Mkapa, Yona wawakoroga viongozi wa dini

lCCT wang’aka, TEC yacharuka, PCT yaja juu,BAKWATA yaduwaa

Joseph Sabinus na Dalphina Rubyema

UHUSIANO mwema uliopo nchini kati ya Serikali na madhehebu ya dini umedondokewa na utomvu unaoelekea kutia doa la dosari, na tayari viongozi wakuu wa jumuiya za kidini wamejipanga kujaribu kuzuia athari zake, imefahamika.

Habari zilizothibitishwa na viongozi kadhaa wa dini zimeeleza kwamba mawasiliano madhubuti yamekuwa yakifanywa miongoni mwa viongozi hao juu ya uamuzi wa Serikali wa hivi karibuni wa kuzitoza kodi taasisi za dini. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Dk. Wilson Ntebe, amepewa jukumu la kufikisha malalamiko ya taasisi za dini dhidi ya uamuzi huo Bungeni.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Dk. Method Kilaini, amelieleza gazeti hili mwishoni mwa wiki kwamba yeye amekabidhiwa kazi ya kufikisha kilio hicho kwa Rais Benjamin Mkapa.

Huku tayari Kanisa Katoliki likiwa limeshaanza kuathiriwa na maamuzi hayo, Padre Kilaini, amesema kitendo hicho kinaonekana kuwa cha kuyumba kwa Serikali au pengine kusahau umuhimu wa misaada ya Wafadhili ambayo wamekuwa wakiipitishia katika mashirika ya kidini.

Baadhi ya mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yameingiwa na hofu na habari zinasema endapo marekebisho katika utekelezaji wa agizo hilo la Waziri wa Fedha hayatafanywa yatawasiliana na Wafadhili wao ili wasitishe misaada kwani hakuna mfadhili atakayekubali kutuma msaada sambamba na fedha za kuulipia ushuru.

Mashirika hayo ni pamoja na Consolata Fathers, Society of Propagation of Faith na Stigmatines Fathers, kwa mujibu wa mratibu wa Clearing & Foading wa TEC Bro. Thadeus Mwasala.

"Kwa kweli sasa Serikali inaonyesha kuyumba, hatujui tunaelekea wapi. Wafadhili wamejitoa muhanga kutoa misaada halafu inakwamia bandarini! Hii inaonyesha kuwa taifa limeridhika na halihitaji tena misaada," alisema Dk. Kilaini na kuongeza kuwa awali Serikali ilikuwa ikishauriana kwanza na taasisi za dini kabla ya kutoa maamuzi ya namna hiyo, lakini anashangaa ni vipi utamaduni huo sasa unatoweka.

Katibu Mkuu huyo wa TEC, alisema barua ambayo Ofisi yake iliipata kutoka Serikalini ilisema kodi hazitatozwa katika vifaa vya ibada,elimu, afya na huduma ya maji, lakini cha kushangaza ni kuwa utekelezaji wa maelezo hayo ni kinyume chake. " Kanisa limelazimika kulipia ushuru hata vifaa ambavyo vililetwa na wafadhili kwa ajili ya kusaidia walemavu na vingine bado vimekwama," alisema Dk. Kilaini kwa mshangao.

Gazeti hili halikufanikiwa kumpata Katibu Mkuu wa CCT Dk. Ntebe, kuelezea hisia za jumuiya yake, lakini taarifa zilizopatikana zinasema hatua hiyo imewaudhi na ndiyo maana amekubali kulivalia njuga suala hilo hadi Bungeni.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Rajab Kundya, yeye alisema kuwa Waziri Daniel Yona ametoa agizo hilo kinyemela na kibaguzi kwani BAKWATA haijapata hata barua ya taarifa juu uamuzi huo wa Serikali. "Tumeshituka tu kuona kwenye magazeti," alisema.

Alipoulizwa endapo kuna mali zozote za BAKWATA zilizokwishakwama bandarini na ni za thamani gani alisema, " Siwezi kutaja thamani kamili, lakini vitu vyetu vimekwama kwa kuwa ni agizo lililotolewa kinyemela."

"Lazima taasisi za dini tukae pamoja mapema tuzungumze la kufanya. Kwa kuwa Katibu Mkuu wa TEC yupo, baada ya Sikukuu hii ya Idi, tufanya haraka tuwasiliane na wenzetu wa vikundi vingine tuamue la kufanya."

Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (PCT) Askofu Sylvester Gamanywa, alisema kama kweli Serikali imepania kufanya hivyo, basi ijue inajiwekea mazingira magumu wakati huu ambapo nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

"Serikali imekuwa ikiyaomba mashirika ya dini kuchangia kuondoa matatizo ya jamii, sijui haioni kuwa inayavunja moyo au labda imeona service za mashirika haya hazifai," alihoji.

