Mhadhiri Chuo Kikuu achambua athari za mabadiliko ya Katiba

lYanatoa mwanya mpana zaidi wa rushwa ya vyeo

lasema Dk.Salmin anachofanya amekirithi CCM

Josephs Sabinus na Peter Domonic

MHADHIRI mmoja Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amezichambua athari za mabadiliko ya katiba na akasema hata yale anayokusudia kuyafanya Rais wa Zanzibar Dk.Salmin Amour, ili aendelee kudumu Ikulu, yasichukuliwe kama suala lake binafsi bali la CCM nzima kwa vile ni utamaduni wa muda mrefu wa chama hicho kubadili katiba kinapoona kitajinufaisha.

Gazeti la Kiongozi lilipotaka kujua maoni yake kuhusu kusudio la mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, Mhadhiri huyo wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii Dk. Mohabe Nyirabu, alidai haoni kama Dk. Salmin anafanya kosa lolote kwa vile anafuata misingi ya CCM, atapitisha katika vikao vya CCM.

Alisema na kuongeza "Dk. Salmini kutaka kubadili katiba ili aendelee kuongoza kwangu naona ni sawa tu.... Sijaona Salmini amekosea popote, kwani ndio utamaduni wa CCM kubadili Katiba inapoona inataka jambo fulani".

Ili kuepusha kuchezewa kwa katiba ya nchi mara kwa mara,Dk.Nyirabu alipendekeza kuwepo kwa katiba moja inayoundwa na wananchi wote ambayo haitamruhusu yeyote kufanya mabadiliko bila ridhaa ya wananchi wenyewe kama ilivyo kwa mataifa kama Marekani.

"Katiba ya sasa ilitegenezwa 1977 na kamati ya watu 20 waliokuwa wameteuliwa kuunda muungano baadaye wakawa waandalizi wa kamati mpya, wakatengeneza proposal zao, mwishowe zikakubalika, ndiyo ikawa Katiba ya nchi ambayo sasa inafanyiwa mabadiliko ya 13," alisema.

Alisema ameshangazwa na Bunge kupitishwa muswada wa Rais kuteua wabunge wasiozidi 10.

Akizungumzia kupitishwa kwa sheria ya kumwezesha Rais kuteua wabunge kumi ambao hawakuchaguliwa na wananchi alisema inatoa mwanya wa marais kujinufaisha."Akija rais mwingie naye atake apewe wabunge 100, akija mwingine aseme aongezewe 20! Anaweza kuchagua marafiki zake, mtu wa nchi nyingine hata pengine mke wake".

Alisema kimsingi ingetamka wazi kuwa sheria hiyo inawalenga watu maalum kama walemavu ili kuondoa utata uliopo, "Hao wengine atakaowateua ni kwamba siku zote watamuunga mkono, hawawezi kumpinga huku amewateua yeye, " alisema.

Katika suala la Haki za binadamu, Mtaalamu huyo wa siasa aliongeza kuwa Tanzania imejijengea msingi wa kuthamini haki za binadamu, lakini upo uwezekano wa utekelezaji wake kuwa mgumu.

"Labda wasiwasi uliopo ni ofisi itakayoshughulikia haki za binadamu kuwa chini ya Ofisi ya Rais..Mtu anayefanya kazi chini ya ofisi ya Rais anaweza kufanya yaliyo kinyume naye hata kama anavunja haki za wananchi?" alihoji na kuongeza kuwa chombo hicho pamoja na Tume ya Uchaguzi bora vingekuwa huru na vikafanya kazi kwa kujitegemea.

"Unajua mpaka sasa Rais anaweza kuamka, akakuweka ndani na hakuna chombo kinachoweza kumuuliza,.Tume ya Nyalali ilipendekeza sheria nyingi ziondolewe lakini hadi sasa bado hazijaondolewa."

"Katika kutangaza matokeo, wawakilishi wengi walikuwa wanasema ni vema Tume hiyo ingekuwa huru na isichaguliwe na Rais na labda angependekeza majina kisha yakachujwa na chombo kingine.

"Mojawapo ya mambo yaliyolalamikiwa na wapinzani ni kutoshirikishwa ndani ya Tume. Sioni ubaya kama kutakuwa na wawakilishi katika Tume".

