Muujiza wa Karne watokea Shinyanga

lMlemavu apona baada ya kugusa msalaba

Na Leocardia Moswery

MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Marietha Gregory, wa Parokia Katoliki ya Ilumya, mkoani Shinyanga, amepona ulemavu baada ya kugusa Msalaba wa Jubilei kuu uliozinuduliwa na Askofu Aloysius Balina, wa jimbo la Shinyanga.

Marieta, ambaye ni muumini wa Kanisa Katoliki wa parokia ya Ilumya, wilayani Magu, alishika msalaba huo na kufanikiwa kupona mikono yake iliyokuwa imepooza kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Paroko wa Parokia ya Ilumya, Padre Emanuel Makolo, tukio hilo lilitokea majira ya jioni katika parokia hiyo wakati msalaba huo uliokuwa ukizungushwa jimboni ukitokea Kanisa Kuu la Mama wa Huruma- Bikira Maria ambako safari ya msalaba ilianzia.

Padre Makolo, ameliambia gazeti hili kuwa Marietha, alikuwa amepooza kwa muda mrefu na alikuwa hawezi kujivisha hata nguo zake isipokuwa kwa msaada wa watu wengine kutokana na mikono yake kupooza na kulemaa kabisa.

Alisema amemfahamu Marietha kwa miaka mingi kama mlemavu, na kwamba tukio hilo lililotokea Desemba 26, mwaka huu liliwashangaza watu wengi walioshuhudia.

Alieleza kuwa baada ya msalaba kufika katika parokia ya Ilumya, Mariettha, alijikokota akapenya katikati ya watu na kuugusa kisha akasikika akipiga kelele za furaha na kurukaruka huku akionekana mzima kwa kunyoosha mikono yake juu.

 

HARAKATI ZA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

CUF yabeza kukamatwa Waziri wa awamu ya Mwinyi

lYadai ni maandalizi ya kampeni za Uchaguzi mkuu, hakuna udhati

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wananchi-CUF kimesema kinapongeza hatua ya Serikali ya Awamu ya Tatu kuwafikisha mahakamani aliyekuwa Waziri wa Ujenzi katika Awamu ya pili Bw. Nalaila Kiula, kwa tuhuma za kula rushwa.

Lakini chama hicho kimedai kuwa CCM haijadhamiria kwa dhati kupambana na walaji na watoaji rushwa bali hatua hiyo ni hila tu ya kupalilia kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao.

Akiongoea na gazeti hili, mwishoni mwa wiki Msemaji mmoja wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Bw. Maole Kuchilingulo, endapo utamaduni wa kuwapeleka mahakamani wale wote wanaotuhumiwa kwa rushwa utadumishwa, ili mradi tu kusiwe na mashinikizo ya kisiasa, mafanikio makubwa yanaweza kupatikana.

Alisema ni vema watuhumiwa hao wawe wanafikishwa mahakamani kwani hapo haki itatendeka, kwa maana kwamba wakiwa na hatia wataadhibiwa na wasipopatikana na hatia wataachiwa huru pia.

Hata hivyo, Msemaji huyo wa CUF ambaye pia ni Afisa Utawala wa Makao Makuu ya chama hicho, alisema haamini kwamba kweli hatua iliyochukuliwa na taasisi za kuzuia rushwa dhidi ya akina Kiula, inamaanisha kwamba sasa hata vigogo watabanwa kuhusiana na masuala ya rushwa.

Alisema kuwa kupelekwa kwa Waziri wa zamani wa Ujenzi Bw. Kiula na Katibu Mkuu wake Mkuu Dk. Mlingwa, ingawa hasema wana hatia au hawana hatia, kwa wakati huu ikiwa imebaki miezi kumi kabla ya Uchaguzi Mkuu, ni mbinu tu ya CCM na serikali yake kuandaa hoja za Uchaguzi Mkuu ujao kwamba wana mapambano dhidi ya rushwa.

