Waziri Yona aitia Serikali majaribuni

Na Dalphina Rubyema

HATUA ya Waziri wa Fedha Bw. Daniel Yona ya kubatilisha Waraka wa Serikali Na.175 wa mwaka 1973 uliokuwa unatoa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini na za hiyari, aliyoichukua hivi karibuni licha ya kuzusha malalamiko kwa viongozi mbali mbali wa dini nchini, imebainika kuwa imeipa wakati mgumu Mamlaka ya Mapato nchini(TRA)kwa vile haieleweki kipi kitozwe kodi na kipi kisamehewe.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaoni kuwa hakuna Ofisa yeyote wa TRA ambaye anaweza kupambanua kinaganaga ni vitu gani hasa ambavyo taasisi za dini zinapaswa kutozwa kodi au kusamehewa kutokana na lugha inayojichanganya iliyoko katika agizo hilo la Waziri Yona.

Uchunguzi huo umebainisha kuwa kufuatia utata huo, Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA amelazimika kuandika barua Wizara ya Fedha ili kupata ufafanuzi juu ya vipengele kadhaa vyenye utata.Kilicho wazi katika agizo hilo ni kwamba vifaa vya ibada vinastahili msamaha wa kodi.

Kutokana na agizo la Waziri Yona, misamaha ya kodi kwa taasisi hizo inayolenga katika elimu,afya na huduma za jamii inastahili msamaha wa kodi, jambo ambalo linaifanya TRA ijikute haina chochote ambacho kinastahili kodi kwa vile mizigo karibu yote ya taasisi hizo inayoingia nchini inaangukia katika moja ya vipengele hivyo.

Hali hiyo imesababisha TRA kushindwa kupambanua bidhaa za kutoza kodi na hivyo kujikuta ikidai kodi hata kwa misaada inayotumwa na wafadhili kwa Kanisa kama vile magari, chakula, vifaa kwa ajili mawasiliano (redio), kompyuta na kadhalika ambavyo kwa kweli navyo huishia katika kutoa huduma kwa jamii.

Wakati huo huo mizigo mingi ya Kanisa Katoliki iliyofika nchini kutoka kwa wafadhili bado inaendelea kukwama Bandarini ikidaiwa kodi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Clearance wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Bro. Thadeus Mwasala, alisema kuwa tangu wapeleke barua za kutaka wachukue mizigo yao hakuna jibu lolote walilokwishapata toka kwa uongozi wa Mamlaka ya Mapato nchini.

"Barua zote tulizopeleka zilikataliwa tu kwa maneno bila maandishi yoyote ya kiofisi...tulipata tu majibu ya mdomo kwamba barua zetu zimekataliwa. Hata hao waliotupa majibu hayo ni wafanyakazi tu wa mamlaka hiyo lakini siyo Kamishna," alisema.

Mratibu huyo alisema kuwa walipofuatilia suala hilo kwa Kamishna Ushuru na Forodha wa TRA ambaye alipokea maelezo ya uhakikisho (documents) toka TEC, aliwaambia kuwa bado suala lao anaendelea kulifuatilia Wizarani.Alisema suala hili linaleta utata kwani taarifa iliyopelekwa kwa viongozi wa Taazisi za Kidini inasema kuwa mizigo ya taasisi hizo itakuwa inalipiwa kodi isipokuwa vifaa vya ibada, huduma ya afya, maji na elimu lakini sasa inashangaza kuona mizigo yao inakwama wakati bidhaa zilizomo ni zile zinazostahili kusamehewa kodi.

