UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU:

Dk. Remmy aahidi kupigia debe CCM

lAahidi kutunga mipasho ya taarabu akaimbe Zanzibar

lAsema Mrema ana nyota ya Uongozi lakini anaichezea

Na Mwandishi Wetu,

MWANAMUZIKI maarufu nchini ‘Dk’ Remmy Ongala ameapa kukipigia debe Chama Cha Mapinduzi, hadi kishinde katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa anaamini ndicho chama pekee chenye pesa na mwelekeo tofauti na wapizania ambao amedai wakipata ruzuku wanafunga maofisi.

Dk. Remmy alitoa ahadi hiyo alipokuwa akijibu swali la gazeti hili lililotaka kujua ni kwanini wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha NCCR_MAGEUZI, Augustine Mrema, alipojiengua toka Chama Tawala, Remmy aliimba nyimbo za kumsifu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, lakini baadaye tena akageuka na kuipigia kampeni CCM katika Viwanja vya Jangwani jijini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Alisema, Mrema alipokuwa C.C.M, alitenda mambo mazuri yaliyostahili sifa ikiwa ni pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ujambazi, mauaji, ubadhirifu na kujenga vituo vingi vya polisi vinavyosaidia kuimarisha usalama hadi sasa katika maeneo mbalimbali nchini.

Remmy alisema, katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani baadaye mwaka huu, yuko tayari kuimba nyimbo za mashairi na taarabu hadi Visiwani Zanzibar ili C.C.M ipate ushindi, kwani ndicho chama pekee chenye uwazi na ukweli na kinachotumia pesa zake kwa manufaa ya umma.

"C.C.M ndicho chama pekee kinachoeleza uwazi na ukweli. Hivi vyama vingine vikipata ruzuku, viongozi wanafunga ofisi na kutumia ruzuku hizo kwa manufa yao, zikiisha wanafungua na kuanza kutumia muda mwingi kwa malumbano hata wao kwa wao," alisema na kuongeza, "Lakini C.C.M, wawe nazo, wasiwe nazo mambo yao ni shwari mpaka kwa wananchi," Hata hivyo hakutaka kusema kama ameshaweka makubaliano yoyote na CCM au la.

Alisema sababu nyingine ya kukipigia debe C.C.M, ni namna kinavyojali kila mwananchi wake bila kujali asili ya utaifa.

Akitoa mfano wa hoja yake, Dk. Remmy, alisema, "Mimi ni raia wa Kongo, lakini nimeishi Tanzania kwa miaka 22, bila kubughudhiwa na serikali wala viongozi wa C.C.M."

Alisema Remmy na kuhoji, "Hivi unafikiri hivi vyama vingine vya upinzani vikishika madaraka, watu wengine si tutakimbilia maporini?"

Remmy alisema ingawa yeye anatafuta pesa kwa kutumia fani yake ya muziki, kamwe hawezi kuwa malaya wa kisiasa kwa kuitwa ovyo ovyo na vyama vya upinzani ili kujipatia pesa za msimu huku anapoteza umaarufu na heshima yake kimuziki.

Hata hivyo Dk. Remmy, alisema kuwa Mrema ni kiongozi mwenye mvuto na "nyota" ya uongozi isipokuwa yeye mwenyewe ana udhaifu wa kujichanganya na hivyo kukosa mwelekeo.

Mapema mwaka 1993 wakati Bw. Augustine Mrema alipojitoa CCM, Dk. Remmy alijitokeza hadharani kumpigia debe kwa nyimbo zake ambazo zina mvuto mkubwa kwa watu.

Miezi michache baadaye Dk. Remmy alivunja ghafla uhusiano wa karibu na Bw. Mrema na habari ambazo hazikuwahi kuthibitishwa zikaeleza kuwa alitishwa na CCM kuwa endapo angeendelea kupigia debe upinzani angetimuliwa nchini kwa vile hakuwa na uraia.

Hatimaye mwaka 1995 katika Vinwaja vya Jangwani kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM, Dk. Remmy alipanda jukwaani kwa kilichoelezwa kuwa kumpigia debe mgombea wa CCM (Benjamin Mkapa)lakini alipopanda jukwaani akafululiza kuimba nyimbo za kumsifu Nyerere, licha ya kuhamasishwa na aliyekuwa ‘MC’ Kapteni Kasapira amsifu mwali wao.

