'Ukitaka kuona vituko hudhuria mikutano ya CUF lakini uwe macho'

Na Masha Otieno Nguru, JR

WIKI hii chama cha Kisiasa cha Civic United Front ‘CUF’ kilifanya mkutano wa hadhara ulioonekana kuwa na kila dalili za kuwa wa kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mkutano huo mkubwa na hadhara uliotawaliwa na vibweka vya hapa na pale ulifanyika kwenye viwanja vya bandari, eneo la Kurasini na idadi kubwa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi hasa ukichukulia kuwepo uchaguzi Mkuu Mwaka huu ambao sasa ni gumzo kona zote za jiji.

Lakini katika vyote vilivyofanyika kwenye mkutano huo wa CUF Jumapili iliyopita kilichonasa hisia, macho na mioyo ya watu waliohudhuria hapo haikuwa hotuba iliyotolewa na mgeni rasmi Bw. Tambwe Hiza kwenye mkutano huo bali ni vibweka na vituko vilivyoonyeshwa na mashabiki na wafurukutwa wa chama cha CUF. Ilikuwa kana kwamba unatazama sinema ya vituko, huku kituo kimoja baada ya kingine vikipewa nafasi ya kuonyeshwa jukwaani.

Ingawa ni jambo la kawaida vituko kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa lakini baadhi ya vituko vilivyoonyeshwa na wafurukutwa wa CUF, siku hiyo vimewaacha watu walioshuhudia wakijiuliza kulikoni.

Kama ilivyo kawaida yetu waandishi wa habari ni nadra kwetu kupitwa na mambo; hivyo pamoja na kuwa siku hiyo ilikuwa ya mapumziko kwangu nyumbani nilijipa moyo na kujisogeza taratibu kwenye viwanja ambako CUF walikuwa wakiendesha mkutano wao kusudi nipate kushuhudia kwa macho yangu nini kinatokea.

Kati ya vibweka vyote vilivyoonekana siku hiyo kilichonasa macho na hisia zangu zaidi si kingine bali kuku mzima wa afya aliyebebwa kwenye ungo huku akidonoa unga.

Mwanzoni sikuamini kuwa ni kuku lakini kadiri jamaa aliyembeba alivyosogea karibu ndivyo nilivyoamini kuwa huyo ni "gweno" kweli kweli kama tulivyozowea kumuita kwa lugha ya mama yangu kule Tarime kwa akina Onyango.

Jamaa aliyembeba kuku huyo hakuwa na tofauti hata kidogo na Mganga wa jadi. Kwanza alikuwa amejitanda shanga na hirizi shingoni mwake na hakuvaa shati. Mkononi mwake alishika usinga ambao alikuwa akiupepea huko na kule.

Mambo hayakukamilia hapo, bali kichwani kwa jamaa huyo alibeba ungo uliojazwa unga, na ndani yake alikuwemo kuku aliye hai, huku wafurukutwa wakimsindikiza kwa vigelegele vya ‘CUF Ngangari - asiyeipenda akameze wembe’, yule kuku aliyekuwa kichwani mwake alikuwa akiendelea kudonoa ule unga taratibu.

Wakati huo Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke Bw, Tambwe Hiza alikuwa tayari amekwishaianza hotuba yake. Wakati jamaa mwenye kuku kichwani mwake alipofikia jukwaa la kutolea hotuba ilimbidi mgeni wa heshima mwenyewe afyate mkia na kusitisha hotuba yake huku maneno ‘Asanteni sana waheshimiwa ‘ yakimtoka. Jamaa mwenye kuku kichwani alizunguka jukwaa mara tatu ndipo akasindikizwa nje ya halaiki ya watu na wapambe wake huku wakipiga ngoma na vigelegele.

Kabla Bw. Tambwe hajajiweka sawa kuendelea na hotuba yake kuliibuka kibweka kingine, safari hii haikuwa kuku tena bali nguo za ndani. Haijulikani nguo zile zilinunuliwa ama kushonwa wapi lakini kwa jinsi zilivyokuwa kubwa hata jitu la miraba minne kama hayati Pepe Kalle wa Kongo angefufuliwa leo azivae zingempwaya.

Nguo hizo tatu zilivalishwa kwenye nyaya zilizokunjwa moja ikiwa na mwandishi ‘Merry Christimas’. Sijui wafurukutwa wa CUF walioziandika hivyo walikuwa na maana gani kwa sababu kama sikukuu ya Krisimasi bado iko mbali nasi kwa miezi 8 mbele kwa sababu hata nusu mwaka hatujafikisha toka tuingie mwaka huu wa 2000.

