ONYO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU UJAO:

'Wanasiasa wasifananishe Watanzania na kata ya pombe'

Elizabeth Steven na Getruder Madembwe

ASKOFU Anthony Banzi, wa Jimbo Katoliki la Tanga, amewaonya wanasiasa wanaopenda kutafuta vyeo kwa rushwa kutothubutu katika Uchaguzi Mkuu ujao kuwafanya Watanzania wajinga ambao wanaweza kununuliwa hata kwa kata ya pombe.

"Tunaweza kurubuniwa kwa kata moja ya pombe huko kijijini au hata wanafunzi wakapigiwa madisko, watu wakapewa kanga, mlo mmoja wa pilau, tukadhani tunasaidiwa, kumbe tunatumika kama ngazi ya watakaotukandamiza,"alisema.

Mhashamu Anthony Banzi, aliyasema hayo alipoongea na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo pia alisema anashangaa kwa nini Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini (PCB) huwa haijishughulishi kabisa na udhibiti wa rushwa kwenye chaguzi za kisiasa.

"Wengi wa wagombea au viongozi wasiofaa, wakati wa uchaguzi wanajidai wema, wakishapewa, huwaoni tena jimboni wala hata kuwasikia bungeni hadi inapobakia miezi mitatu ndipo utawaona tena majimboni na kuwasikia wakiwadanganya watu kwa vimsaada vya siku moja moja ili waonekane ni wema; muwachague tena."

PCB imeshauriwa kuacha utamaduni wakeulioshamiri wa kujishughulisha na walaji na watoa rushwa na wapokeaji wadogowadogo na badala yake, iwashughulikie wale wakubwa na kudhibiti rushwa katika chaguzi za kisiasa pia.

Aliishauri kuwa makini zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao, ili kuwabaini wala rushwa wote, wakubwa na wadogo.

Alisema ingawa katika mapendekezo yake, Tume ya kuchunguza kero za rushwa ya Jaji Joseph Warioba, ilichunguza na kutoa mapendekezo kuhusu mianya na njia za kudhibiti rushwa, bado hali ni mbaya mno kwa vile mapendekezo hayo hayajatekelezwa.

Alisema anashindwa kujua ni kwanini wanaokamatwa mara kwa mara na PCB, ni watumishi wa ngazi za chini na pengine wastaafu peke yao.

Alionya kuwa endapo PCB, haitalivalia njuga zaidi suala hili hasa nchi inapoelekea Uchaguzi Mkuu, ipo hatari ya taifa kuwapata viongozi wabovu wenye ubinafsi, wezi , wabadhirifu wa mali ya umma na wazembe katika kuwajibikia maeneo na jamii zao .

Alisema, anayefaa kuongoza jamii, lazima awe na kipaji cha uongozi, mwadilifu na mwenye kumcha Mungu kinyume na hapo, ipo hatari ya kuwapata hata viongozi wanaohusudisha ushirikina wakati wanajua wanakiuka hata mapenzi ya Mungu.

"Wapo wanaotaka kwenda ikulu na bungeni kwa malengo binafsi. Hata madiwani wapo wa namna hiyo".

Alisema endapo PCB itaelekeza nguvu katika uchaguzi ujao, inaweza kuwakamata wagombea wengi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ambao hata wanaposhindwa, huamua kufungua kesi za kupinga matokeo.

"Hata mimi binafsi, sijawahi kusikia Taasisi hii imenasa watu wa rushwa wakati wa uchaguzi wowote nasidhani kwamba hata hawa wagombea huwa hawatoi rushwa.

Unadhani, ni kwanini hawa wagombea wanaopinga matokeo eti kulikuwa na rushwa, hawasemi wakati ule mpaka wasubiri matokeo wakiona wameshindwa, wanasema kulikuwa na rushwa. Inaonekana wote walikuwa wanatoa isipokuwa, huyu kampiku mwenzake" alisema Askofu huyo.

Amewaasa Watanzania kutokukubali kurubuniwa kwa vitu vya siku moja, kisha wakajutia baada ya kuwachagua viongozi wasiostahili.

"Tunahitaji mtu mwenye uchungu na watu sio wa kuwadanganya kwa kwa kikombe cha chai"

Hata hivyo alibainisha kuwa hali hiyo inachochewa na umaskini wa nchi na akasistiza maombi zaidi ya imani ili Mungu awaepushie balaa hilo Watanzania kwani linahatarisha amani.

