'Chonde chonde ! Mungu tuepushie balaa'

lWalia Bakwata, Wakatoliki na KKKT

l'Hatutaki Tanzania iwe Burundi, Rwanda na Kongo'

Peter Dominic

MAELFU ya Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini wakiwamo viongozi wa taasisi mbalimbali za kidini, wamekesha na kumuomba Mungu kwa muda mrefu aubariki Uchaguzi Mkuu wa Jumapili hii ili uzae matunda bora huku amani na usalama vikiendelea kudumishwa.

Kwa nyakati tofauti wameomba chonde chonde nchi hii isibadilike na kuwa mithili ya mataifa mengine ambayo kwa kuwa walichezea amani, sasa imewaponyoka na wanaitafuta mithili ya almasi lakini hawaipati na wanaililia.

Licha ya kuendesha ibada mbalimbali katika nyumba zao za ibada kwa siku nyingi zilizopita kama matayarisho ya siku hii, kwa nyakati tofauti viongozi wa taasisi za dini waliozungumza na gazeti hili, wameomba chonde chonde kwa wapiga kura na wale wanaogombea nafasi mbalimbali wakubaliane na matokeo baada ya kura.

Sambamba na ombi hilo viongozi hao wamehimiza kwamba kutokana na historia ya Tanzania kusaidia nchi nyingine za Afrika katika maswala mbalimbali zikiwemo harakati za kutafuta uhuru wa nchi hizo kuna kila sababu ya kuufanya uchaguzi uwe huru na haki na kukubaliana na matokeo ili uwe mfano kwa nchi nyingine ambazo zinasuasua katika suala la uhuru wa kuchagua.

Mkurugenzi wa Habari wa Jimbo Katoliki la Singida, Padre Thomas Mangi alisema, "Mungu tuepushie balaa. Kila mtu aende kughagua akijua kuwa uchaguzi huu ni wetu. Apatikane kiongozi anayejali maendeleo ya, haki na upendo."

"Mungu aubariki uchaguzi wetu ili shetani asituvamie tukawa kama rwanda na Burundi...wagombea wote wawe tayari kukubali matokeo kwani asiyekubali kushindwa si mshindani na matatizo yote yatatuliwe na Tume."

"Uchaguzi huu una vyama vingi kila chama kingependa kiongozi wake ashinde lakini mshindi atakuwa mmoja kila nafasi inayogombewa. Sote tukubaliane na matokeo bila kujali aliyemshinda ametoka chama gani," alisema Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la KKKT Mchungaji Adam Kombo.

Aliwaasa Watanzania kuzidi kumuomba Mungu yupo aubariki uchaguzi na kuwapa moyo na ushujaa kuyapokea matokeo huku akiwahimiza wasihofu chochote kwa kuwa Mungu na serikali ipo hivyo, amani itadumu.

"Tulikuwa na sala ambazo zilianza toka kipindi cha nyuma lakini rasmi zilifanyika Jumapili, katika sharika zote na kuna vikundi vya kiroho vitakesha Ijumaa usiku kuamkia Jumamosi katika Kanisa Kuu la Azania Front kuombea uchaguzi," alisema Mchungaji Kombo katikati ya juma.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA), Alhaj Rajabu Kundya, alisema, "Tunaomba Mungu atubariki. Hii ni nchi yetu tunataka tuwe na amani. Tukiiharibu sisi, hasara ni kwetu sisi na vizazi vijavyo na tukifanya hivyo tutakuwa hatukutumia busara.

Zoezi la uchaguzi ni muhimu hivyo liendeshwe kwa utulivu na amani ikiwemo kumuomba Mwenyezi Mungu atupe viongozi bora watakaoweza kulitumikia taifa lao kwa uaminifu ili Tanzania iendelee kuwa kama ilivyo Kisiwa cha Amani."

Alisema BAKWATA kwa kutambua umuhimu wa amani ilianza muda mrefu tangu Aprili kuwafundisha waamini wake juu ya suala la uchaguzi na baada ya elimu hiyo, kila mmoja ameachiwa uhuru wake katika kupiga kura kazi ambayo alisema ilifanywa kikamilifu katika mikoa yote na Shehe Mkuu nchini, Mufti Hemed Bin Jumaa Bin Hemed kwa njia ya nasaha za kiroho.

