Msiuze kura zenu kwa pombe, CPT yawaonya Watanzania

Na Mwandishi Wetu,

Tanzania (CPT), kimewashauri wananchi kutokuhadaika na rushwa ya vitu vyovyote zikiwamo pombe, chumvi na pesa ili kuuza haki yao kwa kuwapigia kura viongozi wasiofaa.

Mratibu wa CPT taifa Bi. Mariamu Kessy, alitoa ushauri huo mwishoni mwa juma wakati akitoa taarifa kwa gazeti hili juu ya semina iliyoandaliwa na CPT kwa kushirikiana na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ili kutoa mwongozo katika kujenga ushiriki wa watu.

Akizungumzia semina hiyo ya siku tatu itakayofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kurasini jijini, Bi. Kessy alisema, "Lengo la semina hii ni kutoa mwongozo kwa wahamasishaji wa majimbo ili wajue wajibu wao na mbinu za kuwa hamasishawaleikutekeleza vema yaliyomo katika kitabu cha "UCHAGUZI WA KISIASA KWA NINI TUNAJALI?" Bila kuleta ugomvi wowte kati ya jamii, Serikali na Kanisa."

Alisema endapo washiriki wa semina hiyo toka majimboni wataelewa vema wajibu wao na mbinu za kuhamasisha jamii kujua inapaswa kufanya nini kwa maufaa ya taifa zima wakisaidiwa na kitabu hicho, watakuwa wameepusha migongano isiyo ya lazima.

Kitabu cha "UCHAGUZI WA KISIASA KWANINI TUNAJALI?"kimeandaliwa na Tume ya Haki na Amani ya baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Februari 2000.

Kuanzia toleo lijalo, gazeti hili litatoa mfululizo mzima wa chapisho la kitabu hiki kwa usahihi kabisa bila kubadili, wala kutafsiri neno lolote ndani yake ili kuepuka upotoshwaji wa tafsiri unaoweza kujitokeza.

Wakati HUO HUO: Akitoa salamu za pasaka katika mahubiri yaliyofanyika Jumapili iliyopita katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Askofu Mkuu Msaidi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Mhashamu Method Kilaini amesema chuki, utengano, dhuluma,na rushwa unaofanya na watu wenye nyadhifa mbalimbali katika maeneo yao ya kazi havina budi kuepukwa mara moja kwa kuwa si mapenzi ya Mungu.

"Unanyanyasa walio chini yako na kula hongo zao ili wabaki kazini. Mungu ndiye aliyekupa uwezo, mamlaka na nguvu, mrudie yeye kwa sababu atakuuliza juu ya dhamana uliyopewa. Mrudie Mungu, amefufuka nawe fufuka naye na kuwa na moyo mpya. Afadhali umaskini wa amani kuliko utajiri wa dhuluma." Alisema na kuongeza,

"Vurugu zinazoibuka hapa na pale, migogoro, kukosa makubaliano na muafaka kati ya watu, viongozi, watu wa siasa viishe. Hatuwezi kufanikiwa kiuchumi, kisiasa au kijamii kwa kuchimbiana mashimo, kulimana, kudhulumiana au kupigana. Undugu wa kitaifa ni lulu yenye thamani ambayo kila mmoja analo jukumu la kuitunza na kuilinda. Tumuombe Bwana Yesu Mfufuka atusaidie." Anaripoti Elizabeth Steven

Kakobe ashushiwa'rungu' kichwani

Na Getruder Madembwe

WAKATI kiongozi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakaria Kakobe,alitangaza hivi karibuni kwamba anakichukia Chama cha Mapinduzi na kuwataka wananchi wakiwemo wafuasi wake waiondoe madarakani, viongozi wa dini nchini wameonywa kutowachagulia waamini wao vyama vya siasa.

Rai hiyo ilitolewa na Askofu Saimoni Buteng’e wa Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Mashariki lililopo Upanga, Dar Es Salaam alipokuwa akizungumza katika ibada ya Pasaka iliyofanyika kitaifa kanisani hapo.

Alisema kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuihubiri Injili na sio kuwapigia wanasiasa kampeni wanapokuwa katika makanisa yao kwani kufanya hivyo ipo hatari ya kuwagawa waamini katika makundi.

