Mkapa mkataze Dakta Salmin asicheze na amani-Waziri

Na Neema Dawson

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ameshauriwa kutumia madaraka yake kumdhibiti Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour na kumzuia kubadili katiba ya visiwani kwa manufaa binafsi, kwani kufanya hivyo ni kuchezea tunu ya thamani ya amani nchini.

Ushauri huo ambao umekuja siku chache baada ya Wabunge wa CCM wapatao 45 kumwandikia barua Rais huyo wa Zanzibar kumuonya juu ya utawala wake wa kimabavu, umetolewa mwishoni mwa wiki na Jumuia ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) katika mkutano wa waandishi wa habari.

Akiongea katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Waziri wa Sheria na Katiba wa Chuo Kikuu hicho Bw. Denis Maringo, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri Rais Mkapa, anao uwezo wa kumdhibiti, ingawa amekuwa akimwachia afanye anavyotaka.

Waziri huyo alisema viongozi wanapaswa kuheshimu katiba kwa hiyo mradi muda wa Dk. Salmin wa kuweza kugombea Urais kikatiba umepita analazimika kuachia madaraka na kubuni shughuli nyingine ya kufanya kum-keep busy.

Akiwa ameongozana na Bw. Stephano Mwalukasa ambaye ni Mbunge wa wanafunzi chuoni hapo na viongozi wengine watatu, Faustine Malecha (Naibu Waziri wa Sheria na Katiba), Owino Maina (Katibu wa DARUSO) na Gideon Ndyamukama, Maringo alisema kama Rais Mkapa ataendelea kumfumbia macho na masikio Dk. Salmin hadi akabadili katiba ya Zanzibar kujinufaisha Jumuia ya Chuo Kikuu itafanya maandamano makubwa kupinga hatua hiyo, kwani huo unaweza kuwa mwanzo wa vurugu zisizoweza kudhibitiwa.

Akizungumzia kufukuzwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar muda mfupi tu baada ya kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza wanachama 18 wa Chama cha Wananchi- CUF wanaokabiliwa na kesi ya uhaini, Maringo alisema anaamini hatua inalenga pia katika kuchelewesha kesi hiyo ili kuwakomoa wanachama hao wa CUF.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour, amekuwa akishutumiwa vikali kwa kutaka kubadili katiba ili kuweza kugombea tena Urais kwa mara ya tatu. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kama ilivyo ile ya Jamhuri ya Muungano mtu mmoja anaruhusiwa kugombea urais kwa vipindi visivyozidi viwili vya miaka mitano mitano, kwa hiyo Dk Salmin ambaye anamaliza kipindi chake cha mwisho mwaka huu hastahili tena kugombea.

Miongoni mwa watu wazito waliojitokeza hadharani kumshutumu Rais Salmin ni Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Jaji Joseph Warioba ambaye aliifananisha hatua hiyo na kurejesha utawala wa Kisultani visiwani humo.

Baadaye Wahadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakipinga mabadiliko hayo ya katiba pia walisema Dk. Salmin si Rais anayeweza kutambulika kimataifa kwa sababu Zanzibar haina hadhi ya nchi, bali sehemu yake na ndio maana haina hata jeshi. Kauli hiyo kwa mujibu wa vyombo vya habari imepelekea wanasheria hao Dk. Harrison Mwakyembe, Dk. Sengondo Mvungi, Dk. Palamagamba Kabudi na Dk. Aggrey Mlimuka, imesababisha waitwe Bungeni Dodoma kujieleza.

Waubge 45 wa CCM waliomwandikia barua Dk Salmin walikuwa wakimtaka afute mara moja kesi ya uhaini dhidi ya wanachama hao 18 wa CUF kwani hata Mwanasheria wa Serikali ya Zanzibar alishatamka mahakamani kwamba kesi hiyo ni ya kisiasa.