Hata hivyo aliwatahadharisha baadhi ya wapinzani kujua kwamba kuwa mwanasiasa siyo lazima kupingana na chama tawala hata kwa mambo mazuri. "Mambo mazuri mnaungana mkono," alisema.

Hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wananchi juu yania ya Rais wa Zanzibar kutaka katiba ya Zanzibar ibadilishwe ili aweze kugombea kwa kipindi kingine cha tatu. Wakati mvutano huo mkali ukiendelea juu ya Katiba ya Zanzibar, Serikali ya Muungano nayo imepitisha mabadiliko ya 13 ya Katiba ambayo yanampa Rais uwezo wa kuteua Wabunge wapatao 10 nje ya wale wa kawaida. Kadhalika mabadiliko hayo tofauti na awali yametoa ruksa kwa mgombea nafasi ya kisiasa kutoa takrima ya chakula kwa wasaidizi wake katika kampeni. Awali jambo hilo lilihesabiwa kuwa rushwa na lingeweza kufanya ushindi wa mgombea utenguliwe mahakamani. Kipengele kingine kilichopitishwa kuwa ni kwamba mtu anayepinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge aweke dhamana ya Sh. milioni 5 mahakamani, kwa vile kesi za namna hiyo zimekuwa na gharama kubwa.

 

Wanasheria wawataka Wazanzibari wasikubali kutukanwa

KUDAI kuwa katika umma wote wa wananchi wa Zanzibar hakuna mwananchi hata mmoja mwenye uwezo wa kuiongoza Zanzibar kama Rais hivyo ni lazima kufanya mabadiliko ya katiba kwa madhumuni ya kumruhusu Rais wa sasa Dk. Salmin Amour kugombea tena nafasi hiyo kwa awamu ya tatu mfululizo ni kuwatusi Wazanzibari na hawapaswi kuikubali, wanasheria wameonya.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichopo jijini Dar es Salaam katika taarifa ya maandishi iliyotolewa kwa gazeti hili na kituo hicho kilicho chini ya Uwenyekiti wa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT),Elinaza Sendoro ikiwa imesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Bi. Helen Bisimba,imesema kudai hivyo si tu kuwatusi Wanzanzibari bali hata kubinafsisha taasisi ya urais visiwani humo.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa kama lengo la kubadilisha katiba ya nchi hiyo litafanikiwa Dk. Salmin atakuwa ameongezeka kwenye orodha ya viongozi duniani wanaojitahidi kubadili Urais kuwa usultani.

"Inashangaza kuona kitu kama hiki kinafanyika.Ikiwa Tanzania ilipata bahati ya kuwa na Rais wa kuanza aliyetoa mfano wa kuachia madaraka kwa hiyari, hatua inayoshangiliwa na kuigwa na marais katika nchi nyingine duniani, sasa kwanini Dk. Salmin aendelee kung’ang’ania madaraka?" inahoji sehemu ya taarifa hiyo.

Kituo hicho pia kimesikitishwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya kukemea watu wa upande wa Bara wanaoshutumu hatua hiyo ya kubadili katiba pale viongozi hao wanapotoa sababu kwamba watu wa Tanzania Bara hawapaswi kuzungumzia mambo ya visiwani.

"Kauli hizi zinashangaza kwani ukweli ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, kwa mantiki hiyo tatizo la Zanzibar ni tatizo la Tanzania na hii ndiyo maana ya Muungano," inasisitiza sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo kituo hicho kimeitaka Serikali ya Mapinduzi ifahamu kuwa wanaopinga hatua hii ya "kubinafsisha" urais si wapinzani wa CCM tu bali ni Watanzania walio wengi- wakiwemo wana CCM wenyewe hata wa Upande wa Zanzibar.