Aliongeza kuwa kwa asili ya mashirika ya kidini sio ya uzalishaji , hivyo kuyapa mzigo wa kodi ni sawa na kutaka kuyaua kabisa yasiwepo.

"Kwa nature (asili) taasisi za dini na non-profit making (zisizoendeshwa kibiashara) na hata watumishi wake wanajitolea; au labda serikali inataka dini zibadili mfumo wake wa utendaji, au basi labda vyama vya dini vifutwe yabaki makampuni ya biashara," alisema Gamanywa.

Alisema yeye haamini kama Rais anaweza kupinga kauli yake mwenyewe na hasa kwa kuwa yeye ndiye aliyetamka hivi karibuni kwamba misamaha itaendelea ingepaswa yeye huyo huyo atangaze kama kuna utata. "Labda kuna watendaji wadogo wanaofanya kinyemela. Hii ni historia maana kama wanasema kuna watu wanaotumia vibaya exemption wanashindwaje kuwadhibiti iwapo wana weza ku-identify uwepo wao?" alihoji.

Kiongozi huyo wa Jumuiya ya Wapentekoste nchini alisema inapaswa ieleweke kwamba misamaha ya kodi kwa taasisi za dini sio upendeleo bali suala la kihistoria, imani na la ki-Biblia. "Hii haiwezekani, naamini ni uamuzi wa watu wachache," alisisitiza.

Kanisa moja liitwalo Glory of Christ Tanzania Church, ni miongoni mwa makanisa yaliyokwishaonja uchungu wa uamuzi huo kwani Desemba 20, mwaka huu liliandikiwa barua na TRA kuarifiwa kwamba ombi la kusamehewa ushuru kwa mali zake zilizoingia nchini halitawezekana kwa vile kuanzia Desemba 1999 misamaha hiyo haitolewi tena.

Barua hiyo Na. TRA/DC/CE/DSM/P.20/1 ilisainiwa na Naibu Kamishna wa Ushuru na Forodha Bw. J.S. Kimwaga.

Barua hiyo ikiwa katika Kiingereza inasomeka kama ifuatavyo: This is to inform you that your application for tax exemption has not been successful on the grounds that tax exemptions under the provisions of GN No. 175 of 1973 to Religious and Charitable Orgainisations are no longer granted by this department. This is due to the fact that the said GN has since been revoked with effect from December 1999.

Kimwaga J.S- Depute Commisioner for Customs and Exercise, Dar es Salaam.

 

 

...Msaada wa Kanisa kwa ajili ya walemavu washikiliwa bandarini hadi ulipiwe kodi

Na Waandishi Wetu

LICHA ya agizo la Waziri wa Fedha kuzitaka taasisi za dini kufutiwa misamaha ya kodi isipokuwa kwa vifaa vya huduma za ibada, elimu, afya na maji, Kanisa Katoliki limelazimishwa kulipa kodi ya Sh. Millioni 1.9 kwa ajili ya vifaa vya walemavu na vingine vya elimu na afya kung’ang’aniwa hadi kodi ya mamilioni ya pesa itakapolipwa, imefahamika.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Clearing & Forwading wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Bro. Thadeus Mwasala, vifaa hivyo vikiwemo vya afya ni msaada kwa walemavu vilivyotumwa na wafadhili wa Shirika la Capuchin Fathers la Italia kwa ajili ya kusaidia huduma mbalimbali za kituo cha Walemavu cha Mlale kilicho kati ya Dodoma na Morogoro.

Alisema tangu Desemba 14 mwaka jana, vifaa vya kituo hicho vimekuwa vimeshikiliwa na kituo kulazimishwa kulipa kodi zaidi ya sh milioni 1.9/= hadi Desemba 31 mwaka jana, kiasi ambacho kimelipwa kuokoa vifaa hivyo vya thamani ya sh 10m/= visipigwe mnada.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili mwishoni mwa juma, Bro. Mwasala alisema, "Ingawa katika taarifa ya Serikali ilisema kuwa vifaa vya taasisi za dini vinavyohusiana na huduma za ibada,elimu, afya na maji vitaendelea kusamehewa kodi, bado wanajikontradikti wenyewe maana vifaa vyote vya Kanisa wanavyoshikiliwa na kung’ang’aniwa vilipiwe kodi vimo katika makundi hayo. Sijui sasa Serikali ina kusudio gani?"Alidai hali ya huduma na misaada kwa jamii inaelekea kuwa mbaya kwani wawakilishi wa wafadhili wameanza kuonekana kusita kuendelea kuleta misaada na akaongeza kudai kuwa siyo kazi ndogo kulipia mamilioni ya pesa kwa ajili ya huduma inayotolewa bure."Kumbuka Kodi iliyolipwa ya milioni 1.9/= haihusiani na malipo ya kawaida ya bandari, pamoja na usafiri hadi Mlale ya Sh mil. 1.6. Sasa kama sio kukatisha tamaa, malipo hayo yanayofikia milioni 3.5/= kwa vifaa vya milioni 10/= visivyouzwa inawezekana ?" alihoji kwa mshangao.

