KUZUIWA KUZUNGUMZIA MAISHA BINAFSI YA WAGOMBEA UONGOZI

Tanzania kuongozwa na wahuni?

lMsingi wa uadilifu uko katika maisha binafsi

Na Josephs Sabinus

WANANCHI kadhaa wameipinga vikali rasimu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayopiga marufuku vyama kwa kuzungumzia maisha binafsi ya mgombea wa nafasi yoyote katika Uchaguzi Mkuu ujao na wakasema hali hiyo italifanya taifa kuongozwa na wahuni.

Mwishoni mwa wiki Gazeti hili lilipofika katika ofisi za Tume hiyo jijini kufafanuliwa chimbuko na lengo la rasimu hiyo, Afisa Habari Mkuu wa Tume hiyo Bi. Mwajuma Mponji alisema,

"Hiyo ilikuwa ni rasimu tu , na hata hivyo vyama vilikubaliana kwenda kulijadili hilo ili baadae walete mapendekezo ya vyama vyao. Still is a working paper." alisema na kuongeza, "Hicho ndicho pekee ninachoweza kukueleza."

Kiongozi liliongea na wananchi wa kawaida wapatao 15 ambao 12 walionyesha kutoafiki na watatu tu kuunga mkono rasimu hiyo.

Rajab Mnubi, mkazi wa Kunduchi jijini, ambaye ni mfanyabiashara wa matunda sokoni Kariakoo alisema,

Maisha binafsi ya kiongozi hayawezi kutenganishwa na uongozi wake.

"Mkifanya hivyo mtawaweka hata mashoga madarakani mkailetea nchi laana," alisema kwa kung’aka na kuongeza, "Lakini mimi siamini hoja hii imetoka tu hewani, kuna jambo hapo au mtu anayelindwa."

Bi.Synthia Moses mwenye biashara ya kuuza nguo za kike katika Mtaa wa India jijini, alisema huenda utaratibu huo unawekwa ili kuwalinda wanaume ambao wana utamaduni wa kunyanyasa familia zao. "Inawezekana kuwa mtu ana skendo kama ya Mrema na yule mwanamke aliyezaa naye, sasa wanaogopa wataumbuliwa.Huku sio kupanua demokrasia ni kulindana tu."

Clement Uiso anayemiliki kampuni moja ya ujenzi nchini (hakutaka itajwe) amesema maisha binafsi ya Kiongozi sio tu kwamba ni muhimu kuzungumziwa anapowania uongozi, bali pia yanapaswa kuwa kigezo muhimu cha kumpa kiongozi kura.

"Kwa mfano kama kiongozi ameapa mbele ya padri au Mchungaji kwamba atalinda ndoa yake na hatahangaika na wanawake au wanaume wengine, halafu akitoka hapo anaanza kuzaazaa hovyo, utamwaminije atakapokuwa akiapa kuilinda katiba ya nchi?" alihoji na kufafanua kuwa ndiyo maana Rais Bill Clinton wa Marekani alinusuruka kuutema urais kwa tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke asiye mkewe.

Hata hivyo wananchi wapatao watatu walitoa hoja zinazofanana kutetea rasimu hiyo wakidai kuwa kinachohitajika katika kampeni ni kunadi sera na wala sio kufuatanafuatana katika maisha binafsi.

Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uenezi wa Chama cha Wananchi (CUF) Bw. Julius Samamba alisema hatua ya tume kuleta rasimu hiyo ni ya kidhaifu na hatari kwani inaweza kulipeleka taifa katika kuongozwa na watu majambazi wasio waadilifu hata kidogo.

alisema, wagombea lazima maisha yao yajulikane wazi ili jamii iwatazame kama kioo chao.

" Na hii inatokana na kuwa Tume haijiamini na ni ya watu wa CCM. CCM haina kiongozi bora baada ya kupoteza miiko ya uongozi ndani yake. Inapendekeza tu viongozi wasio na sifa, wafanya biashara ya madawa ya kulevya na mafuska ndio wamejazana CCM. Kwa hiyo rasimu hii inalenga kuwapa msaada CCM kwa sababu hawana viongozi wazuri."

Bw. Samamba aliwatahadharisha Watanzania kuwa makini ili nchi isipelekwe pabaya na akaitaka Tume hiyo ya Uchaguzi kutokuburuzwa na serikali ya CCM iliyopo madarakani.

