Walokole wapigwa marufuku kusalimiana 'Bwana asifiwe'

lHatua hiyo yazua kasheshe na kumfanya mchungaji asuse kanisa

lKadhalika waumini watakiwa kutosalimiana kwa Shikamoo

Na Arnold Victor, Kibaha

KANISA la Pentekoste nchini (KLPT) limewataka waumini wake kuachana na salamu yao maarufu ya "Bwana asifiwe," kwa vile imegeuka ya kinafiki.

Akihubiri katika semina iliyowashirikisha waamini wa Kanisa hilo Wilaya ya Kibaha, katika Kanisa la Mailimbili, Mwangalizi (Askofu) Mkuu wa kanisa hilo, Mchungaji Philemon Tibanenason, alisema salamu ya Bwana Asifiwe hivi sasa imekuwa fasheni hata kwa walevi kwenye mabaa na haina tena heshima kama iliyokuwa nayo mwanzoni.

Askofu huyo alisema matumizi ya salamu hiyo kama ishara ya waliookoka sasa hayana maana tena kwa vile imekuwa ikitumiwa vibaya na watu wasiostahili kufanikishia unafiki na utapeli wao.

Badala ya salamu hiyo, Askofu huyo sasa amewataka waumini wake wasalimiane "Shalom" neno la Kiyahudi lenye maana ya "Amani."

Hata hivyo, habari zinasema mara baada ya semina ya Askofu kumalizika, Mchungaji wa Kanisa hilo la Mailimoja, ambako semina iliendesha Mch. Frederick Makulala, alitoa mafundisho yaliyopingana na yale ya Askofu wake juu ya matumizi ya salamu hiyo akisisitiza kuwa haijapitwa na wakati, na kwamba kutumiwa vibaya kwa salamu yoyote hakuwezi kuzuilika.

Askofu Tibanenason, pia alisema Wakristo wa Kanisa lake hawapaswi kuambiana "shikamoo" kwa vile asili ya salamu hiyo ni kuabudu watu na ilitokana na utumwa wa Waafrika kwa Waarabu.

Hatua hiyo ya Mchungaji Makulala (49) ambaye mwaka jana alikabiliwa na kesi Mahakamani ya kumbaka muamini wake Bi. Consolata Ngonyani (26) lakini Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Bi. Pelagia Khodai, akamwona hana hatia, ilimletea mfarakano mkubwa na waamini wake.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kanisani hapo Mchungaji huyo alipopata upinzani kutoka kwa waamini wake, wiki iliyopita aliamua kukabidhi kanisa kwa Askofu na kutoweka.

Salamu ya Bwana Asifiwe ilianzishwa na kuenezwa na jamii ya Wakristo Wapentekoste zaidi ya miaka 50 iliyopita na baadaye kuambukizwa hadi kwa baadhi ya madhehebu makubwa ya kiprotestanti wakiwemo Walutheri na Waanglikana.

Baadhi ya madhehebu wamekuwa wakitumia salamu kama vile "Uhuru wa Yesu" na kujibizana "Ni wa milele."

Kadhalika yapo baadhi ya madhehebu Wasabato na Mashahidi wa Yehova ambao kwa kawaida hawana salamu yoyote rasmi.

Serikali isipambane na vyama bali wahalifu-Askofu Sambano

lAtumia Biblia kukanusha sera ya ‘jino kwa jino’Z.bar

Na Neema Dawson

SERIKALI ya Jamhuri na ile ya Zanzibar zimeshauriwa kupambana na watu wanaosababisha ghasia kwa sababu za kisiasa kama wahalifu binafsi badala ya kuwahusisha na vyama vyao, kwani kufanya hivyo kunaleta uwezekano wa kuhatarisha zaidi amani.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Askofu wa Kanisa la Kianglikana, Dayosisi ya Dar Es Salaam, Basil Sambano, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili Ofisini kwake.

