SMZ yakiita CUF- Chama cha Uchochezi na Fujo

lYatamba: China, India, Libya,Iran, Misri na Japan zinaisaidia

Arnold Victor

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzabar (SMZ) imedai kuwa sera za "Jino kwa Jino" zinazotangazwa na CUF zinaonyesha kuwa chama hicho si chama cha wananchi kama kinavyoitwa bali ni chama cha uchochezi na fujo. Wakiongea na waandishi wa habari jijini katikati ya wiki, mawaziri wa Zanzibar, walisema hawana imani na mwafaka waliowekeana na CUF kwa vile chama hicho kimekuwa kikitoa kauli zinazotishia amani tangu kuanzishwa kwake.

Waziri anayeshughulikia masuala ya nchi za nje wa SMZ, Balozi Isaack Sepetu, alidai katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini kuwa chama cha CUF kiliwahi kutamka hadharani kuwa kitakomesha utawala wa mtu mweusi Tanzania Visiwani, jambo ambalo linaashiria ubaguzi wa hali ya juu wa rangi na ambao unaonekana kuwa kiini kikubwa cha kukwama kwa usuluhishi wa mvutano wa kisiasa visiwani humo.

Alidai pia kuwa CUF kimewahi kutangaza kuwa wanawake wa visiwani wajiandae kuishi kizuka(bila waume) kwa vile kuna hatari kuwa waume zao wote watakufa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kauli kama hizo, alisema Sepeku zinaonyesha kuwa CUF si chama kinachowatakia Watanzania mema.

Hata hivyo, SMZ na CCM wamekuwa wakishutumiwa kwa kuvunja haki za binadamu na kukandamiza demokrasia, kiasi cha kukatiwa misaada na nchi mbali mbali hususan zile za Nordic.

Hali hiyo imelifanya jina la Zanzibar kuwa chafu katika Jumuiaya ya kimataifa.

Serikali hiyo imesema kuwa haijali sana kukatiwa misaada kwa vile nchi nyingine kama China,India,Iran, Libya, Misri na Japan zimekuwa zikiisaidia.

Maonesho ya mavazi ya Kikristo kufanyika Dar

Na Getruder Madembwe

WAZIRI Mkuu Fredrick Sumaye Jumamosi hii anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilei Kuu yatakayoambatana na maonesho ya mavazi(Fashion Show) ya Kikristo.

Maadhimisho hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Karimjee Jumamosi hii yataandamana pia na maonesho ya kazi mbali mbali za mikono za akinamama hao.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake hivi karibuni, mmoja wa wanakamati wa Kamati ya Maandalizi ya Jubilei hiyo Bibi Grace Katina, alisema, mavazi yatakayooneshwa ni yale yanayotunza heshima ya wanawake na sio yale yanayotia aibu na kuwadhalilisha.

Alisema kama ilivyo kwa maonesho ya mavazi ya "walimwengu," akina mama Wakristo waliovalia mavazi hayo watapita mbele ya jukwaa ili kuweza kuyaonesha.

Bibi Katina, ambaye ni mfanyabiashara wa mapambo ya akina mama, amesema katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonesho ya mavazi(Fashion show) ambayo yanafaa kuvaliwa na akina mama pamoja na akina dada yaani mavazi ya Kikristo.

Mbali na maonesho hayo, pia kutakuwepo na mada mbalimbali zitakazotolewa zikiwa ni pamoja na "Umoja na Mshikamano" ambayo itatolewa na Askofu Charles Salala wa African Inland Church (AIC),

"Wajibu wa Mwanamke" itakayotolewa na Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Mama Olive Luena, wakati Padre Lugendo, wa Kanisa la Anglikana Kurasini, atazungumzia "Amani."

Uenezaji wa Injili, ni mada ambayo itatolewa na Mama Grace Kulambo wa shirika la Kiinjilisti la African Evangelistic Enterprises-AEE).

