Tutawapa wananchi uwezo wa kubaini hila za wanasiasa - Kanisa Katoliki

lKitabu kingine juu ya Haki za wafungwa kusambazwa magerezani

Dalphina Rubyema na Getrude Madembwe

TUME ya Haki na Amani iliyo chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki(TEC)Tanzania (TEC), imesema haina nia ya kupambana na chama chochote cha kisiasa bali kuwaongoza wananchi wawe na uwezo wa kuchuja hila za wanasiasa nyakati za kampeni za uchaguzi na kuweka vipaumbele vyao.

Sambamba na ufafanuzi huo Tume hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki nchini(CPT), wataandika kitabu kinachohusu haki za wafungwa ambacho kitasambazwa bure kwa walengwa ambao ni wafungwa wenyewe.

"Sisi hatuwafuati kwenye vyama, kazi yetu kama Kanisa, ni kuongoza wananchi kiroho na pia kuwasaidia wajue haki zao," alisema Padre Vic Missiaen, ambaye ni Katibu wa Tume hiyo ya Haki na Amani katika semina ya Tume hiyo iliyomalizika jijini mwishoni mwa wiki.

Akizungumzia kitabu kilichotolewa hivi karibuni na tume hiyo kiitwacho- "UCHAGUZI WA KISIASA KWA NINI TUJALI?" ambacho tokea toleo hili gazeti hili la Kiongzi linakichapa kama kilivyo, Padre Vic, alisema nia ya kitabu hicho sio kushambulia chama chochote wala serikali, bali kuwaelimisha wananchi wajue namna ya kuhoji kwa usahihi haki zao za kisiasa wakati wanapoombwa kura ili kuwaweka wanasiasa madarakani.

Akitoa mfano, alisema, endapo mwanasiasa atawaahidi wananchi kuwajengea shule, barabara au hospitali, hawana budi kumuuliza atatoa wapi pesa kwa ajili mradi huo.

"Mgombea anapaswa aulizwe atatoa wapi hizo pesa na aseme kama zitatokana na jasho la wananchi wenyewe au wapi na kwa namna gani," alisema Padre Vic.

Naye Mwenyekiti wa CPT Jimbo Kuu la Dar es Salaam Bw. Agapiti Meiseyeki, alisema,

Wao kama wanataaluma hawataogopa kusema yale wanayoona yanafaa kusemwa kwa manufaa ya jamii, na kwamba hawataingilia au kujihusisha na siasa za chama chochote. "Hatuzungumzii chama chochote, lakini yale yanayohusu jamii hatuogopi kuyaeleza," alisema.

Akifungua semina hiyo ya siku tatu iliyoanza Mei 2, mwaka huu katika kituo cha Kiroho cha Mbagala kilichopo jijini Dar-Es-Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Mhashamu Paul Ruzoka ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, alionya juu ya tabia ya baadhi ya viongozi kujilimbikizia mali na kuwasahau wanyonge na akatahadharisha kuwa hali hiyo inaweza kuvunja amani.

Mhashamu Ruzoka, alisema mali zilizopo duniani ni mali ya Mungu na kila mwanadamu ana haki sawa na mwingine katika kuzishiriki na kuzifurahia.

"Kanisa linalo dhamana ya kuhubiri kwa kutumia sauti ya wanyonge kwa kukemea ama kukosoa jamii," alisema.

WAKATI HUO HUO: Tume ya Haki na Amani ikishirikiana na CPT, iko katika mipango kabambe ya kuandika kitabu kitakachochambua na kueleza haki za wafungwa nchini.

Akizungumza katika semina hiyo, Padre Vic Missiaen alisema kuwa kitabu hicho kinatarajiwa kuanza kuandikwa hivi karibuni na kwamba kikikamilika, kitagawiwa bure kwa wafungwa ili waweze kufahamu haki zao.

Alisema kitabu hicho siyo tu, kitawasaidia wafungwa na mahabusu peke yao, bali pia kitawasaidia mahakimu hususani wale wa Mahakama za Mwanzo ambao watapata mwongozo zaidi katika utendaji wao wa kazi.

"Kwetu Wakristo ni kweli wafungwa ni wale watu waliofanya makosa lakini bado ni watoto wa Mungu na wameumbwa kwa mfano wa Mungu, hivyo hatuwezi kuwaacha watendewe isivyo halali eti kwa vile ni wafungwa," alisema.