Askofu Buteng’e alisistiza kuwa kazi nyingine ya viongozi wa dini ni kuiombea nchi idumu katika amani nchi yetu na kumwomba Mungu atupe viongozi wanaofaa pamoja na kukemea maovu.

"Jamani sisi viongozi wa dini hatufai kuwachagulia waumini wetu chama cha siasa eti hiki ndiyo kinafaa hiki hakifai. Kazi yetu ni kumwomba Mungu atupe watu wenye uwezo na hata kufunga kwa kuomba kwa ajili yao.

Jamani viongozi wenzangu, tusifanye hivyo kwani siasa ina wenyewe," alisema Askofu Buteng’e.

Aidha Askofu Buteng’e aliwataka wakristo na wananchi wote kutohongwa na mtu au chama chochote cha siasa wala wagombea na wapiga debe wao hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

"Wakristo tusihongwe na mtu yeyote yule hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ila tumwombe Mungu atusaidie kuchagua viongozi wanaofaa," alisema.

Akielezea baadhi ya sifa za kiongozi anayefaa, Askofu Buteng’e alisema kiongozi anayefaa ni yule asiyependa kujinufaisha mwenyewe, anayeichukia rushwa na mpenda haki na amani.

Alisema kuwa kiongozi asiyependa vitu hivyo kamwe hafai kuingoza nchi kama Tanzania.

Hivi karibuni kiongozi wa Kanisa la Full Gospel, Zakaria Kakobe, alisema hadharani kuwa anaichukia CCM kwa vile imejaa unafiki na inataka itikadi zake ziabudiwe kama Mungu.

Kakobe alidai CCM inatakiwa iondolewe madarakani, kauli ambayo ilionekana ni sawa na kuwataka wafuasi wake wasiipe CCM kura, kitu ambacho ni kuingilia uhuru wao wa kuchagua.

Kauli hiyo ilizusha majibizano makubwa kati ya Kakobe na viongozi wa CCM hususan Umoja wa Vijana wa chama hicho tawala, ambapo Kakobe alishutumiwa kuwa anachanganya siasa na dini na kutakiwa achague moja, siasa au dini.

Wapentekoste wawaachia Wamoravian Kanisa

lWaamua wawasubiri mlangoni mpaka watoke

lWamoravia wasema hawakwenda msikitini kwa makusudi

Na Josephs Sabinus

KATIKA hali inayoonekana kutokuwa ya kawaida, Kanisa la Pentekoste Tanzania limeliachia jengo lao Kanisa la Moravian Tanzania

ili walitumie katika ibada zao.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na wachungaji wa makanisa hayo yaliyopo Keko wilayani Temeke, jijini Dar Es Salaam, hatua hiyo inafuatia ujenzi wa jengo la Kanisa la Moravian Tanzania, Usharika wa Keko, katika Wilaya ya Mashariki Jimbo la Kusini, ambao umefikia hatua ya kuweka zege katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo hali iliyowafanya Wamoravian kukimbilia Pentekoste kupata hifadhi.

Wachungaji hao Luther Shumba wa Kanisa la Pentekoste Tanzania, parishi ya Keko, jimbo la Mashariki na Pwani, na Salatieli Mwakamyanda wa kanisa la Moravian , Usharika wa Keko, katika Wilaya ya Mashariki Jimbo la Kusini, walisema uamuzi hatua hiyo inatokana na wao kutambua na kuamini kuwa makanisa yote ni ndugu katika Kristo hivyo ni vyema kushirikiana katika mambo muhimu ya Kimungu na kuondoa tofauti zote za kimadhebu.

Habari zinasema Wapentekoste hao watawahifadhi Wamoravian kwa takribani miezi miwili hadi ujenzi huo utakapokamilika na kwa mujibu wa makubaliano yao, kanisa la Moravian litaanza kutumia jengo hilo kwa ibada za Jumapili tangu saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi ambapo wenyeji wao(Wapentekoste)badala ya kuanza ibada yao saa 3:00, sasa wamewaachia Wamoravian na kwamba watakapofika watawasubiri nje hadi wamalize na wao kuanza saa 3:30 asubuhi.

Awali mwaka jana wakati Kanisa la Pentekoste linaendesha ujenzi wao, Wamoravian waliwafadhili kwa huduma ya umeme kwa zaidi ya miezi sita baada ya wenyeji wa eneo yaliyopo makanisa hayo ambao wengi ni wafuasi wa dini ya Kiislamu kuwanyima Wapentekoste umeme.

