Kanisa Katoliki lapata uongozi mpya

Askofu Samba ampisha Niwemugizi, apongezwa kwa kazi nzuri

Maaskofu wote wakutana Dodoma kwenye maadhimisho ya Ekaristi

Waamini waalikwa kuungana na wenzao duniani

Na Waandishi Wetu

Wakati Kanisa Katoliki nchini, chini ya Baraza lake la Maaskofu, limepata marubani wapya wa kuliongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitatu baada ya uongozi uliokuwapo awali kumaliza kipindi chake, karibu maaskofu wote wanatarajiwa kukutana katika Maadhimisho ya Ekaristi yanayofanyika kitaifa Jumapili hii jimboni Dodoma.

Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), imewahimiza Wakatoliki nchini kujitokeza katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, yatakayofanyika kitaifa Jimboni Dodoma, Jumapili hii na kutarajiwa kuhudhuriwa na maaskofu wote.

Katibu wa Idara hiyo ya Kichungaji, Padre Theobald Kyambo, alitoa wito huo wakati wa sherehe za Mama Bikira Maria zilizofanyika Jumapili iliyopita katika u parokia ya Kawe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Alisema Wakristo wote nchini hususani Wakatoliki, wanaalikwa na hawana budi kuungana na wenzao wa maeneo mengine duniani katika kuiadhimisha kwa shangwe, furaha na matumaini, siku hii ya Ekaristi ili kumuomba Mungu awaimarishe zaidi katika kutafuta, kulinda na kudumisha amani na upendo aliouacha Bwana Yesu Kristo.

"Hii ni nafasi ya pekee tunayopewa na Kanisa kuonesha heshima yetu kwa Yesu Kristo Mkombozi wetu," alisema.

Kanisa kote ulimwenguni linaadhimisha Siku ya Ekaristi ambapo kitaifa (Dodoma), itahudhuriwa na maaskofu wa majimbo yote nchini.

WAKATI HUO HUO: Akitaja uongozi mpya katika Baraza wakati wa ibada ya wiki iliyopita katika kanisa la TEC, kuwashukuru na kuwapongeza maaskofu waliopata Daraja hilo la Uaskofu kwa miaka ya hivi karibuni, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alisema, Mkutano Mkuu wa maaskofu uliofanyika jijini hivi karibuni, ulimchagua Askofu Severine NiweMugizi, wa Jimbo la Rulenge, kuwa Rais mpya wa TEC.

Alisema Makamu wa Rais wa TEC, ataendelea kuwepo yeye mwenyewe (Pengo) wakati, Padre Pius Rutechura, amekabidhiwa nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Baraza hilo.

Viongozi wengine, waliopata nafasi ya kuongoza idara mbalimbali za TEC, ni, Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, ambaye amekabidhiwa Idara ya Fedha, akiwa Mwenyekiti na Katibu wake ni Bw. Manasse Kally ambaye anakaimu nafasi hiyo.

Awali, Kardinali Pengo, ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Idara hiyo.

Idara ya Mawasiliano, inaongozwa na Askofu wa Jimbo la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi na Katibu wake, ni Padre Raphael Kilumanga ambaye pia anakaimu.

Idara ya Elimu, haikuguswa na mabadiliko na hivyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Norbert Mtega, anaendelea kushikilia usukani sambamba na Katibu wake, Padre Elias Msemwa.

Askofu Tarcius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa, anaongoza Idara ya Liturujia akiwa Mwenyekiti na Katibu wa Idara ni Padre Julian Kangalawe.

Wengine wanaoliongoza Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ni Mhashamu Telesphor Mkude, wa Jimbo la Morogoro, anayeiongoza Idara ya Katekesi na Katibu ni Sista Claudia Mashambo.

Idara ya CARITAS, Mwenyekiti ni Askofu wa Jimbo la Mahenge, Mhashamu, Agapitus Ndorobo na Katibu ni Bw. Peter Maduki ambapo Askofu wa Jimbo la Same, Mhashamu Jacob Venance Koda, ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei na Katibu, ni Padre Nicholaus Segeja.

Idara ya Kichungaji imeendelea kuwa chini ya Askofu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Amedeus Msarikie ambaye ni Mwenyekiti, na Katibu ni Padre Theobald Kyambo. Nayo Idara ya Afya inaongzwa na Mhashamu Aloysius Balina, Askofu wa Jimbo la Shinyanga na Katibu wake ni Dokta Alban Hokororo.

Viongozi wengine wa baraza na tume zao zikiwa kwenye mabano ni, Askofu Mkuu Mario A. Mgulunde, wa Jimbo Kuu la Tabora (Uajiri), Mhashamu Bruno Ngonyani, Askofu wa Jimbo la Lindi, (Ekumene na mahusianao na dini nyingine), Askofu Paul Ruzoka wa Jimbo la Kigoma (Haki na Amani), Askofu Gabriel Mmole wa Jimbo la Mtwara (Wahamiaji na Wasio na Makazi Maalumu).

Wengine ni Askofu wa Jimbo la Musoma, Mhashamu Justin T. Samba (Sheria za Kanisa), Askofu Damian Kyaruzi, wa Jimbo la Sumbawanga (Magereza na Majeshi), Askofu wa Jimbo la Mbulu, Mhashamu Juda Thadei Ruwa’Ichi, (Teolojia), Askofu Augustine Shao, wa Jimbo la Zanzibar, (Uinjilishaji) na Askofu Nestor Timanywa, wa Jimbo la Bukoba, (Watawa).

Katika ibada hiyo, Kardinali Pengo aliwaambia waamini Wakatoliki kuwa wana kila sababu ya kujivuna kwa kuwapata maaskofu wanaokubalika na kujituma katika kulieneza Neno la Mungu.