Kadhalika hivi karibuni Dk. Remmy ambaye aliomba uraia alikuwa akilalamika kuwa anasumbuliwa mno kupata uraia huo kiasi cha kuzusha maswali mengi kwa wanajamii kwa vile mwanamuziki huyo ameshaishi nchi kwa miaka 22 sasa.

Endapo Dk Remmy atapanda majukwaani kukipigia debe Chama cha Mapinduzi bila shaka atakuwa ameweka chachu ya aina yake kwa vile yeye binafsi ni kivutio kikubwa kwa watu popote anapokuwa na ana sanaa yenye ushawishi mkubwa wa mioyo ya watu.

 

Hongera: kumbe Nyerere 'bado yupo CCM'

Na Joseph Sabinus

KANISA la Kiinjilisti la Kilutheri (K.K.K.T), limeipongeza Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kwa kuupiga kikumbo mpango wa kubadili ukomo wa vipindi viwili vya uongozi huko Visiwani uliolenga kumwezesha Dk. Salmin kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Limesema limefurahi kuona kwamba kumbe 'nguvu' za Marehemu Mwalimu Nyerere za kudhibiti wakorofi bado zimo ndani ya CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini katikati ya juma, Askofu Msaidizi wa K.K.K.T, dayosisi ya Pwani na Mashariki, Adam Kombo, alisema uamuzi wa NEC kuilinda Katiba ya nchi isichezewe ovyo kwa manufaa ya wachache hasa wakati nchi inapoelekea Uchaguzi Mkuu na hivyo kuweza kuhatarisha amani, ni wa busara na hauna budi kupongezwa na wote wenye mapenzi mema.

"Katika kikao chao cha Dodoma, ni dhahiri waliongozwa na hekima ya Mungu na hivyo kuilinda Katiba ya nchi kwa amani," alisema Askofu Msaidizi huyo na kuongeza,

"Kibinadamu, wengi walihofu kuwa Salmin akikataliwa, mambo yatakuwaje; maana wapo wenye ubinafsi waliojua kuwa wataumia ingawa huo ndio uliokuwa utaratibu na ni hekima ya Mungu kuulinda.

Huko Dodoma wameonyesha kuwa hekima alizoziacha Nyerere bado zinaendelezwa kupitia watu wake kwani mpaka sasa hakuna mgawanyiko wowote kwa Watanzania ; hata huko Zanzibar."

Akiunga mkono, Askofu Msaidizi, Kombo alisema kimsingi huu haukuwa wakati muafaka kujadili marekebisho ya Katiba kwa ajili ya Uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. "...Nikiwa miongoni mwa raia wa Tanzania, naiunga mkono C.C.M; wametumia hekima kubwa," alisema.

Akizungumzia Uchaguzi huo Mkuu ujao, alimtaka kila mwanajamii kwa nafasi yake, kuhakikisha kuwa unakuwa wa huru, haki na amani.

"Wananchi, vyama vya upinzani na CCM, wapige kura na serikali idhibiti uchaguzi uwe huru na wa haki."

Hivi karibuni umekuwepo mjadala mkali uliopelekea Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kukutana Dodoma hivi karibuni na kuahirisha mjadala juu ya marekebisho ya Katiba ya Zanzibar hadi baada ya Uchaguzi Mkuu ujao na hivyo kumzuia Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour kugombea urais kwa kipindi cha tatu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 1995, kifungu cha 30 (1) (b): "Mtu hatofaa kuchaguliwa kuwa rais ikiwa: amechaguliwa kushika madaraka hayo katika vipindi viwili mfululizo vilivyokwisha."

Kifungu hicho kinasisitizwa zaidi na kifungu kilichotangulia cha 28 (1) (f) kisemacho: "Kufuatana na Katiba hii, mtu ataendelea kuwa rais mpaka: kwa sababu yoyote nyingine ameacha kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vingine vya Katiba hii."

Nacho kifungu cha 28 (3) kinasema kuwa, "Bila ya kuathiri chochote kilichomo katika kifungu hiki cha katiba hii, hakutakuwa na mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa zaidi ya vipindi viwili mfululizo vya miaka mitano mitano kila kimoja."

