BAADA YA KUSALI KATIKA PAROKIA YA MAKUBURI:-

Maaskofu wa Brazil waacha Wimbo wa Kireno

lWataka utafsiriwe, wasema Waafrika wengi watakwenda mbinguni

lWakatoliki wajawa na shauku, wataka wajue una maana gani

Na Agnes Bisake

LICHA ya kukiri kuwa muziki wa Kiafrika utapokelewa na kuweza kuwafikisha wengi mbinguni, Maaskofu wakuu Wakatoliki wa Brazili wameacha Wimbo wa Kireno katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Makuburi na wakataka na utafsiriwe na kuimbwa makanisani.

Maaskofu Wakuu hao wanne Antonio Marchetti, Liccio Ignacio Baumgaertuer, Meacyn Jose Viit na Serbio Arthur Braschi, walisema hayo walipoungana na Wakristo wenzao wa Parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, kusali Ibada ya Dominika iliyopita na kuusifia muziki wa Afrika ambao walisema ni wenye maadili mema ya Kimungu, unaotoa mafundisho yanayowawezesha watu kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

Waliwashukuru waamini wa parokia hiyo na kusema kuwa, ingawa mbinguni watu wengi wataingia, lakini kama kuna muziki wa kwenda mbinguni, basi ni muziki wa Afrika tu, utakaopokelewa na kuwapeleka wengi mbinguni.

Maaskofu hao waliambatana na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Brazil, Padre Carlos Alberto Chiquim pamoja na mwenyeji wao, Padre Daniel Giacomelli, ambaye ni mwalimu wa Seminari ya Morogoro ambaye aliyesaidia kutafsiri.

Walisema lengo lao kuja kusali katika baadhi ya makanisa ya Afrika likiwamo hilo la Makuburi jijini Dar-Es-Salaam, ni kutimiza Neno la Mungu lisemalo, "Nendeni duniani kote..."

"Mungu hana ubaguzi wa rangi, na sisi sote ni ndugu na tunaweza kuhubiriana Neno lake bila wasiwasi wowote," alisema mmoja wao .

Walisema wamechagua parokia ya Makuburi baada ya kusikia kuwa ina waamini wengi wanaoimba na kuendesha ibada kwa furaha na Utamadunisho.

Katika Misa ya Pili waliyoishiriki, waamini walichangamka sana wakiongozwa na kwaya ya Sayuni, na watoto walicheza vizuri na kwa utaratibu mzuri ibada nzima.

Waamini wengi waliimba kwa sauti na kucheza hali iliyowafanya wageni hao viongozi wa Kanisa kujikuta wanacheza na kupiga makofi. Wakati wa kupeleka vipaji, waamini wa Jumuiya Tabata Kisiwani walitoa zawadi nyingi akiwamo mbuzi aliyepambwa vizuri aliyesababisha waamini kushangilia na kupiga vigelegele huku wakiimba wimbo wa kikwao ambao waliukabidhi kwa Paroko wa Parokia hiyo ili utafsiriwe katika lugha ya Kiswahili na kutumika katika makanisa mbalimbali hapa nchini.Hadi sasa Wakatoliki wengi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, wana shauku kubwa kujua ujumbe ulipo ndani ya wimbio huo.

Walikiri kuwa ingawa walikuwa wakisimuliwa habari za makanisa mbalimbali barani Afrika na hasa Tanzania bila kuamini, sasa wameojionea wenyewe yalivyowaka upendo wa Kimungu na, waahidi kwenda kuwa mashahidi na kuwasimulia watu wa Brazil jinsi Mungu anavyoshangiliwa na Waafrika.

Askofu Mkuu KKKT 'aponda' kufutiwa madeni

lAsema bado wananchi wanateseka

Na Steven Mchongi, Mwanza

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Samson Mushemba anasema msamaha wa madeni kwa Tanzania ni kiini macho na wala hausaidii uchumi maendeleo ya huduma muhimu za wananchi.

Askofu Mushemba aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Wanawake wa kanisa hilo jijini hapa.

Alisema msamaha wa madeni uliotolewa na mataifa ya nje kwa Tanzania ni porojo na maneno matupu kwa kuwa hautatui matatizo ya nchi na wananchi wa kawaida.

Alisema inashangaza kuona serikali inazungumzia tu msamaha wa madeni lakini, haiyaoni matatizo ya kiuchumi na matokeo yake wananchi wanazidi kuwa masikini kwa kuwa hawapati huduma muhimu kama elimu na afya badala yake, gharama inazidi kuongezeka katika huduma hizo.

Akitoa mfano, alisema kutokana na hali ya uchumi kuwa mbovu, wakulima wa kahawa na pamba wameanza kukata tamaa kulima mazao hayo kwa kuwa wanalipwa bei kidogo na hivyo kushindwa kumudu kuendesha kilimo chao.