Ama ndio tuseme huu mkutano wa Kurasini aliokuwa akiuhutubia Bw. Tambwe Hiza hapa Kurasini ndio ulikuwa Krisimasi ya wafurukutwa wa CUF jijini?. Hebu hayo na tuwaachie wenyewe wanayajua wao.

Lakini kwa vile wafurukutwa waliobeba zile nguo za ndani walikuwa ni wa kutoa chama cha CUF tawi la ‘Washington Manzese’ nahisi walizitoa kwenye marobota ya mitumba wanayoyauza pale Manzese darajani, sijui; nimebahatisha.

Lakini funga kazi akawa Mzee mpuliza zomari aliyeonyesha kila dalili kuwa alijaza pombe kichwani kabla ya kuja kwenye mkutano huu uliomleta karibu kila mfurukutwa wa CUF hapa Kurasini.

Huku akiwa kavalia ‘Over roll’ ya kijani, Mzee huyo aliyekuwa akiyumbisha yumbisha kichwa chake kwa kukolewa na kilevi alikuwa akipuliza zomari yake huku akishangiliwa. Muda wote huo vijana wakereketwa wa CUF walikuwa wakipokezana kumbeba kwa zamu.

Pembeni ya mzee huyo mwenye zomari nako alikuwepo jamaa mwingine mwenye ndevu ndefu mithili ya za manabii wa kale na mitume wa zamani. Jamaa huyo mwenye ndevu ndefu ambazo nikiziita ‘kichaka cha ndevu’ sijakosea alikuwa akisindikizwa na wafurukutwa wa CUF waliokuwa wakipiga makelele ya ‘Osama- Osama - Osama - Bin Laden.’ Sikupata fursa ya kuwauliza ni kwa nini waliamua kumbatiza palepale huyo jamaa jina la ‘Osama’ yule gaidi wa Saudi Arabia anayesakwa kwa udi na uvumba na Serikali ya Marekani. Lakini kwa waliopata kuziona picha za Bin Laden watakuwa na jibu tosha tayari kwa nini jamaa mwenye kichaka cha ndevu alipewa jina hilo.

Majina ya matawi yaliyo mengi ya CUF yalikuwa ni ya maeneo mbali mbali duniani yaliyotawaliwa na migogoro ya kisiasa na vita. Moja ya matawi hayo yalikuwa ni pamoja na ‘Chechnya, Bosnia, Palestina, Kosovo, Kwazulu Natal na Irak. Kana kwamba hilo halitoshi, kwenye mabango yenye majina ya matawi hayo kulichorwa mafuvu ya binadamu na mifupa yake na mengine yalichorwa picha za wapiganaji wenye silaha.

Kuonyesha kuwa mabango hayo yalikuwa na ujumbe wa kivitendo zaidi ya jina tu, kabla hatujataharuki Bw. Tambwe alitangaza kuwa wafurukutwa wa CUF waliompa kipigo kikali mwandishi wa habari wa gazeti la Majira warejeshe mkoba wake na lensi ya kamera mara moja ili kuepuka kuchafua jina la CUF. Ndipo nikaamini kweli Kosovo imehamia Dar es Salaam. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Waislamu Dar wamtishia mwenye bar jirani na msikiti

lWasema watamshughulikia, ni Muislamu mwenzao

Na Dalphina Rubyema

WAISLAMU wa Msikiti wa Makukula eneo la Buguruni Jijini Dar-Es-Salaam,wamemlalamikia mmiliki na wahudumu wa baa ya Kigongo kwa madai kuwa wanafungua muziki kwa sauti ya juu hali inayowafanya wasielewane na kuwa kikwazo wakati wa swala.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,Waislamu hao walisema ingawa wenye baa hiyo ambayo ipo jirani na msikiti huo wanajua muda na vipindi vyote na swala zao,bado wamekuwa wakifungua muziki kwa sauti ya juuhasa wakati wa swala na wakasema ni vyema wangethamini dini hiyo kwa kufungulia kwa sauti ya chini muziki huo wakati wa swala wasiwe kikwazo.

Imamu wa Msikiti huo Bw.Shaban Hija alisema "Mwanzoni tulipo uambia uongozi wa baa hiyo uwe unapunguza sauti wakati wa swala,mwanzoni ulianza kutii lakini baada ya muda si mrefu ,muziki ulianza kupigwa tena kwa sauti ya juu huku uongozi ukijua kuwa sauti kubwa inatukwaza na kutufanya tusindwe kuelewana katika swala".

Aliongeza kuwa hadi sasa msikiti huo haujui nia ya uongozi wa baa hiyo kufuatia hali hiyo inayofanywa kwa makusudi.

