Dk. Omar ashindwa kumvumilia Makamba

lAsema ingawa haipendezi viongozi wa Serikali kupingana hadharani, imebidi

Peter Dominic na Arnold Victor

MAKAMU wa Rais Dk.Omar Ali Juma, hivi karibuni alilazimika kumpinga hadharani na mbele yake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusufu Makamba, kufuatia maagizo yake yasiyoambatana na utafiti wa hali halisi ya mambo.

Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni wakati Dk. Omar alipotembelea shamba la Chama cha Wanataaluma Wakatoliki nchini (CPT) akiwa katika ziara yake ya kutembelea maeneo mbali mbali ya mkoa wa Dar es Salaam.

"Japo haipendezi serikali kupingana hadharani lakini napenda kusahihisha uamuzi na kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba wananchi wana haki ya kuvamia mashamba ambayo hayajaendelezwa na kuyachukua," alisema Dk. Omar na kuongeza kuwa inafaa inapobidi hatua kama hiyo kuchukuliwa basi sheria ifuatwe na sio ubabe.

Awali wakati akimkaribisha Dk. Omar kujibu risala ya wana-CPT, Luteni Makamba, aliwaonya wana-CPT waachilie shamba hilo lililopo Bunju A, nje kidogo ya Jiji ambalo limegawiwa kwa wananchi kwa maagizo yake (Makamba) akidai kuwa wao kama Wakristo hawastahili kudai warejeshewe.

"Ninyi ni Wakristo. Mmepewa bure, toeni bure," Luteni Makamba aliwaambia wana-CPT akinukuu Biblia.

Hata hivyo, akijibu risala ya CPT ambayo ilieleza kwamba shamba hilo lenye mazao ya wananchi ni lao na kwamba wanakusudia kulitumia kwa ajili ya maendeleo ya jamii, Dk. Omar aliasa kwamba Tanzania inaongozwa na sheria, hivyo Mkuu wa Mkoa wala uongozi wa kijiji cha Bunju A, hawakuwa na haki ya kuligawa kwa wananchi kabla ya kuwasiliana na wenyewe (CPT).

Makamu wa Rais Dk.Omar alifuatana na viongozi kadhaa wa Serikali wakiwemo Mkuu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Ritha Mlaki na viongozi wengine wa Serikali.

Risala ya CPT iliyosomwa na Mwenyekiti wake Bw.Camilus Kasala, pamoja na mambo mengine ilikuwa ya kuushukuru uongozi wa Serikali ya kijiji kwa kuwapatia ekari 50 za shamba, pia kuishukuru serikali ya Wilaya ya Kinondoni kuwaamuru wavamizi waondoke katika eneo la shamba hilo.

Lakini bila kujua hatua ambayo uongozi wa Wilaya na hata Tume ya Jiji walishafikia ya kuwataka waliovamia eneo hilo waondolewe, Mkuu wa Mkoa aliinuka na kutaka CPT iache kuwaita wananchi wavamizi, kwa vile wana haki ya kulima shamba hilo. " Mnataka wakale wapi?" alihoji Luteni Makamba huku akishangiliwa na baadhi ya wananchi waliohudhuria ziara hiyo.

Lakini baada ya Makamu wa Rais kumkosoa, Makamba alionekama mnyonge na kuinamisha kichwa kwa muda mrefu na kukaza macho anapoinuka.

Wakati Makamba "akichemka" na kauli zake hizo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Ritha Mlaki alionekana kumnong’oneza kitu Dk. Omar, hali iliyoashiria kwamba alikuwa akimweka sawa kuhusu hali halisi ya suala hilo.

Kwa muda mrefu kumekuwepo na mvutano wa ardhi kati ya wananchi wavamizi na wamiliki wa shamba hilo CPT lenye ekari 50 ambazo serikali iliwagawiakwa ajili ya kujenga kituo cha mafunzo ya kilimo na ufugaji bora.

Shamba hilo ambalo CPT walilipata katika miaka ya 1980 liligawiwa kwa wananchi tangu Septemba 1998 na kusababisha mgogoro mkubwa ambao ungali haujamalizika.

Hata hivyo uongozi wa kijiji cha Bunju A, umesema kuwa wananchi wanaolima katika shamba hilo, walipewa kwa muda tu kwa maana kwamba wenyewe (CPT) watakapolihitaji inabidi wawapishe.

