MKUTANO WA INJILI NA UPONYAJI DAR:

Wakatoliki waambiwa amkeni kumekucha

lWalokole, Wamoravian, GRC washangilia; wasema neema imelishukia Kanisa

lAnglikana, KKKT wasema anayetaka kwenda Ukatoliki, aende mradi asitukane

Na Josephs Sabinus

WAKATI Mhubiri Padre John Baptist Bashobora kutoka Uganda, amewaambia Wakatoliki, "Amkeni kumekucha", Makanisa mbalimbali yakiwemo ya kilokole yamevutiwa na mahubiri ya Kikatoliki yaliyofanyika jijini Dar-Es-Salaam na pia Askofu kufafanua maana ya mkutano huo wa wanauamsho.

Kufuatia maelfu ya wakazi wa jiji wakiwamo Waislamu na Waprotestanti kumiminika katika mkutano huo uliosifiwa na makanisa, kwa madai kuwa uliandaliwa "kisomi", Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Eneza T. Abraham, amesema, kwa kuwa muamini ana uhuru, anayetaka kuingia Ukatoliki endapo amevutiwa, ruksa mradi tu, asitukane wala kukashifu alikotoka.

Pia, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini, amesema mkutano huo wa hivi karibuni ulizua maswali mengi,

"Uamusho ni nini? Ni wa Kikatoliki au ni wa Walokole au Kiprotestanti tu:" Askofu Kilaini amesema, Uamsho sio kwa ajili ya vikundi hivyo tu, bali ni kitu kilichokubaliwa na Kanisa tangu muda mrefu uliopita."Uamsho wa Kikatoliki ulianzishwa mwaka 1967 huko Dusquene USA.

Mwaka 1975, Papa Paulo VI alialika Mkutano Mkuu wa Roma, Papa Yohana Paulo II 1992. Novemba 27, 1995 (ambapo wanauamsho) walikubaliwa na kusimikwa rasmi na Kanisa Katoliki ili karama hizo zisaidie Kanisa zima."

Akinukuu maneno ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alipoongelea suala la wawakilishi wa Uamsho , Askofu Kilaini alisema, "Ni kundi linalotoa ushuhuda wa mapaji ya Roho Mtakatifu likileta mwamko mpya wa kuthamini Biblia, mwelekeo mpya wa sala na kutamani utakatifu ili kufundisha juu ya upendo wa Mungu aliye na huruma na aliyetuletea furaha, hao, wameleta furaha kwa wengi."

Akijibu swali endapo kutoka Jangwani maana yake ni kuokoka, Askofu alisema, Iwe hapo Jangwani au sehemu yoyote ya maisha yako, ukisikia umeguswa na Yesu Mwokozi na ukaamua kumfuata kwa nguvu zako zote, basi uko katika njia nzuri za wokovu. Mk 13:33-37 Kesheni. Kwa kuchukua uamuzi na kuuimarisha."

Alisema kuwa, kwa bahati mbaya, uamsho umejulikana kwa wengi kuwa ni kuponya na kupiga kelele na akasema kuponya ni moja ya karama za Roho.

Alisema sio lazima kwa waamini kuwa katika Uamsho ila, ni muhimu kujiunga na vyama mbalimbali vya kitume.

WAKATI HUO HUO: Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jijini, viongozi kadhaa wa makanisa walisema uamuzi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, kufanya mkutano huo wa wazi wa Injili na uponyaji, ni wa busara na wa kishujaa unaoonesha namna Kanisa linavyozidi kufunuliwa neema za Mungu.

"Pengo kubwa lililokuwapo, linazidi kupungua miongoni mwa Wakristo na hii ni ishara kuwa ipo siku huenda Wakristo wakaandaa mkutano wa madhehebu yote kwa pamoja," alisema Katibu Mkuu wa KKKT.Mwenyekiti wa kitaifa wa kanisa la "The Gospel Revival Centre (GRC), Mchungaji George Kilango, alisema, "Wakatoliki wamefanya jambo zuri kwa kuwa sasa wameamua kumtangaza Mungu kwa uwazi zaidi na watu wote hata wa madhehebu mengine wanakwenda. Mimi kama alivyo Mungu, siangalii dhehebu maana wote ni ndugu zangu katika Kristo... wanahitaji sasa semina za mara kwa mara ili waimarike zaidi katika imani."Naye Kasisi Kiongozi (Vicar General) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar-Es-Salaam, Mchungaji Frank Kajembe, licha ya kuwapongeza Wakatoliki, alisema, "Wakuu wa makanisa wawaruhusu tu waamini wao bila kinyongo waende kushiriki ibada hizo. Nafurahi maana hii inaonesha kuwa Mungu hana dhehebu na nashukuru hata Waroma, wameanza kuhubiri na kuponya."

"Tatizo kwa baadhi ya watu wa madhehehebu, wanahubiri madhehebu mengine badala ya kuhubiri Biblia. Njoo kwangu, njoo kwangu; mhubiri anayehubiri dhehebu, huyo ana lengo la faida yake binafsi"

Mchungaji Salatieli Mwakamyanda wa Kanisa la Moravian Tanzania, ushirika wa Kekomachungwa, Jimbo la Kusini, Wilaya ya Mashariki, alikuwa na haya, "Wakatoliki wamefanya tendo la ushujaa; wametimiza unabii. Makanisa mengine yawape ushirikiano kwa kuwa mtu hatawasha taa na kuiweka uvunguni."