Alisema katika hali hiyo ya uchumi mbovu wanawake ndio wanaoathirika zaidi katika jamii ya Watanzania na kwamba yote hayo yametokana na sera mbaya zisizothamini wananchi wa hali ya chini.

Mkutano huo wa wanawake wa Kilutheri ulishirikisha wajumbe 150 kutoka dayosisi za kanisa hilo la KKKT zipatazo 20 hapa nchini.

Yaliyozungumzwa katika mkutano huo ni msamaha wa madeni na uhuru kwa maskini ambayo, mada zilizotolewa na Mchungaji Fidolin Mwombeki.

Mada nyingine iliyojadiliwa katika mkutano huo ni kuhusu jinsia na maendeleo iliyotolewa na Bi. Veronica Swai, kutoka Dayosisi ya Kaskazini.

Bi. Alice Kabagamila kutoka dayosisi ya Kaskazini Magharibi Bukoba, ambaye ni Mwanamke wa kwanza Mlutheri mteolojia hapa nchini, alitoa mada ya Somo la Biblia.

Ujumbe wa mwaka huu wa mkutano huo ulihudhuriwa na watu wa jinsia na rika tofauti, uliofanyika katika kituo cha mafunzo na mikutano cha KKKT katika ofisi Kuu ya Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Nyakato ni, "fumbua uwapatie Maskini na Wahitaji haki zao." (Mithali 31:9)

Mara kwa Mara Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Benjamin Mkapa, imekuwa ikijisifia kwa juhudi zake zilizoiwezesha Tanzania kufutiwa baadhi ya madeni na mataifa makubwa.

Askofu wa TAG azikwa kwa mbwembwe za harusi

lAliusia hivyo kabla ya mauti

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MAZISHI ya Askofu Jason Lugwisha (71) wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Jimbo la Kanda ya Ziwa, yamefanyika kwa mtindo wa sherehe na kuwashangaza wengi kuwa marehemu aliagiza atakapofariki azikwe kwa shamrashamra za sherehe na shangwe.

Katika mazishi hayo yaliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa hilo, Kirumba jijini hapa, na kuhudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo viongozi wa kanisa na Serikali Julai 6, mwaka huu, mjane wa marehemu, watoto na ndugu wa karibu, walivaa nguo zenye mapambo zikiwemo shela na kuomboleza kwa mbwembwe na shangwe bila kulia.

Mjane wa marehemu Bi. Hellen Lugwisha alisema kabla ya kifo chake, marehemu aliagiza mazishi yake yafurahiwe kwa kuwa ni sherehe au harusi yake ya mwisho hapa duniani.

Katika mazishi hayo, serikali iliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Steven Mashishanga ambaye kwa niaba ya serikali, alitoa rambirambi ya shilingi laki 2.5.

Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG nchini Renwell Mwenisongole na Makamu wake Mchungaji Regat Swai, Askofu wa TAG Jimbo la Magharibi, William Lusito na Mkuu wa Mission Tanzania, Scot Hanson.

Askofu Lugwisha alifariki Julai 2, mwaka huu kutokana na maradhi ya tumbo.

Katika uhai wake, alilitumikia kanisa la TAG kwa miaka 20, na amekuwa Askofu kwa miaka 16.

Hapo kabla, marehemu Lugwisha alianza kazi ya uchungaji katika kanisa la African Inaland Church Tanzania (AICT), mwaka 1970 hadi 1979 alipojiengua kutoka ushirika wa kanisa hilo baada ya kutokea tofauti baina yake na wenzake.

Alijiunga na kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) mwaka 1980 ambapo mwaka huo alifungua tawi la kanisa hilo eneo la Kirumba Mwanza na akawa Askofu wa kwanza wa Kanisa hilo.

Marehemu Askofu Lugwisha ameacha mjane mmoja watoto saba na wajukuu wanne.

Udini, ukabila katika uchaguzi ni hatari, Pengo aonya

Na Dalphina Rubyema, Kigoma

WAKATI Taifa linaelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu, waamini wa Kanisa Katoliki nchini wameshauriwa kutotumia vigezo vya udini wala ukabila kuwachagua viongozi na badala yake, wapime uwezo wa wagombea kuwachuja na hatimaye, kuwatupilia mbali wasiofaa.

Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wakati wa maadhimisho ya ibada ya Siku ya Jubilei ya Dhahabu ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma na Jubilei ya Fedha kwa Askofu wa jimbo hilo, Mhashamu Paul Ruzoka na mapadre wa jimbo hilo,akina Paul Kibanda na Matheo Ntamaboko.