Akitoa mfano zaidi wa vifaa vinvyong’ang’aniwa hadi sasa bandarini kwa madai ya kodi ingawa vimetajwa kusamehewa, Bro. Mwasala alivitaja kuwa ni pamoja na gari la thamani ya sh milioni 10/= mali ya Seminari ya Mtakatifu James, ingawa lina hati zote zinazoonesha kuwa ni la shule (Seminari) na limetoka Shirika la Uenezaji Injili.

"Sijui kwa nini hawakutaja kabisa wanaposema vifaa vya elimu wana maana gani maana inashangaza sana kwani document zikija wanakataa.

Hivi sasa kontena tatu za vifaa vya maabara,friji, lori la kubebea vifaa, chakula cha wanafunzi na vifaa vya ujenzi wa Sekondari ya Msolwa ya Morogoro inayoendeshwa na shirika la Stigmatines Fathers wa Italia, vimeng’ang’aniwa; eti mpaka vilipiwe kodi kwa madai kuwa St. James ni taasisi inayojitegemea. Mimi hata sijui kwa nini Serikali inajichanganya yenyewe," alisema.Akizidi kuilalamikia Serikali kwa hatua yake inayoweza kuleta madhara katika huduma za jamii, Mwasala alisema vifaa kadhaa vikiwemo vitanda 60, chakula na nguo kwa ajili ya huduma za afya kwa ajili ya wagonjwa wa hospitali ya Parokia ya Usokeni katika Jimbo Katoliki la Iringa vya 13ml= vimeng’ang’aniwa hadi kodi ya sh.2,593,411 itakapoliwa.

Vifaa hivyo ni msaada toka kwa mapadri wa Jimbo la Bogna huko Italia.

 

 

Tusifanye mizaha na Ugonjwa wa Ukimwi - TEC

Na Mwandishi Maalum

KATIKA kikao cha 33 cha Kamati ya Utendaji katika kikao cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kilichokaa Kurasini Centre Novemba 10 hadi 12 Novemba 1999,Maaskofu wa Kamati hiyo wamewaasa Watanzania kutofanyia mzaha na baa la ugonjwa wa UKIMWI.

Hiyo ilitokana na ripoti iliyotolewa katika kikao hicho na Idara

ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Ripoti ilielezea kuwa kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI

kunazidi kuendelea kwa kasi kubwa katika mikoa yote ya Tanzania.

Ijapokuwa ni watu 110,000 ndio walioripotiwa mahospitalini kuwa na ugonjwa wa UKIMWI tokea mwaka 1983, lakini inakadiriwa kuwa idadi halisi ya waliopatwa na ugonjwa ni karibu nusu milioni.

Watu wapatao milioni moja na nusu hivi sasa wana virusi vya UKIMWI idadi ambayo ni karibu (10%) ya watu wazima Tanzania.

Vijana zaidi ya 5,000 wenye umri wa miaka 15-24 ambao ni 20% ya jamii waliambukizwa 1998, kwa mujibu wa taarifa hiyo. Hivyo vijana walichangia 60% ya maambukizo mapya katika mwaka 1998, ambapo jumla ya maambukizo mapya ilikuwa 8,675.

Maaskofu walikumbusha tamko walilotoa mwaka 1997, na

kusisitiza jamii kulipa kipaumbele tatizo la UKIMWI kwa kubadili tabia. Tabia inayotakiwa kubadilika ni ile ya uasherati.

Maaskofu wameonya kuwa siyo busara kutafuta njia za kufanya uasherati uwe salama; kwa sababu uovu upo katika tabia ya uasherati na ugonjwa wa UKIMWI ni matokeo ya uasherati.

Maaskofu walilaani tabia iliyoenea hivi sasa Tanzania ya kuficha ugonjwa huu na pengine kusingizia magonjwa mengine kama kisukari, shinikizo la damu na kadhalika, na badala yake walishauriWatzania wazungumzie tatizo la UKIMWI kwa ukweli na uwazi ili kuweza kunufaika na ushauri- nasaha.

