Mungu wangu ! Mbeya hawaogopi Ukimwi!

lKukanyaga mapito ya mwenzio kwao ni sifa

Na Dalphina Rubyema

WAKAZI wa Mkoa wa Mbeya wameelezewa kama watu wakusikitikia kwa kuwa mstari wa mbele kuupuza ugonjwa wa ukimwi kwa kufanya vitendo vya uasherati kwa makusudi licha ya kujua wahusika ni waathirika.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi jijini hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo kwa Watu wanaoishi na Virus vya Ukimwi (SHDEPHA+), Bw. Joseph Katto, alisema kuwa uchunguzi wa kina uliofanywa na chama chake mkoani humo umebaini kuwa wakazi wake wanaambukizana Ukimwi kwa kujuana na kwa kujitakia makusudi tabia aliyosema inashangaza na kusikitisha.

Alisema mtu fulani anapokufa kwa ugonjwa wa Ukimwi watu huanza kumfuata mwenzake aidha mme au mke na kutembea naye wakijua fika kufanya hivyo wanaambukizwa ugonjwa huo.

"Mkoa wa Mbeya kwa kweli wakazi wake wanashangaza sana, yaani inapotokea baba au mama akafariki kwa Ukimwi, bila woga watu huanza kumfuata yule aliyebaki na kufanya naye mahusiano ya kimwili wakati wanajua ni hatari," alisema.

Katto aliongeza kuwa mbali na hivyo, wapo hata wale ambao wanafahamu kuwa mtu fulani anatembea na baba ama mama aliyeondokewa na mwenza wake lakini hata wao bila woga wanajitumbukiza pale pale.

"Unakuta mtu anatembea na shemeji yake ambaye ameondokewa na mkewe ama mumewe lakini, hata mjomba mtu naye anataka ajitumbukize hapo hapo. Hivi kweli hapa si kuambukizana ugonjwa huo wazi wazi na kwa kujitakia?" alihoji Bw. Katto.

Alisema katika juhudi za kuwanusuru wakazi wa mkoa huo chama chake (SHDEPHA+), kinatarajia kutoa semina ya wazi mwishoni mwa mwezi huu.

"Tunatarajia kutoa semina kwa watu wa rika zote ambayo itafanyika wazi katika maeneo mengi mkoani humo ili kumruhusu kila mmoja kupata ujumbe wa semina hiyo ambao utakuwa ni kuwapa elimu sahihi juu ya Ukimwi" alisema.

Wakati huo huo: SHDEPHA+ inatarajia kufungua matawi yake katika maeneo ya Bagamoyo na Kibaha mkoani Pwani.

Hivi karibuni alipotembelea kituo cha Faraja kilichopo Morogoro, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Al-Haji Ali Hassan Mwinyi, aliufananisha ugonjwa wa ukimwi na dudu la kutisha ambalo kila mtu hana budi kuliogopa kwani hautibiki, hauna kinga na umeua maelfu ya watu.

Njia kubwa ya maambukizo ya ugonjwa huu hatari, ni kupitia vitendo vya kujamiiana na endapo jamii ya Watanzania wakiwemo wakazi wa Mbeya, haitakuwa macho na kubadili tabia mara moja, ipo hatari ya taifa kuangamia mno hata kufikia hatua ya msiba kukosa mtu wa kukaa matanga kwa kuwa jamii kubwa itakuwa imetumbukia ndani ya mdomo huo wa mamba.

Mkoa wa Mbeya umekuwa na sifa ya matukio ya ajabu yakiwemo mauaji ya mara kwa mara na watu kuchunwa ngozi na hivi karibuni, watu wapatao 30 walifariki kwa kuungua moto wakati wakijaribu kuiba mafuta katika malori yaliyokuwa yamepata ajali.

 

Tunafarijika viongozi wanapojiuzulu -CHADEMA

Na Peter Dominic

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kinapata faraja viongozi wanapojiuzulu baada ya kuona wameshindwa kazi ya kuwatumikia wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa chama hicho kitaifa Bw,Victor Kimesera, alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake yalipo makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini kufuatia gazeti kutaka kujua sababu za viongozi mbalimbali kukihama chama hicho na kujiunga na vyama vingine vya siasa.

Wiki iliyopita gazeti moja litolewalo mara mbili kwa juma, lilipoti kuwa Katibu wa CHADEMA mkoani Dar es Salaam Bw, Abdalah Himba, amejiuzulu na kukihama chama hicho.