Katika ibada hiyo iliyofanyika juma lililopita katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mshuhudiwa, Kardinali Pengo alisema kupiga kura kuwachagua viongozi wa ngazi muhimu za urais, ubunge na udiwani kwa kutumia vigezo vya dini na ukabila, ni hatari kwa jamii kwa kuwa hali hiyo inatoa mwanya kwa jamiii kuwapata viongozi wasio na sifa na wasiojali maadili ya uongozi na hivyo kulipeleka taifa mahali pabaya.

Wito wa Kardinali Pengo umekuja wakati muafaka ambapo baadhi ya wananchi bado hawajatambua umuhimu wa kuepuka kuwachagua viongozi wabovu wenye muelekeo wa kuongoza nchi kwa misingi mibovu ya ubaguzi wa rangi, dini, kabila, nafasi ya mtu kiuchumi na itikadi za kisiasa.

Baadhi ya vyama vya siasa na viongozi wa kisiasa, wamekuwa wakilaumiwa kwa kuonesha dalili za waziwazi za kuimarisha udini na ukabila huku vyama vingine vikidaiwa kutangaza hadharani sera zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Wakati huo huo; Askofu Paul Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Kigoma, ametoa wito kwa serikali, taasisi za kidini na mashirika mbalimbali ya kibinafsi(NGOs), kulisaidia jimbo lake na mkoa wa Kigoma kwa kuupelekea misaada mbalimbali ya wahudumu mbalimbali wakiwamo wa kiroho kufuatia ongezeko la wakimbizi toka nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

katika sherehe hizo muhimu za Jubilei Askofu Ruzoka alisema hadi sasa jimbo lake lina wakimbizi 103503 toka Kongo wakati wengine 233,103 wanatoka Burundi.

"Wakimbizi ni wengi mno tunaomba mtusaidie kwa kuwatuma wahudumu wa kiroho na wengine ili waje kutusaidia," alisema Askofu Ruzoka.

Sheikh TLP asema Watanzania ni wepesi kughiribiwa, kuiga mkumbo

lAziponda sera za jino kwa jino, mtu kwa mtu

lAsema CCM, CUF walitumia Quran kuzipata

Peter Dominic na Elizabeth Steven

WATANZANIA wengi wameelezewa kama watuwenye jazba, ushabiki, wepesi wa kughiribiwa na wanaofuata mkumbo kabla ya kuchunguza na kujua lengo la kinachotaka kufanyika na hivyo, waepukane na tabia hiyo ili wawachague viongozi bora wakatakaowafaa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Hayo yalisemwa na Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais kwa tikiti ya chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Sheikh Ally Idd Ally, alipokuwa akihutubia halaiki ya watu waliokusanyika katika viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar-Es -Salaam, mwanzoni mwa juma lililopita ili kusikiliza wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki Oktoba 14, mwaka jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari, siku hiyo Mwenyekiti wa TLP, ngazi ya taifa, ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho Bw. Augostine Mrema, angesoma wosia uliodaiwa kuwa aliachiwa na Marehemu Nyerere na kwamba sasa ulikuwa ni wakati wake muafaka kutangazwa kwa umma.

Hata hivyo, badala yake umati huo uliambulia porojo za kisiasa na kisha kusomewa nakala mbalimbali za magezeti ya siku za nyuma yaliyoelezea udhaifu wa serikali ya CCM.

Katika Mkutano huo, Sheikh alisema Watanzania hawana budi kujenga tabia ya kutaka kujua asili, maana na hatima ya jambo kabla ya kukubaliana nalo.

Alisema wakati taifa linaelekea Uchaguzi mkuu Oktoba 29, mwaka huu, wananchi hawana budi kuepuka jazba, ushabiki usio na msingi na tabia ya kufuata mkumbo na badala yake, wawe makini kumchagua kiongozi bora atakayewafaa.

"Nimewastadi Watanzania, wengi ni watu wanaopenda kufuata jazba, ushabiki na mkumbo tu;...hata ukipita na ngoma unaimba, watakufuata tu, hata kama hawajui wimbo huo una maana gani," alisema.

Akitoa mfano wa Waislamu kuelezea Watanzania walivyo wepesi wa kughiribiwa na kufuata mkumbo, Sheikh alisema, "Nimeingia katika misikiti na kama mnavyosikia, mimi ni Sheikh Ally Idd Ally, tena ni Sheikh wa kusoma, si yule wa kupigiwa kura kama diwani.

Nimeingia misikitini kwa miaka mingi, waislamu wanakaa misikitini, anakuja mtu na madevu yake hadi hapa, anatoka Pakstani, Iran au Iraq; wananyanyua mikono juu, anasema maneno ambayo ni ya Kiarabu msiyoyajua, lakini kazi ya Watanzania ni AMEN ! AMEN," alisema na kuufanya umati mzima kucheka.