Ili kuhakikisha Kanisa Katoliki na Jumuiya yote ya Watanzania, Maaskofu wa Kamati tendaji wameandaa Baraza la Ushauri, litakaloongozwa na Mhashamu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo la Geita, lenye wajumbe 13, kutoka majimbo tofauti Tanzania.

Majukumu ya Baraza la Ushauri (UKIMWI) yatakuwa kuota mafundisho ya mbinu zote za utekelezaji wa jitihada za kudhibiti UKIMWI chini ya Baraza la Maaskofu Tanzania.

Baraza la Ushauri litakutana mara tatu kwa mwaka na litatoa maelekezo kwa majimbo ya Kanisa Katoliki Tanzania kupitia Idara ya Afya ya Baraza la Maasofu Katoliki Tanzania.

 

'Polisi,Magereza wasikiuke haki za binadamu'

Na Neema Dawson

KITUO cha Sheria na haki za binadamu nchini kimeyataka majeshi ya polisi na Magereza kuzitumia vizuri nguvu walizopewa na Serikali na kutokiuka haki za binadamu.

Huo ni wito wa mwanasheria wa kituo hicho Bw, Evord Mmanda wakati akitoa mafunzo kuhusiana na haki za binadamu kwa maafisa wa Magereza na polisi wapatao 30 kutoka Tanzania bara na visiwani lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa haki na adhabu zinazotolewa zinazingatia haki za binadamu. Mafunzo hayo yalitolewa jijini hivi karibuni.

Mwanasheria huyo alisema kuwa kuna mikataba iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwalinda watu wachache na kuhakikisha wanapata haki zote wanazostahili hususani watoto wa Wanawake kwa kutokuwa tofauti na wengine na hilo lazima liangaliwe.

"Tunaelewa kuwa Serikali ina nguvu za kutosha na ina mchango mkubwa katika kulinda haki za binadamu na pia inachangia kwa kutumia vyombo vyake vya dola hivyo haikusita kuwaruhusu viongozi wake kutoa mafunzo kuhusiana na haki za binadamu ili wazijue na kuzifanyia utekelezaji pale zinapokosewa ndiyo maana kituo hiki kimefikia hatua ya kutoa mafunzo kwa watendaji wa Mahakama,wenye vyama vya siasa, mapolisi, magereza ili kuhakikisha kuwa haki zote za kiraia na kisiasa zinatendeka kuanzia ngazi za kikanda,kitaifa na kimataifa," alisema Bw. Evord.

Aidha alisema kuwa jamii imekuwa ikiwalalamikia mapolisi na magereza kwa ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwanyanyasa pale wanapobainika kupatikana na makosa, na kwamba jamii yenyewe pia inatakiwa kuelewa kuwa majeshi ya polisi na Magereza wanamchango mkubwa katika kuchangia ulindaji wa haki za binadamu pale wanapoona kuwa hajatendewa haki huomba msaada na hupatiwa.

Sambamba na hayo pia alisema kuwa jamii nayo inachangia kwa kiasi kikubwa kukiukwa kwa haki za binadamu kwa kukiukwa kwa sheria zilizowekwa, hivyo endapo sheria za nchi zitatekelezwa na hazitatumiwa kinyume na raia hali hiyo itapelekea kutokiukwa kwa haki za binadamu.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Sheria na kufunguliwa na Kamishna wa Magereza Bw. Egno Komba yalitolewa kwa maafisa hao kwa muda wa siku tano katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzaia uliopo Kurasini jijini.

 

Wanaume watakiwa wajitokeze kusomea ‘unesi’

Na Pelagia Gasper

VIJANA wa kiume wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika kuendeleza fani ya Uuguzi badala ya kuendelea kuamini kuwa uuguzi ni kazi ya wanawake.

Mkuu wa Chuo Kikuu kishiriki cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili (MUCHS), Profesa Jacob Mtabaji ameliambia KIONGOZI kuwa uwiano uliopo katika fani ya uuguzi kwa vijana wa kiume ni mdogo ukilinganisha na ule wa wasichana.

Amesema kutokana na uwiano mdogo uliopo kwa vijana wa kiume, imepelekea wauguzi wa kike kuanza kuwahudumia wagonjwa wenye ugonjwa wa akili, wakati ambapo wale wa kiume kwa sababu ya maumbile yao wangefaa zaidi kwa vile wagonjwa hao wengi wao ni wakorofi.Akasema, jamii imezoea kuona wauguzi wa kike katika hospitali mbalimbali kutokana na wazo potofu la kudai kuwa fani hii ya uuguzi ni ya wanawake kitu ambacho si cha ukweli.Akitaka jamii kuondokana na mawazo hayo potofu ya kudai fani hiyo ni ya wanawake tu, aliwataka vijana wa kiume kujitokeza kwa wingi.

