Wanaotumia makanisa, misikiti kwa siasa ni hatari waogopwe - Askofu

lAsema nyumba za ibada haziwezi kuwa uwanja wa kampeni za siasa

lAwataka wasiwafanye wapiga kura kuwa vipofu

Na Josephs Sabinus

"WANASIASA wanaotaka kutumia nyumba za ibada kutangaza sera za vyama, ni hatari kwani wanataka kuweka mgawanyo wa kisiasa ndani ya nyumba za Mungu na wanataka raia wawachague bila kujua mambo yao hata kama hawafai na hao ni wa kuogopwa sana"

"Makanisa na misikiti ni sehemu ambazo watu wa vyama vyote wanakutanika na kuabudu na siyo sehemu za kupigia kampeni za vyama vya siasa. Ukiona mwanasiasa anatumia mbinu zake au kuwafuata wanadini makanisani au misikitini ili kuwashawishi wamchague, ujue mwanasiasa huyo ni hatari, hafai na anajijua mwenyewe kuwa hafai na hakubaliki katika jamii ndiyo maana anataka atumie dini bila kujua kuwa dini zote, ni kwa ajili ya waamini na hakuna dini kwa ajili ya siasa za vyama."

Askofu Mkuu Norbert Mtega, wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, aliyasema hayo jijini Dar-Es-Salaam, alipozungumza na KIONGOZI Ijumaa iliyopita, juu ya baadhi ya vyama na viongozi wa kisiasa wanaojaribu kutumia mtandao wa vikundi vya dini kupiga kampeni za kisiasa.

Alisema hali hiyo ni hatari kwa kuwa si tu kwamba inaweza kuleta mgawanyiko wa kidini miongoni mwa vikundi vya siasa, bali pia inaweza kuwagawa waamini hao katika misingi ya kisiasa na kwamba haina budi kukemewa wapenda amani wote wenye upendo wa kidugu.

Hata hivyo, Mhashamu Mtega alisema vikundi vyote vya kidini vinalo jukumu kubwa la kuielimisha jamii kwa ujumla juu ya Uchaguzi bila bila kuwa na chaguo au ushabiki kwa chama chochote.

"Dini zote zina wajibu wa kuwaelimisha watu mambo, kanuni muhimu na athari zinazoweza kujitokeza endapo hawatakuwa makini katika uchaguzi ili wananchi wasiende kupiga kura wakiwa vipofu"

Askofu huyo Mkuu alisema anashangazwa na wanasiasa wengine wanakosea na kudhani kuwa kwa kuwaelimisha wananchi mambo muhimu ya kuelewa, kuzingatia na kutekeleza bila kuingilia wala kushabikia chama chochote, ni kuingilia siasa kitu alichosema si sahihi.

"kuelimisha wananchi hasa katika Uchaguzi huu Mkuu wa Pili wa vyama vingi ni kazi ngumu ambayo haipaswi kuachwa tu, kwa serikali na vyama vya siasa, bali hata taasisi nyingine kama dini kwa kuwa haina mwelekeo au ushabiki wowote wa kisisasa.

Alisema Kanisa popote halitakubali vitendo hivyo vya kubadili nyumba za ibada kuwa uwanja wa siasa na kampeni.

Kumekuwa na madai kuwa baadhi ya vyama vya siasa, vinatumia vikundi vya dini kupiga kampeni za chinichini na endapo hali hiyo haitakemewa kwa nguvu , ipo hatari ya taifa kujikuta limegawanyika katika msingi wa udini.

Mkazi wa Bunda atengwa na jamii akidaiwa kuwa mchawi

lHatakiwi kuchota maji kisimani, marufuku kuzungumza na mtu

Na Mathias Marwa, Musoma

MKAZI mmoja wa wilayani Bunda katika mkoa wa Mara, ametengwa na jamii na mwingine wa Magu mkoani Mwanza, kunusurika kifo baada ya kukatwa na mapanga wote wakituhumiwa kwa imani chafu za kuhusika na vitendo vya kichawi.