Kiongozi huyo alihoji kwa kusema kuwa tuhuma za akina Kiula ni za tangu mwaka 1992, iweje leo hii ndio suala linakwenda mahakamani?

Isitoshe, alidai kuwa Kiula ni miongoni mwa viongozi wengi ( baadhi wako madarakani) waliokuwa wametajwa na Tume ya Warioba kuzingirwa na "shombo" la rushwa, lakini hawajaguswa, na badala yake wamekabwa ambao waliondoka madarakani miaka karibu mitano iliyopita.

Bw. Kuchilingulo, amesema angetegemea kuona mlolongo wa vigogo, hasa walioko madarakani wakitinga mahakamani kuhisiana na rushwa kwani kufikia mahali ambapo Tanzania ni moja ya nchi tano zinazoongoza kwa rushwa duniani, haamini kwamba wanaoweza kunaswa ni watu wadogo wadogo na viongozi wa serikali zilizopita. "Tunao wala rushwa wengi mno serikalini ila tu udhati wa kupambana nao haujakuwepo," alidai na kuendelea kueleza kwamba kwa imani yake karibu mfumo mzima wa utawala hapa nchini umeathiriwa na rushwa hivyo, hali ya kuoneana aibu isipoondolewa rushwa itaendelea kushamiri.

Alipoulizwa iwapo CUF ina mchango gani katika kuisaidia Serikali katika vita dhidi ya rushwa, alisema kazi ya chama chao ni kuishauri Serikali iondoe mambo yanayochochea rushwa ikiwa ni pamoja na dhuluma, mishahara midogo na umaskini, lakini kwa bahati mbaya Serikali haina utamaduni wa kuheshimu ushauri wa wapianzani.

Alitoa mfano wa hoja za upinzani zinazotolewa bungeni ambazo baadhi yake alisema ni manufaa makubwa kwa wananchi na taifa, lakini zinapokuwa zimetolewa na mpinzani hupingwa na wana-CCM kwa ushabiki wa kisiasa.

Wiki iliyopita Taasisi ya kuzuia Rushwa nchini iliwafikisha mahakamani aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati wa Utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Nalaila Kiula pamoja na maafisa wake kadhaa kwa tuhuma za kujitajirisha kibinafsi kwa kutumia nafasi walizokabidhiwa na umma.

Kadhalika Chama cha CUF kimesema hakikufurahishwa na tukio la hivi karibuni la kulipuliwa kwa bomu kituo kimoja cha kuuzia bia huko Zanzibar, kwani ipo haja kubwa ya kuheshimu na kulinda tunu za amani na kuvumiliana zilizojengeka nchini kwa muda mrefu.

Hata hivyo akasema njia za kuepusha matukio kama hayo si mabavu bali ni kuhakikisha watu wanatendewa haki, kwani mtu anaweza kuudhiwa na jambo jingine na akaenda kutolea hasira zake pengine na katika jambo hata lisilohusiana.

Wananchi wamshangaa Waziri Yona kumpinga Rais

Na Neema Dawson

HUKU kukiwa na taarifa kwamba amesusa ofisi kutokana na kutofautiana na rais, baadhi ya wananchi wameshtushwa na agizo lililotolewa na Waziri wa Fedha Bw. Daniel Yona, kuiagiza Mamlaka ya Mapato nchini kuzitoza kodi taasisi za dini kinyume na tamko alilolitoa Rais Mkapa hivi karibuni kuwa taasisi za dini zitaendelea kusamehewa kodi.

Baadhi ya wanachi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema wameshitushwa na agizo hilo la Waziri kwani litasababisha kuondoka kwa unafuu wa gharama za huduma mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na taasisi za kidini kwa unafuu zaidi kuliko zile za serikali au watu binafsi.

Mmoja wa wananchi hao Bw. Efrahim Rwambano, alisema kuzifutia misamaha ya kodi taasisi hizi ni kuiangamiza jamii yenye maisha duni na hali hiyo itasababisha hospitali na shule zinazomilikiwa na vikundi mbalimbali vya dini zitoze gharama kubwa.