Akaongeza, "Hawajui kama wanaombewa ama wanalaaniwa ama wanaapishwa, hawajui wanaombewa nini wao ni mkumbo tu, wanafuata mkumbo . Hili usifuate mkumbo. Lazima ufanye kazi hii kwa uangalifu...Tupime wagombea na tupime uwezo wao"

Akizungumzia sera za jino kwa jino na mtu kwa mtu, Sheikh Ally , alisema katika Quran, jino kwa jino maana yake ni ukiingia, unapelekwa pengo kwa pengo na ile ya mtu kwa mtu, maanayake ni kuuana.

"Mimi ni Shekh, niliposikia sera ya jino kwa jino, na mtu kwa mtu na ngumi kwa ngumi, nilitafuta kwenye Quran Sura ya 5, aya ya 45 sura inayoitwa Maidah(Suratul Maidah 5:45), nikakuta ngumi kwa ngumi, mtu kwa mtu na jino kwa jino...nikaona CCm na CUF wamekitumia kitabu kimoja, sura moja, aya moja isipokuwa CUF, walichukua neno la kwanza na CC Mwakachukua la pili, nilijiuliza mbona wanafanana kwa sera?"

Alionya kuwa sera hizo zinaweza kuwahatarisha Watanzania kwa kuwapeleka katika mapigano ambayo hawayahitaji,"... Sera hizo zinatupeleka tunakotaka? Hivi Watanzania shida yetu ni ugomvi? Au matatizo yetu ni kupigana?" alihoji

Katika mkutano huo, Mrema alisema anashangaa Serikali ya Rais Mkapa inamnyanyasa kana kwamba amemrogea (Mkapa)mtoto wake ingawa wamefanya naye kazi kwa muda mrefu wakiwa katika nyadhifa mbalimbali zilizozidiana baila manyanyaso kama aliyodai anayapata sasa.

"Nilikuwa bosi wake sikumwadhibu namshangaa ananiwekea mapolisi ananifuatafuata kwa kunisingizia kesi za uongo sijui kwanini ananifanyia hivi," alisema.

Askofu Kilaini 'achuma matunda' ya Kanisa

lAsema kumwambia mtu ukweli ni kumsaidia

Na Mwandishi Wetu

KWA mara ya kwanza, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ametoa Daraja ya Upadre kwa mashemasi wawili, mmoja akiwa wa jimbo na mwingine wa shirika la Makapuchini.

Akizungumza katika Ibada ya Upadrisho katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini hivi karibuni, Askofu Method Kilaini alisema,

"Shambani kwa Bwana kuna mavuno mengi lakini vitendea kazi ni vichache mno. Leo hii tunawapa upadre lakini wakumbuke kwamba hamshindani na ulimwengu, hamna uwezo kisiasa, na siyo matajiri, bali ni kujitoa mhanga ili kutumikia taifa la Mungu," alisema.

Waliopewa Upadrisho siku hiyo ya Julai 14, mwaka huu na Mhashamu Kilaini ni waliokuwa mashemasi, Andrew Huwanda wa Jimbo na Charles Raymod wa shirika la Makapuchini anayetokea parokia ya Upanga katika Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Alisema mapadre ni chumvi ya dunia na kwamba endapo watapoteza chumvi hiyo, ni vigumu itakuwa vigumu kuwarudisha na chumvi yao na hali hiyo, kumrudisha iwapo siyo chumvi, ni balaa zaidi na akawataka kujaribu kuishi kitakatifu.

Kwa sababu siyo wote wanaomwita Bwana watakaoingia katika ufamle wa mbinguni, aliwataka kuwa mfano mzuri kwa waamini wakishirikiana kwa pamoja na jamii nzima ya Kanisa.

Ibada hiyo ilihudhiriwa pia na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, mapadre kutoka parokia mbalimbali, watawa, mabruda, mabradha pamoja na waamini mbalimbali jimboni.

Askofu Kilaini amewataka waamini wote kushirikiana kwa karibu na mapadre hao na endapo atatoka nje ya matakwa, asaidiwe na wala siyo kumsemasema, "Unachotakiwa ni kumsaidia; mfuate umwelekeze siyo kumsemasema tu; huu siyo Ukristo, mjue kuwa padre ni binadamu kama nyie", alisema Mhashamu Kilaini.

Asiyeweza kuumba uhai, akome kuuchezea- Mwinyi

Na Leocardia Moswery

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, Al-haji Ali Hassan Mwinyi, amesema ingawa ulimwengu mzima unashuhudia maendeleo ya sayansi na teknolojia, bado hakuna aliyefanikiwa kujua siri na hatimaye kuumba uhai hivyo ni dhambi na makosa makubwa kuungamiza kwa njia yoyote.