Alisema muundo wa maaskofu wa TEC, ni mfano bora wa kuigwa kwa kuwa hakuna hata askofu mmoja anayejiona wa maana kuliko mwingine tofauti na ilivyo kwa baadhi ya madhehebu mengine ambapo maaskofu ndio wanaonekana kuwa vyanzo vya matatizo na uelewano mbaya baina ya waamini, "Katika Baraza hili, hakuna askofu anayejiona yeye ni mrefu kuliko mwingine," alisema. (Picha katika chati ya uongozi huo, Uk. 6)

BAADA YA KUDAI KADHI MKUU WA WAISLAMU:

Biblia ni jibu wamchachamalia Mrema

Wamtaka afafanue makafiri ni akina nani

Na Dalphina Rubyema

Kikundi cha Kikristo cha Huduma ya Biblia ni Jibu, kimemjia juu Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha upinzani cha TLP, Bw. Augustine Mrema na kumtaka afafanue kauli yake ili ieleweke makafiri ni akina nani.

Mkurugenzi wa Huduma ya Biblia ni Jibu, Mwinjilisti Cecil Simbaulanga, ameliambia KIONGOZI kwa maandishi kuwa, kauli aliyoitoa Bw. Mrema kuwa kesi nyingi za migogoro ya Waislamu, zinaamriwa na "makafiri", haiwezi kufumbiwa macho na kwamba Mwenyekiti huyo wa TLP, hana budi kutoa ufafanuzi wa kutosha kwa Watanzania.

Alisema bila suala hilo kufafanuliwa na kufanyiwa tafakari ya kina katika vipengere vyake, ipo hatari ya Watanzania kukumbatia na hata kuvichagua vyama vya ajabu ajabu vitakavyoeneza udini nchini.

"...Serikali na chama tawala huwa vinatukumbusha kauli za Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, juu ya kukumbatia udini, ukabila ujimbo kuwa ni hatari kwa taifa letu. Hata Rais Benjamin Mkapa huko Dodoma, alikemea jambo hili katika kipindi hiki tunachoelekea Uchaguzi Mkuu,

Tayari sisi wananchi tunashuhudia baadhi ya vyama vya upinzani, dhahiri vinaotesha mizizi ya udini jambo ambalo linatuchanganya sisi wananchi wapenda amani." Inasema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza,

"... Kauli hii ya Mrema ina vipengele vingi sana vya kutafakari bila kufanya hivyo, tutajikuta sisi wananchi tunakumbatia vyama vya ajabu ajabu."

Akianza kuchambua juu ya kauli kuwa hakuna Uislamu nchini bila Kadhi...(SOMA BARUA KAMILI KWA BW. MREMA Uk. 4)

Makamba ajifananisha na malaika

Asisimua wananchi kwa hadithi tamu

Na Arnold Victor

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusufu Makamba, hivi karibuni aligeuka kiburudhisho tosha katika mkutano wa hadhara aliohutubia wilayani Temeke, jijini baada ya ufunguzi wa Shina la Wakereketwa wa chama hicho.

Mara baada ya kufika katika eneo la mkutano, Mtoni Bokolani, eneo ambalo linakaliwa na idadi kubwa ya Waislamu, Luteni Makamba alifungua mkutano kwa salamu ya Kilokole, "Bwana Asifiwe," na kujibiwa "Aaaamen."

Baada ya kugundua kwamba sauti zilizojibu ni za watu wachache, Makamba, hakukosa la kusema, akaanza kwa kunukuu Biblia. " Kumbukeni Biblia inasema: Msiache kuwapokea wageni, maana kwa jinsi hiyo mnaweza kuwapokea malaika," alisema na kuendelea: Hivyo mjue kupokea wageni ni Amri ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hiyo nastahili kupokelewa, mtajuaje kwamba mimi ni malaika?"

Kisha, Makamba ambaye ni miongoni mwa viongozi wachache wenye ucheshi wa hali ya juu na wachekeshaji wawapo jukwaani, akasimulia hadithi inayoihusu familia ya baba yake.

" Wakati fulani, mimi nilipokuwa bado kijana, baba yangu na mama yangu waligombana. Baba akaamua kumpa mama talaka. Hali hiyo haikunipendeza," akasema Makamba na kuendelea:

"Nikamwendea baba na kumuuliza tatizo hasa lilikuwa nini hata akafikia uamuzi huo. Akanijibu kwa kusema tatizo ni kwamba mama yako ana makapu mawili," Makamba anasema alishitushwa na jibu hilo na akadodosa zaidi ili apate ufafanuzi.

"Baba akaniambia, mama yangu ana makapu mawili, moja amelitundika bega la kushoto na jingine kulia. Lile la kushoto limetoboka na lile la kulia ni zima," alieleza na kuongeza: Baba akaniambia-mema yote ninayomtendea mama yako anayaweka kwenye kapu la kushoto na makosa yote kwenye lile kapu zima la kulia. Sasa, kila anapochungulia anayaona yale mabaya tu, mema yote yamemwagika."

Baada ya hapo Makamba alisema, alikwenda kwa mama yake ambako pia alikutana na mfano huo huo.

"Tayari baba alishaandika talaka mpaka za ukoo wa mama na hata makaburi ya kwao. Lakini nikamwambia baba: Mimi nina jina la baba yako (Makamba ni jina lake la babu) kwa hiyo mimi ni baba yako, nikazichana zile talaka mbele yake.Wakati wote huo wananchi walikuwa wamekaa kimya wakisikiliza kwa makini kama vile babu anavyokaa na wajukuu zake kando ya moto usiku wa mbalamwezi na kuwapigia hadithi.

Hatimaye Makamba akapasua jipu. " Hivyo ndivyo walivyo wapinzani wengi wa CCM. Wanasema eti CCM haijafanya lolote jema kwa nchi hii, wao wana makapu mawili, waambieni wawaoneshe mema yalikomwagika."