Mtu huyo aliyetajwa kwa jina moja la Bukuku, amekumbwa na masaibu hayo ya kutengwa na kuzuiliwa kutumia visima vya eneo lake wala kuzungumza na mtu yeyote wa eneo kwa kipindi kadhaa akidhaniwa kuwa ni mchawi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mendeleo ya Wanawake na Makundi mengine, Bi. Maria Kamm, aliyekuwa katika ziara ya kuwatembelea wanawake na makundi hayo katika wilaya za Magu, mkoani Mwanza na Bunda ya mkoani hapa, mtu aliyemtaja kwa jina la Magdalena Ndira, wa kijiji cha Yitimila wilayani Magu, mwaka 1996, alinusurika kifo baaada ya kukatwakatwa mapanga kwa tuhuma hizo hizo za uchawi.

Bibi Magdalena, alipatwa na mkasa huo baada ya kutuhumiwa kumuua kwa uchawi, kijana mmoja aliyetajwa kwa kwa jina moja la Aloyce, ambaye baadaye ilibainika wazi kuwa alikufa kwa ugonjwa wa ukimwi.

Uchunguzi wa kamati hiyo inayoundwa na wabunge 19 wa vyama mbalimbali vya siasa nchini, umebaini ukweli kuwa wakazi wengi wa maeneo ya vijijini bado wamegubikwa na wingu chafu la kutumia muda mwingi kwa mambo ya imani za kishirikina na kusababisha vifo kadhaa kwa imani kuwa wagonjwa wanalogwa na imani zilizopitwa na wakati kama tohara kwa wanawake badala ya kufanya shughuli za maendeleo kama elimu.

Bibi Kammm ameyalaani mauaji na na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wanavyofanyiwa akinamama wanaotuhumiwa kwa uchawi na watoto wadogo hususani wa kike kunyanyaswa na akaongeza kuwa vitendo hivyo vinavyotokana na imani zilizopitwa na wakati, vinadhalilisha utu na kuathiri maendeleo ya jamii.

Amesema vitendo hivyo wanavyofanyiwa wanadamu hao, havina tofauti na kuwaua huku jamii ikishudia kimya, hivyo havina budi kukomeshwa mara moja.

...Hatukubali kutumiwa ng’o!- Kanisa

Na Steven Mchongi, Mwanza

KANISA limesema viongozi wake hawatajihusisha na ushabiki wa siasa kwa chama chochote, wala hawatakubali kutumiwa na vyama vya siasa kuvipigia "debe" katika kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani.

Padre Richard Makungu, wa Kanisa Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Ilemela mjini hapa aliyasema hayo katika semina hivi karibuni ya Baraza Kuu la Parokia hiyo juu ya mwenendo wa jamii ya Watanzania kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wakati huu ambapo Kanisa limo katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya Ukristo duniani na nchi inaelekea Uchaguzi Mkuu wa Pili unaovihusisha vyama vingi vya siasa utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu

Alisema kwa kuwa sio vibaya kwa viongozi wa Kanisa kushauri, kutoa maoni, kukosoa uongozi mbovu unapoonekana au watu wasioifaa jamii wanapopewa uongozi, kama taasisi nyingine zilizopo kwa ajili ya maendeleo ya jamii, mapadre, wachungaji na maaskofu hawana budi kuijadili hali ya siasa nchini bila kufungamana na chama chochote cha siasa ili kuweka dira ya kupata viongozi bora watakaoleta maendeleo kwa jamii ya Watanzania.

Alisema Kanisa lina wajibu wa kutoa mafundisho ya kiroho na kimwili na hivyo, hata viongozi wake wanayo haki na wajibu wa kutoa sera, dira na mipango sahihi ya maendeleo kwa waamini ili wawachague viongozi bora na kuinufaisha badala ya kuiangamiza jamii kimwili na kiroho.

"Kanisa lipo kwa ajili ya waamini wake, ili kuwapa mafundisho ya kiroho na kumcha Mungu, kuwa na upendo kwa jamii na pia Kanisa lipo kwa ajili ya kuwapa mafundisho ya kimwili waamini wake kwa ajili ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni,"alisema na kuongeza,

"Hivyo, hakuna ubaya kwetu mapadre au maaskofu kuzungumzia siasa ya maendeleo ya jamii kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodai".

Alisema kwa kuwa viongozi wa serikali wanatoka ndani ya jamii ambayo ni pamoja na Wakristo, Waislamu na wapagani, ni jamii hiyo hiyo watokayo, ndiyo itakayoathirika endapo haitaandaliwa vyema kuwachagua viongozi bora kwa faida na maslahi ya taifa zima.

Semina hiyo ya pili iliwahusisha washiriki 60 kutoka vigango vinne vya parokia parokia hiyo ambayo ni Lumale, Nyamilolelwa Kabageye na Ilemela.

