Waziri Mkuu wa zamani atakiwa ajieleze kuhusu uchochezi kanisani

lWanaodai Dayosisi sasa wasali shuleni, waazimia muanzisha dhehebu lao

lWengine wajitoa na kudai walitaka dayosisi sio dhehebu jipya

Na Mwandishi Wetu, Mwanga

JOPO la Maaskofu wa KKKT waliotembelea Dayosisi ya Pare hivi karibuni,akiwemo Askofu Mkuu Dk. Samson Mushemba, limemtaka Mbunge wa Mwanga, Bw. Cleopa David Msuya, kuweka wazi msimamo wake juu ya tuhuma ambazo zimekuwa zikimwandama kwamba anahusika na uchochezi wa kikundi kinachofanya vurugu kikidai kuundwa kwa dayosisi mpya ya Mwanga kutoka ile ya Pare.

Habari zimeeleza kuwa Maaskofu hao waliongozana na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu ya KKKT kitaifa, zinadokeza kuwa Bw. Msuya, alikana kuhusika na uchochezi huo.

Kwa mujibu wa habari hizo walitaka kusikia kauli ya Bw. Msuya mwenyewe juu ya tuhuma ambazo zimekuwa zikimkabili.

Wakati huo huo, habari kutoka tarafa ya Ugweno, wilayani Mwanga, zimesema kuwa Jumapili iliyopita waumini wanaodai dayosisi ya Mwanga, walisali katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Minja, baada ya Serikali kuweka wazi msimamo wake kuwa kuanzia siku hiyo (Machi 26,2000) itamkamata na kumfungulia mashitaka mtu yeyote atakayevuruga utaratibu wa ibada za Dayosisi inayotambulika kisheria ya Pare.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Profesa Philemon Sarungi, ambaye alifuatana na ujumbe wa Maaskofu kutoa msimamo wa Serikali mbele ya Waumini wa Usharika wa Kifula, kwamba haitambui kitu kinachoitwa Dayosisi ya Mwanga, kwa vile haipo kisheria.

Kabla ya kutangaza msimamo huo ambao umeboresha hali ya usalama wilayani Mwanga, Sarungi aliomba asomewe Biblia, (Rumi 13:1-6) mistari ambayo inaagiza kuheshimiwa kwa mamlaka zilizopo kwani zimewekwa na Mungu.

Alilaani vikali vitendo vya uharibifu wa mali za Kanisa ambao umekuwa ukifanywa na waasi wa dayosisi ya Mwanga, hususan matukio ya hivi karibuni ya kung’oa mlango na kuvunja vioo vya Kanisa la Kifula.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Samson Mushemba, huku akipigiwa vigelegele, alisema bado msimamo wa Kanisa ni kutounda dayosisi ya Mwanga kwa vile bado haijastahili kwa mujibu wa Katiba na mipango ya Kanisa hilo.

Katika hatua nyingine imeelezwa na vyanzo vyetu vya habari kuwa waumini wanaodai dayosisi ya Mwanga, sasa wamekata tamaa, na baadhi yao wamekuwa wakirejea na kutubu huku wengine wakishindwa kufanya hivyo kwa vile walikuwa mstari wa mbele kudai dayosisi, jambo ambalo linawatia aibu.

Kutokana na hali hiyo tayari mazungumzo yameanza ya kikundi hicho kutunga katiba yake ili kiweze kuandikishwa kama dhehebu jipya.

Baadhi ya wafuasi wa kikundi hicho wamekasirishwa na kitendo hicho wakidai kwamba wao walichokuwa wanahitaji ni dayosisi na wala sio kuunda dhehebu jipya, kama viongozi wao wanavyotaka kufanya.

Machi 25, mwaka huu, Msaidizi wa Askofu Mteule wa Dayosisi ya waasi ya Mwanga, Mchungaji Maulidi Sifaeli, alitubu mbele ya waumini wa sharika mbali mbali za Dayosisi ya Pare, na mbele ya Maaskofu na Halmashauri Kuu ya KKKT, na kurejea kundini.