Chuo hicho kinatarajia kuanzisha Shahada ya uuguzi ili kuinua zaidi fani ya uuguzi kwa kupata wauguzi walio bora zaidi.

 

 

Kuna hatari zaidi kwa vijana siku za usoni ikiwa .......

Na Mwandishi Wetu

IMEELEZWA kuwa matatizo yanayowakabili vijana yataweza kupungua iwapo jamii yote itaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na mashirika binafsi za kujenga malezi bora ya vijana.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Athuman Mdoe, wakati akifunga semina ya uhamasishaji kwa vijana iliyomalizika hivi karibuni kwenye ukumbi wa hoteli ya Valley View iliyopo jijini.

Bw. Mdoe alisema kuwa siku za usoni vijana watakabiliwa na matatizo mengi zaidi kuliko ilivyo kwa wakati huu endapo hapatachukuliwa hatua za haraka.

Alisema watu wengi hawaoni tatizo linaliwakabili vijana kwa hivi sasa la kupotoka kimaadili na malezi lakini matatizo makubwa yatakuja kuonekana siku za usoni.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Mradi wa Elimu ya Malezi ya Ujana (EMAU) vijana wapatao 27 walijifunza mbinu za kuhamasishana katika maendeleo yao, jinsi ya kuwasiliana, mila na desturi na jinsi ya kuendesha miradi.

Awali Mkurugenzi wa EMAU Bw. Stewart Chisongela alisema kuwa washiriki wa Semina hiyo walikuwa ni wale ambao walikwishawahi kupata mafunzo ya EMAU siku za nyuma.

"Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwaandaa washiriki kuweza kupata ujuzi na utaalam zaidi wa kufanya kazi zao lakini hata hivyo washiriki walikwishapata mafunzo ya EMAU siku za nyuma," alisema Bw. Chisongela.

Washiriki katika semina hiyo walitoka katika nyanja mbalimbali ikiwemo Afya na Taasisi za Ushauri Nasaha.

 

 

Mfuko wa maendeleo watakiwa usiwachekee wanasiasa

Na Dalphina Rubyema

WANASIASA wote nchini wameonywa kutotumia mfuko wa kusukuma mbele maendeleo Tanzania (Tanzania Social Action Fund-TASAF) kama mwanya wa kuendeshea siasa zao.

Tamko hilo lilitolewa hivi karibuni na Washiriki wa Warsha ya kujadili rasimu ya TASAF na mipango mbalimbali ya mfuko huo iliyomalizika wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani, hivi karibuni.

Washiriki hao ambao ni kutoka katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Singida, Shinyanga, Mtwara, Kagera na Kilimanjaro walitoa dukuduku lao kuwa endapo TASAF itatumiwa kwa masuala ya siasa, walengwa ambao ni wananchi wa kawaida hawatapata huduma za mfuko huo ambao una lengo la kupambana na umaskini.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo Bw. Emanuel Kamba aliwatoa wasiwasi washiriki hao kwa kuwaambia kuwa TASAF ikiwa ni mfuko wa serikali wenye lengo la kusukuma mbele maendeleo ya jamii haitakuwa tayari kutumiwa na watu wenye lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa.

"TASAF itasimama imara katika kuhakikisha kwamba wanasiasa hawaivurugi daima, itasimamia malengo yake ya kusukuma maendeleo ya jamii, haitakuwa tayari kubagua makundi yoyote ya wananchi kwa misingi ya kisiasa, hivyo ndugu washiriki wa warsha hii naomba msiwe na wasiwasi juu ya suala hilo," alisema Bw. Kamba.

Vile vile wajumbe hao waliiotaka TASAF kuchukua juhudi za haraka kuinua kilimo hapa nchini kinyume na hapo malengo ya mfuko huo ambao ni kupambana na umasikini itakuwa ni ndoto.

Mbali na wajumbe kutoka katika mikoa hiyo pia walishiriki Wakuu wa wilaya na mikoa hiyo, wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Waandaaji wa warsha hiyo siku saba walikuwa ni TASAF yenyewe ambayo imeundwa na Serikali kwa msaada wa Benki ya Dunia.

 

Makasisi watakiwa wasiishiwe pumzi kuionya jamii

Na Getruda Madembwe

VIONGOZI wa dini wametakiwa kutochoka kukemea maovu yanayotokea kila siku katika jamii yetu ili duniani pawe mahali pa amani na upendo.

