Wala rushwa wakubwa wanajulikana hawaguswi- Jaji Mkuu ashangaa

lTaifa litaangamia na sote tuliomo

Na Mwandishi Wetu

JAJI Mkuu Mstaafu Francis Nyalali, amesema inashangaza kuona kuwa wapo watumishi wa umma nchini wanaojulikana wazi wazi kwamba wamejilimbikizia mali katika mazingira ya rushwa lakini hawachukuliwi hatua. Nyalali pia ameonya kuwa endapo hali itaachwa iendelee kama ilivyo taifa la Tanzania litaangamia pamoja na wote waliomo.

Mheshimiwa Nyalali, alikuwa akiongea katika sherehe za Siku ya Sheria, Februari 2, mwaka huu katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

"Ingawa ni haramu kisheria mtumishi wa umma kujilimbikizia mali kwa njia zisizoeleweka, na ingawa waliovunja mwiko huu katika taasisi mbali mbali za umma wapo na wanajulikana, hadi sasa hawajachukuliwa hatua," alisema Jaji Mkuu huyo ambaye amestaafu mwezi uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Barnabas Samatta na siku hiyo alikuwa akiaga rasmi.

Wakati Jaji Nyalali, akitoa onyo hilo, hivi karibuni Serikali imetangaza mkakati wa kitaifa wa vita dhidi ya wala rushwa, lakini hata hivyo wanaokumbwa na fagio hilo wamekuwa watu wa ngazi za chini na kati tu, ukiachilia mbali Waziri wa zamani wa Ujenzi Nalaila Kiula na maafisa kadhaa wa zamani wa wizara hiyo ambaye ana kesi ya ulaji rushwa mahakamani.

Nyalali alisema pia kwamba kimantiki mapambano dhidi ya mienendo inayoendana na rushwa hayatakiwi kukomea kwenye ulimbikizaji mali pakee kwani wapo wasiolimbikiza kwa vile wana matumizi makubwa yasiyoeleweka.

"Kwa kuwa rushwa kila mara huendana na mwenendo usioelezeka na kueleweka wa ukiukaji taratibu zilizowekwa kwa kumyima haki anayestahili kwa maslahi ya asiyestahili, ni vema kuharamisha kisheria mwenendo huo," alisema.

Jaji Nyalali pia alisema watu wanaopinda sheria na taratibu zilizowekwa katika hali isiyoeleweka wanastahili kushitakiwa kwa kosa la jinai la kutumia vibaya madaraka waliyopewa na umma.

 

Kaeni Chonjo: Kakobe amemwaga wahubiri 800 wenye baiskeli mikoani

Na Peter Dominic

ZAIDI ya wahubiri 800 wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship kutoka jijini wengi wao wakiwa na baiskeli wametawanywa nchi nzima katika tarafa mbalimbali ili kuwashawishi wakazi wa huko kujiunga na kanisa hilo.

Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo Zakaria Kakobe, amewawakea mikono wahubiri wa kundi la mwisho la watu 134 Jumapili iliyopita katika ibada maalum iliyofanyika katika kanisa hilo Mwenge jijini Dar es Salaam, imefahamika.

Hatua ya kutawazwa na kuwa wachungaji rasmi inatokana na wafuasi hao kufuzu mafunzo ya kichungaji ya kanisa hilo yaliyowachukuwa takribani kipindi cha mwaka mzima.

Timu ya wachungaji hao inakwenda sambamba na wake zao ambao nao kwa mujibu wa kanisa hilo walihitimu mafunzo hayo na kuwekewa mikono ili waweze kufuatana na waume zao.

Pamoja na kuwekewa mikono na jopo la viongozi wakuu wa kanisa hilo kutoka kila mkoa, watumishi hao walikabidhiwa baiskeli kila mmoja wao.

Baiskeli hizo ambazo waliandaliwa watumishi hao ziliingizwa ndani ya kanisa hilo na kusukumwa hadi madhabahuni ambapo zilishuhudiwa na kila muumini na kusababisha kanisa lilipuke kwa makofi na vigelele.

Kwa kuwatia moyo waumini wake Mchungaji Kakobe alisema,"Kanisa linaweza kujitegemea bila kupata msaada wowote kutoka nje."

Baiskeli hizo zipatazo 111 zimenunuliwa na kanisa hilo kwa utaratibu wa kuweka nadhiri ya kuchangia kanisa hilo kuanzia sh. Milioni moja hadi shilingi 500.

Wachungaji hao wamepelekwa mikoa 15 wakiungana na wengine ambao walitawanywa awali katika mikoa mingine na kufanya idadi ya wahubiri wote ifikie 800.

