BAADA YA DK. LAMWAI KURUDI ALIKOTOKA:

CCM yawasubiri kwa uchu Marando,Tegambwage

lWadaiwa kuvizia kwanza kitita cha mwisho bungeni

lMangula auita upinzani, gari bovu

Na Neema Dawson

WAKATI baadhi ya wanasiasa maarufu wakizidi kurudi katika chama tawala cha CCM, Chama hicho kimedaiwa kufanya mikakati ya kuzidi kuwarejesha wanasiasa wengine maarufu na kwamba sasa kinawasubiri kwa hamu, Bw. Mabere Marando na Ndimara Tegambwage.

Pia, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Bw. Philip Mangula, amevifananisha vyama vya upinzani na magari mabovu ambayo hukimbiwa na abiria na hata madereva wake na akasema ndio maana vinakimbiwa kwani hata viongozi wa vyama hivyo wamebaini kuwa havitawafikisha popote kimaendeleo.

Habari zilizopatikana toka ndani ya chama hicho tawala juu ya wanasiasa wengine maarufu wa vyama vya upinzani wanaotarajiwa kujiunga na CCM, zinasema wanasiasa hao, Bw. Mabere Nyahucho Marando ambaye ni mbunge wa jimbo la Rorya (NCCR-MAGEUZI) na Ndimala Tegambwage Mbunge wa NCCR, jimbo la Muleba, wanasubiri Bunge la Mwisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limalizike ili walipwe posho zao za Bunge na kuwa huru baada ya Rais kuvunja Bunge.

"Bunge litakapo vunjwa, ni dhahiri kuwa hata viongozi wengine wa upinzani mbali na hao, watazidi kurudi CCM kwa kuwa wanajua wakijitangaza kwa tiketi ya CCM kugombea hata ubunge, watapata kuliko kwenye vyama vyao ambavyo muda wao mwingi umekuwa kwa ajili ya malumbano ya wenyewe kwa wenyewe ...Na sisi hao hatutakuwa na neno nao maana sisi tunachokitaka, ni kuboresha chama," alisema mwishoni mwa juma katika Ofisi Ndogo za Chama hicho, mmoja wa vigogo wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msema ji wa chama.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi hizo za CCM zilizopo Lumumba jijini, Katibu Mkuu wa CCM, Bw.Philip Mangula alikanusha madai ya baadhi wa wanachama wa vyama vya upinzani kuwa CCM wamekuwa wakiwarubuni viongozi wa vyama vyao ili wajiunge CCM

"Kumekuwa na maneno ya uzushi kuwa viongozi CCM wanawarubuni hawa watu wa upinzani ili warudi CCM; na hayo ni maneno ya uzushi tu, hayana ukweli wowote kwa sababu hakuna kiongozi yeyote anayeweza kumrubuni kiongozi mwenzake akubali. Lakini, kama mtu ameridhika na chama chetu akaamua kukihama chake, tunamkubali."

Alisema Bw. Mangula na kuongeza, "Siyo kweli kwamba tunawarubuni watu kuhamia CCM, lazima jamii ielewe kuwa vyama vya upinzani vimekwisha chemsha sasa vipo tu, kama magari mabovu ambayo yanashindwa kuendelea na safari mpaka abiria na hata madereva wengine wanayakimbia na kupanda mengine."Wakati nchi nzima imeanza kuwa katika hekaheka za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, baadhi ya viongozi na wanasiasa maarufu wa vyanma vya upinzani nchini wamekuwa wakijitoa kwenye vyama vyao na kurudi kujiunga na chama tawala cha CCM na hata kiongozi wa chama cha TLP, Augustine Lyatonga Mrema, alisema hivi karibuni kuwa endapo CCM itampa nafasi ya kugombea urais, atajiunga nao.

Baadhi ya viongozi wa upinzani waliojiengua katika vyama vyao na kujiunga na CCM kwa siku za hivi karibuni ni pamoja na Bw. Makongoro Nyerere aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, (NCCR_MAGEUZI), Bw. Salum Seif Msabaha aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Mkunazini Visiwani Zanzibar (CUF), Dk. Luther Nelson , mbunge wa Kibaha (CHADEMA), wakati chama cha TLP kiliondokewa na mjumbe wake wa Seneti, Abasi Mtemvu.

Dk. Masumbuko Lamwai aliye kuwa mbunge wa RahaLeo (NCCR_MAGEUZI) miezi ya hivi karibuni alimuomba radhi Rais Mkapa, na serikali yake ya CCM, na wiki iliyopita, amejiunga rasmi na chama hicho tawala na viongozi mbalimbali wa upinzani wamekuwa wakimponda kwa madai kuwa anahangaishwa na njaa.