Viongozi wengine waliojiuzulu na kujiunga na vyama ni pamoja Dk. Lutta Nelison aliyewahi kuwania Ubunge wa Jimbo la Kibaha, kwa tiketi ya CHADEMA lakini akahamia CCM.

Wengine ni aliyekuwa Katibu Mwenezi, Bw. Tozzy Matwanga, Naibu Katibu wa Chama Nathaniel Chilambo, Naibu Mratibu wa Vijana wa chama, Bw. Francis Haule, na Mratibu wa Wanawake Wilaya ya Ilala, Bi. Monica Mathias.

Bw. Kimesera, alidai chama hakitaharibikiwa kwa kuondokewa na wanachama hao kwa kile alichokisema kuwa walikuwa na nia mbaya na sasa baada ya kushindwa kutimiza azma yao, wanaamua kukimbia wenyewe.

"Chama kingeyumba kama kingeondokewa na vingozi wakubwa kitaifa, tena wenye nia nzuri kwa chama. Labda ningekuwa mimi au Mwenyekiti wangu basi tungesema chama kitakufa," alisema.

Hata hivyo alisema chama hakitambui kujiuzulu kwa Katibu wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam Bw,Abdalah Himba, kwa vile hajawakilisha rasmi barua ya kujiuzuru kwake kwa mujibu wa katiba ya Chama.

Hivi karibuni Bw, Himba, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amejiuzulu wadhifa na uanachama wa chama hicho mapema mwezi huu kwa madai kuwa chama kimekosa miundo na mbinu sahihi za kufurukuta katika ulingo wa siasa.

Alizitaja sababu nyingine kuwa ni chama kushindwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara na viongozi kukitumia chama kwa manufaa yao binafsi hali aliyosema ndio chanzo cha kuoza kwa chama.

Alidai Mwenyekiti wake Bw. Alfonce Masikini, amekuwa akionesha tofauti baina yao.

Alisema sababu nyingine iliyomfanya ajiuzulu ni pamoja na Mwenyekiti wake kutoyaheshimu maamuzi ya Kamati Tendaji ya Mkoa ambapo katika kikao cha 51 Kilimsimamisha nafasi ya uenyekiti Jimbo la Kinondoni Bw. James Masawe kwa vile alishindwa kuitisha mikutano na kuandaa ziara za mkoa na kusababisha kusambaratika kwa chama eneo hilo lakini, Mwenyekiti huyo akamrejesha madarakani.

Wakatoliki waanzisha shule ya msingi ya Kimataifa

Na Dalphina Rubyema

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limeanzisha Shule ya Msingi yenye hadhi ya kimataifa (English Medium) inayojulikana kama ‘Christ the King’ iliyopo katika Kanisa la Kristo Mfalme Parokia ya Mbagala.

Akizungumza katika mkutano wa wazazi Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Sr. Clarapia Manyanga alisema shula hiyo inayokuwa wanafunzi toka madhehebu yote, ilifunguliwa rasmi kwa muhula wa masomo Januari 17 mwaka huu.

Alisema shule hiyo ambayo hadi hivi sasa inao wanafunzi wa darasa la kwanza inafundisha kwa kufuata mtaala wa kimataifa na wale wanafunzi watakaofuzu mtihani wa elimu ya msingi watakuwa na nafasi ya kuendelea na Sekondari kwenye shule zenye hadhi kama hiyo.

Alisema ujenzi wa madarasa zaidi unaendelea na wazazi wametakiwa kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu. Kwa mujibu wa ratiba ya shule hiyo masomo yanayofundishwa ni hisabati, Kiingereza, Sayansi, Elimu ya Fizikia, michezo ya kuigiza, uchoraji, mazoezi ya kuandika,mdahalo, afya. Nidhamu ya mwanafunzi na usafi ni miongoni mwa sheria za shule hiyo ambayo karo yake ni sh 170,000/= kwa mwaka na sh 100,000/= inatakiwa kulipwa mwanzoni mwa temu ya kwanza ambapo sh 70,000/= inalipwa mwanzoni mwa temu ya pili.