"Ni kweli huduma za afya na shule za kidini zinatolewa kama msaada tu maana ni za gharama nafuu zaidi na karibu kila mwananchi anaweza kuzimudu na ndizo kimbilio letu na kama zitatozwa kodi, ipo hatari ya kuongezeka kwa idadi ya wasiokwenda shule na vifohata watu kufa ovyo kutokana na ukosefu wa pesa za matibabu kwa jamii nyingi", alisema Bw.Rwambano.

Naye Mganga mmoja wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke Bi.Victima Munishi, alisema kabla Waziri Yona hajapitisha agizo lake alipaswa kuchunguza na kujua umuhimu mkubwa wa taasisi za dini uliopo katika utoaji wa huduma za jamii kwani ni taasisi hizo ambazo zimekuwa zikitoa misaada kwa wasiojiweza na akasema endapo misamaha hiyo ya kodi itaondolewa, basi mambo yatakuwa magumu kwa jamii iliyoishi kwa kuzitegemea taasisi hizo.

Alitoa wito kwa serikali kutoa maamuzi yake ikizingatia kwanza hali ya watu na madhara yanayoweza kuikumba jamii endapo agizo lake litatekelezwa bila umakini kutokana na kuangalia maslahi ya upande mmoja tu na kutoa amri.

Mwananchi mwingine aliyekataa kutaja jina lake gazetini alisema ameshangazwa na Waziri Yona kupinga kauli ya Rais wa nchi juu ya kuzipa misamaha ya kodi taasisi za kidini hapa nchini hali baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa kodi hizo hawafuatiliwi ingawa wanafahamika.

Wakati sakata hilo la kutangaza kuzitoza kodi taasisi za dini kuna taarifa kwamba kwa zaidi ya wiki mbili sasa Waziri Yona amekuwa haonekani ofisini kwake kiasi kwamba baadhi ya watu wananong'ona kwamba amesusa ofisi yake kwa 'kupishana' na Rais. Hata hivyo Yona alikaririwa na gazeti moja mwishoni mwa wiki akisema kuwa madai hayo ni uzushi.

Kunguru, Nyuki washiriki maandamano ya Msalaba

lWaandamaji wasema ni baraka

Na Josephs Sabinus

KATIKA hali iliyoelezwa kuwa ni muujiza wenye baraka, Kunguru na Nyuki wameshiriki maandamano ya Msalaba wa Jubilei Kuu na kuwatia kiwewe waandamaji waliokuwa wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Pengo akishirikiana na Mjumbe wa Baba Mtakatifu na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Luigi Pezzuto.

Tukio hilo la kufungia karne ya ishirini na Milenia ya pili lilitokea Desemba 25 mwaka jana wakati waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam walipoungana na Wakatoliki kote duniani kuandamana huku wameubeba msalaba maalum wa Jubilei Kuu ya mwaka 2000.

Msalaba huo katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam ulibarikiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo katika Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Petro (Osterbay) yalikoanzia maandamano na kuishia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu ambapo Kardinali Pengo alizindua rasmi Mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya Ukristo. Baada ya kupigwa mbiu ya Jubilei, Nyuki waliingilia maandamano katika makutano ya Ocean Road na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi wakati maelfu ya waandamaji wa Parokia ya Upanga walipokuwa wakijiunga na wenzao na hivyo kuzua kizaazaa kwa waandamaji wa Parokia ya Hananasif waliokuwa wametangulia wale wa Mtakatifu Petro (Osterbay).

Hali hiyo iliwapa kazi ya ziada askari polisi waliokuwa wakilinda Usalama na kuwafanya wawazuie waandamanaji kuvuka barabara hovyo wakikwepa nyuki.

Katika kujihami waandamaji walikuwa wakijipeperusha matawi ya miti na nguo zao na baadhi ya askari polisi walionekana wakikwepa eneo hilo la nyuki. Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa na nyuki hao.

