Wasiotaka kusali na Wanawake msikitini mbaroni

lWasema ni nuksi kusali nao msikiti mmoja

Na George Ramadhani PST, Dodoma

POLISI mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki waliwatia mbaroni watu watatu kufuatia ghasia zilizozuka hivi karibuni katika msikiti mmoja mjini hapa.

Waislamu hao wanaoamini kuwa ni haramu wanawake kusali msikitini, bali majumbani, walitaka kuvunja ukuta unaotengenisha wanawake na wanaume msikitini hapo ili asiwepo mwanamke atakayethubutu kusali msikitini hapo.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Bw. Rashid Hemed, amethibitisha kukamatwa kwa baadhi ya watu hao ambao wanatuhumiwa kutaka kuvunja msikiti huo wa Majengo.

Waliokamatwa kwa mujibu wa Kamanda Hemed, ni Bw. Ayoub Chadai (30), Adam Shomari (43) na Khalfan Nungu, maarufu kama "Supa Maridadi."

Hata hivyo imeelezwa kuwa baada ya kushikiliwa kwa saa 24 na kuhojiwa kwa kirefu na Polisi walichiwa huru kwa masharti kuwa wasijihusishe kwa namna yoyote na shughuli za msikiti huo.

Watuhumiwa hao wameonywa na Polisi kwamba endapo watashindwa kutii masharti hayo watakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuvuruga amani.

Mwenyekiti wa Msikiti wa MajengoSheikh Juma Sadiki, aliiambia PST mwishoni mwa wiki kuwa mgogoro msikitini hapo ulianza muda mrefu lakini wiki iliyopita ndipo ulipamba moto na kusababisha ghasia zilizotishia kuchafuka kwa amani.

Sheikh Saidiki amesema kuwa gia waliyoingia nayo vijana hao kutaka kubomoa msikiti ni kwamba sehemu ambayo wanaume wanasalia ni finyu mno kiasi cha kuwalazimu baadhi yao kusali nje na hivyo ufumbuzi wake ni kuwaondoa akina mama kwa vile hawastahili kusali misikitini.

Alisema kuwa kundi dogo la waumini wakiongozwa na vijana hao watatu baada ya Sala ya Alasiri Jumapili Februari 27, walitaka kuvunja ukuta unaowatenga wanawake na wanaume kwa madai kuwa Sheria ya Kiislamu inawataka wanawake wasalie nyumbani hivyo ni nuksi kusali nao katika mazingira kama hayo.

Alisema kuwa kundi dogo la waumini wakiongozwa na vijana hao watatu baada ya Sala ya Alasiri Jumapili Februari 27, walitaka kuvunja ukuta unaowatenga wanawake na wanaume kwa madai kuwa Sheria ya Kiislamu inawataka wanawake wasalie nyumbani.

Alisema kuwa kundi dogo la waumini wakiongozwa na vijana hao watatu baada ya Sala ya Alasiri Jumapili Februari 27, walitaka kuvunja ukuta unaowatenga wanawake na wanaume kwa madai kuwa Sheria ya Kiislamu inawataka wanawake wasalie nyumbani.

"Sisi kama viongozi wa msitikiti tuliwashauri kwamba kama nia yao ni kupanua msikiti wabomoe ukuta wa nje na waupanue kuelekea nje na sio kubomoa sehemu wanayostahili kusalia wanawake," alisema Sheikh Sadiki na kuongeza kuwa wamewataka vijana hao kama hawataki wanawake wasalie hapo basi wajenge msikiti wao.

Bakwata, Makanisa wampinga Waziri Nagu, Kuleana

lKuleana wadai aya za Biblia, Koran zimepitwa na wakati

Na Dalphina Rubyema

WAISLAMU na Wakristo nchini, kwa pamoja wameungana kupinga kampeni iliyozinduliwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake na Watoto, Bi. Mary Nagu na shirika lisilo la Kiserikali la Kuleana ya kutaka adhabu ya viboko kwa watoto majumbani na shuleni ipigwe marufuku kisheria.