WAKATI HUO HUO: Washiriki hao wamelishauri Kanisa Katoliki nchini kuanzisha elimu ya utamaduni kwa waamini wake ili kuzuia mmomonyoko wa maadili na kutoweka kwa utamaduni asilia wa Kitanzania.

Walisema Kanisa halina budi kutoa elimu ya utamaduni na maadili mema katika familia na shule ili kujenga jamii ya Watanzania iliyo bora.

Akichangia mada, Bw.Victor Lodovic, alishauri kuwaelimisha wazazi kwa njia za Semina, warsha na makongangamo ili wazazi hao wawaelimishe vijana madhara ya utumiaji wa madawa ya kulevya, utoaji mimba, vitendo vya zinaa na kuiga baadhi ya tamaduni mbaya za kigeni.

Naye Bi. Hellen Magonji, alishauri Kanisa kuanzisha utaratibu wa mafunzo ya kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, vigango, parokia hadi jimbo na akashauri Kanisa kukemea vikali vipodozi vikali vinavyotumiwa na wanawake "kujichubua"na hivyo kuharibu ngozi zao asilia.

Tume ya Uchaguzi yasema haigopi mtu

Na Josephs Sabinus, Bagamoyo

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imesema itahakikisha inavitendea haki vyama vyote vya siasa na kuwa huru katika utendaji wake wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao, bila kujali wala kuogopa matakwa ya mtu, chama chochote wala serikali.

Hayo yalisema mwishoni mwa juma na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Augustino, S.L. Ramadhani, wakati akijibu maswali mbalimbali ya washiriki wa kongamano la siku moja la vyama vya siasa, vyombo vya habari lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Paradise Hotel, mjini hapa.

Kongamano hilo liliandaliwa na Tume ya Taifa ya Utangazaji kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Lilifadhiliwa na Ubalozi wa Denmark nchini.

Mwakilishi wa chama cha UPDP, Abdallah Nassor, alionesha wasiwasi na kusema kuwa huenda vyama vya upinzani visishiriki vyote katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi sio huru na hivyo, haitafanya kazi zake kwa misingi ya haki.

Akijibu hoja hiyo, Jaji Ramadhani alisema, "Mimi nashindwa namna ya kukuhakikishia kuwa tunajitahidi iwezekanavyo kuwa huru na haki bila kufuata maagizo ya serikali wala kuiogopa serikali. Nakuhakikishia hilo."

Alitoa mfano kuwa wakati wa utawala wa chama kimoja, magari ya CCM yalikuwa na namba za CCM, lakini tume hiyo ilitoa maagizo ya kuzuia gari lolote lisionekane katika kampeni likiwa na namba za CCM. "Afisa wa CCM anayetka kumpigia debe mgombea wao, kama hana gari, basi akodi teksi lakini, tusione gari yenye manamba kama hayo. Kuanzia pale, zile namba zikapotea kabisa."

Jaji Ramadhani, alivitaka vyama vya siasa kukubaliana na matokeo sahihi ya uchaguzi pindi yanapotangazwa na kuilaani tabia ya wapinzani wengi kutokubali matokeo wanposhindwa hata uchaguzi unapokuwa huru na haki.

"...Kwa wengine inapotokea hata serikali na mabalozi kutoka nje, kama serikali iliyokuwepo, chama kilichokuwepo hakikushindwa, basi wanasema huo uchaguzi sio huru na haki, mpaka chama kilichokuwepo na serikali iliyokuwepo ianguke na kushindwa, ndipo uchaguzi uwe huru na haki.

Wengine kama mimi mwenyewe nagombea, sikushinda, uchaguzi sio huru na haki mpaka mimi tu, nishinde. Je, kama mko watu 13 mnagombea na kila mmoja anashikilia uzi huohuo, nisiposhinda mimi sio huru na haki, huru na haki maana yake ni nini?" alihoji.

Alisema tangu siku rasmi ya kuanza kampeni , Tume yake itavimiliki vyombo vya habari vya serikali ambavyo ni pamoja na RTD, Sauti ya Tanzania Zanzibar, Daily News na Television ya Taifa (TVT) ili vitoe nafsi sawa kwa vyama vyote kuvitumia.