Mchungaji wa kanisa la "Fire General Gospel International Church, yeye alitoa tahadhari, "Sasa, wasitokee wengine kati yao wakataka kujiona ndio wa maana kuliko wengine, au wakataka kuvuruga taratibu za Kanisa, hao ni hatari katika makanisa."

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Wanauamsho Wakatoliki wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, watu wenye shida mbalimbali waliombewa na kuponywa huku wengine wakitolewa mapepo.

Katika siku ya mwisho ya mkutano huo iliyokuwa ya Uponyaji wa Yesu katika Ekaristi, Padre Bashobora aliwaoya Wakristo kutokufanya kosa la kumkaribisha shetani katika maisha yao japo ni kwa muda mfupi, Alisema baadhi ya wanajamii wamepotoka kwa kuwa wanawatumia waganga wa kienyeji kutaka kuondoa matatizo yao, lakini badala yake, hali zao huzidi kuwa mbaya.

"Unataka upone, utajiri, eti unakwenda kwa waganga wa kienyeji, lazima ujue hiyo siyo roho safi; ni roho mchanganyiko.

Katika mkutano huo Padre Bashobora aliwaambia Wakatoliki waamuke kwa kuwa sasa wakati umefika, Mkutano uliohubiriwa pia na Askofu Method Kilaini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Padre Monsignore Mbiku wa Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na Padre B. Michupu kutoka Nairobi na semina kadhaa ziliendeshwa.

Semina yamuweka 'kiti moto' Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi

Na Dalphina Rubyema, Morogoro

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame alijikuta katika wakati mgumu pale viongozi wa vyama vya upinzani nchini waliohudhuria warsha juu ya Uchaguzi Mkuu ujao, walipomjia juu ambapo baadhi yao wamedai Tume yake ipo kwa maslahi ya CCM na inawanyanyasa wapinzani.

Sakata hilo lilitokea katikati ya wiki katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Oasis iliyopo mjini hapa katika ya siku mbili juu ya umuhimu, kanuni na wajibu wa vyombo habari wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao wa madiwani, rais na wabunge.

Warsha hiyo iliyowashirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, waandishi wa habari, Tume ya Taifa Uchaguzi na viongozi mbalimbali wa Baraza la Habari nchini (MCT), akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Baraza hilo, Jaji Joseph Warioba, ilimpa nafasi kila mshiriki kutoa dukuduku lake.

Nafasi ya kwanza ilikuwa ya Jaji Makame kutoa mada juu ya umuhimu wa vyombo vya habari vya umma wakati wa uchaguzi.

Katika mada yake, Jaji Makame, alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi, vyombo vya habari havina budi kuuelimisha umma juu ya suala zima la uchaguzi ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo wa upigaji kura.

Alisema, vyombo vya habari ni lazima visimame kidete katika kuandika habari za vyama vyote bila kuvionea aibu wala kuvipendelea, wala kuvionea baadhi ya vyama na wagombea wake ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi na kuhoji

Kisha kilifika kipindi cha maswali na kuchangia mada.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha United Demratic Party(UDP),Profesa Lwanyantika Masha, alikuwa wa kwanza kupata nafasi.

Profesa Masha alianza kwa kusema "Jaji Makame nafurahi umekuja mbele yangu! Naomba niombe radhi kwa maneno nitakayosema mbele yako".

Aliongeza, "Kwanza kabisa napenda uelewe kuwa wewe pamoja na kamati yako nyote ni watu wa CCM. Nasema hivyo kwasababu pamoja na kwamba mnateuliwa na serikali, ndiyo, sikatai; lakini, hiyo serikali ni ya CCM yenyewe!

Isitoshe hata vitendo vyenu vimekaa kaa ki-CCM CCM. Achia mbali hilo, nina imani kuwa wewe na kamati yako mmeishajua kuwa hivi sasa baadhi ya vyama vimeishaanza kampeini japokuwa mmetwambia kuwa tarehe rasmi ni 19/8/2000,sasa mbona bado mmenyamaza kimya?" alihoji.

Kisha alifuatia Afisa Elimu wa Mafuzo wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Mazemule Shija, aliyesema, "Jaji Makame; Tume yako inatunyima nyaraka, nyaraka zote muhimu za uchaguzi hatuzipati. Tukifika kwenu tunaambiwa wahusika hawapo, kwanini mnazikalia? Kwanini msizitoe mapema ili kama tunadaiwa tulipe madeni yetu kabla ya uchaguzi? "

Akaongeza, "Makame, simamia haki msiwe ngangari, unatunyanyasa sana Makame!"

Kabla Jaji hajajiweka, "akarushiwa rungu" lingine kutoka kwa Bw. Charles Haule wa NLD.

Yeye akavifananisha vyama vya siasa kama maziwa na tui la nazi ambapo alisema ukiangali kwa haraka vitu hivi viwili huwezi kuvitofautisha kwa macho hadi uvionje.Alisema maziwa ukiyaacha yagande, utakunywa mtindi, ukiyachemsha utakunywa freshi lakini hali ni tofauti kwa tui la nazi ambalo ukiliacha muda mrefu litaharibika na ukilichemsha bila kulikoroga vizuri litaharibika vilevile.