Sheikh asema Mbeya inaonja ghadhabu ya Mungu

lAdai Rais Mkapa anaelewa ndiyo maana hakutuma rambirambi kwa waliokufa kwa moto

Na Sadick Mgonja

SHEIKH Omar Athumani, wa msikti wa Taqua, Mwananyamala jijini amedai kuwa mkoa wa Mbeya unaongoza kwa uovu nchini, ndiyo maana Mungu ameamua kuwaangamiza kwa moto waliokuwa wakijaribu kuiba mafauta katika ajali.

"Nawasihi Waislamu wenzangu muuhame mkoa wa Mbeya kwa kuwa kiama kimeanzia huko. Hii sio siri tena kwani hata Rais Mkapa anafahamu hilo ndiyo maana hakutuma hata rambi rambi," alisema Sheikh huyo alipokuwa akihutubia waumini wa Kiislamu, Jumatano iliyopita, katika msikiti wa Taqua. Kwa kawaida Rais hutuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa mkoa husika yanapotokea maafa.

Sheikh Athumani alisema kuwa mfano dhahiri wa hasira za Mungu juu ya wanadamu ni tukio la kuungua moto kwa watu zaidi ya 30 huko Mbeya hivi karibuni.

Aliwataka Waislamu kote nchini kuanzisha operesheni maalumu ya kuondoa maovu katika maeneo yao ili kulinusuru taifa lisikumbwe na kiama.

"Kwa kuanzia, tutaonesha mfano baa zote katika maeneo ya makazi na kuwaadhibu kwa bakora wanawake wote wanaovaa nguo fupi," alitishia na kufafanua kuwa zoezi hilo litaanzia Buguruni, bila kueleza kwa nini lianzie huko.

Akielezea kiwango cha uovu mkoani Mbeya, Sheikh huyo, alisema huko ndiko kunakoongoza kwa Ukimwi na matendo ya kikatili na ya aibu nchini.

Alisema kwa mfano vitendo vya kuwachuna binadamu ngozi na kuziuza, kuwaibia majeruhi wa ajali na wafiwa hadi sanda na kadhalika, ni machache tu kati ya maajabu yanayofanyika huko Mbeya.

Askofu aonya:Tusiwaachie wachawi waongoze nchi yetu

lAwataka waumini wake wajitose kuwania nafasi za kisiasa Uchaguzi Mkuu ujao

Na Josephs Sabinus

WATUMISHI wa Mungu wametakiwa kutokwepa jukumu la uongozi serikalini na badala yake, wagombee katika chaguzi zijazo ili watumie hazina za busara za Mungu kuwaondoa baadhi ya viongozi wanaotumia ushirikina na rushwa kujipatia vyeo na hivyo kulifanya taifa lizidi kuangamia.

Mwangalizi Msaidizi wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Reuben A. Shimba, aliyasema hayo alipokuwa akihubiri katika ibada ya kuwatangaza rasmi viongozi wa parishi mpya ya Kekomachungwa jijini Dar Es Salaam Jumapili iliyopita.

Alisema licha ya kuwa na wito na hata kuombwa na jamii, watumishi wengi wa Mungu wamekuwa wakikwepa jukumu la kuiongoza nchi katika nyadhifa mbalimbali wakidhani kuwa kazi yao ni kukaa makanisani tu na kuombea ingawa wanaona taifa linaangamia kutokana na baadhi viongozi wasio waadilifu kuongoza kinyume na mapenzi ya Mungu hali aliyoiita kuwa ni kulala kwa Kanisa.

"Katika taifa letu, tatizo siyo nchi, tatizo sio viongozi, siyo sera wala katiba, na wala tatizo sio miundo mbinu wala hali ya hewa. Mungu anahitaji zaidi watu walio tayari kufanya naye kazi ili taifa lipone.

Tazama mauaji na hata hali ya uchumi ilivyo; uhalifu unaongezeka kwa kasi ya kutisha. Kazi ya utawala na uongozi katika taifa ni lazima ihusishe Kanisa maana Mungu anatafuta watu wa kusimama nao ili taifa lipone," alisema Shimba.

Akinukuu katika Biblia, (Kumb. 16: 18-20,), Shimba alisema Viongozi kutoka ndani ya Kanisa ndio wanaoweza kuondoa upendeleo na rushwa ambayo ni adui wa haki.