Jaji Ramadhani, alivishauri vyama vya siasa kufanya jitihada za kuwatafuta mawakala wakereketwa watakaosimamia zoezi la uchaguzi kwa kuwa bajeti ya gharama za uchaguzi, haina uwezo wa kumudu gharama za mawakala hao.

Alisema katika uchaguzi ujao, tume yake itajitahidi kihakikisha kuwa matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita yakiwemo ya kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupia kura na kupungua kwa makatarasi, hayatokei.

Aliongeza kuwa katika Uchaguzi uliopita, baadhi ya mawakala walipewa pesa lakini siku ya uchaguzi hawakufika katika vituo vyao vya kazi na hata viongozi wengine wa vyama walichukua pesa wakagawana bila kuwalipa mawakala wao.

Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, Mark D. Bomani, alivitaka vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa wagombea wa vyama vyote bila upendeleo wala kuwapigia debe baadhi ya wagombea wa vyama.

Hata hivyo, alivitahadharisha kuwa makini na kutoaandika au kutangaza habari za kashfa, uzushi na uchochezi ili kulinda hadhi ya taaluma ya habari kwa kulinda maadili.

Kuweni makini na TV, Video ashauri Askofu Banzi

Na Leocardia Moswery,

"Wanaozalisha vitu hivi wao kazi yao ni kuleta tu. Mkitaka TV, wanaleta, mkitaka video wanaleta.na kile mnachotaka wawaoneshe, wanaonesha tu hawajali kama ni kizuri au kibaya. Sisi wenyewe ndio tunatakiwa kuwa makini kujua tujifunze nini kwa sababu dunia sasa imekuwa kama kijiji."

Askofu Anthony Banzi, wa Jimbo Katoliki la Tanga, aliyasema hayo katika ibada ya kubariki nyumba ya Vijana Wakatoliki Wanafunzi wa Sekondari na Vyuo (TYCS) iliyopo eneo la Upanga jijini Dar-Es-Salaam, hivi karibuni.

Mhashamu Banzi, aliishauri jamii kuwa makini katika matumizi ya Sayansi na teknolojia ya kisasa ili kuepuka kuiga mambo mabaya yanayooneshwa katika television na video ambayo yanachangia kuibomoa jamii kimaadili na kiroho.

Alisema iwapo jamii haitakuwa makini katika matumizi ya television na video na mtandao wa kompyuta, ipo hatari jamii ikazidi kuangamia kwa kuiga upotofu wa maadili unaooneshwa katika vyombo hivyo vya kisasa vya mawasiliano unashamiri katika mataifa ya ng’ambo.

Alikemea vitendo vya upotovu wa maadili ndani ya jamii hali inayosababisha siku hizi hata mtoto akikusalimia, unajua dhahiri kuwa anataka akuombe pesa.

Katika sherehe hizo, Mlezi Mkuu wa TYCS kitaifa, Padre Lucas Mzuanda, alikemea vikali tabia ya baadhi ya watu kujenga mazoea ya kudharau kwaya na akasema mtu yeyote mwenye tabia hiyo hana budi kuungama mbele za Mungu.

"Mtu yeyote anayedharau kwaya, hata awe padre au nani, akaungame kwa askofu kwa kuwa kwaya ni kiungo muhimu kinachochangamsha ibada na kuhubiri kwa nyimbo,"alisema.

Licha ya kuwapongeza wanakwaya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kushirikiana na kwaya mbalimbali kueneza Neno la Mungu, Padre Mzuanda, aliwahimiza pamoja na vikundi vingine kuwa tayari kufanya kazi yao pindi wanapotakiwa na mahali popote kwa kuwa huduma yao ni muhimu katika ibada za Kanisa.

Bado milioni 67 zahitajika kujenga Seminari

Na Joseph Simba, Mbeya

ZAIDI ya shilingi milioni 7.5/= kati ya 75m/= zinazohitajika, zimechangwa na wananchi katika Jimbo Katoliki la Mbeya kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule ya Sekondari ya Seminari ya Mtakatifu Maria iliyopo eneo la Mbalizi, nje kidogo ya Manispaa ya Mbeya.

Katika hafla maalumu iliyofanyika shuleni hapo hivi karibuni kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa bweni, maktaba na maabara, shilingi milioni nne, zilichangwa papo hapo , wakati milioni 3 na laki 3 zilitolewa na wananchi mbalimbali wakiwamo wazazi na viongozi mbalimbali wa chama, serikali na vikundi vya dini, kwa ahadi.