 

Mchungaji chupuchupu kuchomwa kisu na muumini

Na Mwandishi Wetu, Mwanga

MKEREKETWA mmoja wa Walutheri wanaodai kwa nguvu kuigawa Dayosisi ya Same ili iwepo nyingine ya Mwanga, Bw. Samwel Mathayo Mkwizu hivi karibuni alimwendea na kutaka kumchoma kisu Mchungaji Nkima wa Usharika wa Mcheni (KKKT) mtii wa Dayosisi ya Pare.

Habari kutoka Ugweno, wilayani Mwanga zimesema kijana huyo alimkuta Mchungaji Nkima, akiwa katika ofisini peke yake.

Kijana huyo ambaye ni Mtoto wa Mwanakamati aliyekuwa muasisi wa Dayosisi ya waasi ya Mwanga Mzee Mathayo Mkwizu(marehemu) inadaiwa aliingia ofisini na kumwambia Mchungaji kwa jina huyo kuwa amefika kumchoma kisu.

Habari zinasema Mchungaji alimwambia kuwa atimize dhamira yake lakini la kushagaza yule kijana alianza kutetemeka na kuomba mchungaji Nkima amsamehe kwani sio dhamiri yake.

Mchungaji alishikwa na butwaa ndipo alipotoka nje na kuwaita watu waliokuwa wakipita nje ili waje wamshuhudie yule kijana.

Wakati huo yule kijana alikuwa pale ofisini huku amezubaa asijue la kufanya na ndipo mchungaji alipomwambia tena atimize dhamira yake, lakini akazidi kumwomba asamehewe. Baada ya hapo habari zinasema Mchungaji alipomwambia "nimekusamehe...nenda," akaondoka.

Hadi tunakwenda mitamboni hakuna taarifa zozote zilizoeleza kuwa kijana huyo amechukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huo huo: Mchungaji wa kundi la waasi wa Dayosisi ya Same Abraham Mshana ambaye kwa muda sasa amekuwa mwiba kwa Usharika wa Kifula,Ugweno katika Jimbo la Kaskazini la KKKT, amepigwa marufuku na Polisi kujihusisha na masuala ya kichungaji katika Usharika huo.

Habari za uchunguzi zimeeleza kuwa Polisi wamelazimika kufanya hivyo ili kuepusha uwezekano wa kuvunjika kwa amani kwa vile mara kadhaa amekuwa akituhumiwa kuvutuga ibada na kusababisha hali ya wasiwasi kwa waumini.

Mwishoni mwa wiki Dayosisi ya Pare iliwafungulia mashitaka katika Mahakama Kuu kwa kusababisha mmomonyoko wa kiroho na kiimani kwa waumini wa Kanisa hilo pamoja na kuhodhi mali za kanisa isivyo halali.

Walioshitakiwa katika mkumbo huo ni ‘Askofu’ Mteule Edward Mbaruku, Msaidizi wake Sifaeli Maulidi na wakuu wa majimbo mawili akiwemo Mchungaji Abraham Mshana (jimbo la Ugweno) na Samwel Mziray (jimbo la Mwanga).Wengine ni Bw. Walter Mrisha na Bw. Stanley Mbaga. Mashitaka hayo yatakayosikilizwa jumatatu ijayo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Eusebio Munuo yamewasilishwa na niaba ya Dayosisi na Pare na Wakili Profesa Robert Msanga.

 

Askofu Mteule kuzindua tamasha kabambe la Kwaya

Na Dalphina Rubyema

ASKOFU Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Method Kilaini ameanza kushirikishwa katika shughuli za jimbo lake na Jumapili hii anatarajiwa kuzindua sherehe za Jubilei Kuu Jimboni kwake atakapofungua Tamasha la Kwaya.

Akizungumza na KIONGOZI jijini mwishoni mwa juma, Katibu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Padre Stefano Kaombe alisema ufunguzi wa tamasha hilo la siku moja utafanyika katika Kanisa Katoliki la Msimbazi na Mwadhama Polycarp Pengo anatarajiwa kufunga tamasha hilo.

Katibu huyo alisema baada ya kusimikwa uaskofu Machi 18 mwaka huu, Askofu Mteule Kilani na Mwadhama Pengo wataongoza ibada ya ndoa mpya zipatazo 140 ibada itakayofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu ikiwa ni moja ya shamrashamra za Jubilei Kuu.

Akielezea zaidi juu ya tamasha la kwaya, Padre Kaombe alisema, kila Parokia inatakiwa kuwa na wanakwaya wasiozidi 60 ambapo kila kikundi kitatakiwa kuimba nyimbo tatu kwa kutumia muda wa dakika 9.