Amani ya taifa sasa yahitaji magoti ya kanisa

KANISA la Kianglikana nchini halitaingilia tofauti za kisiasa nchini lakini waumini wake wametakiwa kupiga magoti na kuomba zaidi ili mambo yaende vema, hasa wakati huu tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Dk.Frank Kajembe wa Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Dar es Salaam na Pwani alipokuwa akizungumza na KIONGOZI alipohojiwa juu ya msimamo wa kanisa katika tofauti za vyama vya kisiasa ambavyo vinaonekana kuwa na uchochezi ambao unaweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

"Tukikumbuka wakati kilipotokea kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Nyerere Watanzania wengi walidhani kuwa baadhi ya watu watashikana mashati na kupelekea kuvurugika kwa amani lakini viongozi wa dini tulipiga magoti na kumuomba Mungu kuendelea kuwepo kwa amani" Alisema Mchungaji Kajembe. Aliendelea kuelezea kuwa hali hiyo ya kuwepo wasiwasi kwa Watanzania imeanza kujitokeza katika kipindi hiki kinachoelekea kwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani hali ambayo Watanzania wengi wanadhani kuwa uchaguzi huo utakuwa wa kushikana mashati kwa kugombea madaraka na kama Kanisa tunalo jukumu la kuomba mambo yote ya shughuli za kisiasa yaende vema na yale yakumpendeza Mungu kwani uwezo wa kuongoza unatolewa na mwenyezi Mungu na si miujiza.

Aidha alisema kuwa Watanzania lazima wawe makini, na wafahamu kabisa kuwa uchaguzi mkuu si wa kushikana mashati na kujiepusha na watu ambao wanaleta fedha kwa ajili ya kuharibu uchaguzi kwa kufanya kampeni za kuhonga pesa ili kupata madaraka bila kufahamu kuwa hali hiyo itaharibu amani ya nchi na ifahamike kuwa Amani ya nchi hainunuliwi kwa fedha bali inanunuliwa kwa amani na wale ambao wanayafuata maandiko matakatifu watu baini kuwa "Wapiganao kwa upanga wataangamia kwa upanga" kwani wanaotaka madaraka ya kuongoza nchi kwa manufaa binafsi na si ya wananchi wataangamia kwa upanga.

Sambamba na hayo pia alisema kuwa Maaskofu wa Kanisa la Anglican nchini Tanzania wapatao 16 wanatarajia kufanya mkutano wa kiroho utakaofanyika wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro utakaongoza na Askofu Mkuu Donald Mtetemela ambapo maja ya mambo muhimu yatakayofanywa ni maombi ya kiroho ikiwa ni kuiombea nchi hii ya Tanzania iendelee kuwa na Amani.

Hatuingilii siasa,tunafanya Unabii- Askofu

BAADHI ya watu wanaopotosha jamii na wenye nia mbaya, hukerwa na maangalisho (unabii) wa Viongozi wa dini na kisha kuwazulia lawama viongozi hao wa kiroho kuwa wanachanganya dini na siasa, amesema Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Paul Ruzoka kama anavyoripoti Josephs Sabinus.

Mhashamu Ruzoka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam katikati ya juma alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hii katika mazungumzo yake na Kiongozi kuwa yeye kama Mtanzania (mwanajamii) na pia Kiongozi wa kiroho, anajisikia vipi Viongozi wa kiroho wanapozungumzia jambo linalokwenda vibaya na pengine linaloweza kuhatarisha amani, wanatafsiriwa kwamba wanachanganya dini na siasa.

Alisema kwa kuwa kimsingi viongozi wa dini ni sawa na wanajamii wengine hawawezi kujitenga na mambo ya kijamii na kwamba ni lazima wayazungumzie ili kuchangia maendeleo ya ustawi wa jamii na pia kuifanya idumu katika amani na upendo.

"Kazi ya padre au shehe ni kuangalisha na kuelezea unabii na uchungaji ili jamii isipotoshwe wala kupotoka. Hata hivyo, wanaopotosha wanaweza kukerwa na ushauri au uangalisho huo; wakaanza kusema padre anaingilia siasa.

Hakuna sababu kwa mtu au kiongozi yeyote kusema viongozi wa dini wanaingilia siasa au kupanda majukwaa ya siasa," alisema Mhashamu Ruzoka na kuongeza,

"A human being is a political animal (Binadamu ni mnyama mwenye siasa), na siasa inahusu jamii na hivyo basi kwa kuwa mapadre ni miongoni mwa watu wa jamii, hawawezi kujitenga na maisha ya jamii kama wanajamii wengine"

Wakati huo huo: Askofu huyo wa Kigoma amesema kuwa tamaa ya mali, upotofu wa maadili pamoja na imani duni, ndivyo vimechangia kushamiri kwa vitendo viovu vilivyopelekea kuibwa kwa msalaba Jimboni Rulenge mkoani Kagera.