Akifungua hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Padri Ernest Mwashiuya, alisema kuwa ujenzi huo unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 75.

Kupatikana kwa kiasi hicho cha mchango, kunafanya sasa zaidi ya shilingi milioni 67, zihitajike ili kukamilisha shughuli hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Alisema maabara itapewa kipaumbele zaidi kwa kuwa hadi sasa shule hiyo haina maabara hali inayowalazimu wanafunzi kutumia moja ya madarasa yao kama maabara.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Basil Mramba, aliyekuwa mgeni rasmi, aliwataka wakazi wa mkoa huo kujenga tabia ya kuchangia maendeleo yao kwa hali na mali bila kutegemea tu, serikali ifanye kila kitu.

Mkuu huyo wa mkoa alichangia jumla ya shilingi laki sita na akasema serikali pekee haiwezi kukamilisha miradi yote ya maendeleo bila kusaidiwa na nguvu ya wananchi.

Aliwataka wananchi kutumia nguvu zao kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya na maji ili kuipa unafuu serikali katika kuunga mkono juhudi hizo.

Vijana wa KKKT Mbeya wahimizwa juu ya elimu

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

VIJANA kote nchini wametakiwa kuzingatia elimu ili waweze kuwasaidia katika kujiletea maendeleo na kujikwamua katika janga la umaskini.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk. Samson Mushemba, alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya tano ya chuo cha Ualimu Mbeya, kinachomilikiwa na kanisa hilo.

Alisema vijana hawana budi kutilia maanani kwa kuwa ni elimu pekee itakayowapa uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za halali kwa kiwango na ubora muafaka katika uzalishaji mali na kuanzisha miradi yenye kuwapatia kipato halali cha kuwaendeshea maisha.

Alisema, hali vijana kuwa na miradi inayowapatia mapato, itawaondolea umaskini na pia kuwawezesha kujiepusha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na jamii kwa ujumla.

Mkuu huyo wa KKKT pia, aliwataka vijana kukemea vitendo vya rushwa na ujambazi ili nchi hii iendelee kuwa nchi ya amani na utulivu.

Dakta Mushamba pia aliishukuru serikali kwa kuyawezesha madhehebu ya dini kufanya shughuli mbalimbali za kutoa huduma za jamii kwa wananchi licha ya kutoa huduma ya kiroho.

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 15 walitunukiwa stashahada za ualimu baada ya kufuzu mafunzo yao ya miaka miwili ya ualimu.

Wananchi wote wanahitaji kujua sheria za barabara

Na Dalphina Rubyema

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye mabasi nchini nchini(TABOA),Bw. Mohammed Abdalah, amesema ipo haja kubwa ya kuwaelimisha zaidi wananchi juu ya sheria za barabarani kwani si ajali zote zitokeazo barabarani ambazo zinatokana na makosa ya madereva.

Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kurasini Jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni.

Bw.Abdalah alisema kuwa serikali haina budi kuelimisha jamii juu ya suala zima la sheria za barabarani kwani watu huvuka tu barabarani bila kuangalia kama kuna gari linalokuja.

Mbali na hao wavuka kwa miguu pia imeelezwa kuwa hata waendesha baiskeli na pikipiki nao pia ni chanzo kikubwa cha ajali za barabarani kwani huendesha kwa kuyumbayumba wakitoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine hali inayosababisha madereva wa mabasi kukosa mwelekeo na kujikuta wakipindua magari au kuwagonga.

Mwenyekiti huyo wa TABOA alisema kiburi cha madereva wa magari moshi nao ni sababu tosha ya ajali kwani madereva hao huendesha vyombo vyao kwa kiburi kwamba wao wana haki ya kupita bila kujali katika makutano ya reli na barabara hata kama kuna gari lolote litatokea kukatisha barabara bila kujua kama garimoshi linakuja.

"Watembea kwa miguu nao huvuka barabara pamoja na kuvusha mifugo yao bila wasiwasi wa kusababisha ajali,waendesha pikipiki na baiskeli nao pia elimu ya barabara kwao ni ndogo kwani huendesha tu bila kufahamu ni upande gani wa barabara wanapashwa kukaa, hivyo serikali haina budi kutoa elimu kwa jamii nzima"alisema.