Vile vile Bibi Katina alisema kuwa kutakuwa na maombi maalum ambapo Kanisa Kikatoliki litaombea amani ndani ya familia pamoja na Taifa kwa ujumla, Kanisa la Baptisti litaombea tishio la maisha ya wengi pamoja na waliopatwa na ugonjwa wa Ukimwi, wajane na wengine waliokata tamaa kutokana na hali ngumu ya maisha. Kanisa la Kilutheri litaombea Umoja na Mshikamano wa Makanisa udumu.

Kuwaombea wanawake wote wawe walezi bora wa familia zao, ni maombi ambayo yatafanywa na Kanisa la Moroviani na maombezi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao yatafanywa na Kanisa la Presybiterian.

Epukeni wagombea wanaogawa vitenge, pilau kupata kura zenu, mtavuna kilio

Elizabeth Steven na Peter Dominic

"WATU watumie ukomavu kiakili katika kushughulikia maamuzi na majukumu muhimu. Sio eti wagombea wawadanganye kwa pilau, vitenge na chumvi. Mgombea anayekuja namna hiyo, ni mwanasiasa uchwara ambaye kesho atawageuka aanze kufidia kwa kuwaibia na kutokuwajibika."

"Mgombea hata kama ni Mkristo, afanye kazi; si tu kwa manufaa ya Wakristo wenzake, wala ndugu zake; eti aseme, nawafaidisha ndugu zangu wenyewe, bali kwa manufaa ya jamii yote,"

Alisema Askofu Mteule wa Jimbo la Geita , Mhashamu Damian Dallu, alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini katikati ya juma alipotakiwa kuzungumzia Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani na kutoa hisia zake baada ya kuteuliwa kwake kuwa askofu.

Alisema jamii haina budi kumchagua kiongozi ambaye hata yeye mwenyewe anaamini na kuthamini ukweli kwamba maendeleo hayana budi kutiliwa mkazo kwa watu na wala sio kwa vitu kama jamii nyingi zinavyoelekea kuthamini mali kuliko utu.

Akisisitiza umuhimu wa kuthamini maendeleo ya watu kuliko vitu, Mhashamu Dallu, alisema, "Hata kiimani ni wazi maendeleo yanayokubalika ni maendeleo ya watu kiroho na kimwili na sio vitu kwa sababu hatuwezi kusema eti Watanzania tuna maendeleo kwa kuangalia magari na majumba; vingine vikiwa ni mali za wizi, mpaka pale tutakapoona watu wanapata mahitaji muhimu kwa njia inayompendeza Mungu. "

"Viongozi hao hata kama ni madiwani, au Rais au hao wabunge, tuchague wale wanao lilia maendeleo ya jamii sio wale wanaotaka wao wenye wawe matajiri wa kupindukia. We kiongozi hukupelekwa kule kupaparamia vitu na kuwa tajiri wa kupindukia, hasa kwa Mkristo uliyeiva!

Lazima kiongozi aone kuwa ni dhambi asipotimiza wajibu kwa watu wake. Na suala hili si tu, eti ni Wakristo pekee au Waislamu, bali watu wote; hatuwezi "ku- locallize" vitu vya namna hii" "Mtu anyetaka kugombea nafasi yoyote iwe ni urais,ubunge au udiwani ajiulize maswali kwanza atawasaidiaje watu wa Mungu,kama kweli wewe umeumbwa na mungu unatakiwa umsaidie mwenzako kwa nafasi yako uliyopo,isiwe ni kutumia porojo,wakati kundi kubwa la watu wanaumia ukisahau kabisa maana ya kutawala",

Askofu Mteule Dallu ambaye ni Mkuu wa Taaluma katika seminari Kuu ya kiteolojia ya Segerea na mwalimu wa maadili, alisema kuwa na mali sio mwisho wala ruksa ya kutotazama maendeleo na hadhi ya watu wengine, bali iwe ni alama nzuri ya kuwashirikisha watu katika kuyafanya mapenzi ya Mungu.

"serikali haina budi kushughulikia zaidi maendeleo ya mtu na kumpa nafasi ya kufanya maendeleo yake binafsi bila kutoa uhuru kwa mtu binafsi kuingilia na hatimaye kuvuruga mahaitaji ya jamii," alisema.