Luteni Makamba alimshutumu Mwenyekiti wa CUF-taifa Profesa Ibrahim Lipumba, kwa kudai kwamba kama CCM haijafanya lolote alisomasomaje hadi kuwa Profesa.

Hivi karibuni Lipumba alikaririwa akisema kuwa CCM haina lolote la kujivunia na kwamba imewarudisha wananchi wa Tanzania nyuma na haijafanya lolote zuri nchini.

Makamba pia aliiponda sera ya CUF ya jino kwa jino, akisema kwamba hata vitabu vitakatifu vinapingana nayo.

Alisema katika Biblia Yesu alisema, "Akupigaye shavu moja, mgeuzie na la pili, na akunyang’anyaye kanzu yako mpe na joho pia."

Katika Kuran Tukufu, Makamba alisema kuna kisa kimoja ambapo jirani mmoja wa Mtume Muhammad, alikuwa akimchokoza kwa kujisaidia kila siku asubuhi mlangoni kwake na Mtume akawa anazoa kile kinyesi kwa siku tano mfululizo bila kulalamika wala kumchukulia hatua. Siku moja, Makamba alisema, Mtume alipoamka na kukuta hamna kinyesi, akamuulizia yule jirani akaambiwa anaumwa na akaenda kumpa pole.

"Yule jirani alimuuliza, umejuaje naumwa? Mtume akamwambia leo sijaona kinyesi. Basi yule mtu akaamua kuanzia siku hiyo asilimishwe. Sasa kama Mtume angeleta sera kama za wenzetu (CUF) huyu jamaa angesilimu?" alihoji.

Maalbino walilia makanisa, vyama vya siasa

Mwenyekiti asema kansa inamuua na mkewe

Na Josephs Sabinus

WAKATI nchi inaelekea Uchaguzi Mkuu, maalbino 1800 wa mikoa ya Dar-Es-Salaam na Pwani, wamevililia vyama vya siasa na vikundi vya dini kuwapa msaada wa miavuli ili kunusuru afya na maisha yao.

Akizungumza na gazeti hili jijini, Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi wa Jamii na Uchumi Tanzania, Bw. D. Nicholaus Lameck, alisema katikati ya juma kuwa kiasi cha miavuli 1800 sawa na shilingi 4,500,000/=, kinahitajika ili kuyanusuru maisha ya albino hao yaliyopo hatarini kutokana na kuathirika sana na kansa ya ngozi inayosababishwa na mionzi ya jua.

Alisema kwa kukosa miavuli, yeye mwenyewe na mke wake, Bi. Mwanaisha Athumani (30), tayari wamekwisha athirika na ugonjwa wa kansa ya ngozi; wote kwa miaka sita mfululizo na kwamba baada ya kuteseka, maalbino hao, wameona kimbilio lao pekee, ni katika makanisa na vyama vya siasa ili wawaokoe kwa kuwa ndio tumaini lao.

Alitaja misaada mingine ambayo wanahitaji kuwa ni kofia, sabuni na mafuta kwa kuwa wanalazimika kuoga mara nne zaidi ya mtu wa kawaida.

Alisema, ingawa kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakiomba misaada hiyo katika makanisa mbalimbali, bado hali si nzuri na wanazidi kuteseka mno.

"Tumeshindwa hata kuomba msaada wa kwenda kutibiwa nje na mimi hii kansa yangu ina miaka 6 hata mke wangu nae, ina miaka 6.

Sasa tunasubiri tu, mapenzi ya Mungu kwa kuwa kama miavuli inakuwa vigumu namna hii, vipi hiyo hela ya kutibiwa nje? Tunachoomba kusaidiwa ni miavuli, shida yetu siyo pesa taslimu lakini kama mtu anashindwa kutafuta miavuli, alete fedha tutatafuta wenyewe." Alisema kwa huzuni.

Alivishauri vikundi vya dini kuiga mfano bora wa mtindo walioutumia waamini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ukonga kwa kuwatangazia waamini wa misa zote tatu na wao wenyewe kuchangia kila alichokuwa nacho muamini kwa hiari na upendo wake.

Alisema kwa mtindo huo, hivi karibuni, walifanikiwa kupata msaada wa shilingi 175,000/= toka kwa waamini wa parokia hiyo na wakashauri makanisa mengine kuwasaidia kwa mtindo huo ili kuepuka kuvuruga ama kushindwa kusaidiwa kwa madai ya kuwa mifuko ya makanisa hayo hairuhusu.

Hata hivyo, alisema vyama wahisani, wanashauriwa kutumia njia yoyote wanayofikiri itasaidia.

Bw. Lameck, alisema wanawake maalbino wanaathirika zaidi kuliko walemavu wengine na kwamba jamii haina budi kuwaonea huruma mno na kuwasaidia.

"Unajua kiwete akija, utamhurumia kwa kuwa unamuona, hata asiyeona. Lakini sisi maalbino kwa kuwa tunatembea, jamii inatusahau kabisa; haijui matatizo tuliyo nayo ni makubwa na ni mateso mno.

Lakini ukweli ni kwamba tunaathirika sana kwa kuwa hata ajira hatupati hasa wanawake. Wanawake maalbino wanashida kweli kuliko hata wanaume. Hawawezi kuomba pesa wakapewa, hawapati elimu kutokana na matatizo ya macho, na bado wanazalishwa ovyo mitaani na kupata watoto bila kutaka," alisema na kuongeza,

"Tunaomba wafadhili, jamii na hata vyama vya siasa, viwasaidie kwa hali yoyote. Viwape ajira zozote; kazi ni kazi tu, hakuna anayechagua eti hii ni mbaya maana mwenye shida hachagui kazi."