WAKATI NCHI INAELEKEA UCHAGUZI MKUU

Tume ya Haki na Amani kuelimisha wanafunzi juu ya Uchaguzi Mkuu

Na Getruda Madembwe

Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Paul Ruzoka, amesema Tume yake itahakikisha kuwa somo la uraia linatiliwa mkazo katika shule za Sekondari kwa kusambaza vitabu vya somo hilo ili kujua mambo muhimu wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.

Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Kigoma, aliyasema hayo wakati akifunga semina ya siku tatu iliyoandaliwa na Tume ya Haki na Amani iliyofanyika hivi karibuni katika Kituo cha Kiroho kilichopo Mbagala Jijini Dar-Es-Salaam na kuhudhuriwa na watendaji wa Tume hiyo kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki.

Alisema nia ni kuwahamasisha wanafunzi kujua mambo muhimu juu ya Uchaguzi Mkuu ujao ambao alisema ndio vijana wa kutegemewa na watawala wa jamii ya Watanzania kwa siku za usoni kwa vile ndio wenye nguvu na wanaopaswa kufahamu zaidi jukumu lao katika kulijenga taifa katika misingi ya amani na utulivu hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kuingia Awamu ya Pili ya uongozi wa serikali katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Uchaguzi wa pili utakaovihusisha vyama vingi vya siasa nchini, unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, wakati wananchi watamchagua rais, wabunge na madiwani.

Mhashamu Ruzoka, alisema vitabu hivyo vya URAIA vitasambazwa katika shule zote za sekondari zisizo za Serikali ili iwe rahisi kwa kila mwanafunzi kukipata na kukitumia ipasavyo.

"Nia ya Maaskofu wote ni kuhakikisha kuwa vijana wanahamasishwa vilivyo na si kwa Wakatoliki tu, bali hata imani nyingine," alisema na kuongeza, "Tumeamua kuwahamasisha vijana hao na tunahakikisha kuwa tunatilia mkazo katika vitabu hivyo ambavyo vitasambazwa bure katika shule zote ambazo si za kiserikali"

Alisema ipo haja kwa Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha kuwa maamuzi muhimu yanayotolewa nchini hayawaumumizi wanajimii na akasisitiza kuwa azma ya watu wanaotaka kuingia madarakani kuwa waaminifu katika matendo kwa kuwa hao ndio watakaolitumikia vema taifa.

"Kama Kanisa Mama, linasali kwa pamoja na si kwa kanisa tu bali ni kwa watu wote ili wawe na umoja" alisema Mhashamu Ruzoka na kuhoji kuwa, "Ni nani angependa damu yake imwagike? Lakini ikimwagika ya mwingine tunafurahi, hivyo basi tunatakiwa kuhakikisha kuwa umoja hauharibiwi"

Mwanasheria awashitaki Wamasai, Wabarbeig kwa serikali

lAsema wanawaua watoto walemavu, eti ni mkosi

Na Leocardia Moswery

MWENYEKITI wa Kituo cha Haki za Binadamu na Mjumbe wa kamati ya SHAHRNGON, Bw. Gidione Kaino, ameishauri serikali kuyatupia macho makabila ya Wamasai na Wabarbeig ili kukomesha mila mbaya za kuwaua watoto wanaozaliwa wakiwa na ulemavu.

Akizungungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake ilipo hosteli ya SIDO jijini hivi karibuni, Bw. Kaino alisema,makabila hayo ya mkoani Arusha, yanahitaji kumulikwa na kuelimishwa zaidi ili kuepuka tabia hiyo ya kuwaua viumbe hao wadogo wasio na hatia kwa kisingizio cha ulemavu ambao alisema sio kosa lao kuwa walemavu na kwamba mila inayowatuma kufanya hivyo, inawatuma kufanya mauaji hali ikiwa bayana kuwa ni kinyume cha haki za binadamu.

"Hivi hata wewe (mwandishi) ulishamuona Mmasai mlemavu wa aina yoyote? Au, unadhani wao wanaujanja gani hawazaliwi vilema. Inasemekana kuwa mtoto akizaliwa huko akiwa na ulemavu wowote, anauawa au kunyimwa kabisa huduma zozote maana anakuwa hathaminiki tena." Alisema Bw.kaino ambaye ni mwanasheria na kuongeza,

"Ni kweli, hebu wewe mwenyewe fanya utafiti. Kama utamkuta Mmasai au Mbarbeig mwenye ulemavu, ni mmoja ambaye labda hakuzaliwa kule."

Bw. Kaino alisema yeye akiwa mlemevu ni mlemavu wa macho, amefanya utafiti binafsi mkoani Arusha, hususan katika wilaya za Hanang na Monduli ambapo aliwakuta ni watu wa makabila hayo pekee wasio na walemavu.