Alisema siasa katika nchi zenye mfumo wa vyama vingi ni kama biashara ya nyanya sokoni ambapo mnunuzi hutaka kuziona nyanya nzuri ili azinunue na kwa mantiki hiyo wagombea uongozi wowote lazima ajulikane wazi maisha yao kwani ndio kioo ambacho jamii ongozwa inaweza kujifunza na kuiga mtindo wao wa maisha adilifu.

"Mwanasiasa anayeogopa kusemwa historia ya maisha na matendo yake, hafai na ni vema akae huko jikoni," alisema na kuongeza, "Hata kama mke wa mgombea ndiye anayefanya maovu lazima atajwe maana huyo mme wake ndiye anamuongoza na kumlea pale nyumbani."

Alisema anashangaa kwani imekuja wakati huu wa uwazi na ukweli na kufafanua kuwa kuficha maisha ya viongozi ni kuwafanya watoto wa baadhi ya viongozi kuwa machangudoa na walevi waliobobea kama walivyo wengine.

"Kwa mfano, nchi zilizoendelea kama Uingereza, mgombea hata kama anazini, hutajwa wazi hata siku aliyozini wakijua kwamba kiongozi lazima tabia yake ina uhusiano wa karibu na maadili ya uongozi. Lazima isemwe hadharani vinginevyo taifa linaweza kuongozwa hata na muuaji."

Naibu Mkurugenzi huyo alisema ni juu ya aliyetuhumiwa kudai kama amekashfiwa na kuomba vielelezo hivyo akaitaka Tume ya Uchaguzi isiwakingie kifua wagombea uongozi wenye historia mbaya ya matendo yao kwa kisingizio kuwa ni maisha binafsi ya mgombea.

Bw. Samamba ambaye chama chake cha CUF kilikataa kuchangia rasimu hiyo alisema msimamo wa chama chake uko kinyume kabisa na rasimu hiyo.

"Ndiyo maana hata siku ile hatukutaka kusema chochote tuliona hatuwezi kukubaliana na upuuzi kama huo."

Alidai kuwa rasimu hii ni kwa manufaa ya CCM na huenda ni mipango ya chama tawala, "...mpira huu unachezwa na CCM kwa sababu Mkapa ndiye anayemchagua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na ndiye Mwenyekiti wa CCM; na huku ni Rais wa nchi ndiyo maana CCM siku hiyo ya kikao walikubaliana na hoja hiyo kiurahisi," alisema.

Aliwaasa wagombea uongozi wa Tanzania kuiga mfano wa Rais Bill Clinton wa Marekani aliyekumbwa na kashfa ya ngono na mwanamke Monika Lewnsky na baada ya kusemwa hadharani akajitetea, akakiri na kuomba radhi familia yake. "Kama Rais wa Taifa kubwa vile watu wanamwambia hadharani kuwa wewe ni fuska, anajitetea na kuomba radhi, sisi tunaogopa nini?"

Aliongeza kusema, "Kama unagombea tu kwa kuwa wewe ni mtu wa CCM, bila kujulikana tabia yake, basi hiyo ni hatari lazima ajulikane kwa kuwa yeye ni kiongozi, kioo cha watu anao waongoza".

Katika mkutano huo wa uliofanyika Februari 23, mwaka huu katika ukumbi wa IFM jijini Dar Es Salaam,Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwasilisha rasimu hiyo mbele ya vyama 13 vya siasa vyenye usajili wa kudumu ili kujadili maadili.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, ni marufuku kuzungumzia maisha binafsi iwapo hayana uhusiano na shughuli za umma au vyama.

"Vyama vya siasa au wagombea wasijihusishe kabisa kukashfu maisha binafsi ya mtu ambayo hayahusiani na shughuli za umma au vyama vya siasa" inasisitiza sehemu ya rasimu hiyo. Mkutano kama huo ili kuwasilisha mapendekezo ya vyama hivyo utafanyika tena Machi 18 mwaka huu kupata mapendekezo ya ndani ya vyama.

 

Serikali inajali fedha kuliko uhai wa jamii- Maaskofu

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Maaskofu Katoliki nchini (TEC) limesema lina wasiwasi mkubwa na mwenendo wa kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini.

