KUFUATIA MABADILIKO YA KATIBA:

Askofu amlilia upya Nyerere

lAsema alikuwa jasiri na mkweli

lanatamani kauli ya Rais kuhusu Zanzibar

Na Josephs Sabinus

"Nyerere alikuwa shupavu na jasiri. Akijua ukweli akapata nafasi, anausema bila kujali uso wa mtu. Si rahisi kumpata mwingine kwani binadamu wengi wanaepuka magumu, wanatoroka yanayotisha na kuwaogopa watu ambao ni tishio na wana kauli ngumu."

Ndivyo alivyosema Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Norbert Mtega, gazeti hili lilipotaka kupata maoni yake binafsi juu ya hali ya kisiasa nchini tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Oktoba 14, mwaka jana.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa juma jijini Dar Es Salaam, Askofu Mtega, alisema uzoefu wa siasa,ujuzi wa hali ya nchi na utafiti wa ukweli na misingi yake na kisha kuuelezea kwa misingi ya ukweli na uwazi kama alivyoangaziwa na Mungu, ndivyo vilivyompa Nyerere "ubavu" wa kukemea uovu wowote ndani ya chama na taifa kwa ujumla bila kuogopa wala kumuonea haya mtu yeyote anayekwenda kinyume.

Alisema anatamani sana na anawaombea viongozi wote wa Tanzania wapate karama ya namna hiyo na kuiga mfano bora wa Mwalimu.

akigusia suala la mgogoro wa Zanzibar, Askofu Mkuu huyo alisema mpaka sasa hajasikia kauli ya msingi inayozuia majibizano yasiyo ya lazima ili taifa lizidi kuimarika katika misingi bora ya upendo, amani na mshikamano wa kitaifa.

Alisema kimsingi suala la hali ya mivutano ya kisiasa ya Zanzibar halina budi kushughulikiwa pamoja kitaifa ndani ya serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema madai ya baadhi ya Wazanzibar kuwa suala hilo ni la Wazanzibari pekee na hivyo liachwe kwao wenyewe, hayana msingi na akabainisha wazi kuwa wenye mawazo hayo wana nia mbaya ya kutaka kuvunja Muungano.

"Hamu yangu ni kupata kauli ya Rais au viongozi wengine wakielezea misingi na msimamao juu ya ufumbuzi sahihi wa suala hili kwa kuwa ni la kitaifa. CCM ya Zanzibar pekee haitoshi. Kauli ya kitaifa (Muungano) ndiyo ya msingi," alisema na kuongeza,

"Hili sio suala la Wazanzibari peke yao, ni suala la Muungano na liamuliwe kimuungano. Kinyume na hivyo hao wanaotaka lizungumzwe Kizanzibari, labda wangeomba kwanza kuvunja Muungano."

Alitoa wito kwa serikali kuielimisha jamii mapema juu ya Uchaguzi Mkuu ujao ili wagombea wajulikane mapema na wapiga kura kupata fursa ya kuwachambua mapema kuona kama wanawafaa.

"Chaguzi nyingi huchafuka na kuleta mapato ya udanganyifu, wapiga kura wanapoenda kwenye masanduku ya kura wakiwa na giza na moshi- moshi juu ya masuala ya msingi.," alisema Askofu Mtega.

Kumekuwepo na mjadala mkali uliopelekea kukaa kwa Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM huko Zanzibar kwa siku nne tangu Jumapili iliyopita ili kupata uamuzi juu ya uwezekano wa kuifanyia mabadiliko Katiba .

Katika kikao hicho kilichomalizika usiku wa kuamkia Jumatano, imeamuliwa kuwa pendekezo la kutaka Katiba ya Zanzibar ibadilishwe ili pamoja na mambo mengine, imruhusu Rais kuongoza kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano, sasa lipelekwe katika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ili kutolewa maamuzi zaidi.

Wadadisi wa mambo ya kisiasa wanasema mgawanyiko ambao umekuwa ukijitokeza ndani ya vikao mbalimbali kujadili suala hilo, huenda ukawa mwanzo wa kuvunjika kwa nidhamu ndani ya chama hicho tawala ambacho kimekuwa kikiheshimika kwa msimamo juu ya masuala yake ya ndani.

Wanasema hii inatokana na kuondokewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikuwa na ubavu wa kumkemea mtu yeyote ndani ya chama na serikali na hivyo hivi sasa hakuna mtu mwingine anayeweza kumzuia Dk. Salmin, asitimize lengo lake.