Alisema kuwa alipozungumza na baadhi ya Wamasai na Wabarbeig, walimueleza kuwa ni vigumu kumkuta mlemavu katika jamii yao kwa kuwa nayezaliwa katika hali hiyo hunyimwa huduma na pengine kuuawa kabisa.

Alisema kuwa Wamasai na Wabarbeig hao walibainisha kuwa kuwepo kwa mtoto mlemavu katika jamii yao, ni hali inayoashiria na kutafsiriwa kuwa mkosi unaoaminika kuwa ni laana inayotolewa na Mwenyezi Mungu katika familia.

"Hata mimi mwenyewe waliniambia kuwa ningezaliwa katika makabila hayo, tayari ningeshauawa ingawa walishindwa kuelewa na kuomini kuwa mtu kipofu ninawezaje kusoma na kuwa mtaalamu," Alisema Kaino na kuitaka jamii nzima ya Watanzania kukemea kwa vitendo mila hiyo chafu.

Amezidi kuishauri serikali kuwasaidia kwa kuwatetea na kuwaelimisha walemavu hao wanaoonekana nuksi katika familia ili kuzidhihirishia jamii hizo kuwa mawazo yao dhidi ya walemavu ni potofu na kwamba na walemavu ni watu sawa na wengine na wanaweza kufanya mambo ya maendeleo katika jamii kwa kadri ya maumbile yao endapo watasaidiwa kwa hali na mali.

Alisema chama hicho kisicho cha kiserikali kinaandaa utaratibu ili kiweze kutoa elimu na afya katika mkoa wa Arusha hususan wilaya zenye makabila hayo ili kuyaelimisha yaelewe kuwa ulemavu ni jambo la kawaida na hata mlemavu mwenyewe ana haki sawa miongoni mwa wanajamii.

Askofu awakandia wanaume wakware, awatetea 'machangudoa'

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, Basil Sambano, amewatetea machangudoa na wakati huohuo, kuwalaumu baadhi ya wanaume na viongozi wa serikali kwa kuwa chanzo na chachu ya kushamiri kwa biashara ya ukahaba.

Aliyasema hayo ofisini kwake jijini wiki iliyopita wakati gazeti hili lilipotaka kujua Kanisa lake linaisaidia vipi jamii katika kupambana na vitendo viovu ambavyo vimekuwa vikiongezeka siku hata siku na kuifanya serikali ihitaji zaidi msaada wa vikundi vya kidini katika kuboresha maadili ya jamii.

Askofu Sambano, alisema, si vyema kuwalaumu wanawake wanaofanya kazi hiyo pekee (Machangudoa) peke yao, kwa kuwa wanaungwa mkono na kusaidiwa na wanaume na baadhi ya viongozi wa juu wa taasisi mbalimbali ambao alisema, hawana budi kuionea aibu hali hiyo ya kuwa wateja wa biashara hiyo haramu inayohatarisha afya na kuudhalilisha utu wa mwanadamu.

Alisema jami

"Jamii imekuwa ikiwaangalia wanawake kama wao ndio wakosaji kutokana na biashara hiyo wanayoifanya. Jamii inawalaumu tu, bila kuchunguza biashara hiyo inawapendeza watu gani, ambao wanakuwa ndio wateja wao" alisema.

Alionesha wasiwasi wake juu ya juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam, Luteni Yusufu Makamba, za kuwaondoa machangudoa jijini,na akasema huenda zisizae matunda bora au zisifanikiwe kabisa kwa kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaume wakubwa wanaojenga urafiki wa karibu na machangudoa hao.

Alisema badala ya viongozi hao ambao hakutaka kutaja majina yao kushiriki uhalifu huo na kumpa kazi ngumu Luten Makamba, wanapaswa kuziunga mkono juhudi zake ili kulinusuru taifa katika maangamizi hayo ya kimaadili kwa kuwa uhusiano wa karibu kati ya machangudoa na vigogo hao, unaweka ukomo wa mafanikio ya kazi ya Luteni Makamba.

Akisisitia azma yake ya kuwalaumu wanaume wanaoshiriki biashara hiyo ya ukahaba, "Huwezi ukafanya biashara kwa muda mrefu bila kupata faida na bado ukaendelea kujihusisha na biashara hiyo bila ya kukata tamaa.

Hawa wanawake nao wameamua kuitumia miili yao kwa kufanyia biashara kwa kuwa wanapata wanapata faida ya kutosha. Wanajua wateja wao wapo na wengine ni watu wakubwa, hawawezi kuiacha hata kama Mkuu wa Mkoa ataendelea kuwazuia"

Alisema na kuongeza kuwa dawa ya kutibu tabia hii mbaya ni wanaume wote wenye tabia hiyo kuachana nayo kabisa kwa kuwa hawatapata mteja.