Katika taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Maaskofu wamesema wakati taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu na wanasiasa wakiwa katika hekaheka za kugombea uongozi, raia wengi hawajatambua kinachoendelea na wale wanaotambua wamejawa na wasiwasi.

"Sisis Maaskofu kama wachungaji tunaona na kusikia mengi ambayo yanatupatia wasiwasi sana," inasema sehemu ya taarifa hiyo.Maaskofu wamesema katika mwenendo wa sasa wa kisiasa na kijamii tabaka la wenye nacho(uwezo) linazidi kuimarika, na wanyonge kuzidi kuwa na wakati mgumu, huku Serikali ikionyesha kujali zaidi uhai wa uchumi wa kifedha kuliko uhai wa maisha ya jamii.

"Kwa mfano idadi ya vijana na watoto wasioweza kulipa ada na michango ya shule inazidi kuongezeka," taarifa imesema na kuongoeza:

Katika familia, hasa akinamama na watoto wengi wanakosa huduma za afya.

Maaskofu wamesema hivi sasa Wakulima nchini wanakosa nyenzo na wanahangaishwa na soko huria, huku wakiwa hawana utetezi na ushauri wa kufaa dhidi ya wanunuzi binafsi.

Wamesema mambo hayo pamoja na vijana wengi kukosa ajira vinakuza matabaka.

Juu ya harakati za kujenga demokrasi nchini, Maaskofu wamehoji endapo ni kweli mabadiliko ya Katiba ambayo yamefanyika kutokana na maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba yamefanywa kwa maslahi ya umma au ya wenye madaraka na kikundi cha watu fulani.

Wamehoji pia kama kuna mshikamano ndani ya chama tawala au kuna kuogopana na kutumia mbinu za ujanja kuhodhi madaraka. "Je ndani ya chama tawala kuna nafasi ya kutathmini kwa kina na makini sera na mifumo mbali mbali?" wameuliza.

Maaskofu pamoja na kuonya juu ya tabia ya matumizi ya fedha kuwarubuni wapiga kura katika chaguzi mbali mbali, wametaka fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya jamii zisitumiwe kama nyenzo ya kampeni. Taarifa kamili ya Maaskofu Ukurasa wa 7.

Rais Mkapa na Kigoda nani mkweli, wananchi wahoji

Na Dalphina Rubyema

BAADHI ya wananchi wamelalamikia kauli ya hivi karibuni ya Rais Benjamin Mkapa, kuwa bei ya Umeme haitapungua wakati Waziri wa Nishati na Madini Bw.Abdallah Kigoda, aliliambia Bunge hivi karibuni kuwa bei ya umeme itapungua kwa kati ya asilimia 30 hadi 50.

Kwa makusudi gazeti hili mwishoni mwa wiki liliamua kupata maoni ya wananchi wa kawaida jijini Dar-Es-salaam ambao ni miongoni mwa wananchi wengi walioguswa na kauli hizo za kupunguzwa na kisha kutopunguzwa kwa gharama za umeme.

Bw. Hamadi Salim Mango mkazi wa Ubungo Kibangu ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki duka katika eneo hilo alisema tabia hiyo ya viongozi kuwatangazia wananchi kauli tata kama hizo zinawavunjia heshima viongozi wenyewe na kuondoa imani ya wananchi kwao.

Alisema anashangaa kwa nini Rais awe anapingana na mawaziri wake aliowateua. "Au hawashirikishani katika maamuzi au wanaonyeshana ubabe?" alihoji

"Rais angefikiria kwanza kabla ya kutamka kufuta punguzo la umeme kwani hali halisi ya kipato cha wananchi wake anakifahamu." Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa Rais Mkapa hana budi kufikiria kabla hajatoa uamuzi kwani huo uamuzi wake unawaathiri zaidi wananchi na siyo yeye wala Waziri Kigoda.

Bw. Alli Maalim mkazi wa Tabata Aruma jijini yeye amechukulia suala hilo kuwa kufuatia viongozi kuzoea Umeme wa bure ndio maana hata hawawezi kwafikiria wananchi ambao wanapata pesa ya kununulia umeme huu kwa kutokwa na jasho karibu ‘la damu’.

Yeye (Rais Mkapa) wakati wote umeme upo tu hata siku moja hakatiwi. Sasa unafikiri atasikia uchungu kuwatoza watu gharama kubwa? alihoji.