Naye msemaji wa CPT Bi. Mariam Kessy, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa wao wamewapa wananchi muda wa kuvuna mazao yao ndipo waanze ujenzi wa kituo katika shamba hilo, japo wawili kati ya wananchi hao ambao jumla yao ni wanane wanakataa kabisa kuondoka, licha ya kuahidiwa kupewa kifuta jasho.

KKKT yaandamwa tena na mgogoro

lMamia ya wanauamsho wakusanyika Dar kumpinga Askofu

Justin Kivugo na Arnold Victor

MAMIA ya Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) jumapili iliyopita walikusanyika katika Parishi ya Kariakoo ya kanisa hilo, kupinga hatua ya uongozi wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya kuwadhibiti wanaumsho wasio na elimu ya teolojia kuhubiri bila usimamizi.

Waumini hao walikusanyika chini ya chama chao kiitwacho New Life Crusade, ambacho kwa mujibu wa viongozi wake kinawahusisha pia walokole wa madhehebu mengine.

Mkusanyiko huo umekuja baada ya Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jerry Mngwamba, kutoa waraka miezi miwili iliyopita ambao uliosomwa mfululizo kwa majuma manne ndani ya makanisa ya dayosisi hiyo ukiagiza kwamba muumini yeyote ambaye hajapitia katika vyuo vya Biblia vya kanisa hilo asipewe jukwaa au mimbara ya kuhubiri katika maeneo ya dayosisi.

Waraka huo wa Askofu ulitokana na kikao cha wachungaji wa kanisa hilo waliokaa na kuona kwamba kuna hatari ya misingi ya imani ya kanisa hilo kuathiriwa na wanauamsho, maarufu kama wana-fellowship ambao huendesha shughuli zao katika mtindo wa Kipentekoste.

Uongozi wa KKKT pia umekuwa ukiifananisha New Life Crusade kama kanisa jipya lililozuka kinyemela ndani ya kanisa hilo.

Hata hivyo baada ya waraka huo, vikundi vya wanauasho (fellowship) na viongozi wao katika makanisa yote ya dayosisi walipinga hatua hiyo wakishikilia msimamo wao kuwa Neno la Mungu linaweza kuhubiriwa na mtu yeyote bila kupitia chuo cha teolojia kwa vile hutegemea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Katika uchunguzi wake gazeti hili lilithibitisha kufanyika kwa vikao kadhaa kati ya Askofu Mngwamba, na viongozi wa New Life Crusade, ambayo ilizaliwa katika miaka ya awali ya tisini kutokana na fellowship za Walutheri wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Hata hivyo imeelezwa kuwa vikao hivyo licha ya kwamba havikuwa na maelewano lakini pia havikuweza kuzaa muafaka.

Mvutano huo unatajwa kuwa unaotishia amani katika kanisa hilo, kwa vile karibu theluthi moja ya waumini katika makanisa ya Kilutheri ni wanauamsho na kubwa zaidi wapo wachungaji kadhaa ambao nao pia ni wanaumasho.

Tishio jingine linalotajwa kuufanya mvutano huo uwe mgumu kusuluhishwa ni imani ya wanaumsho (walokole) hao ya kuamini kuwa Mchungaji asiyewaunga mkono haongozwi na Roho wa Mungu bali roho ya shetani, wakati wachungaji wasiowaunga mkono nao wanawaona walokole hao kama watu wanaojikweza, wenye kiburi na wasio na elimu juu ya Mungu.

Katika kuzidi kupigilia msumari uamuzi wa kuwadhibiti " wahubiri wasiosomea" ndani ya KKKT, kuanzia Aprili 9, 2000, Uongozi wa Dayosisi umesitisha ushirikiano uliokuwepo kati yake na New Life Crusade wa kuwalea "wanaookoka."

Mkutano wa Jumapili iliyopita wa NLC ulitoa tamko lake katika kuweka wazi msimamo wake juu ya mahusiano yake na Kanisa la KKKT, tamko ambalo pamoja na kusomwa mbele ya mamia ya waumini waliofurika katika kanisa la Kariakoo limepelekwa kwa Askofu Mngwamba.

"New Life Crusade imeanzisha fellowship nyingi na ina wanachama wengi katika sharika zilizo chini ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani, LAKINI NEW LIFE CRUSADE HAIMILIKIWA NA DAYOSISI YA MASHARIKI NA PWANI," kinasema kifungu kimoja cha tamko la "Walokole" hao.

Licha ya maneno hayo NLC inakiri katika kifungu cha kwanza cha tamko lake kuwa: "Hadi sasa New Life Crusade Dar es Salaam inafanya kazi zake zote kwa misingi ya katiba yake huku ikitumia majengo ya makanisa yaliyo chini ya KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani."