Hayo yalisemwa na watoto wa Jimbo Kuu la Dar es salaam katika risala yao kwenye adhimisho la Jubilei Kuu ya Watoto iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam.

Watoto hao walisema kuwa kuna mambo mengi mabaya ambayo hufanyiwa kama vile kutupwa mara baada ya kuzaliwa, baadhi ya watoto wengine kuuawa kwa mapigano ya vita na hata watoto wengine hufa kutokana na njaa.

Watoto hao walisema kuwa mbali na matatizo hayo kuna baadhi ya watoto wengine hubaki yatima kutokana na wazazi wao kufa na kubaki wenyewe bila ya msaada wowote.

"Ninyi viongozi wa kanisa msichoke kukemea maovu haya na sisi tunaahidi kusali daima ili kumwomba Mungu awashushie upendo wale wote wanaokuwa na moyo wa kikatili ili wawe na moyo wa upendo na huruma", walisisitiza watoto hao.

Watoto hao pia walimuomba Mwadhama Kardinali Pengo azidi kuwahamasisha na kuwaelimisha wazazi wao ili wawalee vizuri kama kanisa linavyoeleza walisema, mazingira tunayoishi ni ya kutatanisha sana na wengi wetu hatupati malezi mazuri toka katika familia zetu" na kuongeza kuwa "tunaomba hata Wanawake Wakatoliki Tanzaia(WAWATA) wazidi kutolea na kutufadhili katika ngazi zote".

Katika kuadhimisha Jubilei hiyo, watoto hao walitoa vyakula na nguo kwa watu wasiojiweza na kwa watoto yatima ambao huhifadhiwa katika maeneo maalum yaliyopo hapo Msimbazi.

Awali katika misa iliyoongozwa na Kardinali Pengo aliwataka watoto waendelee kupiga kelele (akiwa na maana ya kusali) bila kuchoka " nyinyi bado ni watoto hivyo muendelee kusali sala zenu hizo hizo ambazo ni fupi wa msijali kuwa sala zenu ni fupi na kuwa Mungu hatawasikia, lakini nawaambieni endeleeni kusali tu kwani Mungu huwasikia kila mumuombapo kwa kila jambo" alisema Kardinali Pengo.

 

 

Balozi wa Papa awataka Watanzania kutembelea wafungwa,makaburi

Na Josephs Sabinus

MJUMBE wa Baba Mtakatifu na Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Mhashamu Luigi Pezzuto amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuwatembelea wafungwa, wagonjwa na sehemu za makaburi ikiwa ni moja ya ishara na kanuni za Jubilei Kuu ya mwaka 2000.

Askofu Mkuu Luigi aliyasema hayo alipokuwa akitoa ujumbe wa Vatican nchini katika ibada rasmi ya uzinduzi wa Jubilei Kuu kijimbo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu la Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam hivi karibuni.Alisema katika kipindi ambacho kanisa kote duniani linaadhimisha miaka 2000 ya Ukristo, waamini hawana budi kujenga utamaduni wa kuwatembelea watu wenye mateso mbalimbali wakiwemo wafungwa na wagonjwa popote walipo.

"Sehemu hizo ni mahekalu mapya ambamo uwezo wa Mungu unakaa katika matendo yenye faida na hata katika udhaifu wa kibinadamu, ni muhimu pia kutembelea makanisa yetu makuu, makanisa ya maparokia katika vituo vyetu vya hija na katika makanisa yetu madogo ya kimisionari" alisema Balozi huyo wa Papa na kuongeza.

"Tukiwa na moyo huu, twendeni kutembelea sehemu za mateseko;hospitali, magereza na hata kwa watu binafsi wanaougua katika familia zao" "..Twendeni pia kutembelea sehemu ambazo wamemaliza safari yao ya hapa duniani na sasa wapo katika ardhi ya milele".

Alifafanua kuwa kwa Kanisa Katoliki kupita lango Kuu hakumaanishi kupita kimwili bali ni hatua ya kutoka kwenye dhambi kuelekea neema ya Mungu.

Wakati huo huo: Akihubiri katika ibada hiyo iliyofanyika jioni, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo amewahimiza Wakatoliki kutunza miti na mazingira ikiwa ni ishara ya kumheshimu Mungu kwa kuumba miti iliyotengeneza msalaba na kuwa Wokovu wa wanadamu.

"Jubilei ni mwaliko kwetu sisi watu wote kutunza, kuthamini, kuheshimu mazingira ambayo kutokana na Mungu alivyoyaumba, kulipatikana na mti wa msalaba ukawa ni wokovu wetu...." Alisema Kardinali Pengo.