Akizidi kusisitiza, Mwangalizi Msaidizi huyo alisema, "Katika uchaguzi ujao, tunataka kuona tunapata vingozi toka ndani ya Kanisa.Tunataka watendaji wa kata na vijiji wawe watu wa Kanisa, tunataka wabunge, ma-DC na wakuu wa mikoa wawe watu wa Kanisa: hata rais na uongozi mwingine."

Shimba alisema kukataa uongozi serikalini kwa visingizio vya kutochanganya siasa na dini ni kukwepa majukumu kwa taifa na Mungu.

Akaongeza kwamba Tanzania ni taifa la Mungu , hivyo ni lazima liongozwe na watumishi wa Mungu wanaoweza kusikia na kuelewa Mungu anasema nini ili kutimiza mapenzi yake.

"...Inasikitisha kusikia kuwa hata baadhi ya viongozi nchini hasa wabunge licha ya kwenda kwa waganga wa kienyeji ili wapate ubunge, bado wengine wanaendelea na mambo ya namna hiyo ili wapate vyeo vingine huku wakiwa hawawajibiki ipasavyo kwa jamii.

"Hii ni kwa kuwa Kanisa limelala, lazima sasa watumishi wa Mungu wazinduke ili taifa lipone. Kuwa kiongozi wa serikali hakukuzuii kuwa mtumishi mwadilifu wa Mungu.

Fanya kazi yako sawasawa na tumia hazina yako ya hekima; Mungu atakupa hicho cheo maana kiongozi mkuu wa nchi na dunia yote ni Mungu," alisema.

Huku waumuni wa parishi hiyo wakishangilia, Mwangalizi Msaidizi huyo wa Jimbo la Mashariki na Pwani (KLPT), aliyeambatana na Mweka Hazina na Katibu wa Jimbo, alimtangaza rasmi Bw. Luther Shumbi kuwa Mchungaji wa parishi hiyo na mabwana Yohane Maimba, Bosco Kisioro Chacha na Elia Ng’onya, walitangazwa kuwa wazee rasmi wa Kanisa katika parishi.

Shimba aliwaachia waumini wa Parishi hiyo kupanga siku kwa ajili ya kuwasimika viongozi hao.

Wito huo wa kiongozi huyo wa Kipentekoste limekuja wakati baadhi ya viongozi wa vikundi vya dini wamekuwa wakitupiwa lawama hasa wanapozungumzia mambo yanayoulaumu viongozi wa serikali kwa madai kuwa wanachanganya dini na siasa bila watoa lawama kujua na kuzingatia kuwa moja ya majukumu ya viongozi wa kiroho ni kukosoa na kurekebisha mienendo mibaya katika jamii.

Epukeni kuamini watu, mwaminini Yesu - Mchungaji

Na Getruder Madembwe.

WAKRISTO nchini wametakiwa kujenga msingi wa imani yao kwa kumtegemea Yesu na wala si kwa mwanadamu kama ilivyo kwa watu wengine ambao wanajenga msingi wa imani zao kwa wanadamu.

Hayo yalisemwa na mchungaji Moses Maarifa, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kawe, katika ibada ya Jumapili iliyopita ambayo ilifanyika kanisani hapo.

Mchungaji Maarifa, alisema kuwa mtu anapojenga msingi wa imani kwa binadamu mwenzake huwa anapata shida pindi binadamu mwenzake apoanguka dhambini.

"Utakukuta mtu anajenga imani yake kwa binadamu mwenzake na pindi binadamu mwenzake huyo anapoanguka hupata shida kwani hata kama alikuwa anatoa mahubiri mazuri kiasi gani atashindwa pa kwenda kwani aliyekuwa anamtegemea ameanguka dhambini"

Mchungaji Maarifa alisema kuwa kwa mfano wale watu ambao waliangamia kwa pamoja huko Uganda na waliangamia kwa sababu wao walijenga msingi wa imani kwa binadamu na wala si kwa Yesu kwani wangekuwa wamejenga msingi wa imani yao kwa Yesu kamwe wasingekubali kuangamia kwa pamoja.