Mahujaji watakiwa kuuombea Uchaguzi Mkuu ujao

Na Dalphina Rubyema

MAHUJAJI wa Kanisa Katoliki walioondoka nchini mwanzoni mwa wiki kwenda katika hija ya Jubilei Kuu katika nchi takatifu ya Israeli,pamoja na kupeleka maombi mbalimbali yaliyomo katika mioyo yao, vilevile wametakiwa kuliombea taifa amani na utulivu katika uchaguzi Mkuu wa Rais wa wabunge utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wito huo ulitolewa na Askofu wa Jimbo la Rulenge, Mhashamu Severine

Niwemugizi, wakati wa misa takatifu iliyowashirikisha mahujaji hao saa chache kabla ya kuondoka nchini iliyofanyika katika kanisa la TEC.

Mhashamu Niwemugizi ambaye ni miongoni mwa watu 28 walioshiriki hija hiyo siku kumi alisema kuwa hivi sasa Taifa linaelekea katika kipindi kigumu cha uchaguzi Mkuu hivyo mahujaji hao hawanabudi kutoa sala maalum kwa ajili ya kuliombea Taifa la Tanzania utulivu na amani na kuwa na uchaguzi huo ni wa haki.

"Pamoja na kuombea mambo mbalimbali tunayokwenda nayo mioyoni mwetu vile vile tuweke sala maalum ya kuliombea Taifa letu tulivu na amani katika kipindi cha uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge" alisema Askofu Niwemugizi.

Awali katika kikao cha maandalizi kwa mahujaji hao Mratibu wa hija hiyo Padre Theobald Kyambo alisema kuwa mahujaji hao watakapoingia katika nchi hiyo takatifu watatakiwa kuvaa kichwani kofia zenye bendera ya Tanzania kwa ajili ya kutangaza utaifa wao ambapo kila mmoja aliondoka na kofia hiyo yenye rangi ya njano.

Aliwatahadharisha mahujaji hao kuwa asisahau kuvaa kofia hizo zaidi ni wakati wa kuingia hekaluni ambako hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia huko bila kufunika kichwa.

Hija hiyo imewashirikisha Maaskofu 6 ambao ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhamana Polycarp Kardinali Pengo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini wa jimbo la Musoma Mhashamu Justine Samba, Askofu wa jimbo la Rulenge Mhashamu Seveline Niwemugizi, Askofu wa jimbo la Shinyanga, Mhashamu Alosius Balina, Askofu wa jimbo la Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude na Askofu wa jimbo la Moshi Mhashamu Amedeus Msarikie, washiriki wengine ni padre Julian Kangarawe, Bro. Jose Varghasse, Bi. Fedilika Lyimo, Sr. Filothea Kiseda, Bi. Rosemary Makongoro, Bw. Edward Masika toka jimbo la Dar es Salaam na jimbo Dodoma washiriki ni padre Onesmu Wissi, Bw. Stephen Masangia na Bi. Oliver Masangia. Jimbo Kuu la Songea limetoa washiriki wawili ambao ni Br. Ayubu Alois Mbepera na Bw. Adam Mwendo wa saa, ambapo jimbo la Same walioshiriki hija hiyo ni padre Andrew Kidaisho, Bro. Valence Mkwizu, Bi. Rose Mdee na Bw. Joseph Mkomba na jimbo la Moshi washiriki ni Padre Agapit Aman na Sr. Piala Olemi washiriki wengine ni Bw. Paskal Nade (Mbulu) Bi. Christina Van Laak,(Morogoro), Bw.Dustin Komba (Mbinga). Bw. Mathias Kiazile (Njombe) na hawa wamesindikizwa na mratib wa shughuli zote za hija hii nchini Theobald Kyambo.

Watanzania watakiwa waachane na demokrasia takataka

WATANZANIA kote nchini wametakiwa kutojihusisha kabisa na mwenendo wowote potofu hata ukibatizwa jina la demokrasia wakati wanajua dhahiri kuwa hatima yake si kitu kingine, bali ni mauti.

Onyo hilo kali limetolewa na mtaalamu mmoja wa masuala ya maadili katika Seminari Kuu ya Kiteolojia ya Segerea jijini Dar es Salaam alipkuwa akitoa mada katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na wanafunzi Wakatoliki (TYCS) tawi la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na kuwahusisha wawakilishi kutoka sekondari na vyuo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jumapili iliyopita..