Kampeni hizo zilizozinduliwa hivi karibuni ambapo Waziri Nagu, aliziunga mkono kwa kuvunja fimbo hadharani kama ishara ya kuonyesha kuwa adhabu ya fimbo kwa watoto haifai, pia ziliwahusisha Sheikh mmoja na Mchungaji ambao walidai kuwa vitabu vya dini zao haviagizi watoto wachapwe.

Mkurugenzi wa Idara ya Dini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Hassan Chisenga, alipohojiwa juu ya suala hilo mwishoni mwa wiki alisema si kweli kwamba kitabu cha Kiislamu (Korani) kinakataza watoto wasichapwe bali kinaagiza wachapwe ili kuwaadabisha na kuwaokoa na Jehanamu (kama Biblia nayo inavyosema).

Alisema kuwa katika mafunzo ya Mtume Mohamad S.A.W amesema "Waamrisheni watoto wenu kuswali wafikiapo miaka saba na wapigeni kwa kuipuuza..."

Alisema kuondoa adhabu ya viboko ambayo iliwekwa kwa nia ya kurekebisha tabia za watoto kwa sababu tu wapo wanaoitumia sheria hiyo vibaya ni sawa na kuondoa dawa ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya kutibu magonjwa kama malaria kwa hoja kuwa wako wanaozitumia kujiua.

Sheikh Chisenga alisema kwa maamrisho haya na kwa kutumia misingi ya QIYAS inajuzu mtoto kumwadhibu kwa kuchapwa kwa nia ya kurekebisha tabia yake.

Alisema mzazi anapofuata amri ya Koran kwa kuchapa mwanawe ni moja ya utekelezaji wa haki ya mtoto kwani mtoto ambaye hakulelewa kwa njia hiyo atakuja kumlaumu mzazi wake siku ya hukumu mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa hakuchukua hatua za kumjenga kiimani ndio maana akawa muovu na hadi kustahiki adhabu.

"Ni bora sheria hii ya kuwa mtoto asipigwe ikaangaliwa imeacha athari gani katika nchi ambazo imetumika; hali ya huko ni mbaya sana. Hivi sasa mauaji yanafanywa na watoto wadogo, yote haya yakiwa ni matunda ya sheria hiyo potofu, " alisema Sheikh Chisenga.

Alisema badala ya kuondoa sheria hii ya viboko ni bora wangetumia busara ya kuwachukulia hatua wale wanaoitumia vibaya adhabu ya viboko.

Katibu Mtendaji wa Idara ya Litrujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Padre Julian Kangarawe alipohojiwa juu ya suala hilo alisema kuwa kumkataza mzazi asimchape fimbo mtoto wake ni malezi bandia kwani wajibu wa mzazi ni kumpenda mtoto wake kwa kumpa ushauri na kumkosoa pale anapokosa ikiwa ni pamoja na kumchapa fimbo pale inapobidi.

Alisema Taifa halina budi kulichunguza kwa kina suala hili na siyo kulichukulia tu kijuujuu kwani linaweza kuleta madhara makubwa siku za baadaye.

"Inawezekana kuna NGOs ( taasisi zisizo za kiserikali) zinazotumiwa na mataifa ya nje kuvunja maadili ya taifa letu. Hili suala la kuondoa sheria ya kumpiga mtoto ni neno jema, lakini lina sumu ndani yake" alisema.

Kuhusu lile la kusema kuwa Bibilia haikuandikwa chochote juu ya fimbo kwa mtoto,Padre Kangarawe alisema kuwa hapa waigizaji waliichukulia vibaya Biblia kwani katika kitabu hicho kitakatifu inaonyesha bayana kuwa mtoto lazima aadhibiwe kwa fimbo.