Alisema na kuongeza wananchi wawe pamoja kwamba uhuru wa wananchi na suala la amani vinakwenda pamoja ndipo amani itadumu.

‘Tulipigania nchi nyingine za Afrika zipate uhuru tunachokitegemea uchaguzi wetu uwe huru na haki ili uwe mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika’, alisema

Wakati huo huo: Kanisa Katoliki parokia ya Kilimahewa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam liliandaa ibada maalumu kila Alhamisi kuombea uchaguzi mkuu ufanyike kwa amani na utulivu.

Mwenyekiti wa Halmashauri Walei parokiani hapo, Bw. Joseph Vakunema, alisema pia parokia yake iliandaa utaratibu wa kuuombea uchaguzi katika misa za kila siku ili Mwenyezi Mungu ashushe baraka zake na kuliepushia taifa vurugu zinazoweza kujitokeza ambazo hakuna Mtanzania hata mmoja anayezihitaji.

Katibu wa parokia ya Mtakatifu Maurus- Kurasini, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Bw. Cletus Majani, alisema, "Watanzania tuombe Mungu atuzidishie hekima uchaguzi wetu uishe vizuri ili mwenye jicho lake abaki nalo na mwenye miguu yake , abaki nayo kwa amani."

Maaskofu mbalimbali na viongozi wa ngazi na vitengo mbalimbali wamekuwa na mfululuzio wa sala katika ibada maalumu wakiuombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa wenye mafanikio, amani na utulivu.

Kikongwe wa miaka 73 ajiunga na SHDEPHA+

lNi baada ya kubainika kuwa na virus vya UKIMWI

Na Dalphina Rubyema

WAKATI Taifa lipo katika mapambano kabambe ya kutokomeza ugonjwa wa UKIMWI huko mkoani Shinyanga, kikongwe mmoja mwenye umri wa miaka 73 amejiunga na chama cha Afya ya maendeleo kwa watu wanaoishi na Virus vya UKIMWI (SHDEPHA+), imefahamika.

Taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa SHDEPHA+ Taifa Bw. Joseph Katto zinasema kuwa tukio hilo lilitokea katikati ya Septemba mwaka huu wakati uongozi wa SHDEPHA+ Taifa ulipokuwa katika ziara ya kutembelea matawi yake kwenye mikoa ya Kagera, Kigoma na Shinyanga.

Bwana Katto alisema kuwa Bibi huyo ambaye jina lake linahifadhiwa aliamua kujiunga na SHDEPHA+ baada ya kubainika kuwa na Virusi vya UKIMWI.

"Washauri wetu huko walimpa ushauri mama huyo apime damu naye alikubali kufanya hivyo na hatimaye ilibainika kuwa na Virus hivyo kujiunga na Chama chetu cha SHDEPHA+" alisema Bw. Katto.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa alipomuhoji mwanamke huyo kikongwe jinsi gani amepata ugonjwa huo, aliambiwa kuwa pengine amepata kutokana na kumuuguza mwanae aliyekuwa akiumwa UKIMWI.

"Unajua huyo mama ni mkunga, hivyo alisema kuwa pengine alipata ugonjwa huo kwa kumuuguza mwanae aliyefariki kwa UKIMWI alisema Bw. Katto.

Wakati huo huo: Bw. Katto amewataka wafadhili wajitokeze kwa wingi kuwapa misaada waathirika wa UKIMWI ambao wanaonekana wapiganaji wazuri wa vita hii ya UKIMWI.

Alisema kwa upande wa mkoa wa Shinyanga, kampuni ya simu Mobitel imetoa sh. 50,000 kusaidia tawi la SHDEPHA+ mkoani humo ambapo kwa upande wa tawi la Bukoba shirika la Umeme nchini (TANESCO),limeahidi kutoa misaada.