Alishauri serikali zote kuwa makini zaidi wakati zinapo washughulikia watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa chama cha wananchi cha CUF, walioanzisha fujo huko visiwani Zanzibar hivi karibuni na kusababisha askari polisi kadhaa kujeruhiwa na kunyanganywa silaha baada ya kutaka kuzuia mkutano wa ndani wa CUF.

Alisema tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa Pili wa vyama vingi Oktoba Mwaka huu, serikali haina budi kutumia nguvu zake zote kulinda amani, usalama na haki za wananchi na wala usiwepo mwanya kwa wachache wanaotumia vigezo vya vyama vya kisiasa kujipatia umaarufu na hivyo kuvuruga amani ya nchi.

"Wendawazimu ni baadhi ya wale wanaojiita kuwa ni viongozi na wanachama wa CUF waliofanya fujo na si chama. Hivyo inatakiwa iwashughulikie wahusika kwa uangalifu kama watu binafsi na si chama kwani chama hakihusiki; anayehusika ni mtu aliyejeruhi.

Tukio la watu wachache waliofanya vurugu kwa kukitumia chama kwa kuwajeruhi askari halikunifurahisha kwani ni kinyume cha utu, amani na upendo.

Chama chochote kile hakifanyi fujo bali wanaofanya fujo ni watu walio na akili timamu hivyo ni kazi yetu kuwaonya watu na si vyama vya siasa vilivyopo , kwani chama hakiwezi kushika silaha bali binadamu," alisema Askofu Sambano.

Aliendelea kusisitiza kuwa viongozi wa dini kama raia, na wala sio "visiwa", hawana budi kuzidi kuiombea amani serikali ya Tanzania na kukemea vikali kila panapoonekana kuweza kuleta machafuko kwa taifa bila kujali chama , kabila , dini, jinsia wala tabaka la mtu au kikundi.

Alisisitiza maneno ya Yesu katika Biblia, (Math.5:38-42) yasemayo, "Mmesikia kwamba imenenwa jicho kwa jicho na jino kwa jino lakini mimi nawaambia msishindane na mtu mwovu, lakini mtu akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la kushoto na mtu atakaye kukushitaki na kutwaa kanzu yako, mwachie na joho pia na mtu atakaye kulazimisha mwendo wa maili moja nenda naye mbili; akuombaye mpe."

Hivi karibuni chama cha CUF kilitangaza kutumia sera ya jino kwa jino na jicho kwa jicho wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao kwa madai ya kwamba ni njia ya kudhibiti uchaguzi huo ili haki itendeke.

Hata hivyo hoja hiyo imetafsiriwa kuwa yenye lengo la kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi na imekemewa na jamii kubwa ya Watanzania wanaopenda amani.

Msishabikie mauaji - Wito

Na Elizabeth Steven

WITO umetolewa kwa jamii ya Watanzania kutoshabikia mauaji yoyote yakiwemo ya vibaka na vikongwe wanaotuhumiwa kwa ushirikina kwani kufanya hivyo ni kuvunja Amri ya Tano ya Mungu inayozuia mauaji.

Akitoa mada katika siku ya mwisho ya semina ya teolojia ya maadili iliyoandaliwa na Umoja wa Wanataaluma Wakristo (CPT), Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Pius Rutechura alisema,

"Inashangaza baadhi ya watu wanakuwa washabiki wa mauaji, mfano mzuri kama mwizi ameshikwa na tayari hana ujanja wa kumdhuru mtu, ni vizuri badala ya kushabikia muue! Muue! mkamfikisha katika ngazi zinazohusika ili aadhibiwe kiroho au kisheria.

Kushabikia mauaji au hata eti sisimizi, unampiga kwa rungu ukutani, hii inaonesha unaishi maisha ya hofu," alisema.

Alionya dhidi ya kutawaliwa zaidi na tabia mbalimbali zinazowanyima nafasi na muda wa kufanya mambo mema ya Mungu na akaiita tabia hiyo kama ni kuwa na vimungu vya ovyo ovyo.