Bi. Zainabu Kashaga, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Alli alisema kuwa tatizo hili linatokana na kuwa shirika moja linalozalisha umeme ndio maana kila mtu anataka apandishe ama kushusha bei kama anavyojisikia yeye mwenyewe.

"Rais amejisikia kupandisha bei ya umeme kwa vile anaona TANESCO pekee ndiyo mzalishaji wa umeme hivyo anaona hata akipandisha bei bado wananchi wataendelea kununua tu," alisema.

Kwa kuongeza kwenye maoni yaliyotolewa na Bi. Zainabu mkazi mwingine wa Mtoni Mtongani jijini aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Mwanyika Msuya, alisema kuwa Serikali kama inaona mzigo wa kuzalisha umeme ni mkubwa basi iruhusu makampuni binafsi ambayo yatakuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo bila kuwawekea masharti magumu.

"Iwaruhusu watu binafsi hata kusambaza umeme kwa nguzo zao badala ya kulazimisha waupitishe kwenye gridi ya taifa ili watozwe pesa nyingi na kuwafanya walazimike kuuza umeme ghali," alishauri.

Julai mwaka jana Waziri wa Nishati na Madini Bw. Abdalah Kigoda alitangaza kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kuwa serikali inakusudia kupunguza gharama za umeme kwa asilimua 30 hadi 50 .

Waziri Kigoda akarudia kauli yake hivi karibuni alipofungua mkutano wa 30 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TANESCO huko Morogoro.

Kauli hiyo ya Waziri Kigoda imekuja kufutwa na Rais Benjamini Mkapa aliyetangaza kuwa serikali haikusudii kupunguza viwango vya gharama za umeme.

Rais aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihutubia mamia ya wakazi wa mji wa Babati mkoani Arusha ambapo alizindua mradi wa umeme wa Electricity Four.

 

Msitumie misamaha kuyanyanyasa makanisa- Warsha

Na Josephs Sabinus

WATU wenye tabia ya kuyafanyia makosa makanisa kwa lengo la kuomba radhi baadaye, wametakiwa kujitambua kuwa wanafanya makosa yanayostahili kuadhibiwa kiroho na kisheria na hivyo kuachana na tabia hiyo mara moja.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mshauri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Mafunzo wa Shirika la CORATAFRICA Bw. Arthur N. Shoo, katika warsha ya siku tano juu ya maendeleo, uendeshaji mikutano, uandishi wa michanganuo na namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano iliyoandaliwa na ofisi ya Wamama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa (RWSAT) na kuwashirikisha Wamama Wakuu na wawakilishi wa mikoa na majimbo wa RWSAT toka kanda tano.

Katika warsha hiyo iliyodhaminiwa na shirika la CORATAFRICA, Bw. Shoo alisema imezuka tabia ya baadhi ya wanajamii kufanya makosa makusudi kwa watu wa kanisa ili baadaye wakaombe radhi. Alisema kuomba radhi pekee na kusamehewa hakusaidii katika kuepuka kurudia makosa na kuyafanya mapenzi ya Mungu, bali cha cha msingi ni kujiuliza kama hiyo radhi unayoiomba inatoka moyoni au ni ya juu juu tu.na kwamba wanaoomba radhi kijuujuuu kwa makusudi hayo lazima wajitambue kuwa wanastahili kuadhibiwa na jamii.

"Mwingine anaamua kumuibia hata sista kwa kuwa anajua masista na watu wa kanisa ni wenye huruma, watamsamehe. Tabia hiyo haina budi kukomeshwa na hata wanaofanya vitendo hivyo bila dhamira njema wakati wa kuomba radhi wanapokosea, wanastahili kuwa displined," alisema Bw. Shoo.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha hiyo iliyafanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar Es Salaam, Katibu Mkuu wa Shirika la kitawa la RSAT na Mkurugenzi wa CPT, Padre Vic Missiaen, Katibu wa RWSAT, Sista Fides Mahunja alisema wakina mama hawana budi kufutilia mbali dhana ya kusubiri kupangiwa shughuli zao za maendeleo kwani hali hiyo inachangia mno kukwamisha na kubaki nyuma kimaendeleo ya jamii husika.