Alisema hivyo hivyo,serikali inapotoa ruzuku kwa baadhi ya vyama na vingine kuvinyima haina budi kuelewa kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima wengine haki na nguvu huku wengine wakiendela kwa kasi kubwa.

"Pamoja na kuvisisitiza vyombo vya habari kuwa na haki na usawa katika uchaguzi ujao, hivi hauoni kuwa nyie ndiyo wanyanyasaji wakuu kwa kuvinyima ruzuku baadhi ya vyama," alihoji.

Akijibu, Jaji Makame alikanusha vikali na kusema Tume yake haina U-CCM kabisa na yeye siyo mwanachama wa chama hicho.

Kuhusu kuanza kwa kampeini, alisema Tume inaelewa kuwa Agosti 19,mwaka huu ndiyo siku rasmi ya kuanza kampeini na mwisho ni Oktoba 28, 2000.

Kuhusu madai kuwa CCM imewaweka vijana katika makambi ili kuwafundisha namna ya kuvuruga uchaguzi, jaji Makame, alisema anachoelewa ni kwamba wanapewa elimu ya kusimamia uchaguzi kwa haki na amani na siyo kwa ajili ya kufanya vurugu."Mimi najua ‘security power’ katika mambo ya kampeini atakuwepo rasmi kuanzia tarehe 19/8 mwaka huu, hivyo siwezi kuwa na uhakika kama kweli baadhi ya vyama vimeisha anza kampeini na suala la ruzuku, hili nadhani Msajili wa Vyama anaweza kulijibu vizuri"alisema.

Askofu awataka Wakurya kuacha mila za ‘nyumba ntobhu’

Na Pd. Alfred Rweyemamu, Musoma

PAMOJA na mila nyingine mbovu, Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Mhashamu Justin T. Samba, ameitaka jamii ya Wakurya kuepuka mila potofu ya wanawake kuwaoa wanawake wenzao kwa kuwa hali hiyo inadhalilisha na kuhatarisha afya za wahusika.

Katika ndoa hizo zinazojulikana kama "nyumba ntobhu" au "nyumba mbhoke", ambazo ni za kawaida kwa jamii ya wenyeji hao wa mkoa wa Mara, mwanamke ambaye hakuzaa au hana mtoto wa kiume, anaruhusiwa kumuoa mwanamke mwenzake na huyo huwa na mamlaka juu yake na pengine huweza hata kumchagulia mme.

Askofu Samba alitoa wito huo katika ziara yake ya kichungaji aliyoifanya katika parokia Katoliki ya Kiagata(wilayani Musoma-Vijijini) jimboni humo ambapo alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakatoliki 44, wa vigango vya Ryamesanga, Kitaramanka, Kongoto na Kyankoma.

Mambo mengine ambayo Mhashamu Samba aliyakemea na kutaka yaepukwe ndani ya jamii hiyo alipokuwa katika ziara yake ya kichungaji, ni pamoja na fitina, hasira, wivu na uadui ambao hupelekea wenyeji wa mkoa huo kuwa na sifa mbaya ya "kugechana" yaani kupigana kwa kukatana mapanga.

"Kuchukua Msalaba na Yesu, ni kuachana na mambo yote ya giza na ya kishetani kama uzinzi, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, wivu, hasira, fitina na hii mifarakano inayoleta kugechana ovyo. Yote hayo yasisike vinywani mwenu na kumuondoe tofauti zote mlizo nazo," alisema.

Aliwataka wazazi wa maeneo hayo kushirikiana katika malezi ili watoto wa familia zao, waishi katika maisha yenye maadili mema ya Kikristo.

"Wakristo wa Ryamisanga, kama kweli mnawapenda wenzenu na watoto wenu, mtawakabidhi mila nzuri ndiyo maana hata katika Maagano ya Ndoa, mnaulizwa kama mko tayari kuwapokea kwa mapendo watoto mtakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake," alisema.

Licha ya kuwasifia Wakatoliki wa parokia za Ryamisanga na Kitaramanka kwa kupata vigango vipya, Askofu Samba aliwataka waamini kuweka utaratibu na akashauri kila familia kutengeneza benchi kwa ajili ya matumizi ya kanisa na ikibidi, kuandika jina.

Aliwahimiza Wakristo kutumia nguvu zao kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga shule na zahanati na kuondokana na dhana ya kutegemea misaada ya wafadhili.

"Kanisa, tujenge familia zetu na kujiletea maendeleo kwa jasho letu. Tuondokane na kukemea kabisa tabia ya kuwa tegemezi na ombaomba," alisema katika parokia ya Ryamisanga.

Askofu aliwataka waliopata Sakramenti ya Kipaimara, kuwa mfano bora wa kuwavuta na kuwaleta watu wengine katika utumishi wa Bwana Yesu kwa maneno na matendo bora na pia, wadumu katika maombi yao.

Akiwa katika kigango cha Kyankoma, alitoa zawadi ya Biblia kwa kila jumuiya na kuwahimiza waamini kujitahidi kupata nyingine na kuzisoma kwa makini ili kuzielewa.

KINYANG’ANYIRO CHA UCHAGUZI MKUU UJAO:

Hata nife kama Yesu, sirudi CCM ng'o - Mrema

lAimba na kucheza, ‘Mtu mzima hovyo’ jukwaani

lAmlilia Nyerere eti alimkingia kifua, amwita Mkapa Shemeji

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha TLP, Bw. Augustine Mrema amesema yuko tayari kufa kama Yesu, msalabani kuliko kuthubutu kurudi CCM kama wapinzani wengine wanavyofanya.