Aliyashukuru na kuyataja baadhi ya makanisa ambayo yamejaribu kuwasaidia kwa kadri ya uwezo wao kuwa ni pamoja na Kanisa Katoliki la Manzese, Waadventisti Wasabato wa Mwenge, KKKT Mwenge, Anglikana Mwenge na KKKT Kijitonyama.

Maalbino ni walemavu wa ngozi na macho na huathirika sana wanapotembea juani bila kofia ama mwavuli na huathirika zaidi wakikosa mafuta ya kulainisha ngozi.

Watoto huwa hawaoni vizuri na hivyo, kutokufanya vizuri kimasomo na kwa maana hiyo wana maisha magumu kwa kuwa wengi wao hawana kazi kwa kuwa hawakusoma vizuri.

Viongozi wengi wa dini wanatafuta kujineemesha-Mchungaji

Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI wa dini na waamini wanaovuruga amani makanisani mwao ili wajitenge na kuanzisha madhehebu yao, wameshauriwa kuacha tabia hiyo kwa kuwa sio mpango wa Mungu, bali ni tamaa za kibinadamu kutaka mali na madaraka zinazolenga kuwaneemesha kibinafsi.

Hayo yalisemwa mwanzoni mwa juma lililopita wakati Mchungaji wa Kanisa linalojiita, Fire Gospel General International Church, lenye makao yake eneo la Kurasini Shimo la Udongo jijini Dar-Es-Salaam, Samson J. Mushy, akizungumza ndani ya ofisi za gazeti hili.

Alisema baadhi ya viongozi, kutokana na tamaa za kujineemesha, wamekuwa vyanzo vya kusambaratika na kuyahama makanisa yao ya asili kwa kuwa wanachochea vurugu ili wajitenge na dini zao na hivyo kufaidi kibinafsi michango ya waamini na wafadhili bila kuzingatia mapenzi ya Mungu.

"Wengine wanaleta chokochoko kwa kwenda makanisani, wanasali lakini hawafuati Amri za Mungu. Hawamtii bali wamepagawa tu, na roho za shetani zenye machafuko ya kila aina, vita, mauaji ya kishetani. Wanapanga hata mipango mibaya ndani ya makanisa na misikiti yao."

"Tukiachana kwa kuwa tumegombana huku tukinyang’anyana na kila mtu akaenda kuanzisha dini yake, unakuwa si mpango wa Mungu. Mpango wa Mungu kuanzisha makanisa namna hiyo, ni pale ambapo mmeachana kwa kuwa mazingira yamewalazimisha. Labda mmefukuzwa; huyu akaenda huku na huyu akaenda huko, mkaanzisha makanisa ili kueneza zaidi Neno la Mungu," alisema.

Alisema uzoefu wake binafsi, unaonesha kuwa makanisa mengi yaliyoanzishwa kwa miaka ya hivi karibuni, yametokana na ugomvi ndani ya makanisa asilia hali aliyosema haina budi kuogopwa na kila mwenye mapenzi mema.

Hata hivyo, Mchungaji Mushy, alishindwa kuwa wazi endapo kwa maneno yake, yeye mwenyewe yuko tayari kujiunga na kanisa lingine ili kuondoa ubinafsi aliousema ndio unachochea ongezeko la utitiri wa makanisa.

Mchungaji Mushy, alionya kuwa viongozi wenye kuanzisha makanisa kwa lengo la kukidhi tamaa zao, ni hatari na wako tayari kuiangamiza jamii kimwili na kiroho ili mradi tu, wajinufaishe wao wenyewe kwa namna wanayoweza na akadokeza kuwa ndiyo sababu mara nyingi makanisa mengi hupata migawanyiko kabla hata hayajakomaa.

Alisema wakati taifa linaelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, mwaka huu, jamii haina budi kuwa makini, tulivu na watunza amani ili waombe na kuwapata viongozi wazuri kwa kadri ya mipango ya Mungu.

"Mungu mwenyewe alishatuchagulia viongozi wetu. Hivyo, lakufanya ni watu kutumia busara, amani na upendo kuwachagua kwa utulivu na amani," alisema.

Wizara, NGO's waombwa kuwaongeza mikopo vijana

Leocardia Moswery na Elizabeth Steven

ILI vijana waweze kujikwamua kimaisha, Wizara ya Mambo ya Ndani na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs),vimeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kwa vijana kwa kuwa kinachotolewa hakitoshi.

Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa juma na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Kikristo (Christian Workers), Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Bw. Cyrilo Lubinga, wakati akizungumza katika ofisi za gazeti hili jijini.

Alisema mkopo wa shilingi 50,000 unaotolewa hivi sasa hutolewa na Wizara au, baadhi ya NGO’s, hauwasaidii kitu katika kuinua hali zao kimaisha na uchumi wa taifa kwa ujumla kwa kuwa ni kidogo mno na hakichochei maendeleo.

Alisema kwa hali halisi ya maisha ilivyo, licha ya baadhi ya vijana kupata mikopo hiyo, bado wanashindwa kulipa kodi ya nyumba, matibabu na mahitaji mengine ya lazima ukiwemo usafiri kwa ajili ya shughuli zao.

"Mikopo inayotolewa kwa vijana haitoshi kabisa!, 50,000/= ni kiasi kidogo sana; ndiyo maana wengi wanaiweka katika biashara isiyokuwa hata na leseni; hii ya umachinga.

Hata huyo Mmachinga, sasa anatembea kwa miguu toka Mbagala hadi Bunju, bila kuuza nguo hata moja matokeo yake, unakuta huo mkopo mzima unaishia kwenye kula," alisema.

Makamu huyo aliongeza kuwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali, hayana budi kuelewa kuwa vijana wanahitaji mikopo yenye kiasi kikubwa cha pesa ili wamudu gharama za uendeshaji wa miradi wanayoanzisha na hivyo, kuziboresha hali zao za maisha.