Alisema Kanisa litazidi kutimiza jukumu la kuwahamasisha watu kuwa macho ili wasirubuniwe na wagombea uongozi wanaokuja na zawadi feki zitakazoiliza jamii baadaye.

Akizungumzia suala la viongozi wa dini kutakiwa kuchangia maendeleo ya jamii lakini wanapokemea makosa ndani ya serikali hususani masuala ya kidemokrasia, wanaambiwa wanaingilia masuala ya siasa, alisema,

"Kiongozi wa dini kupigania ubunge na kujiunga na chama cha siasa, ndiko kuingilia masuala ya siasa; tena siasa za vyama na kama kiongozi wa dini, ni kukiuka maadili.

Lakini, kama kiongozi wa watu wa vyama vyote ninayetakiwa kukemea mambo yasiyostahili katika jamii, eti nisiseme wewe unaiba, unasema uongo, usitoe rushwa, usifanye fujo wala kugandamiza watu wala kunyanyasa, niyanyamazie hayo kwa kuwa ni kiongozi wa dini! Nisiseme hapa unaongoza vibaya?" alihoji kwa mshangao na kuongeza,

"Lazima nimwambie hapa unakwenda vibaya, sitaacha eti kwa vile yeye ni mwanasiasa na mimi ni kiongozi wa dini. Hapo ndipo kazi yangu inatimizwa."

Alisema ni lazima jamii ijue wazi kuwa demokrasia (utawala wa watu) ina mipaka isiyoingiliana na mambo ya Mungu, lakini theokrasia (Utawala wa Mungu), inaingia sehemu zote kwa kuwa Mungu ni mkubwa kwa yote.

Alisema hawajihusishi na siasa za vyama lakini, kama wanadamu wengine ndani ya jamii, lazima washiriki mambo muhimu ya kuiletea jamii maendeleo na amani.

Alipoulizwa kama ni demokrsia ya haki kwa CCM kuwataka wagombea wake wa urais kulipia sh. Milioni moja, kwa ajili ya fomu na kuwa lazima wawe na angalau digrii moja, Askofu Banzi alisema, "Hizo sasa ndizo siasa za vyama ambazo hatuwezi kuingilia," akakataa kulizungumzia zaidi.

Lipumba awaonya Waislamu wanaokielewa vibaya CUF

Na Dalphina Rubyema

WAISLAM nchini wametakiwa kuacha kujenga dhana potofu akilini mwao kuwa Chama cha Wananchi (CUF) ni chao hivyo kutumia nafasi hiyo kuhubiri misikitini mwao kwamba Waislamu wasitoe kura zao kwa makafiri na badala yake wazitoe kwa Waisalamu wenzao.

Taarifa hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF,Profesa Ibrahim Lipumba,alipohojiwa na gazeti hili nje ya Ukumbi wa Idara ya habari (MAELEZO) jijini juu ya dhana iliyojengeka miongoni mwa wananchi kuwa chama chake ni cha Waisalamu.

Alisema sera na katiba ya chama chake haielezi hata kidogo juu ya dini ya Uislamu na kuongeza kuwa wale wanaotaka kutumia jina la chama hicho kujenga mizizi ya udini hawana budi kuacha mara moja katika hawajafikia ambapo haiawezekana kurekebisha.

"Sisi CUF hatumiliki msikiti hata mmoja hapa nchini,sasa kama kweli kuna Waislamu wanaodhania kuwa CUF ni chama chao,nawambia hivi;CUF ni chama cha wananchi wote na kama ni huo Uislamu,mimi pamoja na kwamba ni muumini wa dini hiyo lakini bila shaka nisingechaguliwa kuwa Mwenyekiti wake kwani sina sifa za kutosha kuwa kiongozi wa chama cha Kiislamu.

Kuna Waisalamu wengi wanaonizidi ambao wangeweza kuongoza chama kama hicho,"alisema.

Wakati huo huo,Profesa Lipumba, aliwambia waandishi wa habari kuwa chama chake bado kinashikilia msimamo wake kwamba hakitakubali kudanganywa kwa namna yoyote ile kwenye uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani kama hautafanyika kwa uwazi,ukweli na haki.

