PADRE KILAINI ATEULIWA KUWA

ASKOFU MSAIDIZI WA DAR ES SALAAM

 

Nilipata ajali fuvu la kichwa likagawanyika vipande

lNikiwa njiani kwenda hospitalini ndege yetu ikatekwa na wahaini

lCha ajabu ubongo haukuathirika, sasa utatumika kwa kazi ya Uaskofu

Na Dalphina Rubyema

KAMA si rehema za Mwenyezi Mungu pengine tusingesikia tangazo la Januari 8, mwaka huu wakati Baba Mtakatifu Yohane Paulo ll, alipomteua Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Method Kilaini kuwa Askofu Msaidizi wa jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Ile ajali mbaya ya gari ambayo aliipata Novemba 15,1981 eneo la Pasiansi,mkoani Mwanza, ndiyo msingi wa hisia hizi.

"Ajali ilisabaisha fuvu la kichwa changu kugawanyika vipande, japo kwa juu ngozi ilionyesha sina tatizo, nilipoteza fahamu kwa wiki nzima. Hata hivyo cha kushangaza ubongo ulikuwa mzima kabisa," Kilaini aliliambia KIONGOZI muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa Askofu alipotakiwa kueleza baadhi ya misukosuko ambayo hauwezi kuisahau katika maisha yake.

Akaongeza; Nililazwa Hospitali ya Bugando kwa mwezi mmoja; sitamshau Dk. Makwani, alinisaidia sana. Kisha nilihamia KCMC Moshi ambako nilikaa kwa wiki mbili zaidi."

Mkosi huja juu ya mkosi; wakati "Padre" Kilaini, ametoka hospitalini hapo akielekea huko Roma, Italia kwa uchunguzi zaidi, ndege aliyokuwa ameipanda ikatekwa na wahaini waliokuwa wakipinga Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Kisa kizima soma makala ya wasifu wake Ukurasa wa 7,8.

Akielezea hisia zake baada ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Method Kilaini amesema kuwa alijisikia kushtuka baada ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Yohane Paulo wa II kumteua kushika wadhifa huo.

Askofu huyo mteule aliyasema hayo hivi karibuni ofisini kwake wakati akihojiwa na Mwandishi wa bahari hizi.

Alisema kuwa hakuwa na wazo lolote kama angeweza kuteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa Askofu, bali alichokuwa anajua ni kwamba baadaye mwaka huu alitarajia kwenda kufundisha katika Chuo Kikuu kimoja nchini Marekani.

"Kwa kweli nilishtuka, kwa sababu wazo la kuteuliwa kuwa Askofu halikuwa kichwani mwangu kwa vile Juni, mwaka huu nilikuwa namaliza kipindi changu cha tatu hapa TEC na nilipanga kwamba nipumzike kidogo na Septemba mwaka huu ningeenda Dayton University huko Marekani na huko ningekaa kipindi cha mwaka mmoja- miwili nikifanya utafiti na kufundisha juu ya theolojia ya historia ya Kanisa. Tayari mambo yalikuwa yameanza kukamilika," alisema.

Hata hivyo Askofu huyo mteule alisema kuwa mshtuko wake ulikuja kupungua baada ya kubaini kuwa atafanya kazi na Mwadhama Polyarp Kardinali Pengo, ambaye ameshafanya naye kazi kwa muda wa miaka 9 aliyokaa TEC.

Aliongeza kuwa yeye na Mwadhama Kardinali Pengo, wanashirikiana kwa karibu sana katika masuala ya utendaji kazi ndio maana amefarijika kuwa msaidizi wake. Askofu mteule alisema kuwa bado anaonyesha woga kuongoza jimbo la Dar es Salaam kwani ndipo makao makuu ya karibu kila kitu. "Serikali iko hapa, mawaziri karibu wote hapa hapa na kadhaika... hakuna kitu kidogo ndani ya Dar," alisema. "Niliahidi kwa Mungu kwamba kokote nitakakoitwa nitaitika, hivyo hata kubaki Dar Es Salaam nimeitikia kwa roho nyeupe," Kilaini alieleza.

