

MGOMBEA Urais kwa tiketi cha Chama cha UDP, John Cheyo, amesema kulingana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Jumapili iliyopita, haamini kama wananchi wamemnyima kura na kwamba labda kuna jini ama jinamizi ambalo lilikuwa likipita na kubadilisha kura alizopigiwa kama si njama za CCM.

Mgombea huyo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar-Es-Salaam, juu ya mwenendo mzima wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Alisema kinachomshangaza ni hali ya kupata kura chache katika maeneo ambayo chama chake kinakubalika jambo ambalo amedai kuwa kuna mchezo wa kunyanganywa kura zake uliofanywa na CCM.

"Kitu cha kushangaza ni kama Kigoma, huko nina wanachama zaidi ya 6,000 katika wanachama wote hao nimeambulia kura 50 tu!. Hivi kweli inakuja jamani,kura 50 tu!,"alisema Bw.Cheyo na kuwafanya Waandishi kuangua vicheko, kisha akaongeza,

"Siyo mimi tu, hata wagombea wa viti vya ubunge na udiwani kwa tiketi ya UDP, nao pia wamekumbwa na balaa hili!" alisema Bw. Cheyo.

Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa UDP Taifa, aliongeza kusema, "Unakuta mgombea ana familia ya watu 15 wenye sifa za kupiga kura achia mbali majirani na ndugu wengine wa karibu lakini pamoja na watu hao, anaambulia kura mbili tu! Hivi kweli hali hii inakuja akilini! Hata kama wanachama watamnyima kura, asiambulie hata kura ya mama, mkewe ama za watoto wake! Ama kweli CCM imeamua kuua upinzani."

Bw. Cheyo pia amedai kuwa kitu kilichomsikitisha na kuchangia kumkosesha kura, ni hali ya serikali ya CCM kutumia nguvu nyingi za dola na rushwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha kwamba, wapinzani hawapati kura.

"Kampeni zilienda vizuri lakini siku tatu za mwisho, CCM walikuwa wakitoa hongo hadharani zikiwemo khanga, bakuri za plastiki, chumvi na vitu vingine, isitoshe, hata vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi, viliwanyanyasa sana wagombea, mfano mzuri ni kupigwa kwa mgombea wa kiti cha Ubunge Jimbo la Sengerema kupitia UDP, Bw. Masha Lwanyantika na mtoto wake ambaye alikuwa akipiga picha wakati wa kampeini za baba yake, walipigwa na hivi sasa wana ngeu,"alisema.

Bw. Cheyo pia amedai kuwa CCM imekinyang’anya chama chake zaidi ya majimmbo 13 ambapo ameyataja baadhi ya majimbo hayo kuwa ni Bariadi, Kisesa, Magu (zote mbili), Mwanza Vijijini na Mjini, Sengerema na Geita.

Hata hivyo, Cheyo ambaye hadi hivi sasa chama chake tayari kimekwisha shinda viti vitatu vya nafasi ya Ubunge, amesema kuwa mwisho wa kampeni hizi za mwaka 2000, ni mwanzo wa kampeni za 2005 na sera za chama hicho ni zile zile za kuwajaza watu mapesa.

Kwa upande wa hali ya Zanzibar, Mwenyekiti huyo wa UDP alisema kuwa chama chake kinaungana na vyama vingine vya upinzani kikiwemo CUF kwamba, Uchaguzi Visiwani humo lazima urudiwe nchi nzima (Tanzania Visiwani) badala ya Majimbo 16 ya Mjini Magharibi kama ilivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)

"Kuvurugwa kwa uchaguzi Visiwani Zanzibar, ni janja ya CCM, imeona mambo yanakuwa mazito ikaamua isitishe uchaguzi, ni kama ilivyofanya mwaka 1995 kwani walipoona wameshindwa, ikabidi NEC isitishe uchaguzi wa mkoa wa Dar-Es-Salaam, safari hii imebainika, uchaguzi urudiwe tuone huo mchezo wao watauchezea wapi!" alisema.