"Wengine wametawaliwa na mambo ya dunia kama, mfano mtu anasema ni lazima kila siku nisikose kipindi cha TAUSI, sasa tabia kama hizo ni sawa na kukifanya kitu kuwa mungu. Kuwa na vimungu vingi vingi bila mpango ni utumwa,"

Akijibu swali la mshiriki mmoja aliyetaka kujua kama kwenda kupata tiba kwa waganga wa jadi ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu, Padre Rutechura alisema, " Kupata tiba za jadi sio tatizo, tatizo linakuja pale ambapo mtu anakwenda kwa mganga ili kupiga ramli na kuongeza imani za ushirikina kwa kutafuta aliyemloga.

Waganga wengi ni matapeli wanaochezea akili za watu hasa wenye shida. Waganga wa kweli walio wengi huwa hawatozi pesa bali mgonjwa mwenyewe ndiye hupeleka baada ya kupona.

Na shida hii inakuja pale ambapo hata wasomi wengine wanataka njia za mkato. Vitu vyote vya kutumia njia ya mkato kufikia malengo, ni vya mashaka sana," alisema.

Waenda kwa miguu 1900 wafariki kwa ajali nchini

Na Josephs Sabinus

ZAIDI ya waenda kwa miguu 1903, wamefariki dunia katika ajali mbalimbali za barabarani nchini kote katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliyopita.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, ACP, Luther J. Mbuthu ameliambia KIONGOZI ofisini kwake hivi karibuni kuwa matukio mengi ya waenda kwa kwa miguu kuhusika katika ajali za barabarani yamechangiwa pia na ukosefu wa elimu na uzoefu wa kutumia barabara hususani kwa watu wengi wanaohamia mijini toka vijijini na hivyo kushindwa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani.

Sababu nyingine ni kulewa pombe karibu na barabara kuu, kufanya maongezi katikati ya barabara na kushindwa au kukataa kutumia vivuko vya waenda kwa miguu.

"Watembea kwa miguu kukataa kutumia kivuko cha daraja lililoko eneo la Manzese jijini, ni moja ya mifano hai inayopelekea kundi hili la watumiaji wa barabara kuathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na ajali za barabarani," alisema ACP Mbuthu.

Akifafanua takwimu hizo kwa maandishi, kamanda huyo alisema mwaka 1997, waenda kwa miguu 663, walifariki na 3565 kujeruhiwa. Mwaka 1998, walifariki 619 na waliojeruhiwa walikuwa 3179 . Mwaka jana, waenda kwa miguu 621, kwa mujibu wa takwimu walizo nazo, walifariki wakati 3883 walijeruhiwa.

Alisema kila mtumiaji wa barabara ana wajibu kuhakikisha analinda usalama wake na watumiaji wengine wa barabara.

"Kwa upande wa madereva, wajibu huu umeelezwa kwa kina kwenye kifungu Na. 50 cha Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973 kama kilivyorekebishwa na kifungu Na. 11 cha Sheria ya Usalama Barabarani Na. 16 ya mwaka 1996"

"...Wajibu wa mtembea kwa miguu umeelezwa katika kifungu Na.65 Cha Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973 kama kilivyorekebishwa na kifungu Na. 15 cha Sheria ya Usalama Barabarani Na. 16 ya mwaka 1996," alisema.

Aliongeza kuwa kifungu hiki kinaelekeza jinsi gani anatakiwa kutumia barabara ikiwa ni pamoja na kuzingatia mwendo na umbali yalipo magari kabla ya kuanza kuvuka barabara.

"Kushindwa kwa mtumiaji wa barabara kuzingatia maelekezo ya kanuni na Sheria za Usalama Barabarani, ndicho chanzo cha ajali nyingi zitokeazo hapa nchini..." alisema na kuongeza kuwa ili kukabiliana na hali hii, Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na idara nyingine za serikali na taasisi zinazojihusisha na masuala ya usalama barabarani, limekuwa likitoa mafunzo mashuleni.