Mratibu huyo aliongeza kuwa pamoja na kupeleka nyaraka zote zilizoambatana na mizigo hiyo bado TRA inaendelea kuweka ngumu kuruhusu mizigo hiyo itolewe bandarini. "Kama taarifa ya Waziri Yona inasema kwamba vifaa vya ibada, elimu, afya na maji vitaendelea kusamehewa kulipa kodi, sasa mimi nashindwa kuelewa ugumu uko wapi, kwani sisi mizigo yetu iliyokwama inahusiana na mambo hayo. Alisema mfano mzuri ni kontena la shule ya Msolwa ambalo awali ilitaka ikabidhiwe vielelezo vyake na hati ya usajili wa shule hiyo lakini hata baada ya kukabidhiwa bado kinachofuata hakijawa wazi. Akitoa ufafanuzi zaidi, mratibu huyo alisema kuwa mizigo hiyo ya Sekondari ya Msolwa iliyoshikiliwa ni makontena 3 ambayo yana vifaa vya ujenzi vya shule hiyo na gari ya tani 3 kwa ajili ya kubebea mizigo ya shule hiyo ambayo iko katikati ya Dodoma na Morogoro na thamani ya mizigo yote hiyo iliyotoka shirika la Stigmatines Fathers - Italia ni zaidi ya milioni 20.

Aliitaja mizigo mingine iliyokwama bandarini hapo kuwa ni katoni 914 za maziwa ya Caritas ambayo husambazwa katika vituo mbalimbali nchini zikiwemo Zahanati na Kliniki na gari aina ya Pick-Up lenye thamani ya sh. milioni 10 mali ya seminari ya Mtakatifu James ya Moshi.

Hata hivyo Brother Mwasala, alisema kuwa mizigo mingine imechukuliwa kutoka bandarini baada ya kulipiwa kodi kufuatia kuhitajika haraka (urgency) na wahusika.

Aliitaja mizigo hiyo kuwa ni kontena 6 za Jimbo la Iringa kutoka Bogna Fathers - Italia ambalo lilibeba vifaa vya hospitali vikiwemo vitanda 60,chakula na nguo kwa ajili ya wagonjwa, thamani yake ni zaidi ya milioni 13.

"Askofu wa Iringa imebidi akubali kutoa kodi kiasi cha shilingi milioni 2.4 kwa ajili ya kulipia mizigo ya jimbo lake. Pia hata shirika la Consolatha Fathers na Capuchin Fathers nao pia wamelipia kodi ya mizigo yao,"alisema Brother Mwasala bila kutaja aina ya mizigo hiyo na kiasi cha kodi walicholipa.

Hali nyingine iliyojitokeza ni kwamba pamoja na taarifa ya Waziri kuonyesha kuwa kodi itakayotozwa kwa Taasisi hizo za kidini ni kodi tu ya kawaida tofauti na ile ya ongezeko la thamani (VAT) lakini hali imekuwa kinyume kwani waliochukua mizigo yao wametozwa hata VAT.

Alisema inashangaza mizigo ya jimbo la Iringa iemtozwa kodi ya shilingi milioni 1.2 na VAT shilingi .1.2"

Matonya amhakikishia Makamba kuwa atatumia 'uninja' arudi jijini

Na Dalpina Rubyema

OMBAOMBA maarufu jijini Paul Matonya, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Saalaam Luteni Yusufu Makamba kuwa ingawa amemkamata katika operesheni yake ili pamoja na ombaomba wenzake apelekwe kijini kwake, hatakaa huko na baada ya muda mfupi tu, atakuwa jijini.

Ingawa haikufahamika njia atakazotumia, ombaomba huyo maarufu jijini kwa kuomba huku amelala chali akiwa amenyanyua kopo, alimhakikishia Mkuu huyo wa mkoa Luteni Makamba wakati anampa msaada wa kaptura na fulana ili pindi Matonya atakapofika nyumbani, awe mtanashati kama alivyosema Makamba mwenyewe.

Kwa mara kadhaa katika mazoezi yaliyopita ya kuwarudisha ombaomba vijijini kwao, Matonya amekuwa akirejea jijini ndani ya wiki moja tu tangu kufikishwa kijijini kwake mkoani Dodoma.

Wakati huo huo:Baadhi ya ombaomba walionusurika katika kamatakamata hiyo, wamebadilisha staili yao ya kuomba na sasa badala ya kusimama barabarani, sasa wanatembelea maofisini na madukani.