"Wakitembea kwenye mitaa yao bila kupata wanaume kwa muda wa wiki moja mfululizo wao wenyewe wataamua kuacha kujishughulisha na kazi hiyo na kuamua kufanya shughuli nyingine zenye manufaa na maendeleo katika jamii" alisema.

Aidha, aliwashauri viongozi wengine wa dini kukemea vikali tabia hiyo kwa kuwa kazi za viongozi wa dini ni kuponya roho za watu.

Miezi ya hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar-Es Salaam, Luteni Yusufu Makamba, alianzisha operesheni maalumu ya kusafisha jiji kwa kuwaondoa ombaomba na machangudoa ili warudi makwao na kutumia nguvu kazi zao kufanya shughuli halali za uzalishai mali.

Askofu awataka wasomi wasiwe kupe

Na Josephs Sabinus

WAHITIMU wa taasisi za elimu wametakiwa kutokuwa kupe kwa kutofanya kazi huku wakijivunia elimu waliyoipata, bali waitumie katika kuboresha maisha yao na maendeleo ya taifa.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini, alipokuwa akizungumza katika mahafari ya saba ya kidato cha sita ya sekondari ya St. Anthony, jijini Dar-Es-Salaam ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 109 na kutoa tuzo na vyeti kwa walimu na wanafunzi bora katika masomo mbalimbali.

Shule hutoa "St. Anthony Schoolarship" kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kwa kuwapunguzia sehemu ya ada au kutokulipa kabisa kwa mwaka unaofuata ikiwa ni njia ya kuhamasisha mwamko zaidi wa kitaaluma.

"Hakikisheni hamuwi kupe, eti kazi iwe ni kula tu, lazima mfanye kazi. Watu wa wanaowajibika ndio taifa linawategemea kwa sababu huwezi kwenda popote ukafanikiwa, kama hauna juhudi na maarifa katika shughuli na mipango yako."

"Hata kama baba yako ana pesa, ukingoja tu, eti kazi iwe ni kula tu, bila kufanya kazi, maisha yako yamo hatarini na utaishia kwenye madawa ya kulevya tu, na madhara yake kila mtu anayajua."

Aliilaani tabia ya baadhi ya wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kujitenga na kutoshirikiana na wanajamii wengine huku wakichagua kazi na akabaini kuwa mawazo ya namna hiyo na kutegemea kuajiriwa serikalini yamepitwa na wakati.

Akizungumzia suala la madili, alisema, "Huko muendako, mkijiheshimu, mtaheshimika; lakini mkitenda vitu vya ajabu, mtakuwa na kuonekana wa ajabu."

Aliwataka wahitimu hao kuimarisha nidhamu ili asiwepo mwanafunzi anayewashawishi walimu kutumia kiboko kumuadhibu.

"Inasikitisha, ni vipi afikie hatua ya kubidi kupigwa kiboko katika shule ya Kanisa. Mwanafunzi anayeona hawezi kulinda nidhamu yake, ni bora arudi nyumbani achapwe viboko na wazazi wake kwanza, akielewa maana ya maadili, arudi,"

Alisema na kuongeza, "Msiwaone hata hao mapadre, hivi mnadhani wao wana tofauti na watu wengine? Hawana tofauti bali tu wamenolewa katika maadili mema na nidhamu. Hilo hata nyie mnaweza. Nataka muwe wazalendo wenye nidhamu." Alisema Askofu.

Akisoma risala yake kwa Askofu Kilaini aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafari hayo Jumamosi iliyopita, Mkuu wa Shule hiyo, Bro. Pius Kihuru alisema, shule yake inalenga kuhakikisha inapunguza au kuondoa kabisa idadi ya wanafunzi wanaofaulu kwa daraja la tatu na la nne na kuongeza wanaofaulu kwa daraja la kwanza na la pili.

Alisema katika kufanikisha azma hiyo, shule ina mpango wa kuongeza idadi ya kompyuta kwani 15 zilizipo hazitoshi kwa wanafunzi 1300, kupanua maabara na kuboresha huduma za maktaba na maslahi ya walimu.

Katika risala yao kwa wahitimu iliyosomwa na Bi. Dorina Kilana wa kidato cha tano kwa niaba ya wanafunzi wanaobaki, waliwata wahitimu hao kutokuringa na kuwadharau ambao hawajafiki kidato cha sita.

Mwaka 1998, shule ilikuwa ya 49 kati ya 128 na mwaka 1999, ilikuwa ya 38 kati ya 138 za kidato cha sita. Kwa kidato cha nne, mwaka 1998 ilikuwa ya 33 kati ya 611 wakati mwaka 1999, ilikuwa ya 33 kati ya shule 666.