 

' Wanasiasa hukwepa ushauri wa kitaalamu kwa sababu za kisiasa'

Na Pelagia Gasper

WANASIASA wengi nchini wamekuwa wakikwepa ushauri wa wataalam hata kwa mambo yanayowaathiri wananchi kwa kutetea maslahi yao ya kisiasa.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Afisa Afya Mfawidhi Kanda ya Temeke, Bw. Lucian Munna, akiongea na KIONGOZI ofisini kwake wakati alipoulizwa kwa nini maafisa afya hawashirikiani kikamilifu na watendaji wa serikali katika ukaguzi wa afya.

Alisema wanasiasa hukataa kutoa ushirikiano kwa maafisa afya ili kuepuka lawama toka kwa wapiga kura wao.

Bw. Munna, amesema maafisa afya ili kuondoa kero kwa wafanyabiashara kupaswa kushirikiana na watendaji wa serikali katika maeneo watakayokagua, lakini kutokana na viongozi hao kukwepa lawama za kisiasa, hawajihusishi katika ukaguzi huo.

Amesema uzoefu uliopo umeonyesha kwamba pale ambapo viongozi wa Serikali kuanzia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ametoa ushirikiano kwa maafisa wa afya katika ukaguzi wa magonjwa ya kuambukiza ikiwa ni pamoja milipuko ya magonjwa kama kipindupindu hutoweka.

"Kiongozi mwenye kushirikiana na wataalamu katika kusimamia vema sheria ni lazima ataonekana mbaya na mwenye kuchukiwa na wachache wasiotaka kufuata taratibu, kanuni na sheria lakini baada ya mazingira kuwa safi na kupungua magonjwa ataheshimika na anaowaongoza", alisema Bw. Munna.

Pia alisema kuwa baadhi ya malalamiko yatapungua endapo wafanyabiashara wataepuka kuvunja sheria kwa kuhakikisha maeneo wanayofanyia biashara ni safi, kupima wafanyakazi, kuweka vema ubora wa chakula ikiwa ni pamoja na masharti yote wanayopaswa kuyatekeleza kabla ya kuanza biashara zao.

Alisema, mfanyabiashara atakayekwenda kinyume na maelekezo kutoka kwa wataalam wa afya atakuwa amevunja sheria na hatua nyingine ikiwa ni pamoja na kumpeleka mahakamani zitafuata.

Bw. Munna amewataka viongozi wa serikali kushirikiana na wataalamu mbalimbali waliopo katika maeneo yao ili kukuza na kulinda afya za wananchi.

 

Wanaohubiri mafichoni usiku waonywa

Na Getruda Madembwe

WACHUNGAJI wa makanisa mbalimbali wametakiwa kuhubiri Injili waziwazi badala ya mahali palipofichika nyakati za usiku kama vinavyofanya baadhi ya vikundi vya dini vilivyoibuka hivi karibuni.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Moses Maarifa, alipokuwa akihubiri katika Kanisa hilo Usharika wa Kawe, jijini Dar es Salaam.

Alisema inashangaza mno kusikia kuwa zipo dini zinazoabudu usiku bila nguo na kwamba huo sio uhubiri wa wazi wa Injili.

Mchungaji Maarifa aliwataka watu wasijishuhudie wenyewe utakatifu, bali wawaachie wengine ndio wawashuhudie. "Eti utakuta mtu anajishuhudia mwenyewe kuwa anatenda mema au eti yeye ni mwema. Hiyo wala haitakiwi; waachie watu wengine ndio wakushuhudie ya kuwa wewe ni mwema," alisema.

Wakati huo huo: Mchungaji huyo wa KKKT amewataka waamini wa dhehebu hilo kuondokana na tabia ya kuhamahama makanisa wakitafuta imani nyingine na akasema hizo siyo taratibu alizokuwa nazo Bwana Yesu Kristo.

Alisema waumini wa dhehebu la Kilutheri wanaongoza kwa kuhamahama wanapookoka na akawashauri wanaopata mabadiliko hayo ya kiroho watulie walipo ili watu wawaige kama mfano bora. Hata hivyo hakutoa takwimu za madhehebu mengine juu ya kuhama waumini.