Hata hivyo Askofu huyo Mteule alisema kuwa mwa mambo anayoweza kujivunia wakati wa uongozi wake katika TEC ni ushirikiano mzuri wa TEC na madhehebu mengine ikiwemo BAKATWA, CCT, PCT na kusisitiza kuwa mshikamano huo udumishwe.

Januari 8 mwaka huu, Kiongonzi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa pili alimteua Padre Method Kilaini kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Padre Kilaini hadi anateuliwa kushika wadhifa huo alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na alishika nafasi hiyo tangu mwaka 1991 na alikuwa anamaliza muda wake Juni, mwaka huu.

Padri Kilaini ambaye ameingoza TEC kwa awamu tatu mfululizo atapewa rasmi daraja la Uaskofu Machi 18, mwaka huu na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Kardinali Pengo, katika Ukumbi wa Msimbazi Centre jijini.

Caritas Tanzania yatumia mil.130/= kusaidia wenye njaa

Na Dalphina Rubyema

Shirika la Misaada la Cartas -Tanzania lililo chini ya Kanisa la Katoliki limetumia zaidi ya shilingi milioni 130 kusambaza chakula cha misaada katika majimbo yanayoathirika kwa njaa nchini.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni ofisini kwake ,Katibu Mtendaji wa Caritas Tanzania Bw.Clement Rweramila alisema usambazaji wa chakula hicho umefanyika katika awamu mbili tofauti ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Agosti hadi Oktoba na awamu ya pili ilifanyika kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana .

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji huyo ugawaji wa chakula hicho ambacho kilitokana na ufadhili wa nchi za Ujerumani ,Ufaransa na Korea ,umekuja baada ya wakurugenzi wa Caritas majimboni kufanya tathimini ya njaa kufuatia kikao cha tathimini kilichofanyika Machi, mwaka jana ambapo iliazimiwa kuwa kila Mkurugenzi afanye tathmini katika maeneo yanayoathiriwa na njaa jimboni kwake na kupeleka taarifa CARITAS-Tanzania makao makuu.

BW. Rweramira alisema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo kutoka majimboni ofisi yake ilianza kutafuta wafadhili wa kutoa misaada na ilipopatipkana usambazaji ulianza mara moja.

Aliyataja majimbo yaliyopata msaada huo wa chakula (mahindi)katika awamu ya tatu na kiasi kilichopelekwa kikiwa katika mabano kuwa ni Mbulu(tani50),Singida (tani 40),Dodoma (tani 52),Morogoro (tani 52) na Same (tani 52).

Majimbo yaliyopata msaada kwa awamu ya nne ni Singida(tani40),Mbulu (tani90)Morogoro (tani 40)Arusha (tani 120),Same (tani 80) na Iringa (tani 20)

Hata hivyo alisema kuwa kuna majimbo ambayo yalichelewa kuleta taarifa, hivyo kuchelewa kupata chakula cha awamu ya nne, yataanza kupatiwa msaada huo mwishoni mwa Januari, mwaka huu.

Aliyataja majimbo hayo yanayotajiwa kupata chakula kuwa ni Shinyanga,Musoma na Tanga.

Alisisitiza majimbo yote kuleta tathimini ya maeneo yaliyoathirika na njaa kwenye ofisi za Caritas ili ofisi hiyo iweze kupeleka taarifa wafadhili.

Katibu huyo Mtendaji pia amewataka Watanzania wakazanie kilimo na wanapopata chakula wasikiuze kwa walanguzi bali wakiuze majimboni kwenye vitengo vya udhibiti wa chakula (food security) vilizoazishwa na Caritas yenyewe, ili wanapokwamba viwarudie.

Shule ya msingi Kurasini kutoa mafunzo ya Kompyuta

Na Mwandishi Wetu

SHULE ya msingi ya Kurasini wilayani Temeke inatarajia kufungua darasa la kompyuta mapema mwaka huu ili kukabiliana na karne mpya ya Sayansi na Teknolojia.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kurasini, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw.Madoshi Manoni, alisema kompyuta hizo zinatarajiwa kuwasili shuleni hapo mapema mwezi huu na kwamba wataalamu wa vifaa hivyo walitarajiwa kuanza kazi ya kuandaa mahali zitakapofungwa.