Alisema uongozi wa msikiti huo una mpango wa kuishtaki baa hiyo endapo hautajirekebisha ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Gazeti hili lilipoonana na Meneja wa baa hiyo Bw.Edward Alieza alikiri kupokea taarifa hiyo na akasema kitendo hicho kilikuwa kinafanyika siku za nyuma lakini hivi sasa baada ya kujua ratiba ya msikiti huo baa yake imekuwa makini na suala hilo.

Alisema kama kitendo hico kimekuja kurudiwa tena siku za karibuni basi kimetokana na mabadiliko ya ratiba ya swala kwenye msiti huo na mabadiliko hayo yatakuwa yamefanyika bila baa hiyo kujulishwa.

"Kama hali hiyo imejitokeza tena siku za hivi karibuni basi imetokana na kubadilika kwa ratiba ya swala msikitini hapo bila sisi kujulishwa,ratiba tuliyonayo ni kwamba inapofika saa12.55 jioni tunazima muziki hadi saa 1.25 jioni na inapofika saa 1:55 jioni tunauzima tena hadi saa 2:25 usiku"alisema Meneja huyo.

Aliongeza "Kama makosa hayo yalifanyika ni wazi kuwa hatukujulishwa juu ya mabadiliko ya ratiba ya swala msikiti hapo,tunachokiomba ni kwamba wakaifanya mabadiliko ya ratiba wawe wanatufahamisha".

Hata hivyo Meneja huyo alisema kuwa ili kuwapa nafasi nzuri ya kuswali kwa utulivu ,mmiliki wa baa hiyo Bw.Kigonho ambaye naye ni Muislamu anampango wa kuiamishia baa hiyo sehemu nyingine.

"Hatuna nia mbaya kabisa na msikiti huo kwani hata mmiliki mwenyewe ni muislamu,isitishe hata Baba yake mzazi anaswali kwenye msikiti huo"alisema

‘Watanzania ni wepesi kughilibiwa’

Elizabeth Steven na Getruder Madembwe

WATANZANIA wameelezwa kama watu wenye tabia ya kuridhika mapema kutokana na wanayoyaona au kuyasikia kabla ya kuyafanyia uchunguzi ili kujua chanzo, sababu na hatima yake hali ambayo ni hatari kimaadili.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Pius Rutechura alipokuwa akitoa mada katika semina iliyofanyika katika ukumbi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar Es Salaam, juu ya maadili na kuwashirikisha walei wa parokia zote za Jimbo Kuu la Dar Es Salaam.

Alisema migogoro na migongano mingi ya kimaadili katika jamii inatokana na watu kujipangia wenyewe mipango yao bila kuzingatia mipango na maadili ya ki- Mungu.

"Watanzania tunaridhika mapema mno bila kuchimba kwa undani wa jambo. Mfano mzuri ni hawa watu walioungua huko Uganda na kule mkoani Mbeya.

Watu walikuwa wanasoma kwenye gazeti tu, basi wamemaliza, hakuna anayetaka kuchimba ili ajue undani wa matukio hayo."

"Na hata hiyo migogoro na migongano inayojitokeza katika jamii inatokana na watu kujiwekea maadili yao wenyewe na kumuweka Mungu kando.

Sehemu nyingi za maisha watu wanajipangia mipango yao bila kujali mipango wala mapenzi ya Mungu," alisema Padre Rutechura.

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kutambua kuwa maadili ni kuishi kwa furaha na kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Alisema mtu mwenye maadili bora ni yule mwenye kuweza kuangalia na kuchambua kizuri au kibaya katika kuishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu.

"Dawa ya kujua haya ni kujiuliza, nifanye nini ili niweze kuurithi uzima wa milele?"

Semina hiyo iliyoandaliwa na CPT Jimbo KUU la Dra Es Salaam, inaendelea Jumamosi hii na kumalizika jumamosi ijayo katika ukumbi wa Mikutano wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini.

Wamorovian wasema nchi za Ulaya zinawajibika kuisaidia Afrika

Na Josephs Sabinus

LICHA ya kuwataka Wakristo nchini kuacha tabia ya kutegemea misaada ya wafadhili wa nje ya nchi kujenga makanisa na kueneza Injili, Kanisa la Morovian limesema, mataifa ya Ulaya yana wajibu wa kuboresha uchumi wa Tanzania kwani ndiyo yaliyoudidimiza wakati wa ukoloni.

Wakizungumza katika ibada Jumapili iliyopita jijini, Mchungaji Salatieli Mwakamyanda, na Mwinjilisti Barnabas Mwakaluka wa Kanisa la Morovian (T), Ushirika wa Keko, Wilaya ya Mashariki katika Jimbo la Kusini, walisema wakati umepita wa kutegemea kusaidiwa kila kitu toka kwa wafadhili ili kujenga makanisa pamoja na kufanya shughuli za uinjilishaji.