Muda mfupi baadaye, makundi ya Kunguru yalijitokeza toka katika miti na kutanda angani wakienda sambamba na maandamano hayo huku wakitoa sauti kama za ishara ya ushangiliaji.

Baadhi ya waandamaji walioulizwa na gazeti hili kuwa kitendo cha Nyuki na Kunguru kushiriki maandamano hayo kwa takribani dakika kumi hivi walisema hiyo ni baraka za Mungu.

Wakiunga mkono kauli hiyo katika mazungumzo tofauti wafanyakazi wa huduma ya kwanza waliokuwa na gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) la Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili walisema hadi wanaondoka hakuna mtu yeyote aliyedhurika.

"Hakuna mtu yeyote aliyedhurika kwa namna yoyote tangu kule Osterbay hadi hapa, (St. Joseph) hatujapata mgonjwa yeyote. Hizi ni heri na Baraka za Krisimasi," alisema mmoja wa wahudumu watatu wakiwa ndani ya gari hilo dakika chake kabla ya kuondoka.

Uchunguzi zaidi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa siku hiyo ya Krismasi watu wengi hawakuwa na nguo wala viatu vipya kama ilivyokuwa katika sherehe ya miaka ya nyuma kutokana na hali ngumu ya kipesa.

WAKATI HUO HUO: Kardninali Pengo na Balozi wa Papa nchini siku hiyo walipanda miti miwili katika bustani eneo lilipo katika pango la Bikira Maria katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu kama kumbukumbu ya Jubilei Kuu.

Wachumba waonywa dhidi ya wanaovaa ‘vinyago’

Na Getruda Madembwe

WANAUME na Wanawake wenye tabia ya kujifanya wakarimu na wema kinyume na tabia zao halisi wakati wa uchumba wamefananishwa na jambazi anayevalia kinyago kwa nia ya kuficha sura yake halisi.

Hayo yalisemwa na Mwinjilisti Ruben Ng’wala, wa Kanisa la African Inland Church (AIC) la Magomeni jijini Dar Es Salaam wakati wa ibada ya ndoa iliyofanyika hivi karibuni kanisani hapo.

Mwinjilisti Ng’wala alisema mwanamke au mwanaume kila mmoja ana wajibu wa kumpenda mwenzake na kujiweka wazi kwa dhati tangu mwanzo wa mahusiano yao na sio kumpenda kwa kujifanya mwema kwa malengo ya ndoa na baadaye kubadilika kitabia, maana ndoa za namna hiyo hazipati baraka za Mungu.

"Wajibu wa mume ni kumpenda mke na mke kumtii mume kwa mapenzi ya kweli lakini ndoa za kudaganyana kitabia kamwe hazibarikiwi" Alisisitiza.

Aliwataka wanandoa kushirikiana katika mambo mbalimbali ukiwemo ushauri bila hila kwa yeyote. Akisisitiza juu ya kauli yake, Mwinjilisti Ng’wala alisema, " katika ndoa nyingi kila mtu anatenda mambo kwa kujiamulia mwenyewe bila kushirikiana; Ukimwondoa mke wako katika ushauri wako unakuwa umemtenga. Mke anapaswa kujua mambo yako yote wala hakuna haja ya kumficha kitu maana mmekwisha kuwa kiungo kimoja."

Mwinjilisto huyo alikemea pia tabia ya baadhi ya wanandoa kutowapa nafasi wazazi kutoa mawazo yao katika kusaidia kutatua migogoro ndani ya ndoa zao.

"Wengine hata kuombana msamaha huambizana: nenda kwanza ukawaambie wazazi; wakikubali, sawa." Alieleza Mwinjilisti na kuilaani vikali tabia hiyo mbaya ya kuwa ya kuweka urasimu katika msamaha.