Mwandishi wa habari hizi alimshuhudia mmoja wa ombaomba hao Bw. Mbaraka Maulidi mkazi wa Vituka akiwa kwenye studio moja ya picha eneo la Kariakoo akiendesha shughuli zake za kuomba huku akimlalamikia Luteni Makamba hakufanya vizuri kuwamata ombaomba wote na badala ya kuwakamata wenye uwezo wa kufanya kazi.

Ombaomba huyo libahatika kupewa sh. 1500/= toka uongozi wa studio hiyo.

"Kwa kweli Bw. Makamba kitendo alichokifanya siyo cha kiungwana, hatumwombei mabaya kwa Mwenyezi Mungu, hapana Mungu azidi kumjalia, inshalah. Ila alichotakiwa kufanya ni kwamba angekamata wale ambao wana uwezo wa kufanya kazi, sisi tusioweza kitu akatuacha maana hata tukipelekwa huko vijijini tutazidi kuwa mizigo tu kwa familia,"alisema Bw. Maulid ambaye ni mlemavu asiyeona.

Hata hivyo uongozi wa Studio hiyo ulimwonea huruma ombaomba huyo na kumpatia pesa kiasi cha shilingi 1500.

Hata hivyo Bw. Maulidi alisiskika akimwambia mtoto wake kwamba baada ya kutoka katika studio hiyo waende kwenye ofisi zilizopo eneo la mnazi mmoja kwa kukusanya riziki zaidi, kitendo ambacho mtoto huyo alionekana kupinga.

Mwandishi alipomuuliza Bw. Maulid ni jinsi gani ameweza kunusurika katika kamatakamata ya Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa yeye hufanya shughuli zake (za kuomba) na kurudi nyumbani wakati waliokamatwa ni wale wanaolala mjini kwani kamatakamata hiyo ilifanyika usiku.

"Hata hivyo bado sijanusurika maana nasikia bado zoezi hili linaendelea, na watu wanakamatwa kila siku," alisema.

Uchunguzi wa mwandishi huu umeonyesha kwamba japo ni vigumu kukutana na Ombaomba jijini kama ilivyokuwa awali lakini katika baadhi ya mitaa ukiwemo Bibi Titi na Msimbazi bado Omba omba wachache hususani wenye ulemavu wa viungo wamekuwa wakiendelea na kazi yao kwa uangalifu mkubwa.

Hata hivyo Luten Makamba amesema kuwa ombaomba wote watapelekwa vijijini kwao wakalime na wale watakaorudi jijini watakamatwa na kupelekwa mahakamani ambapo watashitakiwa kwa kosa la uzembe na uzurulaji.

Luteni Makamba aliyasema hayo katikati ya wiki wakati alipotembelea kambi ya ombaomba waliokamatwa na kupelekwa katika eneo la shule ya Msingi Buguruni ambapo alisema utaratibu wa kuwapeleka makwao ombaomba hao unafanyika.

Idadi ya ombaomba waliokwisha kamatwa hada sasa hivi ni zaidi ya 470 na zoezi hilo bado linaendelea.

Kampuni ya ulinzi yaonyesha umahiri katika kuigiza ububu

lNi katika kuficha tuhuma za ulaghai

Na Josephs Sabinus

MAOFISA wa kampuni binafsi ya ulinzi jijini ya Eastern Security Services hivi karibuni walifanya kitendo kinachofanana na cha sanaa ya maigizo baada ya kuamua wote kwa pamoja kunyamaza kimya bila jibu la shari wala la heri baada ya mwandishi wa habari hizi kuwasalimia alipokwenda kufuatilia malalamiko ya dhuluma dhidi ya wafanyakazi wa ngazi ya chini.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni wakati mwandishi huyu alipokuwa akifuatilia malalamiko ya walinzi wa kampuni hiyo waliodai kuwa kampuni ya "Eastern" inawalaghai kuwa imebadili jina na kuwa Instant Security Services, hivyo walete wadhamini upya bila wao kujua sababu ya hatua hiyo. Hata hivyo imeelezwa kuwa Instant ni kampuni mpya na wala sio Eastern iliyobadilishwa jina.