Wajumbe wa semina hiyo ambao wananaandaliwa kuwa wahamasishaji bora katika kuekeleza yaliyopo katika kitabu hicho cha "UCHAGUZI WA KISIASA KWA NINI TUJALI?" na wengine wakiwa viongozi wa tume hiyo ngazi ya Taifa walieleza dukuduku lao kuwa siyo kweli kwamba wafungwa wote na mahabusu wanakuwa na hatia bali baadhi yao hubambikiziwa kesi hivyo kujikuta wakisota gerezani bila hatia.

Wakitoa mfano wakati wa kuchangia hoja katika semina hiyo, wajumbe hao walisema kuwa, gereza la Isangya lililopo Dodoma ambalo ndilo kubwa kuliko yote nchini na wakasema lina makundi matatu ya wafungwa ambayo ni mahabusu, wafungwa na la waliohukumiwa kunyongwa ambalo lina matatizo makubwa zaidi.

Aliyataja matatizo hayo kuwa ni kubanana, uchafu, magonjwa ya kuambukiza na kula chakula kibovu.

Mmoja wa wajumbe hao alisema gerezani hapo watu wanaumwa lakini hawapati wala dawa kwa ajili ya matibabu, "Pale bwana mtu utaumwa homa ya matumbo(typhoid) lakini hakuna cha kupata dawa. Hapo wanapolala na nguo wanazovaa kama hautakuwa mvumilivu huwezi kukaa muda hata mfupi tu."

Hata hivyo mjumbe huyo alisema pamoja na hali hiyo, Kanisa Katoliki Jimboni humo limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma gerezani hapo zikiwemo zile za kiroho na uongozi wa gereza umekuwa ukionesha ushirikiano mzuri.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kahama Askofu, Matthew Shija, aliueleza mkutano huo kuwa hali kama hiyo pia ipo katika gereza la Kahama lililojengwa enzi za mkoloni, lina uwezo wa kubeba watu 70 lakini sasa linabeba kati ya watu 300- 400.

Alisema gereza hilo linakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mfereji kwa ajili ya kusafirisha uchafu, hali inayosababisha kujisaidia katika mapipa na madebe yanayowekwa mahali wanapolala hadi asubuhi ambapo uchafu huo hufukiwa shimoni.

"Utengenezaji wa Sewage System ni muhimu kwa ajili ya kusaidia wafungwa katika gereza hilo," alisema.

Mjumbe mwingine wa semina hiyo kutoka Tanga, alisema mtu anapoingia katika gereza la Maweni lililopo jimboni humo huona kama umeingia katika ulimwengu mwingine kwani harufu mbaya inakuyozingira huko ni tofauti sana na ile ya uraiani.

Alisema katika gereza hilo na mengine, watu wa jinsia moja hukaa pekee yao kwa muda mrefu bila kukutana na wale wa jinsia nyingine, jambo ambalo huwafanya kujikuta wanafanya mchezo mbaya wenyewe kwa wenyewe na tatizo hili zaidi linawakumba wanaume kutokana na sababu na maumbile ya kibaiolojia.

Naye mshiriki kutoka Jimbo katoliki la Musoma, alisema kuwa gereza la huko lina wafungwa wapatao 800-900 hivyo inakuwa vigumu kupata mahali pa kulala hadi umwombe Mnyapara kwa kuhongwa sabuni na vitu vingine ili kupata chakula.

"Ukihonga sabuni mche mmoja una uhakika wa kupata sahani kumi za ugali ikiwa na na maana una uhakika wa kupata chakula cha kutosha kwa muda wa siku zaidi ya tano," alisema mjumbe huyo.

Kufuatia maelezo hayo yaliyotolewa na baadhi ya wajumbe waliofanya uchunguzi katika magereza kadhaa mbali na kuandika kitabu cha haki za mfungwa, Senmina hiyo iliona kuna haja yakuzidisha nguvu katika kutembelea magereza na kutoa huduma ya kiroho na kimwili zikiwemo ibada, sala, maombi na huduma mbalimbali kama madawa, nguo, sabuni na vyakula, kazi iliyoelezwa kuwa itafanyika katika ngazi ya jimbo.

"Suala zima la huduma za wafungwa ni lazima kufanyika, ndio maana hata Ijumaa Kuu tunasema milango ya gereza ifunguliwe," alisema Mwenyekiti wa Tume na Haki na Amani, Mhashamu Askofu Paul Ruzoka.

Hata hivyo alisisitiza kuwa yafaa wahudumu watakaoenda kutoa huduma katika magereza wapewe semina ya pamoja ya kufahamu mbinu za utendaji wao.