 

Wakatoliki wakwepa kodi sasa kuungama mbele ya mapadre

Damas Masanja Tabora

KANISA Katoliki nchini linaandaa kitabu cha mafundisho kinachofafanua kuwa uvivu na kutokulipa kodi ni dhambi hivyo mtu anayejihusisha na mambo hayo atalazimika kuungama kama za dhambi zingine.

Hayo yamesemwa na Padre Leons Maziku, Paroko wa Parokia ya Ipuli wakati akitoa mahubiri katika kanisa la Familia Takatifu mjini hapa, Jumapili iliyopita.

Paroko huyo alikemea vikali tabia ya uzembe, uzururaji,upokeaji na utoaji rushwa pamoja na suala la ukwepaji kulipa kodi halali serikalini ambapo alisema hizo ni dhambi na zinapaswa kuchukiwa na kila mtu mpenda amani na haki kwa nchi yetu.

Padre huyo alisema jamii haina budi kutoa malezi mema kwa vijana ili wawe watu wema na wa msaada kwa jamii kwani bila malezi hayo hawawezi kukwepa kuwa wahalifu na wahuni.

Paroko huyo alitoa mifano mbalimbali ya watu wenye historia ya malezi mabaya na baadaye wakapata dhamana ya kuongoza jamii kuwa ni dikteta Nduli Idi Amini pamoja na viongozi wa vikosi au vikundi vinavyofanya uhalifu mbalimbali wa kimataifa kwani historia zao zinaonyesha malezi yao hayakuwa mazuri.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa maendeleo ya Sayansi na teknolojia duniani, ndiyo mojawapo ya vitu vinavyovunja au kuporomosha imani na maadili mema ya dini mbalimbali duniani.

Akifungua semina ya siku tano ya uenezaji injili iliyofanyika mjini hapa, Askofu Mkuu Mario Mgulunde, alisema kuwa watu wengi sasa na hasa nchi za Ulaya wanaenda mahakamani kufuta majina yao ya kidini na kuachana nayo kabisa.

Askofu Mgulunde aliendela kusema kuwa mapadre wanapaswa kufundisha kwa nguvu suala la kujitegemea kwa kanisa la Afrika kwa kuwa misaada kutoka nje ya bara hili haipo tena.

Kiongozi huyo wa dini alisema pia kuwa kanisa lolote linajengwa kwa mambo makuu matatu ambayo aliyataja kuwa ni sala, ushuhuda wa maisha, sadaka pamoja na michango mbalimbali ya kanisa.

Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa kanisa la Ulaya sasa linahitaji umisionari kutoka Afrika kwa kuwa ndiyo bara pekee lililobaki na imani kubwa kwa Kristu, tofauti na Ulaya wanakofikiria mambo ya kompyuta zaidi kuliko Mwenyezi Mungu anayewawezesha kutengeneza kompyuta hizo.

Katika semina hiyo iliyokuwa chini ya usimamizi wa padre Alfons Ndekimo, ambaye ndiye Mkurugenzi wa mashirika ya kipapa nchini, ilihudhuriwa na washiriki 23 kutoka majimbo ya Kigoma, Singida,Sumbawanga na wenyeji wa Tabora.

Mambo waliyojifunza katika semina hiyo ni pamoja na njia za uenezaji injili, ushuhuda wa maisha ya ubatizo na umisionari wa mtoto kwa mtoto.

Semina nyingine kama hiyo itafanyika katika Jimbo la Singida kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu ambapo ratiba ya kudumu ya semina kama hizo itakuwa ni mara mbili kwa mwaka yaani mwanzoni mwa mwaka na mwishoni mwa mwaka kwa kila kanda

 

Taasisi za dini,Jiji wajadili kuoza kwa maadili

Na Neema Dawson

ILI kupunguza tatizo la Umaskini na Uhalifu kwa jiji la Dar es Salaam Taasisi mbali mbali za dini zimeombwa zisaidiane na serikali kutatua tiatizo hilo na hata kuliondoa.

Hayo yalisemwa na aliyekuwa Kamishna wa Biashara na Uchumi wa Tume ya Jiji iliyovunjwa mwishoni mwa Januari mwaka huu baada ya kumaliza muda wake Bibi Bertha Swai, alipokuwa akizungumza na viongozi mbali mbali wa Taasisi za Dini katika mkutano uliofanyika hivi karibuni hapa Jijini.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwakilishi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mratibu wa Maafa Jimbo la Dar es Salam kutoka Idara ya Caritas, Afisa Ustawi wa Jamii Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mkurugenzi Idara ya Dini Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), mwana-Kamati ya Elimu wa Shia Ithnaasheri Jamaati na Mkurugenzi wa Uinjilisti wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam. Wengine Mratibu wa Amana Vijana Centre, Umoja wa Makanisa ya Pentekoste Tanzania UMPT/PCAT, Afisa Maendeleo ya Jamii Kanda ya Kinondoni, Maafisa wa Polisi kutoka Makao Makuu, na Mratibu wa Uwekaji Miji Salama (Safer Cities) Bibi Anna Mtani.