Wakristo wanaodai haki kwa nguvu ni wanafiki-Kauli

Na Leocardia Moswery

WAKRISTO wanaoshabikia vitendo vya kutumia nguvu katika kudai haki, wameelezwa kuwa ni wanafiki na ni viongozi wasiofaa kwa na maadui wa Yesu kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha umwagaji damu kinyume na kiapo chao cha ubatizo.

Kauli hiyo ilitolewa na mtoa mada juu ya haki na amani kwa jamii, katika mkutano wa 25 wa Taifa wa Wakurugenzi wa Habari katika majimbo mbalimbali ya kanisa Katoliki nchini Tanzania, Bw. Cyprian Njige.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), eneo la Kurasini jijini Dar-Es-Salaam kuanzia Oktoba 16 hadi 19.

Bw. Njige ambaye ni Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu ya Amani ya Uhimili Migogoro, alisema kuwa inamkera anapoona baadhi ya Wakristo vitendo vya kutumia nguvu kudai haki na kibaya zaidi, wengine kujadili vitendo vya kipuuzi vinavyoweza kusababisha umwagaji damu.

"Ninakerwa sana na kusikitika ninapoona baadhi ya Wakristo wanashabikia vitendo vya kutumia nguvu katika kudai haki zao. Na wengine hata wanadiriki kushiriki matendo na mawazo ya kumwaga damu; eti kwa kisingizio cha kudai haki," alisema.

Aliongeza kusema kuwa, hata katika hotuba ya Baba Mtakatifu, Yohane Paul wa Pili, alikemea vitendo vya utumiaji nguvu na kuwaambia wasikilizaji wake kuwa, Ukristo hauifanyi jamii ifumbe macho ili isiyaone matatizo ya binadamu.

Pia, alisema Ukristo hauruhusu kufunika maovu yanayotendwa na wanajamii au maonevu katika jamii ya kitaifa lakini, kitu ambacho Ukristo unatukataza ni kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya kwa njia ya chuki mauaji ya watu wasio na hatia kwa kutumia nguvu.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo wa Elimu ya Amani na Uhimili Migogoro, aliongeza kusema kuwa, kwa mwelekeo huo anashawishika kuamini kuwa Wakristo wana namna hiyo ni wanafiki kwa Yesu Kristo na hata hapa duniani.

Alisema watu wenye tabia ya unafiki hawafai kuwa viongozi aidha katika kanisa au jamii nyingine kwa jumla.

"Ni wanafiki kwa sababu wanaweza kwenda kinyume kabisa na ahadi za uaminifu walizotoa wakati wa Ubatizo wao kwamba watamkataa shetani na hila zake zote," alisema.

Katika Mkutano huo uliofunguliwa na mwenyekiti wa Idara ya habari wa baraza la Maaskofu katoliki Tanzani, Mhashamu Askofu Anthony banzi wa jimbo katoliki la Tanga, Bw. Njige aliishauri idara ya Mawasiliano ya TEC,kuweka mpango wa majadiliano ya hotuba mbalimbali za Baba Mtakatifu, juu ya haki na amani katika majimbo kama njia mojawapo ya kuielewesha na kueneza amani ya kristo kwa waamini wote na jamii kwa jumla.

Jimbo la Iringa lagubikwa majonzi

lLapoteza watumishi wanne wa Mungu kwa wakati mmoja

Na. Leocardia Moswery

JIMBO Katoliki la Iringa limegubikwa na simanzi baada ya kupoteza watumishi wa Mungu wanne kwa kipindi cha wiki moja.

Askofu wa Jimbo hilo la Kikatoliki, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, aliwataja watumishi hao kuwa ni Padre Mathias Mdemu(38) aliyefariki jimboni humo kutokana na maradhi ya kawaida.

Wengine kwa mujibu wa mhashamu Ngalalekumtwa ni Sista Mansueta Pagos(84) wa Shirika la Wakonsolata aliyefia jimboni humo, Sista Asila Rozalia Madenge(50) wa Shirika la Mterezina aliyeugua kwa muda mrefu na kufia katika hospitali ya Mikocheni ya jijini Dar-Es-Salaam, na Sista Gioconda Lucato wa Shirika la Wakonsolata aliyefia jimboni Iringa.