Alisema kushindwa kurudia kwa uchaguzi wa Zanzibar kutaifanya serikali ya Muungano ikose Rais kwani huyo wa sasa (Rais Mkapa) kulingana na katiba, muda wake wa miaka mitano wa kushika madaraka umefika ukingoni.

Apoteza jicho akishangilia ushindi wa CCM

lMwingine akatwa mapanga na kuporwa ng'ombe

Na Christopher Gamaina, Tarime

MKAZI mmoja wa wilayani hapa, Bw. Kyongo Kikene(18), amejeruhiwa vibaya

jicho lake la kushoto baada ya kupigwa na jiwe na mtu asiyejulikana wakati akiwa kwenye gari la mgombea ubunge kwa tikiti ya CCM, Bw. Kisyeri Chambili.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Hospitali ya Wilaya alipolazwa katika Wadi Namba 7, Bw. Kikene alidai mkasa huo ulimkumba majira ya saa tano asubuhi Jumatano iliyopita.

Alisema akiwa na wenzake katika kushangilia ushindi wa mbunge wa CCM wakiwa ndani ya gari la mgombea huyo kabla ya matokeo kutangazwa rasmi, alishitushwa kwa kupigwa na jiwe jichoni bila kujua aliyemjeruhi.

Wakati huo huo: Mwita Chacha(26) mkazi wa kijiji cha Mogabiri wilayani hapa, amejeruhiwa vibaya na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi waliomvamia akiwa machungani.

Akizungumza na gazeti hili katika Hospitali ya Serikali wilayani hapa ndani ya wadi saba alipolazwa, Bw. Mwita amesema alipatwa na mkasa huo majira ya saa sita mchana katika maeneo ya mpaka wa kijiji hicho cha Mogabiri na Kilibo.

Alisema akiwa na wenzake, Nyangoro Chinka huko machungani, walitokea watu wawili ambao hawafahamu walioanza kumshambulia kwa kumkata kwa mapanga na kumjeruhi kichwani na mkononi na kuanza kuwatorosha ng’ombe wake .

Alisema mwenzake alikimbia huku akipiga kelele hali iliyowafanya wananchi wa kijiji hicho kukusanyika na kuwafuatialia.

"Tulikuwa tunachunga ambapo ghafla walitokea watu wawili ambao sikuwafahamu. Kwa haraka wakiwa na mapanga, wakaanza kunishambulia kwa mapanga na kunikata kichwani na mkononi. Muda huo, mwenzangu alikwisha kimbia," alisema Bw. Chacha.

Kwa mujibu wa kaka wa Bw. Chacha, Samweli Nyamhanga, kufuatia kelele hizo, majambazi hao waliamua kuwatelekeza ng’ombe hao ambao walikuwa wamewapora na kukimbia nao umbali kadhaa na kisha wao wenyewe kufanikiwa kutokomea.

Juhudi za kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara Bw Paul Ntobi kuzungumzia matukio hayo, hazikufanikiwa kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya simu baina yake na gazeti hili mjini hapa lakini, polisi wilayani hapa wanaendelea na uchunguzi.

Tatizo la nchi maskini ni rushwa sio madeni - IFM

Na. Dalphina Rubyema

IMEELEZWA kuwa suala la kufutiwa madeni kwa nchi za Ulimwengu wa tatu halitamaliza matatizo ya nchi hizo, bali ufumbuzi pekee ni nchi husika kuweka mikakati kabambe ya kuondoa rushwa na mizizi yake.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF), Bw.Ko’hler wakati akijibu kilio cha Wanawake Dunia cha kutaka nchi za Ulimwengu wa Tatu zifutiwe madeni.

Wanawake hao walitoa kilio hicho wakati wa Maandamano ya Dunia ya Wanawake yaliyofanyika nchini Marekani.

Mmoja wa wajumbe waliohudhuria maandamano hayo kutoka Chama cha Mtandao wa Kutetea Haki za Wanawake Afrika(WILDAF) kutoka Tanzania, Bi. Judith Odunga, alisema kuwa maandamano hayo yaligawanyika katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza, iliwashirikisha wajumbe kuwa kuonana uso kwa uso na Wakurugenzi wa Benki ya Fedha na Shirika la Kimataifa la Fedha(IMF).