"Eti mtu akiokoka anahama ili akakae na wenzake waliookoka! Sasa ukihama kwenye dhehebu lako ni nani ataleta mabadiliko? Ni wewe ndiye utakayeleta mabadiliko; sasa kwa nini uhamie kwingine?" alihoji.

 

Wengi wapona baada ya kutembelewa na Msalaba

Na Charles Hililla, Shinyanga

WATU kadhaa wamerudia masakramenti na wengine kuingia dini na kuanza mafundisho ya Katekisimu ya Kikatoliki baada ya kushuhudia watu wanapona na kupata nafuu walipotembelewa na Msalaba Mtakatifu wa Jubilei Kuu ya 2000.

Hali hiyo ya watu kuingia na wengine kuimarika kiimani, imethibitishwa hivi karibuni katika parokia za Ilumya, Ng’wanangi, Chamgasa na Malili.

Kwenye parokia hizo, Msalaba Mtakatifu wa Jubilei ulikaa kwa muda wa siku 14 kila parokia ambapo waumini wa parokia hizo walifanya ibada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuombea wagonjwa.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti katika Parokia hizo, umegundua kuwa; waumini wengi waliokuwa wamezorota kiimani wamesisimka na kuwa hai kiimani. Vile vile wengi wamerudia masakramenti baada ya kufanya toba na kuwa waumini safi wa Kanisa.

Aidha baadhi yao wengine walifunga ndoa na wengine kurekebisha ndoa zao. Sakramenti zingine zilizovuta watu wengi ni Ubatizo, kitubio na Ekaristi ambapo baada ya kupata Sakramenti hizo waumini hao walijiona wapya kwa kuacha utu wao wa zamani waliokuwa wakiishi nje ya Sakramenti hizo.

Upande wa wagonjwa, msalaba Mtakatifu wa Jubilei Kuu uliwapa faraja na matumaini katika familia, vigango vya Parokia hizo. Wagonjwa wengi walipata nafuu na wengine kupona kabisa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua. Kati ya wagonjwa walioombewa kwenye ibada wakati wa ziara ya Msalaba huo wengine walikuwa na dini za asili na dini zingine ambazo siyo za Katoliki.

Katika hali isiyo ya kawaida, idadi ya watu wanaokesha na Msalaba wakati wa usiku imeongezeka sana hasa baada ya kisikia kuwa msalaba mwingine kama huo umechukuliwa na wezi huko Rulenge mwezi uliopita wengi wa wanaokesha ni pamoja na wale waliokuwa wameuguliwa na ndugu zao na sasa wamepona au kupata nafuu.Pia ushirikiano kati ya madhehebu mengine umehusika katika ulinzi pamoja na Serikali za vijiji.

Hivi sasa Msalaba huo umeanza ziara katika Parokia ya Old Maswa ambapo utakaa kwa muda wa siku 14 kabla ya kukabidhiwa kwa parokia nyingine ya Bariadi hapo Machi 8 mwaka huu. Matembezi ya Msalaba katika jimbo la Shinyanga kama yalivyo majimbo mengine hapa nchini ni mojawapo ya shamrashamra za kanisa kusherehekea Jubilei Kuu ya mwaka 2000 tangu Kristu kuja hapa duniani.

Mwaka 2000 ni mwaka wa Jubilei Kuu, Pia ni mwaka uliofadhiliwa na Bwana. Ni mwaka wa kusamehe dhambi na adhabu zake na kufanya toba. Pia ni mwaka wa kupatana kwa waliogombana na wa kuongoka mambo hayo ni ya muhimu sana kwa mwaka huu kwani ni matakatifu kama alivyoyataja Baba Mtakatifu (UMT Namba 14a) yanafaa kuendelezwa katika kipindi chote cha mwaka Mtakatifu wa 2000.

 

Mila ya Wasukuma ya 'chagulaga' yatajwa kudhalilisha wanawake

Na Leah Samike, PST Igunga

SERIKALI imeshauriwa kupiga marufuku mila ya "chagulaga" inayotumiwa kwa Wasukuma na Wanyamwezi wakati wa kutafuta mchumba kwa kuwa inawadhalilisha wanawake na kuhatarisha usalama na maendeleo ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa Mwenyekiti wa CCM (w) Bw. Mashauri Mleka, alisema mtindo huo wenye maana ya chagua unadhihirisha jamii hizo kutokana na muingiliano wa makabila tofauti na siku za nyuma.