Mhashamu Ngalalekumtwa alisema kuwa watumishi hao wa Mungu wote walizikwa katika makaburi ya Tosamaganga yaliyopo jimboni humo ambapo Padre Mathias na Sista Mansueta walizikwa Oktoba 20, mwaka huu wakati sista Ansila na Sista Gioconda walizikwa oktoba 23 mwaka huu.

Akitoa hisia zake kutokana na vifo hivyo, Mhashamu Ngalalekumtwa aliyezungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alisema kuwa kutokana na vifo hivyo, ni dhahiri kuwa jimbo lake limeungana na Bwana Yesu kwa kushiriki kifo chake na baadaye ufufuko.

"Kanisa limepokea sehemu ya Mwaka Mtakatifu kwa ajili ya kuungana na Bwana Yesu kwa kushiriki kifo na baadaye ufufuko kwa ndugu zetu wapendwa wanne walioaga dunia kwa kipindi cha juma moja," alisema Askofu.

Dumisheni amani, upendo muwe marafiki wa Yesu

Na. Josephs Sabinus

SHIRIKA la Kimisionari la masitasta wa Mtakatifu Augustine (Augustinian Missionary Sisters), lenye makao yake makuu mjini Roma, limewaambia Wakristo kote duniani kuwa, ili wadhihirishe umoja na urafiki baina yao na Yesu, hawana budi kutumia nguvu zao zote kudumisha amani, umoja na upendo katika jamii.

Mama Mkuu wa Shirika hilo Sista Angela Cecilia Traldi, aliyasema hayo wakati alipozungumza na gazeti hili jijini Dar-Es-Salaam, katika siku ya tatu ya ziara yake ya wiki mbili nchini Tanzania. Alifika nchini Jumamosi iliyopita akitokea Roma.

Alisema namna mojawapo ya kuishi kama rafiki wa Yesu ni kujenga utamaduni sahihi wa kuthamini utu wa mtu kuliko mali na akalaani mapambano baina ya vikundi mbalimbali yanayosababisha jamii isiyo na hatia kuathirika wakiwamo wanawake, wazee, watoto na walemavu na akaongeza kuwa, hali hii inasababishwa na ukosefu wa umoja, amani na upendo miongoni mwa jamii.

"Shirika letu linafanya kazi ya kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali yakiwamo ya kutetea haki za wanyonge katika mashule, vyuo vikuu, mashambani, hospitali na katika shule za awali. Tunataka watu wajali utu zaidi kuliko mali na waache migogoro ya vikundi kwa kuwa wanapopambana tembo, nyika ndizo huumia," alisema Sista.

Akizungumza kwa pamoja na Mkuu wa Shirika hilo katika nchi za Tanzania na Kenya, Sista Hery Garcia, na Sista Isabel Martinez, SistaAngela Traldi alisema kuwa, shirika lake lenye nchi 15 wanachama na masista 500 wakiwamo 14 wa nchini Tanzania, alisema shirika hilo linalenga kuwatetea wanyonge na kuwafanya wajijue wanachohitajika kufanya ili kuboresha maisha yao kimwili na kiroho.

Alisema shirika lake halitoi misaada kwa kila mtu bali kwa wanajamii ambao uwezo wao kimaumbile na hali halisi ya kijamii inawaruhusu kusaidiwa namna hiyo kwa kuwa hawajiwezi na hivyo kutafuta namna ya kuwasaidia.

Alifafanua kuwa kumpa kila mtu msaada wa bure bila sababu ya lazima, siyo kumsaidia bali ni kumdumaza na kumfanya azidi kuwa tegemezi hali inayozidi kukwamisha maendeleo yake na jamii kwa jumla.

Masista hao kwa pamoja walizisifia nchi za Tanzania na Kenya kwa kuongeza muitikio katika miito yao na wakazisifia nchi nyingine zenye muitikio mzuri wa miito kuwa ni pamoja na India, Amerika Kusini, Argentina, Brazil na Colombia.