Amesema jamii yote yenye mapenzi mema haina budi kushirikiana ili kuona kuwa wanajamii wana enenda kimaadili na kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

Akilaumu kitendo hicho, Askofu Ruzoka alisema hana shaka kuwa aidha msalaba huo uliibiwa na wenye uchu wa pesa ili wakauze na kujipatia donge nono, au uliibiwa kwa makusudi na watu wenye imani tofauti, baada ya kutishwa na mwamko wa kiroho wa Wakatoliki. Amewahimiza waamini wa kikatoliki kudumu katika imani thabiti.

"....walifikiri wataviza imani ya Wakatoliki au kupunguza mzizimo wa Kristo ambao ni ukombozi aliotufikishia kwa njia ya msalaba.

Hivi karibuni katika mazingira ya kutatanisha msalaba wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, wa Jimbo Katoliki la Rulenge uliibiwa parokiani Rwinyana na baada ya sanamu ya Yesu kufunguliwa kiufundi, wezi hao waliondoka nayo na kutelekeza mbao kichakani.

 

Watakiwa kuachana na kasumba kuwa misheni kuna pesa bwelele

Na Leocardia Monswery

MLEZI Mkuu wa kituo cha kulelea watoto wadogo cha Alamano Nursery School cha Mbagala jijini Dar es Salaam, Sista Elvina Antonici Sour wa Shirika la Konsolata, amewataka wazazi kuchangia huduma mbalimbali za shule hiyo, badala ya kuwaachia mzigo wote masista.

Akizungumza na wazazi katika kikao cha hivi karibuni shuleni hapo , Sista Elvina alisema, wazazi wengi wamekuwa na kasumba mbaya kuwa watu wa misheni wana pesa nyingi za kuweza kufanya kila kitu na akasema hiyo si kweli.

"Hatuna msaada wowote isipokuwa tunajitegemea. Hivyo basi ni vema wazazi mkachangia ada ili tuweze kuendesha shule yetu badala ya kuwaachia mzigo wote masista kuwapa misaada watoto wetu" alisema.

Aliongeza kuwa ingawa watoto wanahitaji elimu, wazazi wasipojenga moyo wa dhati kwa kuwapenda kwa kuchangia maendeleo ya huduma zao muhimu kama elimu, ipo hatari ya walimu kushindwa kulipwa pesa zao na hivyo kuwavunja moyo, hasa ikizingitiwa kuwa kazi ya malezi kwa watoto wadogo ni kubwa mno.

Mama Mlezi huyo ametoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema na malengo wa maendeleo, kuchangia huduma za watoto hao kwa chochote kinachopatikana ukiwemo unga, sukari, maziwa au hata pesa kidogo ili kuwaendeleza vema watoto hao.

Katika kikao hicho, Sista Antonaci Sour alidokeza kuwa uongozi wa shule umepata kiwanja kwa ajili ya michezo ya watoto lakini ukosefu wa pesa umesababisha kukwama kuanza kwa shughuli za ujenzi.

Akijibu swali la mzazi mmoja aliyetaka kujua sababu za baadhi ya watoto kutokuelewa kusoma na kuandika, Sista Antonace alisema, "Shule ya awali ni ya watoto wadogo. Lengo lake sio kufundisha kusoma na kuandika bali ni kuwaandaa watoto kiakili na kimaadili".

Waanglikana wagawa mbegu kwa wananchi

Na Neema Dawson

KANISA la Kianglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam na Pwani limetoa msaada wa mbegu kwa wakulima wanaokabiliwa na njaa na tishio la njaa zaidi mkoani Pwani ili kuweza kuwaokoa katika janga hilo.

Afisa maendeleo wa Dayosisi hiyo Bw. Uhuru Mathayo Mpalaza, amesema hivi karibuni kuwa msaada huo ulitolewa na shirika la The Mary Summer House la nchini Ujerumani kupitia umoja wa akina mama Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam na Pwani (UMAKI) na msaada huo umegawanywa kama ilivyokusudiwa bila kujali dini, rangi wala kabila.