Walipoulizwa kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi sababu iliyofanya waamue kufanya ibada ya pamoja ya mapokezi Jumapili hii katika kanisa hilo ambapo wenyeji wataongoza, Mchungaji Salatieli Mwakamyanda wa Kanisa la Moravian alisema,

"Tumekwenda pale kwa kuwa ndio Wakristo wenzetu walio jirani na hii ni kwa kuwa tunajua wote ni watoto wa Kristo aliyekufa msalabani. Wewe unafikiri ni kwanini hatukwenda kwa Waislamu?"

"Unajua huwa ninashangaa sana baadhi ya madhehebu ya Kikristo yanaleta masuala ya kukashifiana, Ooh! Hawa wanafanya hivi, hawa wanafanya hivi, Unajua ni kwa kuwa hawajui kuwa Yesu anashangazwa na vitendo hivyo tunavyovifanya sisi Wakristo wenyewe kwa wenyewe,"

Naye Mchungaji Luther Shumba wa Kanisa la Pentekoste alisema, " Lazima Wakristo tufike mahala tujue kuwa ni ndugu katika Kristo na sidhani kuwa tofauti za madhehebu zinatosha kutufanya tushishirikiane kufanya kazi ya Kristo.

Ni sawa na nyumba kubwa yenye vyumba vingi tu, sasa hivyo vyumba ndiyo haya madhehebu lakini wote ni kitu kimoja."

Katika mazungumzo tofauti na gazeti hili wachungaji hao walisema ili kuthibitisha kuunga mkono juhudi za kueneza Ukristo kwa kasi na upendo, wako tayari kualikwa na kukubali kufanya mahubiri katika makanisa mengine na kuwaalika viongozi wa makanisa mengine kuhubiri makanisani kwao ili mradi wasije kwa lengo la kuhubiri siasa wala kashfa dhini ya madhehebu mengine.

Hata hivyo, ili kueneza zaidi Ukristo duniani kote, madhehebu ya Kikristo hayana budi kuungana na kurudi kuwa kitu kimoja ili kudumisha umoja , mshikamano na upendo katika Kristo ili Injili ihubiriwe na makanisa haya ni mfano bora wa kuigwa.

Ukishindwa kutunza mimba niletee, usiue - Askofu

Na Charles Hililla, Shinyanga

Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina amekemea vikali tabia ya utoaji mimba kwani ni mauaji na akasema msichana yeyote jimboni kwake atakayeshindwa kulea mimba amuone amsaidie kuitunza mpaka kuzaa kuliko kuua kwa njia hiyo.

Askofu Balina aliyasema hayo hivi karibuni wakati akiwahubiri vijana wapatao 1000, katika ibada ya ufunguzi wa kongamano la Pasaka la Wanafunzi wanachama wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wa Sekondari na Vyuo (TYCS), tawi la Shinyanga.

Aliowanya vijana kulinda maadili na kuzitunza heshima zao kama vijana

kwa kuepuka uasherati na tabia nyingine chafu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuepukana na matatizo ikiwa ni pamoja na kupata mimba nje ya ndoa na zile zisizotarajiwa hali ambayo alisema inachochea mauaji kwa njia ya utoaji mimba.

"Kutoa mimba ni kuvunja Amri ya Tano ya Mungu inayokataza kuua. Hakuna binadamu mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wake au binadamu mwenzake isipokuwa Mungu mwenyewe.

Msichana yeyote atakayepata mimba na anaona hawezi kuitunza, aje kwangu (Askofu) anione, nipo tayari kumsaidia kwa kumtunza hadi mtoto atakapozaliwa nitamtunza pia. Hivyo msijaribu kamwe kuua au kujiua kwa sababu yoyote ile," alisema Askofu

Askofu Balina alisema maovu mengi kwa vijana katika jamii yanasababishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuiga mambo ya kigeni, tamaa mbaya, anasa, uvutaji bangi, madawa ya kulevya, pamoja na utoaji wa mimba ukiwa ni matokeo ya kutotunza maadili safi ya ujana.

Aliwataka wana-TYCS hao kuwa wabunifu na wachapa kazi ili kuliletea taifa maendeleo na kuwa viongozi safi wa baadaye kwani endapo watalegea, taifa litakuwa legelege na kuwa mwanzo wa kuangamia taifa la Mungu katika nyanja zote hasa zile za jamii.