Mwinyi aliyasema hayo mwishoni mwa juma wakati akifunga semina ya kimataifa juu ya madhara ya kuzuia na kutoa mimba kwa njia za kisayansi na athari za ugonjwa wa ukimwi katika jamii katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya mtakatifu Anthony, Mbagala jijini Dar-Es-Salaam..

Semina hiyo ya siku sita iliandaliwa na shirika la kutetea Uhai la Pro-Life (TANZANIA) na kudhaniwa na Shirika la Kimataifa la HUMAN LIFE INTERNATINAL la Marekani.

"Maisha ni zawadi toka kwa Mungu. Pamoja na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, hatujawa tayari kujenga uhai na hauuzwi wala hauzibiki," alisema.

Alisema maendeleo hayo ya Sayansi na Teknolojia yaliyopelekea matumizi ya kompyuta na television, yamechangia pia jamii wakiwamo wazee, kukosa maadili hali inayochangia pia utoaji wa mimba na matumizi ya madawa katika kuzuia mimba hali ambayo ni kinyume na utamaduni wa maisha.

Mwinyi alisema ili jamii iepuke idadi isiyokusudiwa ya wanafamilia, haina budi kupanga uzazi kwa kutumia njia za asili ambazo hazipingani na madili ya Kanisa na jamii katika kuepuka uzinzi na mauaji ya namna hiyo.

"Familia zisizoweza kutunza watoto wengi zipange uzazi lakini sio kwa kutumia abosheni au njia zisizofaa," alisema Mwinyi na kutoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea taifa kuepukana na maambukizo ya ugonjwa wa ukimwi.

Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Kulinda Maisha, Imani na Familia la "Human Life International," iliyowahusisha washiriki kutoka Tanzania, Kenya , Uganda na Zimbabwe. Padre Matthew Habiger, OSB, alisema kila mwanadamu ana wajibu wa kulinda na kutetea uhai tangu kutungwa kwa mimba hadi kifo kitokanacho na mapenzi ya Mungu.

Katika Hafla hiyo, Mwenyekiti wa Pro-Life (TANZANIA), Bw. Emil Hagamu, alisema jamii kwa kushirikiana na vyombo vya habari,haina budi kukemea njia zote za utoaji mimba na matumizi ya kondomu kama kinga ya ukimwi kwa kuwa zinachangia kwa kiasi kikubwa maambizo.

Padre Julian Kangalawe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzani (TEC), alisema

Iwapo juhudi za makusudi zitafanyika kuwaelimisha vijana juu ya kuepuka vitendo vya ndoa kabla na nje ya ndoa, upo uwezekano mkubwa wa kushinda katika vita dhidi ya utoji mimba na ugonjwa wa ukimwi.

Wengine waliozungumza na kuunga mkono juhudi hizo ni padre Boniface M. Waema wa Seminari ya Tindinyo nchini Kenya na mkurugenzi wa Kituo cha Vijana cha Don Bosco jijini dar-Es-Salaam, Padre Joe Prabu.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la dar-Es-salaam, mhashamu Method kilaini na Mkurugenzi wa Elimu ya Dini wa baraza Kuu la Misikiti Tanzania (BAKWATA), Sheikh Hassan Chizenga ambaye awali katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala, aliilaani tabia ya baadhi ya watu kutegemea kondomu kama nia ya uhakika ya kuepuka mimba na magonjwa ya zinaa na wengine kushiriki tendo la ndoa kwa lengo la kujifurahisha kabla na nje ya ndoa.

Naye Jenifer Aloyce wa DSJ, anaripoti kuwa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu, Salma Kauli amewataka viongozi Kiislamu kutoa mafundisho ya kidini kwa watu ambao wanatarajia kufunga ndoa.

Alisema ndoa nyingi za Kiislamu huvunjika kutokana na kutokuwa na makubaliano kati ya maharusi watarajiwa.

"Unajua ndoa nyingi za Kiislamu huvunjika kwa sababu mafundisho yake yamejificha na wala sio ya wazi kama wanavyofanya Wakristu kwa sababu wao maharusi watarajiwa hupata mafundisho pamoja" alisema Bi. Kauli.

Mjumbe mmoja kutoka Zimbambwe, Harith Kachasu alisema kuwa mpango wa Taifa wa kuzuia kutoa mimba, umeanza kuwafundisha vijana madhara ya utoaji mimba.

Semina hiyo iliyowajumuisha viongozi wa dini za Kiislamu, Kikristo ililenga kuwapa mwongozo viongozi wa dini juu ya kazi wanazofanya katika juhudi za kuzuia utoaji mimba.