Walinzi hao wamekuwa wakihofia mafao yao kwa ajira ya Estern kwani wanadai kuambiwa kampuni imebadili jina ni njama ya kuwafanya wasaini mkataba na kampuni mpya na hivyo kupoteza haki zao dhidi ya kampuni ya Eastern.

Wafanyakazi wanadai kuwa hatua hiyo ya Eastern kuwahamishia kinyemela kwenye kampuni nyingine inalenga katika kubana na kuzika haki zao wakati wowote watakapoachishwa au kuacha kazi au kustaafu.

Aidha, wamedai ingawa wateja wa kampuni hiyo huiajiri kampuni kwa gharama ya zaidi ya sh. 120,000/= kwa kila mlinzi, bado wao hulipwa kiasi cha sh. 30,000/=, malipo yanayofanywa kidogo kidogo hadi mshahara mzima (30,000/=) wa mwezi kuisha.

"Sasa mtu unalipwa sh. 2000/= 3000/= kati ya sh. 30,000/=hadi mshahara uishe, itakusaidia nini! Au basi unaugua wanakupeleka hospitali wanayoijua wenyewe kwa gharama ya juu halafu wanakukata mshahara, ni nini kama huo sio unyanyasaji?" alihoji kwa masikitiko mlinzi mmoja aliyekataa kutaja jina kwa kuhofia usalama wa ajira yake.Baada ya kufuatilia ofisini hapo kwa siku tatu mfululizo huku kila mara gazeti hili likiambiwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw.Said Salum Said na wasemaji wengine hawapo, mmoja wa maafisa wa kampuni aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Charles huku akikataa kuzungumza kwa madai kuwa sio msemaji Ahamisi ya Januari 13, alilishauri gazeti hili kurudi ofisini na likafanya hivyo mara tatu bila mafanikio. Hatimaye Bw. Charles alimpa mwandishi namba za simu za mkurugenzi huyo.Cha ajabu,siku iliyofuata yaani Ijumaa asubuhi, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo alipomuona mwandishi, alikimbia ghafla na kuingia ofisini. Mwandishi alipofika mapokezi alikutana na jopo la maofisa wapatao sita wakitoka ofisini mwao.

Licha ya mwandishi kuwasalimia mara kadhaa, hata maofisa waliozungumza nae siku za nyuma, hakuna hata mmoja aliyeitikia salamu na aliporudia kumsalimu kwa mara ya nne, mtumishi wa mapokezi alicharuka, "Bw. Hakuna mwenye shida na salamu zako," kisha maofisa hao wakatokomea na kumuacha ameduwaa huku mlinzi huyo wa mapokezi akiendelea kuchezea radio call bila usaidizi na kisha afisa mwingine ambaye hakutaka kujitambulisha akasema, "Watu wasifanye kazi wakalie magazeti yako!"

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya malalamiko kwa majuma mawili mfululizo umebaini kuwa Eastern Security Services Company Limited imekuwa ikiwaambia baadhi ya wateja wake kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imeitaka ibadili jina hilo na sasa inaitwa Instant Security Services Company Limited.

Kwa mujibu wa barua ya kampuni hiyo kwa Kaimu Katibu wa Mfuko wa Pensheni (P.P.F) yenye Kumb. Na. ISS/GC.1/004/99 ya Desemba 10, mwaka jana, iliyosainiwa na mkurugenzi Mtendaji Bw. Said Salum Said, sehemu yake inasomeka hivi, "...Tungependa kukufahamisha kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia barua Na.SOI/PS/VOL.1/127, imeagiza kuwa Eastern Security Services Co. LTD isiendelee kuwepo na badala yake imetupa kibali cha kuendesha shughuli kwa jina la Instant Security Services Co. LTD na masharti mengine yanaendelea kubakia yale yale..."