Aliwashauri Watanzania kuondoa kasumba ya kutegemea kuongezwa kwa mishahara kila yanapofika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, bila kujali hali halisi ya uchumi na pato la taifa.

Akitoa hisia zake kufuatia kuteuliwa kwake kuwa askofu Jimbo la Geita, Mhashamu Dallu , alisema, "Ingawa mwanzo wa taarifa hizo zilinishitua nikahofu kama mtu mwingine yeyote, sasa ninafarijika kwa kuwa najua sitaifanya kazi hiyo peke yangu bali kwa ulinzi na msaada wa Bwana Yesu maana sasa ninaenda kuwa Mwalimu wa watu wengi mno; tena wa ngazi tofauti; wakubwa kwa wadogo tofauti na hapa (Seminari ya Segerea) ambapo nilikuwa mwalimu wa kikundi fulani cha watu."

Mei 6, mwaka huu, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, kupitia ubalozi wake nchini, alitangaza uteuzi wa Damian Dallu (44),aliyekuwa Padre na Mwalimu wa Taaluma katika seminari Kuu ya Segerea kuwa Askofu Jimbo la Geita

Nitajipendekeza nipewe ubunge - KK

Na Leocardia Moswery

MBUNGE wa Jimbo la Kigamboni Bw. Kitwana Kondo amesema anaamini kuwa yeye na Rais Mkapa wataendelea kushika nafasi za uongozi hadi mwaka 2005 kwani watajipendekeza kwa Mungu awahurumie na kuwarudisha madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kitwana Kondo aliyasema hayo Jumapili iliyopita katika sherehe za kumpongeza Bw. Kassim Ngamba, baada ya kushinda nafasi ya uenyekiti wa eneo la Mbagala_Kizinga, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji.

Katika Uchaguzi huo uliofanyika mwaka jana, CCM ilishinda na kujinyakulia viti vyote katika eneo hilo.

Bw.Kondo maarufu kwa jina la KK, alisema anaamini kuwa ubunge alipewa na Mungu kupitia kwa wapiga kura, na hivyo atazidi kujipendekeza kwa sala na huduma bora kwa wananchi ili Mungu ampe tena nafasi hiyo ya ubunge kwa mara nyingine katika Jimbo la Kigamboni jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema, kwa nguvu za Mungu, hata kama mpiga kura hamtaki, atajikuta tayari amekwisha mpigia kura. "Hata kama ulikuwa unataka kumpa tiki kijana au mgombea mwingine, utasahau tu; na utajikuta ukinitiki mimi", alisema na kuongeza.

"Nimetumia uzee wangu kuleta maendeleo jimboni kwangu kwa kuwa nikienda kwa Waziri au Rais, naambiwa pita mzee. Mzee anathamani mno na huu uzee umenisaidia kutimiza wajibu wangu katika kata ya Mbagala."

Aliyataja baadhi ya maendeleo anayoamini kuwa yametokana na juhudi zake katika eneo lake kuwa ni pamoja na kuweka klinki ya wazazi, shule, barabara na visima na huduma nyingine.

Wakati huo huo: Katika sherehe hizo, Kitwana Kondo amewakabidhi kadi za CCM, kwa wanachama wapya wapatao 20 ambao wameamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.

Uchaguzi mkuu wa Rais,Madiwani na Wabunge unatariwa kufanyika Oktoba mwaka huu na hii itakuwa ni mara ya pili tangu uingie mfumo wa vyama vingi.

 

SHDEPHA+ yahofia bei ya dawa ya ukimwi nchini

Na Dalphina Rubyema

Chama cha Maendeleo kwa Watu wanaoishi na Virus vya Ukimwi (SHDEPHA+), kimesema kina wasiwasi ya kutokupungua kwa bei ya dawa ya kuwasaidia wagonjwa wa ukimwi kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kusema hicho ni kitendawili.

Mwenyekiti wa SHDEPHA+ kitaifa Bw. Joseph Katto, ameliambia KIONGOZI ofisini kwake jijini kuwa ana wasiwasi kuwa, huenda Wizara ya Afya ikagawa dawa hizo majeshini, kwa viongozi wa ngazi za juu na kuwasahau waathirika wenye kipato duni na kuongeza kuwa hali hiyo badala ya kupunguza, inaweza kuongeza bei ya dawa hizo.