Uchagani waiba mbuzi sita wa sadaka Kanisani

lParoko achinja tisa waliosalia na kuwapa wakata majani

lWabeba pia unga na masufuria

Mary Kimaro na Agatha Rupepo, Moshi

WAKATI wa mkesha wa ukumbusho wa kufufuka kwa Yesu Kristo vibaka waliibuka na kuiba mbuzi wapatao sita, unga na vifaa vingine vilivyotolewa kama sadaka ya Pasaka kanisani katika Parokia ya Useri, Rombo, mkoani Kilimanjaro, hali iliyomfanya Padre achinje mbuzi tisa waliosalia na kuwatoa waliwe na wakata majani.

Hayo yamesemwa na Padre Makiponya wa Kanisa Katoliki Parokia ya Useri Wilaya ya Rombo wakati wa Ibada ya Pasaka.

Kwa mujibu wa Padre Makiponya, vitu vilivyoibiwa ni mbuzi sita, sufuria, mahindi na unga ambavyo vilitolewa sadaka na waumini wa kanisa hilo.

Padre alianza kuwasifia waumini hao akisema "kwa kweli waseri ni watu wazuri sana katika Parokia zote ambazo nimewahi kukaa sijapata kuwa na watu wazuri kama ninyi, sasa yaani mmeamua kuniibia vitu ambavyo mmenileta ninyi wenyewe?"

Kwa masikitiko alisema watu wa Mungu wameamua kuvunja amri ya saba tena wameivunja katika nyumba ya Mungu kitendo ambacho ni aibu kubwa.

Alisema ‘Kwakuwa mmeamua kuiba mbuzi hao basi na mimi nimeamua kuchinja mbuzi wote tisa waliobaki na kuwapa nyama vijana wangu ambao walikuwa wakinisaidia kuwakatia majani.

"Watu walioiba mbuzi mnawafahamu,ama wapo hapa Kanisani au majumbani kwenu,

alisema Padre huyo na kuongeza, "wewe uliyeuziwa mbuzi umrudishie huyo aliyekuuzia na kama wewe uliyeiba umeamua kumchinja mbuzi huyo ukala wewe na watoto wako basi mbuzi huyo atalia tumboni mwako."

Kwa masikitiko padre huyo alisema "Kabila langu nimekutendea nini au nimekusikitisha nini naomba uminijibu."

Tukio la namna hiyo ni la pili kutokea katika Parokia hiyo na hakuna mtu yeyote aliyekwishakamatwa.

Walioleta machafuko KKKT Pare watishia kuyafufua

Na Mwandishi wa PST,Moshi

SERIKALI imeombwa kutambua kuwa hali ya usalama ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania katika Wilaya ya Mwanga siyo shwari bado kutokana na Kanisa hilo Dayosisi ya Pare kushindwa kutekeleza muafaka ambao ndio ungeliwezesha waamini wa Kilutheri Mwanga wanaodai kuwa na Dayosisi yao kubadili nia yao.

Hayo yameelezwa na waliokuwa waasi wa dayosisi ya Pare ambao walitengwa na KKKT kutokana na hatua yao ya kutangaza Dayosisi ya Mwanga. Walikuwa wakiongea na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Profesa Philimon Sarungi ofisini kwake wiki iliyopita.

Waasi hao 12 ni pamoja na kiongozi wao Bw. Onesmo Sabuni, Elienea Mrutu, Alfred Melita, Geofrey Kinenekejo, Melkizedeki Noah na Washington Msuya.

Alisema kuwa Dayosisi ya Pare bado haijakamilisha muafaka wa kumaliza mgogoro huo amabao ni kutekeleza makubaliano yatokanayo na taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo iliyotolewa na Kamati ya Tume ya Askofu Elinaza Sendoro ambayo ilitaka viongozi wote waliokiuka maadili katika Dayosisi ya Pare waondolewe.

Hadi sasa, walimwambia Mkuu wa mkoa kuwa hawashiriki wa chakula cha Bwana chini ya wachungaji wa Dayosisi ya Pare.

Wakizungumzia juu ya masuala ya kurejeshwa kwa amani walisema kuwa kitendo cha viongozi wa Dayosisi ya Pare kutangaza kuwa wameanza kurejea katika Dayosisi hiyo kwa aibu kinachochea fujo, kwani si kauli ya upatanishi.

Bw. Mrutu, alisema kuwa Dayosisi ya Mwanga bado ipo palepale na waamini wake na kuwa wanachotafuta ni itambuliko wa kwa mujibu wa sheria za nchini na kanisa na kupata wachugaji wacha-Mungu na wapenda maendeleo wasiojali ukabila.

"Tunahakikisha kuwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi yetu bila ya kufanya fujo tutapata dayosisi yetu," alisema mjumbe huyo kuonyesha kwamba kiu yao ya kutaka dayosisi haijafa.