Hata hivyo, waraka wa Polisi wenye Kumb. Na.SO.1/PS/VOL.1/127 wa Novemba 9, mwaka jana uliotumwa kwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Instant Security na kusainiwa na Kamishna Mkuu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (S.A.C.P) A.A. Mwamunyange, unaonesha kuwa Instant Security Services Co. LTD ni kampuni mpya iliyoomba kibali na kuruhusiwa kufanyakazi.

Ikirejea barua ya kampuni ya Instant ya Novemba Mosi mwaka jana yenye Kumb. Na.ISSC/CL/VOL.001/99, barua hiyo yenye kichwa cha habari MAOMBI YA KIBALI CHA KUANZISHA KAMPUNI BINAFSI YA INSTANT SECURITY SERVICES COMPANY LIMITED DAR ES SALAAM, ilisema,

"kibali kimetolewa cha kuanzisha kampuni yako binafsi ya ulinzi jijini ijulikanyo kwa jina la INSTANT SECURITY SERVICES COMPANY LIMITED jijini Dar es Salaam. Unatakiwa pamoja na mambo mengine hata hivyo kukamilisha mambo muhimu haya yafuatayo kabla ya kuanzisha kampuni yako;

Unatakiwa kuisajili mara moja na kutuletea nakala ya usajili wake,...unatakiwa pia kuhakikisha kwamba unawalipa vizuri mishahara walinzi/ askari wako.

Gazeti hili lilipofika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini kujua kama kweli jeshi hilo ndilo lililoiamuru kampuni hiyo kubadili jina na sababu ya uamuzi huo , Kamishina Msaidizi wa Polisi Henry Kosseyi alisema, "... Jaribu kumuona Mwamunyange(Msemeji Mkuu wa Jeshi la Polisi), ila mimi ninachofahamu, haya mambo ya kusajili majina ya kampuni ni kazi ya Msajili wa Makampuni katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Lakini jina la Eastern bado tunalo."

Juhudi za Gazeti hili kumpata Kamishna Mkuu Msaidizi wa Polisi BW. Aden Mwamunyange hazikuzaa matunda kwani siku hiyo alikuwa kwenye kikao.

Askofu Chengula kufungua juma la Utamadunisho

Na Christopher Kidanka, Morogoro

ASKOFU wa Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evaristo Chengula atafungua juma la Utamadunisho lililoandaliwa na Chuo cha Falsafa na Teolojia (SIPT) cha mjini hapa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa chuoni hapo hivi karibuni na KIONGOZI kupata nakala yake, juma la Utamadunisho litakalofunguliwa Machi 20 na kufungwa machi 24 mwaka huu, litakuwa na kichwa ‘jinsi ya kufanya mashirika ya kitawa Tanzania yaishi karama zao na papo hapo yawe sehemu ya kanisa mahalia kikamilifu’.

Aidha ratiba hiyo inaonesha kuwa watoa mada wakuu katika kongamano hilo la utamadunisho watakuwa Pd. Aylward Shorter, M. Afr. Kutoka chuo cha Tangaza cha jijini Nairobi Kenya na Pd. Sahaya Selvan, SDB atakayetoa mada kuhusu ‘maana ya kuwa mtawa katika kanisa mahalia’

Juma la Utamadunisho ni kongamano ambalo huandaliwa kila mwaka na SIPT kwa nia ya kuendesha mijadala juu ya namna ya kutamadunisha karama mbalimbali za mashirika ya kimisionari na namna ya kuoanisha kazi za mashirika yaliyo washiriki wa chuo hicho na hali halisi ya Tanzania.

Takriban mashirika kumi ya kimisionari hushiriki kila mwaka katika mjadala na kushirikishana mafanikio na matatizo ya kazi zao na kutafuta utatuzi kwa pamoja.

Askofu Samba kuongoza msafara wa wahujaji Israeli

Na Dalphina Rubyema

RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Justin Samba na Makamu wake, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wanatarajiwa kuongoza msafara wa watu 28 watakao kwenda kwenye hija itakayofanyika katika Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, Januari 25 mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni, Mratibu wa shughuli zote za hija hiyo hapa nchini padre Theobald Kyambo, alisema hija hiyo ambayo inawashirikisha wahujaji kutoka katika majimbo 12 ya Tanzania itachukua muda wa siku kumi.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Same, Mbulu, Moshi, Musoma, Rulenge, Shinyanga, Mbinga, Njombe na Jimbo Kuu la Songea.