Akisaidiwa na Padri Filimoni Machagija ambaye ni mlezi wa vijana pamoja na paroko wa Kanisa Kuu la jimbo Padri Kizito Nyanga, katia ibada hiyo iliyohudhuriwa na vijana kutoka shule 20 kati ya 30 zilizopo katika jimbo lake,

aliwahimiza walimu kutofundisha tuisheni kwani inapingana na maadili ya kazi yao.

Alisema tuisheni inawapunguzia walimu ari ya kufundisha wanapokuwa katika vipindi vya kawaida shuleni wakitilia maanani tuisheni ambayo ni mradi.

"Shule za seminari hawafundishi tuisheni lakini kila mwaka wanaongoza kwa nini wasiongoze wale wanaofundishwa tuisheni kwa vile wanasoma sana?" Alihoji huku akishangiliwa na umati wa wanafunzi waliokuwa wamefurika kanisani hapo.

Baada ya ibada hiyo, ilifuatia michezo mbalimbali ya jukwaani uliyokuwa imeandaliwa na vijana hao ikiwa ni pamoja na maigizo, nyimbo, jiving, kwaya na vichekesho.

Pia walimpatia Askofu Balina zawadi ya ng’ombe wa maziwa na mifuko mitano ya saruji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujenzi mfano seminari ya jimbo na kituo cha Redio. Askofu alifurahishwa na zawadi hizo ambapo naye akatoa jumla ya sh 500,000/= kwa ajili ya kuchangia kutunisha mfuko wao.

Sipo tayari kusomesha matajiri -Pengo

lPia "hatutaki umaarufu"

lAsema kanisa halina haja ya kupindua Serikali

Na Leocardia Moswery

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo amesema hayupo tayari kusaidia kusomesha matajiri walio na kipato cha juu, wakati wapo watu wengine wasio jiweza kabisa na wanahitaji msaada huo.

Kardinali Pengo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Ibada ya Shirikisho la Kwaya Katoliki(SHIKWAKA)iliyofanyika kigangoni Msewe katika parokia ya Ubungo jimboni Dar Es Salaamam. Ibada hiyo kwa kawaida hufanyika kila mwaka siku ya Jumatatu ya Pasaka.

"Sipendi kusomesha matajiri ambao wana uwezo wakati kuna maskini ambao hawajiwezi", alisema Kardinali Pengo na kuongeza, "Nilitumwa kuhubiri Injili kwa watu wote na wala siyo kuwasaidia matajiri peke yao lakini hata kwa maskini na siyo kwa watu wema bali kwa wenye dhambi".

Alisema kuwa elimu ni kitu muhimu kwa kila Mtanzania na wala siyo kwa ajili ya Wakatoliki ndiyo maana Kanisa Katoliki linajenga mashule na hospitali ili kuwapatia raia elimu na huduma mbalimbali za ustawi wa jamii ili kufanya kazi ya Uinjilishaji na wala sio kutafuta umaarufu.

Misa hiyo ilihudhuriwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo Method Kilaini, Mkurugenzi wa Walei Jimbo Padre Brain Mkude pamoja na Paroko wa Parokia ya Ubungo na msaidizi wake pamoja na Mwenyekiti wa SHIKWAKA, Bw.Starniley Mjwahuki.

Pengo alisema yeye wala Kanisa halitafuti umaarufu bali wanafanya hiyo ili kila jamii yote itambue kuwa Kristo alifufuka kwa ajili ya kila mtu na siyo kwa Wakatoliki tu.

Aidha, kardinali Pengo alisema Kanisa Katoliki nchini halina haja ya kuzipindua serikali za watu ili kujitengenezea majina, linachofanya ni kuwaletea watu Habari Njema na kuwasaidia Watanzania wote.

Alisema hivi sasa kuna watu wanaoibuka kulipaka matope na kuharibu jinazuri la Kanisa Katoliki kwa ajili ya manufaa yao binafsi na vikundi vyao.

Aliongeza kuwa hivi sasa amechoshwa na baadhi ya magazeti yenye nia mbaya ya makusudi ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiandika habari za uongo dhidi ya kanisa ili lionekane kana kwamba linakwenda kinyume na serikali na kudai kuwa "kama kuna mtu anayetaka kuniuliza na awe na maana na siyo hawa wanaoandika upumbavu ambapo magazeti mengi yamenichosha," Pengo.