Aliinukuu Biblia Takatifu (Mithali 13:24) ambayo inasema "Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanae" na kuongeza kuwa katika kitabu hicho hicho cha Nabii Suleiman aliyeshuhudiwa na Mungu mwenyewe kuwa mwenye hekima sura ya 23:13-14 kuna maneno yasemayo, "Usimunyime mtoto wako mapigo maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa,utampiga kwa fimbo na kumuokoa nafisi yake kuzimu".

Msaidizi wa Askofu wa KKKT,Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Adam Kombo, alisema kuwa fimbo ni dawa iliyo bora zaidi ya kuadabisha watoto ambayo ilikuwepo tangu zamani na inajenga maadili mema kwa mtoto endapo itatumiwa vizuri; hivyo kuiondoa inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii na hata laana.

"Sisi zamani tulikuwa tukichapwa; na fimbo zilitufanya tutii,tulijua fika kwamba tukifanya kosa tutachapwa,"alisema.

Kwa upande wa Biblia, Mchungaji Kombo hakuwa tofauti na Padre Julian Kangarawe ila yeye aliongeza kipengele kingine cha Biblia ambacho ni Mithali 22:15 kisemacho ‘Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto lakini fimbo ya adhabuitaufukuzia mbali’.

Walifanya vibaya (KULEANA) kusema kuwa katika Biblia haikuandikwa kuwa mtoto lazima aadhhibiwe kwa fimbo,"alisema Mchungaji Kombo.

Mwakilishi wa KULEANA, Bw.Peter Mwangose, alipohojiwa juu ya upotoshaji wa Biblia na Korani alisema kuwa wakati wa uigizaji wahusika hawakuwa na muda wa kutosha kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sula hilo.

"Haukuwepo muda wa kutosha kutoa ufafanuzi lakini Sheikh Fereje kutoka Mwanza na Mchungaji Macha wa Arusha ambao walijibu swali hili katika Igizo hilo nina imani kuwa wanaelewa fika nini kimendikwa kwenye Korani na Biblia kuhusiana na haki za mtoto ila sema tu hawakuwa na muda wa kutosha kulitolea ufafanuzi,"alisema.

Hata hivyo Mwakilishi huyo wa KULEANA alisisitiza kuwa hata kama imendikwa kwenye Biblia na Korani kuwa mtoto lazima aadhibiwe kwa fimbo, suala hilo halina budi kuangaliwa kwani vitabu hivyo vitakatifu vina baadhi ya mambo yaliyopitwa na wakati likiwemo hilo la viboko.

Wakimbizi 3000 wa Kisomali wajaa Handeni, 15 kila wiki

Na.Thobias Mwanakatwe. PST-Handeni.

Wakimbizi wapatao 3466 wakitokea nchini somalia wameingia katika kitongoji cha Mkuyu kilichopo kijiji cha Mafuleta, Handeni mkoani Tanga hadi kufikia Septemba mwaka jana.

Mkuu wa makazi wa Kambi ya wakimbizi Bw.Cyril Msofe alitoa taarifa hiyo hivi karibuni kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi.Halima Hatibu, ambaye yupo ziarani wilayani hapa kutembelea shughuli za maendeleo na miradi ya wanawake duniani ambazo kitaifa zilifanyika mkoani Tanga.

Bw.Msofe alitoa mchanganuo kuwa wakimbizi hao walianza kuingia kitongojini hapo tangu mwaka 1992 na kwamba kati ya idadi hiyo wanawake ni 777 wanaume 465 na watoto 2224.

Amesema sababu ya Wasomalia hao kukimbia makazi yao nchini Somalia kulitokana na machafuko pamoja na vita inayoendelea nchini humo ya kugombea madaraka nchini.

Aliendelea kutoa taarifa kuwa wakimbizi hao ambao wanahudumiwa na Shirika la Misaada kwa Wakimbizi bado wanaendelea kumiminika kitongojini hapo kwani kila wiki zaidi ya wakimbizi 15 toka Somalia huwasili.

Mkuu huyo wa kambi alisema kwamba idadi hiyo huenda imeongezeka kwa kuwa sensa ya mwaka 1997 ndiyo inayoeleza takwimu hizo.