"Lengo siyo wawe matajiri, bali wanachohitaji, ni ule mkopo utakao wawezesha kujikwamua na kuwezesha kujimudu kimaisha hata wanapotaka kuoa au kuolewa, waweze kuhudumia familia zao bila kumalizia mikopo yao katika kula tu," alisema.

Polisi waambiwa wasibweteke vituoni

Na Neema Dawson.

JESHI la Polisi nchini limeshauriwa kuacha kukaa vituoni mwao tu, kusubiri kupelekewa taarifa za uharifu badala yake, lishirikiane kwa karibu na wananchi kuwasaka waharifu.

Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Bw. John Mgeja aliyasema hayo wakati akifunga mkutano juu ya utekelezaji wa mpango wa miji salama, ulioandaliwa na Tume ya Jiji la Dar-Es-Salaam, kupata matokeo ya utafiti juu ya uhalifu jijini Dar-Es-Salaam.

Takwimu za Jeshi la Polisi zinabainisha kuwa,kati ya asilimia 25-27 ya matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi nchini, yaliyotokea jijini Dar-Es-Salaam.

Katika kipindi cha miaka ya 1995-1997 kumekuwepo na ongezeko la asilimia 8 kila mwaka kwa matukio ya uhalifu jijini.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1990 hadi 1999, matukio yaliyoripotiwa kwenye vituo hivyo kila baada ya saa moja, yaliyoongezeka kwa asilimia 56.

Takwimu hizo zinaonehs kuwa, kati ya asilimia 7-10 ya matukio ya uhalifu yanaotokea katika jamii hayaripotiwi katika vituo vya polisi.

Aidha Bw. Mgeja alisema kuwa, uhusiano wa polisi na raia na hasa viongozi wa serikali za mitaa, kata, jumuiya na taasisi mbalimbali, unatakiwa kuimarishwa zaidi.

"jamii nayo haina budi kuwa inazingatia na kuyaelewa matatizo ya polisi katika utekelezaji wa kazi zao, ambayo ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi.

Hata idadi ndogo ya askari tulionao kwa kuwa takwimu zetu zinaonesha kuwa kuna askari mmoja kwa kila kaya 200 hadi 300 au hata 1000 hivyo tatizo la uhaba wa polisi linaweza kupatiwa ufumbuzi unaostahili pale ambapo polisi watashirikiana zaidi na vikundi vya Sungusungu, mgambo na vikundi vingine vinavyojitokeza katika jamii," alisema.

Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Karimjee. Ulifunguliwa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Kingunge Ngombare Mwiru na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam, Luteni Yusufu Makamba, mabalozi, na viongozi wengne toka nje na ndani ya jiji la Dar-Es-Salaam.

Ioneni Jubilei kama dhahabu- Askofu

Na Peter Dominic

BALOZI wa Papa Nchini, Askofu Mkuu, Luigi Pezutto, amewahimiza Wakristo kuichukulia Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, kama dhahabu ili wapate kuongoka kutokana na neema zake.

Balozi huyo aliyasema hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Parokia ya Mbagala, katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, iliyofanyika parokiani hapo na kuwawezesha waamini wa ndoa zipatazo 30, kurudia ahadi zao.

Alisema sasa ni wakati wa kila Mkristo kuachana na matendo, mawazo na maneno yanayokwenda kinyume na msukumo na nafsi yake ili kuifanya vema kazi ya kumtumikia Mungu.

"Kila mtu ajiulize ni kwa kiasi gani anampa Kristo nafasi katika maisha yake.

Tumshirikishe na kumpa nafasi ya kutawala," alisema.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo Bw. Emil Hagamu, alisema jubilei hiyo imefungua kampeni rasmi za kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Hija na Kigango cha Misheni Msalabani ili kulilinda eneo hilo na kuleta maendeleo ya kiroho parokiani hapo.

Hagamu alisema ujenzi huo utawasaidia waamini wa eneo hilo kwa vile ibada zitafanyika mahali hapo tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wanatembea mwendo mrefu kuelekea kanisa la Kijichi Zakhem au Kituo cha Kiroho cha Mbagala na akadokeza kuwa ujenzi huo hautathiri eneo hilo takatifu kwa kuwa utaruhusu msalaba kuonekana kwa hali halisi asilia.

Katika kufanikisha ujenzi wa kigango hicho eneo la Misheni Msalabani, zaidi ya shilingi 38000/= na zawadi zilichangwa na zitapigwa mnada kuchangia mfuko wa ujenzi huo.

Akizungumza katika hafla fupi baada ya sherehe hizo iliyofanyika katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini, (Spritual Center), Mkurugenzi wa kituo hicho, Padre, Manfred Birrer, alisema robo tatu ya waamini wa eneo hilo ambao ni zaidi ya 600 kwa misa zote tatu, wanasalia nje ya kanisa kwa kukosa nafasi ndani.

Ili kukidhi mahitaji, Parokia ya Mbagala imeandaa mikakati ya kujenga kigango katika Kituo Kitakatifu cha Hija eneo la Misheni Msalabani.

"Ingawa tunajitahidi kuweka magogo na mabenchi nje ya kanisa hatujakidhi mahitaji ya waamini wetu ambao idadi yao inazidi kuongezeka siku hadi siku," alisema na kuongeza kuwa hivi sasa watu wanaosalia kanisani hapo idadi yao inapata 1000 hivyo wengine hulazimika kuelekea makanisa ya mbali

Aliasa pia juhudi za haraka zifanyike ili kufanikisha ujenzi huo wa kigango hicho ili kujikwamua na tatizo hilo la msongamano wa waamini.

Mikakati iliyowekwa na parokia hiyo ni pamoja kuandaa fomu 50 zilizogawiwa kwa waamini ili kuchangia ujenzi na kuhimiza waamini kujitolea kwa hali na mali ili juhudi zao zifanikishe suala hilo.