NLC imetamba kwamba hata kama itazuiwa kutumia majengo ya KKKT, itakutana na wananchama wake mahali ambapo itawatangazia, lakini inadai wanachama hao watatakiwa kuendelea kuwa wanachama wa makanisa yao.

Ikijibu hatua ya Uongozi wa KKKT, kuwa itaanzisha fellowship zake zitakazoendeshwa kwa taratibu za Kilutheri, NLC imesema, "Tunaomba ieleweke kuwa hiyo ni haki ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya kimsingi na New Life Crusade inawatakia kila la heri. New Life Crusade itafurahi kushirikiana na fellowship zitakazoanzishwa katika sharika za Kanisa la Kilutheri, lakini (NLC) haitakuwa sehemu ya fellowship hizo"

Akifafanua juu ya tamko hilo katika mahojiano maalum na gazeti hili wiki hii , Katibu Mkuu wa New Life Crusade, Bw. Alyson Mmanyi, alisema kuwa chama chao si cha kidhehebu kwa vile kinawashirikisha hata aliowaita "wenye maisha mapya" au "waliookoka" wa madhehebu mengine.

"Siwezi kulazimishwa kuruka na mbuni wakati mimi ni shomoro. Ndege wa aina moja huruka pamoja," alisema Mmanyi akimaanisha kwamba waliookoka hawawezi kuwekewa masharti na "wasiookoka."

Naye Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT, Adam Kombo, alipoulizwa juu ya suala hili, nje ya ofisi yake wakati akipanda gari kuelekea Arusha, Jumatatu iliyopita, alisema hawezi kuliongelea suala hilo juu juu kwa vile ni nyeti, hivyo asubiriwe hadi atakaporejea mwishoni mwa wiki.

Askofu Mngwamba aliondoka kwenda Marekani mwezi uliopita na anatarajiwa kurejea Julai, mwaka huu.

Hata hivyo, Askofu Kombo alikiri kuwepo kwa mgawanyiko mkubwa katika kanisa hilo na kwamba pia wapo baadhi ya wachungaji walioungana na wanafellowship.

Wakati hayo yanatokea ndio kwanza mgogoro wa baadhi ya waumini wa Dayosisi ya Pare ya KKKT waliotaka dayosisi hiyo igawanywe umepoa, baada ya kudumu kwa miaka kadhaa ukitishia amani.

Lipumba kutembezwa Dar kama mwali wa Kizaramo

lCUF wadai hawataiarifu polisi, na wakiwaingilia watakiona

Na Peter Dominic

MWENYEKITI wa taifa wa chama cha Upinzani (CUF),Prof. Ibrahimu Lipumba Jumapili hii anatarajiwa kuchukua fomu za kugombea Urais tawini kwake, Mnazi-mageuzi Temeke, mapema saa 3 za asubuhi. Atatembea kwa miguu kutoka Buguruni hadi Temeke akisindikizwa na washabiki wake.

Mwanasiasa huyo Profesa wa uchumi ni wa kwanza kuchukua fomu katika chama hicho kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Habari zimesema, amekuwa akishawishiwa na wanachama wengi kugombea kwa mara nyingine baada ya kugombea na kushindwa mwaka 1995.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi yalipoa makao makuu ya Chama hicho mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Vijana wa Taifa Bw.Shahibu Akilombe, alisema Prof. Lipumba atasindikizwa na vijana kuanzia makao makuu ya chama hicho Buguruni kuelekea tawini kwake Temeke kwa miguu.

Bw. Shahibu alisema kilichopelekea kiongozi huyo kushindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita ni kuibuka katikati kama mwanachama na kuomba nafasi ya kugombea urais akiwa hafahamiki kwa wanachama walio na wananchi wengi, tofauti na sasa ambapo amejipatia umaarufu mkubwa akiwa Mwenyekiti wa taifa wa chama.

Alisema kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha baada ya uchaguzi, watu wengi wamekuwa wakimshauri agombee tena nafasi hiyo.

"Hata sisi vijana tunashukuru amekubaliana na mawazo yetu. Tunamwona ni kiongozi pekee atakayeweza kuiongoza nchi hii kulingana na taaluma yake ya uchumi," alisema.

Sahaibu, alisema chama hicho kimeandaa huduma ya kwanza katika matembezi hayo ya kusindikiza mgombea wao kuchukua fomu.