Akizungumza baada ya taarifa hiyo, mkuu huyo wa wilaya Bi Hatibu aliwataka wakimbizi hao kudumisha umoja,upendo amani ili waweze kuishi kwa kipindi kirefu hapa Tanzania, badala ya kujihusisha na vitendo viovu kama ujambazi.

 

Wachungaji wapigwa marufuku Kanisani

Na Mwandishi Wetu, Mwanga.

MCHUNGAJI Abrahamu Mshana na Mwinjilisti Sadikieli Mika wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) ambao ni miongoni mwa wanaoshinikiza kugawanyika kwa dayosisi ya Pare wameshindwa kuendesha ibada baada ya kuzuiliwa kufika kanisani huku wakikabiliwa na kesi.

Habari zilizopatikana mjini hapa zinasema viongozi hao wamepigwa marufuku kujihusisha na masuala ya kanisa kwa vile wanakabiliwa na kesi kadhaa za jinai ikiwa ni pamoja na kuvuruga ibada Februari 20,mwaka huu katika Usharika wa Kifula, iliyokuwa ikiendeshwa na Mchungaji wa Usharika huo Aminiel Ndoveni.

Zinasema kufuatia viongozi hao kutokuonekana kanisani Februari 27, mwaka huu wafuasi wao walivamia ibada ya wale watiifu kwa Dayosisi halali ya Pare ambapo kijana mmoja maarufu kwa jina la Kanyoka, alipopenya kwenye mlango wa ofisi waliokuwa wakivalia wachungaji kabla ya kutiwa nguvuni.

Hata hivyo baada ya ibada ya siku hiyo Mchungaji Dk. Mtaita, ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya Kikristo wa Dayosisi ya Pare, alisema kwa mujibu wa tamko la Mkuu wa Kanisa (Askofu Mkuu KKKT) ni ndoto kuwa na dayosisi ya Mwanga wala Serikali haiwezi kulilazimisha Kanisa kuiunda na akawataka waasi kurudi watubu na kuketi pamoja na wenzao kwa upendo.

Alisema KKKT kamwe haitaruhusu ibada mbili tofauti katika eneo lake lolote isipokuwa zile zinazoongozwa kwa utaratibu muafaka wa kanisa hilo.

Habari zaidi zinasema baadhi ya waasi wa Dayosisi ya Pare wameanza kujirudi lakini wanashindwa namna ya kuwarudia wenzao ili wasali pamoja kutokana na hofu.

Mgogoro wa dayosisi ya Pare unatokana na kikundi kidogo cha waumini wa KKKT katika wilaya ya Mwanga, ambao kwa sababu za ukabila, siasa na kisiasa wanataka wawe na Dayosisi yao wenyewe licha ya katiba ya Kanisa hilo kutoruhusu mahali penye makanisa machache kama Mwanga kuunda dayosisi.

Uongozi wa KKKT pia unataka hata kama ungekuwepo uwezekano wa kuundwa kwa dayosisi hiyo utaratibu wa vikao vya kikatiba ufuatwe, tofauti na sasa ambapo ubabe, uhalifu na kiburi vinatumika kudai dayosisi hiyo.

Mzee 'Ruksa' adaiwa na shule

Elizabeth Steven na Josephs Sabinus

SHULE ya msingi Tandika wilayani Temeke mkoani Dar Es Salaam, inamdai shule ya sekondari ya Kutwa, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, kufuatia ahadi aliyoitoa kuwa pindi watakapokamilisha ujenzi wa uzio, maji na umeme atawasaidia kuijenga.

Katika risala ya shule kwa Rais huyo Mstaafu iliyosomwa na Mwalimu Mkuu wa shule ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya shule, Bi. Mwanahawa Mwailafu, shule imemuomba Mwinyi atimize ahadi aliyowahi kuitoa shuleni hapo kuwa endapo watakamilisha ujenzi wa uzio wa shule, maji na umeme, atawasaidia kujenga shule ya sekondari ya kutwa.