Mashirika 290 yabinafsishwa

Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya mashirika 290 kati ya 385 yaliyokuwa yamekusudiwa kubinafsishwa, tayari yamebinafsishwa na hivyo kufanya zoezi hilo lifikie asilimia za mafanikio 77.33.

Msemaji wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mfumo wa Mashirika ya Umma (PSRC) Bw. Joseph Mapunda, aliliambia gazeti hili hivi karibuni jijini, kuwa ubinafsishaji wa mashirika mengine makubwa kama vile TTCL na DAWASA uko mbioni kukamilika.

Bw. Mapunda, alisema zaidi ya nchi 100 duniani zimefanya zoezi la ubinafsishaji kwa mafanikio makubwa na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeanza kuonja matunda mazuri ya mfumo huo mpya.

Alisema tofauti na inavyodaniwa na watu wengi, ubinafsishaji huongeza ajira, licha ya baadhi ya wafanyakazi kupunguzwa kutoka mashirika yanayobinafsishwa.

Alifafanua kuwa kila shirika linapobinafsishwa kiwango cha ufanisi na uzalishaji huongezeka na hivyo kuzaa tena ajira zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa na viwanda au mashirika hayo.

Raia wa Norway washangaa namna walemavu wa akili wanavyoangaliwa Tanzania

Na Seraph Kuandika Morogoro

MAAFISA kutoka chama cha ustawi wa jamii nchini Norway wameshangazwa nahali mbaya inayoikabili jamii ya walemavu hapa nchini na kuifananisha Tanzania ni kama nchi iliyo katika sayari nyingine kutokana na kutowajali watu wa aina hiyo.

Maafisa hao walitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita walipokuwa katika ziara za kutembelea maeneo ya Mvomero, Muhonda na Turiani wilaya ya Morogoro Vijijini kuangalia shughuli za kuwasaidia walemavu wa akili hususani elimu zinazoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Norway na Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili cha Amani kilichopo hapa Morogoro.

Akizungumza na Kiongozi huko Muhonda Turiani, mmoja wa maafisa hao, Solveis Nilsen, alisema hali ya kuwajali watoto wenye Ulemavu hapa Tanzania ina tofauti kubwa ya huko kwao Norway, ambako walemavu hawana tofauti na jamii ya watu wa kawaida na hupatiwa huduma kama ilivyo kwa wengine.

"Kwa jinsi tulivyoangalia hali ya walemavu katika maeneo tuliyotembelea, kuna tofauti kubwa ya kuwajali watoto wenye ulemavu wa akili ukilinganisha na kule kwetu. Hapa Tanzania ni kama ulimwengu mwingine au sayari nyingine," alisema Solveis kwa mshangao.

Aliongeza kuwa watu wenye ulemavu wana haki ya kuishi na kupatiwa huduma maalum kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote na hawapaswi kutengwa na jamii kwa namna yoyote.

Alisema nchini Norway wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma na malezi ya walemavu kwa kuwa suala hilo hushughulikiwa mapema wakati watoto wanapozaliwa ambapo hupimwa mapema kuangalia iwapo wana matatizo ya ulemavu hasa wa akili.

Ziara hiyo ya kutembelea maeneo hayo ya Morogoro vijijini iliandaliwa na kituo cha Amani, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wazazi na jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuwajali na kuwahudumia watoto wenye walemavu wa akili.

Wakati huohuo: Ujenzi wa jengo kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa akili, tarafani Mvomero wilayani Morogoro Vijijini, umesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

Jengo hilo litakalotumika kwa chakula na ukumbi wa mikutano, limejengwa na wananchi wa eneo hilo kwa msaada wa shirika la maendeleo la Norway, (NORAD) na kituo cha Amani.

Mratibu wa Utengamano wa Jamii (CBR), Bw. Japhet Wadelanga, ameliambia KIONGOZI tarafani Mvomero kuwa kiasi cha shilingi milioni 3.5, kinahitajika kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo ambalo hadi sasa limeshagharimu kiasi cha shilingi milioni moja ambapo limeishia kuezekwa bati upande mmoja.

Wapinzani waambiwa wawaogope wanaotoka CCM

Na Getruda Madembwe

CHAMA cha siasa cha National League for Democracy (NLD) kimevitaka vyama vya upinzani kuwaogopa viongozi wanaotoka CCM kwa kutowatetemekea kuwapa vyeo kwa kuwa wengine huingia katika upinzani wakiwa hawana nia nzuri.

Akizungumza na gazeti hili katikati ya jumajijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Vijana ngazi ya Taifa wa chama hicho, Livingstone Joseph Lusinde, alisema kuwa watu hao ni waongo na wala hawana upendo wa kweli katika vyama wanavyohamia toka CCM.

Akitoa mfano wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Bw. John Guninita, aliyeamua kukihama CCM na kwenda CHADEMA ambako alipewa wadhifa wa Katibu Mwenezi ngazi ya taifa.

"Sisi wapinzani tunatakiwa tuwaogope watu hao sababu sio kweli wanakuja kutuletea maendeleo kwani wao walishindwa kuleta maendeleo walipokuwa CCM, sasa wataweza kuleta maendeleo hayo kwenye upinzani?" alihoji Bw. Lusinde.

Aliongeza kuwa, wao kama wapinzani, wanachotakiwa kufanya ni kuwaandaa watu wao wenyewe na wala sio kuwategemea wale ambao wanataka CCM kwa kuwa eti majina yao ni maarufu na akasema kuwa umaarufu wa chama hautokani na mtu mmoja bali wanachama wote.

"Sio sifa kuwachukua watu kwa kujiambia kuwa eti watu hao wanafahamika na chama chetu kitajulikana eti sasa, tuwaweke katika uongozi." alisisitiza Bw. Lusinde.