Zoezi hilo lilifanyika mjini Washington DC kuanzia Oktoba 14 hadi 16 mwaka huu.

Aliitaja sehemu ya pili kuwa ni ile iliyohusu maandamano yenyewe yaliyofanyika New York nchini Marekani kuanzia Oktoba 17 hadi 18, mwaka huu.

Bi. Odunga ambaye ni Mratibu wa WILDAF alisema kuwa mambo muhimu yaliyofanyika wakati wa maandamano hayo mjini New York, ni pamoja na kuwasilisha vikapu vyenye baadhi ya kadi zenye kutiwa sahihi za kupinga vitendo vya unyanyasaji wa wanawake duniani ambazo zilitoka katika mataifa mbalimbali.

"Jumla ya kadi milioni saba kutoka nchi 159 zilizoshiriki maandamano hayo, ziliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan na katika kadi hizo, 511 zilitoka Tanzania baada ya kukusanywa na wawakilishi mbalimbali wa WILDAF nchini," alisema Bi. Odunga.

Aliitaja mikoa ya Tanzania iliyowasilisha kadi hizo kuwa ni Dar-Es-Salaam, Iringa, Tanga, Morogoro, Mara, Kilimanjaro, Mtwara, Bukoba, Mwanza, Tanga, Arusha, Singida, Kigoma, Shinyanga na Dodoma.

Katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hii nje ya ukumbi wa idara ya habari (MAELEZO), jijini Dar-Es-Salaam baada ya kuzungumza na jopo la wandishi jijini, Bi. Odunga alisema suala la Mkurugenzi wa IMF kusisitiza kuota kwa mizizi ya rushwa kwa nchi za Ulimwengu wa Tatu, ni changamoto kwa Taifa la Tanzania.

"Hili ni changamoto kwa Watanzania tukiwa ni sehemu ya Dunia ya Tatu, hivyo, hatuna budi sisi kama wanaharakati kwa ushirikiano na serikali, wasomi, taasisi za dini na wananchi kwa jumla, kuwajibika kwa pamoja katika kuendeleza vita dhidi ya rushwa," alisema.

Mratibu huyo wa WILDAF alisema kuwa maandamano hayo hayakuwa tu, kwa ajili ya kutembea, bali yalibeba mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuangalia chanzo cha unyanyasaji na ukatiri wa wanawake dunia.

Uvumi wa wanyonya damu wasababisha hofu kwa wanafunzi Dar

Na. Peter Dominic

KUMEKUWEPO uvumi uliotanda katika baadhi ya shule za msingi katika manispaa ya Temeke kuwa, wamezuka mumiani wanaodaiwa kuwanyonya watu damu.

Hali hiyo isiyokuwa na ukweli wala uthibitisho wowote ambayo pia ni moja ya imani potofu za kishirikina, imewatia kiwewe wanafunzi wa shule za Wailes na Kibasila ambao kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili kuwa wakati wowote wanahofia usalama wao kwa kunyonywa damu na hivyo kutembea katika makundi.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema Siku ya Alhamis ya Oktoba 26, mwaka huu uvumi ulitanda juu ya kuwapo kwa hali hiyo.

Siku hiyo katika shule ya Wailes inadaiwa kuwa mwanafunzi mmoja ambaye hadi sasa jina lake halijapatikana, alizuka na kuwatia hofu wanafunzi wengine juu ya watu hao wanaodaiwa kunyonya damu na hivyo kuwafanya wote kukimbilia nje ya shule licha ya juhudi za walimu na mlinzi kuwazuia .

Habari tulizopata awali zilisema katika shule ya Kibasila, siku hiyo hofu ilitanda baada ya mlezi wa mwanafunzi kufika shuleni hapo kumdai mtoto wake ili amuepushe na hali hiyo iliyodaiwa kuwapo.