"Tunajitahidi kuona kuwa wale wasiojiweza, tunatafuta njia za kuwasaidia ingawa kuna mazingira mengine yanakuwa magumu kwetu kufanya kazi hasa sehemu zenye migogoro," alisema Mama Mkuu huyo.

Shirika hilo ambalo lina jumuiya zake mbili nchini Tanzania ambazo ni Mahanji na Wino katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, lilianzishwa mwaka 1890 na kuingia nchini mwaka 1993.

Lengo la ziara hiyo ya wiki mbili ya Mama Mkuu huyo wa shirika ni kushiriki katika shughuli mbalimbali pamoja na masista wengine wa shirika lake nchini.

Kwa heri Sista Regina

Na Mwandishi Wetu

Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Ayu 1:21. Tulipewa na Mungu zawadi nzuri; Sr Regina Chamtwa; tulifurahi na tuliifurahia zawadi hiyo. Lakini, Mungu alipoona kuwa ni wakati muafaka kwa wokovu wake na wetu akamtwaa mtumishi wake saa na siku tusiyoitegemea tukabaki na mshtuko mioyoni mwetu.

Sista Regina alilazwa juni 28, 2000 na Julai 21, 2000, saa 12 alfajiri, akamkabidhi Mungu roho yake akiwa katika hali ya utulivu na amani katika hospitali ya Mtakatifu Fransisko iliyopo Ifakara.

marehemu alizaliwa Julai 22, 1952, kijijini Igawa katika parokia ya Biro, na alibatizwa kwa jina la BLANDINA. Alikuwa mtoto wa saba kati ya 10 wa familia ya Baba na Mama Chamtwa.

Alijiunga na Shirika la Masista wa Upendo wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi Sali ,na alifunga Nadhiri zake za Kwanza Desemba 8,1970 Itete.

1971 hadi 1974 alisoma l katika Sekondari ya Masista Kurasini Dar-Es-Salaam(siku hizi ni ofisi za Maaskofu Katoliki Tanzania TEC).

1975 hadi 1979 alichukua mafunzo ya uuguzi Ndanda, Mtwara na akawa Nesi na Mkunga.

Desemba 8,1980 alifunga Nadhiri za daima katika shirika na baadaye, alifanya kazi kwa muda mfupi katika hospitali ya Mt. Fransis, Ifakara.

Aliteuliwa kuwa Katibu wa Shirika na aliifanya kazi hiyo kwa furaha.

Kwa kuwa mahitaji ya kanisa huongezeka kila wakati kwa kulihudumia shamba lake, 1982 Sista Regina alikwenda Uingereza kwa masomo ya ulemavu wa akili, na mwaka 1983, akapata Diploma na kurudi nyumbani akiwa kati ya masista watatu waliochukua masomo hayo.

Kati ya mwaka 1984 na 1985 Novemba, alihudumia kama amuuguzi Nyumba Mama Itete. Desemba 1985, alianza kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa akili katika kituo cha Bethlehemu, Ifakara.

Akiwa hapo, aliwahi kuwa kocha wa michezo maalum kitaifa kwa watoto walemavu wa akili na aliwahi kushiriki pamoja na watoto huko Arusha, Dar-Es-Salaam, Dodoma na kwingine alipohitajika.

Alikuwa mlezi(Matron) wa kituo hicho cha Bethlehemu tangu 1992 hadi 2000, alipoaga dunia.

Sista Regina aliwahi kumsindikiza na kumuhudumia Hayati Mhashamu Askofu Patrick Iteka katika matibabu yake Uswisi, Nairobi na Ethiopia akiwa kama muuguzi.

Alianza kutetereka kiafya kwa ugonjwa wa kansa tangu mwaka 1994, lakini hakuonesha kuwa ni mgonjwa bali, alivumilia maumivu yake mpaka mwisho.

Alikuwa mtu wa fadhila ya pekee ya kuvumilia maumivu makali hata kifo huku alionesha tabasamu na maneno ya kuwatuliza waliomuuguza na waliokwenda kumwona hospitalini.