Katika mkutano wa hadhara alioufanya mwanzoni mwa juma eneo la Kekomachungwa katika manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, licha ya kumkumbuka kwa majonzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa alikuwa akimkingia kifua serikali ya CCM ilipotaka kumnyanyasa, aliuchekesha umma baada ya kusaidiana na wafuasi wake kuimba na kunengua akiwa jukwaani wimbo wa taarabu usemao ‘...mtu mzima hovyo’ ulioimbwa na kikundi cha Muungano Cultural Troupe ambao ulikuwa unaimbwa na wapiga matarumbeta na wananchi.

Nyimbo nyingine zilizomshawishi Mrema kunengua jukwaani hata wakati wa matembezi yake katika eneo hilo ni "wape wape vidonge vyao, wakitema wakimeza shauri yao" na ule ulioimbwa na bendi ya Bantu Group unaosema "Hayo maneno yao wameyataka wenyewe sasa mwaiona ngondo mwafunga milango" ambazo nazo ziliimbwa na wapiga matarumbeta.

Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho cha Upinzani cha TLP, alisema Serikali ya CCM imekuwa ikimnyanyasa na kumwekea mizengwe ya makusudi ili asigombee nafasi ya Urais katika Uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka huu lakini, kwa mapenzi ya Mungu amefanikiwa kufanya hivyo.

‘Niko tayari kufa kama Yesu Msalabani lakini nisirudi CCM. Siwezi kula matapishi yangu... kwa kuwa CCM ina yake na Mungu ana yake juu ya Mrema, leo niko jukwaani ninagombea urais," alisema Mrema.

Aliongeza kuwa licha ya wapinzani kufanya kazi katika mazingira magumu, yeye binafsi hawawezi kuacha kazi takatifu ya kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kimaisha kwa ujumla.

"Siwezi kuacha kazi takatifu ingawa wapinzani tunafanya kazi katika mazingira magumu".Aliuchekesha umma aliposema hakuwahi kumtukana wala kumkashifu Rais Mkapa kwa kuwa ni shemeji yake."Mara nyingine wananikamata eti nimemtukana Mkapa; nimtukane Mkapa amenikosea nini shemeji yangu. Kwani amemfukuza dada yangu! Angekuwa amemfukuza dada yangu, ndipo labda ningechukia nimtukane. Sasa kwa nini nifanye hivyo; nimtukane wa nini.," alisema.

Bw. Mrema ni Mchagga mzaliwa wa Mkoani Kilimanjaro, kama alivyo mke wa Rais Mkapa, Mama Anna Mkapa.

Hivi karibuni kumekuwa na mlipuko mkubwa wa wapinzani kurejea CCM na kudai kuwa vyama vya upinzani havina muelekeo.

Miongoni mwa wapinzani vigogo waliorejea katika chama hicho tawala ni pamoja na Bw. Masumbuko Lamwai aliyekuwa NCCR_MAGEUZI, Bw. John Guninita, aliyekuwa CHADEMA, DK. Lutter Nelson naye wa CHADEMA.

Wengine ni Bw. Makongoro Nyerere (NCCR)aliyedai amerejea katika CCM kama njia ya kumuenzi baba yake, Marehemu Julius Nyerere na Bw. Msabah (CUF).

Albino ajitokeza kuomba msaada kulelewa watoto

lAsema aliwahi kupata ugonjwa wa akili

Na Peter Dominic

ALBINO mmoja mkazi wa Vijibweni jijini Dar-Es-Salaam, Bw. Musa Kidole (42), amejitokeza hadharani kuomba asaidiwe kuitunza familia yake yenye mke na watoto wanne kwa madai kuwa, imemshinda.

Bw. Kidole alifika katika Ofisi za gazeti hili katikati ya juma akisema amekuwa akihangaika kwa muda mrefu kutumia juhudi zake kuitunza familia hiyo kwa kuipa mahitaji muhimu lakini, ameshindwa kwa kuwa hana kazi, biashara wala eneo la kulima.Alisema ameona ni vyema atumie vyombo vya habari ili kuutangazia umma hali hiyo inayoisibu familia yake kwa kukosa mahitaji muhimu ya kibinadamu yakiwamo malazi, chakula na malazi ili wenye mapenzi mema, wamsadie na familia yake badala ya yeye kukaa kimya huku hali inamshinda na familia ikizidi kuteseka.

"Kuliko kukimbia na kuwaacha watoto wangu bila baba, ni heri niombe jamii inisaidie kwa kuwa ingekuwa siku za nyuma, ningeweza hata kwenda kuomba omba kwa watu barabarani lakini, Makamba alishakataa; nikienda nitakamatwa," alisema.

Akiyataja baadhi ya matatizo yanayokuwa kikwazo kwake, Bw. Kidole alisema kuwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba na kwamba hivi sasa yeye anaishi kwa mtoto wa binamu yake .

Liingine ni wa kuwasomesha watoto wake katika elimu ya msingi kwa kuwa umri wao umeanza kutishia uwezekano wao kupata elimu katika karne hii ya sayansi na teknolojia."Sina nyumba wala kazi ingawa nina mke na watoto wanne, anayenihifadhi ni mtoto wa binamu yangu. Watoto wangu wanahitaji elimu, na wala sina uwezo wa kuwasomesha.

anawataja watoto wake kuwa ni Raheli (10), Olivia(7), Mariam(4) na John(1).