"Hatutakubali kabisa kudanganywa kama tulivyodanganywa kwenye uchaguzi wa 1995,sasa tutapambana kikamilifu kama uchaguzi wa mwaka huu hautafanyika kwa haki. Endapo utafanyika kwa uwazi,ukweli na haki hata kama tutakuwa tumeshindwa hatutakuwa na neno,"alisema Profesa Lipumba ambaye aliwahi kuwa mshauri wa mambo ya Uchumi wa Serikali ya Awamu ya Pili, na baadaye Mshauri wa kiuchumi wa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, nchini Uganda.

Akizungumzia suala la taarifa ya fedha 1999/2000 iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Fedha nchini,Bw.Daniel Yoha,Profesa Lipumba ambaye pia ni mwanauchumi alisema kuwa serikali bado ina ugonjwa wa matumizi yake kuwa makubwa kuzidi mapato na makadirio.

Zingatieni haki, msijali sura - Askofu

Na Leocardia Monswery

ASKOFU Nestory Timanywa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, ameitaka jamii yote ya Watanzania kujenga utamaduni wa kuthamini na kutenda haki kwa wengine bila kujali sura wala uwezo wa mtu.

Aliyasema hayo wakati akiongoza ibada katika Kanisa dogo la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lililopo Kurasini katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wiki iliyopita.

Askofu Timanywa, alisema kutenda haki ni jukumu la kila mmoja na wala siyo suala la kupakaziana na kutupiana mzigo wa jukumu hilo muhimu kwa jamii yenye mapenzi mema.

"Siyo kuangalia sura, ukarimu, uwezo wa mtu, wala elimu, haki ya mtu izingatiwe na kuheshimiwa," alisema.

Askofu Timanywa, aliyekuwa jimboni Dar-Es-Salaam kikazi, alisema upendo kwa watu, ni kiungo kilichotolewa na Mungu na kuletwa na Mwokozi wa Ulimwengu ili kuwafanya watu wakombolewe katika dhambi ambayo ingewapelekea kuishi katika maisha ya tabu na mashaka yatokanayo na ukiukwaji wa mapenzi ya Mungu.

Aliwata Wakristo wote kutokuyumbishwa kiimani na hata kudumisha amani miongoni mwa jamii ya wanadamu na kuimarisha mshikamano katika Krsto, baina yao.

"Kuweni na msimamo katika imani zenu siyo kuyumbayumba katika maisha yenu maana Mungu ni mmoja katika utakatifu wake," alisema.

Rambirambi za Nyerere zamfanya DC aombe radhi

Na Mathias Marwa, Musoma

MKUU wa Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, Kapteni Aseri Musangi, amewaomba radhi walimu wa shule za msingi za Halmashauri ya Mji wa Musoma kufuatia kukatwa shilingi elfu moja katika mishahara yao kwa ajili ya kutoa rambirambi kwa familia ya marehemu Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na walimu katika ukumbi wa MCC mjini hapa, Kapteni Musangi, alisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Musoma Bw. Henry Owiso, na Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo Bw. Aloyce Nyato, hakikuwa cha haki kwa kuwa walikata kiasi hicho bila ridhaa ya walimu hao.

Alisema suala la michango ya rambirambi sio la lazima na akawataka viongozi hao kuwa makini mara nyingine kwa kufanya mawasiliano na makubaliano badala ya kujiamulia wenyewe kukata mishahara ya walimu, hali ambayo huweza kusababisha chuki fitina na utendaji mbovu wa kazi.

Walimu hao wamesema kuwa wanakusudia kuwafikisha mahakamani Mkurugenzi wa Afisa Elimu hiyo kwa kuwa kitendo walichokifanya ni kuvunja sheria ya kazi Kifungu Na.366 ibara ya 63, sehemu ya 1 na 2, kinachosema ‘ni kosa kwa mwajiri kukata mshahara wa mtumishi bila ridhaa yake, isipokuwa makato yaliyohalalishwa kisheria’

Walimu hao walikatwa mishahara yao hivi karibuni kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoa mchango kwa ajili ya rambirambi kwa familia ya Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hali ambayo waliipinga kwa madai kuwa haikuwa ridhaa yao.

Hata hivyo wamekubali fedha hizo ziwasilishwe katika familia hiyo kama zilivyo na kuonya kuwa endapo zitawasilishwa pungufu watawafikisha mahakamani Mkurugenzi na Afisa Elimu hiyo hawakutaja idadi ya fedha zote.