Mkurugenzi huyo wa vijana alidai kuwa lengo la kutembea kwa miguu kutoka Makao Makuu Buguruni hadi Temeke ni kutaka kumuonesha Prof. Lipumba hali halisi ya mazingira ya nchi hii ili ajue matatizo yanayowakabili wananchi zikiwemo barabara mbovu na ukosefu wa ajira.

Alipoulizwa endapo wameshaiarifu polisi kwa ajili ya masuala ya usalama, alisema hawana haja ya kufanya hivyo, kwa madai kuwa wanachofanya sio maandamano.

Alisema endapo polisi watathubutu kuwazuia wasimsindikize mwenyekiti wao watapambana nao.

"Sisi ni ngangari ngangari bwana," alitamba akimaanisha kuwa wao ni watu wa mikikimikiki na sugu.

Naye Dalphina Rubyema anaripoti; Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Bw.Samweli Malicela amemtuhumu Profesa Ibrahimu Lipumba kwa madai kuwa amekuwa akishinikiza wanachama wake kueneza sera za udini na chuki miongoni mwa raia hali inayokuvuruga amani.

Malecela alitoa kauli hiyo wakati akiwapongeza wenyeviti wa serikali za mitaa waliochaguliwa hivi karibuni katika tawi la CCM tawi la Tabata Liwiti.

Katika mkutano uliofanyika juzi eneo la Tabata- Posta jijini.

Aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na chama hicho kwa madai kuwa kinaweza kuleta umwagaji damu kwa sababu ya udini.

Malicela alisema kuwa Profesa Lipumba anatumiwa na Seif Shariff Hamad kwa manufaa yake binafsi na baadaye atakuja kumtelekeza.

"Lipumba ni fundi wa matusi na kupotosha na mbaya zaidi hajui yeye mwenyewe atakuwa wapi ,Sharif Hamad anamtumia kwa faida yake binafsi na baadaye atamtelekeza" alisema.

Alimshauri Profesa Lipumba kujiuliza walipo wenyeviti wa chama hicho waliotangulia ambao ni James Mapalala na Musobi Magenyi.

Askofu atembeza msalaba kilomita 60 msituni kwa miguu

lHuko, aadhimisha ibada huku akinyeshewa mvua

lMsalaba wasafirishwa kwa mtumbwi

Na Mwandishi Wetu, Bukoba

KATIKA kushirikiana na "kondoo" kama Mchungaji mwema bila kujali ugumu wa mazingira, Askofu ameushangaza umma baada ya kutembeza Msalaba kwa miguu mwendo wa kilomita 60 msituni huku akipita tope, kuteleza na kunyeshewa mvua akiongoza ibada.

Kwa mujibu wa Katibu wa Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Nestor Timanywa, Padre Adeodatus Rwehumbiza alisema tukio hilo la kihistoria lilitokea hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya Msalaba wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, baina ya parokia za Bunyago (Kibashana) na Kassambya yaliyofanyika Aprili 16 mwaka huu.

Msalaba ulikuwa unavuka mipaka ya dekania ya Kiziba kuingia Ikimba ambapo makabidhiano hayo yalifanyika ukingoni mwa mto Minziro (upande wa Kassambya0 na msitu wa Kikulu (upande wa Buyango)

Habari zinasema, msalaba huo sambamba na Askofu Timanywa ulilazimika kupita njia hiyo ya Buyango, kukwepa kurudia njia uliokwisha pita kuelekea dekania ya Ikimba kutoka Buyango.

Zinasema, Askofu alipenda kuungana na waamini katika hija hiyo ngumu kuliko zote za msafara wa Msalaba jimboni na hivyo kudhihirisha kimatendo kuwa kama mchungaji mwema anapaswa kuwa pamoja na "kondoo" wake wakati wote bila kujali ugumu wa mazingira.

Padre Rwehumbiza, alisema safari ilianza kwa gari siku moja kabla ya Jumapili ya Matawi hadi parokia ya Kassambya ambapo asubuhi iliyofuata, iliendelea hadi Minziro, sehemu iitwayo Gera, iliyopo kwenye kilima kinachoteremkia bonde la msitu wa Minziro, kilomita 27 kutoka parokia ya Kassambya ambapo safari ilianza kwa miguu.

Mwendo wa miguu toka Gera kushuka kuelekea msituni hadi ukingo wa mto Kagera na kurudi unakadiriwa kuwa kilomita 60. Msafara huo wa mahujaji wapatao 40, ulipita katika mashamba mengi ya migomba, mibuni na mahindi.