Mkuu wa Wilaya kutekeleza falsafa ya toa kwanza boriti

Na Agatha Rupepo, DSJ

MKUU wa wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani Kapterni James Yamungu,amewataka viongozi wa ngazi zote wilayani kwake kupalilia mashamba yao ya mikorosho ili wawe mfano bora wa kuigwa na wananchi vinginevyo atawachukulia hatua za kisheria.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili mjini Kisarawe juma lililopita, Kapteni Yamungu alisema, "Ninatarajia fanya ziara ya kukagua mashamba ya viongozi halafu yatafuatia mashamba ya wananchi ili iwe mfano kwa wananchi wengine kujifunza kutoka kwa viongozi wao," alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema operesheni hiyo itawajumuisha viongozi wote wanaomiliki mashamba na akaongeza kuwa kila kiongozi lazima awe na miti 70 ya mikorosho na heka mbili za muhogo ili kupambana na tishio la njaa wilayani humo.

Aliongeza kuwa lengo la operesheni hiyo ni kufufua zao la mikorosho ili lichangie juhudi za kuinua na kuboresha elimu katika wilaya hiyo pamoja na kuimarisha kampeni za kitaifa za kuthifadhi mazingira kwa lengo la kupanda miti milioni moja.

"Nitahakikisha viongozi wote mashamba yao yamepaliliwa na yamepandwa miti 70 ya mikorosho tuliyokubaliana, " alisema.

Katika sekta ya elimu Kapteni Yamungu alisema atakwenda kukagua shule mbili za sekondari za Chole na Mzenga ambazo zinatarajiwa kufunguliwa mwaka huu ambazo zote zitakuwa ni za kutwa.

Pia alisema ukaguzi huo utakwenda sambamba na ukaguzi wa nyumba za walimu na hali ya vyoo katika shule hizo.

Seminari kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu

Na Fr. Raphael Kilumanga

Seminari ya Mt. Fransis ya Kasita, Mahenge inatarajia kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu Januari Mosi 2001.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gombela wa seminari hiyo, Padre Octavian Linuna, pamoja na pilikapilika za Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 zinazoendelea jimboni Mahenge, seminari ya Kasita inajiandaa pia kufanya ukarabati wa majengo ya shule, nyumba ya mapadre, masista na ujenzi wa nyumba mpya ya mapadre pamoja na zahanati mpya.

Alisema ukarabati huo utahusisha shughuli kadhaaukiwemo upigaji rangi, kuezeka, shughuli alizosema zitagharimu fedha nyingi.

Taarifa hiyo imewaomba watu wenye mapenzi mema kuchangia shughuli hiyo kwa hali na mali ikiwa na pamoja na kutumia akaunti za Kasita Seminari A/C 6801007214 na A/c 6801009387 zilizoko tawi la Mahenge.

Seminari ya Mt. Fransis ilianzishwa na Wamisionari wa Shirika la ndugu Wakapuchini Waswisi Januari mosi 1951.

Hadi sasa Seminari hiyo imetoa mapadre zaidi ya 100 wakiwemo maaskofu wazalendo wa pili na wa tatu wa Mahenge wahashamu Nicas Kipengele na Patrick Iteka.

Majimbo mengine yaliyopeleka pia waseminari huko Kasita ni pamoja na Jimbo Kuu la Dar es Salaam, majimbo ya Iringa na Njombe, mashirika mbalimbali ya kitawa nchini yakiwa ni pamoja na ya ndugu Wakapuchini, Wakonsolata na Wabenediktini waafrika wa Hanga.

Vile vile mamia ya Walei nchini ambao sasa wanafanyakazi katika nyanja mbalimbali wamepitia katika seminari hiyo.