Alisema Mahujaji hao watakapokuwa kwenye nchi hiyo takatifu watatembelea maeneo mbalimbali ambayo Yesu Kristo alitembelea na kufanya kazi.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Yerusalemu, Nazareth, Bahari ya Galilaya pamoja na kutembelea sehemu ya Cana kwenye Kanisa ambalo Yesu Kristo aliyabadilisha maji na kuwa divai.Mratibu huyo aliyataja maeneo mengine kuwa ni Mto Jordan, Mlima Beatitudes, Kanisa la Yohane Mbatizaji, kutembelea kijiji cha akina Maria,martha na Lazaro pamoja na makumbusho ya Waisraeli.

Mratibu huyo ambaye pia ndiye atakayekuwa Mtendaji Mkuu katika kuangalia mipango yote ya hija alisema kuwa kulingana na ratiba mahujaji hao watalala katika mji wa Teberias siku tatu za mwanzo ambapo siku nyingine zitakazokuwa zimebaki watakuwa wanalala katika mji wa Yerusalemu.

Wakazi wengi Dar huishi maeneo ‘bomu’

Na Pelagia Gasper

ZAIDI ya asilimia 70 ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaishi katika viwanja visivyopimwa kutokana na kuvinunua kwa bei nafuu, imefahamika.

Akiongea na KIONGOZI ofisini kwake jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Ardhi na Usanifu Majengo (UCLAS) Bi. Agnes Mwaisalage, alisema kuwa licha ya viwanja hivyo kupatikana kwa bei nafuu, lakini vinaweza kusababisha athari mbalimbali.

Bi.Agnes alisema kuwa mkoa wa Dar es Salaam ni wa nne kwa wakazi wake kuishi katika viwanja visivyopimwa.

Alitaja mikoa mingine ambayo wakazi wake huishi katika viwanja visivyopimwa kuwa ni Rukwa (asilimia 95), Mbeya (asilimia 86) na Tabora (asilimia 82).

Amesema kuwa hapa jijini sehemu kubwa ya wakazi ambao huishi katika viwanja hivyo ni wakazi wa vitongoji vya Tandale na Kigogo.

Wakati huo huo; Serikali imeshauriwa kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa zitokanazo na misitu ili iweze kuwavutia wawekezaji katika sekta ya misitu hapa nchini.

Ushauri huo umetolewa na Dk. Felician Kilahama wa mradi wa kuhifadhi na kusimamia misitu, wakati alipohojiana na Kiongozi ofisini kwake jijini wiki hii. Dk. Kilhama ameelezea kuwa ongezeko hilo, limepelekea bidhaa ya mbao kuanza kupungua jijini, jambo ambalo wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wameanza kupungua siku hadi siku.

Alisema mwishoni mwa wiki kuwa bidhaa ya mbao ni moja ya bidhaa inayoongezea pato Taifa katika uzalishaji wa thamani mbalimbali na ujenzi.

"Serikali inabidi ijue umuhimu na faida za mbao, basi ipunguze VAT, ili wawekezaji waweze kujitokeza na kuwekeza katika sekta ya misitu" alisema.

Dk. Kilahama alieleza kuwa, hivi sasa huku katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Lindi, Mwanza, na Songea, bidhaa ya mbao inazidi kuongezeka lakini kutokana na kodi hiyo imepelekea kurundikana ambapo wafanyabiashara wake wameanza kufanya miradi mingine.

"Mbao nyingi sana mikoani,lakini mtu anashindwa kuzisafirisha. Licha ya kodi hii nayo kuwa juu sana, huoni kama mtu hapati faida yeyote, wapunguze kodi ili mbao hizo ziuzwe hata nje ya nchi," amesema.