"Watu kama hao moja kwa moja wameonesha ni kwa jinsi gani wao walikuwa wamejenga msingi wa imani kwa mwadamu na kama wangekuwa wamejenga msingi wa imani kwa Yesu wasingekubali kuambiwa sasa mwisho wa dunia umefika halafu wakaangamizwa kwa pamoja"

Mchungaji Maarifa, aliwataka waumini wa dhehebu hilo kuishi katika mazingira mazuri yaani ya utukufu kwa kumtukuza Mungu na pia kwa kumtazama Mungu na kamwe mambo ya uasherati, uchoyo pamoja na ubinafsi visitajwe machoni petu.

PSRC kuwanoa wanahabari juu ya uchumi

Na Josephs Sabinus

TUME ya Rais ya kurekebisha mfumo wa Mashirika ya Umma (PSRC), imeandaa warsha ya siku mbili kwa waandishi wa habari 20 toka vyombo mbalimbali nchini juu ya uandishi bora wa habari za uchumi na biashara.

Ofisa habari wa Tume hiyo Bw. Joseph Mapunda, amesema hivi karibuni jijini kuwa taasisi nyingine zilizoshiriki kufanikisha maandalizi ya warsha hiyo itakayoanza Jumanne ijayo katika ukumbi wa Bodi ya Tanzania Audit Corporation (TAC) jijini ni Adam Smith Institute ya Uingereza na Idara ya inayoshughulikia maendeleo ya kimataifa (DIPT).

Alisema warsha hiyo itakayoendeshwa na mkufunzi aliyebobea katika mafunzo kwa wanahabari kutoka London, inalenga kupanua upeo wa waandishi katika mambo ya uchumi na biashara nchini.

Baadhi ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa na wananchi juu ya sera ya ubinafsishaji ni pamoja na maana yake namna mwananchi wa kawaida anavyonufaika na sera hiyo nafasi ya wawekezaji wazalendo na kama nchi haitaathirika huduma muhimu zikiwa chini ya wawekezaji wa kigeni.

Mengine ni kwa nini ubinafsishaji unaendana upunguzaji wa wafanyakazi na hofu ya wawekezaji wa nje kutishia uhuru wa nchi.

Kwa mujibu wa PSRC, ubinafsishaji ni sera ya kurekebisha mfumo wa uchumi toka mikononi mwa Serikali na kuwa katika sekta ya watu au mashirika binafsi ndani na nje ya nchi inatoa nafasi kwa wananchi kupata huduma bora na kwa gharama nafuu.

Chini ya sera ya ubinafsishaji watanzania wana nafasi ya kujihusisha katika zoezi hilo kulingana na uwezo wao kifedha na upunguzaji wa wafanyakazi hutokea wakati shirika lina wafanyakazi wengi kuliko mahitaji.

Waziri ashauri wagonjwa wa Ukimwi wasikimbiwe na jamii

Na Leocardia Moswery

WAZIRI wa Afya Dk. Aaron Chiduo amewataka wananchi pamoja na madaktari kuwa na uhusianao mzuri kwa walioambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na magonjwa mengine ili kuwahudumia vema na kuwafariji.

Akifungua Semina ya siku tatu iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania {TEC} mwishoni mwa juma, iliyoandaliwa na Kituo cha Tiba cha Muhimbili kwa kushirikiana na Mradi wa Taifa wa kuzuia UKIMWI, Waziri Chiduo alisema,

"Wizara yangu inashauri kwamba sekta zote na rika zote zishirikiane kwa pamoja katika kupunguza ugonjwa huo mbaya wa kuambukiza ili uweze kupungua kama mkoa wa Kagera unavyoonyesha Idadi ya watu wa UKIMWI kupungua".

Alisema baadhi ya wataalam wa afya wanakatisha tamaa hasa katika kujaribu kurefusha maisha ya mgonjwa wa UKIMWI kutokana na ugonjwa wenyewe kutokuwa na tiba wala kinga.

Waziri Chiduo aliendelea kudai kuwa semina hiyo ni kwa ajili ya kuelimisha na kupeana mikakati ya uzuiaji wa kuenea vijidudu vinavyoshambulia watu wazima na watoto, mijini na vijijini na kusababisha vifo vingi mahospitali vinavyotokea na ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema, semina ya kwanza ya namna hiyo ilifanyika tangu ukimwi ulipoingia nchini miaka 17 iliyopita na sasa wanasisitiza kitu hicho hicho kwamba watu wajilinde na gonjwa hatari.