"Tunakukumbusha ulituahidi kuwa tukikamilisha uzio, maji na umeme, utatusaidia kujenga shule ya sekondari ya kutwa. Sasa ni wakati muafaka," alisema Bi. Mwailafu.

Akijibu risala hiyo, Mwinyi ambaye ni mlezi wa shule hiyo alisema ni vema walimu, wazazi na wafadhili wakaelekeza kwanza juhudi zao katika kupambana na tatizo la upungufu wa madarasa ili wanafunzi wakabiliane vema na masomo ili wajiunge na sekondari wakiwa wameiva kitaaluma.

"Kufundisha watoto wafahamu, waondoke werevu ni 30, wasizidi 40. Wakizidi 40, watakuwa hawaelewi lakini wanahudhuria...Tukazane kwenye madarasa, kila mtu kwa upande wake," alisema na kuongeza,

"Mimi nitasaidia matofali ya shilingi laki mbili; wahisani na hata walimu , mjipigepige ingawa nafahamu mshahara wenu ni kama mkia wa mbuzi."

Awali katika risala, Bi. Mwailafu alisema shule hiyo yenye watoto 2325, ina upungufu wa vyumba 27 kati ya 48 vya madarasa vinavyohitajika na kwamba upungufu huo unaathiri kwa kiasi kikubwa maaendeleo ya taaluma.

Mwinyi aliyetembelea shule hiyo kuona maendeleo katikati ya juma, ameupongeza uongozi wa shule kwa kukamilisha ujenzi wa uzio wa shule hiyo ambao yeye mwenyewe aliuchangia vifaa vyenye thamani ya shilingi 1.8m/=

Katika ziara hiyo ambayo Mwenyekiti wa kamati ya shule Bi. Joyce Mhando, aliahidi kuchapa kazi ili kuuonesha umma kuwa hata wanawake wana uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi, Mwinyi aliahidi kutoa miche ya michungwa na miembe kwa ajili ya kivuli, matunda na kufundishia katika bustani ya shule.

"Tunapanda miti ya matunda ili kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Wapate kivuli; haya mambo ya mazingira, wapate matunda na faida ya tatu, wapate kusoma juu ya miti ya matunda," alisema.

Walei wote nchini watakiwa kuchanga 500/=

Na Mwandishi Wetu

ILI kukamilisha ujenzi wa kituo cha Baraza la Walei ngazi ya Taifa cha Bakanja kinachojengwa katika eneo la Sitakishari -Ukonga jijini kila Mkatoliki ametakiwa kutoa kiasi cha shilingi 500.

Katika mkutano maalum uliondaliwa na Halmashauri ya walei Taifa kwa kushirikiana na ofisi ya Idara ya Baraza la Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) uliofanyika katika eneo la Sitakishari ambako kituo hicho kinajengwa, ilijadiliwa kuwa endapo mchango huo kutoka kwa waumini utapatikana mara moja shughuli za kumalizia ujenzi huo hazina budi kukamilishwa haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa Bibi Mary Mwingira, na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw.Emil Hagamu,ujenzi uliobaki ili kukamilisha kituo hicho ni pamoja na ukumbi wa mikutano, ukumbi wa chakula, mabweni na chapel(Kanisa)ambapo walisema kuwa vifaa vyote vipo ila kikachosubiriwa ni pesa ya kuanza ujenzi.

Awali akifungua mkutano huo uliowajumuisha viongozi wa Halmashauri ya Walei Majimboni, Katibu Mtendaji wa Baraza la Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Nicholaus Segeja alisema kuwa waamini hawana budi kutoa mchango wao wa hali na mali ili kuweza kutimiza lengo la ukamilishaji wa ujenzi huo ambao ni ndoto ya muda mrefu.

Pamoja na kwamba ujenzi wa kituo kushindwa kukamilika hatua kubwa imepigwa kwani ofisi mbalimbali za vyama vya kitume tayari zimekwisha malizika na vyama hivyo tayari vimekwisha hamia huko ikiwa ni moja ya uhamasishaji wa ujenzi huo.

