Rais Mkapa shuhuda katika ndoa ya Kilaini na Kanisa Na Dalphina Rubyema

RAIS Benjamini Mkapa, ni miongoni mwa wageni waalikwa katika ibada takatifu ya kutoa daraja la Uaskofu kwa Mhashamu Methodius Kilaini leo katika Kituo cha Msimbazi,jijini.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni,Katibu wa Jimbo hilo,Padre Stefano Kaombe, alisema kuwa mbali na Rais Mkapa, wageni wengine watakaohudhuria ibada hiyo ni Mabalozi wa nchi mbalimbali,viongozi wa dini wa madhehebu mbalimabli na wageni wengine kutoka ndani na nje ya nchi.

Mbali na wageni hao,Maaskofu kutoka katika Majimbo yote ya Kanisa Katoliki nchini wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo takatifu.

Akielezea mambo yatakayofanyika katika ibada hiyo itakayoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturjia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC)Padre Julian Kangalawe, alisema kuwa katika ibada hiyo, Mhasham Kilaini, atatakiwa kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa Mwadhama Polycarp Pengo.

Alisema baada ya kujibu maswali hayo ambayo hakuyataja kinaganaga, hatua itakayofuata ni maaskofu wengine kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki kumwekea mikono Mhashamu Kilaini.

Padre Kangalawe, alisema kama zilivyo taratibu za ibada ya kutoa daraja la Uaskofu,baada ya kila Askofu kumwekea mkono Mhashamu Kilaini,itafuata sala ya wakfu itakayofuatiwa na tukio la Mwadhama Kardinali Pengo, kumwekea kichwani mafuta ya Krisma takatifu kama ishara ya kutangazwa rasmi kuwa sasa amekuwa Kuhani Mkuu.

"Unapobatizwa unawekewa mafuta ya krisma juu kidogo ya uso. "Unapopewa daraja la upadre, mafuta hayo yanapakwa mikononi na unapopata daraja la Uaskofu unapakwa mafuta hayo kichwani; na huo ndio mwisho wa mafuta hayo,"alisema Padre Kangalawe.

Alisema wakati Mwadhama, akiwa anaendelea na sala ya misa Mhasham Kilaini,atakuwa amekaa kama watakavyokuwa wamefanya waamini wengine na mashemasi wakiwa wameshika Biblia Takatifu juu ya kichwa cha Mhashamu Kilani.

Alisema hatua itakayofuata ni ya Mwadhama kukabidhi zana za Uaskofu kwa Mhashamu Kilaini, ambazo ni Biblia,pete,kofia kubwa (mitra) na fimbo (bakora).

Akielezea maana ya zana hizo, Padre Kangalawe, alisema kuwa pete ina maana kuwa Mhashamu Kilaini amefunga ndoa na Kanisa; hivyo inamtaka kuwa mwaminifu kama mchumba wa Kanisa.

Kwa upande wa kofia yenye sehemu mbili zinazomaanisha Agano la Kale na Agano Jipya. Utepe unaoziunganisha sehemu hizo ni Kristo katika utimilifu ikiwa na maana ya utimilifu na utakatifu. Askofu anapopewa kofia hiyo ina maana anajitakatifuza na kuwatakatifuza wengine.

Kwa upande wa fimbo (bakora),Padre Kangalawe, alifafanua kuwa fimbo hiyo inaashiria kuwa sasa Mhashamu Kilaini, anakuwa mchungaji wa kondoo ambao ni waamini na anatakiwa kila atakaposhika fimbo hiyo lazima mkwaju wake uangalie kwa watu anaowachunga.

Baada ya hatua zote hizo kufanyika,hatua ya mwisho kabla ya kuhitimisha ibada hiyo itakuwa ni ya Mhashamu Kilaini kupokea mkono wa pongezi kutoka kwa Maaskofu,Mapadre,wazazi na Rais wa nchi.

Januari 8, mwaka huu,kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani,Papa Yohane Paulo wa Pili,alimteua Padre Method Kilaini, kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.Hadi anachaguliwa kushika wadhifa huo,Mhashamu Kilaini alikuwa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) tangu mwaka 1991na angemaliza muda wake Juni, mwaka huu.