Katika msafara huo ulioongozwa na Mhashamu Timanywa, Padre Rwehumbiza amesema hali ilikuwa ngumu mno kutokana na sehemu hiyo kujaa tope na madimbwi makubwa na madogo ya maji machafu huku mahujaji akiwamo Mhashamu Timanywa wakipata hekeheka za kuteleza na kuanguka hali iliyowapelekea kutumia magongo na mikongojo kujiegemeza wasianguke zaidi topeni.

Hakuna aliyejeruhiwa katika safari hiyo ambayo pia walikuwa na kazi ngumu ya kuruka miti ya zamani iliyoanguka na kuziba njia.

Mamia ya waamini wa parokia ya Buyango wakiongozwa na Padre Edward Furahisha, waliokuwa wamepiga kambi ng’ambo ya mto Kagera, waliuvusha Msalaba sehemu tatu za misitu na eneo la Tingatinga lenye maji mengi kabla ya kufika Kabaya, ukingoni mwa Mto Kagera ulipolala.

Msalaba huo wa Jubilei Kuu ulisafirishwa kwa mtumbwi huku umeshikiliwa na Padre Furahisha, kutoka kambi ya Buyango kwenda Kassambya.

Viongozi na wengine wakiwamo Katibu huyo wa Askofu, mpiga picha za video, masista wawili na waamini wawili toka parokia ya Bukoba, walitumia mitumbwi yenye uwezo wa abiria wawili.

Ingawa wakati wote wa kukabidhiana msalaba na kubariki matawi Jumapili hiyo mvua ilikuwa ikinyesha hadi ilipokatika ghafla baada ya kubariki matawi na maandamano kuanza kuelekea Bulembe ambapo Misa Takatifu ya Jumapili ya Matawi ilifanyikia, waamini walitulia.

Mwendo huo wa kilomita 2.5, ulikuwa wa kukwea kilima kuelekea mahali lilipokuwa kanisa la Jumuiya ya Waamini wa Bulembe kabla ya kuezuliwa mara kadhaa na hatimaye kusambaratishwa na nyani.

Pamoja na mambo mengine, katika homelia zake, Askofu Timanywa, aliwapongeza mapadre na waamini wa dekania hizo katika kufanikisha makabidhiano hayo. Aliwahimiza kudumu katika imani ya Kristo.

"Uchovu, shida na matatizo mbalimbali tunayoyapata kutokana na shughuli za msalaba ni njia ya kushiriki kwetu katika mateso ya Kristo. Hayo ndiyo yanatustahilisha neema ambazo Kristo ametuwekea tayari kwa njia ya mateso, kifo na ufufko wake." alisema,

Msalaba wa Jubilei kuwa jaji wa siku ya Pasaka majimboni

Na Dalphina Rubyema

IMEPENDEKEZWA kuwa mwisho wa mzunguko wa Msalaba wa Jubilei Kuu katika majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini usiwe ni Januari mwaka kesho na badala yake msalaba huo uendelee kutumika katika matukio mbalimbali ya jimbo na Parokia zake na kuamua pa kufanyikia maadhimisho ya pasaka kijimbo.

Mapendekezo hayo yalitolewa na washiriki wa semina ya kitaifa ya Liturujia kutoka majimboni iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Wajumbe hao ambao ni waratibu wa Liturujia majimboni na Kamati ya Muziki na tafsiri, walipendekeza kuwa msalaba huo utakapofikia kilele chake usiwekwe tu na badala yake uendelee kuzungushwa katika Parokia mbalimbali.

Walipendekeza kuwa parokia itakayo angukiwa na msalaba huo siku ya Pasaka ukiwa katika mzunguko wake wa kawaida, iwe ndipo maadhimisho ya Pasaka kijimbo yatafanyika.

Pia, wajumbe walipendekeza kuwa panapotokea maafa kama wizi wa kikanisa na maafa mengine kama ukame, mafuriko na moto msalaba huo upelekwe pale. Pia walipendekeza uwe unatumika katka maadhimisho ya Jubilei majimboni.

Katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Severine Niwemugizi alifafanua juu ya kitabu kipya cha Daraja la Ndoa kinachoitwa IBADA YA SAKRAMENTI YA NDOA.

Alisema inabidi jamii ibadilike na siyo kukazia sherehe za kisasa hali inayogeuza Sakramenti ya Ndoa kuwa inayoshindaniwa kwa ufahari kwa watu na kusahau kujitoa muda wa tafakari juu ya tunu na wajibu wa maisha mapya.

Mhashamu Niwemugizi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge alipendekeza kuwa mafundisho ya ndoa yawe ya muda mrefu usipungua miezi mitatu.