Wahitimu wengi wa shule hiyo kutokana na maendeleo mazuri kitaaluma, wamekuwa wakiendelea na masomo ya elimu ya juu katika vyuo vikuu vya Dar-Es-Salaam, Chuo cha Usimamizi wa Fedha na wengine wapo Uingereza na Marekani kwa masomo ya juu.

Vyombo vya kutetea haki za binadamu, msibweteke-Paroko

Elizabeth Steven

VYOMBO vya kutetea haki za binadamu nchini vimeshutumiwa kwa madai kuwa vinabweteka na vyenyewe kuanza kwenda kinyume kwa kushughulikia maslahi binafsi huku vikiiacha jamii na ikizidi kuathirika.

Shutuma hizo zilitolewa na Paroko Brian Mkude wa Kanisa la Katoliki Parokia ya Makuburi jijini Dar-Es-Salaam, alipokuwa akiendesha ibada kanisani hapo Hivi karibuni.

Alisema kuwa uchunguzi wake binafsi umembainishia kuwa vyombo kadhaa vilivyoanzishwa kwa lengo la kutetea haki za binadamu havifanyi kazi inayokusudiwa na badala yake vinatetea maslahi ya watumishi wake binafsi.

"si kweli kuwa vinatetea haki, vinatetea maslahi yao binafsi. Nenda sehemu mbalimbali utakuta kibao kimeandikwa, TUME YA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU, lakini si kweli, wanatetea maslahi binafsi," alisema na kuongeza, ‘"Mara nyingi vituo hivyo huwa vya kwanza kusikiliza kesi za watu lakini haviwajibiki katika kuyatatua matatizo yao".

Akizidi kuulaumu utendaji kazi duni wa vituo hivyo vya kutetea haki za binadamu, padre Mkude alisema, "Vituo hivyo vinafanya nini wakati watoto katika vyombo hivyo hawapelekwi shule sababu hawana ada, wanazuiwa kuingia ndani ya daladala na si kwa sababu eti hawana nauli, laa! Ni kwa sababu vyombo hivyo haviwajibiki".

Amewalaumu wamiliki wa makampuni mbalimbali nchini kwa kuweka mabango makubwa ya matangazo yanayogharimu kiasi kikubwa cha pesa badala ya kuchangia walau kiasi kidogo katika kusaidia kuondoa matatizo yanayosababisha uduni wa huduma muhimu za kijamii.

"Mfano, bango moja linagarimu shilingi milioni mbili ambapo faida yake ni ndogo sana,hailingani na pesa hiyo. Shule nyingi zina upungufu wa madarasa utakuta darasa moja lina wanafunzi 100 je hizo fedha zilizotumika kuweka tangazo kama hilo, zingelitumika kujengea madarasa, yangejengwa mangapi?" alihoji.

Ameitaka jamii kutowasifia na kuwafanyia sherehe viongozi ambao wanachaguliwa katika chaguzi mbalimbali kwani kufanya hivyo ni kuwaambia wasiwajibike katika kazi zao na badala yake wajineemeshe katika nafsi zao na sherehe hizo zikiwa sehemu za kuanzia.

Alisema mchungaji mwema ni yule anayeangalia "kondoo" wake, aliyejitoa kwa hiari yake bila kulazimishwa na anayefahamu na kuwa na kiu ya kushughulikia matatizo ya kondoo wake.

Akitoa mfano, Padre Mkude alisema, mara nyingi mtu anapoenda hospitali atakuta madaktari ni wengi lakini kati yao lazima atakuwepo daktari ambaye anapendwa kwa vile anawajali watu wake, mwepesi wa kufahamu matatizo yao na mkarimu kwa watu.

Aliongeza kusema kuwa ‘katika mazigira yetu tunafahamu kuwa mchungaji mwema anaweza kuwa mwanasiasa mwalimu, baba au mama lakini kila mtu anaweza kuwa mchungaji ili mradi awajibike vema kufanya kazi ya Mungu.

Madiwani wamng'oa madarakani 'mzito' wa Wilaya

Na Mathias Marwa, Musoma

KIKAO cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kimepitisha azimio la kumuondoa madarakani mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo. Bw. Maguta Nyakiha.

Baraza hilo la madiwani lililoketi Mei 24, mwaka huu lilidai kuwa halina imani na utendaji kazi wa Mwenyekiti huyo kutokana na kughushi muhtasari ripoti ya baraza hilo mwaka 1998 na Muhtasari No 87 wa mwaka 1999.

Baraza hilo pia lilimuondoa madarakani aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halamashauri hiyo Bw. Teobald Rugira, kwa kushirikiana na Bw. Nyakiha kughushi mihtasari hiyo. Bibi Elizabeth Kitundu aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi awali alikuwa ni Afisa Mipango wa Wilaya.