Katika mkutano huo walijadiliana jinsi ya kuwaandaa vizuri vijana kuanzia shule za awali hadi sekondari kwa kuwaelimisha juu ya ubaya wa uhalifu na umuhimu wa elimu ya kujitegemea, ili waweze kufanya kazi za uzalishaji pindi wamalizapo masomo.

Pia vyombo vya dola (Polisi na Mahakama) vimetakiwa visaidiane na taasisi za dini katika kupambana na uhalifu.

Mkutano huo ulisema kuwa uendeshaji wa shule binafsi umekuwa ni wa kibiashara mno na hivyo shule hizo hazitilii mkazo mafundisho ya dini na maadili na ilipendekezwa kuwa shule hizo zifanyiwe ukaguzi wa mara kwa mara na zile zinazoenda kinyume na maadili na utaratibu wa elimu ya Taifa zifungwe.

Wajumbe walijadili jinsi ya serikali inavyotakiwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi za dini ikiwa ni pamoja na kuwalipa walimu wa dini wanaoshiriki kufundisha mashuleni ili kuwahamasisha na kuwatia moyo katika kujenga maadili mema.

Walisema wakati umefika kwa taasisi za dini kuanzisha vyuo vya elimu ambavyo vitatoa walimu waliofuzu vizuri kuchukua wajibu wa kutoa elimu ya dini mashuleni. Hata hivyo taasisi hizo za dini zilivisifu vyombo vya habari vinavyotoa habari za kukemea kuporomoka kwa maadili na kuzuia umaskini.

Ilielezwa kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi za dini kushguhulikia suala la kuimarisha ndoa katika familia na kutoa mafunzo maalumu kwa kionvozi wa familia yaani baba na taasisi za dini zihimize mambo ya maendeleo katika maisha ya jamii.

WAKATI AGIZO LA MENGI LADHARAULIWA:

Serikali yaombwa idhibiti machimbo haramu ya mchanga Tegeta

Na Getruder Madembwe

WAKAZI waishio maeneo ya Tegeta, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wameiomba Serikali iwasaidie kuwadhibiti wachimbaji haramu wa machanga katika maeneo hayo kwani kuna baadhi ya watu wanaoendelea kuchimba licha kupigwa marufuku.

Wakazi hao walisema hayo wiki hii walipokuwa wakiongea na KIONGOZI, kuwa wapo hatarini iwapo tahadhari za kuzia uchimbaji huo haramu wa mchanga hazitachukuliwa haraka.

Walisema kwa sasa hivi wamezungukwa na bonde na hivyo kuwatia wasiwasi pindi mvua za vuli na masika zitakapoanza kwani bonde hilo linakaribia sana na nyumba zao na licha ya kuifikiria mali na nyumba zao wao wanachofikiria zaidi ni wapi watakwenda iwapo kutatokea mmomonyoko mkubwa na mafuriko kutokana na uchimbaji huo.

"Sisi hapa kwa sasa tunakaa tu kwa vile hakuna mvua lakini tabu itakuja pale mvua zitakapoanza kunyesha sasa hatujui maicha yetu yatakuwaje hapo baadaye," alisema mmojawao kwa huzuni akiungwa mkono na wenzao.

Wakazi hao wanashangaa kuona ni jinsi gani polisi wa kituo kidogo cha Mtongani inavyowaachia watu hao wakivunja sheria kwa sababu walishaambiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Hifadhi na Utunzaji wa Mazingira Bw. Regnald Mengi, kuwa watu watakaopatikana maeneo hayo wakichimba mchanga wachukuliwe hatua kali ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Bw. Reginald Mengi aliwataka polisi kufanya doria kila mara ili kuhakikisha eneo hilo halichimwi mchanga na kama mtu au watu wakionekana wakifanya hivyo wachukuliwe hatua kali, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani lakini inaonekana bado hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, kwa mujibu wa wananchi hao.

 

Makandarasi watakiwa wajipendekeze kwa umma

Na Josephs Sabinus

MKUU wa Wilaya ya Temeke Kapteni John Chiligati, amewashauri makandarasi nchini kujenga tabia ya kujipendekeza kwa wananchi ili kujenga majina ya makampuni yao kwa wateja kwa kujenga tabia ya kujitolea kufanyakazi za maendeleo kwa ufanisi badala ya kukazania tu malipo makubwa.