Anasema hakupata urithi wowote kwa kuwa marehemu baba yake alikuwa na wake wengine mbali na mama yake huku akiwa na idadi kubwa ya watoto 16.

Alisema matatizo yamemuandama baada ya kuugua ugonjwa wa akili wakati akiwa mfanyakazi katika zahanati hiyo ya Kijiji cha Makuja, Mkoani Dodoma kabla hajahamia Dar-Es-Salaam miaka ya 80."Tulichaguliwa wawili katika kijiji chetu kwa kazi ya kutoa huduma ya kwanza, nikaendelea vizuri na kazi ila baadaye, kichwa kilianza kuniuma sana hadi nikalazwa Hospitali," anasema na kuongeza,

"Niliporejea kazini, badala ya kutoa dozi ya "Panadol" kwa mgonjwa, nikawa ninachanganyikiwa na kumpa klorokwini au vidonge vingine badala ya dawa niliyotakiwa kumpa mgonjwa. Kumbe tayari nilishaanza kuchanganyikiwa akili. Wakanishauri niache kazi," alisema. Maalbino ni walemavu wa ngozi na macho. Huathirika sana wanapotembea juani bila kofia ama mwamvuli na huathirika zaidi wanapokosa sabuni na mafuta ya kutosha kulainisha ngozi kwa kuwa hulazimika kuoga mara nne ya mtu wa kawaida.

Watoto huwa hawaoni vizuri na hivyo kutofanya vizuri kimasomo na kwea maana hiyo wana maisha magumu kwa kuwa wengi wao hawana kazi kwa kuwa hawakusoma ipasavyo.

Wazichangia seminari magunia 37 ya chakula

Na Steven Mchongi, Mwanza

Wakatoliki katika Jimbo la Mwanza wamechanga magunia 37 ya chakula kwa shule za Seminari za Nyegezi, Makoko na Sengerema.

Chakula hicho kitakachotumiwa na wanafunzi wanaosoma katika seminari hizo, kimetolewa na Wakristo wanaoishi katika kata za Ilemela, Kabageye, Nyamilolelwa na Lumale mjini hapa.

Taarifa iliyotolewa na Kanisa Katoliki hapa Mwanza ilisema kuwa waumini wa Ilemela wamejitolea majunia 10 ya mahindi, Kabageye magunia 10 Lumale magunia 7 na Nyamilolelwa magunia 10.

Taarifa hiyo ilisema kuwa kila muamini wa Kanisa Katoliki katika majimbo ya Mwanza, Geita na Musoma, ametakiwa kuchanga chakula kupitia kwa uongozi wa parokia zao.

Hatua hiyo imekuja kufuatia gharama kubwa za uendeshaji wa seminari hizo ambapo kwa sasa Kanisa pekee halimudu mzigo wa kugharamia kila kitu kwa wanafunzi wake.

Wakati huo huo: Kanisa Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Ilemela limo mbioni kujenga chuo cha Maarifa kwa ajili ya kuwaendeleza watoto wanaomaliza elimu ya msingi.

Padre Richard Makungu, wa Parokia hiyo ameliambia KIONGOZI kuwa, tayari uongozi wa parokia yake umewasilisha ombi la kupatiwa kiwanja kwa Idara ya mipango mji ya Manispaa ya Mwanza.

Alisema kuwa mara watakapopatiwa kiwanja ujenzi wa Chuo hicho utafanywa kutokana na michango ya waumini wenyewe, Kanisa na wafadhili mbalimbali.

Jiandikisheni kupiga kura, Askofu awambia wananchi

Na Charles Hililla, Shinyanga

WAKAZI wa mkoa wa Shinyanga wamepewa wito kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura katika chaguzi mbalimbali zinazolikabili taifa hivi sasa

Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu wa Pili katika mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa, Oktoba 29, mwaka huu ili kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais.

Wito huo ulitolewa na Askofu Aloyisius Balina, wa Jimbo Katoliki la Shinyanga hivi karibuni wakati wa ibada ya kusherekea Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa parokia ya Gula, zilizofanyika parokiani hapo.

Askofu Balina alisema kutojiandikisha kupiga kura ni dhambi kwa kuwa ni kutotimiza wajibu na huko ni kuvunja Amri ya Kanisa.

"Lazima kila mtu mwenye umri unaotakiwa kupiga kura, kujiandikisha na kisha kumpigia kura mtu yule unayeona anafaa kuwa kiongozi wako. Kinyume na hivyo, ni kupata viongozi ambao hawana sifa za kuwa viongozi kwa sababu yule anayefaa hakumpigia kura na huyo asiyefaa hakupingwa. Sasa unapata kiongozi asiyefaa ingawa hakumchagua au hakupenda akuongoze," alisema Askofu.Katika shehere hiyo, vijana 240 walipewa Sakramenti ya Kipaimara na ndoa nne kufungwa.

Askofu aliwaambia waliopata sakramenti hizo kutovuruga jinsia na maumbile yao kwa kupuuza kuiga tabia, mila mbovu za asili na tamaduni za kigeni zisizofaa kwa kuwa zinahatarisha maadili ya utu na kanisa.