Alisema nyimbo hizo zinatikiwa ziwe katika makundi matatu ambapo wimbo wa kwanza utalenga Jubile ya Kimataifa, wa pili utamadunisho na wimbo wa tatu, ni wa kawaida.

Akifafanua zaidi, Padre Kaombe alisema wimbo wa pili na wa tatu lazima

ziongelee mojawapo ya haya, msalaba,jumuiya ndogondogo, ndoa, Kitubio, Ekaristi, Maandiko Matakatifu pamoja na hija na tayari parokia 25 zimekwisha jitokeza kushiriki tamasha hilo.

Akielezea zaidi juu ya mambo kadhaa yatakayofanyika wakati wa sherehe hizo za Jubilei katika jimbo lake ambazo kilele chake ni Machi 20 mwaka huu, Padre Kaombe alisema Machi 16 watu wapatao 250 waliodumu katika Sakramenti ya Ndoa kwa muda wa miaka 25 na kuendelea watarudia ahadi zao za ndoa.

 

Tanzania yahitaji kudhibiti mionzi mikali

Na Dalphina Rubyema

MATUMIZI ya nishati za kinyuklia na zana zenye mionzi mikali yameongezeka kwa kasi katika nyanja mbalimbali za uchumi na maendeleo hivyo hayana budi kudhibitiwa ili kuepuka athari zake.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Sayansi na Teknolojia Bw. Titus Mteleke wakati akifungua mkutano wa utekelezaji wa sheria ya kudhibiti mionzi katika chakula uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar Es Salaam.

Bw. Mteleke alisema kuwa Tume ya Taifa ya Mionzi iliyokuwa mwandaaji wa mkutano huo uliowajumuisha makampuni na wafanyabiashara mbali mbali wanaohusika na uigizaji wa vyakula nchini haina budi kuwa makini katika kupima vyakula vyote vinavyoingizwa nchini kuona kama vimeathirika na mionzi.

Alisema ulimwengu wa karne ya tatu ambao utaendeshwa zaidi kwa Sayansi na Teknolojia ya hali ya juu Tanzania ikiwa mshiriki na hasa katika biashara huria umo katika hatari kubwa kupata madhara ya vyanzo vya mionzi endapo vyakula vinavyoingizwa katika kila nchi havitaangaliwa.

Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa Tume ya Taifa ya mionzi haina budi kuondoa ulegevu wake iliouonesha kwa kipindi kilichopita na badala yake iwe mtekelezaji wa sheria ndogo ndogo zilizo tungwa na wizara yake ili kudhibiti matumizi ya vyanzo vya mionzi.

Wakati huo huo, msajili wa Tume ya Taifa ya Mionzi na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Abraham Nyanda, alisema, ili kukwepa tatizo la mionzi katika chakula, wananchi hawana budi kusisitiza matumizi ya vyakula vinavyozalishwa hapa nchini na siyo vitokavyo nje ya nchi

 

Changanyikeni wachanganyika kuunda umoja

Na Mwandishi Wetu

WAKAZI wa Changanyikeni, nje kidogo ya jiji la Dar Es Salaam, wameanzisha chama cha maendeleo kinachojulikana kama Changanyikeni Iniative (CHAIN) kwa lengo la kuimarisha shughuli za maendeleo na huduma za jamii katika kijiji hicho.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni jijinI, Mwenyekiti wa chama hicho cha hiari, Dk. Simeoni Mesaki, alisema kuwa chama hicho kina lengo la kuboresha huduma mbalimbali za jamii kijijini hapo.

Alizitaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni pamoja na kushughulikia huduma ya maji ambayo hupatikana kwa shida kijijini hapo,ujenzi wa zahanati na barabara pamoja na kubuni mipango mbalimbali ya kuondoa umaskini.

Dk.Mesaki ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuuu cha Dar es salaam, alisema tayari jitihada za kuwapata wahisani kwa kushirikiana nao katika kutekeleza mikakati hiyo zimeanza huku juhudi za kusajili chama hicho zikiendelea.

Mbali na CHAIN, wakazi hao pia wameunda ushirikiano wa ulinzi wa sungusungu unaojulikana kama Jirani Tulindane (JITU) ambapo lengo kuu ni kukubaliana na matukio ya wizi yaliyoshamiri katika eneo hilo.