Akina mama wa Kahama 'watajirika'

Na Charles Hillila, Shinyanga

Akinamama 82 kutoka katika vikundi vitatu vya wilaya ya Kahama wamefaidika na mikopo ya shilingi zipatazo milioni 4.1 kutoka kwa shirika la kimataifa la FINCA linalojishughulisha na kusaidia vikundi vya akina mama wafanyabiashara ndogondogo ili kuinua hali zao za maisha.

Vikundi vilivyofaidika na mikopo hiyo ya Finca ambalo makao makuu yake yapo hapa nchini mjini Mwanza ni cha Jitegemee kutoka mji wa Isaka kikundi kina idadi ya wanachama 27 na kimepata kiasi cha sh. 1,30,000.00. Kingine ni kutoka Kahama mjini cha Jembe Kazi chenye fedha kilichotolewa kwa vikundi hivyo kinafanya idadi ya sh. Milioni 1.4 ambazo kila mwanachama atafaidika na kiasi cha sh 50,000 kutoka kwenye kila kikundi.

Akiongea wakati wa utoaji wa mikopo hiyo wilayani Kahama Mei 27 mwaka huu kwenye Hotel ya Picnic. Meneja wa Finca Tanzania Mama Anna Mlalo alisema kuwa Lengo la mikopo hiyo si kama msaada bali ni mtaji unaotolewa ili kuongeza nguvu au mtaji katika biashara kwa akina mama na kisha kurudisha ili na wengine waweze kupewa mikopo hiyo.

Wakati huo huo: imeelezwa kuwa pamoja na sekta ya madini hapa nchini hususan wachimbaji wadogo wadogo kuchangia kwa asilimia kubwa ajira kwa wananchi wenye kipato cha chini lakini haijaleta maendeleo yeyote miongoni mwao na taifa kwa ujumla hasa katika Elimu, Mawasiliano na afya.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa viongozi wa wachimbaji wadogo wadogo wa mkoa wa Shinyanga ‘SHIREMA’ Shinyanga Regional Miners Association, uliofanyika Mei 27 mwaka huu wilayani Kahama. Mkuu wa wilaya ya Kahama Mama Hawa Mchopa aliwaambia wachimbaji hao kuzingatia utunzaji wa mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi kwa ajili ya afya zao badala ya kuangalia uchimbaji peke yake.

Mama Mchopa aliendelea kusema kuwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini katika mkoa wa Shinyanga wamekuwa chanzo cha kuharibu mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi zao.

 

Watawa nchini watakiwa kufuta ukabila

Na Getruda Madembwe

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka Wamama Wakuu wa Mashirika mbalimbali ya watawa kukomesha tabia ya ukabila ambayo imeonekana kuzuka katika mashirika yao.

Mwadhama aliyasema hayo wakati wa ibada ya misa ya ufunguzi wa mkutano wa Mama Wakuu kutoka majimbo ya Kanisa Katoliki nchini, iliyofanyika katikati ya wiki katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katokili Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Mwadhama Pengo, alisema tabia ya ukabila siyo nzuri kwenye mashirika mbalimbali hususan ya kidini kwani inaweza kusababisha maafa mbalimbali likiwemo hili baya la kubaguana kwa misingi ya ukabila kimajukumu.

"Nyie Wamama Wakuu mkitaka kuwa wamama wazuri wa Kanisa la Tanzania na Afrika kwa ujumla, wenyewe mkubali kuukomesha katika mashirika yenu au katika jumuiya zenu kwani unaweza kusababisha maafa makubwa ingawa yanaweza yasifikie yale ya Rwanda na Burundi," alisema Mwadhama.

Aliongeza kusema kuwa, "Mkifanya kazi kwa ukabila, mnaweza kuiangusha kazi yenu ya utawa katika Kanisa. Na ikiwa hivyo, mtakuwa mnapoteza muda wenu bure afadhali mngeondoka na kwenda kujifanyia shughuli nyingine."

Mwadhama amewaonya Wamama Wakuu hao kutolichukulia kimzahamzaha suala hilo kwani litaharibu maana halisi ya neno utawa.Alisema hawana budi wenyewe kujua kuwa utawa ni changamoto katika maisha yao ya Kikristo na kwamba wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa kufuatia umoja wao katika Kanisa.