Walisema badala yake, sasa ni wakati wa kutumia juhudi, maarifa na moyo wa upendo na kujitolea kwa Mungu ili kusaidia uinjilishaji kwa kizazi cha sasa na kile kijacho.

"Wengine wanashindwa kuchangia Kanisa kwa kuwa hawajui Kanisa ni kwa ajili ya nani. Kanisa ni kwa ajili yetu na kizazi chetu kijacho. Mara nyingi tunafanya kosa kuangalia karibu. Hatuangalii habari za kesho na kesho kutwa hata katika kujenga nyumba zetu.

Tazama Marekani, hawauzi mafuta na badala yake wananunua toka Uarabuni, hii ni kwa kuwa wanakitunzia kizazi chao kijacho," alisema Mwinjilisti Mwakaluka na kuongeza,

"Ukijisikia kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa, changa kwa upendo wako kwa Mungu na kwa faida ya kizazi kijacho. Mambo ya mtu kutokuchanga kwa kudhania fedha zake zitaliwa ni upungufu wa imani na upendo. Ukiwa na wasiwasi, nunua kitu ulete kijenge Kanisa la Mungu."

Akizungumza ofisini kwake baada ya ibada, Mchungaji Mwakamyanda alisema,

"Lazima Wakristo na Watanzania kwa ujumla tujenge moyo wa kujitegemea,; hata zaidi ya 85% ili Wazungu wasituone kwamba tunawategemea sana ingawa ni wajibu wao kutusaidia kwa kuwa ndio waliobeba vitu vyetu na kuvipeleka kwao wakati wa ukoloni. Hata hivi sasa misaada wanayotupatia, wanachokifanya ni kurudisha walivyochukua."

Awali katika ibada, viongozi hao wa kiroho waliwahimiza waumini kuchangia kwa hali na mali ujenzi wa kanisa lao na shilingi 35000/= zilichangwa papo hapo kwa jili ya ununuzi wa nondo.

Katika mahubiri yake wakati wa ibada, Mwinjilisti Mwakaluka alitahadharisha,

"Hivi sasa wanaibuka ovyo ovyo tu, watumishi wa Mungu wasio waaminifu; wanapiga Injili za ajabuajabu. Wao wanacho angalia, ni mifuko yao na mambo yao ya kibinafsi.

Wanaibuka na kujiita manabii kwa interest zao wenyewe; kiuchumi na hata kisiasa."

Ujenzi wa Kanisa la Morovian , Usharika wa Keko ulioanza mwaka1996, umekwisha gharimu jumla ya shilingi milioni 25/= kati ya milioni 100/=.

Wakristo hao bado wana kazi kubwa inayohitaji moyo ili kukamilisha ujenzi huo wa jengo la kanisa ambalo ni la gorofa mbili na litakuwa na shule ya chekechea, hospitali, ofisi ya mchungaji na huduma mbalimbali.

Hata hivyo viongozi hao wametoa wito kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi kusaidia ujenzi huo ambao sasa unahitaji shilingi milioni 75/=, ili kuukamilisha.

Makamba amtaka Ritha Mlaki avae suruali

Na Leocardia Moswery

MKUU wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Luteni Yusufu Makamba, amemshauri Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Ritha Mlaki, kuvaa suruali ili aweze kukagua vizuri utaratibu wa viwanja Wilayani kwake.

Alitoa ushauri huo wakati akifunga semina ya siku moja juu ya mpango wa uboreshaji wa Serikali za Mitaa, iliyofanyika katika ukumbi wa Vatican Hotel, maeneo ya Sinza jijini Dar Es Salaam, katikati ya juma lililopita.

Mkuu huyo wa mkoa alisema, Bi. Mlaki kama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, hana budi kufanya kazi kwa bidii na akamshauri kuvaa suruali ili aweze kutembelea sehemu zote ambazo watu wake wanahitaji kupewa maeneo licha ya hali yoyote ambayo anaweza kukutana nayo zikiwamo tope kutokana na mvua.

"Mlaki ana viwanja 100 tu, ni vizuri akaenda hata kwa Rais na kumuomba ampatie viwanja vingine ili na watu wale waliojenga mabondeni wapewe viwanja vyao."

Makamba aliitaka Halmashauri ya Jiji kuwabomolea mara moja wale wote waliojenga mabondeni na akaishauri Hamashauri hiyo kuweka utaratibu wa kuwapatia magari kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao.