Alifafanua kwa kusema kuwa wamenunua mbegu kwa kuzingatia ubora na maeneo ambayo yanahitaji mbegu hizo za mahindi aina ya TNVI ambazo katika miezi mitatu tangu kupandwa huweza kuvunwa.Afisa maendeleo wa Dayosisi hiyo alieleza kuwa kabla ya ugawaji huo wa mbegu kufanyika uongozi wa kanisa uliwasiliana na uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kibaha na ule wa mkoa wa Pwani ili kujua takwimu na maeneo yanayokabiliwa zaidi na matatizo ya njaa na uhaba wa mbegu. Ugawaji huo wa mbegu pia ulizingatia hali ya hewa, rutuba na mazingira ambayo yanafaa.

Maeneo yaliyonufaika na msaada huo ni vijiji vya Jisunyara, na Mlandizi ambapo wamepata mbegu za mpunga kutokana na hali ya bonde la mto Ruvu ambao unahifadhi maji kwa muda mrefu, Kijiji cha Mpangani ambako wamenufaika na mbegu za mahindi. Maeneo yote hayo ni ya mkoa wa Pwani, lakini hata hivyo imeelezwa kuwa mkoa wa Dar es Salaam pia utanufaika na msaada huo.

Maeneo ya Dar es Salaam yatakayonufaika na msaada huo ni Nzasa Chanika, Buza na Mbagala.

Wafanyabiashara wa korosho, ufuta wajizatiti

Na Peter Dominic

CHAMA cha Ushirika wa kuuza na kununua mazao ya korosho na ufuta cha Dar es salaam (CHACASIMCO) kinaandaa mikakati mipya ya ununuzi wa mazao hayo ili kuinua ufanisi wake.

Akizungumza katika ukumbi wa DDC Keko, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kushika nafasi yake Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Nassor Shabani alisema chama chake kitaadaa mipango madhubuti katika kuboresha utendaji na ufanisi wake ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa masoko yake.

"Wateja wetu wakubwa ni wahindi, tutajitahidi kuwatumia ili tupanue masoko yetu," alisema mwenyekiti.

Awali ushirika huo ulikuwa na utaratibu wa kutathmini maendeleo yake kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni pamoja na kuwachagua viongozi wa Muda hivi sasa kumekuwa na maafikiano kuwa viongozi wapya waliochaguliwa watakiongoza kwa miaka mitatu iwapo hawataboronga.

Afisa ushirika kanda ya Temeke bi. Zainabu Muhomba ambaye alishirikiana na Bw.Omar Kyamba kusimamia uchaguzi wa viongozi hao wapya, alisema viongozi wanatakiwa kuwa waadilifu na kwamba ikitokea wakatumia madaraka kujinufaisha Sheria itawabana.

Aliwasisitiza wanachama wake kuepuka vitendo vya kukwepa kulipa kodi na ushuru kwa kupitia mlango wa uani kwani ni kosa la jinai linalorudisha maendeleo nyuma",alisema Afisa huyo.

Maafisa hao walisema kwa vile viongozi wamechaguliwa na kwa demokrasia na mkutano mkuu, wanachama wanao uwezo wa kuitisha mkutano mwingine na kuwaengua viongoz i hao iwapo watafanya makosa.

 

TLP nayo yawaonya Wazanzibari

Na Mwandishi Wetu

WAZANZIBARI wametahadharishwa kutokubali kufanya mabadiliko yatakayomruhusu Rais wa sasa wa Zanzibar Dk. Salmin Amour kugombea tena urais kwa awamu ya tatu mfululizo kwani kufanya hivyo ni kujenga msingi wa hatari dhidi ya amani katika visiwa hivyo.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Chama cha upinzani cha Tanzania Labour Party (TLP) kupitia kwa mwenyekiti wa kitengo cha Vijana bw. Msafiri Mtemelwa, wakati alipokuwa akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni jijini.

Bw. Mtemelwa alisema kuwa kitendo cha kutaka kubadilisha katika ya Zanzibar kinaonyesha jinsi gani Tanzania ilivyo na watu ambao hawako tayari kuongoza kidemokrasia.