WAKATI HUO HUO: Kati ya shule 666 za sekondari zilizofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ambao matokeo yake yanazidi kutangazwa sasa, shule za kanisa zimezidi kutia fora kwa ushindi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana toka kwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu, Baraza la Maaskofu Katokili Tanzania Padre Elias Msemwa, Kanisa Katoliki lina shule 118 zilizosajiliwa na kati ya hizo shule 8, zilikuwa miongoni mwa shule kumi bora.

Takwimu zinaonesha kuwa shule saba kati ya hizo 8, ni seminari na moja ni shule ya wasichana ya Mt. Francis ya Jimbo la Mbeya.

Seminari zilizokuwa katika kundi la 10 bora ni pamoja na Sengerema (Geita-1), St. James Moshi (2), Rubya Bukoba (3), Mafinga, Iringa (4) Katoke, Rulenge (5); St. Francis Girls Mbeya (6) Nyegezi Mwanza (8 ) Maua Seminari Moshi.

Ripoti inaendelea kueleza kuwa katika shule bora 20, 17 ni za kanisa wakati shule tatu zikiwa za wasichana ambazo ni Mt. Fransis ya Mbeya, Kifungilo na Mazinde Juu, ya jimboni Tanga.

Aidha katika shule 30 bora, 26 ni za kanisa; katika 50, bora, shule 34 ni za Kanisa wakati kati ya 100 bora, 42 ni za Kanisa.

Katika shule zote zilizofanya mtihani seminari ya Sengerema iliyokuwa na wanafunzi 13 ilishika namba moja ikiwa na daraja la kwanza 10 na daraja la pili 3.

Serikali yatakiwa kuiangalia upya adhabu ya kifo

Na Dalphina Rubyema

SERIKALI imetakiwa kuangalia upya adhabu ya kifo ambayo bado inatolewa nchini kutokana na ukweli kuwa hukumu hiyo ni kinyume cha haki za binadamu.

Akizungumza wakati wa kuchangia mada ya Mikataba ya Kimataifa katika warsha ya siku tano ya mahakimu wa Mahakama za Mwanzo hivi karibuni, Mkurugenzi wa Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC), Bibi Hellen Bisimba alisema kuwa sheria hiyo imepitwa na wakati.

Alisema kuwa adhabu hiyo inakwenda kinyume na haki za binadamu duniani na ameomba serikali kuitazama upya adhabu hiyo na kuiga mfano bora wa nchi zilizoamua kuiondoa ikiwemo Afrika Kusini.

Mkurugenzi huyo alisema mbali ya adhabu hiyo, hata ile ya kuweka watu kizuizini ina walakini na ni vema serikali ikatangaza kuzifuta ili kuonesha kuwa inajali haki za binadamu tofauti na nchi nyingine zilizo kinyume.

Alizitaja nchi nyingine zilizofuta adhabu ya kifo kuwa ni pamoja na Namibia, Madagaska na Malawi na akasema hali hiyo inatokana na Tanzania kushindwa kuridhia mkataba wa nyongeza wa Haki za Binadamu.

"Mkataba huo wa nyongeza haujaridhiwa lakini ni vema ukaangaliwa ili kuondoa ukiukwaji huo," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kituo hicho kitaendelea kuwaelimisha wananchi haki zao ili waweze kuzidai jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga jamii yenye usawa na inayoheshimu haki za binadamu.

Katika warsha hiyo mada mbali, mbali zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, sheria za ndoa na mirathi na haki zingine za raia.

Hananasif kufaidi huduma za maji ya vioski

Na Dalphina Rubyema

WAKAZI wa eneo la Hananasif wilayani Kinondoni katika mkoa wa Dar-Es-Salaam mwishoni mwa mwezi huu wataanza kufaidi huduma za maji kutoka katika vioski vinavyojengwa na Mradi wa Maendeleo kwa Wakazi wa eneo hilo (CDA).