Dk. Mesaki alisema tangu ulinzi huo uanzishwe yapata miezi minne sasa wamefanikiwa kuokoa ng’ombe wanne wa mwanakijiji mmoja wenye thamani ya shilingi milioni moja.

Ametoa msisitizo kwa wakazi wa eneo hilo kuwa hawana budi kujituma wakati muda wa doria unapowadia na siyo wasubiri kuamshwa.

"Ulinzi huanza saa 6.00 usiku -10.00 alfajiri ambapo kila mtu hutakiwa kufanya doria mara moja kwa wiki.

Anatoa wito kwa wale wanaopenda kulala muda wa doria unapowadia, kuwa ni lazima wawe na ari ya kujituma badala ya kusubili waamshwe.

Alisema pia juhudi na utaratibu unafanywa ili kuwashirikisha wanakijiji wengine ambao ni wanafunzi wa chuo kikuu wanaoshi eneo hilo pamoja na wanawake ambao hawana waume ili waweze kuchangia huduma za ulinzi.

Hatimaye kilio cha walimu nchini chasikilizwa

Na Neema Dawson

SERIKALI imesema imetoa shilingi bilioni moja ili kulipa walimu madeni yao ikiwa ni juhudi za kupunguza deni la shilingi bilioni 4.01 ambalo serikali imekuwa ikidaiwa na walimu wa shule za msingi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo gazeti hili limezipata hivi karibuni, wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa wameishatumiwa kiasi cha fedha zilizotolewa kwa halmahauri zote ambapo walimu wote wa shule za msingi hapa nchini wanatarajiwa kulipwa malipo yao ya malimbikizo ya miaka ya nyuma ambayo walimu walikuwa wakiidai serikali na malipo hayo yatafanyika muda wowote kuanzia sasa hivi.

Waziri mkuu Mheshimiwa Frederick Sumaye ambaye hivi karibuni alikutana na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania CWT na kutoa maagizo kuwa walimu wanatikwa kulipwa fedha zao haraka iwezekanavyo na kusisitiza kuwa viongozi wa chama cha walimu wa wilaa zote nchini washirikishwe kikamilifu katika zoezi la kuwalipa walimu sehemu ya madeni yao ili kuondoa malalamiko yoyote yale yanayoweza kutokea.

"Pesa ziliotlewa hazitoshelezi kulipa madeni yote na nimewaandikia wakuu wote wa mikoa Tanzania bara ili kila Mkurugenzi wa Halmashauri ahakikishe utaratibu mzuri ulio wazi unatumika katika ulipaji wa madeni hayo na kiongozi yeyote atakayetumia fedha hizo kwa madhumuni ambayo hayakukusudiwa atachukuliwa hatua kali za kinidhamu,"imesema sehemu ya taarifa ya CWT ikimkariri waziri mkuu.

Ataka vijana wakingwe na athari za Teknolojia

Na Josephs Sabinus

WAKATI ulimwengu umeingia katika karne ya sayansi na teknolojia, vijana wametakiwa kuelimishwa zaidi ili kukabiliana na athari za kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano hivyo kuwaimarisha kiroho na kisaikolojia badala ya kuwatenga kimawasiliano kama kisiwa.

Hayo yalisemwa na Askofu Mteule Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, Mhasham Method Kilaini alipokuwa akizungumza katika warsha ya siku nne juu ya muundo wa wanaseminari kwa Kanisa la Afrika katika millenia hii mpya.

Alisema kwa kuwa si rahisi na haina maana kumzuia kijana kufanya mawasiliano na sehemu mbalimbali duniani hasa baada ya kupanuka kwa teknolijia ya mawasiliano, vijana hawana budi kupewa mafunzo ya kutosha kuwawezesha kukabiliana na teknolojia hiyo kwa kujengwa na kupewa moyo na akili bora ili wawe tayari kuchambua na kutenganisha mabaya na mema wanayoyaona kwa manufaa ya Kanisa.

Alisema kwa kuwa vifaa vya mawasiliano vya kisasa kama Television, Video, E-Mail na mtandao wa kompyuta ambazo sio rahisi kumuwekea mtu mipaka ya kupata mawasiliano kwa kuzitumia, ni vema vijana wakaeleweshwa zaidikuhusu mazuri na mbaya watakayo kutana nayo katika vyombo hivyo.