Profesa asema Teknolojia ya Kompyuta haijatumiwa vizuri nchini

Na Dalphina Rubyema

IMEELEZWA kuwa licha ya viongozi mbalimbali nchini kusikika wakiimba wimbo wa kuingia karne ya Sayansi na Teknolojia ,Taifa limekuwa likitumia Kompyuta kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na uwezo wa mashine hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni Jijini Dar-Es-Salaam na Mrataibu wa kijiji cha Sayansi na Teknolojia Profesa Leonard Shayo wakati alipokuwa akizungumzia progaramu mpya kwa tiba kutumia kompyuta iliyobuniwa na kijiji hicho.

Profesa Shayo alilinganisha uwezo unaoelekezwa kwa kompyuta kutoka kwa Watanzania walio wengi kuwa ni sawa na ule wa lori la tani hamsini kubeba mkungu mmoja wa ndizi toka toka Nairobi hadi Dar-Es-Salaam.

"Kwa kweli ni jambo la kutia uchungu kuwa karne ya ya ishirini ilikuwa ni ya kompyuta na Intrenet lakini mashirika mengi hapa Tanzania yamekuwa bado yakituimia mafaili ya karatasi hata katika hospitali ambapo muda na uadilifu ni vigezo muhimu katika kuamua vifo ama uhai wa mwanadamu,Watanzania wameipa uwezo mdogo sana ni sawa na kubeba mkungu mmoja wa ndizi kwenye lori la tani hamsini toka Nairobi hadi Dar-Es-Salaam"alisema.

Kutokana na hali hiyo Profesa Shayo alisema kuwa Tanzania itaingia katika karne ya ishirini na moja kama watazamaji wa Sayansi na Teknolojia na kama hatua za haraka hazitachukuliwa mapema kuna uwezekano wa Taifa kutokweka kabla ya karne hiyo kumalizika.

Profesa huyo atajisifu kwa kusema kuwa Kijiji chake cha Sayansi na Teknojia kimeitumia kompyuta ipasavyo na yeye binafsi kwa niaba ya kijiji hicho amebuni utaalam wa programu ya kutumia kompyuta hospitalini itakayo wasaidia madaktari kuwa waadilifu zaidi katika kazi zao.

"Utaalam huu pia unaweza kutumiwa na watu binafsi kutambua magonjwa pamoja na dawa kwa magonjwa yote yanayojidhihirisha kwa dalili zake"alisema.

Akitaja sifa za programu hiyo inayojulikana kama IVST-ICT Hospital Expert System,alisema daktari anayetumia programu hiyo kwanza anapaswa kutafuta faili la mgonjwa katika kompyuta linaloonesha historia ya matibabu ya mgonjwa.

"Iwapo programu hiyo itapewa dalili za magonjwa yanayomkabili mgonjwa basi kopyuta itaweza kutafuta na kupendekeza vipimo halisi vya kutibu magonjwa yanayopatikana ,kuchapisha karatasi yenye dawa na kuweka takwimu za kila dakika za madawa yaliyopo hospitalini.

Profesa Shayo alisema kuwa programu ya ubunifu wake ameitengeneza kwa kuongozwa na kitabu cha mwongozo wa Madaktari nchini kinachojulikana kama ‘Standard Treatment Guidelines (STD) and The National Essential Drug List For Tanzania (NEDLIT).

Pengo atamani silaha zichomwe moto kutibu mchafuko wa amani

Na Josephs Sabinus

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema ili amani ya kweli ipatikane duniani, i ilifaa silaha zote kugeuzwa kuni na kuchomwa moto kwani si vitu vinavyoweza kuleta amani.

Kardinali Pengo alitoa kauli hiyo alipokuwa akihubiri katika usiku wa mkesha wa Sikukuu ya Krismasi kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu la Jijini Dar Es Salaam.

Alisema dunia nzima hivi sasa ipo katika hali ya kuhuzunisha na kufedhehesha kutokana na vita, mauaji, unyanyasaji na magonjwa mbalimbali ya ajabu na kuongeza kuwa maafa na kwamba vita vinavyotokea katika ulimwengu huu wakati tunaingia katika Karne ya 21 na milenia ya tatu, vinatokana na wanadamu kudhani kipotofu kuwa vita ni njia ya kuwaletea suluhisho katika matatizo na migogoro ya maisha yao.