Alisema mila hii iliyotumika awali kama kipimo cha kupendeka kwa mwanamke au mwanaume anapofika umri wa kuolewa au kuoa, iliambatana na ngoma ambapo vijana walipata fursa ya kuchagua wapenzi.

Akisimulia mila hii, Mzee huyo mkongwe alisema ngoma hiyo ilipomalizika msichana aliweza kukimbia na kufuatwa na kundi la wanaume.

Walipomfikia, mwanaume (vijana) hao waliweza kumzunguka na alipopata nafasi, msichana huweza kuangalia na hata kumchagua anayempenda huku wanaume wakiwa wamenyoosha mikono yao kuomba kuchaguliwa.

Akielezea zaidi mitindo huo, Bw Mleka alisema katika mila hii inayodhalilisha watoto wa kike na kuhatarisha, kujeruhi na hata kusababisha kifo wakati wa makimbizano kama wanyama, msichana anapokaribia nyumbani au kukutana na mzazi wake, wanaume wanamfukuza hutawanyika.

Alisema tofauti na ilivyokuwa awali, siku hizi msichana anapokuwa amechagua bado vijana wengine huendelea kumlazimisha awachague huku wakimshikashika.

Aliongeza kuwa hali hiyo wakati mwingine huchochea ubakaji na maambukizo ya magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi.

Aidha Bw. Mleka alisema awali wasichana walipotoka ngomani waliulizwa na bibi zao iwapo wamefukuzwa na kwa wanaume kama wamechaguliwa ili kuondoa hofu ya kuwepo utata wakati wa kuoa au kuolewa.

Bibi anamuuliza mtoto wa kike kama amekimbizwa na wengi na kama hakukimbizwa kabisa, wanadiriki kwenda kwa waganga" alisema.

Alisema mila hii inaathiri pia maendeleo ya uchumi kwani vijana wanatumia muda wao mwingi katika ngoma hizo na hivyo kuathiri shughuli zao kikiwemo kilimo.

"Siku hizi ngoma inachezwa tangu mwezi wa 5 hadi wa 9 hii inasababisha kudidimia kwa maendeleo na uchumi invunja hata ndoa kwa kuwa vijana wanakaa nje ya nyumba zao kwa kipindi kirefu" alisema na kuongeza,

"wengine wanadiriki kuacha hata shule ili wafuate ngoma toka kijiji hadi kijiji kingine"

 

Viboko mashuleni vitaendelea - Kapuya

Na Neema Dawson

WAZIRI Wizara ya Elimu ya Utamaduni Profesa Juma Kapuya amesema kuwa viboko mashuleni vitaendelea ili kuhakikisha kuwa nidhamu ya wanafunzi inaendelea.

Profesa Kapuya aliyasema hayo katika kongamano lililofanyika hapa jijini lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam juu ya kujadili matatizo yanayoikabili sekta ya Elimu nchini.

"Viboko mashuleni vitaendelea ili kudhibiti nidhamu mashuleni kwani wanafunzi ni wengi kuliko walimu na viboko visipotembezwa na kuwalealea wanafunzi watafikia hatua ya kuwapiga walimu wao kwa kujifanya wababe.

Viboko ni ruska mashuleni ili kurekebisha mienendo ya tabia," alisema Profesa Kapuya.

Katika kongamano hilo lililowahusisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao waliitaka Wizara ya Elimu itamke rasmi msimamo wa kuchapa viboko mashuleni.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na kampeni kubwa za kutaka watoto wasichapwe viboko kwa madai kuwa ni kinyume cha haki za binadamu, lakini viongozi wa dini nao wamekuwa wakionya kuwa kuwachapa watoto viboko kwa mujibu wa Biblia ni jambo la muhimu.

Profesa Juma Kapuya alisema kwa sasa Serikali itaendelea kuruhusu viboko mashuleni kwa vile inaonekana ndiyo nyenzo bora zaidi ya kudhibiti nidhamu wakati wakiendelea kusikiliza maoni ya wazazi kuhusiana na hali hiyo.

 

Daktari wa UNDP asema elimu ya Ukimwi nchini bado nyonge

Na Getruda Madembwe

Dk. Edger Ndyetabula wa Shirika la maendeleo ya Jamii la Umoja wa Mataifa (UNDP) amesisitiza kwamba ili kuboresha vita dhidi ya Ukimwi ni vema elimu juu ya ugonjwa huo itolewe kwa kuzingatia makundi maalum bila kuwachanganya.