"Ulimwengu wa sasa umebadilika na kuwa sawa na kijiji. Haiwezekani ukamzuia kijana kutumia TV au Internet, atajifungia chumbani aone kila kitu anachoweza kukutana nacho. Lazima ijulikane kuwa katika njia hizo watakutana na vitu vingi vingi; hata devals na Virusi.

Ueleweke ukweli kuwa wanafunzi wetu wanakwenda katika ulimwengu usio na mipaka," alitahadharisha Askofu Mteule huyo na kuongeza, "Lazima wawe trained kuchuja mazuri yale mabaya kuyatupilia mbali."

Katika warsha hiyo ya hivi karibuni iliyowashirikisha wajumbe 54 wakiwemo wakuu wa seminari na wakurugenzi wa mafunzo stadi, Askofu Mteule Kilaini, aliwatahadharisha washiriki hao kuwa makini wakati wa uchaguzi wa vijana wanaojiunga na seminari zao.

Alisema hali hii itasaidia kwa kiasi kikubwa, kuwaepuka wanaojiunga na seminari kwa lengo la kupambana na ugumu wa maisha badala ya kufanya hivyo kufuatia miito ya kufanya kazi ya Mungu.

"Wengine wanaweza kuwa wakimbizi wa maisha; labda kwa kukosa ajira, au ugumu wa wowote wa maisha. Lazima muwajue kama kweli wana nia kuwa watakapomaliza elimu yao watafanya kazi ya Kanisa,au la." alisema na kuongeza,

"Ni kweli, lazima muwe makini kwa sababu kama una mayai machache yaliyooza ndani ya kikapu, kikapu chote lazima kitanuka."

Katika warsha hiyo, Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Elias Msemwa, aliwahimiza wajumbe hao na walimu wengine wa seminari, kuhudhuria semina, warsha na kozi mbalimbali ili kujiendeleza zaidi kitaaluma.

Makanisa nchini yagongana

Josephs Sabinus na Peter Dominick

WAKATI Kanisa la The Gospel Revival Center, linasema, viziwi hawahitaji Injili bali uponyaji kwanza, Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri, limekiri kuwanyima haki ya kushiriki Injili kwa kutowapa vifaa vya kukuzia sauti wala wakalimani ili kuwatafsiria mahubiri kwa lugha ya ishara.

Kupingana huko kwa mitazamo ya makanisa hayo kumefuatia gazeti hili kutaka kujua makanisa na madhehebu mbalimbali, yana mpango gani wa kuwawezesha viziwi kushiriki kikamilifu kupata Neno la Mungu wakati mahubiri mbalimbali yanapotolewa.

Uchunguzi wa muda mrefu uliofanya na gazeti hili katika makanisa mbalimbali ya Kikristo nchini, umebaini kuwa karibu makanisa yote nchini hayatoi kwa waumini wao wasiosikia, vifaa maalumu vya kukuzia sauti ili kuwawezesha kusikia mahubiri yanayotolewa na viongozi wa kiroho.

Aidha, licha ya kukosekana kwa vifaa hivyo maalumu kwa viziwi, bado makanisa na madhehebu mengi hayajafikiria walau mpango wa kuwatafuta wataalamu wa kutafsiri lugha ya ishara inayotumiwa na viziwi ili kuwawezesha kupata moja kwa moja ujumbe wa Injili wakati wa mahaubiri.

Uchunguzi huo umebaini kuwa hali ya kukosa wakalimani hao na vifaa maalumu vya masikioni, imewafanya viziwi wengi kukwazika na kukata tamaa ya kiroho na hivyo kutokutaka kwenda makanisani wala kujishughulisha na mambo ya kikanisa.

KIONGOZI lilipo onana na Mwenyekiti wa makanisa ya The Gospel Revival Center (GRC), Mchungaji George Kilango, jijini juma lililopita, alisema kuwa ni vema kabla ya kufikiria kuwatafutia viziwi wakalimani au vifaa maalumu vya kukuzia sauti, wakafanyiwa uponyaji kwa njia ya maombezi kwanza.

"Dawa ya kudumu ni kuwaleta viziwi katika mikutano ya Injili ili wakapate kuponywa katika Jina la Yesu. Hilo ndilo jambo la msingi kwanza."