Akizungumza na KIONGOZI, Mwenyekiti wa mradi huo Bw. Nestory Joseph, alisema kuwa ujenzi wa vioski hivyo umeanza na vitakuwa 10 katika maeneo tofauti na wakazi watalazimika kuchangia kidogo ili kupata huduma hiyo.

Alisema ujenzi huo umefanyika kutokana na tatizo la maji linalowakabili wakazi wa eneo hilo kwa kipindi kirefu sasa jambo ambalo linaonekana kuwa kero kwa wakazi wa sehemu hiyo.

Alisema awali, wakazi hao walilazimika kuamka usiku wa manane na kutumia muda mwingi katika foleni kusubiri huduma hiyo jambo ambalo linazorotesha shughuli zingine za maendeleo na uzalishaji mali.

Bw. Nestory alisema kwa kuzingatia hilo ndio maana jumuia hiyo imeamua kubuni mradi huo ambao unatarajiwa kupunguza tatizo la maji katika eneo hilo kwa asilimia zaidi ya 80.

Sheikh Mbukuzi ataka ombaomba wasaidiwe, wasifukuzwe

Na Dalphina Rubyema

SERIKALI na wafadhili wa michezo mbalimbali ikiwemo ya mashindano ya urembo, wametakiwa kushirikiana kwa michango ya pesa na vitu vingine ili kuwasaidia wasiojiweza badala ya kuwafukuza jijini na kuwarudisha makwao.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Sheikh Juma Bin Salum Mbukuzi wakati alipotembelea msikiti wa Makukula uliopo Buguruni jijini Dar es Salaam.

Akitoa salamu kwa Waislamu wa msikiti huo wakati wa swala ya Maghaibi, Sheikh Mbukuzi, alisema kuwa watu wasiokuwa na uwezo (ombaomba) nao ni raia wa Tanzania kama walivyo raia wengine na kwamba wana haki ya kuishi mahali popote nchini.

Alisema kitendo cha Mkuu wa mkoa wa Dar es Salam, Luten Yusufu Makamba kuwarudisha makwao ni kuwanyanyasa kuwatendea kinyume cha haki kama raia wa nchi.

"Makamba alikaa na mwenzake ambaye sitataja jina lake na kuamua kuwarudisha ombaomba kwao hapa hakuwatendea haki kwani nao kama raia wengine wanayo haki ya kuishi popote wanapotaka, cha maana, ni serikali kukaa na kuwakusanya matajiri wenye uwezo ambao hufadhili michezo na mashindano ya urembo na kuwaomba pesa na vitu vingine washirikiane kwa ajili ya ombaomba lakini kuwarudisha makwao siyo haki" alisema.

Sheikh Mbukuzi alihoji kuwa, "Kwanini wakimbizi wanao kuja nchini wanapokelewa kwa ukarimu, lakini ukarimu kama huo hautendeki kwa ombaomba ambao ni wazalendo wa Tanzania?"

Sheikh Mbukuzi pia ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto kutenga pesa kwa ajili ya watu wasiokuwa na uwezo na siyo kutenga pesa kwa ajili ya bili za umeme na maji tu.

"Wizara ya jamii inatenga pesa kwa ajili ya umeme na maji lakini halitengi fungu fulani la pesa kwa ajili ya ombaomba kwanini? Alihoji Sheikh Mbukuzi.

Serikali yaombwa kudhibiti ongezeko la baa

lYadaiwa kuwa sasa wazee ndio wanawazika vijana

Na Josephs Sabinus

SERIKALI wilayani Temeke imeombwa kudhibiti kasi ya ongezeko la baa kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa biashara ya ukahaba ambayo hueneza kwa kasi ugonjwa hatari wa ukimwi.

Ombi hilo lilitolewa na vijana wa Kanisa La Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T) Temeke, wakati wa tamasha la kuhamasisha kupambana na ugonjwa wa UKIMWI na madhara ya madawa ya kulevya lililofanyika Temeke Jumapili iliyopita.