Daktari huyo ameyetaja makundi hayo kama vile vijana, wanawake, watu wazima, wafanyakazi au wanafunzi alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hizi jijini alipotakiwa kueleza kwa nini licha ya kutolewa elimu juu ya Ukimwi, bado jamii inaathirika kwa maambukizo na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo hatari.

Alisema mfululizo wa elimu inayotolewa ni mdogo ukilinganisha na watu wenyewe kwani wanahitaji kuelimishwa kila wakati badala ya siku ya siku maalum tu hali inayowapa mwanya wa kujisahau na hivyo kushindwa kubadilika kitabia.

"Badala ya kufundisha suala la Ukimwi kwa jumla elimu itolewe kwa vikundi na vikundi kama vile vijana kwa vijana. Hii itasaidia kueleweka vizuri kwa suala la Ukimwi," alisema Dk.Ndyetabula.

Dk. Huyo alidai kuwa hivi sasa shirika lake linapanga mikakati zaidi ya kupambana na janga la Ukimwi na namna ya kuwasaidia wenye Ukimwi ili wapate huduma bora na kuishi kwa matumaini.

Mlaki awataka wanawake wawe mafundi seremala

Na Dalphina Rubyema

WANAWAKE kote nchini wametakiwa kufanya kazi za ufundi ukiwemo wa useremala na kuondokana na dhana kwamba kazi hizo ni kwa ajili ya wanaume peke yao.

Pendekezo hilo lilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bi. Ritha Mlaki wakati akifunga semina ya mafunzo ya Mama na Baba Lishe wa kanda ya Dar es Salaam iliyofanyika kwenye Chuo cha Ufundi Chang’ombe kilichopo wilayani Temeke.

Bi.Ritha alisema kuwa katika karne hii ya Sayansi na teknolojia wanawake hawana budi kujiunga na vyuo mbalimbali vya ufundi vilivyopo chini ya VETA ili kupata ujuzi unaohusiana na masuala ya ufundi.

"Wanawake tuna nguvu na uwezo mkubwa sana. Sasa sioni kwa nini tunafikiri kuwa kazi zetu ni unesi, ualimu na kupiga mashine tu, kwanini tusiwe mafundi makenika, seremala na mafundi umeme?" alihoji Bi. Ritha.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka akina mama na Baba waliohitimu mafunzo yao ya siku 11 kutoka katika wilaya zote tatu za mkoa wa Dar es Salaam, kuzingatia kanuni za usafi zaidi hususan katika kipindi hiki ambapo mkoa unakabiliwa na mlipuko wa kipindipindu.

Awali akisoma risala mbele ya Mkuu huyo wa wilaya, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Bi. Nantaika Maufi, alisema kuwa muda wa mafunzo uongozwe kutoka siku 11 hadi 20 ili wahusika waweze kupata ujuzi zaidi. Aliomba pia wahusika kupatiwa vitendea kazi kama vile mikokoteni na kutengewa eneo maalum kwa ajili ya kuenda shughuli zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bw. Mateso watu 76 wamehitimu mafunzo hayo, ambapo wanawake ni 58 na wanaume 18.

Balozi ataka Tanzania iige Japan

Na Mwandishi Wetu

BALOZI wa Japan nchini Tanzania Bw. Keitaro Sato, ameufananisha umuhimu wa wafanyabiashara wenye viwanda vidogo (VIBINDO) kuwa ni sawa na ule wa almasi inayohitaji kung’arishwa tayari kwa kutumiwa.

Bw. Sato aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua warsha ya siku moja aliyowajumuisha wawekezaji wadogo kutoka VIBINDO na Pride Tanzania na kufanyika katika ukumbi wa British Council hivi karibuni, jijini.

Bw. Sato aliwataka wananchi wa Tanzania kufahamu kuwa uchumi wa nchi zilizoendelea zaidi unategemea wafanyabiashara wa Viwanda vidogo.

Alitoa mfano wa nchi yake ya Japan ambapo asilimia 80 ya wakazi wa nchi hiyo ni wafanyabiashara wadogo wadogo na kati na hii inaleta nguvu na mvuto mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo.

Balozi huyo wa Japan pia amewataka wananchi wafahamu kuwa viwanda vikubwa sana vya kuzalisha bidhaa mbalimbali haviji tu mara moja bali vinaanzia kwenye viwanda vidogo vidogo.