"Hata nyie watu wa ndoa, muwe na kiasi na muwe na adabu na utaratibu katika ndoa zenu. Msifanye mambo ya kipuuzi kwa kisingizio cha teknolojia na demokrasia. Teknolojia na demokrasia ziinazopingana na mapenzi ya Mungu ni takataka."

"Hiyo teknolojia takataka ndiyo muifanye hata badala ya watoto kuzaliwa ndani ya ndoa takatifu, wakazaliwe toka kwenye chupa, kwa kisingizo cha teknolojia na demokrasia?

Ndivyo alivyohoji kwa uchungu Mtaalam wa Maadili katika Seminari hiyo ya Segerea Padre Damian Dallu, alipokuwa akitoa mada katika semina hiyo juu ya ndoa na mahusiano ya Kijinsia iliyofanyikia DIT jijini.

Alisema maendeleo ya Sayansi na Teknolojia hayapaswi kuwa kigezo cha kufanya mambo kunyume na mapenzi ya Mungu na akailaani hatua ya Bunge kuridhia na kujiunga na kituo cha kimataifa cha Uhandisi wa Kijenetiki na kibaioteknolojia.

Aidha, Mtaalam huyo Padre Dallu, alisema hali ngumu ya maisha isigeuzwe kuwa kisingizio cha vijana kujihusisha na vitendo vya ufuska vikiwemo ushoga na usagaji vinavyozidi kushamiri katika magareza, shule na vyuo vyenye mabweni ya jinsia moja na akasisitiza umuhimu wa kila mtu kujilinda dhidi ya tamaa mbaya na hivyo kuepukana na vitendo vya utoaji mimba na madhara ya kiafya kiroho na kisaikolojia.

Alisema tendo la ndoa ni halali kwa wenye ndoa iliyobarikiwa na kujihusisha nalo nje au kabla ya ndoa au kinyume na maumbile ni dhambi kubwa inayoweza kusabababisha mauti na magonjwa hatari ya zinaa ukiwemo Ukimwi "Ukiendekeza uzinzi ili baadaye eti uzae, huku unadanganywa kwa kufunga uzazi; mjue mnafanya dhambi na unaweza usimpate kabisa mtoto' alisema.

Novemba, mwaka jana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliridhia kwa kauli moja, kujiunga na Kituo cha Kimataifa cha Uhandisi wa Kijenetiki na Kibaioteknolojia ambapo wananchi wengi walikasirishwa na hatua hiyo hata viongozi wa dini wakiwemo Masheikh, Maaskofu na Wachungaji wamekuwa wakitoa maneno makali kushutumu hatua hiyo, ambayo ilielezewa na gazeti moja la kila siku kuwa inatoa ruksa kwa watu kubadili jinsia zao.

Uchunguzi wa gazeti hili hata hivyo ulibaini kuwa Serikali ilichukizwa na tafsiri ya vyombo vya habari kuwa azimo hilo linamaanisha kuwa Watanzania sasa wanaruhusiwa kubadili jinsia zao kwa maana kwamba mwanamke kuwekewa viungo vya mwanaume na mwanaume kuwekewa vya kike na pia kwamba mtoto anaweza kupatikana kwa kuchanganya madawa katika maabara.

Gazeti hili lilipokuwa likifuatilia kupata ufafanuzi kutoka Wizara ya Sayansi na Teknolojia Novemba, mwaka jana, Wizara hiyo iliahidi kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuwaeleza wananchi ukweli wa jambo hilo, lakini hadi leo bado ufafanuzi huo haujatolewa. Spika wa Bunge Mheshimiwa Pius Msekwa, aliliambia gazeti hili kwamba kilichoelezwa na magazeti ni porojo tu, lakini pia hakutaka kufafanua mkataba huo kwa maelezo kuwa ni kazi ya Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu.