Bw. Katto alidai kuwa kwa mujibu wa habari ambazo zimekuwa zikifikia ofisi yake bila kuthibitishwa popote, serikali ya Tanzania imekuwa ikiagiza dawa hizo hata kabla Marekani haijapunguza bei yake lakini, haijulikani ni akina nani wamekuwa wakizitumia.

Hata hivyo Bw. Katto amewasisistiza Watanzania kujua kuwa dawa hizo si kwa ajili ya kutibu ukimwi bali tu, zinawasaidia kuzuia kasi ya magonjwa yanayomshambulia mgonjwa wa ukimwi na kumuongeza nguvu na siku za kuishi mgonjwa.

"Tusifungue milango ya uasherati kwa kujipa matuini kuwa dawa imepatikana, hiyo siyo ya kutibu, ni ya kupunguza makali yaukimwi.

Pro-Life yalaumu mashirika yasiyo ya Kiserikali

Na Peter Dominic

CHAMA cha kulinda na kutetea uhai wa binadamu PRO-LIFE (TANZANIA), kimeyashutumu vikali mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’S) yanayoshughulikia masuala ya afya ya kizazi kwa vijana kutaka kuishawishi Serikali iruhusu elimu hiyo ifundishwe mashuleni.

Shutuma hizo zimetokana na mashirika hayo kufanya warsha ya afya ya kizazi, Mei 3 na 4, mwaka huu huko Tanga na kuripotiwa na gazeti moja la Kiingereza hapa nchini litokalo kila siku ambalo liliandika kuwa somo la utumiaji wa kondomu hufundishwe masuleni.

Akitoa shutuma hizo kwa mashirika hayo, Mwenyekiti wa PRO_LIFE (TANZANIA), BW. Emil Hagam, alisema katika semina hiyo, Kiongozi wa Mradi wa Afya wa Shirika la Ushirikiano la Kiufundi la Ujerumani (GTZ) alitaka somo la uzazi wa mpango lifundishwe mashuleni jambo ambalo litawasababishia watoto kujishirikisha katika vitendo viovu.

"kuwapatia watoto wa shule za msingi elimu ya uzazi na matumizi ya kondomu.

inajenga mawazo potofu na kutoa uhuru kwa watoto kushiriki vitendo vya uasherati kwa kujamiiana bila kuwekewa vizuizi na kujenga ujasiri kwa watoto wa kike kuwa hawatapata mimba zisizotarajiwa pamoja na magonjwa ya zinaa kwa kuwa watatumia kondomu"alisema Bw.Hagamu.

Alielezea hali hiyo kuwa ni ya hatari na inalielekeza pabaya taifa kwa kuwa itachangia kupata mimba na kumpa uwezo wa kutoa mimba.

"Iwapo wanasemina walifikia hatua ya kuishawishi Serikali ili watoto wa shule za msingi wafundishwe matumizi ya kondomu hawaoni kwamba ni kuwatumbukiza katika dimbwi la ufuska na vifo vitokanavyo na magonjwa kama Ukimwi!"

licha ya watengenezaji wa Kondom kuwatahadharisha daima kuwa kuna uwezekano wa kupata maambukizo ua ugonjwa huo. alisema

Kwa mujibu wa Bw. Hagamu, takwimu zilizotolewa na jarida la ‘Population Reports’ (Series H. No: 8 Septemba 1990 zilitoa sababu kuwa kupasuka kwa kondomu hotokana na matumizi mabaya, mazingira mabaya ya hifadhi na kuathirika zaidi kwa joto.

Alisema pia, utafiti uliofanyika huko Indonesia mwaka 1986 ulionesha kuwa asilimia 7 ya kondomu mpya zilipasuka wakati wa kujamiana na asilimia 20 ambazo zilihifadhiwa katika mazingira ya joto zilipasuka,

"Hivi elimu juu ya matumizi ya kondomu ndiyo tunayopenda watoto wapewe mashuleni na si ndiyo sawa na kuwapa watoto wetu urithi wa ngono?" alihoji Bw. Hagamu.