...'Youth Alive' nusura wamlize Mwinyi ukumbini

lFuraha yamtoweka ghafla

Na Josephs Sabinus

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Al-Haji Ali Hassan Mwinyi, mwishoni mwa juma alijawa na simanzi la ghafla baada ya kusikiliza tumbuizo la nyimbo toka kwa kikundi cha Youth Alive, cha Jijini Dar-Es-Salaam.

Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Rais huyo mstaafu, kumaliza hotuba yake ya kufunga semina ya kimataifa ya siku tano juu ya utoaji mimba na ukimwi.

Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Pro-Life(TANZANIA) na kufanyika Alhamisi jioni katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Anthony ya Mbagala jijini, ambapo tangu kuingia kwake, Mwinyi alikuwa ametawaliwa na tabasamu usoni na kicheko mdomoni hata baada ya hotuba yake.

Ghafla, Mwinyi alibadili uso na kuwa wenye huzuni na simanzi, baada ya vijana wa Youth Alive kuanza kutumbuiza katika hafla hiyo kwa nyimbo mbalimbali zinazokemea utoaji mimba na madhara yake, pamoja na athari za ugonjwa wa ukimwi katika jamii na hatima ya Tanzania ya kesho.

Miongoni mwa nyimbo zilizomtia simanzi Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi, ni "Stop Abortion" unaosema, "Unaua kiumbe asiye na hatia...Kama wazazi wote wangefanya abosheni, sisi tungekuwa hapa?"

Mwingine ni ule walioimba huku wameshika tama kwa simanzi wakisema, "Nalilia kizazi changu, nalilia taifa langu. Taifa la kesho litakuwaje kama tunaua watoto na wengine yatima wanaongezeka? Taifa la kesho, vijana wa kesho, ni nani atakuwa mrithi kama vijana tunakwisha kwa utoaji mimba na ukimwi?"

Burudani hiyo pia ilishuhudiwa na viongozi wa dini akiwamo Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la Dar-Es-salaam, Mhashamu Method Kilaini, Sheikh Hassan Chizenga na katibu wa Idara ya Liturgia wa TEC,Padre Julian Kangalawe

Mkapa kushuhudia saini za CUF, CHADEMA

Na Neema Dawson

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kutiliana saini makubaliano ya muungano wa vyama vya CUF na CHADEMA zitakazofanyika jijini Dar-Es-salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Bob Makani, shughuli hiyo ya kutiliana saini kwa vyama hivyo itafanyika Agosti 2, katika Viwanja vya Mnazi-Mmoja.

Makani aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini juu ya maandalizi ya chama chake kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Bob Makani alisema vyama hivyo vimeamua kuungana ili kuimarisha nguvu ya upinzani na hivyo kujinyakulia urais na viti vingi vya madiwani na wabunge.

Alipoulizwa sababu ya uamuzi wao wa kumualika Mkpa kuwa mgeni rasmi katika shrehe za kutiliana saini wakati ni Mwenyekiti wa Chama tawala ambacho ni mpinzani wao mkubwa, maknai alisema,

"Ili kuhakikisha muungano huo haubomolewi wala kuyumba, tumeamua tumualike Rais Mkapa ili ashuhudie makubaliano na hii tumemualika kama Rais na sio kwamba tunaalika CCM. Isitoshe, unajua Mkapa ni mtu mstaarabu sana.

Tutawaalika hata mabalozi na viongozi wa vyama mbalimbali vya upinzani na wananchi wote watakaohitaji kuhudhuria sherehe hizo, tunawakaribisha. " alisema Bob Makani.

Alisema shuguli za kutia saini katika kitabu maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya muungano, zitafanywa na wenyeviti, makatibu na mdhamini mmoja mmoja kutoka vyama hivyo vya siasa vya upinzani.

"Tumekuwa tukimwalika Rais Mkapa katika mikutano mingi kwani ule wa Juni 1998 tulimualika katika Mkutano Mkuu wa CHADEMA uliofanyika katika Hotel ya Starlight, lakini kwa kuwa alikuwa na kazi nyingi za kitaifa, hakuweza kuhudhuria.

Hata hivyo, mkapa ni mstaarabu, alituma barua na mwakilishi katika Mkutano huo hivyo, tunajua atahudhuria bila kukosa kwani hata tatizo na chama chochote, ni la Rais wa nchi nzima," alisema.

Bob Makani alisema baada ya shuguli hiyo, sherehe hizo za Muungano Agosti 3 atakwenda Shinyanga kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea ubunge Jimbo la Shinyanga mjini kwa tiketi ya CHADEMA.

Alisema chama cha CHADEMA kinatarajia kuanza kutoa fomu za udiwani na Ubunge Julai 22, mwaka huu na kuzirudisha Agosti 8 mwaka huu.