WAPENTEKOSTE WALIA NA KUSEMA

Ingawa dini zinaleta maendeleo, zinatengwa bungeni

Na Elizabeth Steven

BARAZA la Maaskofu wa Kipentekoste nchini (PCT) limesema kwa kuwa Bunge ni sehemu ya uwakilishi ambapo hata sheria za kudhibiti na kuweka sawa mambo ya dini hutungwa, ni vema wakawapo wawakilishi wa vikundi vya dini.

Mwenyekiti wa umoja huo, Askofu Silyvester Gamanywa wa Kanisa la Peace Makers (PMC), alisema hayo hivi karibuni katika mazungumzo na gazeti ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema inashangaza kuona kuwa licha ya Serikali yenyewe kukiri kuwa vikundi vya dini vinachochea maendeleo ya nchi katika kuleta amani,na kuboresha elimu na huduma za afya, bado uendeshaji wake unatengwa na mambo ya nchi, hali aliyosema inawapa mwanya baadhi ya viongozi waliopo madarakani kufanya mambo na maamuzi kwa maslahi ya dini zao.

"Unapokuja muswada ili uwe sheria, huwa haubagui dini, kabila, jinsia wala rangi. Pia zipo sheria zinazodhibiti na kuweka sawa mambo ya dini. Sasa kama hakuna mwakilishi nani atawakilisha dini hizo kama Wabunge wanavyowakilisha majimbo yao?

"Tazama mfano mzuri ni hapa hapa Tanzania Wakatoliki ni wengi mno kuliko chama chochote lakini hawana mwakilishi bungeni hata vyama vya siasa ingawa vina sera tofauti vina wawakilishi bungeni lakini taasisi za dini ambazo ni Unique na Sensitive, hazijapewa nafasi hiyo ya uwakilishi".

Sasa sijui wanataka Pengo agombee ubunge ili apate nafasi ya kuwakilisha Wakatoliki ambao ni wengi kuliko jimbo wala chama chochote; haiwezekani," alisema Gamanywa.

Kiongozi huyo wa PCT alisema kwa kuwa serikali ina mamlaka juu ya dini kisheria ni vema dini nazo zikapewa nafasi ya kujieleza kwani mambo ya dini ni mguso na yanahitaji kutafsiriwa kidini.

"Hivi sasa hata Political Scandle tunashindwa kuzikemea; utazikemea kwa mamlaka ipi kama siyo wakati wa mahubiri tu ambapo wengi wao wanayaignore kuwa ni mahaubiri ya kawaida? Ili tuweze kukemea zaid hata maovu ya viongozi tunahitaji authority" alisisitiza.

Alidai katiba ya nchi haijafafanua vizuri juu ya mahusiano ya dini na serikali tofauti na kusema kijuu juu kuwa taasisi za kidini zitafanya mambo yake nje ya mamlaka ya nchi na akasema kauli hiyo tu, haitoshi wala kueleweka wazi.

Hata hivyo alisema siyo vema viongozi wa dini kugombea uongozi wa siasa kwani hatua hiyo itaweza kuwagawa waamini katika misingi ya kisiasa.

Mwinyi awatetea walemavu, watoto dhidi ya ukimwi

Na Neema Dawson.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Ushauri Juu ya Ukimwi, Rais Mstaafu Ali Hasani Mwinyi, ameitaka jamii ya Watanzania kutowaonea vipofu, mataahira, watoto na walemavu kwa kuwaambukiza ukimwi kwa makusudi kwani ni kuwaonea.

Mwinyi aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwaelimisha walimu wa wanafunzi walemavu juu ya kujikinga na ukimwi iliyofanyika Shule ya Msingi ya Uhuru-Mchanganyiko jijini Dar-Es-Salaam hivi karibuni.

"Imefikia hatua jamii haioni aibu kabisa na wengine wanajifahamu kuwa wameathirika na ukimwi, lakini bado wanawaingilia kimwili hata watoto wa shule na kuwaambukiza." Alisema, "Wanawaingilia hata walemavu ambao hawawezi kujitetea. ulemavu unatofautiana; upo ule wa wasioona , wasiosikia na ule wa akili ambao wakati wanafanyiwa vitendo hivyo vya kinyama hawawezi kujitetea."

Alisema, jamii nzima haina budi kuwatetea watoto na walemavu wanaoonewa na kuwachukulia hatua wale wanaofawafanyia vitendo hivyo vya kinyama ili kuinusuru jamii isiangamie zaidi kwa makusudi kutokana na janga hili la ukimwi.