"Kinachotokea hivi sasa visiwani Zanzibar kinaonyesha kuwa Tanzania ina watu ambao hawapo radhi kuongoza kidemokrasia bali wanatangauliza mbele ubinafsi na kuweka nyuma maslahi ya wananchi na Taifa lao," amesema Bw.Mtemelwa .

Mwenyekiti huyo wa Kitengo cha Vijana amemtaka Dk. Salmin, kuiga mfano wa Rais wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi ambaye hakuwa na uchu wa madaraka kwani bila hiyana aliachia Ikulu baada ya muda wake wa uongozi kukamilika.

Amemtaka Rais huyo pia kufahamu kuwa Katiba ni utaratibu maalum wanaojiwekea wananchi kwa manufaa ya nchi yao na wala siyo utaratibu wa kulinda maslahi ya mtu mmoja.

"Inatakiwa Dk. Salmin akubali kutoka madarakani bila kupinga na wala kupiga chenga, asitumie mabavu ya Urais kutaka kubadilisha Katiba," alisema na kuongeza

"Kama Wanzanzibari watacheza, iko siku atatokea mtu ambaye atataka kuibadili zaidi katiba ya nchi yao ili aweze kuwa Rais wa maisha".

Hivi sasa kuna mgogoro mkubwa visiwani Zanzibar baada ya Rais wa nchi hiyo kutaka kubadilisha katiba ili kumruhusu kugombea kipindi cha tatu cha Urais wakati katiba ya sasa haiamuru kufanya hivyo, inamruhusu kugombea kiti hicho kwa vipindi viwili tu ambapo kwa hivi sasa muda huo unakamilika na haruhusiwi kugombea tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hapo Oktoba mwaka huu. Hata hivyo uamuzi huo umeleta mgawanyiko baina ya Wabunge wa Chama tawala cha CCM ambapo baadhi yao wanaupinga na wengine wanauunga mkono.

Katika suala hili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar , Mhesimiwa Benjamin Mkapa bado hajaonyesha wazi msimamo wake, hali inayoleta utata kwa wananchi ambao wengi wao wanafikiri pengine anaunga mkono uamuzi wa Dk.Salmin.

Thomas Lyimo kuwainua wenye kipato kidogo

Na Dalphina Rubyema

MMILIKI wa Kiwanda cha Maziwa cha Tommy Diaries na mfanyabiashra maarufu nchini Bw. Thomas Lyimo anakusudia kuwasaidia Watanzania wenye kipato cha chini kupitia taasisi moja isiyo ya kiserikali inayotoa mikopo kwa wananchi wa aina hiyo.

Habari ambazo gazeti hili limezipata na zikathibitishwa na Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya mikopo ya jijini, Liberty Fund zimesema Bw. Lyimo yuko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Liberty Fund juu ya namna mikopo hiyo itakavyotolewa na marejesho yake.

Katibu Mkuu huyo Bw. Isaack Michael,alipoulizwa na gazeti hii juu ya taarifa hizo alikiri kwamba ni kweli wanawasiliana na mfanyabiashara huyo, lakini alisema uamuzi wa mwisho haujatolewa juu ya makubaliano hayo kati ya taasisi yake na Bw. Lyimo.

Ikiwa makubaliano hayo yatafikiwa Liberty Fund itasimamia shughuli za ukopeshaji wa fedha hizo pamoja na marejesho yake na kwamba riba itakayotozwa itabaki Liberty Fund na kiasi cha fedha zilizotolewa na mfadhili huyo zitarejeshwa na Liberty Fund bila riba. Bw. Isaack alisema ni mapema mno kutaja kiasi cha fedha ambacho Bw. Lyimo anatarajiwa kukitoa lakini hata hivyo gazeti hili limebaini kuwa zinatarajiwa kuwa si zaidi ya Sh. Milioni 30.

Kardinali Pengo kukosa kiwanja kujengea shule ya kimataifa?

JUHUDI za Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kutaka kujenga shule ya msingi yenye hadhi ya kimataifa katika eneo la kurasini ili kupambana na tatizo la elimu, bado ni kitendawili na huenda zikagonga mwamba kutokana na ukosefu wa kiwanja.