Madiwani hao 21 kati ya 27 waliohudhuria kikao hicho waliazimia pia kuwafikisha watuhumiwa mahakamani baada ya kuorodhesha majina yao kuhalalisha uamuzi huo.

Hata hivyo Bw. Nyakiha ambaye hakuwepo katika kikao amesema kuwa yeye bado ni mwenyekiti kwa kuwa uamuzi wa madiwani hao haukufuata taratibu za kisheria hivyo akauita kuwa ni batili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti huyo alidai kuwa sheria Na 7 ya mwaka 1982 kama ilivyorekebishwa 1995 inayozungumzia tararibu za kumuondoa mwenyekiti madarakani haikufuatwa.

SHDEPHA+ kufanya tamasha Mbeya

Na Dalphina Rubyema

KUFUATIA kukithili kwa vitendo vya uasherati mkoani Mbeya Chama cha Maendeleo kwa Watu wanaoishi na Virus vya Ukimwi nchini (SHDEPHA+) kwa kushirikiana na shirika la kudhibiti magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi (GTZ) wanatarajia kuendesha tamasha ya siku moja mkoani humo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa SHDEPHA+ Taifa Bw. Joseph Katto, tamasha hilo la wazi litafanyika Juni Mosi, mwaka huu ambayo washiriki watakuwa ni watu wa rika zote wakiwemo wazee, vijana na watoto.

Bw. Katto ameyasema ofisini kwake hivi karibuni kuwa wakiwa mkoani humo wenyeji wao watakuwa shirika la kibinafsi linaloshughulikia masuala ya kulea wagonjwa la mkoani humo linalojulikana kama ‘KIOMBE’.

Alisema lengo la tamasha hilo ni kupeleka mwamko wa Ukimwi kwa wananchi wote wa Mbeya ili wakazi wa maeneo hayo wapate elimu sahihi ya ugonjwa huo hatari."Mbeya wameathirika sana hivyo ni lazima tukae kidete katika kupiga debe la kuwahamasisha wana Mbeya waachane na mambo ya starehe yanayowapelekea kujisahau na kupata nafasi ya kuambukizana maradhi," alisema.Bw. Katto ambaye ni Mwenyekiti wa mtandao huo, alisema matawi yake yapo katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Shinyanga, Ulanga, Iringa,Tanga, Mbeya na Dar es Salaam.

Wanunuzi wapamba watakiwa kulipa taslimu

Na Dalphina Rubyema

WANUNUZI wa zao la Pamba nchini wametakiwa kulipa pesa taslimu kwa wakulima wakati wakati wa msimu mpya wa ununuzi utakaofunguliwa rasmi Juni 19, mwaka huu.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Meneja Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mbegu Tanzania (Tanzania Cotton Lint and Seed Board) Dk. Joe Kabissa wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini.

Alisema kila mkulima ni lazima ahakikishe anapewa pesa yake taslimu pamoja na stakabadhi baada ya kuuza pamba yake na kuwataka kuuza pamba yao kwa wale wanunuzi wenye vibali.

Meneja huyo amewataka pia wakulima wa zao hilo kuzingatia ubora wa mazao yao na akawakumbusha kuvuna mara tu, inapokomaa na kuihifadhi mahali pasafi kwa makundi kulingana na ubora kabla ya kuiuza.

Bw. Kabissa amewahimiza wanunuzi kuangalia kwa makini ubora wa pamba na kuipima kwa ufasaha kwani kitengo cha upimaji kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kitapitia tena upimaji wa pamba hiyo kabla ya kuipeleka kunakohusika.

Amewataka wazingatie kuiweka pamba yao kwenye maboksi yatokayo onesha kundi A na B na kila kundi lizingatie ubora wake.

Katika kufanikisha yote hayo Mamlaka ya Wilaya na Mkoa zimeombwa kulinda vyama vyake vya msingi vilivyo chini ya mamlaka husika kwa kusimamia ipasavyo zoezi hili.

Shule ya Kanisa yaiomba serikali msaada wa barabara

Sr. Dafrosa Msemwa na Keneth Lyanga Morogoro

SERIKALI imeombwa kuisaidia shule ya sekondari ya Kikristo ya Msolwa iliyoko katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ili iweze kutengenezewa barabara yenye umbali wa kilomita 50 kutoka mikumi kwa kuwa iliyopo sasa iko taabani.

Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni na kiongozi wa shule hiyo Padre Patric Rakeketsi wakati wa ufunguzi wa shule na sherehe za kuwaaga wanafunzi waliomaliza kidato cha sita shuleni hapo.