 

Marufuku kuhubiri bila kupitia chuoni

Na Getruder Madembwe

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limesema wanaotakiwa kuhubiri Injili katika mikutano yake, ni waliopitia kozi za kichungaji na kiinjilisti na likawatahadharisha waamini dhidi yao kwani wanaweza kupotosha mafundisho.

Tahadhari hiyo ilitolewa kimaandishi hivi karibuni na Askofu Mkuu wa KKKT dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jerry Ngwamba, na kusambazwa katika sharika zake zote ikitaka isomwe kwa Jumapili tatu mfululizo ambapo hii ndiyo ya mwisho.

Ilisema kumekuwa na mikutano mingi inayofanyika sharikani na kuendeshwa na watu ambao hawajapitia mafunzo au kozi zozote za kichungaji au kiinjilisti lakini wanapofika katika sharika hizo na huanza kuhubiri huku wakijiita wachungaji na wainjilisti.

Katika taarifa hiyo, Askofu Ngwamba amewatahadharisha waamini wake kukaa chonjo na watu hao.

Siku hizi kumekuwa na ongezeko la watu wanaojiita maaskofu, wachungaji au wainjilisti katika makanisa na sharika mbalimbali hali hawajapitia katika kozi au mafunzo yoyote ya kichungaji au kiinjilisti.

Waziri Kapuya, akanyaga nyayo za Mzee ‘Ruksa’

Peter Dominic na Josephs Sabinus

WAZIRI wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya, amefuata nyayo za Rais Mstaafu Mwinyi kwa kuichangia shule ya Msingi Tandika ya jijini 200, 000/= ili kusaidia ujenzi wa madarasa pamoja na mipira minne kwa ajili ya michezo.

Profesa Kapuya alitoa mchango huo mwishoni mwa juma alipotembelea shule hiyo kuzungumza na walimu, wazazi na wafadhili juu ya maendeleo ya shule.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, zaidi ya 450,000/= zilichangwa ili kusaidia lengo la shule la kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema wazazi kote nchini hawana budi kushirikiana uongozi wa shule zao kujadili na kuondoa matatizo yaliyo chini ya uwezo wao na akawataka kutokusita kuiomba serikali msaada kwa masuala yaliyo juu ya uwezo wao kama vile upungufu wa walimu na vitabu,

"Mfano, hivi kama mmeungana, mnaweza kushindwa kujenga choo? Kama wazazi hawawezi kufanya hivyo, kuna hatari ya watoto 100 kupanga foleni wakisubiri kuingia chooi kimoja huku mwalimu anaendelea na kipindi darasani."

Alisema na kuongeza, "Hivi katika mazingira kama hayo, mtoto achague lipi,: aende darasani kwanza, au asubiri kwanza foleni huko chooni ?"

Alisema Watanzania hawana budi kuwajengea walimu wa shule za msingi mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba mashuleni kwao na hivyo kuwaondolea adha za usafiri, kuwaondolea vishawishi vya uzinzi na hivyo kuwaongezea ufanisi katika kazi.

Aliwataka walimu kuipenda kazi yao kama walivyo madaktari na wanasheria. "Walimu ipendendeni kazi yenu ndipo hata wenyewe mtataka kujiendeleza. Japan kila mwalimu wa shule ya msingi ni profesa. Kuweni kama madaktari na wana sheria, wanaipenda kazi yao ndiyo maana wanakuwa smati na anaye onekana tofauti wanamwambia, bwana; unaiabisha taaluma yetu," alisema.

Awali akisoma risala ya shule, mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Shule Bi. Mwanahawa Mwailafu, alisema shule yake inakabiriwa na upungufu wa vyumba 27 vya madarasa kati ya 48 na walimu 13 kati ya 63 wanao hitajika.

Alisema kwa ushirikiano, Balozi Isaya Chialo na mama Chialo wameitafutia shule wafadhili toka Japan walioipatia shule madawati 188, viti 192, meza za ofisi na viti 72 na kwamba hivi sasa wazazi wanawalea watoto 8 wa darasa la tano kwa kuwapa mahitaji yao ya shule

Hivi karibuni alipotembelea shule hiyo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliahidi kusaidia matofali ya sh. 200,000 ili kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Saidieni Ombaomba kupitia vikundi - wito

Na Josephs Sabinus

WITO umetolewa kwa wahisani kuwasaidia walemavu na wasiojiweza kupitia vikundi mbali mbali ili kupunguza kasi ya ongezeko la omba omba mijini na hivyo kuwaepusha na adha ya kukamatwa kwa uzururaji na kuwawezesha kusaidiwa kwa pamoja.