Aliishauri Serilaki itunge sheria za kuwabana madereva wa magarimoshi, kwani wanaona hata wakisababisha ajali ya garimoshi kugongana na gari,wao hawana hatia hivyo hawajali.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amekiri kuwa ubovu wa magari nacho ni chanzo cha ajali hizo na ameishauri Mamlaka ya leseni kuacha tabia ya kutoa leseni kwa mfanyabiashara yeyote anayetaka barabara ya kuweka gari lake kusafirisha abiria bila kuangalia uwezo wa mfanyabiashara huo kifedha ambapo amependekeza kuwa leseni itolewe kwa mtu mwenye magari ya abiri yapatayo 24-25 na yote yawe yanaaminika.

Mkoa wa Pwani ahueni kwa elimu

Na Agatha Rupepo DSJ

VIONGOZI wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuinua kiwango cha elimu katika mkoa wa Pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bw. Nicodemus Banduka aliyasema hayo katika sherehe za siku ya Elimu kimkoa zilizofanyika katika Wilaya ya Kisarawe hivi karibuni.

Bwana Banduka alisema katika sekta ya elimu mkoa wa Pwani umefanikiwa kuinua kiwango cha taaluma kwa kutoka nafasi ya 14 kitaifa kwa mwaka 1997 na 1998 hadi kufikia nafasi ya nane kitaifa kwa mwaka 1999.

Aliongeza kuwa kwa kuipa jamii elimu itaisaidia jamii kushiriki ipasavyo katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ambazo zitaisaidia jamii kujitegemea kiuchumi.

Bwana Banduka alisema miaka ya hivi karibuni sekta ya elimu katika mkoa wa Pwani sekta ya elimu katika mkoa wa Pwni imekuwa inakabiliwa na matatizo mbalimbali kama vyumba vya madarasa ya kudumu na madawati ambavyo viliathiri sana katika utoaji wa elimu.

Tatizo lingine lilikuwa ni uhaba wa Walimu hasa katika shule za vijijini ambapo baadhi ya shule zilifundishwa na mwalimu mmoja kwa muda mrefu wakati katika maeneo mengine tatizo la ukame lilikuwa kwa walimu kurundikana katika shule chache.

Akaongeza kuwa baada ya kubaini matatizo yaliyokuwa yanaikabili sekta ya elimu uongozi wa mkoa uliamua kubuni mikakati ya kuondoa matatizo hayo ambapo mkoa uliandaa kijitabu kinachoitwa ‘Education Profile’

Akasema lengo lake ni kuyaweka bayana matatizo yote yanayoikabili elimu na kuonyesha mikakati iliyopangwa na kila wilaya katika kuondoa matatizo hayo.

Nitaendelea ‘kumpiga dongo’ Kakobe-Kapteni Komba

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Kikundi cha Sanaa za Maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT),Kapteni John Komba, amesema ataendelea kutunga nyimbo za kuelezea alichokiita mwenendo wa kuichafua CCM wa kiongozi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship,Mchungaji Zakaria Kakobe.

Kapteni Komba,alitoa kauli hiyo jijini hivi karibuni ambapo alisema yeye kama Mwana-CCM tena mpiga debe wa chama hicho, hatakubali kuona Mchungaji Kakobe akichafua jina la chama hicho, kisha anyamaze kimya. Badala yake alisema ataendelea kutunga nyimbo za kuweka bayana mwenendo wake."Sitakubali hata siku moja Kakobe akichafulie jina Chama Cha Mapinduzi,nami kwa vile najua bayana mwenendo wake; lazima nitunge nyimbo za kumpiga madongo.Lazima dongo litue kichwani mwake,"alisema.

Mkurugenzi huyo pia amemtaka Mchungaji Kakobe, aelewe kuwa anayetoa laana ni Mungu peke yake na wala siyo yeye"Anayetoa laana ni Mungu tu, sasa huyo Kakobe anayetumia vitisho kuwa atatulaani,aelewe kuwa mimi sitasita kumtungia wimbo wa kumpiga dongo kwa kuogopa laana zake.

"Akae chini na kuhubiri dini kama wafanyavyo viongozi wengine wa dini na siyo kukalia mambo ya kutulaani," alifoka.Mchungaji Kakobe katika siku za hivi karibuni amekuwa akikilalamikia kikundi cha TOT kuwa kinatumiwa na chama tawala cha CCM kuwapumbaza wananchi ambao wana dhiki nyingi lakini badala ya kusaidiwa wanaimbiwa nyimbo.