Lusinde ambaye amekwishachukua fomu ili kugombea Ubunge katika Jimbo la Kawe kupitia chama hicho cha NLD, amevionya vyama vya upinzani kutoendesha upinzani kama kioo cha kuionesha CCM makosa yake na hivyo kuipa mwanya wa kujirekebisha kabla uchaguzi haujafika.

"Unajua kama chama cha upinzani kikitoa makosa CCM wanarekebisha maana hivyo sio vizuri tunafanya upinzani kuwa kama kioo cha CCM kwani mtu akijiangalia katika kioo akiona makosa sehemu yeyote, hujirekebisha na CCM nao wanajirekebisha," alisema Bw. Lusinde.

Hivi karibuni kumekuwa na mishangao baada ya baadhi ya viongozi wa waliojitoa CCM na kujiunga na vyama vya upinzani kwa maneno mengi dhidi ya chama hicho tawala, kuvihama tena vyama walivyohamia na kurudi CCM ile ile.

Miongoni mwao ni Bw. Guninita ambaye katikati ya juma lililopita, alikihama CHADEMA na kurudi CCM.

Wengine ni Dk. Masumbuko Lamwai na Makongoro Nyerere walio kuwa NCCR Mageuzi.

Ruzuku yatakiwa kujenga shule ya Shauritanga

Na Leocardia Moswery

JUMUIYA ya Wazazi Tanzania, imeiomba serikali kuendelea kuipa ruzuku ili izidi kuboresha huduma ya elimu na kuajiri walimu na kuzipa vifaa muhimu vya kutolea mafunzo na kujenga bweni la shule ya Shauritanga lililoungua kwa moto

Akisoma risala ya Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la jumuiya hiyo mbele ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Benjamini Mkapa, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Bw. Julius Ngalla, alisema hivi karibuni katika Ukumbi wa Karimjee jijini kuwa, ushahidi mkubwa wa jumuiya hiyo katika mchango bora wa elimu nchini, ni idadi kubwa ya vijana waliojiunga na kidato cha tano na kufuzu chuo kikuu kwa miaka minne kwa kuwa wakati huo, serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwa jumuiya hiyo ambayo ilisaidia kutoa huduma hizo.

"Hivi sasa tunashida sana na tunahitaji vifaa na walimu ili kuboresha kazi zetu," alisema.

Alifafanua kuwa pia lengo la jumuiya yake kuomba ruzuku hiyo ni kujenga bweni la wanafunzi lililoungua katika ajali ya moto ya shule ya sekondari ya Shauritanga miaka ya hivi karibuni na kuwaua wanafunzi 41, ili iwe kumbukumbu ya kudumu ya kuwaenzi marehemu vijana hao ambao taifa lilikuwa linahitaji mchango wao.

Alisema, Jumuiya ya Wazazi imekwisha fungua shule 80 za sekondari na kwamba nyingi ya hizo zipo maeneo ya vijijini ambapo wananchi hawana uwezo wa kuwapeleka wanafunzi wao katika shule za binafsi au za mbali, zinazotoza viwango vikubwa vya ada.

Padre gwiji wa habari afariki

Na John Mbonde, Songea

PADRE Mkatoliki aliyebobea katika taaluma ya habari, Gerold Rupeer OSB(92), amefariki dunia na tayari amekwisha zikwa eneo la Abasia Peramiho.

Padre Rupeer, ambaye alikuwa mahiri katika taaluma hii ya upashanaji habari, alizaliwa Julai 18, 1908 huko Switzerland na alifariki dunia Juni 21, na kuzikwa Juni 22, mwaka huu.

Alipata Daraja ya Upadre Aprili, 1933 na kisha alipelekwa Uingereza kwa mafunzo ya Ualimu.

Mwaka 1934 ,alisafiri kuja Afrika. Tangu 1934, Padre Gerold Rupeer, amekuwa akiishi Abasia Peramiho hadi kifo kilipomfika.

Katika siku za uhai wake, Padre Rupeer amemudu kazi mbalimbali kwani kati ya mwaka 1934, alianza kufundisha vijana katika seminari Ndogo ya Peramiho hadi mwaka 1938, ambapo alikuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu cha Peramiho.

Moja wapo ya mazao bora ya kazi ya ualimu ya Padre Rupeer akiwa Mkuu wa Chuo hicho, ni walimu walioazimwa kufundisha katika majimbo ya Kikatoliki ya Musoma, Mwanza, Rulenge, Kigoma, Sumbawanga, Dodoma, Mbeya, Tabora, Singida na Mahenge.

Baadhi ya wanafunzi wake ni pamoja na Mhashamu Askofu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Padre Venant Hunja, Padre Pirmin Gama, Padre Dk.Cosmas Haule na idadi kubwa ya walimu na wanataaluma mbalimbali wanaofanya kazi serikalini na katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Amepata kuwa mkaguzi hodari wa Shule (Education Secretary) zilizomilikiwa na Jimbo la Peremiho (sasa Songea-Njombe na Mbinga).

Hodari wa upashanaji habari

Amepata kuandika vitabu vingi vya kufundishia kikiwemo kile kitabu cha nyimbo "CHIRIKU". Kuanzia mwaka 1942, alianza kuchapisha kijigazeti "BARUA KWA WALIMU", halafu, akabadilisha jina na kuitwa "MAPYA NA YA KALE".

Hatimaye likaitwa" THE TANGANYIKA TEACHERS’JOURNAL" kwa kifupi "TATEJO" na kuanzia mwaka 1964 alikuwa Mhariri wa Gazeti la MWENGE.

Mwaka 1969 alianzisha gazeti la MLEZI ambalo hadi sasa linachapishwa kila baada ya miezi miwili na kuwa msaada mkubwa kwa mapadre na makatekista.

Alidhamini na kugharimia uchapishaji wa vitini vya kila Jumapili, UTAMADUNISHO KATIKA UINJILISHAJI akisaidiwa na John Mbonde na Vitus Nduguru.