Wito huo ulitolewa wiki iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Kapteni John Chiligati alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini.

Alisema ni vema wasamaria wenye moyo wa kuwasaidia walemavu na wasio jiweza, wakatoa misaada yao kupitia taasisi mbali mbali zikiwemo za dini, vituo vya kulelea watoto wa mitaani na vijiji maalumu vya wasiojiweza.

Akitoa mfano, Kapteni Chiligati alisema kijiji (kituo) cha walemavu na wazee wasiojiweza cha Nunge kilichopo Kigamboni katika Wilaya yake ni miongoni mwa vijiji vinavyostahili kusaidiwa na wahisani wenye mapenzi mema kwa kuwa wanaostahili kusaidiwa wapo pamoja hivyo ni rahisi kuwahudumia.

Alisema, "Kama mtu ana wasiwasi kuwa msaada wake utaliwa, anaruhusiwa kusimamia ugawaji wa msaada huo ili uwafikie walengwa. Hii itawafanya hata wale wanaokimbilia mjini kwa makusudi ili kuombaomba ingawa wana uwezo wa kujitegemea, wafanye shughuli zao halali za uzalishaji mali na kujipatia riziki."

Alisema endapo wasamaria wema na wahisani wote watashirikiana vyema na serikali kuzingatia hili, hapatakuwepo na ombaomba na pia walemavu wote na wanaohitaji msaada watasaidiwa kiurahisi na kuepushwa na adha ya kukamatwa wakiomba omba mitaani.

Chiligati amewapiga marufuku ombaombao hao wa kijiji cha Nunge kwenda mjini bila kibali maalumu cha uongozi wa kituo hicho.

"Tabia ya kwenda mjini kujifedhehesha kwa kuombaomba mitaani hali wanajua ni kuvunja sheria, marufuku na ikome. Matatizo yao wayatatue kituoni kwao. Kama ni njaa, waitatue kwa utaratibu wa kisheria. Huwezi kusema eti una njaa; sasa eti ukaibe, au ukaombeombe mitaani, huu ni uvunjaji wa sheria. Waache tabia hiyo maana wakikamatwa watakwenda jela ambako kuna njaa na shida zaidi ya hiyo".

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Luten Yusufu Makamba alianzisha operesheni maalumu inayoendelea hadi sasa ya kuwakamata ombaomba na makahaba ili kuwaondoa jijini wakatumie nguvu kazi zao kujiendeshea maisha vijijini kwao.

WAKATI HUOHUO:Hivi karibuni alipokuwa akikabidhi msaada wa vyerehani viwili kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Walemavu Bw. Resmo Ekalapa mbele ya wanakijiji wengine, uliotolewa na Jamii ya Wayemeni waishio Dar es Salaam (Dar es Salaam Yemen Community), Mkuu huyo wa wilaya alitahadharisha,

"Msiwe kama klabu za mpira, zikipewa zawadi au msaada, wanaanza kugombania, pangeni wenyewe namna bora ya kuzitumia na kuzitunza kwa manufaa yenu na popote mnapokwama waoneni viongozi maana serikali ya CCM iko tayari kuwasikiliza wananchi wote wakati wowote".

 

Ishini kama watawa wa Kiafrika- RWSAT

Na Waandishi Wetu

CHOMBO kinachoyaunganisha mashirika ya watawa wa kike nchini Tanzania (RWSAT), kimesema, hali ya masista kutegemea misaada ya wamisionari ili kufanya kazi za kitume imepitwa na wakati na sasa ni wakati wao kujua na kuishi kama watawa wa Kiafrika wakijitegemea katika kupata mahitaji ya lazima na kuwasaidia wengine.

Akizungumza katika warsha ya wiki mbili ya menejimenti kwa ajili ya masista wanao simamia miradi katika mashirika yao, Katibu Mkuu wa RWSAT, Sista Fides Mahunja, alisema, masista wote wenye kiu ya kujitegemea, hawana budi kujua kuwa, kutegema misaada ya Wamisionari ili kufanya kazi ya Mungu kumepitwa na wakati na hivyo masista hawana budi katika mashirika yao, kubuni na kuendesha miradi ya uzalishaji ili waweze kufanya kazi zao za kitume.