Gazeti hili lilipofika shuleni Kibasila, Mwalimu Mkuu Msaidizi ambaye hakutaka kuzungumzia suala hilo na kukataa kutaja jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa shule, lakini akafahamika kwa jina moja la Joseph alisema ingawa tetesi hizo zimesikika lakini ni uvumi tu, na hauna ukweli wowote.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, baadhi ya walimu wa kike aliowaita kumsaidia kuzungumzia suala hili, walikiri mbele yake kuwapo kwa hali hiyo siku hiyo.

"Hebu mtuelewe kuwa Alhamisi hiyo, ni mzazi mmoja alikuja kumchukua mtoto wake eti naye amesikia kuna wanyonya damu. Yeye ndiye alileta wazo hilo; hapa halikuwapo hata kidogo," alisema mmoja wa walimu hao

"Tangu zamani haya mambo yanasikika lakini ni nani aliwahi kunyonywa damu. Huu ni uvumi tu hatuwezi kuufanyia kazi," alisema.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Wailes, Bi. Elizabeth Njau alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo, lakini akabainisha kuwa wanafunzi wake walitimka na wengine kupitia madirishani bila kujua ni jambo gani limewasibu na walijitahidi kuwazuia bila mafanikio kwa kuwa walivamia lango.

Bi. Njau alisema kufuatia kukurupuka kwa watoto hao na kukimbia hovyo kurudi majumbani kwao, Polisi kutoka kituo cha Chang’ombe walifika shuleni hapo na kupewa maelezo waliyoyataka.

Alisema bado uongozi wa shule unatafuta asili ya uvumi huo shuleni hapo.

Alipoulizwa ofisini kwake kuwa ana mpango gani juu ya hali ya hofu inayotanda kwa wanafunzi wa eneo lake Jumatano iliyopita, Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke, Bw. Mfugale alisema ofisi yake haijapata taarifa zozote kuhusu kuwepo kwa wanyonya damu. "Sina taarifa zozote lakini sidhani kitu kama hicho pengine watoto wanawaogopa watu wanaokuwa katika kampeni," alisema.

Waanglikana Uingereza kuwapiga jeki Watanzania

Na Leocardia Moswery

KANISA la Kianglikana la jijini London, Uingereza, limeahidi kulisaidia Kanisa la Kianglikana la Temeke jijini Dar-Es-Salaam, kwa njia ya sadaka ili kukamilisha shughuli za upanuzi.

Kwa mujibu wa Mchungaji Msaidizi wa Parishi ya Temeke, Mchungaji Daniel S. Mhando, aliyerejea hivi karibuni toka London, Uingereza, waamini wa Kanisa hilo nchini humo katika parokia ya All Halows, iliyopo katika mtaa wa Twicknham, wamekubali kulisaidia kanisa la Temeke kwa njia ya sadaka ili kusaidia kumudu gharama za upanuzi wa kanisa la Dinari ya Temeke.

Mchungaji Mhando alisema kwa niaba ya Halmashauri ya Mtaa wa Twicknham, Kasisi Kiongozi (Vicar General), Mchungaji Neil Evans, alisema kanisa lake limekubali kulisaidia kanisa hilo lililopo Tanzania kwa shughuli ya upanuzi huo unaokadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 21 za Kitanzania.

Mchungaji Mhando aliyeambatana na mkewe Mama Jessie Mhando, katika safari hiyo, alidokeza kuwa pamoja na Halmashauri ya Mtaa wa Temeke, na kwa ushirikiano na Paroko Nathaniel Kipalamoto, walituma maombi kupitia kwa muumini mmoja wa kanisa hilo la Twickenham , Raphael J. Mhando, na kwamba hali ya kukubaliwa ombi lao la kusaidiwa, imewafurahisha na itakuwa changamoto nyingine kubwa katika kuifanya vema kazi ya Mungu.

Kwa mujibu wa Mchungaji Mhando, Mtaa wa Twickenham, utatoa sadaka yote ya siku ya kuadhimisha miaka 60 ya kanisa hilo la Kianglikana itakayoadhimishwa Novemba 9, mwaka huu, kwa ajili ya kulisaidia Kanisa la Tanzania.