Mwinyi aliongeza kuwa bila jamii kuungana kwa pamoja kukemea na kuelimishana juu ya tatizo hili, ukimwi utazidi kuwaondoa Watanzania hasa vijana ambao ndio wenye nguvu zinazategemewa zaidi katika ujenzi wa Taifa ".

Hivi karibu Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia ukimwi limetoa takwimu zinazoonesha kuwa, hali inazidi kuwa mbaya tofauti na ilivyokuwa awali ambapo watu zaidi ya milioni 30 duniani wana virusi vya ukimwi.

Alisema, kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu, nchi maskini yenye asilimia 5 ya watu wenye ukimwi, gharama ya kuwahudumia huongeza bajeti ya afya kwa zaidi ya asilimia 40.

Alisema ili fedha hizo zipatikane sekta nyingine hazina budi zipunguziwe bajeti hali ambayo itaathiri jamii kwa kukosa huduma muhimu.

Alisema, "Ingawa tunajua kuwa wale wenye virusi ya ukimwi watafariki, hatuwezi kuacha kuwahudumia, lazima tuwape dawa kuwapunguzia maumivu."

Rais Mwinyi alitoa rai kwa wazazi na viongozi wa dini kuzungumzia wazi ugonjwa huo na madhara yake kwa watoto na waumini ili wauepuke zaidi na akashauri uwepo uwezekano wa wananchi wote kupewa elimu ya mara kwa mara juu ya ugonjwa huo.

Makamba alilia damu ya Muhimbili

lAsema damu haina Muislamu, Mkristo wala CCM

Na Agatha Rupepo, DSJ

MKUU wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Luteni Yusufu Makamba amewataka Watanzania kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa katika hospitali zinazokabiliwa na ukosefu wa damu ikiwemo Muhimbili hususan wajawazito na majeruhi.

Luteni Makamba ametoa wito huo alipokuwa akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa jengo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T), usharika wa Ukonga jijini Dar Es Salaam Jumapili iliyopita.

Katika uzinduzi huo ambao Makamba alimwakilisha Waziri Mkuu Bw. Fredrick Sumaye, alisema hivi sasa hali ya damu katika hospitali mbalimbali ikiwemo Muhimbili iliyopo katika mkoa wa Dar Es Salaam, ni mbaya kiasi cha kutisha na kwamba endapo Watanzania hawatajitolea kuchangia damu katika hospitali zinazokabiliwa na tatizo hilo, ipo hatari ya watu wengi kupoteza maisha hasa wajawazito na majeruhi katika ajali mbalimbali ambao huhitaji damu za dharura toka katika benki za damu.

Alisema mkoa wa Dar Es Salaam, una wakazi wengi na kwamba karibu nusu ya ajali zitokeazo nchini, hutokea Dar Es Salaam, hivyo ni muhimu kujenga moyo wa kujitolea kukabiliana na upungufu huo bila kujali tofauti za kidini wala kisiasa.

"Damu haina itikadi kwamba utasema, hii ni ya CCM, ya Mkristo wala ya Muislamu. Damu ni damu tu, hakuna hospitali utakayokwenda wakuambie hii ni damu ya Mkristo , au ya Muislamu ,au basi eti hii damu ni ya CCM," alisema.

Amewaomba viongozi wa dini kuwaelimisha na kuwahamasisha waamini wao kushiriki kuondoa tatizo hilo kwa manufaa ya taifa zima ikiwa ni pamoja na kuwafanya waamini kuwa wanafanya kazi ya Mungu.

Wakati huohuo: Makamba ametumia Biblia kukemea vikali vitendo vya utoaji na upokeaji wa rushwa na akasema licha ya Rais Mkapa kuvipiga vita, vitendo hivyo vinazuiliwa na Mungu katika vitabu vitakatifu.

Katika kuchangia ujenzi wa kanisa hilo lililowekwa jiwe la msingi siku hiyo na Askofu wa K.K.K.T. Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jerry Mngwamba, Waziri Mkuu ameahidi kuchangia shilingi 200,000/=, wakati Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kutoa mifuko 10 ya saruji.