Hata hivyo, Luteni Makamba alisisitiza kuwa haiwezekani kumwambia mtu ahame bila wewe kumpatia sehemu nyingine ya kuhamia hivyo Halmashauri hiyo pamoja na viongozi husika hawana budi kuhakikisha kuwa wanawatafutia wananchi watakaoathirika na zoezi hilo maeneo ya kuhamia.

Alisisitiza kuwa watakaobomolewa huko mabondeni, hawatalipwa fidia ya mali zao zitakazo haribika mbali na kupatiwa maeneo mengine ya kuishi.

Luteni Makamba amewataka maafisa wote wa afya kuvaa sare sambamba na vitambulisho ili wajulikane kwa urahisi kwa wananchi wanaotembelewa wa maeneo wanayotembelea.

Vioo vyamfikisha kortini

Na Salutaba Mwakimwagile, DSJ

MKAZI wa Kijitonyama, Heri Masondi, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni jijini Dar Es salaam, kwa kosa la wizi wa vioo vya gari.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu Bi. Mary Mambali, karani wa Mahakama hiyo Bi. Blandina Mayoya alisema, mnamo Machi 24, mwaka huu, katika eneo la Kijitonyama jijini, inadaiwa kuwa mshitakiwa aliiba vioo viwili vya mbele na kioo cha nyuma vya gari mali ya Salome Kasembe, gari hiyo ilikuwa ina namba za usajili TZL 272.

Mshitakiwa amekana shitaka na amerudishwa rumande kwa kukosa wadhamini na kesi itatajwa tena tarehe 18 mwezi huu.

Katika kesi nyingine, mkazi wa Sinza Roiter Temba amemfikisha katika mahakama ya Mwanzo ya Kinondoni, Atu Amini(33) mkazi wa Sinza kwa shambulio la kudhuru mwili.

Akisoma kesi hiyo Karani wa Mahakama hiyo, Mwanahamisi Badri alisema mbele ya hakimu kuwa mnamo Machi 29, mwaka huu, Atu Amini alimshambulia mshitaki kwa kumpiga ngumi na kumkwaruza na makucha usoni hali iliyomsambabishia maumivu makali.

Mshitakiwa alikana shitaka na yuko nje kwa dhamana, kesi yake itatajwa tena tarehe 18 mwezi huu.

Katika kesi nyingine, mkazi wa Kinondoni, Bakari Seneda amepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo kwa kumchoma Kasimu Ramadhani Kisu.

Akisoma shitaka hilo msoma mashitaka, Blandina Mayaya alisema mbele ya hakimu Bi. Mary Mambali alidai kuwa mnamo Desemba 8, mwaka 1999 majira ya saa 8 usiku, mshitakiwa alimchoma kisu mlalamikaji, Kassimu Ramadhani walipokuwa wanatoka kazini kwao Osterbay Hoteli.

Mlalamikaji alidai kuwa mshitakiwa alianza kumtukana wakati yeye na wenzake wakiwa katika basi lao la kazini wakisubiri kwenda nyumbani.

Mlalamikaji alidai kuwa alipojibu matusi hayo, ndipo mshitakiwa alitoa kisu na kumchoma mara tatu.

Mshitakiwa amekana shitaka na kesi yake itasikilizwa tena tarehe 20 mwezi wa 4 mwaka huu.

WAWATA Arusha waadhimisha Jubilei Kuu

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha wameungana na wenzao nchini kote kusheherekea Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya ukristo duniani wakiwa na dhamiri kuu ya kumtumikia Mkombozi Yesu Kristu kadiri ya upendo wake.

Sherehe hiyo ilifanyika Jumapili ya Tatu ya Kwaresma katika Kanisa Kuu la Jimbo lililoko parokia ya Mt.Theresia wa Mtoto Yesu ambapo Paroko wa parokia hiyo, Padre Augustin Temu aliongoza ibada hiyo ya Misa Takatifu iliyojaa vifijo na nderemo kuashiria shangwe na furaha.

Padre Temu ambaye pia ni Makamu wa Askofu Mkuu jimbon ihumo,alikiri kufurahishwa kwake kwa adhimisho hilo la aina yake lilitanguliwa na maandamano ya WAWATA waliovalia sare ya vitenge nadhifu vyenye nembo ya Jubilei Kuu ya miaka 2000 ya ukristu duniani wakibeba aina mbalimbali za zawadi.

Katika mahubiri yake, aliielezea WAWATA kuwa ni chama cha kitume kinachomjumuisha kila mwanamke mbatizwa na Kanisa Katoliki nchini, hivyo haoni sababu ya wanawake wengine Wakatoliki kutoshiriki kikamilifu nafasi yao katika Kanisa kama WAWATA.