Mpango huo wa kisayansi utawafaidisha wanafunzi wa shule hiyo kuanzia darasa la nne hadi la saba, alisema na kuongeza kuwa katika mpango huo ni watoto wa shule hiyo pekee watakaofaidika na elimu hiyo. "Sitarajii kuwapokea wanafunzi wengine tofauti na wanaosoma katika shule hii," alisema Bw. Manoni.

Mwalimu Manoni, alifafanua akisema kuwa ili kufanikisha azima hiyo tayari limekwishatengwa darasa moja kwa ajili ya kuwafundisha watoto hao na kuongeza kuwa kila mtoto mmoja atatakiwa kuchangia shilingi 3000 kwa mwezi kwa ajili ya kukidhi gharama za uendeshaji wa elimu hiyo.

Japokuwa hakutaka kufafanua kwa undani zaidi upatikanaji wa kompyuta hizo, alisema mafanikio ya mpango huo ni kwa ushirikiano na uongozi wa shule ya Sekondari ya (JKT) kitengo cha kompyuta ambapo baada ya kutuma maombi yake katika shule hiyo, uongozi wa kitengo hicho ulifanya ziara shuleni kwake na kuona kuwa shule hiyo inao uwezo wa kutoa elimu hiyo ya Kompyuta.

Hata hivyo, alisema elimu hiyo haitakuwa ya lazima isipokuwa ni kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kuchangia sh 3000 kila mwezi ila alisema watakaoshindwa kulipa gharama hizo watafikiriwa

Wakati huo huo Shule hiyo ya msingi Kurasini imepata msaada wa matofali 5000 kutoka kwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa eneo la Bandari ili kupunguza msongamano wa wanafunzi shuleni hapo.

Manoni, alisema uamuzi wa kujenga vyumba vinne vya madarasa nje ya eneo la shule ya msingi Kurasini umefuatia msongamano mkubwa wa wanafunzi katika shule hiyo na mazingira ya sasa ya shule yake kutoruhusu kujenga vyumba vingine, na idadi ya watoto inaongezeka. "Idadi ya watoto 5000 ni sawa na shule nne ndani ya moja, kwani kwa kawaida shule inatakiwa iwe na watoto 1500. Hata mwaka huu nimepokea watoto 1500 watakaoanza darasa la kwanza" alisema.

Wahaya waunda chama cha kusaidiana

Na Christopher Udoba

WATU na wake zao wapatao kumi wameunda chama chao kinachojulikana kama DECEM Assocoation jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Katibu wa chama hicho Bw. Patric Mutayoba,chama chao kipo mbioni kupata usajili katika wizara ya Mambo ya Ndani wakati wowote.

Madhumuni ya kuunda chama cha DECEM ni kwa ajili ya kusaidiana katika shida na raha pia Bw. Mutayoba amesema katika mahojiano jijini wiki iliyopita.

Kwa mfano. Bw. Mutayoba ametaja kuwa wanachama wao huweza kukopeshana mikopo ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi.

Ameongeza kuwa chama chake kinatarajia pia kuanzisha miradi ya biashara kutokana na michango yao.

Wanachama wanaounda umoja huo sharti watokane na kabila la Wahaya toka mkoani Kagera, amefafanua.

Amemtaja Bw. Fransis Kajuna kuwa ndiye Mwenyekiti wa DECEM na kwamba kuna kamati yenye viongozi watatu na wajumbe wawili.

Mtoto aokotwa katika Sherehe za Jubilei

Na Getruder Madembwe

Mtoto wa kike aliyetambulika kwa jina moja la Getruda (11) amepatikana katika sherehe za Jubilei ya watoto hivi karibuni zilizofanyika katika kanisa la Parokia ya ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam baada ya kupotea siku tatu akiwa mgeni toka Bukoba.

Akisimulia kisa hicho ,Bw.Jackson Ishengoma, alisema usiku wa Ijumaa

(Januari 7,2000)majira ya saa 2.30 usiku katika maeneo ya Nzasa wilayani Temeke,alimkuta mtoto huyo akiwa amezubaa bila kujua pa kwenda wala la kufanya.