Pia ameeleza kuwa wapo watu wanaoagiza mbao kutoka nje ya nchi na akasema hiyo nayo inachangia katika kudidimiza maendeleo ya nchi.

Jeshi la Polisi kuajiri walio na stashahada, Shahada

Na Neema Dawson

JESHI la Polisi nchini linategemea kuajiri vijana wa kike na wa kiume walio na Stashahada za juu au Shahada.

Hayo yalisemwa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi nchini ACP Henry Kosseyi katika mahojiano na gazeti ili kuhusiana na ajira za polisi zinazotegemea kuanza mapema, mwaka huu.

Alisema kuwa walio na Stashahada za juu na digrii watapewa kipaumbele kwa kutuma maombi yao moja kwa moja . Inspekta Jenerali wa polisi wa Jeshi la Polisi nchini alisema watachukuliwa zaidi wale walio na umri wa miaka 28 na waliosomea Ufundi, Sheria na Udaktari. Lakini Afande Kosseyi, alisema hata hivyo wale waliomaliza kidato cha nne na cha sita ambao wao maombi yao yatatakiwa kutumwa kwa makamanda wa Polisi wa mikoa pia wataajiriwa.

Alisema Jeshi hilo limeweka utaratibu huo ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa jeshi hilo linakuwa la watu walio na kiwango cha j uu cha elimu kwa ajili ya kwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya kupambana na uhalifu ambao mwingine unafanywa kisomi.

Ndoa ya Mkristu na Muislamu yafananishwa na dereva wa

daraja A

Na Getruda Madembwe.

PADRE Adrew Mwachibindo ameifananisha ndoa ya Muislam Marium Saidi na Mkatoliki Bw. Constatino Amri kama dereva wa daraja A na hivyo haihitaji kuwa ya wake au wanaume wengi.

Akitoa mahubiri wakati wa Ibada ya ndoa hiyo iliyofanyika katika jumuia ya Mtakatifu Anyesi iliyopo katika Parokia ya Magomeni Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre huyo alisema ndoa yoyote ni kama udereva wenye madaraja matatu ya A,B na C.

Akitoa ufafanuzi juu ya mfano wake, Padre huyo wa Parokia ya Magomeni alisema kuna ndoa nyingine zinazoruhusu wake wengi na zile zisizoruhusu zaidi ya mke mmoja na kwamba ndizo zinzosisitizwa na Kanisa Katoliki ili kuzifanya zidumu na kuwa zenye upendo zaidi.

Alisema kama dereva wa daraja A asivyoruhusiwa kuendesha magari ya dereva wa daraja C ndivyo ndoa kama ya maharusi hao ya mme mmoja na mke mmoja isivyoruhusiwa kujihusisha na maisha ya ndoa ya mme au mke zaidi ya mmoja.

‘Nyie ndoa yenu ni ya mme na mke mmoja na hivyo kamwe msiiruhusu ikawa ya wake au waume wengu maana ndoa ya aina hiyo huwa ina madhara mengi kimwili na kiroho’ alionya.

Wakati huo huo: akisoma risala mbele ya Padre huyo Katibu wa Jumuiya hiyo Bw. Marko Mutabazi alisema idadi ya wanajumuiya 55 waliopo ni kubwa kuliko idadi ya wanaohudhuria misa za jumuiya kutokana na vikwazo mbalimbali sugu.

‘Idadi ni kubwa lakini wanaohudhuria misa ni wachache na hii inatokana na wanaume wengi kuishi muda mrefu na wanawake kabla ya kufunga ndoa na sisi viongozi tunapowafuata wanasingizia vigezo ni mambo yao ya ndani’ alisema

Kurasini kufanya harambee ya majengo

Na Waandishi Wetu

WAZAZI na walezi wa watoto wa shule ya msingi ya Kurasini wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Jumapili hii wanatarajiwa kufanya harambee ya kuchangia ujenzi wa vyumba sita vya madarasa vya nyongeza, ofisi na choo katika eneo la Bandari ili kupunguza msongamano wa wanafunzi wa shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 5,200/=.