Alitoa mfano kuwa utoaji mimba na utumiaji wa madawa vinahatarisha na kuathiri afya za watumiaji katika kupanga uzazi wa mpango kwa kuwa ni kinyume kati ya Mungu na uumbaji.

Binadamu tumeumbwa kwa mfano wa Mungu na miili yetu ni hekalu lake hivyo ni lazima litunzwe na kuheshimiwa usichezewe kamwe.Sherehe hizo zilihudhuriwa na mapadre wa Jimbo la Shinyanga na wawakilishi wa waamini, pia alikuwepo na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu ambaye Dk. Pius Ng’andu.

Katika salamu zake, Waziri Ng’wandu aliwataka wazazi mkoani humo kuwapatia watoto wao urithi bora wa elimu ili baadaye ujinga uzikwe na hivyo kuupatia mkoa huo maendeleo.

Shinyanga(Wasukuma), inakabiliwa na tatizo la kutothamini elimu.

RWSAT yawataka Wamama Wakuu kuthamini Semina, warsha

Na. Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Umoja wa Mama Wakuu wa Mashirika Tanzania (RWSAT), Sista Inviolata Kambanga, amewahimiza wanachama wa umoja huo, kuzithamini warsha na semina mbalimbali zinazotolewa bila kubweteka kwa uzoefu uliopo miongoni mwao ili kuboresha zaidi utendaji wao katika kazi ya Mungu.

Sista Inviolata, alikuwa akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar-Es-Salaam katikati ya juma.Alisema kwa kuwa elimu haina mwisho, masista wa RWSAT, hawana budi kuzichangamkia semina na warsha ambazo RWSAT huziandaa lakini baadhi yao kutozihudhuria, aidha kutokana na shughuli nyingine, au wengine kudhani kwamba hakuna kipya watakachojifunza.

Sista Inviolata ambaye pia ni Mama Mkuu wa Shirika la Masista Wabenediktine Ndanda jimboni Mtwara, alisema semina kama hizo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambazo wanachama wanajadili matatizo mbalimbali yanayowakumba katika mashirika yao tofauti na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuyakabili na ppia kujifunza mbinu mpya za kuyaendesha.

Aliyataja baadhi ya mafanikio ya RWSAT kuwa ni pamoja na wanachama kuboresha ushirikiano baina ya mashirika yao, kuanzisha chombo cha kitaifa kwa ajili ya masista wanaowalea masista wapya katika mashirika na kusaidiana katika kutatua matatizo na kuongeza idadi ya Wakristo Wakatoliki katika baadhi ya maeneo nchini.

Sista Inviolata ambaye Shirika lake la Wabenediktine linajishughulisha na utoaji elimu mbalimbali kwa akina mama vijijini, huduma za hospitali na mafunzo ya ushonaji, pia lina lengo pia la kuinua maisha ya akina mama na hutoa elimu ya shule za chekechea na elimu ya dini.linaendesha shule za Social Center, iliyopo Mtwara, Domestic School, ya Mtua jimboni Lindi na Kilwa Kipatimu pia ya Lindi.

Mwenyekiti huyo ambaye ameshika nafasi hiyo ya uenyekiti baada ya uchaguzi uliofanywa mwezi uliopita ambapo Sista Maura Kimaryo, alistaafu baada ya muda wake kumalizika, alilitaja tatizo la usafiri kuwa si kwamba linalisumbua shirika lake pekee, bali mashirika yote.

Hivi sasa RWSAT ina mashirika wanachama 80, kati yao 60 yakiwa ni ya kijimbo na 20 ya kimataifa.Katibu wake ni Sista Fides Mahunja.

Sumaye ataka Watanzania kuwa kichocheo cha uchumi

Elizabeth Steven na Leocardia Moswery

WAZIRI Mkuu, Fredrick Sumaye, amesema uchumi wa nchi hautokani na serikali, bali wananchi wenyewe kwa kuwa ndio kichocheo cha maendeleo wakishirikiana na uongozi wa serikali yao.

Sumaye aliyasema hayo wakati akizungumza katika Hoteli ya Valley iliyopo ndani ya Viwanja vya Maonesho ya 24 ya Kimataifa ya Biashara katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar-Es-Salaam, alipotembelea maonesho hayo katikati ya juma.

Alisema watanzania hawana budi kuulewa ukweli kuwa uchumi wa nchi hautokani na serikali pekee bali kwa ushirikiano na wanachi katika juhudi za kuuboresha.

Aliwataka watanzania kuongeza juhudi katika kuzalisha bidhaa mbalimbali za mashambani na viwandani kwa wingi na kwa viwango sahihi vya ubora ili nao waweze kuuza bidhaa nje ya nchi kama nchi nyingine zinavyoleta bidhaa zao nchini Tanzania.

Alikipongeza kikundi cha akina mama cha FAWETA kwa kujishugulisha na bidhaa mbalimbalizikiwamo zile za asili ana akasema awali, walionekana kama ni wanafunzi lakini sasa, wamekuwa kama walimu.

Miongoni mwa mabanda aliyotembelea yalikuwa ni pamoja na N.G.P, RSA, TTCL, JKT, THA, NSSF, SNSA, VETA, KOREA, MZINGE,UNILEVER, WIPE na banda la FAWETA.

Profesa apata Uaskofu

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MCHUNGAJI Nungwana Daniel (51), ambaye pia ni Profesa katika Chuo cha Theolojia cha Nasa, wilayani Magu, amechaguliwa kuwa Askofu Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT)Dayosisi ya Mwanza.