Mkuu wa wilaya ya Temeke, Kapteni John Chiligati na Katibu wa Parokia ya Kurasini Bw. Cletus Majani wameliambia Kiongozi kwa nyakati tofauti kuwa ingawa ni muda mrefu umepita tangu Kardinali Pengo alipoomba eneo hili (takribani miaka miwili iliyopita), bado juhudi za kupata kiwanja hicho Kurasini zimekwama kutokana na maeneo yote kuwa na watu.

Alipoulizwa hatua aliyofikia ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, Kapteni Chiligati alisema ofisini kwake hivi karibuni kuwa ugumu wa ufumbuzi wa suala hili unamtonesha kidonda cha moyo wake kwa kuwa bado ni kitendawili kigumu.

"Swali lako linanitonesha kidonda cha moyo wangu ndiyo maana nimekuambia uulize lingine hilo uliache. Linanikumbusha ugumu wa kazi hiyo ambayo Kardinali amejitolea kuisaidia jamii. ... kama angetaka eneo lingine kama Mbagala, ingekuwa rahisi na hata watoto wangelikwisha anza kusoma. Lakini anasema ana special attachment na Kurasini" alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Alisema hivi sasa unaandaliwa mpango maalumu ili wote wasioendeleza maeneo yao, wanyang’anywe na viwanja hivyo kutumika kwa manufaa ya umma.

Naye katibu wa Parokia ya Kurasini alisema ingawa juhudi za kutafuta eneo hili hazielekei kufanikiwa, bado wanalifanyia kazi kwa bidii. "ingawa maeneo kadhaa tuliyoomba kiwanja likiwemo lile la Foreign Relation Centre tulikosa, bado hatujakata tamaa" alisema Majani.

Kiongozi lilipotaka kupata maoni zaidi ya Kardinali Pengo juu ya Tatizo hili, alisema "kwa kuwa mimi ndiye mhusika nisingependa habari hizi zitokee kwangu, eti mimi ndiye nilizungumzie."Siku chache baada ya kushika nafasi yake,Kardinali Pengo aliuomba uongozi wa wilaya ya Temeke pamoja na kamati husika wamtafutie kiwanja katika eneo la Kurasini ili ajenge shule ya msingi yenye hadhi ya kimataifa ili kupunguza tatazo la ukosefu wa shule.

Kata ya Kurasini inayo shule moja ya msingi (Kurasini) yenye zaidi ya watoto 5000 na hivyo kujengwa kwa shule hiyo kutakuwa msaada na changamoto kubwa katika kulikabili tatizo la elimu na kuondoa ujinga Kurasini.

Wanawake Wakatoliki watwaa ubingwa wa soka

Na Damas Masanja, Tabora

TIMU ya mpira wa miguu ya Wanawake Wakatoliki (WAWATA) wa Ipuli, Tabora mwishoni mwa wiki walitawazwa kuwa mabingwa wa mkoa wa Tabora baada ya kuwalowesha mabao 3-1 wanawake wenzao kutoka Tabora mjini katika mchezo uliofanyikia kwenye uwanja wa mkoa mjini hapa.

Katika mchezo huo timu ya Tabora mjini ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa katika dakika ya saba ya kipindi cha kwanza na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Rehema Hamisi.

Bao hilo lilikuwa kama vile mtu anapotupa jiwe ndani ya mzinga wa nyuki kwani liliwafanya washambuliaji wa timu ya WAWATA Ipuli icharuke na kutoa mashambulizi makali kwa wapinzani wao kiasi cha kuwafanya mashabiki na watazamaji watumie karibu muda wote wa mchezo wakiwa wamesimama huku viti vikiwa nyuma yao.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi sana kuipenye ngome ya Tabora mjini ambayo ilikuwa ikiongozwa na beki Valentine Joseph, maarufu kwa jina la Mama Kiti Moto, ikiwahusisha pia beki Stela Haule na mlinda mlango Mary Kahabi.

Hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika timu zote zilikuwa zimefungana mabao 1-1, lakini katika kipindi cha pili WAWATA Ipuli waliongeza mashambulizi na kuwapachika Tabora mjini mabao mengine mawili.

Goli la pili lilifungwa na mwanamama Theresia Simwanzi katika dakika ya 73 kwa njia ya penalti baada ya mlinzi wa Tabora Mjini kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Katika mpira huo uliochezeshwa na mwamuzi Peter Nkomele, Jackline Kayoka ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Tabora Mjini katika dakika ya 81.