Akisoma risara ya vijana hao mbele ya mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Kapteni John Chiligati, Bi. Hilda Mbwana ambaye ni katibu tarafa wa Chang’ombe, mwenyekiti wao Bw. Tullo A. Kipingu, alisema, ongezeko la biashara ya baa (grocery) na ukosefu wa ajira kwa vijana, vimekuwa vichocheo vikubwa kwa vijana kujitupa katika vitendo vya ukahaba na matumizi ya madawa ya kulevya ambavyo huhitimishwa na mauti kwa vijana wengi kutokana na ugonjwa wa ukimwi.

"Ukosefu wa ajira na kipato kidogo kwa vijana vimechangia wengi wa vijana kujitupa katika biashara ya ukahaba na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo ni hatari," alisema Bw. Kipingu na kuongeza kuwa serikali na vikundi vya dini havina budi kuunganisha juhudi zao kupambana vikali na tatizo hili.

Katika tamasha hilo, ofisi ya Mkuu wa Wilaya iliahidi kukichangia kikundi hicho shilingi 50,000/= ili kutunisha mfuko wao wa kuanzisha miradi mbalimbali ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Akifunga tamasha hilo, Mkuu wa K.K.K.T Jimbo la Temeke Mchungaji Astorn Kibona alisema, matumizi ya kondomu sio kinga sahihi ya tatizo hili sugu la ukimwi ambalo athari zake zinaoonekana zaidi kuanzia ngazi ya familia na kwamba kinga pekee ni kuishi maisha ya uaminifu.

"Wakristo tungekuwa watu wa kuzingatia kuwa usizini, wala usiguse, hakika tungekuwa salama...sisi wachungaji ndio tunaoona. Zamani vijana ndio walikuwa wanawazika wazeee lakini siku hizo mambo yamebadilika, wazee ndio wanowzika vijana, inasikitisha sana," alisema Mchungaji Kibona.

Kiongozi wa dini anayejineemesha ni sumu- Kauli

Na Neema Dawson.

MCHUNGAJI wa Kanisa la Pentekoste- Kongowe wilayani Temeke, Michael Mugarura amesema kiongozi yeyote wa dini anayetumia jina la Mungu kwa maslahi yake binafsi, ni hatari na kwamba wakati wowote anaweza kuliangamiza taifa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni, Mugarura ambaye pia ni mwanzilishi wa shirika lisilo la Kiserikali(NGOs)la Feed and Tend International(FTI), alisema jamii yote wakiweamo viongozi wa dini hawana budi kuutambua ukweli kuwa utajiri mkubwa unaostahili kuangaliwa zaidi ni Neno la Mungu ambalo lina hazina ya milele iliyostirika na akaonya kuwa viongozi wa dini wanaotumia Neno la Mungu kwa maslahi yao ni hatari kwa jamii kwani wanaweza kuliangamiza taifa.

"Viongozi wengi wa dini hulitumia Neno la Mungu kufanyia biashara kwa maslahi yao binafsi, watu wa namna hiyo wakiachiwa hivi hivi watalifanya taifa kuteketea hata kabla ya muda wake," alisema.

Mbali na kutoa huduma kwa watoto yatima na ambao wazazi wao hawana uwezo, shirika hilo la FTI pia hutoa mafunzo ya Biblia na kuwaandaa watumishi wa Mungu kwa ajili ya uinjilisti na uchangaji. Pia hutoa huduma ya kliniki na elimu kwa watoto yatima. Lina shule ya chekechea na sekondari.

Naye Elizabeth Steven anaripoti kuwa Wakazi wa maeneo ya Manzese sokoni jijini Dar Es Salaam, wamesema wanahofia kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu endapo jamii itaendelea kulifumbia macho swala la uchafu unaolizunguka soko kwa kuwategemea viongozi pekee ya badala ya kushirikiana nao kuondoa hali hiyo.