Alisema kuwa Kanisa linatumwa na Yesu Kristo kuwahubiria watu wote kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu na afya kwa hiyo hakuna anayepaswa kukata tamaa katika maisha awe maskini, vipofu ambapo sentense ya mwisho ipo ndani ya ufufuko wa Bw.Yesu Kristo.

Hata hivyo Mwadhama aliyalaani mauaji yanayofanwa kwa vikongwe kwa kuwa eti wana macho mekundu wakidhaniwa ni wachawi. Akitoa mfano wa kukilani kitendo hicho cha uonevu na mauaji, kardinali Pengo alisema,

"Kwa mfano, watu wengine wanakunywa pombe na kubadilika macho yao kuwa mekundu kwa hiyo macho mekundu siyo uchawi, hiyo si vyema kuwauwa."

Kumbe dawa ya ukimwi ipo - Makamba, KKKT

Getruder Madembwe na Josephs Sabinus.

MKUU wa mkoa wa Dar Es Salaam na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wamesema wanashangaa kuona jamii ya Watanzania inateketea kwa ugonjwa wa ukimwi huku dawa ipo lakini haitumiki.

Waliyasema kwa nyakati tofauti jijini Dar Es Salaam wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka ambapo Mkuu huyo wa Mkoa Luteni Yusufu Makamba alikuwa mgeni rasmi katika Kanisa la Menonnite Upanga, na Mkuu wa Jimbo la Temeke wa KKKT, Mchungaji Astorn Kibona alikuwa akizungumza katika usharika wa Keko.

Walisema inasikitisha kuona kuwa ingawa ugonjwa huo unalo dawa, bado unaua kwa kasi na kiasi cha kutisha bila kujali umri, kabila, dini au itikadi za kisiasa, bado jamii inafanya uzembe kutumia dawa na kinga yake ingawa ipo, haiuzwi na inafahamika wazi kuwa ni kuepukana na vitendo vya usherati na kuzishika Amri za Mungu ikiwemo ile ya Amri ya Sita isemayo Usizini.

Makamba ambaye katika sherehe hiyo alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu, Mheshimiwa Fredrick Sumaye, aliwataka viongozi wa dini zote za Kiislamu na Kikristo kuwahimiza waamini kutofanya biashara ya ukahaba kwani machangudoa hao ni miongoni mwa waamini wao ambao huwa makanisani na misikitini mchana wakati wa ibada, lakini usiku huwa barabarani wakiuza miili yao.

"Jamani nyie viongozi wa dini mnatakiwa kuwaambia waamini wenu kufanya kazi ambazo ni halali lakini si uchangudoa maana machangudoa mchana wapo makanisanina misikitini lakini inapofika usiku utawakuta wapo barabarani wakiuza miili yao.

Jamani tusaidiane jamii ielewe kuwa dawa ya ukimwi ipo lakini watu hawataki kuitumia. Dawa ya ukimwi ni kuachana na vitendo vya zinaa na uasherati. Shika ile Amri ya Sita ya Mungu tuone kama huo ukimwi utakugusa."

Naye mchungaji Astorn Kibona alisema, "Wakristo wanahofu ukimwi, kwanini wahofie ukimwi kama wanafuata Amri Kumi za Mungu? Usizini ndiyo dawa ya ukimwi.

Kwa vifo vya ukimwi ndipo tunajua kuwa kumbe watu hawafuati Amri za Mungu. Tunazika vijana wengi wa kike na wa kiume wanaokufa kwa ukimwi; tena wengine wana ndoa zao. Tumieni dawa ya ukimwi, hii ni Amri ya Sita; usizini."

Ugonjwa wa ukimwi ambao mpaka sasa haujapata kinga wala tiba, huenea zaidi kwa njia ya vitendo vya uasherati.

Viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii wamekuwa wakiwasisitiza wana jamii kuepukana na vitendo vya ndoa kabla na nje ya ndoa kwa kuwa ndio dawa pekee inayoweza kuwaepusha watu katika janga hili ambalo limeukumba ulimwengu mzima.