"...tusipojipangia wenyewe mipango yetu, wengine watatupangia." alitahadharisha Sista Mahunja.

Katibu huyo wa RWSAT ambayo moja ya majukumu yake ni kutoa elimu kwa wanachama wake, alisema inafurahisha kusikia kuwa baada ya awamu ya kwanza, tayari wahasibu na mameneja wa miradi na makatibu wa mshirika wameweza kukaa na kujadili kwa pamoja masuala ya fedha katika misingi ya uwazi na ukweli.

Aidha, Sister Mahunja aliishukuru CORATAFRICA kwa kuzidhifadhili warsha mbalimbali za RWSAT na kuwafanya wanachama wake kuwa wa kisasa kutokana na vitabu na majalida mbalimbali inayowatumia. CORATAFRICA na RWSAT ziliamua kwa pamoja kuwa warsha za namna hii zifanyike mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja kama ilivyokuwa awali.

Kanisa lashauriwa kuzitumia zaidi jumuia ndogondogo kujiimarisha

Na Peter Dominick

KANISA Katoliki nchini limeshauriwa kufanya kazi kwa kuzishirikisha zaidi jumuia zake ndogondogo ili kujiimarisha zaidi na hivyo kuzidi kujiongezea zaidi waamini wa kweli na wenye utii.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Msaidizi wa Jumuia ya Mtakatifu Yuda Thadei ya Mtoni katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Bw. Anatori Karugaba katika maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa jumuia hiyo.

Alisema wakati huu Kanisa linapoelekea kusherekea Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, ni vema likaimarisha zaidi huduma zake kwa kuzishirikisha zaidi jumuia ndogo ndogo za kikristo ili kuyatambua kiurahisi matatizo yaliyopo ndani ya familia za Kikristo kwa kuwa ndizo zinazowafahamu waamini wa kweli na kwamba halina budi kusikiliza zaidi na kuyaheshimu maamuzi yake.

"Kwa mfano hapa kwetu, tuna kawaida ya kufanya sensa ili kupata idadi kamili ya Wakristo wa kweli na wale wanaobainika kuyumba, hufanya mazungumzo nao ili wajirudi."Alisema na kuongeza kuwa jumuia ndogondogo zina umuhimu mkubwa katika kuchangia maendeleo ya Kanisa endapo zitashirikishwa kikamilifu na kwamba kuongezeka kwa idadi familia toka 83 ilipoundwa hadi 133 ni ishara tosha kuonesha kuwa ni zenye umuhimu wa pekee.

Bw. Kagaruba aliongeza kuwa makusanyo ya shilingi 89,000/= katika kipindi cha mavuno yamebainisha kuwa jumuia yake ina msimamo na mwelekeo mzuri katika Kanisa.

 

Wanavijiji wamshukuru Papa kuwaepushia ulazima wa kwenda Roma

Na Leocardia Moswery

WANAVIJIJI wa Mbande, Mipeko, Mlamleni na Chamazi wamemshukuru Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II kwa kile walichokisema kuwaepushia gharama za kwenda Roma kwa kuwasogezea hija hadi nyumbani.

kile walichosema kuwa amewaletea Hija nyumbani ambapo kila mtu ameweza kuhiji bila garama yoyote wakiwemo wazee pamoja na waumini wengine.

Akiwapongeza wanavijiji hao hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kigango cha Mbande Bw. Geogre E. Mitawa, alisema katika sherehe za mkesha wa Msalaba wa Jubilei kuwa Baba Mtakatifu aliweza kuzindua msalaba huo kama ishara ya kuhiji katika maeneo ya nyumbani na hivyo kuwawezesha waamini wote wakiwemo wazee, watoto na wasio na uwezo wa kifedha kushiriki hija bila kulazimika kugharimia kwenda Roma kwa kutumia mamilioni ya pesa.

Alisema kuwa hija hiyo iliyowafikia hadi nyumbani, imewagusa kiroho watu wote waliokuwa nyuma na kuweza kushirikiana na waamini wengine kitendo ambacho kimeonyesha matumaini makubwa na kuwafanya wajitokeze kupokea msalaba kwa wingi wakiwemo Waislamu walioshiriki kwa upendo hadi mwisho wa ibada hiyo kigangoni hapo.