Aliongeza kuwa, "Walemavu, vipofu, viziwi na wengi wenye shida mbalimbali, wameponywa katika mikutano mbalimbali na sasa wanashiriki vema katika Injili ya Bwana. La msingi ni kuwaombea kwa imani na wao wenye kuamini juu ya uponyaji wa miujiza ya Bwana Yesu."

Gazeti hili lilipotinga katika ofisi za Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) dayosisi ya Pwani na Mashariki, Askofu Msaidizi, Adam Kombo, alikiri kuwa makanisa mengi likiwemo K.K.K.T, yamekuwa hayawatendei haki viziwi kwa kutokuwapa vifaa malumu vya kuwasaidia kusikia au wataalamu wa kutafsiri katika lugha yao ya ishara ili kuwawezesha kushiriki Injili ya Bwana wakati wa Mahubiri.

"Binafsi, sijawahi kusikia kanisa ambalo walau lina wataalamu wa kutafsiri kwa lugha ya viziwi kama yafanyavyo makanisa ya wenzetu huko Ujerumani na kwingine. Hiyo ni kweli tunawanyima haki maana hata Kanisa letu halina kitu cha namna hiyo. Na hii ninakiri kuwa ni udhaifu tulio nao wa kusahau aina zote za watu tulio nao makanisani.""Ni vizuri baadhi ya sharika zetu zikawa na wataalamu ili watu wa namna hiyo (Viziwi), wakusanyike pamoja na kupata huduma hiyo maana sio rahisi kila usharika ukawa na mkalimani wake. ... Na hii ni vizuri hata makanisa mengine yawatafutie ufumbuzi. Wandishi mmefanya vizuri kutukumbusha hili na mimi nitalipeleka katika vikao vyetu haraka," alisema Askofu Msaidizi huyo.

Hata hivyo, uchunguzi zaidi umebaini kuwapo vituo kadhaa vya makanisa vya kulelea walemavu mbalimbali vinavyo watafsiria viziwi katika lugha ya ishara kwa kutumia wataalamu maalumu.

Huduma hiyo sio makanisani na inawachanga walemavu wenye imanai na wa madhehebu tofauti.

Watoto Watanzania wampelekea Papa njiwa

Na Getruda Madembwe

KATIKA maadhimisho ya WATOTO mahujaji wa Kitanzania wamempelekea Baba Mtakatifu njiwa ikiwa ni ishara ya amani na upendo kwa dunia nzima.

Kwa mujibu wa Sista Marihut Mosquera, wa shirika la Terciary Wakapuchini Tanzania Jimbo Katoliki la Morogoro, mtoto mmoja miongoni mwa watoto hao kutoka katika parokia za Kisanga, Msolwa na Madeko alimpelekea Baba Mtakatifu njiwa huyo ikiwa ni ishara ya upendo.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kurejea kutoka Roma Italia alikohudhuria maadhimisho hayo, Sista Marhut alisema watoto hao Helberti Daudi(13, Gloria Saidi(14), Veneranda George(12) na Maria Goreti Saidi(9) ambaye alipelekea Baba Mtakatifu njiwa kama ishara ya amani kwa dunia nzima.

Katika maadhimisho hayo, Baba Mtakatifu aliwataka watoto wote duniani kuwa na ushirikiano na mwenendo bora katika maisha yao ili wawe viongozi bora wa baadaye katika jamii wakiongoza kwa maadili huku wakizingatia mapenzi ya Mungu wakiwasaidia wanao hitaji misaada yao katika nchi zao.

Baba Mtakatifu Paul II, alisema katika maadhimisho hayo kuwa watoto ni furaha ya dunia na akahimza upendo kwao kama Bwana Wetu Yesu Kristo alivyoonesha upendo wake kwa watoto.

"Watoto ni furaha ya dunia hivyo ni lazima wapewe upendo kama Yesu Kristo alivyokuwa akiwapenda watoto hata alipoona wanabughudhiwa na wanafunzi wake aliwakemea na kuwaambia kuwa wawaache watoto hao waende kwake," alisema Sista Marhut akiyanukuu maneno aliyosema Papa.

Watoto hao waliiombea dunia nzima amani na umoja kwani inapotokea kutoelewana kwa watu wengine au machafuko yoyote yale wanaoathirika zaidi kwa vifo, mahangaiko mbalimbali yakiwemo maisha ya uyatima kuwakumba, ni wao watoto