Wakati huo huo: Kwa mujibu wa Mchungaji Kipalamoto, Uchaguzi Mkuu wa Jumapili iliyopita, Oktoba 29, mwaka huu, uliathiri vibaya mahudhurio ya waamini katika kanisa hilo kutokana na baadhi yao kuwahi kwenye vituo vya kupigia kura, na wengine kubaki majumbani kwao kwa kuhofia usalama.

"Katika ibada zote mbili; hapakuwa na waamini wa kutosha. Hii ni kwa kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku ya uchaguzi," alisema

Shinyanga kuonja matunda ya mradi wa dharura wa maji

Na Charles Hililla, Shinyanga

WAKAZI wa Manispaa ya Shinyanga na vitongoji vyake wanaokadiriwa kuwa milioni 1.5, hivi karibuni wataanza kunufaika na mradi wa maji wa dharura, unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Taka katika manispaa hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni ofisini kwake, Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo mjini hapa, Bw.Wales Nkanwa, alisema kuwa mradi huo uliobuniwa na ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na unasimamiwa na ofisi yake hivi sasa upo katika hatua nzuri.

Alisema hatua zilizofikiwa ni nzuri kwa juhudi zao za kufikisha maji toka kwenye visima virefu vilivyochimbwa katika vijiji vya Mwawaza na Negezi, nje kidogo ya mji wa Shinyanga.

Bwana Nkanwa alisema kuwa, kazi inayofanyika hivi sasa ni kutandaza mambomba kutoka katika visima hivyo vipatavyo 19 ambavyo vitasukuma maji kwa pamoja kuleta katika Manispaa ya Shinyanga.

Wazo la mradi huo wa maji ya dharura kwa mji wa Shinyanga limetokana na tatizo la muda mrefu lililokuwa likiwakabili wakazi wa mji huo kutokana na kukauka kwa bwawa la Nig’wa lilikokuwa tegemeo la maji mjini hapo.

Licha ya kukauka kwa bwawa hili, pia vyanzo vyake vya maji vilikauka kwa sababu ya uhaba wa mvua kwa mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha mwaka jana.

Mradi huo dharura wa maji kwa mji wa Shinyanga ulianza mwaka jana kwa kuchimba visima hivyo pamoja na kufanya utafiti wa kisayansi, maabara na kemia ili kujua yanapopatikana maji na kiwango cha ubora wake.

Hadi hivi sasa mradi huo umeshatumia kiasi cha milioni 290 zilizotolewa na serikali na hivi karibuni, umepokea kiasi kingine cha shilingi milioni 170 zitakazosaidia kusafirisha mambomba pamoja na kutengeneza njia ya maji kutoka kwenye visima hivyo hadi katika mji wa Shinyanga.

Kukamilika kwa mradi huo kutaleta nafuu ya maisha kwa wananchi wa mji wa Shinyanga kwa kuwa, hivi sasa ndoo moja ya maji yenye ujazo wa lita 20 inauzwa kati ya shilingi 100 hadi 300 kufuatana na umbali na ubora wa maji aidha ya chumvi, au ya kawaida.

Mkurugenzi huyo alisisitiza mbele ya waandishi hao kuwa, maji hayo ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo kauli ambayo ilikuwa inakanusha taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na uvumi kuenea mjini hapa kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Akithibitisha kauli hiyo, Mkurugenzi huyo aliwaonesha waandishi hao vipimo vya maabara vya maji hayo vilivyoonesha kuwa maji hayo yalipimwa Julai 7, mwaka huu jijini Dar-Es-Salaam.

Yalipimwa katika maabara ya maji na kuonekana kuwa hayana madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Makamba kuchochea mavuno ya KKKT

Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam, Luteni Yusuph Makamba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ibada maalumu ya Siku ya Mavuno itakayofanyika katika usharika wa Sinza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) , Novemba 5 mwaka huu.

Akizungumza na Gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki Msaidizi wa Askofu wa KKKT, dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Adamu Kombo, alisema uongozi wa Usharika huo umemwalika Mkuu wa Mkoa Luteni Yusuph Makamba ili kuhamasisha watu na kuchochea moyo wa kutoa mavuno yao kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.