Katika warsha hiyo inayofanyika katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar Es Salaam, Sista Mahunja , alisema, "Wamisionari waliokuwepo, walianzisha mashirika yetu na kutusaidia ili tuweze kufanya kazi za kitume kadri ya karama za mashirika yetu. Wakati ule ulikuwa mzuri, hatukuwa na wasiwasi wa chakula, malazi wala nguo...lakini siku hizo nzuri zimepita na sasa tunatafuta namna ya kuishi kama watawa wa Kiafrika."

Alisema na kuongeza, "Tujitegemee ili tusikose mahitaji yetu ya lazima na pia ili tuwe na kitu cha kuwasaidia wengine."

Alisema masista wa RWSAT hawana budi kujiunga na wanawake na jamii nyingine duniani ili kujikwamua na tazito la kuwa wategemezi kwa kubuni na kuanzisha miradi na vitega uchumi mbalimbali, kuisimamia na kuitathmini ili izae matunda bora.

Katika warsha hiyo inayofadhiliwa na shirika la CORTAFRICA, Sista Mahunja alisema, Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Wanawake ifikapo machi 8, kila mwaka na kuwaelekeza wanachama wake kutoa kipaumbele katika kumwendeleza wanawake sawa na mwanaume hivyo ni vema wanawake walio wengi katika jamii, hawana budi kutambua umuhimu na nafasi yao kubwa katika kuiongoza jamii na kwamba kuwa ni jukumu lao kujiwekea mikakati ya kujikomboa.

Katika ufunguzi wake, Mkurugenzi wa Senta ya Msimbazi, Padre Benedikt Shayo, aliwatahadharisha washiriki wa warsha hiyo kuwa makini, wakweli na wawazi katika masuala ya pesa wanapoomba misaada kwa wafadhili na pia kuitumia kwa malengo yaliyo kusudiwa.

""Tunapoomba miradi tuwe wazi kwa wafadhili maana wangependa kuona fedha wanazotoa zinatumika kwa lengo lililokusudiwa. Jueni kuwa kinachoharibu heshima ya mtu yeyote wa miradi, ni fedha.... Pesa inaweza kukujengea urafiki na pesa inaweza kukujengea uadui", alitahadharisha.

 

Wananchi walia na ‘mipasho’

lWasema ina matusi mno hasa ‘Mtu mzima hovyo’

Na Neema Dawson

Wananchi wameiomba serikali kuviunga mkono vikundi vya dini kukemea vikali nyimbo zinazotumia lugha ya matusi maarufu kama Mipasho ili kuinusu jamii katika maangamizo ya kimaadili.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti jijini hivi karibuni, baadhi ya wananchi jijini Dar Es Salaam, wamesema wanashangaa kuona serikali ina kaa kimya na kuwafumbia machobaadhi ya wasanii wnaoimba nyimbo zenye "matusi ya nguoni" na kwamba hiyo ni sawa na kuridhika na mmomonyoko wa maadili kuwepo nchini.

Bw. Omary Abdalah, mkazi wa Temeke alisema, "Hizi nyimbo wanazoita eti ‘mipasho’, hazijengi hata kidogo maadili ya Watanzania, ila yanazidi kuyabomoa tu. Hii pia ni kutokana na hizo nyimbo

za taarabu kuwa na ujumbe mchafu, lakini hazikemewi na mtu"

Bw. Omary aliendelea kuwa licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wa dini katika kuona jamii inakuwa katika misingi ya maadili kwa kufichua maovu na kufichua penye uozo, bado serikali na jamii haiviungi mkono na badala yake hata vyombo vya habari kama redio na television zinazipa nafasi nyimbo hizo.

"Kuna wasanii wengine wakitunga nyimbo zinazomgusa mtu mmoja serikali inawakatalia kutoa Albam zao lakini iweje watu wengine kwa vile wako karibu na viongozi wa Serikali ndiyo waruhusiwe kuimba nyimbo za matusi na zilizo na kashfa nzito ndani yake mfano halisi ni zile nyimbo zinazovuma za ‘mtu mzima hovyo’ usishangae kila stesheni ya redio inayofungua, lazima ukutane na nyimbo hizo zinazoharibu watoto na kuwafanya kakue katika hali ya kimatusitusi."