Waziri Chiduo alisema kuwa kwa niaba ya serikali ya Tanzania na Wizara yake anawashukuru waandaji na wahudhuruaji hasa kutoka nje ya nchi ikiwa ni Sweden, Uganda, Kenya na Ethiopia na mikoa mbali mbali ya hapa nchini katika fani zote zinazohusu Afya ikiwa ni pamoja na mabigwa wa Afya na hospitali binafsi zilizoshiriki katika semina hii. kama Kifua Kikuu {TB}, kuharisha na yote yanayofanana na ugonjwa huo.

Wanaonyolewa saluni kuambukizwa Ukimwi?

Na Peter Dominic na Josephs Sabinus

WIZARA ya Afya haijafanya utafiti wowote juu ya maambukizo ya UKIMWI kupitia saluni za kunyolea nywele na huenda watu wengi wakawa hatarini kuambukizwa kwa kuwa vifaa vinavyotumika havichemshwi ingawa baadhi ya wateja hutoa damu wanaponyolewa.

Imesema endapo wananchi wana mashaka ya kusababishiwa vidonda na mashine watumiazo vinyozi wa mitaani labda kutokana na uchakavu basi wajinunulie mashine zao wenyewe na hivyo kuziepuka zile za vinyozi na pia mashaka hayo yaripotiwe kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mary Mwaffisi ameliambia Kiongozi hivi karibuni kwa njia ya maandishi wakati lilipotaka kujua kama Serikali imekwisha fanya utafiti wowote kujua kama saluni hizo zinachangia kueneza ungonjwa hatari wa Ukimwi na hatua za tahadhari zilizokwisha chukuliwa.

Alisema, "Wizara ya Afya haijafanya utafiti wowote kuhusu hatari ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi kwa kupitia mashine za kunyolea.

Aidha, wizara ya Afya haijapokea takwimu zozote za utafiti wa kisayansi uliofanyika mahali popote nchini au kwingineko duniani zilizoonyesha hatari hiyo"

Hata hivyo alisema, "vifaa vitumiavyo na vinyozi wa mitaani ni mashine za kunyolea zitumiazo umeme ambazo kwa matumzi ya kawaida, zinakuwa na uwezekano mdogo sana wa kukata ngozi."

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa ipo hatari ya wananchi kuambukizwa Ukimwi kwa kuwa saluni watumiazo hazichemshi vifaa vyao ingawa watu wengi hutoa damu wanaponyolewa kwa kukangua mapele ya ndevu na kuweka mistari kichwani na hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la saluni na vinyozi ambapo wengine huendeshea shughuli zao chini ya miti bila kutumia umeme wala kubadili nyembe ili kubana matumizi na kuongeza kipato chao.

Wakati huo huo: Mtaalamu mmoja ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Magonjwa ya kuambukizwa na kinga ya mwili (microbiology & Immunology) katika Chuo Kikuu kishiriki cha Muhimbili DK. Willy Urassa, amesema,

"Mimi sijawahi kuona takwimu za namna hiyo lakini ninashauri ili kuavoidi hii risk ya maambukizo ya ukimwi, ni vema kila mtu akawa na vifaa vyake; kazi ibaki kumtafua fundi (kinyozi) akunyoe unavyotaka."

 

Mlalamikaji,hakimu ‘wagongana’ juu ya Uzanzibari

Na Mwandishi Wetu

MLALAMIKAJI katika kesi ya madai, Hassan Halawi(32), ameishangaza Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni baada ya kuulizwa kabila lake na yeye kung’ang’ania kuwa ni Mzanzibari kwa kuwa Zanzibar hakuna makabila hivyo kuzua mabishano kati yake na Hakimu yaliyokuwa burudani kwa waliokuwapo.

Mahojiano na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni jijini, Bibi Matrona Luanda, anayesikiliza kesi hiyo mlalamikaji akimdai Bw. Zinga S. Zinga, mkazi wa Magomeni Mwembe-Chai wilayani Kinondoni katika mkoa wa Dar Es Salaam, amlipe deni lake la shilingi laki tatu anazomdai sasa baada ya kumuuzia, gari lake, yalikuwa hivi:

Hakimu: Mdai taja kabila lako.