Sambamba na bainisho hilo, Padre Temu pia kwa msisitizo mkali aliwataka waumini waelewe tena kuwa WAWATA ni chama cha kitume na wala siyo miradi au mikopo, mikopo hawana budi kuondokana na dhana hiyo potofu ambayo haina tofauti na tabia ile iliyomfanya Bwana wetu Yesu Kristu apindue meza za wafanyabiashara hekaluni na kisha kufunga kikoto na kuwachapa kwani waligeuza hekalu kuwa ni pango la wanyang’anyi na sehemu ya biashara alisema Padre Augustin Temu.

Aidha Mwenyekiti wa WAWATA jimboni Arusha Bi. Wilhelimina Irafay aliahidi kuwa kwa ushirikiano na maparoko na vingozi wenzake wa ngazi zote wataivalia njuga dhana hiyo potofu ili kuondoa kabisa cheche za uhasama na kiburi kwani miradi au mikopo ndani ya WAWATA ni ziada tu na wala siyo lengo msingi.

Halmashauri zote kupewa 40/=m kuboresha Serikali za mitaa

Na Mwandishi Wetu

MPANGO wa kurekebisha Serikali za Mitaa (LGRP) umesema kila halmashauri itapewa shilingi 40/=m, kwa ajili ya Tume ya Kuboresha Mpango wa Serikali za Mitaa (CRT)

Akitoa mada katika semina ya siku tatu iliyofanyika katika kumbi mbalimbali ikiwa ni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Ofisi ya Wakuu wa Wilaya za Temeke na Kinondoni, Mtaalamu na Mshauri wa Maswala ya Fedha wa Serikali za Mitaa Bw. Maheke John Gikene, alisema kila Halmashauri itapewa milioni 40/= ambazo zitagawanywa katika makundi mawili ikiwa ni milioni 15 na milioni 25.

Alisema milioni 15/= zitatumika katika uporeshaji wa shughuli na kupeleka Semina za washirika(DAU)vikao vya CRT ikiwa ni pamoja na gharama zote za usafiri posho na watoka nje ya mikoa.

Nyingine ni uandaji wa taarifa mbalimbali zinazohusu(CRT), Mwenyekiti wa Serikali za mitaa pamoja na usimamizi au ufuatiliaju wa kazi zote.

Aliendelea kudai kuwa milioni 25/= zitatumika kama chachu ya maendeleo ya watu isipokuwa itaruhusiwa kununulia vitendea kazi kama Computer, Typewritter, Photocopy na fenicha za ofisini.

Bw. Gikene alisema kuwa CRT ni lazima itengeneze mpango wa kazi na vipindi vya kazi ambayo CRT itakuwa ikiwakilisha katika ngazi za juu.

Serikali yasema itawasaidia wanaosaidia wengine

Na Neema Dawson

SERIKALI Wilayani Kinondoni imesisitiza kuwa itazidi kuwasaidia watu na taasisi zote zinazotoa misaada kwa lengo la kuiendeleza jamii katika kupambana na hali ngumu ya maisha bila kujali dhehebu, kabila wala jinsia.

Hayo yalisemwa na Afisa Utawala wa Wilaya ya Kinondoni Bi. Beatrice Mwambane wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kilimo na ufugaji bora katika kituo cha Christian Professionals of Tanzania (CPT) kilichopo Bunju ‘A’ wilayani humo chenye vijana wapatao 13.

Aliwapongeza waanzilishi wa kituo hicho na kusema kuwa ni chenye manufaa kwani kinawajenga vijana na kuwakuza katika maadili mema yenye utamaduni wa kuzingatia kufanya kazi ili kujipatia riziki.

Alisema mafunzo hayo yenye manufaa kwa jamii nzima ya Watanzania yatawawezesha kujiajiri wenyewe kwa ufanisi zaidi wanapohitimu mafunzo yao.

Aliongeza kuwa kwa kutumia ujuzi wanaoupata, vijana hao pia wataweza kuwasaidia vijana wenzao wenye nia njema ya kujiendeleza na kutumia mbinu muafaka katika kupambana na ugumu wa maisha.

Kituo hicho cha CPT kilicho ndani ya Kanisa Katoliki chenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, kina eneo la ekari 50 za shamba zilizotolewa na Serikali ya Mtaa wa Bunju miaka ya 1980.

Lengo la kituo hicho ni kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana wasio na ajira ili baadaye waweze kufanya shughuli za kilimo na ufugaji ili kujinufaisha katika maisha yao na vijana hao wamekuwa wakipewa maelekezo ya kilimo cha mboga na namna ya kutayarisha maeneo kwa kilimo cha mazao ya chakula.