'Wamemwalika Mkuu wa Mkoa kwa sababu yeye(Makamba), ni kiongozi wetu wa mkoa.

Afike tu, kuhamasisha watu katika kutoa mavuno yao na tumekuwa tukimuita mara kwa mara katika shughuli zetu. tunataka afike pia atasalimiana na washarika wetu' alisema .

Mchungaji Kombo alisema ibada hiyo itaanza saa mbili na Mkuu wa Mkoa atashiriki ibada moja kwa moja na ibada itendelea ambapo waamini watatoa sadaka maalumu kama mifugo, mazao na vitu vingine kama shukrani maalumu.

Mchungaji Kombo alifafanua kuwa, ingawa waamini toka katika sharika nyingine wanakaribishwa, kimsingi iibada hiyo imelenga washarika wa Sinza kwa vile kila usharka unakuwa na sikukuu yake ya mavuno kila mwaka.

Pia alisema baada ya ibada kutakuwepo na mnada wa kuuza sadaka hizo zitakazotolewa na pesa zitakazotolewa zinalenga kuendeleza uinjilisti na fungu lingine litasaidia zoezi la ujenzi wa kanisa ambalo lipo katika hatua ya awali usharika wa sinza.

Askofu Muanglikana asema kondomu ni madubwasha tu

l Askofu Mkuu ataka serikali na dini kuwa kitu kimoja

Dalphina Rubyema na Leocardia Moswery

ASKOFU wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Western Tanganyika, Askofu Gerald Mpango amezifananisha kondomu na madubwasha yasiyokuwa na thamani yoyote kwa kuwa hazifai na zinachochea kasi ya kuenea kwa UKIMWI badala ya kuuzuia.

Askofu Mpango alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa juma wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-Es-Salaam, ambapo waandishi hao walitaka kupata ufafanuzi kuwa ni kwanini Kanisa hilo linapinga utumiaji wa kondomu katika kujikinga na Ukimwi.

Askofu Mpango ambaye pia ni Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, alisema wenye kuamini kuwa kondomu ni kizuizi cha UKIMWI, hawana budi kuelewa kuwa mawazo hayo siyo ya kweli kwani zina udhaifu mkubwa na hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizo.

Alisema jambo la muhimu badala ya kutegemea kondomu, ni kujenga tabia ya usafi na uaminifu kimwili na kiroho.

Alisema hilo linawahusu wote wakiwamo wanandoa ambao hawana budi kulinda uaminifu katika ndoa zao, na wasio wanandoa, kutojishirikisha katika vitendo vya ndoa hadi watakapooa au kuolewa na wasio ambukizwa.

"Hata hivyo madubwasha haya yana matatizo yake maana unaweza kuliona ukadhani kuwa unajikinga lakini kumbe, ndiyo unaeneza UKIMWI. Hayana thamani yoyote," alisema.

Alisema Kanisa la Anglikana limeamua kulivalia njuga suala la UKIMWI kwani linamaliza Taifa la tanzania na nchi nyingine za Afrika.

"Mkutano wa Maaskofu wa Kanisa la Anglikana uliofanyika Dodoma mnamo Oktoba 10 mwaka huu, ulitoa tamko kuwa, lazima liwe kanisa watetezi wa haki za makundi yanayoathirika zaidi hasa katika kutunza yatima na huduma ya afya ya misaada ya kijamii na kiuchumi kwa watu walioathirika na virusi vya UKIMWI," alisema.

Hata hivyo kanisa hilo linaendelea na warsha inayozungumzia suala zima la UKIMWI, warsha hiyo ya siku tano inayofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC) inatarajia kumalizika Jumapili hii.

Wakati huo huo: Askofu Mkuu wa kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela, ametaka serikali kuenda pamoja na taasisi za dini kwa kushirikiana na kuwekeana wazi juu ya hatari ya UKIMWI kwa kuwa wote wanashughulikia masuala ya maendeleo ya jamii kwa afya ya mwili, akili na roho.