"Mwisho wa Vita kuu ya Dunia, uchumi wa Japan ulikuwa umevunjwavunjwa kabisa; hii ilisababisha mfumuko wa bei kutokana na uchache wa chakula na bidhaa muhimu lakini serikali iliweka sekta isiyo rasmi," alisema.

Aliongeza kusema "Wakati huo nchi yetu ya Japan bidhaa zake hazikuwa na thamani kubwa katika soko la Dunia tukiitwa waigizaji lakini tulizidisha nguvu na ndiyo maana leo hii unasikia viwanda vikubwa nchini Japan kama Sony, Honda, Toyota na vingine vingi," alisema.

Alisema Taifa la Tanzania halina budi kuiga mfano wa nchi ya Japan ambayo ilifanya juhudi kubwa kabisa kujitoa muhanga ili kuondoa sifa mbaya ya viwango vya nchi yao.

"Msikate tamaa zidisheni bidii; makampuni haya makubwa katika Japan hayakuanza yakiwa makubwa bali yalianzishwa kama biashara ndogo ndogo," alisisitiza.

Madhumuni ya warsha hiyo iliyoandaliwa na VIBINDO na kudhaminiwa na umoja wa wafanyabiashara nje ya Japan (JETRO), ilikuwa ni kujenga misingi ya biashara na utawala pamoja na kuhamasisha wafanyabiashara ndogo ndogo kuwa na mtazamo mpana zaidi wa baadaye.

Wazazi wa St. Michael Sekondari wagoma kulipa ada

Na waandishi wetu

 

WAZAZI wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya St. Michael ya jijini Dar es Salaam, wamesema hawatalipa ada ya mwaka huu kwa kile walichokiita mazingira ya ubabaishaji katika utoaji wa elimu shuleni hapo.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti juma lililopita, walisema hawako tayari kulipa ada wakati watoto wao wanasoma katika mazingira ya kuhamahama hovyo huku mahudhurio hafifu ya walimu darasani yakiwaathiri kitaaluma na kisaikolojia.

Walisema hawawezi kulipa ada hiyo hadi shule itakapohamia kwenye majengo yake rasmi. "Watoto wanahamahama ovyo namna hii wataelewa na kuzingatia masomo saa ngapi, siwezi kutoa hela yangu mpaka wahamie kwenye majengo yao".

Alisema mzazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mathias.

Naye mzazi mwingine aliyekataa jina lake lisitajwe gazetini mkazi wa Kurasini alisema, "siwezi kutoa 50,000/= hali najua mtoto wangu hasomi, anachofanya ni kuhamahama tu, Nitalipa wakihamia kwenye kiwanja chao, sio ubabaishaji wa kupanga kwenye mabanda."

Wanafunzi wa kidato cha pili ambao ndio waanzilishi wa shule hiyo, tangu Jumatatu wiki iliyopita wamekuwa wakihudhuria kati ya watatu hadi wanane kati ya 34, baada ya wengine kuacha masomo shuleni hapo na kuhamia shule nyingine na wengine kufukuzwa kwa kutolipa ada.

KIONGOZI lilipowasiliana na mmoja wa walimu aliyejitambulisha kuwa Mkuu wa shule hiyo Bw. Jordson Mwesigwa, alisema pamoja na walimu wengine ofisini kwao kuwa suala la kuhama bado linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu na haliwezi kuwaathiri watoto na lisiwe kigezo muafaka cha wazazi kukaidi kulipa ada kwa wakati muafaka.

Aliongeza kuwa kimsingi hakuna mwanafunzi aliyefukuzwa bali wanarudishwa nyumbani kufuata ada.

Aliwashauri wazazi kutoa taarifa wanapokwama kulipa ada kwa wakati muafaka. malipo kwani hawakutangaza kuwa watasomesha wanafunzi bure.

Awali shule hiyo ilikuwa Mbagala, kisha ikahamia katika banda moja linalotazamana na ukumbi wa PTA, wakahama tena kwenda Mbagala na baada ya siku moja wakahamia banda la Kampuni ya simu ya Tritel katika uwanja huo wa Sabasaba walipo hadi sasa.