Mliookoka,okokeni kimatendo - Mchungaji aonya

Na Mwandishi Wetu

WAKRISTO wanaoamini na kujitangaza kuwa wameokoka wametakiwa waoneshe uokovo wao kimatendo kwa kuachana na njia mbaya na badala yake kufanya yanayompendeza Mungu.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (K.K.K.T) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Ajuaye King’omela, katika ibada ya ufunguzi wa mfuko wa ujenzi katika ushirika wa kawe.

Alisema ingawa wengine wamekuwa wakijitangaza na kushuhudia hadharani kuwa wameokoka baadhi yao wamekuwa wakiendeleza matendo maovu yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

"Wengine wakiokoka hawaachi mambo yao yale mabaya utakuta bado wanaendelea na uchawi, wizi usengenyaji, uchoyo, fitina na mengine mabaya anayosema ameacha.." alisema kwa mshangao.

Katika tukio hilo linaloambatana na Mchungaji Moses Maarifa aliyetokea katika Usharika wa Magomeni Mviringo kuwekwa kazini katika Usharika huo, Mchungaji King’omela pia aliwataka Wakristo kuombeana mema kwani amuombae mwenzie mabaya kwa sababu yoyote hatafika mbinguni.

"Hata Yesu Kristo hakuneneana mabaya na wanafunzi wake na aliongea na wenye dhambi ikiwa ni pamoja na yule mwanamke Msamaria; alipoongea na wanafunzi wake wakamkuta pale kisimani, hawakumfikiria vibaya sasa iweje wenyewe kwa wenyewe au vikundi kwa vikundi au hata ofisi na ofisi mfikiriane nahata kuneneana mabaya"? Alihoji Mchungaji King’omela

TRA yataka michanganuo kabla ya msamaha wa kodi

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezitaka taasisi za kidini kupeleka michanganuo ya miradi yao ili kukomboa mizigo yao iliyokwama bandarini ikidaiwa kodi,kwa vile hata baadhi ya wachungaji hutumia misamaha ya kodi kujinufaisha.

Mkurugenzi wa Elimu kwa walipa Kodi wa TRA , Bw. Protas Mmanda aliyasema hayo alipotakiwa na gazeti hili kutoa ufafanuzi juu ya mizigo ya taasisi za kidini inayong’ang’aniwa bandarini ikidaiwa kodi hali nayo imetajwa miongoni mwa mizigo inayostahili kusamehewa.

Alisema ingawa Serikali imetoa msamaha wa kodi kwa mizigo ya taasisi za dini inayohusu elimu, afya, maji na ibada; taasisi husika hazina budi kuambatanisha mchanganuo wa vifaa hivyo (Project Writte up) ili kuiwezesha mizigo hiyo kuchukuliwa na akazita taasisi husika kutofautisha michanganuo hiyo na barua zinazoambatana na mizigo.

"Sidhani kama kuna taasisi iliyokwishaleta Project Write up iliyiosainiwa na Askofu wa jimbo ama Shirika, ama Sheikh halafu mzigo wake ukaendelea kukwama. Hatujapata kitu cha namna hiyo, sisi tunacholetewa ni barua tu, ambazo hatuamini kama zina ukweli" alisema Mmanda na kuongeza.

"Hatuna nia mbaya na taasisi za kidini na tunaelewa zinatenda kazi zao vizuri na kwa uaminifu; ila kuna watu wachache hutumia mwanya huo kujinufaisha wenyewe na hivyo kuzichafulia jina taasisi husika."

Akifafanua usemi huo, Mmanda alisema hivi sasa yameibuka makanisa mengi madogo madogo ambayo viongozi wake wanaruhusiwa kuoa na kuwa na familia na hivyo baadhi yao hutumia majina ya makanisa kujinufaisha wao binafsi na familia zao.