Kapteni Chiligati, alitoa ushauri huo katikati ya juma alipotembelea wilaya yake katika maeneo ya Yombo, Miburani, Mtoni Kijichi na Mwanamtoli katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara za serikali za mitaa.

Alisema kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea kusaidia maendeleo ya jamii ndiyo njia pekee iliyo bora katika kutangaza biashara za makandarasi na hivyo kuwawezesha kupata zabuni nyingi sambamba na viwango vya ubora wa kazi zao.

"Makandarasi ni kama wanasiasa lazima waishi kwa kujipendekeza kuwasaidia na kuwafanyia mazuri wananchi bila kujali tu malipo na hivyo kulipualipua kazi. Inabidi vi-kazi vingine vidogo vidogo msaidie maana mnapofanya kazi nzuri na kujitolea kusaidia baadhi ya kazi, mnakuwa mmejijengea jina zuri na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa kupata tenda. Hata wanasiasa,bila kuwatumikia vizuri wananchi wakakufahamu vizuri utendaji wako, hakuna atakaye kuchagua’ alisema.

Katika ziara hiyo aliyoambatana na Mhandisi wa Kanda ya Temeke Bw. Enoch Kitundu na kutembelea miradi kadhaa ukiwemo wa ujenzi wa kivuko cha miguu kinachounganisha mitaa ya Sigara ya Yombo Vituka kinachojengwa na makandarasi, Odingidi Construction Co. Ltd, na kugharimu shilingi milioni 9.08/=, Kapteni Chilingati aliwahimiza wananchi umuhimu wa kutunza barabara zao na kuondokana na kasumba mbaya ya kutupa takataka ndani ya mifereji.

‘Bila kujali tofauti zenu, shirikianeni kuleta maendeleo hususani barabara mkijua kuwa adui mkubwa wa barabara ni maji. Wenyewe kwa wenyewe kuweni wakali ili mtu yeyote asitupe uchafu ndani ya mifereji na kuifanya izibe," alisema na kuongoza.

‘Lazima mjenge utamaduni wa kiungwana wa kuzibua na kusafisha mifereji na wala msiruhusu ujenzi wowote juu ya mifereji vikiwemo vioski. Misipokuwa makini na kubaki kuwaonea haya wahalifu hawa, tatizo la barabara halitatutoka.

Tunataka hali ya kubeba wagonjwa migongoni kwa kukosa barabara katika karne hii ibaki ni masimulizi tu kwa watoto wetu.’

Aliwaambia viongozi mbalimbali kuwa kwa kuwa sera za Chama cha Mapinduzi kinachotawala ni kuleta maendeleo, basi washirikiane vyema ili wananchi wajenge na kuendeleza utamaduni wa kutumia nguvu zao kujiletea maendeleo na kwamba pale wanapokwama wasisite kuomba msaada serikalini.

Kufuatia malalamiko ya wakazi wa maeneo ya Mtoni Kijichi, Mbagala Kuu na Mwanamtoti juu ya mkandarasi anayetengeneza barabara ya Mtoni Kijichi hadi Mbagala Kuu kuwa mkandarasi hayo UBCO LTD anazembea kazi kwa kurundika vilundo vidogo vidogo vya kifusi barabarani kwa muda mrefu na kusababisha kero katika barabara hiyo yenye urefu wa Km 5.2 kwa tenda ya sh 16,939,000/= Kapteni Chilingati alimwambia Mkurugenzi Mtendaji wake katika kikao cha pamoja na wakazi wa Mwanamtoti kuwa endapo mwenendo wake hataubali na kuboresha kikazi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidhi ya kampuni ikiwa ni pamoja na kuvunja mkataba.

 

‘Watakaolamba’ misaada ya watoto fukara 'kupigwa panga’

Na Dalphina Rubyema

UONGOZI wa Shule ya Msingi itakayobainika kutumia vibaya misaada inayotolewa na Kamati ya kuwasaidia wanafunzi mafukara lakini wenye uwezo darasani (SEF),shule zao zitaondolewa katika mpango huo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw. Issaya Chialo, wakati akikabidhi msaada wa fedha, nguo, na vifaa vya michezo vilivyotolewa na wakazi wa mji wa Nagoya, nchini Japan kupitia kamati hiyo kwa wanafunzi 8 wa shule ya Msingi Kwembe.