Vile vile, kardinali Pengo amewataka watawa hao wajue kuwa utume wao sio ule wa kujipatia miradi ama kufanya shughuli ambazo wanaona zitawataondolea umasikini na kuwasisitiza wazingatie kuwa hilo haliwezi kuondoa umasikini kwani kundi la watu fukara lilikuwepo tangu zamani.

Aidha, Kardinali Pengo aliwataka Wamama hao wakuu wa mashirika kuleta jimboni kwake watawa walio bora na sio kuwaleta wenye tamaa ya kujishughulisha na miradi yao iliyo nje ya utawa na utume wao kwa lengo la kujinufaisha kibinafsi baada ya kuwaona wameshindikana majimboni kwao.

Askofu Banzi awa Mwenyekiti wa CEPACS

Na Dalphina Rubyema

MWENYEKITI wa Idara ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Anthony Banzi, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu linaloshughulika na upashanaji habari katika Afrika nzima na Madagascar (CEPACS).

Askofu Banzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA), alichaguliwa na kutangazwa katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika nzima na Madagascar (CECAM) uliofanyika mjini Acra Ghana, Mei 16-19 mwaka huu.

Akizungumza jijiji baada ya kurejea nchini akitokea kwenye mkutano huo ambapo alikuwa akiwasilisha AMECEA, Askofu Banzi, alisema kuwa Maaskofu wa CEPACS walipiga kura ya siri ya kuwachagua Mwenyekiti na Makamu wake na kupeleka majina kwenye Kamati Kuu ya CECAM ambayo ilitangaza majina ya washindi.

Alisema aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti ni Askofu Fransis Alonge wa Jimbo Katoliki la Ondo nchini Nigeria ambaye alikuwa ni mjumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki wa nchi za Afrika Magharibi zinazozungumza Kiingereza (AECAWA).

Mkutano huo uliwakilishwa na wajumbe kutoka mikoa 9 inayounda CECAM aliyoitaja kuwa ni mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika Mashariki (AMECEA), Afrika ya Kati (ACERAC), Afrika Magharibi, nchi zinazozungumza Kiingereza (AECAWA) na Baraza la Maaskofu Katoliki la Misri (AHCE).

Mikoa mingine ni Baraza la Maaskofu Afrika Magharibi nchi zinazozungumza Kifaransa (CERAO), CERNA Afrika ya Kaskazini, IMBISA- Afrika ya Kusini na Madagascar.

Akielezea hisia zake baada ya kuchanguliwa kushika wadhifa huo, Askofu Banzi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga na Mwenyekiti wa Idara ya mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) alisema kuwa sasa majukumu yanazidi kuongezeka lakini hana budi kuyakubali kwani ndio wito wake kwa Mungu."Sasa inabidi niwajibike kwa maslahi ya jimbo langu niwajibike tena kwa maslahi ya Taifa hapo hapo tena niwajibike kwa maslahi ya Taifa hapo hapo tena niwajibike kwa maslahi ya AMECEA, pamoja na wajibu huo wote sina budi kuwajibika tena kwa maslahi ya CEPACS ambayo ni Idara iliyopo chini ya CECAM lakini yote lazima niyakubali kwa moyo mkunjufu maana ndio wito wangu kwa Mungu kwamba nitaitika popote nitakapoitwa" alisema Askofu Banzi.

Mwenyekiti wa CEPACS aliyepita ni Askofu wa Abidjan nchini Ivory Coast, Askofu Mkuu Berdard Agre na kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Askofu Banzi ndiye wa kwanza kuchaguliwa tangu CEPACS iundwe mwaka 1973.

 

Teknolojia isiyofaidisha wanawake haifai- Wizara

Agatha Rupepo na Getruda Madembwe

IMEELEZWA kuwa teknolojia yoyote isiyomsaidia wala kumuendeleza mwanamke katika maisha yake si sahihi na wala haifai kuendelezwa katika jamii.

Hayo yalisemwa katikati ya juma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana, Rozi Rugembe, wakati akifunga mkutano wa siku sita wa wajumbe waratibu wa maendeleo ya akinamama wa majimbo ya Kanisa Katoliki nchini(WID)uliofanyika katika ukumbi wa TEC jijini Dar-Es-Salaam.