Kampuni ya madini yawaudhi wananchi wa Shinyanga

Na Charles Hililla - Shinyanga

Wakazi wa mkoa wa shinyanga wameilalamikia kampuni yenye hisa na serikalai ya kuchimba na kuuza madini ya almasi katika mgodi wa Williamson Diamond uliopo kilometa 30 kutoka mjini shinyanga

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mapema wiki hii, wanakijiji hao walisema huduma za jamii mkoani humo zimezopuuzwa na wachimbaji

Na wakazitaja kuwa ni pamoja na elimu, maji, afya na mawasilianao.

Walisema hawaoni manufaa ya kuwepo kwa wawekezaji hao mkoani hapo tofauti na wazekezaji wengine wanaokarabati na kujenga baadhi ya shule, barabara na zahanati katika meneo wanayofanya kazi.

Waliendelea kuhoji taarifa iliyotolewa kwa Rais na ofisi ya madini mkoani hapa wakati wa ziara yake hivi karibuni.

Kuwa jumla ya karati 276,469 zenye thamani ya bilioni 3,344 ziliuzwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo mwaka jana zilipatikana Almasi zenye karati 207,500 zenye thamani ya shilingi 23,240,000,000. Na mwaka juzi zilipatikana karati za almasi 68,969.2, zenye thamani ya bilioni 10.2.

Sasa kwa kipato hicho ilichopata serikali kupitia kwa wachimbaji hao pamoja na kuwa taarifa hiyo siyo sahihi kwa vile Almasi nyingi kutoroshwa, na kumbukumbu gani inayoachiwa mkoa baada ya kupatikana kwa mali hizo.

Kinyume na kumbukumbu za kimaendeleo mkoa unabaki na mashimo yasiyokuwa na mfukuaji baada ya kuchimba almasi na uharibifu wa mazingira kwa vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Aidha kwa upande wa barabara hali ni mbaya hasa unapofika katika mji wa Maganzo ambapo baadhi ya madaraja yamevunjika na barabara hiyo ni kiungo kikuu cha mawasiliano kati ya mikoa mingine ya kanda ya ziwa.

Walisema kuna upungufu mkubwa wa dawa muhimu za binadamu katika zahanati za Maganzo na kituo cha afya cha Songwa ukiachilia mbali uchakavu wa majengo ambayo hayajafanyiwa ukarabati tangu yajengwe enzi za mkoloni kabla ya uhuru kwa vile wao hawaoni maana ya kutoa msaada katika sekta hizo kwa vile wao hawazitumii kuna maana gani kuwepo hapa.

Msiwaweke Wakristo chini ya hofu ya ibilisi-Rai

Na. Fr. Raphael R. Kilumanga

"Mhubiri Kristo mshinda, msihubiri ibilisi na nguvu zake," Rai hiyo imetolewa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa ibada ya kubariki mafuta ya Krisma iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu, jijini.

Akiwaasa mapadre wa jimbo lake katika ibada hiyo ya hivi karibuni, Pengo alisema kwa kuwa kazi ya makuhani siyo kuwatia hofu bali kuwatangazia watu Habari Njema na kuwafanya wajiweke chini ya Kristo toka kwa ibilisi, hawana budi kuwatambua na wenye hofu na kuwaondolea hofu juu ya maisha yao.

Akizungumzia maauaji waliyofanyiwa wafuasi wa dhehebu la Kurejesha Amri Kumi za Mungu, huku Kanungu nchini Uganda hivi karibuni yakiongozwa na Joseph Kibwetere, Pengo alisema inasikitisha mno kusikia kuwa baadhi ya viongozi wa mauaji hayo walikuwa mapadre waasi walioasi Ukatoliki na akaitahadharisha jamii kuwa macho na viongozi wa dini wanaoasi dini zao za awali.

"Nimeshitushwa sana na kitendo cha mapadre hao cha kushiriki katika kuleta balaa na maangamizi ya watu hawa wa Mungu," alisema Kardinali Pengo.

Alisema kwa kuwa kila mtu anajua kuwa ibilisi yupo, mapadre hawana budi kujua na kuzingatia kuwa kazi yao ni kuutangaza uwepo wa Kristo Mfufuka kama Mwokozi na Mshindi wa nguvu zote.

Aliendelea kueleza kuwa Kristo aliwashirikisha mapadre ukasisi wake ili kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika na kuongeza kuwa mapadre walikuwa na jukumu la pekee la kutangaza muongozo huo wa kuwahubiria maskini habari njema ili Jubilei Kuu 2000 ipate nguvu.