"Eti bado tunapopatwa na shida tunaanza kufikiria nani ana nguvu zaidi...ndio maana majirani zetu na hata ulimwengu mzima umekuwa wa vita na mapambano. Tunatafuta ushindi wa silaha tunazozitengeneza sisi wanadamu na kufikiri eti tutapata amani kutokana na nguvu yetu;

sijui kwanini hatukumbuki kuwa bunduki na silaha nyingine si vitu vinavyoweza kuleta amani duniani," alisema.

Akizidi kupinga dhana hiyo na kuwataka wanadamu kudumisha amani, Kardinali Pengo alisema, "Amani ya kweli, ustawi na furaha ya wanadamu itakuwepo tu, watu watakapoamua kuchukua silaha zao za vita, mavazi na vitu vyote vinavyofanikisha vita wakavigeuza kuni, wakavitupa ndani ya moto wakavichoma na kumuachia Mungu atengeneze mambo".

Alisema hivi sasa ulimwengu unapoingia katika Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili na makanisa kote ulimwenguni wanaomba Yesu Kristo mwenye mamlaka pekee mabegani kwake afanikishe shughuli zote za utengenezaji wa silaha zitumike kwa ajili ya utengenezaji za zana bora za maendeleo ya watu zisizohusiana na vita.

"...Kristo aliyezaliwa mwenye mamlaka mabegani mwake afanikishe amani badala ya watu kugeuza silaha kuwa ni chombo cha maendeleo. Badala ya mikuki, watengeneze mundu ili kuandalia mashamba. Badala ya silaha nyingine watengeneze majembe walime . Waache hayo ya kuuana na kupigana; hayaleti faida," alisema Pengo.

Kwa kukosa kiti kwenye basi,Mwanajeshi ampiga dereva

Na Mwandishi Wetu

INGAWA Serikali imekuwa ikikemea vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya askari kwa raia ikiwa ni pamoja na kuwapiga hovyo, askari mmoja wa JWTZ amemshambulia kwa kipigo dereva wa daladala kwa madai kuwa amekataa kusimamisha gari na kumfanya akose kiti.

Tukio hilo linalozidi kulidhalilisha jeshi hilo lilitokea Jumamosi iliyopita saa 8:10 mchana baada ya askari huyo kutaka kumsimamisha dereva wa ‘kipanya’ hicho chenye namba TZN 7985 kilichokuwa kikitoka Posta kuelekea Kawe katikati ya barabara bila kuzingatia athari ambazo zingeweza kutokea kwa kusimama ghafla.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamekieleza kitendo hicho kama unnyanyasaji uliokithiri na wakashauri kuwa ni vema askari wa majeshi yote wakafundishwa kanuni za usalama barabarani ili kupunguza adha wanazowafanyia madereva na makondakta.

Walisema baada ya kumuona askari huyo, dereva aliegesha gari kituoni na ndipo askari huyo mwenye cheo cha Koplo alipopanda na kuanza kumpiga makofi na kumvua kofia yake ya baraghashia kisha akaitupa katikati ya barabara.Mwandishi wa habari hizi alishuhudia askari huyo akimuhoji kwa ukali dereva kwa jeuri "kwa nini nimekusimamisha tangu kule umekataa kusimama;ina maana hukuniona?" Dereva huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja alijitetea akisema "nilikuona lakini nilikuwa katikati ya barabara kwa mwendo mkali."

Hali hiyo ya kupigwa ilimfanya dereva huyo aendeshe kwa kasi huku gari ikiyumbayumba na kuwafanya abiria waanze kuhaha wakihofia usalama wao.

Maalbino waangua kilio baada ya kupewa masaada wa pakiti moja ya sabuni Foma

lWaliotoka Pwani wakosa nauli.