Pengo alifafanua kuwa maandamano ya Msalaba ni ishara kuwa Wakatoliki wako tayari kupokea mateso ili kuleta ushindi wa msalaba katika ulimwengu wa karne na milenia mpya tuliyoanza.

"Mwanadamu asipokuwa tayari kupokea mateso kwa ajili ya wengine na kutaka anasa hata kwa hasara ya wengine, hakuna wokovu" alisema.

Siku hiyo Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam lilifanya maandamano ya Msalaba wa Jubilei baada ya kubarikiwa toka katika kanisa la mtakatifu Petro (Osterbay) hadi kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam.

 

 

Utamaduni wa Mwafrika kutukuzwa kwa michoro

Na Mwandishi Maalum

MSANII Charles Ndege, Machi mwaka huu anatarajiwa kuzindua vitabu viwili vinavyoonesha michoro mbali mbali ya utamaduni wa Kiafrika.

Kwa mujibu wa Mratibu wa uzinduzi huo Padre Joseph Healey, wa Shirika la Maryknoll, uzinduzi huo utafanyika Machi 9, kwenye jengo la Makumbusho ya Taifa, Mtaa wa Shaaban Robert, jijini.

Vitabu vitakavyozinduliwa ni, "Were you there: Stations of the Cross na The Clever Young Man and the Monster."

Katika taarifa yake Padre Healey amesema katika maonesho hayo, vitabu vingine ambavyo Bw. Charles Ndege ametumia michoro yake vitauzwa.

Vitabu hivyo ni "towards An African Native Theology, I have seen your tears, Kugundua mbegu za Injili (kitabu cha pili) na Hekima ya Kisukuma na ya lugha mbali mbali juu ya Familia na Ndoa.

Pia kadi mbali mbali zinazoonesha utamaduni wa Mwafrika zitauzwa katika maonesho hayo ambayo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dk Deogratius Maro Mwita, ambaye ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na Mbunge wa Serengeti.

Charles Ndege ni msanii mwenye kipaji kikubwa cha uchoraji, mwenyeji wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

 

 

Msianze Milenia kwa pupa

Na Neema Dawson

VIJANA wametahadharishwa kutoiingia karne mpya kwa pupa kwa kujihusisha na maovu kwa madai ya kwenda na wakati na badala yake wawe chumvi na mwangaza kwa matendo yao mema katika kipindi hiki Kanisa linapoanza mwaka huu Mtakatifu wa 2000.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na mipango wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Msimbazi Centre, Padri Benedict Shayo alipokuwa akiwafundisha vijana katika mafunzo ya kujiandaa na hija yaliyofanyika Msimbazi Center jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Hija hiyo ilifanyika Januari mosi mwaka huu huko Pugu, Padri Shayo aliwaelezea vijana kuwa wanatakiwa kuwa mstari wa mbele si kwa mambo ya kanisa tu, bali pia katika jamii nzima inayowazunguka na kujiepusha na mambo maouvu kwa kigezo kuwa wanayoyafanya yanaenda na ujana hali ambayo ni utovu wa nidhamu na kwamba hali hiyo inaweza kuhatarisha maisha y ao kimwili na kiroho na hata kuiangamiza jamii.

Alifafanua kuwa vijana wanatakiwa kujiepusha na uchoyo, ubahili wa kujilimbikizia kwa kushindwa kuwasaidia wasio na uwezo, hasira ambazo zinaweza kusababisha mauaji, uvivu ambao utawapelekea wengu kujiingiza katika wizi na mikusanyiko isiyo ya lazima ambayo itawashawishi kujiingiza katika vitendo viovu ambavyo ni hatari.

Aidha aliwashauri vijana kujiheshimu na kupenda kujiendeleza kwa kujisomea ili kuweza kuboresha maisha yao waliyonayo kwani Elimu haina mwisho.

"Kumekuwa na tabia ambazo nyingi zinafanywa na vijana wengi hali ambayo wengi wao wanasema ni kuweka kumbukumbu sehemu fulani na kujitakia sifa zisizo za lazima. Hali hii inatia aibu kwa jamii, lazima vijana kuwa makini na mjiepushe na vitendo viovu kwa ajili ya kujipatia umaarufu. "Alisema Padre Shayo.

alikemea tabia ya baadhi ya vijana wenye upotofu wa kimaadili kukwepa majukumu ya kifamilia kwa kusingizia kwenda kanisani na badala ya kufanya hivyo wanaporuhusiwa, hutumia muda huo kujishughulisha na mambo mengine yanayokwenda kinyume na maadili ya Kanisa na jamii kwa ujumla na akasema vijana Wakristo hawana budi kuepukana na tabia hiyo.