Mwadhama Pengo aliwataka Watawa na Walei ambao pia walihudhuria ibada hiyo kuwaombea mapadre ili wadumu katika huduma yao.

Pia aliwataka waamini wamuone Kristo katika mapadre na wasingoje hadi Kristo mwenyewe maana wakingoja hadi Kristo arudi ili wamuone watachelewa.

Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam Mhashamu Method Kilaini na waseminari wakuu wa Segerea pia walishiriki katika misa hiyo ya Krisma.

Banduka ajivunia Pwani kuiuzia korosho Hoteli ya Sheratoni

Na Leocardia Moswery, Kibaha

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bw. Nicodemus Banduka amefurahia mkoa wake kuyauzia korosho mahoteli makubwa ikiwemo Hoteli ya kimataifa ya Sheraton iliyopo Jijini Dar-Es-Salaam baada ya wakulima kuboresha zao hilo mkoani hapa.

Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Mwendapole katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa mfuko wa kuondoa umaskini(SELF) mwishoni hivi karibuni Banduka alisema kuwa

"Mkoa wa Pwani sasa umeanza kuuza korosho Sheraton baada ya kubanguliwa na mashine nzuri na kupatiwa dawa ya kuzuia wadudu aina ya Sulphur hiyo ni hatua kubwa endeleeni kuziboresha."

Aidha, alisema Mkoa wa Pwani umeanza kukarabati viwanda vichakavu na kufufua vilivyolala kwa muda mrefu vikiwemo vya pamba na mkonge viliyopo wilayani Rufiji.

Alisema Mkoa wake umepiga hatua kielimu mwaka juzi na kwamba ulishika nafasi ya 14 kitaifa ambapo mwaka juzi ulishika nafasi ya 8 ambapo alisema kuwa elimu ya mwaka huu wanatazamia kushika namba ya tano kitaifa.

Bw. Banduka alisema kuwa mkoa umeshajenga shule 39 na nyumba 15 za waalimu pamoja na shule moja ijulikanayo kama kiwanga Sekondari Sikuli.

Shule ya BAKWATA yadaiwa kuwabagua CHADEMA

Na Dalphina Rubyema

UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Kinondoni ambayo inamilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wamekikatalia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutumia majengo ya Shule hiyo kwa ajil ya mkutano wa uchunguzi wa tawi la Kinondoni Shamba.

Kulingana na barua yenye kumbukumbu namba K55/CD/2000 ya Aprili 17 mwaka huu kutoka kwa Uongozi wa shule hiyo kwenda CHADEMA chama hicho hakupewa nafasi ya kufanya mkutano wa Uchaguzi katika madarasa ya Shule hiyo kwa uwa hayalingani na mahitaji yao.

Ilisema barua hiyo kuwa vyumba vya madarasa hayo vinaweza kuchukua watu kati ya 45-50 na si zaidi ya hapo kufuatia ombi la chama hicho kuwa mkutano huo utashirikisha watu wapatao 90.

Barua hiyo ambayo imesainiwa Mkuu wa Shule hiyo Bw. Rajabu Mruma imesema kuwa pamoja na mambo mengine wanachama hao hawataweza kupata huduma mbalimbali wakiwa katika mkutano huo wa siku nzima ambayo ni pamoja na ulinzi.

Katibu wa muda wa Chama hicho tawi la Kinondoni Shamba Bw. Rajab Kondo alipozungumza na kiongozi aliyepinga madai ya Uongozi huo na kudai kuwa hayana msingi na ni ya kisiasa zaidi kuliko ukweli ulivyo.

Alisema kuwa anashangaa kwa chama chake kunyimwa nafasi wakati chama tawala (CCM) kimekuwa kikifanya uchaguzi na mikutano yake madarasa ya shule hiyo bila mizengwe.

"CCM wanakusanya watu zaidi ya 100 katika vyumba vya madarasa ya shule hiyo na kufanya shughuli zao kutwa nzima vipi sisi tukataliwe?" alihoji.

Bw. Kondo ambaye alikuwa mwanachama wa CCM kabla ya kukihama chama hicho hivi karibuni alisema kama uongozi wa shule hiyo umeonyesha walakini kwa kitendo hicho na kudai kuwa suala la ulinzi si la kwao wala haliwahusu.