"Wengine wanajiita wachungaji, wakipata msaada mfano, mabati 300, badala ya kujenga kanisa kubwa kama ilivyokusudiwa, wanajenga kakanisa kadogo tu, bati zinazobaki anajenga nyumba yake... zile project Write up zinatusaidia kuwabana watu kama hawa"

Ingawa alikiri kuwa zoezi hilo linaziathiri taasisi nyingi alishikilia msimamo wa kutoubadili na alipotakiwa kutaja taasisi zinazotumiwa na watu wake vibaya, alikataa kufanya hivyo kwa madai kuwa ni kuzua migogoro isiyo ya lazima. Pia hakuwa tayari kutaja kiasi cha hasara ambacho serikali imepata kutokana na misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini.

Waislamu waanzisha kituo cha Yatima

Na Mwandishi Wetu

JUMLA ya watoto 96 waliofiwa na wazazi wanatarajiwa kupokelewa katika kituo cha kutunzia yatima cha Dar al- Arqam kilichopo Tandika wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ifikapo mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Yatima waliopokelewa mpaka sasa katika kituo hicho ni 60 kwa mujibu wa Bw. Hassan A. Majeja, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu inayotoa msaada kimataifa (International Islamic Relief Organisation).

Aidha kituo cha yatima kinachomilikiwa na taasisi hiyo (I.I.R.) Mkurugenzi Majeja ametaja masharti ya kupokea yatima kwanza umri wake uwe miaka saba.

Yatima hupatiwa elimu ya msingi hadi wanapofikia umri wa miaka 15, ameongeza na wanaachiliwa kwenda kujitafutia maisha makwao.

‘Watoto wanaotunzwa katika kituo chake hawatozwi malipo yoyote’ amesema na kuongeza kituo chake kilichojengwa 1994 kinapewa misaada toka taasisi binafsi ya Saudi Uarabuni.

Pia I.I.R.O linalojihusisha na kutoa misaada kwa watu wanaopatwa na maafa kwa mfano mafuriko na vita, amesema.

Juu ya zawadi ya ng’ombe mmoja aliyetolewa na Rais Benjamin Mkapa kwa kituo chake kwa ajili ya sikukuu ya Idd el Fitril hivi karibuni amemshukuru rais kwa upendo huo.

‘Kunaonyesha wazi jinsi Rais anavyowajali yatima’ amedai na kusisitiza ‘ kwani utoaji wa zawadi kila sikukuu kwa vituo vingine vya yatima kunawapa faraja kubwa’

Waislamu wa Ahmadiyya wadai BAKWATA inawakandamiza

Na Christopher Udoba.

MAKAO Makuu ya Ahmadiyya Muslim Jamaat hapa nchini yanalalamikia Baraza Kuu la Kiislamu Nchini (BAKWATA) kuwa linawanyima haki ya kutangaza imani yao kwenye Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD).

Amiri wa Jumuia hiyo, Muzaffar A. Durran, amedai hayo katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni.

Pia katika mahojiano hayo yaliyofanyika makao Makuu ya Ahmadiyya jijini Dar es Salaam, Amiri Durran, ameongeza kuwa BAKWATA imekuwa ikiwanyima nafasi ya kutumia RTD tangu miaka ya 1980.

Sababu ya kunyimwa haki hiyo Amiri Durran amedai inatokana na Ahmadiyya kutotambuliwa kuwa miongoni mwa Waislamu safi hapa nchini.

Jumuia hiyo pia imekuwa ikiwanyima kibali cha kujiunga na BAKWATA kutokana na tofauti hizo, amesisitiza na kuongeza kuwa kwa Ahmadiyya kutakataliwa kujiunga nao si kitu sana kwanza.

"Si kweli kuwa Ahmadiyya Muslim Jamaat hawatambuliwe kama Waislamu wengine" Shehe Hassan Chizega, Mkurugenzi wa Idara ya Dini katika BAKWATA amekanusha katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini.

Pengine Ahmadiyya wanatafuta sababu za kutaka kudai jambo fulani tu, Mkurugenzi Chizenga ameongeza juu ya hayo Mkurugenzi huyo ameshangazwa na madai ya kutaka wao wapatiwe nafasi kenye RTD kwa ajili ya kutangazia mafundisho yao.