Balozi Chialo, alisema kuwa misaada hiyo imekuja kuwasaidia wanafunzi hao wenye uwezo Kitaaluma ili waweze kumudu masomo yao na watasomeshwa na wahisani hao hadi Chuo Kikuu.

"Tutakuwa makini sana katika hilo" alisema na kuongeza kuwa kwa kuzingatia hili ndio maana kamati hiyo imeanza zoezi hilo la kuwasaidia wanafunzi mafukara wa jijini kabla ya kufanya hivyo mikoani.

Balozi Chialo ambaye alikabidhi Sh. 400,000 kwa ajili ya sare na vifaa vingine kwa wanafunzi hao sambamba na nguo zilizotolewa na wakazi hao jambo ambalo ni kielelezo cha utu wema walio nao wakazi hao ambalo linafaa kuigwa na watu wengine hususan Watanzania .

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Ritha Mlaki alijitolea sh. 70,000 kwa ajili ya ununuzi wa mashati kwa ajili ya wanafunzi 27 wa shule hiyo ambao sare zao zilikuwa zimechakaa.

 

Msiniletee za kuleta,Makamba awaambia maafisa wapya Jiji

Na Dalphina Rubyema.

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusufu Makamba amewataka viongozi walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wasije na mambo yasiyoeleweka kutoka huko walikotoka.

Luteni Makamba aliyasema hayo hivi karibuni wakati kuvunja rasmi kwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam na kuundwa kwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ambayo ina manispaa tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni.

"Kwa wale walioteuliwa kutoka mikoa mingine nawaambia rasmi mbele ya Waziri kuwa Head Prefect wa Dar es Salaam ni mimi, hivyo fanya kazi zenu kulingana na utaratibu wa mkoa huu na si vingine," alisema Luteni Makamba, maneno ambayo yalitamkwa mbele ya Waziri wa Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Kingunge Ngombare Mwiru.

Mkuu huyo wa Mkoa pamoja na kutoa kauli hiyo kali pia ameipongeza Tume ya Jiji iliyovunjwa chini ya Mwenyekiti wake Charles Keenja ambapo alisema imefanya kazi nzuri kwa kipindi cha miaka mitatu na miezi saba ilichoshika madaraka.

Wakati huo huo: Waziri wa Tawala za mikoa na Serikali za mitaa Bw. Kingunge Ngombare Mwiru ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuvunjwa rasmi kwa tume hiyo na kuzikaribisha Halmashauri hizo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee amewataka viongozi hao walioteuliwa kuwa wachapa kazi, waadilifu na wabunifu wa mambo mapya.

Alisema kuwa viongozi hao pia watumie nafasi walizopewa kwa manufaa ya umma na si kwa ajili ya kujineemesha wenyewe na katika kulinda haki alitoa ahadi kuwa atajitahidi kupigania maslahi yao ili yaende sambamba na yale ya watumishi wa Serikali.

 

Waunda kamati kudhibiti uhalifu

Na Dalphina Rubyema

KUFUATIA kukithiri kwa vitendo ya wizi na unyang’’nyi katika eneo la Tabata Msimbazi wilayani Ilala katika mkoa wa Dar es Salaam wakazi wa eneo hilo wameunda kamati ya kusimamia ulinzi.

Kuundwa kwa kamati hiyo kumekuja wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni chini ya mwenyekiti wa Mtaa wa Liwiti Bw. John Katindasa, ambapo wajumbe wa mkutano huo wameeleza tatizo la vitendo viovu kukithiri katika eneo hilo ambapo uamuzi wa kuunda kamati uliotolewa.

Katika mkutano huo ilielezwa kuwa vitendo vya watu kukambwa, kuporwa na kupigwa na vibaka vimeshamiri katika eneo hilo ambapo inaaminika kuwa ni watu wanaoshinda katika dampo la Vingunguti na maeneo ya jirani.

Vibaka hao wamekuwa wakiwavizia wakazi wanaotumia njia inayopita bonde hilo kwenda katika eneo jirani la Vingunguti.

Ilifaiwa na wakazi hao kuwa vibaka hao ni vijana ambao hushinda vijiweni bila kazi yoyote ya kufanya.Mbali na hilo wakazi hao wameamua kuunda kamati ya kusukuma maendeleo eneo hilo kubwa zaidi likiwa ujenzi wa kituo cha polisi, huduma ya barabara na maji, mambo ambayo yanaleta utata katika utekelezaji wake kwa kuwa wakazi hao wamevamia na kujenga eneo hilo la bondeni.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Bw. John Katindasa, aliahidi kusaidiana na kamati hiyo kuondoa kero za wananchi hao na amewataka kuwa wazi na kuacha kuwahifadhi wahalifu.