Alisema alipomuuliza mtoto huyo alikuwa anafanya nini katika mazingira hayo usiku huo badala ya kwenda nyumbani,mtoto huyo alisema hajui aende wapi maana amepotea na hajui nyumbani kwao.

Bw.Ishengoma alisema siku iliyofuata aliamua kumpeleka Mbagala kanisani ambapo kulikuwa na sherehe za jubilei ya watoto ili kumtangaza.

Wakati mtoto huyo Getruda anatangazwa kanisani,msichana Jaqline (15) aliyekuwa miongoni mwa waamini kanisani hapo alijitokeza na kusema Getruda ni mdogo wake .

Akielezea kupotea kwa mdogo wake,Jaqline ambaye ni mkazi wa mbagala kuu wilayani Temeke alisema, "Getruda ni mgeni huku Dar es Salaam.Alitoka Bukoba sio siku nyingi alikuwa hajazoea huku"

Akiendelea kusimulia kuwa siku aliyopotea Jaqline alikuwa akimrudishsa kwa mama yake na wlipofika njiani wlianza kutishiana ili kujua atakaye wahi kufika kuliko mwenzake huku Getruda akidai anapafahamu nyumbani.

"Lakini nilipofika nyumbani kwa mama yake sikumkuta .Tukamsubiri halafu tukaanza kuwa na wasiwasi .Tukaanza kumtafuta mpaka leo bado nyumbani wanamtafuta."alisema Jaqline.Hata hivyo mtot Getruda hakuwa na tatizo lolote na alipoulizwa ilikuwaje akapotea na alikuwa katika mazingira ya namna gani katika kipindi hicho,alitulia tu bila ya kusema lolote.

Wanaokwepa kodi ya mapato wataadhibiwa bila ‘kutazamwa usoni’

Na Neema Dawson.

MENEJA wa Idara ya mafunzo na walipa kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Bw. Augustine Mukandara, amesema wanaokwepa kodi ya ongezeko la thamani (VAT)wakati vipato vyao vinawaruhusu kulipa wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya sh.200,000 bila huruma.

Mukandara, aliyasema hayo wakati akitoa mada katika semina kwa wafanyabiashara mbalimbali wa mkoa wa Dar es Salaam juu ya ulipaji kodi iliyofanyika jijini hivi karibuni .

Alisema ingawa zipo taratibu zinazowapa muda wafanyabiashara ili kujichunguza uwezo wao wa kulipa kodi kutokana na viwango vya mapato yao,wengi wanaostahili hukwepa kulipa kodi hiyo.

Mukandara, alisema watakaobainika kutumia zaidi ya muda wa miezi mitatu ya kujichunguza, mamlaka itawchukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya sh.200,000(laki mbili).

Aliwasisitiza wafanyabiasha kuwa makini na utunzaji wa kumbukumbu wanazopewa wanapolipa kodi ili kuepuka usumbufu Mamlaka inapofanya msako dhidi ya wasiolipa.

Akifafanua juu ya ulipaji kodi,Mukandara, alisema kodi ya mapato inalipwa na mfanyabiashara aliyesajiliwa pale anapokuwa na mlaji, kwani kodi hiyo inakuwa imelipwa na mlaji (mteja) na wala si yeye mfanyabiashara.

Hivyo mfanyabiashara inabidi alipie kodi hiyo kama mlaji," alisisitiza.

Taasisi za dini kutozwa kodi ni uamuzi holela - Cheyo

Na Dalphina Rubyema

Waziri Kivuli wa Fedha na Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Party (UDP) Bw. John Moses Cheyo, amesema hatua ya serikali kuzifutia taasisi za dini misamaha ya kodi na usumbufu na hasara zote zinazotakana na hatua hiyo inatokana na ufinyu wa ushirikiano ndani ya Serikaki.

Cheyo ambaye alikuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Mbezi, jijini mwishoni mwa wiki, alisema kama kungekuwa na mawasiliano na ushirikiano wa kutosha kati ya Rais na Waziri wa Fedha, pengine hatua hiyo isingechukuliwa.