Mchungaji Nungwana, alichaguliwa Juni 28 katika Mkutano Mkuu Maalum wa Sinodi Kuu ya Uchaguzi, uliofanyika katika Kanisa la AICT Makongoro mjini hapa ambapo wachungaji 125 walijitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 377 kutoka Dayosisi Kuu tano za kanisa hilo nchini ni Mwanza, Shinyanga, Geita, Pwani na Mara ambayo inaijumuisha ile ya Ukerewe.

Mkutano huo ulitarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 551 kutoka dayosisi hizo lakini, walihudhuria wajumbe 377 ambao kwa mijibu wa katiba ya AICT, walitosha kuendelea na shughuli ya uchaguzi.

Katika mchuano huo, Mchungaji Nungwana aliongoza kwa kupata kura nyingi za wajumbe katika awamu zote mbili za mwanzo za mchujo.

Katika awamu ya mwisho, Mchungaji Nungwana alipata kura 275 ambazo ni theluthi mbili zilizotakiwa na hivyo kumshinda Mchungaji Mpailehi Shadrack aliyepata kura 82.

Baada ya kuchaguliwa, Mchungaji Nungwana alisema ameshitushwa na matokeo ya uchaguzi lakini akaseama yote yamekuja kutokana na mapenzi ya Bwana.

Alisema anawaomba waamini wa Kanisa hilo wamuombee katika sala ili awe mtumishi mwema.

Aliwaomba wamwombee aweze kuelewana na viongozi wenzake, Wakristo na jamii kwa ujumla katika kuifanya kazi ya Bwana.

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT nchini Mchungaji John Nkele, wachungaji 95 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo walijitoa katika kinyang’anyiro ndani ya ukumbi wa mkutano na wengine 24 kutokufika kabisa.

Uchaguzi huo ulifanyika kufuatia kifo cha Askofu Samweli Masingili Magessa wa Dayosisi ya Mwanza, aliyefariki Januari 9 mwaka huu.

TPP hatujikombi kuungana na chama kingine- Che-Mponda

Na Dalphina Rubyema, Morogoro

CHAMA cha Tanzania Peoples Party (TPP) kimesema hakipo tayari kujikomba kwa kujiunga na vyama vingine vya upinzani ili kumsimamisha mgombea mmoja wa kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge kwa kuwa vingine vina sera za umwagaji damu.

Akizunguza na Kiongozi katikati ya wiki katika Hoteli ya Morogoro mkoani hapa, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dk. Aleck Humphrey Che- Mponda alisema kuwa chama chake hakiko tayari kujiunga na vyama vingine kwa kuwa baadhi vinajiona vya maana kuliko vingine na vingine vina sera tofauti zisizoashiria amani.

"Sisi bwana sera zetu ni za amani tu, sio jino kwa jino, shavu kwa shavu ama jicho kwa jicho hatuwezi kukubali kabisa kujiunga na chama ambacho sera zake zinaashiria umwagaji damu" alisema na kuongeza,

"Unajua sisi mwaka 1995 hatukufanikiwa kusimamisha mbunge yeyote bungeni hivyo hatukupata ruzuku sasa, hivyo vyama vilivyopata ruzuku vinajiona dume. Sisi hatuendi kujigonga kwao, na hatuko tayari kujiunga na chama chochote,"

Alisema hivi sasa chama chake kimejizatiti kunyakua viti vingi vya Ubunge na Udiwani katika maeneo kadhaa ya Bara na Visiwani na kitamsimamisha mgombea urais wake anayeweza kutoka kwa wanachama.

Che-Mponda alitamba kuwa hakina woga wa kushindwa na kinaamini kitapata ushindi mkubwa dhidi ya vingine kwa kuwa hadi sasa kinawasubiri wastaafu kutoka serikalini hususani kitengo cha Sheria akiwemo Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali ambao tayari wanaendelea na mazungumzo ili wajiunge na chama hicho.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema kuwa endapo vyama hivyo vya upinzani vitakubali kubadili sera, chama chake kitakubali kushirikiana nao kusimamisha mgombea mmoja wala hakitajali anayesimama kugombea kiti hicho cha Urais anatoka chama gani ili mradi tu, awe anasifa zinazokubalika kwa umma.

Askofu wa KKKT akabidhiwa laki 2.5 kwa ujenzi wa nyumba

Na Maneno Nguru

Askofu wa Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jerry Mngwamba, amepokea shilingi 250,000/= toka kikundi cha wamama wa kanisa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya uaskofu ya dayosisi hiyo.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar-Es-Salaam, Jumatano iliyopita, wamama hao walichukua nafasi ya kumsalimu na kumkaribisha Askofu Mngwamba ambaye amerejea hivi karibuni kutoka nchini Marekani anakosoma.

Wazo la kuwepo na nyumba ya uaskofu lilitolewa mwaka 1997 na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Rev. Mwatumai Mwanjota, lengo la pendekezo hilo la kuwa na nyumba ya uaskofu ya kudumu ni kumtunza Askofu wa Dayosisi hiyo ili aweze kuishi humo pamoja na Dayosisi hiyo kuwatunza maaskofu wa dayosisi nyingine kutoka ndani na nje ya Tanzania wanapokuwa hapa Dar-Es-Salaam kwa huduma mbalimbali.