Salamu za Kanisa kwa Waislamu

Marafiki wapendwa Waislamu,

1. Mwaka huu mtakuwa mnasheherekea Iddi el Fitr, siku chache baada ya Wakristo kuwa wameadhimisha kuzaliwa kwa Yesu, tukio ambalo ni kitovu cha imani ya Kikristo. Mwaka 2000 unachukua umuhimu wa pekee kwani tutakuwa tunasherekea kumbukumbu ya 2000 ya kuzaliwa Yesu. Hii ni sherehe ya Kikristo, lakini tunapenda ninyi muhusiane nayo. Ndio maana napenda kushirikishana nanyi tafakari fulani mintarafu umuhimu wa Yesu.

2. Kwa Ukristo,Yesu ni Neno la Mungu aliyemwilika, alizaliwa na Bikira. Ni nabii, lakini zaidi ya nabii. Kama Papa Yohane Paulo wa II ni Neno la Mungu aliyemwilika, aliyezaliwa na Bikira ni Nabii, lakini zaidi ya nabii kama Papa Yohane Paulo wa pili alivyotangaza wakati wa mkutano wake na vijana wa Kiislam huko Casablanca, Moroco tarehe 19.8.1985. "Utii unatuhitaji pia tutambue na kuheshimu tofauti zetu. Suala dhahiri la msingi sana ni mtazamo ambao tunao juu ya nafsi na kazi za Yesu wa Nazareti. Mnafahamu kwamba, kwa Wakristo huyu Yesu anawasababishia wao kuingia katika ufahamu wa ndani kabisa wa fumbo la Mungu na katika jumuiya ya wana kwa zawadi zake hivyo yeye wanamtambua na kumtangaza kuwa ni Bwana na Mwokozi. Njia hii ya kumfahamu Yesu kwa namna yoyote haingilii imani ya Mungu mmoja ya Wakristo. Kwa kweli kiri ya imani ya Kikristo huanza :"Nasadiki kwa Mungu Mmoja, muumba wa mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana". Kulinganga na muono wa Kikristo, u-moja wa Mungu hauishiwi katika utengwa, lakini hasa katika jumuiya ya uhai na upendo: hii ni fumbo lisilopenyeka la Utatu Mtakatifu.

3. Juu ya Yesu, kama katika maeneo mengine, tunaitwa Wakristo na Waislam kufahamu na kuheshimu imani ya kidini ya mwingine, kutambua yale ambayo yanatutenganisha sisi na yale yanayotufanya tofauti. Kufahamu na kuheshimiana imani hizi haimaanishi kiulazima kushirikishana imani zenyewe. Kuweza kuzizungumzia kiukweli na kwa heshima hufanya sehemu ya njia tupaswayo kuishi kama watu wenye imani. Je haiwezekani ujumbe wa kijamii na wa kiroho wa Yesu ukachukuliwa kuwa hujenga urithi wetu pamoja?.

4. Tunafikiria kwamba watu wote, lakini wa pekee Waislam, wanaweza kushirikiana pamoja nasi vitathaminiwa tulivyopokea toka kwa Yesu: utii mkamilifu kwa mapenzi ya Mungu, ushuhuda upewao ukweli, unyenyekevu katika tabia, mtu kutawala mazungumzo yake, haki katika maisha, huruma ioneshwayo katika matendo, upendo kwa wote, msamaha kwa makosa uliyotendewa, kudumisha amani kati ya watu wote waume kwa wake. Yesu ni mtu wa kuteseka na pia mtu wa matumaini. Kama sisi, lakini hata zaidi yetu, amekuwa mnyonge, maskini, mfedheheshwa, mfanyakazi, aliyeteseka (tazama hotuba ya Papa Paulo wa VI Manila 29.11. 1970). Je, si Yesu huyu ni mfano na ujumbe unaodumu kwa wanadamu?

5. Katika wakati wa kuingia milenia mpya, sisi Wakristo na Waislamu, pamoja na wafuasi wa dini nyingine na watu wote waume kwa wake wenye mapenzi mema,wote tuna kitu cha kupokea kutoka kwa ujumbe wa Yesu: Ujumbe wa huruma na msamaha, wa ukarimu na undugu, wa haki na amani.

6. Ni katika moyo huu ninayo furaha kuwaandikia ninyi matashi yangu mema kwa ajili ya sherehe ya furaha na maisha ya amani na utulivu.

Kardinal Francis Arinze

Rais

BARAZA LA KIPAPA LA MAZUNGUMZANO YA KIDINI.

VATICAN