Na Neema Dawson

BAADHI ya maalbino wa mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam, wameangua kilio wakihaha kutafuta nauli huku wengine wakiwa na watoto migongoni baada ya kupewa msaada wa pakiti moja ya sabuni foma kinyume na matarajio

Maalbino hao walipewa taarifa na Mwenyekiti wao kitaifa Bw. Lameck Ally ili wakutane ilipo shule ya msingi Makurumla eneo la Magomeni jijini Dar Es Salaam ili wapewe misaada mbalimbali ikiwemo miwani ya jua, kofia, miamvuli pamoja na dawa.

Kilichowashangaza na kuwafanya baadhi yao kuangua kilio baada ya kusota juani kwa masaa kadhaa ni kitendo cha kupewa pakiti moja tu ya sabuni foma licha ya kuwa awali waliambiwa kuwa watumie nauli zao ambazo wangerudishiwa lakini baada ya kufika kituoni Dar Es Salaam, hali ilikuwa kinyume.

Kufuatia ahadi hiyo ya kurudishiwa nauli, wengi wao kutoka mkoani Pwani walidai wamelazimika kukopa na hata kuziacha familia zao katika hali mbaya.

Hali ya kupewa msaada wa kiasi hicho cha sabuni ilipelekea kuibuka kizaazaa huku maalbino hao wakihaha kutafuta namna ya kuwawezesha kurudi makwao.

Hali hiyo iliyojitokeza Jumanne iliyopita iliwapelekea baadhi yao kudai wana wasi wasi kuwa huenda uongozi wa maalbino hutumia chama hicho kujinufaisha wenyewe.

"Tuna wasiwasi huenda misaada ya makanisa huwa inatoka ‘mnatia ndani’ kisha mnakaa kudanganya watu bure," alisikika akisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Amina Salumu Kisamvu.

Hata hivyo akiomba radhi kwa maalbino hao kufuatia usumbufu uliowakumba, Mwenyekiti huyo alisema licha ya juhudi zake kuzunguka huku na huko kutafuta misaada katika makanisa mbalimbali, aliambulia boksi moja la sabuni hiyo, shati moja, suruali moja, jozi moja ya viatu pamoja na pesa taslimu shilingi 10,000/= toka Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenge.

Alidai kuwa makanisa mengine yaliahidi kutoa msaada huo mwakani. Aliyataja baadhi ya makanisa aliyofika kuomba msaada huo kuwa ni pamoja na SDA, Lutherani makanisa ya Lutherani ya Kijitonyama, Magomeni Mviringo, Kariakoo, Anglican la Ubungo na Romani Katoliki la Manzese.

Hata hivyo hakuweza kufafanua ni vipi aliamua kutangaza kugawa misaada hiyo kabla hajapata uhakika wa upatikanaji wake na hivyo kusababisha usumbufu na hasara kwa maalbino hao.

Wachuuzi wa Kisutu walazimika kufuata mikia ya wenye mabasi

Na Dalphina Rubyema

WAFANYABIASHARA wadogo wa kituo cha Mabasi ya Kisutu Mkoani Dar-Es-Saaalam wamekubali kutekeleza agizo la serikali la kuwataka wahamishe ofisi zao kutoka katika eneo hilo kufuatia vituo mbalimbali vya magari mbalimbali yaenedayo mikoani kuhamishiwa katika kituo cha Ubungo.

Mwandishi wa habari hizi alipotembelea eneo hilo kwa siku mbili mfululizo alishuhudia baadhi ya wamiliki wa vibanda hivo vinavyohamishika wakiwa wanabomoa vibanda vyao na wengine kuvipakia kwenye magari vikiwa havijabomolewa tayari kuvihamishia sehemu nyingine.

Mfanyabiashara mmoja wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Bw.Amos Tesha ambaye naye alikuwa katika shughuli nzito na kuondoka bati kwenye kibanda chake alisema kuwa hana budi kutekeleza agizo la serikali na kuongeza kuwa kuhamishwa kwa kituo hicho cha Kisutu kumewaathiri wafanyabiashara kama yeye.