"Teknolojia isiyomsaidia wala kumuendeleza mwanamke, siyo sahihi na lazima iwe muafaka na endelevu. Siyo ya kufanya leo tu, na kesho imekwisha, " alisema.

Katibu huyo wa wizara alisema ni vema wanawake wakafunzwa vema ili uwepo usawa katika kuongoza, na kwamba ni muhimu wakaimarishwa ili kutoa hisia zao kwa usahihi.

"Bila ya kuficha vipaji vyao, wawe mstari wa mbele kufanya mambo ya kijamii kwa usahihi na kimaadili," alisistiza.

Aliwahimiza akina mama hao kuanzisha mifuko ya kuweka na kukopa inayo sisitiza mkopo kutumika kwa miradi na mipango iliyokusudiwa.

"Mkopo lazima ulenge na kutimiza azma ya kuendeleza na kuboresha maisha ya familia" alisema.

Katibu huyo pia ameitaka jamii kujihadhari na ugonjwa wa ukimwi kwa kuachana kabisa na vitendo vya uasherati na akalaani tabia ya kuuficha na vifo vinavyotokana na ukimwi ili kuinusuru zaidi jamii dhidi ya maambukizo.

"Watu wengi maarufu wana kufa kwa ukimwi, lakini wanasemwa eti kafa kwa kisukari, TB na kansa. Tuwe wakweli na waaminifu katika suala la ukimwi kwa kuwa Mungu aliumba watu waishi sio wafe kwa ukimwi."

Awali wakisoma maazimio ya mkutano kwa mgeni huyo rasmi, waratibu wa WID wa majimbo Katoliki ya Mbulu,Tunduru/Masasi, Tabora na Sumbawanga, Bi. Ansila Tembo,Fortunata Mbeya, Bertha Kayila na Rosalie Mwanakulya,

walisema kuwa, kwa kutumia teknolojia muafaka na inayokwenda na wakati, wanawake wanaweza kujiongezea kipato, na kulinda hadhi zao na kujipunguzia mzigo wa kazi na gharama.

Walisema upo wa umuhimu wa wanawake kuelimishana ili watumie teknolojia yenye kuwanufaisha wao na jamii nzima kuondokana na utamaduni wa kuthamini mila potofu kwani zinakwamisha maendeleo ya jamii.

Walisema kwa kutumia teknolojia muafaka jamii inaweza kuhifadhi mboga kwa kutumia mionzi ya jua kukaushia na kutengeneza aina mbalimbali za urembo kwa kutumia mbegu za porini.

Aidha wajumbe hao wamewashauri wanawake kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa ili viweze kuwasaidia katika kujikwamua na hali ngumu ya uchumi.

Kutokana na mpango huo katika nchi za Zimbambwe na Afrika ya Kusini watu wanaweza kukaa pamoja na kushirikiana matatizo na mafanikio kuwa na sauti ya maamuzi na kushawishi masuala mbalimbali ya Kijamii kwa serikali.

Wataka familia za watoto wa mitaani ziwashiwe moto

Na Dalphina Rubyema

ILI kupunguza tatizo la watoto wa mitaani Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) vimetakiwa kuweka utaratibu maalum wa kuubana uongozi wa serikali za mitaa juu ya watoto wanaondoka mitaani mwao na kwenda mijini bila shughuli maalum.

Pendekezo hilo lilitolewa na washiriki wa warsha juu ya uhamasishaji wa masuala ya jinsia kwa kuweka nguvu itungwe sheria ya migogoro ndani ya familia. Warsha hiyo iliandaliwa na chama kisicho cha kiserikali cha kupambana na migogoro ya kifamilia na kufanyika katika jengo la Maarifa (NIP) jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki.

Wajumbe wa warsha hiyo ambao ni mahakimu, waandishi wa habari, wanasheria na wawakilishi wa Wizara ya Sheria na Katiba walifikia muafaka kuwa Serikali na NGOs wazibane Serikali za mitaa kufahamu idadi ya familia na watoto wanaokaa kwenye familia hizo ili endapo mtoto mmoja ama zaidi ataonekana kupotea basi wazazi wa familia husika wabanwe.