Wanapata huduma ya chakula na wamepewa vitendea kazi ambapo kwa kipindi hicho wamekuwa hawachangii gharama zozote zile.

Kituo pia kitatoa mafunzo mengine ya biashara, ushirika, utunzaji wa kumbukumbu na hesabu za fedha, masoko, kuweka na kukopa, Elimu ya malezi na maadili bora pamoja na uraia ambapo kituo kinapokea vijana wa kiume wenye elimu ya msingi na sekondari kuanzia umri wa miaka kati ya 15-25 na Baadye, kituo kinatarajia kupokea na muda wa mafunzo utakuwa mihula miwili ya miezi 18 kwa kila muhula.

Muhula wa kwanza utakuwa kw ajili ya mafunzo ya nadharia na vitendo na muhula wa pili ni wa uzalishaji.

Katika ufunguzi wa mafunzo hayo vijana waliwashukuru CPT kwa kuwasaidia kwa kuanzia katika mazingira mabaya ya Dar es Salaam ambayo yana kila hali ya uozo na kuwapa mafunzo maisha yao.

Awali, Mwenyekiti wa CPT Taifa Bw. Khamillius Kassalla na Mratibu wa kituo hicho Bi. Mariam Kessy waliwataka vijana hao kuongeza juhudi katika shughuli zao ili wawe na maisha mazuri mara watokapo kituoni hapo na kuanza kujitegemea.

Waratibu CARITAS watakiwa kuwa waaminifu

Na Getruder Madembwe

Waratibu wa kitengo cha kuhudumia watu waliopatwa na maafa nchini kilicho chini ya Shirika la misaada la CARITAS TANZANIA wametakiwa kuwa waaminifu pindi wanapopata misaada kwa wafadhili na kuhakikisha misaada hiyo inafika kwa walengwa.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa shirika hilo Mhasham, Askofu Agapiti Ndorobo alipokuwa akifungua semina ya siku nne iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Ktoliki Tanzania(TEC) uliopo Kurasini Jijini Dar-Es-Salam.

Mhasham Ndorobo ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mahenge alisema kuwa ni vyema misaada hiyo kuwafikia walengwa na hapo watakuwa waaminifu mbele za Mungu pamoja na kwa wale wafadhili ambao hutoa misaada hiyo.

"Tunatakiwa tuwe waaminifu katika kazi zetu na pindi tunapopokea misaada inayotoka kwa wafadhili kuwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa," alisema Mhasham Askofu Ndorobo.

Aliyashukuru majimbo ambayo yameshatoa mchango wao na yale ambayo yanaendelea kutoa msaada kwa ajili ya watu waliopatwa na mafuriko nchini Msumbiji.

Awali akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Naibu Katibu Mtendaji wa Caritas Tanzania BW. Peter Maduki aliwataka watendaji wa majimbo hayo kuhakikisha kuwa wanawakilisha kumbukumbu zao katika ofisi za CARITAS taifa pindi wanapotoa msaada kwa wahusika ili iwe rahisi kuyatambua majimbo yaliyokwisha toa misaada pamoja na kiasi na aina ya misaada nam,na inavyotumika.

"Tunaomba tuletewe taarifa mapema pindi jimbo linapotoa msaada kwa watu husika ili iwe rahisi kuwafahamisha wafadhili wetu wajue tumeitumia vipi misaada hiyo," alisema Bw. Maduki.

Semina hiyo iliwahusisha waratibu kutoka majimbo ya Kikatoliki Tanzania.

Mahakimu wanapoteza haki za watuhumiwa

Na Dalphina Rubyema

KUSHINDWA kwa mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuwaongoza walalamikaji au watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanaosimamishwa vizimbani kumepelekea walio wengi kujikuta wakipoteza haki zao.

Akizungumza katika warsha ya siku tano ya Mahakama za Mwanzo za Kanda ya Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC) Bibi Hellen Bisimba, alisema kuwa hilo ni tatizo sugu katika Mahakama za Mwanzo.

MKurugenzi huyo alisema kuwa kuna malalamiko mengi yanayofikishwa katika kituo hicho ambayo chimbuko lake ni mahakimu kushindwa kuwaongoza raia wanaofika mbele yao jambo ambalo linachangia ukiukwaji wa haki za binadamu.

Alisema kuwa kesi inaweza kutolewa hukumu lakini hakimu asimueleze mtuhumiwa kuwa ana nafasi ya kukata rufaa kama hakuridhika na adhabu iliyotolewa ha mahakama hiyo.

"Baadhi ya mahakimu wamekuwa hawawaongozi raia ili kufahamu ni nini wanaweza wakafanya nje na ndani ya mahakama"

Alisema na kuongeza kuwa tatizo hilo lipo na hufikia wakati watuhumiwa wanakuwa hawajui kama wana haki ya kupata dhamana.