 

UNICEF kuboresha huduma ya afya Kisarawe

Na Agatha Rupepo, DSJ

SHIRIKA la kuudumia watoto duniani (UNICEF) limetoa jumla ya shilingi milioni 28.5 kwa ajili ya kuchangia na kuinua huduma ya mama na mtoto katika wilaya ya Kisarawe katika mpango wa Child Survival Protection and Development Programme (CSPD) mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa mipango wa Wilaya ya Kisarawe. Bw. Khalfa Mwanamkuta, alipokuwa akizungumza na Kiongozi ofisini kwake hivi karibuni alisema mpango huo wa CSPD, unalengo la kupanua huduma za afya katika wilaya hiyo hasa upande wa vijijini kwani ndipo kunamatatizo zaidi ya huduma za mama na mtoto ambapo msaada huo utawanufaisha wananchi wa wilaya hiyo. Aliongeza kusema CSPD ina mradi ambayo ni afya, elimu,maji safi kwa wakazi . pia alifafanua katika afya malengo zaidi kudhibiti magonjwa kama Ukimwi pamoja na kutoa chanjo kwa watoto katika wilaya hiyo anapata chanjo na hali yake kiafya inaenda vizuri na kuhakikisha kila anapopima afya yake na uzito unaongezeka.

Pia amesema katika mpango wa elimu wanashughulika zaidi na watoto ambao hawakuandikishwa shule, watoto hao wanafundishwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya kujikinga na maambukizo ya Ukimwi.

"Tunajaribu kuwapa elimu hiyo kwa njia ya sanaa ya maigizo pamoja na kuangalia maambukizo ya ugonjwa huu" alisema Bw. Mwanamkuta.

Aliongeza kusema katika mradi wa upatikanaji wa maji safi mpaka sasa kuna visima zaidi ya 26 ambavyo vimetelekezwa katika mpango huu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wilaya Bwana Victor Msoma alisema lengo ni kupanua mpango huu katika Wilaya yote mwaka huu tofauti na miaka ya nyuma ambapo mpango huu ulikuwa katika tarafa moja ya maneromango.

Wapinzani wa Nyerere wameanza kujitokeza nchini- Rais Mkapa

Na Arnold Victor

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, amesema ikiwa imepita miezi michache tu tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, tayari watu wanaotaka kuvunja misingi na umoja na amani aliyoijenga nchini wameanza kujitokeza.

Akiongea mwishoni mwa wiki katika Kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Marehemu Baba wa Taifa, iliyokuwa imeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (The Mwalimu Nyerere Foundation), Rais alionya kwamba Serikali yake kamwe haitavumilia kuona misingi hiyo ikivurugwa na mtu yeyote kwani kulinda misingi hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, na sio kumsifu tu huku akipingwa kivitendo.

"(Nyerere) atafurahi (huko aliko) akiona tunayaendeleza na kuyalinda yale mema aliyotuachia na sio kumsifu tu," alisema Rais Mkapa.

Rais Mkapa alisema kumbukumbu ya mema ya Mwalimu Nyerere lazima ijichimbie katika moyo wa kila Mtanzania na ifanyiwe kazi.

Alimsifu Mwalimu Nyerere kama mtu aliyependa, kupigania na kuamini juu ya umoja wa kitaifa, ambao ni jambo muhimu linalohitaji kutunzwa.

Alitoa mfano wa Mwalimu Nyerere kukibadili chama cha TAA kuwa TANU ambacho kina neno "Union" yaani umoja. Rais alisema Nyerere aliweza kuyaunganisha makabila zaidi ya 120 ya Tanzania ya leo ambayo hapo awali hayakuwa taifa, na akafanikiwa kuua sumu za ukabila, udini na ubaguzi wa rangi.

Rais Mkapa aliwataka Watanzania wote kupinga kwa nguvu zao zote hisia zozote zinazoweza kuvunja umoja wa kitaifa, hisia ambazo hufanikiwa zinapokutana na mioyo yenye ukabila, udini na ubaguzi wa rangi.

Kumbukumbu hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Nyerere ilihudhuriwa na viongozi wa vyama mbali mbali wa kisiasa nchini, viongozi wastaafu wa kitaifa na watu mbali mbali mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi.

Mapadre wa Shinyanga wazawadiwa ng'ombe, mbuzi

Na Charles Hililla, Shinyanga

MAPADRI wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga wamekumbusha kusali kila siku sala ya Bwana, pia kuwa nadhifu kwa mavazi yao wanayovaa hasa vazi la kanzu ambalo ndiyo vazi rasmi kwa kazi yao. Moja wapo ya kazi ya padri ni kusali kwa ajili ya nia za watu mbalimbali wenye shida na wala siyo kwa ajili yake tu au kikundi fulani.