Katibu Mkuu wa KKKT nchi Bw. Amani Mwenegoha, alinukuliwa hivi karibuni na vyombo vya habari akisema kuwa mgogoro wa dayosisi ya Pare umemalizika baada ya waamini waliokuwa wakitaka kuwepo Dayosisi ya Mwanga kutubu na kujiunga na wenzao wa dayosisisi ya Pare.

Katika mwafaka wa Tume ya Sendoro, ambao PST ilipatiwa nakala yake, Askofu Sendoro alipendekeza waliovunja maadili ya KKKT wafukuzwe kazi.

Hivi karibuni pia uongozi wa KKKT ulikaririwa ukisema kuwa waliotaka dayosisi ya Mwanga sasa wanarejea ndani ya dayosisi ya Pare kwa aibu.

Afande mwanamke afa kwa kunywa pombe yenye sumu

lKabla ya kufa asema alikunywa kwenye baa nne

Na Patrick Chambo PST, Moshi

AFISA mmoja wa polisi mwenyecheo cha "stafu sajini" mkoani hapa Elizabeth Joel (50) amefariki nyumbani kwake ghafla baada ya kurejea kutoka kazini kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kunywa pombe iliyochanganywa na sumu.

Kwa mujibu wa kaka wa marehemu Bw. Saimoni Mtangi ambaye ni mtoto wa baba mkubwa wa marehemu taarifa ya daktari imeeleza kuwa marehemu alikunywa pombe iliyochanganyika na sumu.

"Dada yetu amefariki kutokana na kunywa pombe iliyochanganywa kwa sumu," alisema Bw.Mtangi, bila ya kuelezea aina ya sumu hiyo alipokuwa akizungumza na ndugu na jamaa waliofika nyumbani kwa marehemu kuombeleza msiba.

Inasemekana kuwa kabla ya kuzidiwa marehemu alimuita daktari wake na baada ya kuzidiwa na ugonjwa wa kukatwa na tumbo aliwafahamisha ndugu na majirani kuwa alikuwa amekunywa pombe na baadhi ya rafiki zake wakiwemo wafanyabiashara baada ya kutoka kazini.

Hata hivyo marehemu alisema kuwa hawezi kufahamu kuwa ni wapi alipokunywa sumu hiyo kwa kuwa alikuwa amekuwa katika baa nne tofauti kwa vipindi tofauti kabla ya kurejea nyumbani.

Akizungumzia mazishi ya marehemu Bw.Mtangi, alisema kuwa dada yao aliacha wosia kuwa asije akazikwa nyumbani kwao Bumbuli, Tanga, bali akifa azikwe katika nyumba yake iliyopo mjini Lushoto, mjini Tanga.

Hata hivyo alisema kuwa haitakuwa rahisi kuendelea kutoa heshima za mwisho kwa ndugu na jamaa wote wa marehemu kutokana na hali ya marehemu kuwa mbaya kutokana na kutokwa na damu puani na kuvimba tumbo.

Marehemu alifariki Mei 1, 2000 na kuzikwa wilayani Lushoto kwa heshima zote za kijeshi. Marehemu ameacha watoto na jamaa waliokuwa wakimtegemea.

Kaimu Kamanda wa Polisi Bw. Haruni Bachubila, hakupatikana kuzungumzia kifo hicho kutokana na kuwa katika maandalizi ya msiba, lakini polisi mjini hapa wamesema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa mazingira ya kifo hicho.

Serikali isiwaonee aibu wawekezaji - Ushauri

Na Mwandishi Wetu

ILI kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeshauriwa kutokuwaonea aibu wawekezaji wa nje wanaong’ang’ania kuajiri wageni na badala yake iwabane watoe kipaumbele kwa kuwajiri wazalendo.

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma Wakatoliki Tanzania (CPT) ,tawi la parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Bw. Ludovick J. Mwananzila alipokuwa akizungumza katika semina ya siku moja ya CPT iliyofanyika parokiani hapo hivi karibuni.

Katika semina hiyo ambayo mada kubwa ilikuwa Kazi ni Uhai, Bw. Mwananzila alisema, "Serikali isione aibu kuwabana watu au mashirika ya nje yanayokuja kuwekeza hapa nchini ili watoe ajira kwa wazalendo kuliko hao hao kuleta watu wao tu," alisema na kuongeza,

"Labda walete watu wao pale ambapo hakuna mzalendo mwenye ujuzi na kazi hiyo. Na hii itaokoa hata gharama nyingine na malipo ya ziada yasiyo ya lazima."