"Utaratibu wa kufafanua maana ya hadhi ya ndoa lazima ufanyike kama tunavyo waandaa kwa Komunio ya Kwanza au Kipaimara, ingefaa kila parokia iwe na timu ya kuwandaa wanandoa" alisema.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Julian Kangalawe, kitabu hicho kitaanza kutumika Agosti 15, mwaka huu, kwa mujibu wa mapendekezo ya Maaskofu.

Alisema kitabu hicho ambacho kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka Kiitaliano kitawapa nafasi mapadre kubariki hata wachumba pale watu wawili wanapoanza kuchumbiana.

Padre Kangalawe ambaye pia yumo kwenye Kamati ya Tafsiri, alisema mwisho wa kutumia vitabu vya ndoa vya awali, ni Agosti 14, mwaka huu na kwamba baada ya hapo havitakuwa na nafasi na endapo padre yoyote atavitumia kufungia ndoa, basi hiyo itakuwa batili.

Semina hiyo ya siku tatu iliandaliwa na Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)

Waziri Majogo aishauri Bodi ya SUMA JKT

Na George Jovin,

BODI ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), imeshauriwa kuangalia upya na kuuboresha mfumo wa shirika lake katika uendeshaji wa biashara badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Edgar Maokola Majogo, wakati akizindua bodi hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo Mwenge jijini.

Alisema mfumo wa shirika hilo hauna budi kuangaliwa upya na akasisitiza kuwa shughuli za uzalishaji mali zinazoendeshwa na shirika hilo, zitenganishwe na zile za kijeshi ili kuleta ufanisi.

Akimkaribisha Waziri Majogo, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Jenerali Makame Rashid, alisema shirika hilo lililoanzishwa miaka 19 iliyopita, lilianzishwa bila mtaji kutoka serikalini hali iliyosababisha miradi iliyokuwa ikiendeshwa kiserikali ibadilishwe na kuwa chini ya shirika hilo na hii ilikuwa ni kutaka kuliimarisha kifedha.

Alisema kuwa kuundwa kwa bodi hiyo kutaleta changamoto kubwa katika miradi mbalimbali inayoendeshwa na shirika kwa vile sasa ina wajumbe mchanganyiko, wakiwemo raia na askari ambao wanaweza kukosoana tofauti na kipindi cha nyuma ambapo lilikuwa chini ya uongozi wa jeshi pekee.

Bodi hiyo iliyoteuliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, miezi kadhaa iliyopita, ina wajumbe wanane ambao ni Balozi Issaya Chiaro ambaye ni Mwenyekiti, Balozi Paulo Rupia, Meja Jenerali Makame, Brigedia Jenerali Aristrachus Karubi, Jenerali Sylivester Ryoba, Monica Mbega, Alfred Lucas na Kapten John Mbungo ( Katibu).

Kondomu ni kama ndege iliyobeba bomu - Mtaalamu

Na Fr. Raphael Kilumanga

MTAALAMU wa maswala ya familia kutoka Shirika la Kimataifa kwa ajili ya amani ya ulimwengu, Bw. Kevin Winten amezifananisha kondomu na ndege iliyobeba bomu na akaonya dhidi ya matumizi yake kwani ni moto wa kuotea mbali.

Akizungumza katika mkutano wa siku moja uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Kimataifa ya Sheraton jijini Dar Es Salaam, ambapo alishirikiana na Dk.Tom Walsh wa Shirika hilo raia wa Marekani, alisema anashangazwa kuona nchi zinazoendelea zikishabikia matumizi ya kondomu kama kinga dhidi ya virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Ukimwi na kusema kuwa nchi hizo zinalichukulia swala la ukimwi kimzahamzaha.

"Si kweli kuwa kondomu ni kinga" alikanusha na kuongeza, "Marekani ilipoukumbatia utamaduni wa matumizi ya kondomu maadili yalishuka chini ghafla na tabia ya uzinzi ilipanda na kuwa mbaya na watu wengi waliambukizwa virusi vya Ukimwi".

Alisema kuwa kumshauri mtu atumie kondom ni sawa na kushawishi mtu achague kupanda ndege ya kwenda Marekani kwa tikiti ya bure huku akijua kati ya ndege kumi zilizopo uwanjani, baadhi yao zina mabomu ndani.

"Nani angekubali kuchukua ndege anayojua akipanda haitamfikisha salama huko aendako" alihoji Bw. Kevin na kuongeza kuwa kondomu ni kama bomu lililotengwa katika ndege na mtu akiitumia hana uhakika na usalama wa maisha yake.