Walisema wazazi waulizwe na uongozi wa mtaa mahali alipo mtoto wao na ikibainika kuwa katoweka kwa mazingira yasiyoridhisha hatua za kisheria zichukuliwe kumwajibisha mzazi.

Katika warsha hiyo pia ilielezwa kuwa jamii haina budi kuangalia kwa makini suala la haki kwa watoto wanaozaliwa nje ya ndoa kwani lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa uvunjaji wa ndoa.

Mwakilishi wa Wizara ya Sheria, Bi. Iman Aboud, aliiambia warsha hiyo kuwa suala hilo lisipoangaliwa kwa makini linaweza kusababisha baadhi ya wazazi kuendeleza mambo ya uasherati nje ya ndoa kwa kujipa matumaini kwamba hata akipata mtoto sheria inasema kuwa watoto wote wa nje na ndani ya ndoa wana haki sawa.

"Kwa mawazo yangu binafsi tamaa za kimwili ni moja ya machimbuko ya matatizo katika familia na ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa hivyo kinachotakiwa kuangalia ni jinsi gani watoto hao wanavyojenga ama kubomoa familia. Tuangalie sana tusije tukawa tuna-encourage uzinzi," alisema Bibi Iman.Wajumbe wa warsha hiyo ya siku moja pia walipendekeza kuwa jamii lazima iwe wazi hasa kwa upande wa watu wawili wanapotaka kufunga ndoa kwamba lazima kila mmoja amweleze mwenzake kama ana mtoto aliyezaa na mtu mwingine na siyo mmoja anapokufa ndipo mtoto ajitokeze eti kaja kwenye msiba wa baba au mama yake.

Kwa miaka mitatu tu,watu 4800 wafia barabarani

Na Getruder Madembwe

WATU 4820 wamefariki dunia kutokana na ajali za barabarani zilizotokea nchini nchini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutokana na makosa mbalimbali.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, Kamishna Msaidizi wa Pilsi Luther J. Mbuthu, ameliambia gazeti hili ofisini kwake katikati ya juma kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo ofisini kwake ajali hizo zilitokea miaka ya 1997, 98 na 99.

Ajali zilizotokea katika kipindi hicho ni 40047 ambapo watu 36716 pia walijeruhiwa.

Amesema mwaka 1999, madereva 105, abiria 638, wapanda pikipiki 55, wapanda baiskeli 195 na waenda kwa miguu 619, walifariki dunia wakati mwaka 1998, madereva 97, abiria 623, wapanda pikipiki 46, wapanda baiskeli 192 na waenda kwa miguu 625 walifariki.

"Afande" Mbuthu alifafanua kuwa, mwaka 1997, jumla ya ajali 14,335 zilitokea nchini kote na kusababisha vifo vya watu 1625 na majeruhi 12490.

Mwaka 1998, ajali zilipungua kwa kiasi cha 2101 na kufikia 12,234 zilizosababisha vifo 1583 na majeruhi 11381 ambapo mwaka 1999, ajali zilikuwa 13,478 zilizopelekea vifo 1612 na majeruhi 12845.

Alizitaja baadhi ya sababu za ajali hizo kuwa ni pamoja mwendo mkali na akatoa mfano wa ajali iliyotokea Mei 28, mwaka huu mjini Dodoma katika makutano ya barabara ya Arusha iliyopo mjini hapo, baada ya gari walilokuwa wakisafiria wanafunzi kutoka Kondoa kwenda Dodoma karibu na uwanja wa ndege, kupinduka baada ya dereva kushindwa kukata kona kutokana na mwendo mkali.

Hadi Mei 30, watu wawili walikuwa wamefariki dunia na wengine 87 kujeruhiwa.

Sababu nyingine ni uchakavu wa magari kutokana na kasumba mbaya ya wenye magari kuwaachia jukumu lote la uangalizi madereva na kwamba hali hiyo imechangia ajali kati ya 16%-20% ya ajali zilizotokea nchini.

Nyingine ni uzembe wa watumiaji wa barabara, kukosekana kwa alama za barabarani katika maeneo mengi ya mijini na vijijini na kwamba hali hii imesababishwa na ufinyu wa bajeti kwa mamlaka zinazohusika, ulevi, ujenzi holela kando ya barabara pamoja na ongezeko la watu na magari.