Alisema serikali haina budi kuona kuwa inafuta kivitendo na kwa manufaa ya jamii nzima dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwa kuwa na mfumo wa elimu uliowaelekeza wasomi kutegemea ajira toka serikalini na mashirika ya umma pekee kuwa waajiri wakuu.

Alisisitiza kuwa kufuatia mabadiliko ya mfumo wa uchumi yaliyojitokeza nchini katika miaka ya hivi karibuni, yameifikisha nchi mahali ambapo mfumo wa elimu itolewayo, hauna budi kubadilika na kuendana na hali halisi ya uchumi na mfumo uliopo wa soko huria.

"Mashirika ya umma yamekufa, mengine yameuzwa na hata mengine yameingia ubia jambo ambalo limesababisha watu wengi kukosa na wengine kupoteza kazi zao; na hii imesababisha mfarakano mkubwa na ukosefu wa amani katika familia nyingi na hata ndoa nyingi zimevunjika," alisema na kuongeza,

"Familia nyingi zimekosa mwelekeo; watoto wengi sasa hawapati elimu kwa kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha. Sasa wakati umefika ambao serikali ipende isipende, haina budi kubadili mfumo wa elimu tokea shule ya msingi mpaka chuo kikuu ili watoto wetu wanapomaliza, wawe wamejengewa msingi bora wa kujitafutia riziki bila kutegemea kuajiriwa pekee."

Akichangia hoja katika semina hiyo, mjumbe mmoja aliwalaani baadhi ya wakazi wa mijini wanaoita ndugu zao wa vijijini ili waje wawatafutie kazi mijini na badala yake huishia kukaa nao na baadaye kuwafukuza hali inayoongeza mmomonyoko wa maadili na vitendo vya uhalifu kuongezeka.

Jiji ladaiwa kuchonganisha wananchi na Serikali

Na Peter Dominic

CHAMA cha wapangaji nchini(Tanzania Tenants Association-T.T.A) kimeilalamikia Halmashauri ya Jiji kwa kuwabomolea vibanda wafanyabiashara ndogondogo licha ya viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kuwataka wasitishe zoezi hilo.

Shutuma hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Bw. Rajabu Mhembele alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake Magomeni jijini hivi karibuni.

alisema ubomoaji unaoendelea hivi sasa unawapaka matope viongozi wa ngazi za juu wa Serikali.

Katika ziara yake ya kutembelea wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam mwaka jana, Makamu wa rais Dk. Omar Ali Juma, aliitaka iliyokuwa Tume ya Jiji chini ya Bw. Charles Keenja, kuacha kuwabomolea vibanda wafanyabiashara badala yake iweke misingi imara ya kuwahakikishia maeneo ya kufanyia biashara kabla ya kutekeleza zoezi hilo.

"Mimi nina wasiwasi na wanaotekeleza zoezi hilo huenda hawana nia nzuri na serikali maana hata walipoambiwa wasifanye hivyo bado wanaendelea tena bila woga, hatuelewi nia yao," alihoji.

Alidai kuwa kitendo cha kuwavunjia watu vibanda bila kuwapa sehemu nyingine ni kukiuka haki za binadamu na kuna hatari ya kuwagawa wananchi katika makundi na kuhatarisha amani.

Akiongelea suala hilo, Afisa mmoja wa Halmashauri ya Jiji ambaye hakutaka jina lake lichapishwe Gazetini alisema wao kama watendaji wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na Bunge na si vinginevyo.

"Hatufanyi kazi kwa kumfurahisha mtu wala chama. Wanaosema wanaonewa huenda hawazijui sheria," alisema.

Hivi karibuni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikiendesha zoezi la kuwavunjia vibanda wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo ambayo hayakuidhinishwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya biashara zinazofanyika.

Hadi mwishoni mwa wiki zoezi hilo lilikuwa likiendelea.

Rushwa ya mapenzi ni hatari mno- Mkuu wa Wilaya

Josephs Sabinus na Elizabeth Steven, Kisarawe

RUSHWA zote ikiwemo ya kijinsia, upendeleo wa kindugu na udhaifu wa utendaji kwa viongozi, vimeelezwa kama ni vichocheo vya kuathiri utawala bora na kurudisha nyuma maendeleo na hivyo havina budi kuepukwa na jamii nzima.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Kapteni James Yamungu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani iliyofanyika hivi karibuni mjini hapa.

Akirejea igizo la Kikundi cha Mpango maalum Nje ya Vyuo kilichotumbuiza katika sherehe hizo, Kapteni Yamungu alisema, muombaji na mtoaji wa rushwa yoyote ikiwemo hii ya kijinsia, ni hatari katika maendeleo ya jamii na inawafedhehesha wahusika wote.