Rais Mkapa awahamasisha Shinyanga wachukie umaskini

Na Charles Hililla, Shinyanga

RAIS Benjamin Mkapa amewataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuchukia dhiki na kupiga vita umaskini kwa kufanya ubunifu wa namna ya kupambana nazo kwa kutoka jasho.

Rais Mkapa alitaja siri ya maendeleo kuwa ni kukusanya nguvu za pamoja na kuanza serikali kwa upande wake itasaidia kukamilisha kutoka mahali ambapo uwezo wa wananchi umeishia.

Akiongea baada ya kutembelea ujenzi wa bwawa lililojengwa kwa nguvu za wananchi wa wilaya ya Meatu, mwishoni mwezi uliopita. Rais Mkapa aliwasifu wananchi hao kwa kuwa mfano bora wa kuchangia harakati zao za kujiletea maendeleo.

Mji wa N’gwanhuzi ambao ndio makao makuu ya wilaya ya Meatu una tatizo kubwa sana maji.

Ukubwa wa tatizo hilo uliongezeka pale bwawa lililokuwa likitumika kupeleka maji kwenye mji huo kubomoka hapo mwaka 1994.

Aidha baada ya kupata dhiki hiyo ya maji wananchi hao walikaa na kuamua kujenga bwawa kwa kutumia nguvu zao ambapo serikali baada ya kuona juhudi hizo iliongeza nguvu maradufu na kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambalo lipo nje kidogo ya mji katika kijiji cha Ng’wanyahina.

Ujenzi wa bwawa hilo umechukua takribani miezi kumi hadi kukamilika ambapo maandilizi ya ujenzi yalianza yalianza tangu mwaka 1997. Gharama zilizotumika hadi kukamilika kwa ujenzi huo ni Milioni 600 ambapo wananchi wameokoa kiasi cha Milioni nne.

Sumaye kuzindua Kanisa la Kilutheri Ukonga

Na Agatha Rupepo, DSJ

WAZIRI Mkuu Bw. Frederick Sumaye Jumapili hii anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Ukonga jijini.

Kwa mujibu wa mchungaji wa kanisa hilo, Marko Ndumi aliyezungumza na Mwandishi wa habari hizi katika ofisi za Kanisa hilo Ukonga jijini, ujenzi wa kanisa hilo litakalozinduliwa na Waziri, ulianza mwaka 1994 kwa nguvu za waumini baada ya kuona kanisa lililopo ni dogo chini ya mchungaji wa kike, Deborah Manyerere.

Alisema hadi lilipofikia sasa, kanisa hilo, limekwisha gharimu kiasi cha shilingi milioni 55/= zilizotokana na michango ya waumini.

Aliongeza kusema kuwa ili ujenzi wa kanisa hili ukamilike zinahitajika shilingi milioni 80/= zaidi.

Alisema katika sherehe hizo za kuweka jiwe la msingi, kutakuwa na harambee kwa ajili ya kuchangia kutunisha mfuko wa ujenzi wa kanisa hilo.

Sherehe hizi za uwekaji wa jiwe la msingi zitahudhuriwa pia na Askofu Jerry Mngwamba wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT.

Wakati huo huo: Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ,Usharika wa Ukonga linatarajia kuanzisha chama cha kuweka na kukopa kwa vijana.

Mchungaji Marko Ndumi amesema mpango wa kuanzisha chama hicho ni kuwasaidia waumini waweze kujiajiri wenyewe katika shughuli ndogondogo.

"Serikali sasa hivi haiajiri wafanyakazi, hivyo kupitia chama hiki vijana wataweza kujiajiri wenyewe kwa kuweka na kukopa kutoka katika chama hicho" alisema Mchungaji Ndumi.

Alisema mbali na chama hicho cha kuweka na kukopa kanisa linatarajia kuanzisha darasa la ufundi seremala na uashi ili kuwasaidia vijana wanaomaliza darasa la saba na kushindwa kuendeleza na masomo ya sekondari waweze kujiajiri wenyewe baada ya kupata mafunzo hayo.

Aliongeza kusema kuwa ujenzi huo wa darasa la ufundi utakwenda sambamba na ujenzi ya shule ya awali kwa ajili ya watoto na waumini na watoto wengine. Kutokana na tatizo la maji jijini Dar Es Salaam, Kanisa pia limeamua kuchimba kisima ili kuwasaidia wanafunzi wa darasa la shule ya awali waweze kupata maji karibu. Pialina mpango wa kujenga ukumbi wa mikutano na Hosteli.