Shirika hilo linasisitiza kuwa njia pekee ya kuepuka ugonjwa wa Ukimwi ni kuacha vitendo vya kujamiiana kabla na nje ya ndoa na akawataka wanandoa kuwa waaminifu katika ndoa zao.

Shirika hilo lisilo la kiserikali linalozingatia kanuni kuu tatu ambazo ni pamoja na malezi ya moyo, ya maadili na miliki, likiungana na Shirika la Umoja wa Dini kwa ajili ya Amani ya Ulimwengu, lilianzishwa na Mchungaji Sun Myung Moon, Desemba 19,1998 na kuzinduliwa Februari 6,1999 huko Sesul Korea.

"Malezi ya roho au moyo yanahusu uundaji wa mwelekeo wa jamii kwa wengine na malezi ya maadili yanahusu elimu ya mtu ya kumwezesha kuwa na mahusiano maadilifu na watu wengine" zinaeleza kanuni hizo na kuongeza kuwa ngazi hizo mbili ni za msingi na lazima zifunzwe katika familia ambayo ni shule ya Upendo na maadili.

Aidha, malezi ya milki ambayo ni ya nje ya mtu yanahusu elimu kiakili kiufundi na kimwili na kufanyika katika shule za kawaida ikilenga mchango wa jumla kwa jamii taifa.

Shirika hilo linasisitiza kuwa ingawaje ngazi zote tatu ni za muhimu lakini malezi ya ndani ya mtu yanayofanyika katika familia ni ya muhimu na linatoa wito kwa familia kuwa makini na ngazi hizo mbili za awali ili kulinusuru taifa na ubinafsi.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Ali Ameri Mohamed, Wabunge, Mabalozi, Mawaziri, viongozi mbalimbali wa dini na Serikali, maprofesa na wageni kutoka nchi za nje zikiwamo Kenya na Uganda pamoja na wawakilishi toka sekretarieti za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Jimbo Katoliki la Iringa lavuna tunda

Na Dalphina Rubyema

JIMBO Katoliki la Iringa limepata tunu ya Milenia baada ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kumteuwa Padre Damian Dallu kutoka Jimboni humo kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita.

Uteuzi huo wa Baba Mtakatifu ulitangazwa na Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania Jumamosi iliyopita.

Hadi anateuliwa kushika wadhifa huo,Askofu Mteule Dallu alikuwa ni Padre Mlezi na Mwalimu wa Seminari Kuu ya Segerea iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-salaam.

Askofu Mteule Dallu mwenye umri wa miaka 44 alizaliwa katika eneo la Kiponzelo jimboni humo kwenye familia ya Bw.Denis Dallu na Bibi Theodora Kasimba na alipata daraja la upadre Novemba 15 mwaka 1984 katika parokia ya Ifunda.

Kabla ya kupata daraja la upadre ,Askofu Mteule huyo ambaye alibatizwa mwaka 1956 katika Parokia ya Wasa ,Iringa,kwanza alipitia kwenye Seminari ndogo ya mafinga jimboni humo miaka ya 1974-1978.

Mwaka 1979 hadi 1980,Askofu Mteule Dallu alichukuwa masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Peramiho iliyopo katika jimbo Katoliki la Songea na baadaye aliendelea kusoma katika chuo hicho akichukuwa masomo ya Teolojia ambayo alihitimu mwaka 1984.

Mwaka 1987 hadi 1989 Mteule Dallu alijiunga katika Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika Mashariki kilichopo Nairobi,Kenya ambapo alipata shahada ya masomo ya Teolojia na maadili.

Kabla hajawa Kasisi (Chaplain) wa vijana wa Jimbo la Iringa mwaka 1986-1987,Askofu Mteule Dallu alikuwa Msaidizi katika parokia ya Malangali Jimboni humo na hapo ilikuwa ni mwaka 1985.

Kati ya mwaka 1991 hadi 1994,Askofu Mteule huyo alikuwa padre mlezi na mwalimu katika seminari Kuu ya Peramiho na tokea mwaka 1995 hadi sasa alipoteuliwa kuwa Askofu alikuwa akishika wadhifa kama huo Katika Seminari Kuu ya Segerea.

Uzalishaji wa korosho waporomoka Kisarawe

Na Agatha Rupepo, Kisarawe

UZALISHAJIi wa zao la korosho umeshuka toka tani 2,129 kwa kipindi cha 1991/92 hadi tani 128 mwaka 1998/99, baada ya wakulima wilayani hapa kuyatelekeza mashamba ya mikorosho bila huduma maporini; imefahamika.

Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Korosho (CIDEF), Bw. Ismail Mohammed, aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na baadhi ya wawakilishi wa vijiji mbalimbali vya wilaya hii, katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Kiluvya kilichopo wilayani hapa, juu ya uboreshaji wa zao la korosho.

Alisema kwa kuwa korosho ndilo zao linalotegemewa kwa kuinua pato la wilaya, ni wajibu wa kila mwananchi kuitunza mikorosho yake vizuri ili iweze kutoa mazao bora zaidi na kuinua kipato chao na serikali.

Allisema katika kipindi cha mwaka 1991/92 wilaya ya Kisarawe ilizalisha tani 2,129 za korosho na tokea wakati huo, kiwango cha uzalishaji kimeendelea kushuka na kufikia tani 327 mwaka 1997/98.

Uzalishaji ulizidi kushuka hadi tani 128 mwaka1998/99, na akasema hali imesababishwa na baadhi ya wakulima kuyaacha mashamba yao bila huduma muhimu kama palizi na dawa. .

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Kapteni James Yamungu, aliagiza watu wote wenye mashamba ya zao hilo na wale walioyatelekeza, wakiwamo wakulima, wafanyakazi na viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani kwake, kuanza kuyahudumia.

Aliagiza pia kila mwananchi kuwa na walau miche sabini ya zao hilo vinginevyo atawachukulia hatua watakaokaidi agizo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe, Bw. Mwinyimangara Goma, amesema tatizo kubwa linaloikabili wilaya yake katika kuinua kiwango cha uzalishaji wa zao hilo ni ukosefu wa bomba za kupulizia dawa.

Shinyanga wazindua tawi la Chuo Kikuu

Na Charles Hililla Sinyanga

CHUO Kikuu huria kimezindua tawi lake katika mkoa wa Shinganga ambapo Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Mohamed Babu alikuwa mgeni rasmi.

Matawi mengine ya chuo hicho yaliyokwisha zinduliwa ni pamoja na yale ya mikoa ya Kigoma na Kagera mapema mwezi huu. Mkoa wa Arusha unatarajiwa kuzindua tawi lake Juni 24 wakati Tanga, uzinduzi utafanyika Juni 27, mwaka huu.

Sherehe za uzinduzi huo uliofanyika Mei 9, mwaka huu, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu ya chuo akiwemo Makamu wa Mkuu wa Chuo, Profesa Geofrey Mmari. Bw. Dalotta ambaye ni Katibu wa Baraza hilo na Mkurugenzi wa huduma mikoani Bw. Mmuni na wabunge mkoani hapa, wafanyabishara na wanafunzi wa chuo hicho.

Akizungumza kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Huduma ya Chuo hicho mikoani, Bw. Mmuni aliusifu mkoa wa Shinyanga kwa kuwa wa 16 kati ya mikoa yote ya Tanzania kupata tawi la Chuo hicho.

Hata hivyo alisikitishwa na idadi ndogo ya wanawake wanaojiunga na chuo hicho katika mkoani hapa. Mkoa wa Shinyanga una wanafunzi 226 wanaosoma chuoni hapa, lakini wanawake ni 23 tu.

Mkurugenzi huyo aliutaka uongozi mkoani hapa kushirikiana na wananchi kwa kuwashauri na kuwaelekeza namna ya kutumia rasilimali zilizo kwani alidai ingawa zipo nyingi, bado wananchi hawafaidiki nazo hali inayopelekea mkoa kuwa wa nyuma katika sekta ya elimu.

Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo kuwa ni madini karibu yote yanapatikana kwenye mkoa huo, mifugo na mazao ya biashara kama Pamba na Tumbaku.

Akijibu taarifa ya Bw. Mmuni kuhusu matumizi ya rasilimali zilizopo katika mkoa wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, katika hotuba yake alikiri kuwepo kwa rasilimali nyingi ingawa matumizi yake hayawiani na yamekuwa na maendeleo maendeleo yaliyopo

Alisema moja ya sababu za hali hiyo ni maandalizi duni ya awali ikiwa ni pamoja na kukosa miundo mbinu na mazingira duni ya elimu ikiwa ni pamoja na darasani, vitabu vya kiada na ziada na upungufu wa nyumba za walimu na madarasa.

Tangu kuanzishwa kwake 1994, Chuo hicho kimeshafanya mahafali tatu na hivi sasa kina wanafunzi wapatao 6738 kutoka ndani na nje ya nchi.