Akifungua kongamano la wawakilishi wa kanisa hilo juu ya kupambana na UKIMWI linalo malizika Jumapili hii katika ukumbi wa TEC, Askofu Mtetemela alisema, Upendo wa Mungu ndio utubidishe katika kulinusuru taifa letu dhidi ya janga hili.

Jamii imekabiliwa na mbwa mwitu. Watakaofaulu kupigana na huyo mbwa mbwitu siyo wachungaji wa mishahara, bali wenye mapenzi mema na kondoo wanaoathirika."

Alisema suala la kuielimisha jamii juu ya athari za UKIMWI halipaswi kuachwa kwa vikundi kadhaa pekee hususan vya kidini bali ni jukumula kila mwanajamii.

Alisema Watanzania hawana budi kufanya jukumu hili kwa ushirikiano mkubwa kamawalivyo fanya wananchi wa Uganda hata kufanikiwa kukabili kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi ya UKIMWI.

Askofu Mkuu Mtetetmela alisema vita dhidi ya UKIMWI ni kubwa kwa kuwa ndio ugonjwa unaohujumu afya za raia, pamoja na kuathiri uchumi, ndio unaoongoza kwa vifo vinavyotokea barani Afrika, Tanzania ikwamo.

Warsha hiyo ya siku tano juu ya mada isemayo KUISHI KWA MATUMAINI, iliyashirikisha mashirika yasiyo ya kiserikali(NGOs), Dayosisi 14 za kanisa hilo na washiriki toka Uganda na Marekani.

Makaburi ya maiti za mapadre kuhamishiwa Matola

Na Mwandishi Wetu

MAKABURI ya maiti mbili za mapadre waliokufa katika ajali ya boti Mission Lumbila jimboni Njombe katika Ziwa Nyasa, yanatarajiwa kuhamishwa na kuzikwa upya katika parokia ya Matola wilayani humo toka yalipozikwa kijijini Matema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Askofu wa jimbo hilo, Mhashamu Raymod Mwanyika, aliyoituma kwa Mkuu wa Polisi mkoani humo Kanisa Katoliki jimboni Mbeya, lingependelea maiti hizo mbili zifukuliwe toka zilipokuwa zimezikwa katika kiwanja cha jimbo la Mbeya kwenye kijiji cha na kuzikwa upya katika parokia ya Matola iliyopo wilayani Njombe, kama ilivyo desturi ambapo mapadre wote huzikwa mahali hapo.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba, maiti hizo zilizikwa Mbeya kutokana na kuwa katika hali mbaya baada ya kuopolewa kwenye maji na kwamba, ilishindikana kuzisafirisha na hivyo, ikaamriwa kuzikwa mahali hapo.

"Kwa barua hii, napenda kutaarifu rasmi kwamba tungependa baada ya mwaka mmoja kupita, kufanya zoezi hilo tarehe 9 Novemba 2000 la kwenda kuhamisha hizo maiti mbili toka kiwanja cha Jimbo la Mbeya, Matema na kuzileta jimboni Njombe ili tukazike kwenye shamba la Mungu la mapadre pale Matola Mision, wilayani Njombe," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Watumishi hao wa Mungu ambao ni marehemu Padre Nicolaus Msemwa na Padre Mathias Kayombo, walikufa katika ajali mbaya ya boti ya Mision Lumbila katika Ziwa Nyasa, sehemu ya kati ya Itungi na Lumbila Juni 28, mwaka jana wakiwa karibu nusu ya safari kuvuka ziwa kuelekea Lumbila Mission.

Katika boti hiyo pia kulikuwa na abiria wengine ambapo kati yao ni abiria 16 walionusurika, 21 walipoteza maisha wakiwemo watoto 3 na maiti 16 hadi leo hazijaonekana ilisema taarifa.

Nakala ya taarifa hiyo ambayo gazeti hili linayo, imesambazwa pia kwa Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mkuu wa Polisi wilayani humo (OCD), Paroko wa Kyela Mission, Mkuu wa Wilaya ya Njombe(OCD) wa Njombe, na parokia zote jimboni humo.