Hagamu alizidi kulalamika kwa kusema "najua lengo la warsha hiyo lilikuwa kugawa kwa watoto vidonge vya majira, kondomu, vipandikizi, vitanzi na sindano za depo ili waweze kujamiana bila kupata mimba badala ya kuwajenga kwa kuwafundisha maadili mema kwa kukuza vipawa vyao.

Aliendelea kusema kuwa mawazo ya wanawarsha ya kutaka wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitatu wafundishwe elimu ya kizazi sio mapya bali yanaitikia wito wa mashirika makubwa duniani yanayodhamiria kuharibu maadili ya watoto na vijana popote yanapofundishwa.

Soko la Tandika lamjazia Mkurugenzi sifa lukuki

Dalphina Rubyema na Josephs Sabinus

WAFANYABIASHARA wa soko la Tandika katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar-Es-Salaam, wamempongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Idd Nyundo kwa kuonesha ushirikiano wa karibu na kuwajali.

Wakizungumza kwa pamoja na gazeti hili ofisini kwao katikati ya juma,viongozi wa soko hilo ambao ni Mwenyekiti Bw.Mohamedi Sihoja na Katibu wake Bw.Joseph Boniphace walisema tangu Mkurugenzi huyo ahamie katika Manispaa hiyo miezi michache iliyopita ,soko hilo limeanza kupata maendeleo makubwa na hii yote inatokana na juhudi zake, ushirikiano na upendo wake kwao.

Wakifafanua maendeleo hayo, walisema hatua kubwa imepigwa juu ya uboreshaji wa huduma mbalimbali sokoni hapo ikiwemo ile ya choo iliyokuwa tatizo lililoota mizizi wakati wa uongozi wa Mkurugenzi aliyepita Bw.Idan Munisi.

"Enzi za uongozi wa Munisi hali yahuduma ya sokoni hapa ilikuwa mbaya sana ,vyoo vyote vilifurika lakini baada ya kuja huyu Mkurugenzi mpya hali imebadilika na kuwa nzuri sana ,vyoo vinafyonzwa mara mbili ama tatu kwa wiki,havijai kama ilivyokuwa zamani"alisema Mwenyekiti.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa Mkurugenzi huyo mpya anatembelea soko hilo mara kwa mara na hii yote ni kuangalia hali ya usafi na matatizo ya wafanyabiashara.

Alisema Katika kuonesha ni jinsi gani anajali soko hilo, mwanzoni mwa wiki hii ilitoa vifaa vya usafi ambavyo ni tolori mbili, viatu vya buti pea nne, umma nne za kuzolea takataka na mifagio miwili ya cheleo.

Hata hivyo thamani ya vifaa hivyo hawakuweza kutaja mara moja thamani ya vifaa hivyo.

Katibu wa soko hilo alisema mbali na kupokea vitendea kazi hivyo, uongozi wa soko pia umempelekea maombi Mkurugenzi huyo ya kupatiwa huduma ya maji,umeme na kifusi.

Alisema soko hilo limekuwa likabiliwa na uhaba wa maji takribani miaka ishirinii sasa hali inayowalazimu wafanyabiashara hao kununua maji kwa sh.50-150 kwa ndoo moja kwa ajili ya kusafishia mbogana matunda sokoni hapo pamoja na matumizi mengine.

Wakizungumzia suala la umeme, Katibu huyo Bw.Joseph Boneface alisema kuwa ni tatizo ambalo limedumu kwa zaidi ya miaka mitano na endapo utapatikana utakuwa umepunguza tatizo la ulinzi wa mashakani ambao unasababishwa na kutanda kwa giza wakati wa usiku.

Alitoa ufafanuzi juu ya kifusi,katibu alisema kitatumika kufukia mashimo kadhaa yaliyopo sokoni hapo

WAWATA Arusha wawalaumu wanaowauza wasichana

Reginald Barhe, Karatu

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo la Mbulu, Mwalimu Elizabeti Massinda amewaonya wanawake wanaowatumia wasichana wao kama vitega uchumi kujipatia fedha kwa kuwauzia wanaume badala ya kuhimiza uadilifu kwa kuwa ni hali hiyo ni hatari kiafya na kijamii.