Vyama vilivyohamia huko tangia Februari 18, mwaka huu ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Wanaume Wakatoliki, vijana Wakatoliki (VIWAWA),Legio Maria na Halmashauri ya Walei yenyewe ambapo WAWATA na Chama cha Wenye Taaluma (CPT) navyo viko mbioni kwani ofisi zao tayari zimekamilika.

Mbali na kuzungumzia suala la Bakanja, mkutano huo wa siku mbili pia uliratibu shughuli zote za sherehe za kikanisa zitakazofanywa katika mwaka huu mtakatifu wa Jubilei Kuu.

Vijana Wakristo watakiwa wasichague wanasiasa kwa kuburuzwa

Na Getruder Madembwe

WAKATI tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu, vijana nchini wametakiwa kutumia utashi wao wenyewe kuwachagua viongozi wanaofaa badala ya kungoejea kushawishiwa na watu wengine kwa udanganyifu au rushwa.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa VIWAWA wa Parokia ya Mburahati, Mendolla Sisinga, katika maadhimisho ya Jubilei ya vijana yaliyofanyika hivi karibuni Parokiani hapo katika ukumbi wa Mtakatifu Thomasi.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa katika adhimisho hili la Jubilei Kuu vijana wanatakiwa wazingatie mambo muhimu kwani wana jukumu la kuilinda amani ya nchi hii ili isipotee na wawe msimamo mzuri katika mambo ya uchaguzi.

"Tunaeleka Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo basi katika adhimisho hili tunataka vijana watambue haki yao ya kupiga kura bila ya kulazimishwa na mtu yeyote wachague mtu asiyefaa," alisema.

Naye Katibu wa VIWAWA wa Parokia hiyo alisema kuwa nia ya adhimisho hilo la Tamasha la Jubilei ni pamoja na uhamasishaji kwa vijana katika suala la amani, kwani wao hawana budi kuilinda amani iliyopo isiharibiwe na mtu au kikundi chochote.

Tamasha hilo liliishirikisha mitaa 18 ya Parokia hiyo ni ambayo ni Kilimahewa,Luhanga B,NHC,Makuburi B,Minyonyoni Mabibo A, Kwajongo na Makutano.

Fani zilizohusishwa ni za Maigizo,ngoma,kwaya pamoja na Jiving na mtaa wa Makutano uliibuka kuwa mshindi kwa fani zote. Sambamba na tukio hilo pia kulipandwa mti wa milenia kwa ajili ya kumbukumbu ya adhimisho hilo ambao ulipandwa na Kaimu Paroko wa Parokia hiyo Padri Geogre Sayi ambaye yuko katika parokia ya Chan’gombe.

Makanisa yatumike kwa ibada si kwa kutafutia umaarufu - Pengo

lUlaya wana majengo ya kanisa lakini hayana watu, mengine wamewapa Waislamu

Na Neema Dawson

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ametoa changamoto wa waamini kuyatumia makanisa waliyonayo na wanayoyajenga kwa dhati na kwa madhumuni ya kufanyia ibada na si kujipitia umaarufu.

Askofu Pengo aliyayesema hayo wakati alipokuwa akifungua na kubariki kigango cha Mavurunza ambacho kimefanywa kuwa parokia ya Mavurunza ambayo ilianzishwa ikiwa kama kigango kilichoanzishwa kutoka katika parokia ya Ubungo Msewe.

Alisema kuwa kuna nchi nyingine zilizoendelea kama Ulaya ya Magharibi ambazo zina majengo ya hadhi ya makanisa lakini hawana waamini Wakristo wanaoasali na kuyatumia makanisa hayo hivyo maaskofu wa nchi hizo hulazimika kuwapa Waislamu ili wayatumie wao, hali ambayo Wakristo wa nchi hizo wanapoona hapa nchini Tanzania zinaongezwa juhudi za kujenga makanisa inayowashangaza.