Bw. mitawa amewashukuru wanakarstimatic kwa nyimbo za mkesha ambazo zilisaidia kuhamasisha watu kukosa nafasi ya kulala katika mkesha wa Bwana Yesu Kristo na pia amewataka kurundi tena katika uhamasishaji zaidi wa sala na menginevyo.

Mashirika ya kigeni yaathiri elimu ya dini mashuleni

Na Getruder Madembwe.

Idadi kubwa ya Mashirika yasiyo ya kiserikali imeathiri kwa kiasi kikubwa elimu ya dini itolewayo mashuleni kwani yanawaajiri kwa mshahara mkubwa walimu waliojitolea kufundisha bure na kuwafanya kukimbilia huko.

Akitoa taarifa katika warsha ya siku tano ya watendaji wa Idara za Katekesi katika majimbo iliyofanyika hivi karibuni jijini,Katibu Mtendaji wa Idara ya Katekesi katika Jimbo Katoliki la Rulenge, Padri Remegius Bukuru, alisema kuwepo kwa mashirika mengi yanayoajiri walimu kwa mishahara mikubwa, kumesababisha baadhi ya walimu waliojitolea kufundisha Somo la Katekesi, kuacha kufanya hivyo ili kufuata mishahara mikubwa.

"Baadhi ya walimu walionesha moyo wa kukubali kufundisha somo hili la Katekisi mashuleni mwao lakini, baada ya mashirika haya yasiyo ya kiserikali yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa kuanza kuajiri kwa kiwango kikubwa cha mshahara wale walimu waliokubali kufundisha hilo somo waliacha kufundisha" alisema Padre Bukuru.

Padri Bukuru, alisema kuwa tatizo lingine lilonakwamisha ufundshwaji wa somo hilo, ni walimu wakuu wa shule za jimbo hilo kuwa na tofauti kiimani.

Akifafanua hoja hiyo, Padre Bukuru, alisema kuwa utakuta baadhi ya walimu wakuu ni Waangalikana au Walutheri na hivyo kusababisha Wakatoliki amabao wanasoma mashuleni kwao kukosa somo hilo la Katekesi.

Wakati huo huo: Jimbo Katoliki la Lindi limeanzisha mradi wa ufugaji wa nguruwe ikiwa na lengo la kuwasaidia watu kujikimu na hali ngumu ya maisha kwa kuwakopesha nguruwe hao ili wawalipe baada ya kuwazalishia.

Mkurugenzi Idara ya Katekesi wa Jimbo hilo Padre Amandusi Chilumbi alisema kuwa mradi huo una muda wa miaka mitatu tangu kuanzishwa na una jumla ya nguruwe 31

Komba aitaka jamii kukemea maovu

Na Neema Dawson

MJUMBE wa NEC, (CCM) Kapteni John Komba, amemeitaka jamii yote kuyakemea matendo maovu yanayofanywa bila kujali wadhifa, rika au nafasi ya mtu kimaisha ili kuiweka jamii katika miendo iliyo bora.

Wito wa Kapteni Komba umefuatia ongezeko na kushamiri kwa mmomonyoko wa madili ndani ya jamii huku ukiwahusisha wasanii mbalimbali wa vikundi vya burudani na hata viongozi wa vikundi vya dini wasiofuta maadili ya kazi zao za kichungaji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini hivi karibuni,Kapteni Komba aliwasisitizia waandishi hao wa vyombo mbali mbali vya habari nchini kuyakemea mabadiliko kadhaa ya mienendo ya jamii yanayojitokeza na kupelekea kuporomoka kwa maadili ambayo endapo hayatakemewa, jamii nzima itaathirika.

"Utakuta kikundi fulani cha sanaa au maonyesho ya burudani kinatumbuiza na watu wanokuwepo wengine wanajifanya wameguswa sana na ujumbe uliotolewa na kuamua kuingia kucheza na hata wengine kufikia hatua ya kuvua nguo na kubaki uchi bila kujua watu wanao kuwepo mahali hapo. Hali hiyo inakuwa ni ya aibu sana kwa jamii nzima," alisema Kapteni Komba.

Aliwahimiza waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kukemea maovu hayo ikiwa ni pamoja na kuwaandika kwa kuwataja majina yao katika vyombo vya habari ili waepuke kujihusisha na vitendo hivyo kwa kuhofia kutolewa kwenye vyombo vya habari.