Katika hotuba yake Padre Rakeketsi alisema "Katika karne hii mpya lengo ni kuondoa umaskini na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa hiyo tunaimba Serikali yetu ya Muungano itusaidie ili tuweze kuwaelimisha watoto wa Afrika"

Alisema katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia barabara nzuri, umeme na mawasiliano ni vitu vinavyohitajika sana ili kuiwezesha jamii kufikia malengo na mafanikio yanayotarajiwa katika siku za baadaye.

Pia katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali wakiwemo Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Bw.Lawrance Gama.

Askofu Mkude alisema kuwa shule ya Msolwa ni taasisi ya Kikatoliki lakini, haina maana kwamba shule hiyo itachukua wanafunzi wa Kikatoliki tu, bali hata madhehebu ya dini nyingine.

Hata hivyo alisema sera na kanuni zitakazotolewa zitazingatia imani ya kikatoliki na kuangalia msimamo mwema ili wanafunzi wajiandae kwa maisha ya baadaye.

Naye mkuu wa Mkoa Bw. Gama alitoa shukrani kwa Askofu wa Jimbo la Morogoro kwa kuruhusu shule hiyo kujengwa kwani inasaidia jamii katika masuala ya elimu.

CARITAS TANZANIA yawaambia wanawake, tafuteni maendeleo

Na Getruda Madembwe

WANAWAKE kote nchini wamehimizwa kusimama kidete kupigania maendeleo katika familia zao na taifa kwa ujumla. Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa juma na Mwenyekiti wa Shirika la Misaada la CARITAS- Tanzania lililopo chini ya Kanisa Katoliki, Askofu Agapiti Ndorobo, wakati akifungua mkutano wa maendeleo ya akina mama majimboni (WID) uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)mjini Dar-Es-Salaam.

Askofu Ndorobo alisema kuwa wanawake hawana budi kuachana na mawazo ya kudhani kuwa jamii inapozungumzia suala la maendeleo ya wanawake, linalenga ususi na ufinyanzi na masuala ya uzazi pekee, bali pia wajue kuwa yapo mambo mengine mengi muhimu.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo yanayoweza kuchochea kasi ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla kuwa ni pamoja na shughuli za kilimo na utunzaji bora wa chakula, utunzaji wa mazingira, uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwamo ya afya na kuhimiza uzalishaji na utumiaji wa nishati mbalimbali kama zinazotokana na kinyesi cha wanyama (Bio Gas energy)

"Wanawake ni lazima mhoji pale mtoto wa familia fulani anapoumwa lakini wazazi wake wakakosa kumpeleka hospitali, kabla hata hajafikishwa huko, anafia njiani. Hivyo nyie kama kiungo muhimu katika familia, lazima mhoji mpaka mjue kwanini wasimpeleke huko mapema hadi wasubiri azidiwe" alisema Askofu Ndorobo.

Mkutano huo wa wiki moja unaojadili teknolojia ya kisasa uliandaliwa na Kitengo cha Maendeleo ya Akinamama(WID), kilicho chini ya Shirika la Caritas na kuhudhumiwa na waratibu wake majimboni na wajumbe wengine walitoka katika nchi za Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Ujerumani (Misereore)

Kanisa lazidi kulia na mila potofu

Na Patrick Mabula, Kahama.

Kanisa Katoliki limelaani tabia chafu iliyokithiri ndani ya jamii kutobadili tabia ya uasherati na mila potofu za kurithi wajane,ubakaji ikiwa pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya na ulevi wa kupindukia ambayo huwaondolea ustadi wa kufanya maamuzi ya hekima na busara na kusababisha kuenea kwa ukimwi.

Akizindua Programu ya Kitengo cha Kudhibiti Ukimwi Jimbo la Kahama hivi karibuni, Makamu wa Askofu, Padre Aderade Shija, alisema takwimu zinazopatikana mara kwa mara zinaonesha kuwa ukimwi bado upo na kiwango cha maambukizo kinazidi kuongezeka siku hata siku badala ya kupungua.

Alisema jamii ya Watanzania haina budi kuelewa kuwa inapaswa kujiuliza na kushirikiana katika kukemea tabia zinazochangia kuenea kwa athari za ugonjwa huo na mengine ya zinaa.

Makamu wa Askofu huyo amesema Wakatoliki hawana budi kuushikilia na kuulinda muongozo na msimamo wa Kanisa na kujua kuwa njia bora pekee iliyobaki ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo na isiyo na gharama ni kuachana na kukemea vitendo vya uasherati na kupiga vita vyanzo vyake vyote.

Alisisitiza kuwa moja ya misingi bora ya kujihami na hivyo kutokufikwa na janga hilo la ukimwi ni kuwa na mke mmoja na kwa mke, kuwa na mme mmoja na kwamba watu hao wawe waaminifu katika ndoa yao.