Pia alisisitiza kuwa waamini wanatakiwa kutoweka thamani ya maisha kwenye vitu vya kidunia na kuweka kanisa pembeni.

Alisema makanisa yanajengwa ili yatumike kwa sala na si kwamba yatumiwe wakati wa kufunga ndoa, ubatizo, Sakramenti za Kipaimara, Komunio na Krismasi. Aliongeza kusema kwamba wapo baadhi ya Wakristo ambao huyaasi makanisa hadi wanapokufa ndipo wanafikishwa humo kuombewa kabla ya kuzikwa.

aliokuwa nao Zakayo, ingawa alikuwa ni mtoza ushuru na alikuwa akionekana kuwa ni mkosefu lakini aliposikia Yesu anapita maeneo hayo aliazmia kwamba lazima amwone na akamwona.

WAWATA waonywa kuepuka ulimwengu

Na Dalphina Rubyema

ILI kulinda Kanisa lisiyumbe,Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kama kiungo muhimu katika kanisa wameshauriwa kutokubali kutekwa na mambo ya ulimwengu ambayo yanaweza kuwasababishia wasahau wito wao katika kanisa.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Walei Jimbo la Tunduru Masasi,Padre Jacob Mchopa, wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa WAWATA uliofanyika katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala, jijini.

Padre Mchopa alisema kuwa shetani kwa lengo la kuharibu Kanisa Katoliki anaweza akaanzia kwa WAWATA ambao ni mhimili mkuu na hivyo kusisitiza zaidi kuwa ni muhimu WAWATA kusimama imara kuyashinda majaribu.

"Kuna usemi usemao kuwa ukitaka kumuuwa nyoka uanzie kichwani na hivyo shetani akitaka kuliharibu Kanisa atataka anzie kwa WAWATA, kwani nyie ndiyo kichwa cha Kanisa,"alisema.

Awali katika ibada ya kufungua mkutano huo wa siku mbili Mkurugenzi wa Idara ya Utume wa Taifa,Padre Nicholaus Segeja aliwataka WAWATA kuzitumia pesa za miradi zinazotoka kwa wafadhili kama ilivyokusudiwa na siyo matumizi binafsi.

"Mtu anakopa mkopo kwa miradi yake kwa makubaliano ya kurudisha mkopo huo na riba lakini cha ajabu anavunja makubaliano na akienda kuulizwa, anajibu kwa uwongo" ooh...mtoto aliugua,nilifiwa nikazitumia pesa hizo; tena anajibu kwa hasira. Pesa za mradi siyo za matumizi mengine ni za matumizi ya mradi uliolengwa,"alisema.

Padre Segeja ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Idara ya Utume wa Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) aliwakumbusha viongozi wa WAWATA wasipende kwanza kujikopesha pindi pesa ya inapotolewa.

"Viongozi nawakumbusha msipende kujikopesha pindi pesa za miradi zinapopatikana, kwani hata Kristo mwenyewe hakuwa wa kwanza kujikopesha,angefanya hivyo asingekufa msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu,"alisema Mkurugenzi huyo.

Katika taarifa ya utendaji wa WAWATA kwa kipindi cha miezi 15 kuanzia Oktoba 98-Machi2000 iliyosomwa na katibu mkuu wa WAWATA Bibi Betty Mwaruli ilielezwa kuwa wamefanya mafungo ya mwaka kwa nchi nzima na tafakari ya kiroho ya kila mwezi.

Bibi Mwaruli alielezea mkutano huo kuwa WAWATA bado haijapata mpangaji wa nyumba yake iliyopo Ilala mtaa wa Pangani jijini pamoja na kwamba ujenzi wake tayari umekamilika.

Katika taarifa ya mapato iliyotolewa na Mtunza Fedha wa WAWATA Bibi Elizabeth Twissa, ilielezwa kuwa jumla ya shilingi 156,701,710 zilipatikana kuanzia Oktoba mosi hadi Desemba 31 mwaka 1999 na jumla ya shilingi 197,377,432 Zilipatikana katika kipindi cha Januari-Septemba 1998.