Cheyo, maarufu kwa jina la Bw. Mapesa, alisema hashangai Rais Mkapa kutangaza kuwa misamaha ya kodi kwa taasisi za dini itaendelea, na kisha Waziri wa Fedha akafanya kinyume chake kwani hata Bungeni matukio ya Serikali kugongana yamekuwa yakijitokeza.

Alisema wakati fulani Bungeni Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake na Watoto, Mary Nagu, aliwahi kupingana na Waziri Mkuu Frederick Sumaye juu ya azimio la kubadili wizara hiyo jina. "Bw. Sumaye akasema iitwe ‘Wizara ya jamii jinsia na Watoto’ Kwa kweli ilikuwa kichekesho Bungeni kuona Waziri Mkuu anabishana na Nagu, kwanini hawakukaa kwanza na kuamua jina halisi la wizara hiyo na kuleta pendekezo lenye muafaka Bungeni" alihoji.

Alieleza kuwa hatua hiyo ilionyesha kuwa viongozi hususan mawaziri wamekuwa wakijiamulia mambo hata yale nyeti bila kushauriana na kukubaliana.

Hivi karibuni serikali kupitia Wizara ya Fedha imetangazwa kufuta msamaha wa kodi kwa tasisi za kidini nchini isipokuwa katika masuala ya elimu,afya,huduma ya maji na vifaa vya ibada,hatua ambayo utekelezaji wake umezusha utata mkubwa na kulalamikiwa vikali na viongozi wa dini nchini.

Agosti mwaka jana, Rais Benjamin Mkapa alitangaza kuwa serikali itaendelea kusamehe kodi kwa tasisi hizo,japo kuna watu waliokuwa wakilalamika kuwa serikali inakosa fedha nyingi.

 

Ngedere, nyani na nguruwe wawanyima usingizi wanakijiji

Na Mwandishi Wetu

WAKAZI wa kijiji cha Fukayosi katika wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani wamedai kuwa wanyama waharibifu ambao ni nguruwe, nyani na ngedere wamekuwa ni kero kwa kuharibu mazao katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 3000.

Wakazi hao walitoa malalamiko yao hivi karibuni wakati wajumbe wa warsha ya Mfuko wa kusukuma Maendeleo nchini (TASAF) walipotembelea kijiji hicho kuzungumza na wakazi hao juu ya maendeleo na matatizo yao pamoha na kufanya utafiti juu ya maendeleo ya kijiji hicho.

Wakitoa malalamiko yao kwa washiriki wa warsha hiyo iliyofanyika Bagamoyo wakazi hao walisema kuwa kila mwaka wanyama hao waharibifu wamekuwa wakiharibu mazao yao hali inayosababisha njaa na kudidimiza maendeleo yao.

"Kila tunachopanda hapa kijijini ikiwemo mihogo,mtama, mpunga, choroko na mbaazi huliwa na wanyama hao waharibifu" alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho Bw.Joseph Lyatuu.

Walisema kuwa juhudi za awali za kuwaangamiza wanyama hao kwa kutumia dhana za asili ambazo ni nyavu na kamba, zimekwisha fanyika bila mafanikio.

"Licha ya kwamba baadhi ya wanakijiji tunayomogobole na tunailipia kodi kila mwaka lakini hawafi" alisema mkazi mwingine ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

Washiriki wa warsha ya TASAF iliyomalizika hivi karibuni wilayani Bagamoyo walikuwa wamegawanyika katika makundi matatu ya kutembelea vijiji vya Fukayosi Zinga na Kongo vyote vya wilaya hiyo kwa lengo la kutekeleza mbinu za utafiti zitakazotumiwa ama kufuatwa na mfuko huo katika kupambana na umasikini nchini.

Vikundi hivyo vilivyoongozwa na Wakuu wa Mkioa iliyoshiriki warsha hiyo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Nsa Kaisi na Mkuu wa Mkoa wa Singida Bw. Anatory Tarimo wakiwemo wataalam mbalimbali kutoka Benki ya Dunia.

Mikoa iliyohudhuria Warsha hiyo ya siku saba iliyoandaliwa na TASAF yenyewe ni Pwani,Mtwara,Kagera, Singida, Shinyanga, Dodoma na Kilimanjaro.