Ameonya katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi mjini hapa kuwa athari hali hii imeenea hadi vijijini ambako siku hizi sasa hata wanafunzi wa madarasa ya nne na tano hupata mimba na magonjwa ya zinaa kama ukimwi kutokana na walezi au wakubwa wa wasichana hao kuwauza kwa wanaume.

Massinda amewataka wanaume wawajali watoto hao na kuwaheshimu bila kuwaonea kijinsia na kiumri kwa kuwatumia kama watumwa kikahaba ndani ya maeneo ya starehe, "wajiulize tu je kama ni watoto wao wenyewe je, wangewatendea hivyo?"

Ameonya kuwa endapo Watanzania hawatadumisha uadilifu miongoni mwao, ipo hatari ya kupoteza sifa nzuri ambayo nchi hii imejipatia kwa kuwa kisiwa cha amani, umoja, utulivu, pendo na mshikamano wa kitaifa.

Amewahimiza viongozi wa madhehebu kidini, serikali na vyama vya siasa wahakikishie wanatumia nafasi zao kuielimisha zaidi jamii ya watanzania ili kulinda tunu zote zinazojenga mapendo, maelewano na umoja baina ya Watanzania wote bila kujali tofauti za kidini, kikabila, jinsia wala itikadi za kisiasa.

Aliilaani vikali hali ya kuathirika vibaya kwa maadili miongoni mwa vijana inayozidi kuendelea kutokana na kuchangiwa kwake huku viongozi hao wakizidi kukaa kimya na kuonea haya uharibifu unaoonekana bayana miongoni mwa vijana, wanawake na watoto.

Amesema vitendo vya uhalifu vikiwamo vya ukahaba, unyang’anyi,ubakaji, uvutaji bangi, utoaji mimba na maonevu dhidi ya wanawake na watoto, vinatokana na kubomoka kwa misingi bora ya kijamii ndani ya jamii na baadhi ya viongozi kutokuyapa kipaumbele mazingira yanayostawisha tunu bora za uadilifu uaminifu na upendo.

Amewashutumu wazazi kwa madai kuwa wanachangia uharibifu huo wa maadili kutokana na wao kuupuzia uharibifu huo bila kuukemea huku wakiona jamii inazidi kuangamia ikisingiziwa kuwa inatokana na kisingizio cha kwenda na wakati na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia na kuacha.

Ndoa nyingi na maadili mbalimba ya kidini na kijamii yakitoweka.

Alisema ingawa wanaume wamekuwa wakilaumiwa zaidi kuhusu suala la ubakaji, wanawake wanastahili pia kulaumiwa kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakijiweka katika mazingira yanayochechea matendo hayo maovu.

Aliongeza kuwa hata wazazi ndani ya familia nyumbani, wamekuwa nyuma katika kukemea

Na akasema hali hii pia inachangia kuenea kwa vitendo vya ukahaba na magonjwa ya zinaa ukiwamo ukimwi na kuongezeka idadi ya watoto wa mitaani baada ya familia zao kusambaratika.

‘Ukimwi unachangia ubakaji’

Na Sr. Dafroza Msemwa, Morogoro

UKIMWI umeelezwa kama ugonjwa unaochangia kuwepo kwa vitendo haramu vya unajisi na ubakaji kwa watoto wadogo kwa kuwa baadhi ya wanaume wakwale huwafanyia unyama huo wakiamini kuwa watoto wadogo ni salama dhidi ya ukimwi.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice, katika Jimbo Katoliki la Morogoro, Padre Andreas Maftaha, wakati akifungua semina ya Akinamama wa Shauri Jema kutoka majimbo Katoliki ya Tanga na Morogoro katika Ukumbi wa VETA mjini hapa.

Alisema moja wapo ya madhara makubwa ya ugonjwa wa Ukimwi katika familia, ni kulelegalega kwa ndoa nyingi hasa pale mmoja wa wanandoa anapobaini kuwa mwenzake ana ukimwi na hivyo kutokuwa tayari kushirikiana naye kimwili na hali hiyo ndiyo inayochochea wakimbilie kwa watoto wasio na uwezo wa kuamua kwa usahihi.