Sista Regina, alikuwa mtu wa kutotaka kuwasumbua wengine na ndivyo alivyofanya hata katika dakika yake ya kufa.

Alikuwa mvumilivu na mtendakazi aliyetambua shida za jirani zake na kuwasaidia kadiri ya uwezo wake.

Hilo limejitokeza kwa watoto walemavu wa akili aliokuwa akiwahudumia kujisikia kuwa wana mama anayewapenda na walijisikia wako nyumbani akiwa na watoto wake wote na kwa mapendo ya pekee na huruma.

Wakati huo huo: Shirika la Upendo pia lilimpoteza Sista Kahise (73) aliyefariki dunia Ifakara Oktoba 7, na kuzikwa katika makaburi ya Shirika la Itete Oktoba 9.

RAHA YA MILELE UWAPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE UWAANGAZE APUMZIKE KWA AMANI.

AMINA.

Watoa mimba watumia maduka ya dawa kufanyia mauaji

Na Peter Dominic

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalotetea Uhai(PRO-LIFE Tanzania), limewataka wenye maduka ya madawa kuwakemea wanawake wanaowaendea kutaka ushauri wa namna ya kuwaua watoto walioko matumboni kwa njia ya utoaji mimba.

Akizungumza na gazeti la KIONGOZI, Mwenyekiti wa PRO-LIFE Tanzania, Bw. Emil Hagamu, alisema hivi sasa kasi ya utoaji mimba inaongezeka katika maeneo mbalimbali nchini lakini ni vigumu kupata takwimu kutokana na baadhi ya wanajamii wakiwamo wafanya biashara mbalimbali hasa ya madawa baridi kushiri vitendo hivyo kwa tamaa ya pesa.

Hagamu alisema kuwa, baadhi ya wafanyabishara wa madawa baridi, hukubali kutoa ushauri na madawa kwa wanaotaka kutoa mimba(arbotion)ili wajipatie pesa bila kujali madhara yanayoweza kutokea wala kujali hadhi yao mbele za Mungu.

Alisema wafanya biashara hao hawana budi kuepukana na tamaa ya pesa kwa kushiriki mauaji huku wakijiua dhahiri kwamba wanashiriki mauaji ya viumbe wasio na hatia tena ambao hawajazaliwa kwa kuwa unapomsadia au kumshauri mtu namna ya kuua, hata wewe umeshiriki kuua.

Alisema kwa kuwa utoaji mimba ni kitendo kisicho halali kisheria nchini na hata kwa imani za kidini, wanawake wengi wakiwamo wake za watu, wafanya biashara, wanafunzi na makahaba, wamekuwa wakifanya mauaji hayo kisirisiri majumbani mwao na katika zahanati za vichochoroni baada ya kupata ushauri toka kwa baadhi ya wenye maduka ya madawa.

BW. Hagamu alisema hali hiyo imesababisha ugumu wa upatikanaji wa takwimu za matukio hayo ya kikatili.

"...Unajua Bw.(mwandishi)kama hiki kitendo kingekuwa halali, takwimu zingepatikana bila tatizo lakini sasa, ni illegal, wanaofanya arbotion wanajificha na hii imetufanya tupate ugumu wa kupata takwimu.

Kwa mfano, wanapokwenda kwenye dispensary huko vichochoroni au kwenye baadhi ya maduka phamarcy, huwezi kupata takwimu huko; wanajua ni illegal," alisema Mwenyekiti huyo wa PRO-LIFE Tanzania.

Aliihimiza jamii wakiwamo wafanya biashara hao wa zahanati na madawa baridi, taasisi mbalimbali za kidini na wote wenye mapenzi mema, kushirikiana ili kukemea mauaji hayo yanayofanyika katika jamii kwa njia ya utoaji mimba kwa kuwa licha ya kuwa kinyume cha sheria, pia ni dhambi kwa Mungu.