Wito huo ulitolewa na Mhasamu Askofu Aloysius Balina wakati wa misa ya kubariki matufa matakatifu ya Krisma hapo Aprili 6 mwaka huu kwenye kanisa Kuu la Jimbo la Shinyanga. Misa hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi wa walei kutoka parokia zote 25 za jimbo la Shinyanga waliokuwa wamewawakilisha waumini wa parokia zao.

Akihubiri wakati wa misa hiyo ambayo pia ilikuwa imewakutanisha mapadri wote wanaofanyakazi katika jimbo la Shinyanga. Askofu Balina aliwaambia mapadri wake kutumia elimu yao kwa ajili ya maendeleo ya waumini wao kimwili na kiroho badala ya kuwa kikwazo kwa waumini wao.

Akifafanua maendeleo hayo kwa upande wa kiroho Askofu huyo alisema kuwa ni wajibu wao kuwalisha neno la Mungu pamoja na kuwapatia masakramenti. Aidha upande wa kimwili alisema kuwa ni katika nyanja za elimu na afya hasa kwa akina mama na watoto.

Siku ya kubariki mafuta katika Jimbo la Shinyanga, waumini wa kila Parokia huwapa zawadi mapadri wao kulingana na uwezo wao . Wengi wa mapadri wa parokia za vijijini wamekuwa wafugaji hasa baada ya kupewa zawadi nyingi za mifugo na mazao, wakati wale wa parokia za mijini wanapata fedha.

Jumla ya ng’ombe sita na mbuzi zaidi ya 40 na pesa taslimu shilingi 650,000/=zilitolewa kama zawadi kwa mapadri siku hiyo. Zawadi kama mapadri siku hiyo. Zawadi zingine zilizotolewa siku hiyo ni pamoja na nguo za misa na za kawaida mfano suruari na mashati pamoja na viatu na mashuka.

Aidha waumini hao hawakuwa nyuma kwa upande wa ujenzi wa seminari ya jimbo la kituo cha Redio cha jimbo kinachoendelea kujengwa ambapo kwa upande wa ujenzi wa seminari walitoa jumla ya shilingi Milioni 2.5 na ujenzi kituo cha redio waliota kiasi cha shilingi 100,000/=

Ashauri taarifa za pesa zitolewe

Getruda Madembwe na Elizabeth Stephen

MSHAURI wa Chama cha Wanataaluma Wakristo wa Tanzania (CPT), Padre Vic Missiaen, amesema Watanzania wanadhani viongozi wao wanaiba pesa za umma kwa kuwa hawapati taarifa za kutosha za mapato na matumizi ya pesa.

Padri Vic aliyasema hayo Jumamosi iliyopita alipokuwa akitoa mada katika semina juu ya teolojia ya maadili iliyofanyika katika ukumbi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salam.

Alisema ni muhimu kwa viongozi kutoa taarifa muhimu za mapato na matumizi kwa misingi ya uwazi na ukweli kwani hiyo ni njia mojawapo ya kujenga imani katika jamii.

"Suala la kutoa taarifa ni vizuri sababu wanataka kujua pesa zimetumika kiasi gani na kiasi gani kimebaki. Kwa mfano Kiongozi kama kapokea sh. Milioni 1 halafu katumia laki 9 na laki moja hajaitumia ni vyema kutoa taarifa yake kwao vinginevyo watasema na ni kweli kuwa sh laki 1 atatumia kwa matumizi yake binafsi."

Aidha, alisema jambo jingine ambalo mtu hataki kulitafutia ukweli ni rushwa watu wengi wanakuwa waoga kuuliza sababu wanahofia kuuliza viongozi wa wakati huo kwa kuwa wanajua nao watakuja kuulizwa wakiwa viongozi.

Katika semina hiyo iliandaliwa na CPT Jimbo Kuu la Dar es Salaam, itakayomalizika Jumamosi hii, Padre Vic alisema ni vema watu wakajenga utamaduni wa kufanya utafiti kuhusu mambo mbalimbali na akatoa mfano wa ugonjwa wa Ukimwi ambao alisema jamii haina budi kutafuta chanzo chake na namna ya kuuepuka.

Aliishauri jamii kutoamini na kutumia sayansi kuchunguza na hatimaye kupinga maswala ya ki-Mungu.