Kisarawe watakiwa kusaidia vijana

Na Agatha Rupepo, Kisarawe

VIONGOZI wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, wametakiwa kuweka mikakati ya kuwadhibiti vijana wanaomaliza shule katika wilaya hiyo kwa kuwapatia maeneo maalum kwa ajili ya kilimo.

Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, William Lukuvi,aliyasema hayo wakati wa kufunga warsha ya siku mbili iliyofanyika katika tarafa ya Maneromango.

Alisema umefika wakati kwa wana-Kisarawe, kuwaelimisha vijana ili waweze kutumia rasilimali walizonazo kwa kudumisha kilimo ili waweze kujiinua kiuchumi.

"Hawa kama vijana wetu wanatakiwa kutumia nguvu nyingi katika kilimo ili waweze kuishi vizuri na familia zao kwa kuwapa huduma muhimu"

aliongeza kuwa kuna baadhi ya viongozi wanapenda kutumia madaraka yao kwa kuchukua ardhi kubwa ambayo wanashindwa kuihudumia na kusababisha mapori na vichaka kwa wanyama waharibifu wa mazao.

Amewataka wananchi kutumia mazingira yao vizuri ili wajipatie utajiri kwa njia ya kilimo vinginevyo watabaki kuwa maskini hata kwa kizazi kijacho.

Waziri Lukuvi amewataka wanakisarawe kutumia ardhii yao vizuri kwa kilimo cha korosho kwa sababu korosho ndiyo zao kuu la biashara la Wilaya na Mkoa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa kuanzia sasa Halmashauri ya Wilaya haina budi kuwatambua vijana wote wanaomaliza elimu ya msingi ili iwezekuwapangia kazi za kufanya hasa kuwapa mashamba ili waweze kujiajili wao wenyewe.

Zahanati ya Mt. Consolata pekee kuifaidi AMREF

Na Dalphina Rubyema

HOSPITALI ndogo ya Mtakatifu Consolata iliyopo Mtoni Kijichi wilayai Temeke, ni taasisi pekee itakayonufaika na msaada wa madawa toka kituo cha utafiti wa madawa kwa Kanda ya Afrika (AMREF)kufuatia mchango wake bora katika utoaji wa tiba kwa jamii.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi jijini katikati ya wiki, Meneja wa Mafunzi wa kituo hicho, Dk. Annefrida Kisesa, alisema uamuzi huo wa AMREF, umefuatia zahanati hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi bila kutegemea maslahi ya kibiashara.

Hivi karibuni AMREF iliwachukua wafanyakazi kadhaa wa zahanati hiyo na kuwashirikisha katika mafunzo ya maendeleo ya watoto ambapo walipatiwa pia vitendea kazi ambavyo ni pamoja na madawa.

Alisema zahanati za serikali lakini zile za serikali hazitapata msaada huo kwakuwa kwa kuhofiwa kuwa wanaweza kuyatumia kibiashara.

Dk.Kisesa aliendelea kusema kuwa utafiti unaonesha kuwa mfumo wa utendaji kazi katika zahanati hiyo hauoneshi kama ipo kibiashara na zaidi inaonekana kutoa huduma kwa kuzingatia afya bora kwa jamii jambo ambalo limeishawishi taasisi hiyo kutoa madawa hayo kwa zahanati hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki.

Alisema mgao wa dawa kwa zahanati hiyo utatolewa mara moja baada kukamilika utaratibu wa kuwawezesha kufanya hivyo.

Dk.Kisesa alizitaja dawa hizo kuwa ni pamoja na zile za kutibu magonjwa kipindupindu, Armonia, malaria na maradhi mengine ambayo yamekuwa yakiwasumbua wakazi wa Manispaa ya Temeke.

AMREF imekuwa ikipambana kiafya katika nchi za Afrika na imetoa mafunzo kwa waelimishaji 120 ambo wanawajibu wa kutoa elimu kwa umma ndani ya jamii jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa watoto wanokumbwa na maradhi mbalimbali kabla ya kumkimbiza hospitalini au katika Zahanati ya jirani ili kuepushwa vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Mbali na hilo taasisi hiyo iliwapa mafunzo ya kutambua dalili za kutambua dalili za maradhi mbalimbali na msaada wa madawa na vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 20 na mafunzo hayo yametolewa katika Manispaa pekee.