Rev. Mwatumai Mwanjota amesema kwa wakati huu, dayosisi haina nyumba ya Uaskofu. Gharama ya ujenzi wa nyumba hiyo ilikadiriwa kuwa shilingi milioni 300. Mpaka sasa tayari sharika zilikuwa zimekusanya zaidi ya shilingi milioni 16

MAONESHO YA SABASABA

Gereza lakosa mazao

lBET kufanya Tamasha la Ununuzi

GEREZA la Mang’ola lililopo wilayani Mbulu mkoani Arusha, limekosa mazao ya kuonesha katika Maonesho ya 24 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar-Es-Salaam mwaka huu, kutokana na ukosefu wa mvua mkoani humo; anaripoti Leocardia Moswery.

Naibu Kamishna wa Magereza ambaye pia ni Mkuu wa Viwanda na Maonesho wa Magereza, A. Mursali, alisema wakati akimuelezea mkongwe wa siasa nchini, Mzee Rashid Kawawa, alipotembelea banda la Magereza katika Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba katikati ya juma kuwa, uzalishaji wa mazao ya kilimo katika gereza hilo umekuwa duni kutokana na ukame.

Naibu Kamishna huyo wa Magereza, alisema karibu Magereza zote nchini zinashiriki maonesho hayo ambapo huonesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wafungwa vikiwamo vitanda, nguo aina ya batiki, asali na samani mbalimbali.

Gereza la Mang’ola huzalisha mazao ya kilimo kama maharage, mahindi, mpunga pamoja na matunda.

Alisema wafungwa wengi wawapo gerezani, hupewa mafunzo ya ufundi mbalimbali na kisha kufanya mitihani ya VETA ili kupata cheti cha kitaifa ambacho huwasaidia hata baada ya kutumikia vifungo vyao.

Mursali alimshukuru Mzee Kawawa aliyeambatana na baadhi ya viongozi akiwamo Afisa Tawala wa Manispaa ya Temeke, Bi. Elizabeth Nyambibo huku mwenyeji wao akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Biashara ya Nje (BET), Bw. Emmanuel Buriki.

Naye Getrude Madembwe anaripoti kuwa:

BET inaandaa Tamasha la kwanza la Ununuzi wa Vifaa

(DAR SHOPPING FESTIVAL 2000), litakalofanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini kuanzia Novemba 24 mwaka huu hadi Januari 4, 2001.

Afisa Mkuu wa Habari wa BET, Bw. Edwin N. Rutageruka, ameliambia KIONGOZI kuwa, tamasha hilo linatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye.

"Ni tamasha la kwanza nchini na litafanyika kwenye viwanja hivi vya Sabasaba," alisema Bw. Rutagaruka.

Alisema lengo la tamasha hilo ambalo ni la kwanza nchini, ni kuwapa nafasi wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kushirikiana na wananchi katika masuala ya kibiashara na kwamba zaidi ya wageni laki 3, watahudhuria.

Alivitaja baadhi ya bidhaa zitakazouzwa hapo kuwa ni pamoja na vifaa vya umeme, urembo, mavazi, vifaa mbalimbali vya kuchongwa, vipuli vya magari na vitu vingine.

Mabradha wa SCIM wapata marubani

Na Peter Dominic

SHIRIKA la Mabradha Wa Moyo Usio na Doa wa Bikira Maria(SCIM)katika Jimbo Katoliki la Iringa, limepata viongozi watakaoliongoza kwa kipindi cha miaka sita ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Tarcisiuc Ngalalekumtwa wa jimbo hilo la Iringa, Bradha Raphael Mgohamwende, amechaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika wakati Bradha Thadei Mwasala, amekuwa makamu wa Mkuu wa shirika hilo la SCIM (Vice Superior General)

Taarifa imesema katika uchaguzi huo uliofanyika Julai 4,mwaka huu, ambao ni wa kwanza katika historia ya shirika hilo,Bradha Mwasala pia amekuwa Mjumbe wa Kwanza wa Halmashauri, akifuatiwa na mabradha Daniel Mwinuka, Barnabas Msagamasi na Expedito Ng’owo.

Katika taarifa yake iliyolifikia KIONGOZI, Askofu Ngalalekumtwa , amemshukuru Mungu kwa kuliwezesha shirika kuwa chini ya maongozi yake(Mungu) kwa amani hadi sasa.

Kabla ya Uchaguzi huo, Bradha Mgohamwende alikuwa akikaimu wadhifa huo kwa miaka 12 ingawa wakati huo, shirika lilikuwa chini ya uongozi wa jimbo na halikuwa na uwezo wa kutoa maamuzi yake pekee kama ilivyo sasa.

Shirika hilo lilianzishwa miaka 49 iliyopita huko Tosamaganga Iringa yalipo makao yake makuu.

Katika taarifa hiyo Askofu Ngalalekumtwa aliwataka wakristo kote nchini kuwakumbuka ma Bradha wa Shirika hilo katika sala na Sadaka ili waweze kudumu daima katika kuyatimiza yale anayoyataka Mungu.

"Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa Maongozi yake hii leo. Tufurahi pamoja na ndugu zetu Mabradha wa SCIM kwa hatua ya kihistoria waliyofikia. Tuendelee kuwakumbuka daima katika kuyatimiza yale anayoyataka Mungu mwenyewe".