Hakuchoka kugharimia uendeshaji wa semina, warsha na makongamano katika Kanda hii ya Kusini na alihakikisha kuwa nakala za gazeti la MWENGE zinawafikia wafungwa katika magereza nchini Tanzania na yanasomwa na wagonjwa, vijana katika Makambi ya kujenga taifa, jumuiya ndogondogo na vyama vya kitume katika shule zote ,vyuo vya ualimu na vyuo vingine nchini.

Changamoto katika kilimo

Kama ulivyo moyo wa Wamisionari Wabenediktini wa SALA na KAZI, ndivyo Marehemu Padre Gerold Rupeer, alivyoudhihirisha kwa kuendeleza shughuli za kilimo endelevu (Sustinable agriculture).

Alifanya kampeni kamambe mintarafu udumishaji na ukuzaji kwa nguvu zake zote juu ya matumizi ya mmea wa marejea ili kurutubisha ardhi.

Wanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine walifanya utafiti wa kina kuhusu mmea huo wa marejea.

Mwaka 1986, hayati, Julius Kambarage Nyerere, alimtunuku Padre Rupeer, Nishati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uhodari wake katika kuboresha kilimo kwa njia ya kukarabati ardhi kwa kutumia marejea na hata Hayati Padre Rupeer, alijulikana sana kwa jina la BABA MAREJEA.

Upandaji miti

Kwa kutumia vituo vya vijana alivyoasisi katika vijiji vya Butiama, Morogoro na Lindusi (MOROVITRA), vilivyopo jirani na Peramiho, aliotesha miti mbalimbali na baadaye kununuliwa na kusambazwa katika wilaya za Songea na Mbinga na kwa watu binafsi.

Hayati Padre Gerold Rupeer, alihimiza upandaji wa maharage aina ya soya na uhifadhi wa mazingira.

Hata akiwa na umri wa miaka 90, alikuwa hadari katika kazi na mkakamavu kwa kuwa pia alipenda kujihusisha na mazoezi ya viungo na kuendesha baiskeli.

Alikuwa mkarimu kwa walemavu, wasiojiweza, wazee na hasa masikini na fukara. Tunawapa pole kupitia kwako Mhashamu Abate Lambert Doerr, Mamonaki wa Abasia Peramiho, Mapadre, Watawa na wanafunzi wote mahali popote walipo ndani na nje ya Tanzania.

MUNGU AIWEKE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI, AMINA.

Kuweni na matumani, sala kuokoa roho za tohara, Padre asisitiza

Na Charles Hililla, Shinyanga

PADRE Robert Walwa, amewambia waamini wa Majimbo ya Kanisa Katoliki ya Shinyanga, Geita, Kahama, na majimbo Makuu ya Tabora na Mwanza, kuwa ni vema wawe na matumaini na sala wakati wote wa maisha yao.

Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi ya Padre Edfonce Mabula (38), katika Kanisa Kuu la Jimbo la Shinyanga, Padre Walwa, alisema wakati wa maombolezo yao, waamini hao wakiwamo walei, mapadre na watawa hawana budi kuwa na moyo wa matumaini na sala kwa kuwa Mungu hana upendeleo na hafanyi kosa anapoamua kuchukua uhai wa mwanadamu yeyote, bali hufanya hivyo anapoona inafaa.

Alisema ni ukweli huo ulio bayana, ndio maana hata Mungu alimchukua Bwana Yesu Kristo akiwa angali kijana wa umri wa miaka 33 tu."Kwa njia ya sala na misa mbalimbali, tutakuwa tunaokoa roho zilizopo toharani na sisi wenyewe kujitengenezea njia nzuri ya kwenda na kufika kwa Mungu," alisema.

Akisisitiza umuhimu wa kujiweka tayari wakati wowote, Padre Walwa alitoa mfano akiwafananisha watenda mema na wale wanawake watano waliokesha wakimsubiri Bwana Harusi pamoja na taa zao zilizojaa mafuta, ambao kama inavyoelezwa kwenye Maandiko Matakatifu, ndio waliofurahi na Bwana Harusi baada ya kufika kwake tofauti na na wale wengine wapumbavu ambao hawakuwa na mafuta katika taa zao hadi Bwana Harusi anaingia.

Marehemu Padre Edfonce Mabula, alifariki Juni 13, mwaka huu katika Hosteli ya Jimbo Katoliki la Shinyanga baada ya kusumbuliwa na kifua.Ibada ya Misa ya kumuombea marehemu ilifanyika jimboni hapo Juni 16, mwaka huu na iliongozwa na Padre Mwandamizi wa Jimbo hilo, Amedeus Ndege, akisaidiwa na mapadre Renatus Mashenene na Robert Walwa.

Marehemu alizaliwa mwaka 1962, akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto 4 wa Mzee James Mabula na mama Anastazia Holo. Alibatizwa mwaka 1962, parokiani Kilulu na kupata Kipaimara mwaka 1980 parokiani Nyegezi Mwanza.

Alipata elimu ya msingi katika shule za Ukelewe na Malili hadi mwaka 1977 alipojiunga na Seminari ya Nyegezi tangu kidato cha kwanza hadi cha sita mwaka 1984.

Aliendelea na masomo katika seminari kuu za Ntungamo na Segerea kwa masomo ya falsafa na teolojia hadi mwaka 1991, alipopewa Madaraja ya Ushemasi na Upadre.

Alipewa madaraja hayo na marehemu Askofu Castor Sekwa.

Wakati wa uhai wake, alifanya kazi mbalimbali za kichungaji katika parokia mbalimbali za Kanisa Katoliki akiwa Paroko Msaidizi. Parokia hizo ni pamoja na Busanda, Ng’wangi, Ilumya, Wila, Mipa na Buhangija.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI, AMINA