Mkuu wa Shule hiyo Bw. Rajabu Mruma alikiri uongozi wa shule hiyo kukataa ombi la CHADEMA kupitia barua ya hiyo.

Bw. Mruma alikanusha CCM kupewa fursa shule hiyo kwa namna aliyodai Katibu huyo na kusema kuwa haijatokea wakaruhusiwa zaidi ya watu 50 kufanya mkutano katika shule hiyo.

"Mara nyingi wanakuwaga wachache tu" alisema na kuongeza kuwa suala la ulinzi ni muhimu eneo la hilo kwa kuwa kuna ofisi zenye vifaa vya thamani na mlinzi wao ni mmoja hivyo ni vigumu kwake kuweza kuwadhibiti watu zaidi ya 50 wakatawanyika" alisema.

Aliongeza kuwa huduma ya vyoo nalo linaweza kuwa tatizo kwa idadi kubwa kama hiyo hali inayoweza kusababisha uchafuzi wa mazingira. "Kama wangesema labda vijana wao watakuwepo kusaidia ulinzi labda tungewafikiria na wao waliposema kuwa mkutano ni wa wananchi tuliona kabisa kuwa haifai kufanyika sehemu ya shule ambako hakuna ukumbi isipokuwa madarasa " alisema.

CHADEMA katika uchaguzi huo utakaofanyika Aprili 31 mwaka huo wanatarajia kuwachagua viongozzi wa tawi katibu Mweka hazina, wajumbe 5 wa Kamati ya Utendaji na wawakilishi wa Matawi katika kata.

Katibu huyo alisema Uchaguzi huo sasa utafanyika makao makuu ya CHADEMA yaliyopo mtaa wa ufipa Kinondoni jijini.

Ugonjwa wa ukoma si laana-semina

Na Dalphina Rubyema

IMEELEZWA kuwa ugonjwa wa ukoma ni kama yalivyo magonjwa mengine na wala siyo wa laana ama wakulidhisha kama wengi wanavyodhania.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mratibu wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania,Bw.Said Egwagi wakati wa Semina ya ukoma iliyofanyika jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni.

Mratibu huyo alisema kuwa ugonjwa wa ukoma unatibika tena bure bila malipo yoyote hivyo watu mbalimbali hawana budi kupata matibabu pale wanapijihisi kuwa na ugonjwa huo.

Alisema kuchelewa kutibiwa pale anapojihisi kunaweza kumsababishia muhusika ulemavu wa maisha kwa kukatika pua,vidole ama kuondokewa na kiungo chochote cha mwili.

"Ugonjwa wa ukoma unatibika na hasa ukigundulika mapema ,isitoshe hata Wizara ya Afya sasa inafanya kampeini kwa kutoa tiba ya ukoma bure katika hosipitali ,zahanati na vituo vya afya,kinachotakiwa ni kwenda kupima pale unapojihisi dalili za awali ikiwemo ile ya kuwa na mabaka ya shaba katika sehemu kadhaa za mwili wako,msiogope,ukoma siyo laana wala haulidhishwi,ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine"alisema Bw.Egwaga.

Alisema hivi sasa watu wameanza kupata elimu juu ya ukoma kwani idadi ya waathirika inapungua mwaka hadi mwaka ambapo alisema miaka kumi na tano iliyopita waathirika walikuwa 35,000 ambapo kati yao waliopata ulemavu ni kati ya asilimia 35-40 tofauti na mwaka jana ambapo idadi ya wagonjwa walikuwa ni 5,000 na kati yao asilimia 20 wamepata ulemavu.

Hata hivyo Mratibu huyo alisema kuwa hiyo ni tofauti kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao waathirika wanaongezeka mwaka hadi mwaka na hivyo kuwashauri wale wanaojisikia kukohoa zaidi ya mwezi mmoja kwenda kupima afya zao ili kpata matibabu pale watakapobainika kuathirika na ugonjwa huo wa Kifua Kikuu.

Semina hiyo ya siku moja iliandaliwa na Chama cha Ukoma Tanzania (TLA) kwa kushirikiana na Chama chaWaganga wa Tiba Asilia Tanzania (CHAWATIATA) na kudhaminiwa na Chama Cha Ukoma nchini Ujerumani(GLRA).