Alifafanua kuwa ongezeko la magari na wingi wa watu hasa maeneo ya mijini, haliendi sambamba na upanuzi wa barabara na uwekaji wa taa za kuongozea magari hali inayosababisha msongamano na hivyo kutoa nafsi kubwa ya kutokea ajali.

Alitoa mfano kwa mkoa wa Dar-Es-Salaam kuwa unaongoza kwa ajali ukilinganishwa na mikoa mingine kwa kuwa una idadi kubwa ya watu na ongezeko kubwa la idadi ya magari, ukifuatiwa na mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mbeya na Iringa.

Kamanda Mbuthu alisema kikosi chake, idara mbalimbali za serikali na mashirika binafsi wanaendelea na juhudi kali za kukabiliana na ajali hizo baadhi yao zikiwa ni pamoja na kufanya doria za mijini na kwenye barabara kuu ili kukamata na kuwazuia wanaokiuka kanuni za usalama barabarani.

Nyingine ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuwahimiza wenye magari wayatengeneze au kuwafikisha mahakamani kutokana na kuendesha magari mabovu.

"Utaratibu wa wa mashitaka kwa njia ya notification upo kwa mujibu wa kifungu Na. 95 cha Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30/1973," alisema katika taarifa yake.

Pia kuwatoza madereva wazembe faini ya shilingi 20,000 ili waweze kuzingatia zaidi umakini katika kazi zao kwa kuhofia kulipa kiasi hicho ambacho ni kikubwa kwa mwananchi wa kawaida.

Jeshi la Polisi pia limekuwa likitoa mafunzo kwa umma likishirikiana na idara nyingine na taasisi za serikali kwa kutumia vyombo vya habari na njia nyingine na hivi karibuni, somo la usalama barabarani, limeingizwa katika mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu.

Kamanda Mbuthu amesema kamwe kikosi chake hakitawafumbia macho wanaosabaibisha ajali kutokana na uzembe wao na akawaomba wananchi wote kutoa ushirikiano na kukemea dalili zozote za kuhatarisha usalama barabarani.

Mstawaliwe na pesa-Askofu

Na Dalphina Rubyema

JAMII imetakiwa kuachana na mawazo ya kutawaliwa na pesa ambayo inaweza kumsababishia mtu kuuza uhai wake na badala yake imeshauriwa kumtegemea Mungu ambaye ndiye njia kuu ya kuweza kuwapatia watu ujazo wa mambo mema katika maisha.

Rai hiyo ilitolewa katikati ya wiki na Mwenyekiti wa Idara ya Baraza la Walei katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Magnus Mwalunyungu wakati akifungua mkutano wa majimboni uliofanyika TEC.

Askofu Mwalunyungu alisema kuwa kila mmoja hana budi kutenda mambo yenye kuwa na ukweli ndani yake na siyo kufanya kazi yako kwa kutegemea kuwa lazima upewe kitu fulani.

Alisema hata Mungu alimtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu na wala hakutaka mtoto wake alipwe na hata mtoto mwenyewe hakutaka alipwe.

Alisema kazi hususani zile za kimungu lazima mtu azipende kama mzazi anavyo mpenda mwanae kwa kulazimika kumlea kwa upendo wa hali ya juu bila kupewa ama kudai malipo yoyote.

"Wazazi ni watwana na siyo mabwana wanafanyakazi za kuwalea watoto wao bila malipo , hapa kinachofanyika ni mabadilishano ya upendo!" alisema.

Mhashamu Mwalunyungu ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru, alisema kuwa watu wa dini ni lazima kufanya hivyo watakuwa wanamsindikiza Yesu Kristo aliyeteswa na kufa msalabani kwa ajili ya ulimwengu.

"Mtakatifu Agustino anasema kuwa hakuna mabishano kwamba Yesu Kristo alikuja duniani kukomboa ulimwengu lakini wanadamu walimuuwa sasa na wewe ama mimi na yule lazima tusimame imara pale tunapoteswa tusiogope na kutetemeka katika hayo mateso huenda kuna jambo zuri lina kusubiri" alisema Askofu Mwalunyungu.

Mkutano huo wa siku tatu uliwashirikisha wakuu wa Idara za Walei, Wakurugenzi, Makatibu watendaji na Wenyeviti wa vyama vya kitume ambapo kwa siku ya kwanza ulifanyika TEC na kumalizika kwenye kituo cha Walei Bakanja