Naye Bi. Eliza Magesa, mkazi wa Ubungo-Kibo alisema kuwa Serikali inatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha ni vyanzo gani na vitu gani vinavyochangia kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili.

Alisema ingawa zipo njia ambazo zinatumiwa bila mafanikio, hali hiyo inatokana na kutokujua wala kudhibiti vyanzo vya ongezeko la mmomonyoko huo.

WAWATA ‘wawapiga jeki’ Walei

Na Dalphina Rubyema

UMOJA wa Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA),ngazi ya taifa, umetoa jumla ya shilingi 52,600/=,kama mchango wake katika kusaidia ujenzi wa Kituo cha Baraza la Walei Taifa cha Bakanja jijini Dar Es Salaam.

Akikabidhi mchango huo uliotolewa papo kwa papo na WAWATA walipotembelea kituo hicho hivi karibuni maeneo ya Sitakishari Ukonga jijini kwa Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Walei Taifa, Bibi Mary Mwingira, Mwenyekiti wa WAWATA Taifa, Bibi Oliva Luena alisema WAWATA kama nguzo muhimu katika Taifa, haitachoka kusaidia popote pale panapofanyika kazi ya Kanisa.

WAWATA ambao waliokuwa katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Miito Mbagala hivi karibuni, walionelea kutembelea kituo cha Bakanja kabla wajumbe waliohudhuria mkutano huo hawajarejea katika majimbo yao ili kujionea hali yake halisi.

Awali katika mazungumzo yake na gazeti hili, Mkurugenzi wa Baraza la Walei Taifa Padre Nicholaus Segeja, alisema ili ujenzi wa Bakanja ukamilike, kila muumini anatakiwa kujitoa kwa moyo wake kuchangia jumla ya shilingi 500/=.

Padre Segeja ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema hadi hivi sasa vifaa kwa ajili ujenzi huo tayari vimeisha nunuliwa na kilichobaki ni kukamilisha ujenzi ambao tayari umeisha anza.

WAKATI HUO HUO: Katibu Mtendaji wa Halmashauri ya Walei Taifa, Bw.Emil Hagamu alisema kuwa tayari baadhi ya ofisi za vyama vya kitume ngazi ya Taifa zimeisha hamia katika Kituo hicho kipya cha Bakanja na akavitaja vyama hivyo kuwa ni Regio Maria, Wanaume Wakatoliki na Viwawa.

Wanaoambukiza ukimwi kupelekwa Polisi?

Na Dalphina Rubyema

KATIKA kupunguza kasi ya maambukizo ya ugonjwa hatari wa Ukimwi, Mpango wa Taifa kudhibiti UKIMWI (NACP), inatarajia kuanza kutoa taarifa Polisi ili kuwachukulia hatua za kisheria wanao bainika kusambaza na kuwaambukiza wasio athirika kwa makusudi mara tu muswada utapopitishwa.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Meneja wa wa NACP, Dk. Roland Swai wakati akijibu swali la Mwenyekiti wa Idara ya Afya katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Aloysius Balina wakati wa semina ya ukimwi iliyowashirikisha makatibu wa Idara TEC na wajumbe wa Kamati ya ushauri kutoka majimbo mbalimbali.

Mhashamu Balina ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, alitaka kujua kuwa ni kwanini madaktari na watumishi wa afya hawawi wazi na wakweli katika kutoa majibu kwa watu wanao pimwa na kubainika kuwa wana virusi vya ugonjwa wa ukimwi hali inayosababisha wengi wao kuhamia kwa waganga wa kienyeji huku wengine wakizidi kueneza ugonjwa huo bila kujua kuwa wanawathiri wenzao kwa kuwa waliisha athirika.

Aidha, Askofu huyo wa Shinyanga alitaka kujua Programu hiyo ya kudhibiti ukimwi ina mpango gani wa kuwabana watu wanao wafanyia wengine maambukizo ya ukimwi kwa makusudi huku wakijua kabisa kuwa wanafanya makosa.

Dk. Swai katika majibu yake, pia aliitaka jamii kuelewa kuwa siku hizi mtu anapopimwa damu, anatakiwa akubali majibu yatayotoka na endapo atabainika kuwa ana ukimwi, basi ni vema awe Mungwana, mcha Mungu, mwenye upendo na mvumilivu ili asiwaambukiza wengine.