Ukata kuzuia SMT kushiriki uchaguzi

Na Waandishi Wetu

WAKATI vyama vingine vya siasa vimejaa vuguvugu la Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani, chama kipya cha siasa cha Sauti ya Mshikamano Tanzania(SMT), huenda kisishiriki kwa kuwa hakijapata usajili wa kudumu na pia kinakabiliwa na ukata.

Msemaji wa chama hicho kilichopata usajili wa muda Desemba 1, 1999, Bw. Paulus Mwanja, aliliambia gazeti hili jijini Dar-Es-Salaam, wiki iliyopita kuwa SMT hakitamsimamisha mgombea urais kwa kuwa bado hakijapata usajili wa kudumu na akaongeza kuwa endapo juhudi zao zitafanikiwa mapema, chama kitaangalia uwezekano wa kufanya hivyo.

Alisema hivi sasa chama chake kinashugulikia juhudi za kupata wananchama 250 kila mkoa katika mikoa 10, badala ya wananchama 200 wanaohitajika na Msajili wa Vyama kwa mujibu wa sheria ili kujihakikishia idadi inayotakiwa kabla ya msajili kufanya uhakika katika mikoa hiyo.Alisema hivi sasa tayari wamekishaifikia mikoa minne ambayo ni Dodoma, Mbeya, Dar-Es-Salaam na Tanga na kwamba wakishapata usajili wa kudumu, watafanya uchaguzi wa kupata viongozi wa kidemokrasia ndani ya chama kabla ya kujibwaga katika kinyang’anyiro hicho.

Chama kinatarajia kutembelea mikoa ya Singida, Mwanza, Mtwara, Lindi, Rukwa na Pemba ambako kuna wawakilishi wake ili kupata wanachama hao tayari kwa uhakiki.

"Ili tukamilishe mipango yetu, tunahitaji kiasi cha shilingi laki moja ingawa tayari kiasi fulani kimekwisha patikana"Alisema chama chake hakina mpango wa kuungana na chama chochote lakini endapo mwanachama wa chama kingine atataka kujiunga bila kuwa na tamaa ya uongozi, watampokea.

"Sisi tunajiamini na wala hatuna haja ya kumbembeleza mtu ajiunge nasi. Lakini, akija bila tamaa ya cheo, tunamchukua kama mwanachama." Alisema.Chama cha Sauti ya Mshikamo Tanzania ambacho wanachama wake wanajiita ni walalahoi wa mitaaani, kina lengo la kuwaunganisha Watanzania bila ubaguzi na kumwezesha mwananchi kupata mahitaji na huduma muhimu za kijamii kama chakula, mavazi , malazi, elimu, na afya.Pia kina lengo la kuhahkikisha kuwa demokrasia ya kweli inakuwapo na haki za msingi za binadamu kwa Watanzania hazikiukwi na zinaheshimiwa.

Nyingine ni kuhakikisha unakuwapo utawala wa bora wa kisheria, kudumisha mshikamano wa kitaifa, amani na utulivu.

Kupinga wananchi kuonewa na kutafuta mbinu za kuwapa akina mama na wanajamii mikopo ili waitumie kuzalisha mali na hivyo, kuboresha hali zao za maisha ikiwa ni pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi, wakulima wote nchini.

Wanaharakati wataka wanaogombea uongozi wasiachishwe kazi

Na Pelagia Gasper

MTANDAO wa Wanaharakati Watetezi wa Haki za Wanawake umetaka wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wapewe likizo na kurejea katika ajira zao wanaposhindwa kupata uongozi.

Madai hayo yamo katika ilani ya wapiga kura kwa Uchaguzi wa Mwaka 2000 iliyoandaliwa na mashirika 28 yaliyopo katika mtandao huo wa Wanaharakati watetezi wa jinsia Tanzania.

Wanaharakati hao wanasema kuwa, kuwapa wagombea likizo kutatoa mwanya kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi bila kuhofia kupoteza kazi zao.

Kwa mujibu wa utaratibu wa sasa, kiongozi mwenye wadhifa mkubwa serikalini anapaswa kujiuzulu wadhifa wake kabla ya kugombea kiti katika uchaguzi.

Ilani hiyo iliyozinduliwa mwezi huu pia inataka serikali iruhusu wagombea binafsi.

Inasema fursa hiyo itawapa wanawake mwanya wa kugombea uongozi bila kufungamana na chama chochote cha siasa.

"Serikali haina budi kuweka taratibu za kisheria zitakazowezesha kuwepo wagombea binafsi ili kuwapa fursa wanawake kugombea uongozi bila kulazimika kujiunga na chama chochote" inasema sehemu ya ilani hiyo.

Ilani hiyo imelenga kukumbusha wapiga kura kuwa kura yao ina thamani na kwamba waitumie kudai na kutetea haki zao za msingi.