Alisema wengine hukimbilia kuwabaka hata watoto wachanga kwa kuwa wanaamini kuwa wale bado hawajaathirika na ugonjwa wa ukimwi na hivyo kuwafanyia viumbe hao kitendo hicho cha kinyama kisichomtofautisha mwanadamu huyo na mnyama wa porini.

Aliongeza kuwa ingawa kila mtu atakufa, ipo haja ya kumwamini na kumtegemea Mungu katika maisha yao ya baadaye na akaitaka jamii isijidanganye juu ya matumizi ya kondomu, alizozifananisha na ndege iliyobeba bomu kwani hakuna uhakika wa kutoambukizwa ukimwi kwa mtu anayetumia.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, aliwataka watu wasio na Ukimwi kuhakikisha hawaupati ugonjwa huo na wale walio nao wasikate tamaa wala kuambukiza wengine.

Aliwataka akinamama hao wa Shauri Jema kuwa washauri wema wa wagonjwa wa Ukimwi na wala wasiwakatishe tamaa na badala yake wawatie moyo ili waweze kufa kwa matumaini.

"Ushauri wenu ni lazima uwe mzuri, ujifanye nawe una ukimwi, kwa njia hiyo mtawasaidia watu. Tukumbuke dawa haijapatikana mpaka sasa. Unapoongea na mgonjwa usimdanganye kuwa atapona wakati unajua ukweli kuwaatakufa, ataacha familia, utajiri na mali nyingine, kiroho anakata tamaa anahitaji msaada sana’ alisema Padri Muftaha.

Naye Mratibu Faraja Trust Fund, Batholomeo Tarimo, wakati akizungumza katika semina hiyo, alisema pamoja na kwamba akinamama ni watu wenye huruma lakini wanapaswa kuwa macho katika swala la Ukimwi kwenye maisha yao ya ndoa.

Wabwagieni maiti waajiri wanaokataa kuwasafirisha -TUGHE

Na.Mathias Marwa, Musoma.

Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE)wameshauriwa kupeleka na kuwabwagia maiti za ndugu zao, waajiri wanaokataa kuwasafirisha wafanyakazi wao wanapofariki na

Ushauri huo ulitolewa na Katibu wa TUGHE mkoa wa Mara, Bw. Watson Rushakuzi, wakati akizungumza katika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa uliofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini hapa.

Alisema baadhi ya waajiri wamekuwa wakikataa kwa makusudi kusafirisha maiti za wafanyakazi wao wanapofariki dunia kwa kusingizia kuwa hawana fedha kitu ambacho alisema si kweli na ni kinyume cha mkataba wa kazi kati yao na kwamba ni kuwanyima wafanyakazi haki yao na kutothamini mchango wao kwa kuwa wamekufa.

Bw. Rushakuzi aliwataka wafanyakazi kuwa na umoja na mshikamano katika kudai haki zao na kwamba ikilazimika wabebe maiti ya wafanyakazi ambao ni ndugu zao, waipeleke kwenye ofisi husika hadi watakapokubali kusafirisha maiti hiyo.

Alisema wakati umefika wa kudai haki kwa nguvu zote lakini akawatahadharisha wakati wote wanapodai haki zao, waepukane vitendo vyovyote vya ukiukaji wa sheria za nchi na uvunjaji wa amani.

Katika uchaguzi huo, Bw. Eliapenda Kimaro alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa TUGHE wa mkoa, na Bw. Daudi Chiremeji kuwa mjumbe wa Baraza Kuu.

Wengine waliochaguliwa kuunda Kamati hiyo ya utendaji ni Charles Musiba, Milton Peter, Mwemwa Mulemwa, Perusi Milambo, Hasani Juma na Donald Makuja.

Dawa ya Maendeleo ni ushirikiano-AMREF

Leocardia Moswery na Neema Dawson

ushirikianao umeelezwa kuwa ndiyo njia pekee itakayowezesha kupatikana kwa maendeleo katika jamii katika ngazi zote za jamii na sio kuwatupia mzigo wote wa majukumu viongozi pekee katika uwajibikaji.