Akitoa taarifa ya Programu ya Kitengo hicho katika uzinduzi huo, Mratibu wa shirika la misaada la Kanisa Katoliki la (CARITAS), Bw. Fulgence Kubezya, amesema kitengo hicho ambacho kitashirikiana na jamii kupata idadi kamili ya pamoja ya wale wanoishi na virus vya ukimwi kwa lengo la kuwasaidia.

Alisema Programu hiyo itashughulikia zaidi maeneo ya vijijini ambayo yamekuwa hayafikiwi na kwamba huduma hiyo itatolewa kwa watu wote bila kubagua madhehebu, kabila wala jinsia zao na kufanya kazi hiyo katika wilaya mbili za Bukombe na Kahama ambazo ziko ndani ya Jimbo hilo.

Aidha amesema baadhi ya shughuli zitakazofanywa zitalenga kusaidia jamii kuhusu kubadili tabia kuelimisha jamii kutunza wagonjwa wa ukimwi, kuwapa moyo waishi kwa amani, kujikubali na kutibiwa hospitali badala ya kwenda wa waganga wa kienyeji na pia kuwasaidia kupata wanasheria pindi kunapotokea migogoro ya mirathi. Amesema pamoja na kushirikisha umma katika mapambano hayo, Kanisa litashirikiana na serikali kupitia halmashauri za wilaya zote pamoja na taasisi na mashirika mbalimbali ya umma yasiyo ya kiserikali.

Kitengo cha kudhibiti Ukimwi katika jimbo kinafadhiliwa na shirika la Miserior la Ujerumani lililo chini ya Baraza la Maaskofu na uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, mapadre na watawa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, wabunge wote wa Kahama, Bukombe na Msalala.

Watawa watakiwa kushika nadhiri ya utii

Na Dalphina Rubyema

MENEJA Mstaafu wa Shamba la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC/OLDEANI FARM), mkoani Arusha , Bro. Severin Matandula, amewahimiza watawa na watumishi wote wa Kanisa kuiheshimu nadhiri ya utii katika maisha ili kufanikiwa katika kuifanya kazi ya Mungu.

Bro. Matandula alitoa ushauri huo wakati akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga baada ya kulitumikia shamba hilo tangu mwaka 1987 hadi Aprili27, mwaka huu iliyofanyika jijini katikati ya juma.

Hivi sasa anahitajika na shirika lake la Watawa Watumishi wa Moyo Safi wa Bikira Maria jimboni Iringa kwa ajili ya majukumu mengine ya kikanisa.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa TEC ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Msaidizi wake Mhashamu Methodius Kilaini, mapadre, masista na wafanyakazi wa idara mbalimbali za TEC, iliandaliwa na TEC kwa heshima ya utumishi wake wenye utii , uadilifu na uwajibikaji.

Bro. Matandula aliyehimiza umuhimu wa watumishi wa Kanisa kuzingatia nadhiri hiyo ya utii ya "Nenda, Fanya," alisema haina budi kuzingatiwa ili kuleta ufanisi katika kazi ya Mungu kwa kadri ya maelekezo ya viongozi wa kanisa.

"Hadi sasa niko tayari kufanyakazi yoyote na mahali popote nitakapotumwa na Kanisa na hali hii ninaifurahia sana kwa kuwa, utii ni bora zaidi kuliko sadaka," alisema.

Kardinali Pengo katika hafla hiyo, aliwataka Wakatoliki wote kuiga mfano wa Bro. Matandula kwa kuzitumia nafasi za kimaisha na kiutendaji kwa uaminifu na uadilifu wakiziona sawa na kazi zao binafsi kwa kuwa wote ni wamoja katika Kristo.

Alimhimiza Bro. Matandula kuzingatia ukweli kwamba Kanisa bado linahitaji mchango wake katika kumtumikia Mungu.

Naye Katibu Mtendaji wa Idara ya Fedha wa TEC, Bw. N. Kally, alimuelezea Bro. Matandula kama mchapa kazi hodari na akamtaka azidishe juhudi na ushirikiano katika kutumikia Kanisa.

Shamba la Oldeani, lililopo wilayani Karatu, lina ukubwa wa ekari 970 na lina miti 280 ya kahawa pamoja na mazao mengine kama mahindi, shayiri, ngano na linajishughulisha na ufugaji wa ng’ombe.

Linapata maji toka katika mto MamaHawu ambao husambaza pia maji yake katika shamba la Kiran na hospitali ya tarafa ya Oldeani .

Hivi sasa lipo chini ya usimamizi wa Meneja Bro. Nikolaus Myenzi, akisaidiwa na mabradha, Ponsian Mbwelwa na Jeremia Kigulawaote wa (SCIM).