Wamewalani wanaozibua mifereji ya maji machafu yatokayo katika vyoo kwa madai kuwa yanawapa kero ya harufu mbaya na kufanya uwepo uwezekano mkubwa wa magonjwa.

"wengine wanatupa takataka makusudi na kuzibua miferji ya choo, sasa hiyo maana yake ni nini kama sio kutafutiana kipindipindu? Serikali lazima iwadhibiti kabisa," alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Siwa mkazi wa eneo hilo.

Naye mzee mmoja aliyekataa kutajwa jina lake gazetini alihoji kuwa, "Hivi hawa wanaoachia mifereji ya ili maji yatoke na kusafirishwa kwa mvua hawajui kuwa wapo watu wengine wanaoyatumia wakiwa hawajui yanatoka na kupitia wapi?"

Tanzania yafanikiwa kupunguza walemavu wa ukoma

Na Arnold Victor

TANZANIA imefanikiwa kupunguza kiwango cha ulemavu utokanao na ugonjwa wa Ukoma kwa asilimia 10 kati ya mwaka 1983 hadi 1999.

Kwa mujibu wa Dk. Aman Swai, wa Hospitali ya Serikali ya Mnazi mmoja jijini, kiwango cha ulemavu utokanao na ugonjwa wa Ukoma mwaka 1983 ulikuwa asilimia 30 ambazo hivi sasa zimeshuka hadi kufikia asilimia 20.

Dk. Swai, alikuwa akiongea katika semina iliyoandaliwa na Chama cha Ukoma nchini (TLA) kwa ajili ya kuwaelimisha waganga wa jadi juu ya namna ya kuwatambua wagonjwa wa Ukoma na hivyo kuwaelekeza mahospitalini ili wapatiwe matibabu yafaayo.

Katika semina hiyo iliyofanyika Kurasini jijii Dar Es Salaam, Jumatano iliyopita, Dk. Swai alieleza kuwa ugonjwa wa ukoma unaweza kutibika kirahisi endapo utawahiwa katika hatua za awali na pia hata pale ambapo ulemavu umeanza unaweza kudhibitiwa au kupunguzwa kwa tiba muafaka.

Hata hivyo Daktari huyo alisema kuwa ingawa imefanyika kazi kubwa kufikia mafanikio ya sasa, bado kazi kubwa inahitajika ili kufikia angalau asilimia 5 au kuutowesha kabisa ugonjwa huo unaoambukizwa zaidi kwa njia ya hewa.

Ugonjwa wa ukoma pia unaweza kuambukizwa kwa njia ya kugusana kwa sehemu zenye michubuko kati ya mgonjwa na mtu mzima.

Hata hivyo Dk. Swai, alisema kuwa binadamu wana kiwango kikubwa cha kinga ya ukoma, ndio maana kiwango cha maambukizo si cha kiwango cha juu kama ilivyo kwa ukimwi.

"Ukweli ni kwamba karibu sisi wote na hata mimi binafsi tumewahi kuambukizwa ukoma pengine mara nyingi lakini kwa vile tuna kinga kubwa hatuugui," aliwaambia wanasemina.

Mtaalamu huyo alisema dalili za ukoma zimegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni "dalili changa" na "dalili pevu".

Alizitaja dalili changa kuwa ni pamoja na kuwa na baka au mabaka yenye rangi ya shaba na kingo zinazoonekana. Baka au mabaka hayo huwa na ganzi na hayawashi. Dalili nyingine changa ni kuathirika (kuvimba) kwa mishipa ya fahamu na kuonekana kwa vimelea (bakteria) wa ukoma kwa njia ya darubini.

Dalili pevu huanza na kuwa na dalili zote changa, uvimbe wa (manundunumndu) mwili mzima au masikioni, vidonda au majeraha sugu miguuni, mikononi hasa kwenye viganja na nyayo. Yanayofuata baada ya hayo ni ulemavu wa viungo au kupoteza viungo ya mwili.