Hayo yalisemwa na Mkurungezi wa Shirika la AMREF nchini Dk, Daraus Bukenya alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 21 ya uendeshaji huduma ya Jamii katika masuala ya afya na uhai wa mtoto ambapo wahitmu 120 walitunukiwa vyeti.

Wahitimu hao pia walipewa baadhi ya vitendea kazi vilivyokabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Bw. Iddi A. Nyundo.

Akipokea vifaa hivyo, Mkurugenzi huyo wa Temeke alisema, kuwa kupokea vitendea kazi si njia pekee ya kutatua matatizo yaliyopo bali suluhisho ni kuvitumia ipasavyo na kuhakikisha kuwa hata vilivyopo vinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio kwa mapambano

Vifaa villivyokabidhiwa kwa ajili ya kutoa huduma hizo za afya ni pamoja na pikipiki 3, baiskeeli 25, mizani 23 za kupimia watoto na dawa ya huduma ya kwanza.vyote vikiwa na vikiwa na thamani ya sh. Milion 20.

Dk. Bukenya alisema kuwa Shirika lake la AMREF lilianza kutoa huduma nchini Tanzania tangu mwaka 1960 ambapo wafayakazi wake walikuwa wakitokea nchini kenya na kurudi mara wanapo maliza huduma zao.

Akiusifu ushirikiano mzuri baina ya shirika lake na Tanzania, Dk. Bukenya, alisema, walipoona ukizidi kuimarika, walishawishika na kuona ipo haja zaidi ya kuweka tawi lao ili kuimarisha huduma zao nchini

AMREF lilianza kutoa huduma kwa akina mama na baadaye kwa watoto kuanzia umri wa miaka 5 walioathirika na magonjwa sugu.

TTCL yachuma matunda ya jasho lake

Na Dalphina Rubyema

KAMPUNI ya Simu nchini (TTCL) imepata faida ya shilingi bilioni 26 kwa kipindi cha mwaka 1998 na 1999,imefahamika.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bibi Asenath Mpatwa imesema mwaka juzi Kampuni hiyo ilijipatia mapato ya shilingi bilioni 90 ambapo faida ilikuwa shilingi bilioni 10. Mwaka jana mapato yaliongezeka na kufikia bilioni 105 kwa faida ya shilingi bilioni 16.

Taarifa zaidi kutoka kwa Kaimu huyo zinasema jumla ya wilaya 45 nchini zinanufaika na huduma ya simu zenye kutumia STD na wanaendesha zaidi ya vituo 500 vya simu za kulipia zikiwemo zile za boksi.

Kampuni hiyo ambayo kwa hivi sasa inatarajia kutoa huduma ya simu za mkononi imeahidi kujiingiza ipasavyo katika mashindano ya mtandao katika ngazi ya kitaifa na kimataifa ili kuboresha huduma zake kwa kutumia mitambo yenye uwezo wa kuanzia Kbps 64 hadi Mbps 2 na zintarajiwa kufikia Mbps 8 (E2).

Zoezi hili tayari limeishafanyika katika mikoa ya Dar-Es-Salaam, Arusha, Mbeya, Zanzibar na Mwanza nalinatarajiwa kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania.

Wakati huo huo,Kaimu Mkurugenzi huyo Mtendaji katika taarifa yake aliyoitoa kwenye sherehe za siku ya Mawasliano ya simu duniani ambayo hapa nchini ilifanyika katika hoteli ya Sea Cliff, jijini Dar-Es-Salaam, alisema kuwa uwezo wa simu za moja kwa moja zimeongezeka kutoka 129,998 hadi kufikia zaidi ya 200,000 na hii ni katika kipindi cha mwaka 1994 hadi hivi sasa na akawahimiza watanzania kuendelea kutoa ushirikiano kama uliooneshwa awali na kuzidi kaboresha huduma zake.

Kampuni ya Simu nchini TTCL imekuwa ikisifiwa kwa kuwa imeboresha zaidi huduma zake na watu wengi hivi sasa wanasubiri kwa hamu simu zake za mkononi.