Alisema kuwa hivi sasa Kitengo hicho cha Taifa imeandaa muswada unaosema kuwa endapo mtu mwenye virus vya ukimwi atabainika anawambukiza wengine ugonjwa huo kwa makusudi, atashitakiwa Polisi na endapo muswada huo utakubalika, utaanza kutumika mara moja.

Alisema sera hiyo haiwezi kuanza sasa hivi kwa vile bado haijaruhusiwa na serikali na kwamba wao kuitumia bila kuruhusiwa ni kuvunja maadili ya fani yao ya udaktari.

Mbali na sera hiyo kutumika, vile vile endapo itabainika kuwa mchumba mmoja ameathirika na mwenzake bado lakini kwa makusudi huyo mwathirika anataka kumwathili mwenzake, madaktari na watu wa afya watamjulisha ambaye hajaathirika.

"Hivi sasa maadili yetu yanatukataza kuitaarifu Polisi ama wachumba juu ya suala hili lakini sera hii ikishapitishwa tutakuwa tukifanya hivyo ili kuinusuru jamii"alisema Dk.Swai.

Semina hiyo ya siku mbili iliandaliwa na Idara ya Afya katika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Jamii imekuwa ikiwalaumu madaktari kwa kuacha kuwaambia ukweli wagonjwa wa ukimwi wanpopimwa na badala yake wanwaambia kuwa vipimo vyao havioneshi chochote.

Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa wananchi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji na hivyo kujihusisha na imani za kishirikina na mauaji yasiyo ya lazima pamoja na chuki baina ya watu. Pia imechangia kuongezeka kwa maambukizo kutokana na waathirika na jamii kuamimi kuwa ugonjwa umetokana na kurogwa badala ya ukweli kuwa ni ukimwi hali inaypo punguza umakini katika kujihadhari.

Wanaowauzia wanafunzi pombe baani, kukiona cha moto

SERIKALI wilayani Temeke imewakemea vikali wanao wauzia vileo wanafunzi katika baa zao licha ya kuvaa sare za shule na imesema watakao bainika watachukuliwa hatua kali za kisheria; wanaripoti waandishi wetu Josephs Sabinus na Elizabeth Steven.

Akijibu swali la waandishi waliotaka kujua serikali wilayani kwake ina mpango gani wa kukomesha kasi ya mmomonyoko wa maadili ya jamii unaopelekea wanafunzi kunywa vileo baani licha ya kuvaa sare za shule, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Kapteni John Chiligati, alisema serikali wilayani kwake haitavumilia hali hii ya utovu wa maadili ambayo pia inachangiwa na uchu wa pesa wa wafanyabiashara ya baa.

Alisema watakaobainika kuwauzia wanafunzi pombe baani, wote kwa pamoja watachukuliwa hatua za kisheria, kinidhamu na kimaadili kwa mujibu wa taratibu.

"Wenye baa watakaoruhusu vileo kwa watoto wa shule huku kwa macho yao wanaona na wanajua kabisa kuwa wale ni watoto wa shule, watachukuliwa hatua za kisheria. Kama ni uchu au hiyo tamaa ya pesa, zitawatokea puani.Kumnywesha mtoto wa shule chini ya miaka 16, ni kosa la kisheria. Na hata hao wenye zaid ya 16, ni kosa la kimaadili." Alisema Kapten Chiligati.

Ingawa alisema hakujua hali hiyo, Chiligati alisema atapambana nayona akasisitiza kuwa suala la kulinda maadili ya Kitanzania ni jukumu la jamii nzima wakiwemo wanafunzi na wenye baa hivyo kuwauzia vileo wanafunzi, ni kukiuka kwa makususdi jukumu hilo.

"Hawa wauza baa na hata wateja wengine sijui wanajisikiaje kuwaona baani watoto wa shule wakilewalewa! Huu ndio mwanzo wa kushawishika na hivi vichips-chips na mwishoni wanaambulia mimba na ukimwi," alisema.

Jijini Dar Es Salaam, umekuwapo mtindo wa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutoroka vipindi na kwenda baani kunywa pombe huku wengine wakidanganyia kunywa soda. Wafanyabiashara nao wamekuwa wakiwapa ushirikiano kwa kusem, "Mteja ni mfalme."