Wanawake ni asilimia 51 ya raia wote Tanzania.

Utafiti unaonesha kuwa, wanawake ndio wanaopiga kura kwa wingi na kwamba wakimpiga mtu, hawezi kuchaguliwa na hata hivyo, ni wachache wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Ilani hiyo kwa upande mmoja imeulaumu uongozi uliopo madarakani kwa kudai kwamba haujafanya juhudi zozote za kuubomoa mfumo dume unasaidia kushusha thamani ya mwanamke.

"Hakuna mipango mahususi ya kitaifa ya kuhamasisha masuala ya haki za binadamu kwa raia wa nchi hii ili waweze kukuza na kulinda haki zao," ilani hiyo ilisema.

Haki zinazozungumzwa hapa ni pamoja na uhuru na utu wa kila mwananchi bila kubagua jinsia, dini, kabila, tabaka, nasaba au umri wake.

Kwa upande mwingine, ilani hiyo inavitaka vyama vya siasa viweke taratibu za utendaji na kisera zitakazohakikisha kwamba wanawake wanashiriki katika uongozi kwa uwiano wa idadi ya wanachama wao.

Vyama pia vimehimizwa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata fursa sawa ya kuteuliwa kugombea katika chaguzi na kufanyiwa shime wakati wa kampeni.

Pia, wanataka kuwepo na shinikizo la kuondolewa kwa taratibu na vikwazo vinavyokwamisha wanawake katika ushindani .

Ilani imevitetea viti maalum vya wanawake na kudai kwamba vinasaidia kuuenzi uwezo wa wanawake hasa wakati huu ambapo hawajapata fursa na nyezo sawa na wanaume.

Hata hivyo ilani imeshauri mwakilishi wa viti maalum asipewe nafasi ya kuwakilisha wanawake kwa zaidi ya vipindi viwili mfululizo.

Ili kupunguza adha ya unyanyasaji wa wanawake katika siasa, ilani inataka kiundwe chombo huria kitakachofuatilia na kufikisha mbele ya sheria vitendo vyovyote vya ubaguzi dhidi ya wanawake ndani ya vyama na vyombo vya dola.

TANESCO Shinyanga wanolewa dhidi ya ukimwi

Na Charles Hillila, Shinyanga

KUFUATIA watumishi wengi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi, wafanyakazi 14 kutoka idara mbalimbali za TANESCO Mkoani Shinyanga wamepatiwa semina juu ya kujikinga na maambukizo ya magonjwa ya zinaa hasa ukimwi.

Ugonjwa wa Ukimwi umeonekana ni tatizo kubwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo kutokana na wafanyakazi wengi kufa na wengine kuathirika kwa ugonjwa huo.

Akisoma taarifa ya kumkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina ya siku tano iliyoanza julai 10, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Shinyanga Motel, Meneja wa TANESCO Mkoani hapa, Bw. Mahende Magaya, alitaja kuwa shirika hilo limepoteza wafanyakazi 511 kati ya wagonjwa 664 waliofariki nchini kote toka mwaka 1990 hadi Februari mwaka huu.

Aliwaambia washiriki wa semina kuyazingatia na kuwa walimu na mifano bora kwa watumishi wengine kwa kubadili tabia ili wajinusuru na kuongeza ufanisi katika shirika.

Alisema TANESCO Makao Makuu baada ya kuona ukimwi ni tatizo kwa watumishi wake, liliamua kutenga fedha kwa ajili ya kuelimisha watumishi wake nchini namna ya kujikinga na ugonjwa huo na mengine ya zinaa.

Shirika limetenga shilingi milioni 100 ambazo zimesambazwa mikoani kote kwa ajili ya kutoa elimu ya Ukimwi kwa watumishi.

Akijibu risala hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Mohamed Babu, aliyewakilishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Dk. Ernest Haraka, alilipongeza shirika kwa kutenga fedha hizo ili kupambana na ukimwi.

Alisema hiyo ni changamoto kwa mashirika na taasisi nyingine kufanya hivyo kwa ajili ya afya za watumishi, familia na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa wagonjwa wa ukimwi kwa mwaka 1998 hadi 1999 walikuwa 4973 ambapo kwa mwaka 1999 pekee kulikuwa na wagonjwa 462.

Takwimu hizo zinaonesha pia ongezeko la magonjwa ya zinaa. kwa mwaka 1998 ilikuwa ni watu 3477 waliripotiwa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya mkoani humo.

Katika hali inayoonesha watu kutojali kinga dhidi ya ugonjwa huo mwaka 1999 peke,e kulikuwa na ambukizo la magonjwa hayo kwa watu 21,463 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 51.73 la magonjwa ya zinaa katika mkoa wa Shinyanga.