"Na haya tuliyoyaona katika mchezo huu ni kweli yapo na wote tunayaona. Mtu anakwenda kuomba kazi anazungushwa ili atoe mshiko. Au basi waajiri wengine; anaanza kuleta undugu na anaajiri kwa undugu, ni mbaya sana kwa maendeleo ya taifa," alisema na kuongeza,

"Unakuta mwanamke ana sifa zinazostahili, anaomba kazi anaambiwa, kafikirie namna ya kunifikiria na mimi. Hizi rushwa za kijinsia; rushwa za mapenzi, ziepukeni, ni hatari mno na ndiyo maana kama mko makini mnaona wafanyakzi wanakufa mno kwa ukimwi ni kutokana na hali hii.

Waajiri wote inabidi waepuke rushwa hizi. Wafanyakazi wote watendewe haki sawa bila kujali jinsia, kabila wala mahusiano ya kibinafsi."

Katika sehemu moja ya igizo, kikundi hicho kilimuonesha mwanamke akiomba kazi , lakini licha ya sifa na vithibisho vyake vya kutosha, mwajiri alimwambia akafikirie namna ya kumfikiria (mwajiri) hali iliyowasononesha watazamaji.

Aliwataka wafanyakazi kuchukua tahadhari dhidi ya janga la ukimwi, "Ukimwi unatumaliza na kumaliza nguvu ya taifa letu kwa wachapa kazi na unaleta umaskini kwa kuwa unagharimu mno bila kuokoa maisha," alisema.

Akijibu risala ya wafanyakazi wilayani hapa iliyosomwa na Bw. Seif Zahor ambaye ni fundi wa TANESCO, ambaye pamoja na Mwenyekiti wa TWICO wilayani hapo Bw.Stephano Mfundo, waliishauri serikali kulipa madeni ya ndani badala ya kukazania tu, kulipa madeni ya nje ya nchi huku hali ya wanachi kimaisha ikizidi kudorora, Kapteni ya Mungu alisema,

"Kulipa madeni ni vizuri na ni ungwana na ndiyo maana manufaa yake sasa yanaonekana kwani wadai wengi sasa wanafuta madeni ya nchi, wengine wanafikiria uwezekano wa kuyafuta na ndiyo maana, serikali imeanza kulipa madeni ya ndani."

Aliwaasa kujifanyia kazi za ziada ili kujiongezea mapato. "Inashangaza eti mtu wa Kisarawe; ukanunue mchicha Dar-Es-Salaam , badala ya watu wa Dar-Es-Saalaam kununua mchicha toka huku?" Alihoji Yamungu.

Aliisifu idara ya elimu wilayani hapa kwa kuongeza juhudi zake katika kupambana na tatizo la elimu na akasema wilaya yake imefanikiwa kuwa na shule za sekondari za kutwa katika tarafa zake zote ambazo ni Chole, Mzenga, Maneromango na Sungwi.

Shule mbili kati ya hizo zilifunguliwa mwezi uliopita ambazo ni Chole na Mzenga pamoja na shule za msingi mpya za Kiruga A, Kiruga B, Kibasila, Mroganzira na Kitanga.

Mbulu wanolewa kwa msasa mkali

Na Josephs Sabinus

Jimbo Katoliki la Mbulu linaendesha semina mbalimbali za uhamasishaji wa Jubilei katika parokia na dekania mbalimbali ili kuchochea na kuimarisha zaidi mori kwa walei na viongozi wa serikali juu ya imani yao na Jubilei Kuu

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Utume wa Walei wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Bw. Peter P. Massay, katika programu hiyo iliyoanza Desemba mwaka jana na kutarajiwa kumalizika mwaka ujao, jumla ya walei 508, wanne toka kila parokia, walishiriki semina ya awamu ya pili iliyofanyika kwa siku tatu katika kila tarafa (dekania) jimboni humo.

Bw. Massay aliyezungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma jijini Dar Es Salaam, alisema, walioshiriki semina za awali watakuwa na wajibu wa kuwaelimisha walei wengine ambao hawakupata fursa hiyo katika ngazi za parokia zao na kwamba tayari zoezi hilo limekwishaanza.

Alisema masomo katika programu hiyo yamegawanywa katika sehemu kuu mbili alizozitaja kuwa ni sehemu ya kwanza yenye masomo ya jumla ya; Jubilei Kuu Ituimarishe Katika Imani Yetu, Hija na Wongovu wa Kweli na Msalaba wa Jubilei.