Waajiriwa TPC kurithiwa na wabia

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Tanzaniai hivi karibuni ilikabidhi asilimia 75 ya hisa zake za Kampuni ya Kiwanda cha Sukari (TPC) kwa Kampuni ya Sukari kutoka nchini Mauritus inayojulikana kama Sukari Investment Company LTD.

Kw amujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habarri kutoka Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) Kampuni hiyo kutoka Mauritus ndiyo iliyofanikiwa kuinunua TPC ina mafanikio makubwa ya biashara ya sukari nchini humo, hivyo itaiendesha bila matatizo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hati za makabidhiano ya ununuzi wa kiwanda hicho kilichopo mkoani Kilimanjaro nchini, zilikabidhiwa Machi 25 mwaka huu kati ya Tume ta Kurekebisha Mashirika ya Umma nchini na na Kampuni hiyo ya wanunuzi.

Taarifa hiyo inasema asilimia hiyo 75 ya hisa zilizotolewa na ni sawa na Dola za Kimarekani 7,190,000 ambapo Dola 800,000 zilitolewa kwa pesa ya Mauritus (MOU).Taarifa hiyo inasisitiza kuwa kulingana na makubaliano baina ya serikali na wanunuzi hao,,wafanyakazi katika kiwanda hicho wataendelea na ajira zao kama kawaida na endapo mabadiliko yoyote yatatokea , wamiliki wapya wa kiwanda hicho watawajibika kutoa fidia kwa wafanyakazi hao kulingana na sheria za ajira zilizopo nchini.

Vijana watahadharishwe kuuzwa mijini

Na Getruda Madembwe

VIJANA wametahadharishwa kuwaepuka watu wanaowatoa vijijini kwao kwa madai ya kuwatafutia kazi nzuri katika miji mikubwa na badala yake kuwatumia katika biashara ya ukahaba na kuwauza kwa watu wanaowatafuta "mahausigeli" na hatimaye kuwatelekeza na kuwaacha wakizama katika vitendo vya uhalifu.

Tahadhari hiyo ilitolewa mwishoni mwa juma na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-Es-Salaam, juu ya hali ya maadili nchini.

Alisema ni kitendo cha unafiki na makosa makubwa kwa mtu mzima kumdanganya mtoto kuwa anakwenda kumtafutia kazi nzuri kumbe anakwenda kumtumia katika biashara haramu ya ukahaba na kuwauzia wanaowatafufuta wafanyakazi wa ndani.

"Si kweli kuwa wanakuja kuwatafutia kazi Dar-Es-Salaam, wakati wenyewe hawana hiyo kazi ya maana wanayoisema. Vijana wasidanganywe na watu wa namna hiyo kwa kuwa hata huku mijini kwenyewe kuna watu wengi ambao hawana kazi. Matokeo yake ndiyo hayo sasa wanaingilia vitendo viovu," alisema.

Mhashamu Ngalalekumtwa, ameishauri jamii yote hususan watu wa maeneo ya vijijini, kuwasaidia vijana ili waanzishe miradi na kufanya shughuli mbalimbali ili waepukane na vishawishi hivyo vinavyowaharibia maisha.

Amewalaumu wenye tabia hiyo ya kuwadanganya vijana hasa wa kike na badala yake kuwatelekeza katika maisha na mazingira magumu.

Akitoa mfano, alisema jimboni kwake baadhi ya vijana wameungana na kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kilimo na ufundi seremala ambazo kwa kiwango kikubwa hufanywa na vijana wa kiume wakati vijana wa kike hijishughulisha na ushonaji.

Alibainisha kuwa vijana wanaojishughulisha na kazi hizo huandaliwa tangu ngazi ya kipapa, TYCS na Viwawa na kuongeza kuwa shughuli hizo pia zipo maeneo ya Magulilwa, Kidabaga na zinatarajiwa kuenezwa katika maeneo mengine ya jimbo.

Askofu Ngalalekumtwa alidokeza kuwa jimbo lake linacho kitengo kinachojulikana zaidi kwa jina la "Majozi" (Worldwide Marriage Encounter), chenye lengo la kutoa mafunzo ya upendo kwa wazazi ili wawe na upendo kwa watoto wao na kuwapatia malezi bora.

"Hii ni kwa ajili ya wazazi ambao wanapata mafunzo ya namna kuwalea watoto wao kwa upendo badala ya kuwaacha tu, hao watoto wao wajitafutie kazi wenyewe baada ya kumaliza shule kitu ambacho ni kigumu na sio vizuri," alisema