Amefafanua kuwa madhehebu ya Sunni ndiyo yanayowakilisha Waislamu wengine hapa nchini katika kuandaa vipindi kwa ajili ya kuvitangaza redioni kupitia BAKWATA.

Katika madhehebu ya Sunni ameyataja pia kuwa kuna shafi,Malik, Hanbal na Hanafi; yanayowakilisha shia, Bohora na ibadhi.

Pamoja na hayo Waislamu wengi hawaoneshi kuwatambua Ahmadiyya kwamba nao ni miongoni mwa waislamu kwelikweli, Mkurugenzi amejikanyaga kwa maelezo

Mashemasi watakiwa wawe makini katika utamadunisho

Na Getruda Madembwe

MASHEMASI wa Kanisa Katoliki wameaswa kutozichanganya mila au desturi za maeneo wanayopangiwa kufanyakazi na imani Katoliki na hatimaye kuzigeuza na kuzitumia kama njia ya wokovu, bali tu, wazitunze zilizo njema kwa manufaa ya jamii.

Kauli hiyo yenye changamoto ya kiroho ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alipokuwa akitoa daraja la Ushemasi kwa mafrateri 21 wa Kanisa hilo katika Seminari Kuu ya Kiteolojia ya Segerea jijini dar es salaam wiki iliyopita.

Alisema ingawa mila nyingine za baadhi ya maeneo ni nzuri na zinastahili kuendelezwa kwa manufaa ya jamii, bado hawana budi kuziacha zilivyo na kamwe wasijaribu kuzigeuza na kuzifanya njia ya wokovu.

"Msianze kuchukua mila na desturi mnazozikuta mahali mnapokwenda kufanya kazi ya Mungu, mkazigeuza kuwa njia ya wokovu, bali mnaweza kuzitunza ambazo hazina madhara," alisema Pengo.

Aliwataka Mashemasi hao kuifanya kazi ya kuhubiri Injili mahali pote bila kuchagua maeneo kadhaa wanayopenda wao kwani hata Yesu Kristo aliwaagiza wanafunzi wake kuihubiri Injili duniani kote pasi na Ubaguzi.

"Mnatakiwa muende ulimwenguni kote kuihubiri Injili, sasa iweje uanze kuchagua eneo la kazi badala ya kwenda ulipopangiwa kufanya kazi ya Mungu?" alihoji Kardinali, Pengo kwa msisitizo na kuongeza, "mnapewa daraja la ushemasi kwa ruhusa ya maaskofu wenu, hivyo mnapaswa kuwatii, maana ushemasi ni sehemu rasmi ya Kanisa na mahali mnapofanya kazi ni sehemu ya kanisa pia".

Aidha aliwatahadharisha kutogubikwa na wingu la tamaa ya mali binafsi bali wawe wasafi mbele za Bwana kama wito wao unavyowataka kuwa .

Msalaba wa Jubilei waibiwa Kanisani, 'Yesu' achomolewa

lPolisi ang’atwa kidole akifuatilia

KATIKA mazingira ya kutatanisha, Msalaba wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 wa Jimbo Katoliki la Rulenge umeibwa Kanisani na mbao zake kutelekezwa vichakani na sasa kilio cha "Wamekuweka wapi Bwana wangu" kimetanda jimboni humo; na ili kufuata ratiba ya mzunguko wa Msalaba huo, jimbo limelazimika kutumia msalaba mwingine wa kawaida, imebainika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mkoani Kagera na Katibu Mtendaji wa Idara ya Upashanaji Habari, Jimbo la Rulenge, mkoani hapo, Padre Ivus Tindyebwa, tukio hilo lilitokea Januari 16, mwaka huu usiku katika Parokia ya Rwinyana.

Taarifa hizo zinasema Paroko Msaidizi wa Rwinyana, Padre Justin Bukoma, aligundua wizi huo Januari 17, mwaka huu. Habari zinasema ingawa mlango wa Kanisa ulifunguliwa kiufundi, hakuna kingine kulichoibiwa mbali na Msalaba huo wa Jubilei na ule mdogo wa altareni.