Askofu Banzi awa Mwenyekiti wa Mawasiliano AMECEA

Na Dalphina Rubyema

BODI ya Watendaji ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Executive Board of AMECEA) imemchagua Mwenyekiti wa Idara ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Mhashamu Anthony Banzi, kuwa Mwenyekiti wa Idara ya Mwasiliano wa AMECEA.

Mhashamu Banzi ambaye ni Askofu wa Jimbo la Tanga ameshika nafasi hiyo baada ya kuwa wazi kwa kipindi cha miaka mitano kufuatia kustaafu kwa Askofu wa Jimbo la Arusha,Mhashamu Fortunatus Lukamia ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Idara hiyo.

Kwa mujibu wa habari zilizolifikia gazeti hili kutoka AMECEA na kuthibitishwa na Askofu Banzi mwenyewe zinasema kuwa uchaguzi huo umekuja baada ya Mkutano mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai-Agosti mwaka jana kutoa jukumu kwa Bodi ya Watendaji wa AMECEA kuchagua mtu wa kujaza nafasi hiyo.

Askofu Banzi ambaye alihojiana na Mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za gazeti hili alisema kuwa hakuwa na mgombea mwenza kwani jina lake baada ya kupendekezwa lilipita moja kwa moja bila kupingwa.

Alisema atashika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo anaweza kuchaguliwa tena kwani nafasi hiyo inaruhusiwa kushikwa kwa awamu mbili na baada ya hapo anachaguliwa mtu mwingine.

Akielezea hisia zake baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo,Askofu Banzi alisema kuwa pamoja na kuwa na majukumu mengi yakiwemo ya Jimbo lake na yale ya Kitaifa, hana budi kukubali jukumu hilo kwani ni moja ya kazi za kichungaji.

"Mkutano huo uliofanyika tangu Februari 14-16 mwaka huu katika ofisi za Makao Makuu ya AMECEA yalipo nchini Kenya-Nairobi uliwajumuisha Maaskofu 8 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Katibu Mkuu wa Baraza hilo Padre Peter Mulole.

Papa ataka teknolojia isiwaumize wanyonge

Na Neema Dawson

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa II, amehimiza ufuatiliaji wa maadili ya Kanisa katika taaluma mbalimbali kwa kutumia teknolojia zisizowaumiza wanajamii wakiwemo wenye shida kama wagonjwa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Alosius Balina, wito huo ulitolewa na baba Mtakatifu wakati akiongoza misa ya siku ya wagonjwa ambayo kwa mwaka huu Mtakatifu imefanyika Roma , Italia.

Akielezea gazeti hili muda mfupi baada ya kurejea kutoka Roma alikohudhuria maadhimishi ya siku hiyo ya wagonjwa, Askofu Balina alisema kuwa siku hiyo ya wagonjwa iliyoitishwa na Askofu Javier Barragan, Baba Mtakatifu alisema anasikitishwa na mahangaiko wayapatayo wanadamu kutokana na magonjwa mbalimbali, utumiaji wa madawa ya kulevya, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa huduma bora za msingi zikiwemo za afya.

Papa alisema katika taaluma zao, wataalamu hao wakiwemo madaktari hawana budi kutumia teknolojia walizopewa na Mungu ili wawahudumie kwa moyo wa upendo wagonjwa wote.

Wakati huo huo: Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Shinyanga alisema kazi zote zinazohusiana na afya ya mwanadamu ni lazima zifanywe kwa kuzingatia maadili ya kanisa na pia katika siku hiyo mapandre masista na walei wametakiwa waunde umoja katika nchi zao kwani wakiwa kwa wauguzi vipaji vyao vinahitaji maadili ya kiroho.

Alisema katika nchi zao, maaskofu pia wanawajibika katika imani na maadili ya dini siasa na pia kuwa na msimamo thabiti ili masuala yote ya afya yaongozwe katika moyo wa injili na akasema viongozi wa dini wanapaswa kuwathamini wazee na kukemea mauaji yanayofanywa dhidi yao.

Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na maaskofu toka zaidi ya 25 toka nchi mbalimbali duniani, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Buganda, Dk. Zakaria Berege sambamba na baadhi ya watu kupakwa mafuta pia watu walinawishwa miguu kama ishara ya upendo na kusali sala ya Bikira Maria.

Watu mbalimbali wakiwemo wagonjwa waliobebwa kwenye magodoro,viziwi, walemavu wa akili na viungo walipata fursa kamili kufanyika kiroho kwani lugha zote za nchi zilizohudhuria zilitumika