Makatekista wa Madunda waadhimisha Jubilei ya fedha

Na Getrude Madembwe

CHUO cha Makatekista cha Madunda kilichopo katika Jimbo Katoliki la Njombe, kimeadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Sherehe hizo zilizoambatana na mahafali ya wahitimu 28 wa kozi hiyo ya Ukatekista, zilifanyika Oktoba 24, mwaka huu chuoni hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na Kanisa akiwemo Makamu wa Askofu Padre Justin Sapala.

Akizugumza katika sherehe hizo, Katibu Mtendaji wa Idara ya Katekesi katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Sista Claudia Mashambo, alisema makatekista wote hawana budi kutafuta thamani kubwa ya kumjua Yesu Kristo.

"Hamna budi kupoteza kila kitu ili mumpate Kristo na yeye Kristo awe ndani yenu na mkamfundishe kwa watu wengine ili wapate kumfahamu," alisisitiza Sista Mashambo.

Akiongea katika ibada hiyo, Msaidizi wa Askofu Jimboni humo, Padre Justin Sepula, aliwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kumtanngaza Kristo ulimwenguni pote

Padre Sepula katika kusisitiza kauli yake, alimpatia mhitimu, Biblia na msalaba ili waweze kufanya kazi hiyo ya wito kwa kumtumainia Bwana.

Aidha, Katibu Mtendaji wa Idara ya Kichungaji(TEC), Padre Theobald Kyambo, aliwahimiza wahitimu hao wafanye kazi kwa uaminifu wakishirikiana kwa karibu na mapadre na waamini wengine.

"Mnatakiwa mfanye kazi yenu ya ukatekista kwa uaminifu mkubwa mkishirikiana kwa karibu sana na mapadre," alisema Padre Kyambo.

Katika risala yao, makatekista hao wahitimu, walimshukuru Askofu Mwanyika kwa kuboresha chuo hicho kiroho, kitaaluma na kiuchumi.

Aidha, walimshukuru kwa juhudi zote anazozifanya na vitu vingine vingi ambavyo ameviboresha Baba Askofu Mwanyika.

Mahafali hayo yalikuwa ya nane tangu chuo hicho kianzishwe mwaka 1976 na kozi hiyo inachukuwa muda wa miaka mitatu.

Jamii yashauriwa kubadilika na kumgeukia Mungu

Na Festus Mangwangi, Arusha

JAMII imeshauriwa kuishi maisha mapya kwa kukubali kutubu na kumpokea Mungu kwani kwa kufanya hivyo, itakuwa imepata nafasi ya kuishi maisha bora na endelevu kiroho na kimwili.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Kituo cha Agape(Agape Centre) nchini, Padre Etiene Sion, wakati kituo chake kilipotoa semina ya Wiki ya Neema kwa wakazi wa Ngaramtoni katika Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.

Padre Sion, ambaye pia ni Mratibu wa Karismatiki nchini, alisema matendo maovu yanayoonekana kukithiri ndani na nje ya nchi, yatapungua ama kuisha kabisa endapo jamii itakubali kujirekebisha.

Semina hiyo iliyoendeshwa na wajumbe mbalimbali kutoka Kituo cha Agape, ilihudhuriwa na watu wa dini na madhehebu mbalimbali wakiwemo ya Kikristo na Kiislamu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, baada ya semina hiyo, baadhi ya washiriki walikiri kunufaika na semina hiyo na wengi wao wameahidi kumrudia Mungu.

"Kwa kweli nimeonja upendo na huruma ya Mungu Baba na namna pekee katika wiki hii, namshukuru Mungu kwani nimeweza kuondokewa na maumivu ya titi langu la kulia ambalo kwa miaka mingi halikuweza kusikia dawa," alisema mshiriki mmoja wa semina hiyo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Katika kuishukuru timu hiyo ya Agape, Paroko wa Parokia Katoliki ya Ngaramtoni Padre Pastori Kijuu, alisema kuwa shukrani za dhati zitakuwa na maana zaidi endapo washiriki wa semina hiyo wote kwa pamoja, wataamua kuanza kuvaa tena utu upya na kuuvua ule wa kale kwa maneno na matendo.