"Lazima tukubali bwana kutekeleza agizo la serikali kwani kama hao wenye kumiliki magari makubwa yaendayo mikoani wamekubali kuhama wakati wanao uwezo wa kifedha wa kuweza kuzungumza kikubwa na serikali, itakuwaje sisi ambao katika seikali ni sawa na sisimizi mmoja kwenye kundi kubwa la simba," alisema Tesha na kuongeza "Kuhamishwa kwa kituo hiki kumetuathiri sana sisi wafanyabiashara kama ambao kula yetu tulikuwa tunaipata hapa".

Hata hivyo Mfanyabiashara huyo ambaye alikataa kupigwa picha alimwambia Mwandishi wa habari hizi kuwa bado hajapanga kama atahamishia kibanda chake katika eneo la Ubungo ama la.

"Mimi bado sijaamua kuhamishia kibanda changu Ubungo ,ninachofanya ni kukibomoa na mbao na mabati yangu nitavihifadhi hadi hapo nitakapopata uamuzi"alisema Bw.Tesha mwenye mke na watoto wawili.

Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa hali katika eneo hilo la Kisutu hivi sasa imekuwa shwari,hakuna tena usumbufu wa vijana wakiwemo vibaka kuwakimbilia watu wanaopita eneo hilo na kuwapokea mizigo yao kwa nguvu kwa madai ya kukaribisha wasafiri kama ilivyokuwa awali.

Pamoja na magari yaendayo mikoani kutoonekana katika kituo hicho bado ofisi za mabasi ya Fresh ya Shamba,Dar Express,Shabaha,,Tawfiq na Takrim zinaendelea kufanya kazi ya kukata tiketi kama kawaida.

Uchunguzi kama huo pia umefanyika katika kituo cha Msimbazi na Mnazi mmoja ambapo kwa upande wa kituo cha Msimbazi imebainika kuwa baadhi ya magari yanalala katika eneo hilo na ikifika alfajiri yanahamishiwa kituo cha Ubungo tayari kwa kuanza safari za kwenda mikoani. Katika kituo cha Mnazi mmoja hali ni shwari; hakuna gari lililokuwa limeegeshwa eneo hilo.

Wakati huo huo,Wafanyabiashara ndogondogo wanaofanyia shughuli zao katikati ya jiji bado wanaendelea kufanyia biashara zao kwenye maeneo hayo baada ya kugoma kuhamia eneo la Karume walilotengewa na Tume ya Jiji.

Mwandishi wa habari hizi alipotembelea eneo hilo la Karume alikuta hakuna mfanyabiashara hata mmoja huku tayari Tume ya Jiji ilikwishatenga maeneo ya kuuzia bidhaaa mbalimbali.

Mfadhili wa CCM hakusubiri Mwaka 2000

Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA mfadhili wa kada wa Chama tawala cha CCM tawi la Mnazi Mmoja kata ya jangwani wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Yahaya Salehe Abdalah Maarufu kwa jina la "Mabenzi" amefariki dunia, imefahamika.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi wiki hii akiwa ofisini kwake Katibu wa hilo la Mnazi Mmoja Bw. Ally Sindo, alisema, Kiongozi huyo mkongwe alifariki dunia katika hospitali ya Ocean Road alikokuwa amelazwa kwa muda mfupi.

Bw. Sindo alifafanua kuwa mfadhili huyo alifariki dunia mnamo mwezi Desemba tarehe 20 mwaka huu na kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Kansa ya mguu.

Katibu huyo alisema mazishi ya kiongozi huyo yalifanyika katika makaburi ya External Ubungo wilaya ya Kinondoni na kuhudhuliwa na idadi kubwa ya waombolezaji wakiwamo viongozi na wanachama.

Alisema kiongozi huyo ambaye amekuwa akikifadhili chama hicho kwa hali na mali ikiwa ni pamoja na kuitoa nyumba yake kuendeshea shughuli za chama, ameacha wajane wawili na watoto tisa.