Mkurugenzi huyo wa walei alisema, sehemu ya pili itayahusisha masomo ya Utume wa Familia, Utume wa Biblia, Utume wa Malezi ya Vijana, Uboreshaji wa mazingira Yetu, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Imani na Teolojia ya Maadili, Nafasi ya Bikira Maria Katika Jubilei Kuu na Kalenda ya Jubilei Kuu.

Semina za namna hii ni muhimu kufanyika katika majimbo mbalimbali ili kuwawezesha waamini kujua zaidi mambo ya Kanisa.

Wenye virusi vya Ukimwi Moro waunda chama

Na Seraph Kuandika, PST Morogoro

WATU wanaoishi na virusi vya Ukimwi katika manispaa ya Morogoro wanakusudia kuanzisha chama chao kwa lengo la kusaidiana.

Katika kufanikisha mpango huo, waathiriwa hao hivi sasa wanafanya semina ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kutathmini na kuchambua muundo wa Katiba ya chama chao.

Mratibu wa kitengo cha kutoa huduma kwa wagonjwa majumbani cha shukrani la faraja linalosaidia kuanzishwa kwa chama hicho Bi. Paulina Rwegayura ameiambia PST kuwa chama hicho kitajulikana kwa jina la kuishi kwa matumaini.

Bi. Rwegayura alisema wakiwa katika chama hicho waathirika watapata fursa ya kufahamiana na kutembeleana kwa lengo la kujuliana hali na kusaidiana.

Naye mmoja wa waathirika hao, Bi. Sabina Rocky, akizungumza na PST kwa niaba ya wenzake alisema lengo lao ni kutaka kusaidiana, kushauriana ili waweze kuishi kwa matumaini dhidi ya Ukimwi.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakifa kutokana na kukosa mwamko juu ya Ugonjwa huo, hivyo watakitumia chama chao kuelimisha jamii juu ya madhara ya ugonjwa huo.

"Unajua mtu mwenye kidonda ndiye anayefahamu maumivu anayoyapata, hivyo sisi tutatumia chama chetu kuelimisha jamii juu ya Ukimwi," alisema Bi. Sabina Rocky.

Semina hiyo ya waathirika wa Ukimwi inayomalizika leo ilifunguliwa na mwenyekiti wa bodi ya faraja mchungaji Canon Richard Kadege.

Mbunge kuwaaga wapiga kura wakewapiga kura wake

Na Dalphina Rubyema

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni Peter Kabisa ameanza ziaraya kuwaaga wapiga kura wake kufuatia muda wake wa kuongoza jimbo hilo kabla ya kufikia uchaguzi mkuu kumalizika.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake juzi, mbunge huyo alisema kuwa anafanya ziara hiyo kuwaaga wapiga kura hao kulingana na utaratibu wake wa kawaida.

Mbali ya hilo mbunge huyo atakagua shughuli za maendeleo katika jimbo lake na kuangalia pale ilipofikia baadhi ya miradi hiyo.

Alisema kuwa kuna miradi mingi ambayo ilianzishwa tangu achaguliwe mwaka 1995 na licha ya kupata taarifa zake za karibu mara kwa mara lakini anataka kuigakua mwenyewe na kusikiliza mafanikio na matatizo.

Mbunge huyo alisema kuwa ziara hiyo inafuatia ya awali ambayo aliifanya mara baada ya kuchaguliwa kwake kushika wadhifa huo ambayo ilihusisha ufunguzi wa miradi mbalimbali.

Anaitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ile ya ushonaji ya kinamama wa kata mbalimbli za jimbo hilo, ujenzi wa madaraja na mengine ambayo ni ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine Kabisa atatumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa ushirikiano walioutoa wakati wote alipokuwa madarakani.

Mbunge huyo alisema kuwa kabla ya kumalizika kipindi chake cha kuwepo madarakani kimsingi ni laaimz akague miradi ambayo ilianzishwa chini yake ili hata mbunge mwingine atayekuja aiendeleze.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kitapiga kura ya moni hivi karibuni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za ubunge na katika jimbo hilo tayari mwanaCCM mmoja ameishatangaza nia yake ya kuwania kiti hicho.

Mwanachama huyo wa chama tawala ambaye ametangaza nia yake hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita ni Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Klabu ya Soka ya Yanga ya jijini, Abbas Tarimba.

Njaa ya pesa yakosesha chuo cha Uhasibu wanafunzi

Na Neema Dawson.