Akizungumzia tukio hili jijini wiki iliyopita, Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Severin Niwemugizi, alisema waamini waliposhirikiana na polisi kufuata nyayo za wahalifu, waliambulia mbao bila sanamu ya mwili wa Yesu iliyofunguliwa kiufundi na wezi kuondoka nayo kabla ya kuzitelekeza mbao hizo za msalaba kichakani.

Alisema katika kumhoji kijana mmoja mshukiwa, alimng’ata kidole askari polisi wa kituo cha Rulenge na sasa anashikiliwa na polisi akisubiri kushitakiwa kwa kosa la kumshambulia askari akiwa kazini.

Tukio hili limezua hisia tofauti wilayani Ngara, wengine wanadhani sanamu hiyo imekwenda kuuzwa ili wezi wajipatie donge nono, na wengine wanadhani ni kwa ajili ya kufua na kutengeneza risasi ama kwa ajili ya wapiganaji wa Rwanda .

Wanawake Wakatoliki wakolee'munyu'

Na Waandishi Wetu

KATIBU wa Wamama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa (RWSAT), Sista Fides Mahunja amewahimiza Masista Wahasibu ambao ni wataalamu wa masuala ya Usimamizi wa fedha kuwa chachu na chumvi ya kuutumikia uanadamu ili kuendeleza ufalme wa Mungu kufuatia utendaji wao bora.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu ya TEC, Padre Elias Msemwa katika ufunguzi wa warsha ya wiki mbili iliyomalizika Jumamosi hii katika ukumbi Kituo cha kiroho cha Mbagala Spritual Centre jijini, Sista Mahunja, alisema masista hao (masista) wa majimbo na taasisi mbalimbali za Kanisa Katoliki hawana budi kuishi maisha na utendaji unaogusa na kuwa mfano bora wa unabii kwa wenzao.

"Tunatakiwa kugusa maisha ya wengine kama manabii wanaotia Changamoto kwa wenzao tukiwa walimu waletao ukweli, waponyaji wanao unganisha na kuondoa mgawanyiko, kama watumishi wanaotembea na wenzao na pia kama mashahidi wa kumuiga Kristo ili kujifunza namna ya kulea familia ya Mungu" alisema Sista Mahunja.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwa RWASAT na kuendeshwa na Shirika la CORAT AFRICA, Padre Msemwa alisema kuwa ni ndoto ya mchana kutegemea kuwa maendeleo ya haraka yatapatikana bila kuwa na timu imara yenye wataalamu wenye ujuzi wa kutosha katika masuala ya usimamizi wa fedha.

Aliwataka washiriki wa warsha hiyo kubuni, kubajeti, kusimamia vema na akaongeza kwamba kutoa ripoti muhimu kunahitaji utaalamu wa kutosha ili kuleta ufanisi na kujenga imani miongoni mwa jamii.

"Ni ndoto ya mchana kudhani kuwa tutaharakisha maendeleo bila kuwa na timu imara katika usimamizi wa fedha... msimamizi yeyote mzuri hana budi kuwa makini katika takwimu zake za mapato, matumizi na akiba na kuona kuwa ni kamilifu, sahihi, zilizo wazi na zinazokubalika na hata kuzitunza vema" alisema Padre Msemwa na kuongeza

"Si tu kwamba watu wa fedha mnatakiwa kujali tu,kubana bajeti za mashirika yetu, bali pia kufuata muundo sahihi wa ukaguzi"

Aidha, aliwashauri wataalam hao kujenga utamaduni wa kukarabati mali za kanisa hususan zisizo hamishika kwani zinahitaji gharama kubwa kupata nyingine.

Wakati huo huo: Akizungumza na gazeti hili nje ya warsha hiyo mmoja wa washiriki ambaye ni mwalimu wa CORAT AFRICA Bi. Victoria Mutiso, alisema watumishi na mashirika ya kikanisa hawana budi kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali badala ya kutegemea misaada kwani hivi sasa wafadhili wengi wamepunguza kasi yao.