Mchezo huo wa kumtafuta binwa wa mkoa ulikuwa pia na madhumuni ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la kiaskofu mjini hapa.

 

Chama kipya cha Siasa chataka dini ziwakilishwe Bungeni

Na Josephs Sabinus

CHAMA kipya cha siasa cha Sauti ya Mshikamano Tanzania (SMT) kimesekana kukosekana kwa wawakilishi wa vikundi vya dini bungeni na katika mabaraza ya madiwani, kunachangia kwa kiasi kikubwa kudodora kwa uchumi na huduma za jamii nchini.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho kilichopata usajili wa muda Desemba 1,1999, (kwa mujibu wa nakala ya usajili tuliyonayo) Bw. Paulus M.B Mwanja, aliyesema hayo katikati ya juma lililopita alipokuwa akizungumzia chama chake katika ofisi za gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Alisema licha ya kuboresha mahusiano mema yaliyopo baina ya dini na dini nchini pamoja na Serikali, kushirikishwa kwa vikundi vya dini, mashirika ya kibinafsi na wawakilishi wa walemavu katika bunge na mabaraza ya madiwani, kutasaidia kuleta ufanisi katika kupanga na kutekelezwa masuala ya maendeleo kwa kila kundi.

Alisema ingawa kwa muda mrefu umuhimu wa vikundi vya dini umekuwa ukidhirika bayana, anashangaa kuona kuwa bado havishirikishwi katika maamuzi ya kijamii hadi mambo yanapokweda mrama.

"Suala la madhehebu ya dini kujadili maendeleo ni muhimu kuliko kusubiri mambo yaharibike, ndipo serikali ianze kusema. Oo! Dini ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, sidhani hivi kama umuhimu wao unaonekana wakati huo kwanini basi wasishirikishwe tangu awali katika bunge na mabaraza ya madiwani? Dini, NGOs, na chambers of Commerce viwakilishwe". Alisisitiza na kuongeza, Viongozi wa dini wasizuuliwe kujadili mambo ya maendeleo eti kwa madai kuwa wanachanganya dini na siasa vikao kama hivyo ni mahali muafaka lakini hawashirikishi, watasema wapi ili kutenda wajubu wao?"

Alipoulizwa iwapo hali hiyo haitazua uduni bungeni kila mmoja akitaka kunufaisha wafuasi wake, Bw. Mwanja alisema "Hiyo ndiyo maana ya ukawakilishi,unawakilishi na hata kuwatetea watu wako. Mbona hata wabunge wengine wanatoka Mbeya, Moshi,.... Hawatoki pamoja".

Akizungumzia hali ya kisiasa Bw. Mwanja alisema kwa mtu anayeheshimu demokrasia asingetegemea Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Salmin Amour abadili Katiba ili ajinufaishe na kwamba ukimya wa Rais Mkapa unatia mashaka.

Kama mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu huyo ambaye Mwenyekiti wake ni Bw. Juma Kassim Ngupepe, anadai S.M.T yenye Makao Makuu yake Kurasini jijini Dar es Salaam, kina matari katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Pwani, Mwanza na bado kinatangaza katika mikoa mingine.

Anadai kina malengo ya kuwaunganisha Watanzania bila ubaguzi wowote na kumwezesha mwananchi kupata mahitaji na huduma muhimu kama chakula, mavazi, elimu na afya, pia kuhakikisha kuwa demokrasia ya kweli inakuwapo na kuona kuwa haki za msingi za Binadamu za Watanzania zinakuwepo na kuheshimiwa.

Nyingine ni kuhakikisha kuwepo kwa utawala wa sheria, kudumisha amani utulivu na mshikamano wa kitaifa;kupinga kuonewa na kukandamizwa na serikali na kuwapa akina mama misaada na mikopo ya makusudi ili kuboresha hali zao za maisha na kupeleka nguvu za Serikali vijijini ili wakulima waboreshe kilimo nchini na kuhakikisha kuwa siku zote Serikali ina wajibika kwa wananchi kwa mambo yote ambayo ha yakuendeshwa vizuri