Naye Mwenyekiti wa WAWATA Taifa Bibi Olive Luena, aliuambia mkutano huo kuwa WAWATA itabaki kuwa kiungo hai na mshiriki mkubwa wa Halmashauri ya Walei Tanzania na itaendelea kuwa mwanachama hai wa Umoja wa Wanawake Ulimwenguni na vyama vya hiari Tanzania (TANGO)

Mkutano huo uliwahusisha viongozi wa WAWATA zaid i ya 50 kutoka majimboni wakiwemo wakurugenzi wa utume wa walei.

Jeshi la Wokovu lataka serikali isitumie nguvu kuzuia tohara kwa wanawake

Na Elizabeth Steven

MCHUNGAJI Meja Mwita wa Kanisa la Jeshi la Wokovu mkoani Mbeya, ameishauri serikali kutokutumia nguvu kuzuia tohara kwa wanawake , badala yake iongeze juhudi kuielimisha jamii madhara yake kama ilivyo kwa ugonjwa wa ukimwi.

Mchungaji Meja , alitoa ushauri huo katikati ya juma lililopita wakati akizungumza na gazeti hili yalipo makao makuu ya Kanisa hilo jijini Dar Es Salaam.

Alisema kimsingi haungi mkono kitendo hicho kinachowadhalilisha wanawake kwa kuwa haikuagizwa katika Biblia Takatifu kifanyike, isipokuwa alisema, njia inayotumika ya kuzuia kwa lazima anaiona sio muafaka kwa kuwa inachangia pia kuhatarisha maisha ya wanajamii wengine wanaoifanya kwa siri na kukimbilia maporini wakiogopa kukamatwa.

Alisema, "Jamii haijaeleweshwa kiasi cha kutosha ubaya wa kuwatahiri watoto wa kike ndio maana bado watu hasa mkoani Mara wanatahiri kwa kujificha na hii ni hatari maana huwezi kujua huko atakutana na kitu gani kibaya au hali itakuwaje."

Akifafanua zaidi, alisema hali ya kufanya tohara kwa kificho itasababisha hata vifo kwa wahusika kuogopa kuripoti hospitalini pale waliotahiriwa wanapolazimika kupata matibabu wakihofia kushitakiwa.

Alisema wahusika wanapokimbilia maporini kukwepa kukamatwa baada ya kutahiri ndugu zao, ipo hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali kama nyoka na wengine.

Akitoa mfano wa mila nyingine za Wakurya mkoani Mara zilizojifia zenyewe bila shinikizo la serikali kuwa ni pamoja na kung’oa au kuchonga meno na kuvaa lundo la bangili mikononi na miguuni.

Hata hivyo alisema ingawa tohara hizo zilisaidia jamii kutunza maadili na kuepuka mimba kabla ya ndoa,bado hivi sasa sio wkati muafaka kuindeleza kwa kuwa sasa yamezuka magonjwa mengi yanayoweza kuambukizwa kupitia njia hiyo

Naye Mwandishi wetu anaripoti kuwa, Mwalimu Eliabu Gesase wa shule ya sekondari ya wasichana ya KOWAK wilayani Tarime mkoani Mara, aliyehudhuria semina ya walimu wa somo la Uraia kwa shule za Kanisa Katoliki nchini iliyofanyika jijini hivi karibuni, amesema, tohara kwa wanawake mkoani kwake bado inaendelea na baadhi ya viongozi wa tarafa, kata na vijiji, wameigeuza kuwa mradi wa kujipatia vipato kwa madai ya rushwa.

Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa inayoendesha mila za kuwafanyia tohara watoto wa kike na licha ya juhudi za kuipiga vita mila hiyo yenye madhara mengi kijamii,kiafya na kisaikolojia bado hufanyika kwa kificho na wakati mwingine kumfanyia mjamzito wakati wa kujifungua.