Wakizungumza na gazeti la Kiongozi kwa nyakati tofauti viongozi kadhaa walisema, sambamba na harambee hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Luten Yusufu Makamba anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika majengo hayo ambayo ujenzi wake unaendelea kwa kasi.

Mbungewa Temeke Bw. John Kibaso alisema kata nyingine hazina budi kuiga mfano wa Kurasini kwa kujitolea kupambana na adui ujinga wakitoa michango yao ya hali na mali. "Licha ya Serikali kuagiza kuwa watoto wanaoanza darasa la kwanza walipe sh 2000/=, wazazi wa Kurasini wenyewe wameomba wazidi kuchangia kuondoa tatizo la elimu," alisema Kibaso.

Mwenyekiti wa Kamati ya shule Bw. Juma Kilasa alisema "Walimu wa hapa wanajituma mno ndiyo maana mafanikio ya kielimu yanawatia moyo wazazi hata kujitolea namna hii’ alisema.

Naye Katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kurasini Bw.Madoshi Manoni, alisema anaitiwa moyo wa wazazi katika kupambana na tatizo la elimu.

' watu wanapenda kujua na kuona pesa zao zinafanya nini katika misingi ya uwazi na ukweli’ alisema.Jumapili iliyopita wazazi pamoja na mbunge walifanya harambee fupi na kupata sh.540,000/= zikiwa ni pesa taslimu na ahadi ambapo Mbunge huyo alitoa sh. 200,000/=na Katibu wa chama cha CUF Tawi la Magorofani eneo la Bandari Kurasini Bw.Kasisi Mahushi alitoa sh. 20,000/=. kwa ajili ya kuwawezesha watoto 1050 kati ya 1500 waliokosa nafasi ya kuanza darasa la kwanza.

 

Maelfu ya walioasi Kanisa walishwa keki Dar

Na Peter Dominic

WAUMINI wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship lililopo Mwenge jijini walioliasi kwa muda mrefu, wamerejea kwa vishindo na kufanyiwa tafrija iliyowapa fursa ya kulishwa keki.

Waumini hao ambao idadi yao ilikadiriwa kuwa zaidi ya elfu mbili wamelirejea kanisa hilo hivi karibuni kufuatia kilichoelezwa kuwa maombi ya waumini wenzao ambao waliazimia kufunga kwa siku moja na kuomba kwa wiki mbili mfululizo.

Mchungaji Zakaria Kakobe, aliyeonekana kuwa na furaha toka mwanzoni mwa ibada hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita kutokana na idadi kubwa ya waumini waliofurika siku hiyo pamoja na kuwapo na baadhi ya watu waliodondoka kwa mapepo, alinukuu baadhi ya Maneno Matakatifu toka ndani ya Biblia. Aliwaelezea waumini hao kuwa ibada hiyo ni ya pekee kwa vile kundi kubwa la kondoo waliopotea kwa mda mrefu walikuwa wamerejea kwa Bwana.

Akielezea furaha aliyokuwa nayo, Mchungaji Kakobe alikinukuu kifungu cha Biblia juu ya mtoto aliyemuibia Baba yake na kutapanya mali zake lakini zilipoisha alirudi kuomba msamaha na kusamehewa.

"Japo Baba yake alimpokea kwa furaha na kumchinjia ndama mnono, ndugu yake hakupendezwa na hali hiyo" kadhalika aliwaonya waumini wa kanisa hilo kutowachukia wenzao waliorejea kutokana na matendo yao maouvu, bali wawe na furaha na kushirikiana nao.

Waumini hao waliorejea katika kundi walikaa pamoja na mchungaji Kakobe wakila naye keki (140) zilizoandaliwa maalum kwa waumini kwa mtindo wa mashindano ya keki bora kuliko zote.

Sherehe hizo ambazo ziliendelea zilipelekea Mchungaji Kakobe kufanya kazi ya utangazaji (MC) na kuamuru keki hizo zikatwekatwe vipande na kumlisha kila mmoja wao.