SERA ya Uchangiaji wa Gharama za Elimu imefanya idadi ya wanafunzi katika Chuo cha Uhasibu jijini- DSA kupungua, imeelezwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Chuo hicho Profesa Leticia Rutashobya, alisema wakati wa mahafali ya 21 ya chuo kuwa wanafunzi wa kozi za Stashahada ya juu ya Uhasibu Serikalini wamekuwa haba ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisema hata idadi ya wanafunzi wanaojiunga hivi sasa na kozi za cheti cha uhasibu serikalini (CGA) na uboharia (CMM) wamekuwa adimu hasa katika matawi ya Singida na Mtwara ambako ilitokea kukosa kabisa wanafunzi kuanzia mwaka 1997 hadi hivi sasa.

Rutashobya alisema katika risala iliyosomwa mbele ya mgeni Rasmi aliyemwakilisha Waziri wa Fedha kuwa vyeti na stashahada ya juu ya uhasibu Serikalini zimeshindwa kabisa kuvutia wanafunzi na akatoa mfano kwama mwaka 1996 usajili wa wanafunzi katika ngazi ya cheti ulikuwa wanafunzi 139 ambapo idadi hiyo imepungua hadi kufikia wanafunzi 21 kwa mwaka 1999.

Katika kozi ya Stashahada ya juu ya Uhasibu Serikalini wanafunzi 54 walisajiliwa mwaka 1996 lakini mwaka 1998 hakuna mwanafunzi aliyesajiliwa kwa kozi hiyo kutokana na ukosefu wa udhamini.

Hali hiyo ya upungufu wa wanafunzi wa uhasibu serikalini imepelekea matawi ya chuo ya Singida na Mtwara kukosa wanafunzi kwa kozi hizo mpya hivyo bado matawi hayo ya chuo yanaendelea kufundisha kozi za kawaida zinazosimammiwa na kitengo cha Consultancy Unit ambapo wanafunzi hao hufanya mitihani ya bodi za Taifa yaani NBAA (T) na NBMM (T).

Katika Risala hiyo pia alisema kuwa licha ya wanafunzi kushindwa kujiunga chuoni kwa kushindwa kuchangia gharama za elimu pia chuo hicho kinakabiliwa na ukosefu wa vivutio (Incentives) kama vile mishahara mizuri, nyumba na posho mbali mbali kwa wakufunzi wa chuo, hali ambayo imechangi baadhi ya wakufunzi kutodumu katika ajira zao hapo chuoni kwa sababu maslahi wanayoyapata hayalingani na vyuo vingine vya kati vilivyo sawa na chuo hicho cha uhasibu.

Pia alisema kuwa tatizo kubwa la ajira serikalini limepelekea wazazi kusita kusomesha vijana wao , kwani uwezo wa chuo ni jumla ya wanafunzi 910 lakini hivi sasa chuo kina wanafunzi 334 tu yaani wanafunzi wa kozi ya cheti ni 21 na stashahada za juu ni 313.

Akijibu risala hiyo kwa niaba ya Waziri Yona , Naibu katibu Mkuu wa wizara ya Fedha Bw. Lyimo alisema kuwa wasomi wote hapa nchini kuvitumia ipasavyo vyuo vyote vilivyo hapa nchini badala ya kupenda kukimbilia vyuo vilivyo nje ya nchi kwa kudhani kuwa ndivyo vinavyofaa licha ya kuwa na gharama kubwa aliyasema hayo wakati wa kuwatunuku vyeti na stashahada ya juu wanachuo 312.

Hata hivyo Bw. Lyimo alisema kuwa Serikali yake inafanya jitihada ili kuhakikisha kuwa Watumishi wanapata mishahara ya kuvutia ili kuongeza ufanisi na tija na ikizingatiwa kuwa utekelezaji utakuwa kwa awamu. Pia alisema kuwa Wakufunzi na Wafanyakazi wengine wapate mafunzo zaidi kwa kuwa kusoma nje ya nchi ni gharama zaidi kuliko hapa nchini, aliwashauri wakufunzi wote kuvitumia ipasavyo vyuo vyetu vingi havijaweza kutumika kikamilifu kulingana na uwezo wake na hivyo vitumike ipasavyo na si kuvikimbia na kupenda vya nchi za nje.

"Ajira hivi sasa ni tatizo kubwa ambalo tunategemea kuwa litaanza kupata ufumbuzi kadri uchumi wa nchi unavyoimarika kwa kuzingatia mafanikio ya kuimarisha uchumi katika miaka ya karibuni na kwa kuzingatia kuwa wahitimu wengi wa chuo cha Uhasibu ni wa fani ya Uhasibu Wizara yangu itajitahidi kutoa ajira kila inapowezekana"