Mdai: Mimi kabila langu Mzanzibari

Hakimu: Hilo siyo kabila bali ni eneo unalotoka, kutamka hivyo ni sawa na mimi mtu aniulize kabila langu ni nani na nimjibu kuwa ni Mtanzania Bara; wakati Bara kuna Wangoni, Wadengereko, Wasukuma na makabila mengine, sasa wewe kabila lako ni lipi?

Mdai: Mheshimiwa mama Hakimu sisi huko Zanzibar hatuna mambo ya makabila kama ilivyo huku Bara, ninacho fahamu mimi ni Mzanzibari, basi.

Awali mdai pia alitoa mpya alipong’aka alipotakiwa na mwendesha mashitaka ambaye ni Chema Kombo, kusema neno, "Bismilahi" wakati wa kuapa kabla ya kutoa ushahidi wake hadi Hakimu alipoingilia kati.

Katika ushahidi wake, mdai aliiambia mahakama kuwa Mei 19, 1996, alimuuzia Zinga S. Zinga gari aina ya Toyota Hiace, yenye namba za usajili TZL 6685 kwa shilingi milioni 3.

Aliendelea kuwa siku hiyo Bw. Zinga alilipa sh. Milioni 2.6 na kuahidi kulipa kiasi kilichobaki cha shilingi laki 4, baada ya mwezi mmoja.

Aliongeza kuwa tangu wakati huo hadi sasa mdaiwa alikuwa hajamlipa kiasi cha pesa kilichobaki mbali na shilingi laki moja aliyompa mdogo wa malamikaji bw.Omari Ifaya.

Mdaiwa likiri madai hayo na mahakama kumtaka alipe kiasi anachodaiwa pamoja nagharama ya kesi hiyo ambayo ni shilingi 40,000 na malipo hayo yafanyike kwa awamu.

Serikali nchini yatakiwa ijifunze kutokana na maafa ya kidini Uganda

Na Dalphina Rubyema.

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imetakiwa kulichukulia tukio la hivi karibuni la waumini wa kanisa moja nchini Uganga kama fundisho na hivyo kuwa makini katika usajili wake wa vikundi vya dini.

Changamoto hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturjia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Juliani Kangalawe, alipozungumza na mwandishi habari hizi ofisini kwake.

Alisema ili kuepukana na balaa kama hilo la kitendo cha mamia ya wafuasi wa dini ya Movement for Restoration of Ten Commandments of God, kufungiana ndani na kulipuana kwa moto, serikali kabla ya kukisajili kikundi chochote cha kidini, haina budi kuchunguza na kuelewa utendaji na maadili ya kikundi hicho kwa misingi ya uwazi.

"Kusajili vikundi vya dini ambavyo havina mwavuli na wala havitambuliki historia yake ni hatari kubwa, mfano mzuri ni huo wa Uganda.Hii ni changamoto kwa nchi nyingine ikiwemo Tanzania," alisema Padre Kangalawe.

Alisema Serikali haina budi kushikilia msimamo wake kwamba dini isilete vurumai ndani ya nchi kwani kuruhusu hali hiyo ni kuvuruga amani, hasa ikizingatiwa kuwa dini inagusa mioyo ya wengi.

Akizungumza juu ya mapadre waliotengwa na Kanisa Katoliki nchini Uganda kuwa miongoni mwa kikundi hicho, alisema kuwa hiyo ni ishara ngumu sana.

"Mapadre waliotengwa na Kanisa Katoliki kujihushisha katika kikundi hicho kilichojichoma moto ni ishara ngumu sana kusema; kweli inatisha," alisema Padre Kangarawe bila kutoa ufafanuzi zaidi.

WAKATI HUO HUO:Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste, Askofu Silyvesta Gamanywa amesema kwa kuwa dini sambamba na kusali sio vitu vya siri, serikali ichunguze na kudhibiti dini zote zinazoendesha shughuli zote kwa siri.

"Uenezaji wa dini lazima uwe identified clearly. Hakuna haja ya kunyamazia dini za sirisiri," alisema.

Takribani wiki mbili zilizopita waumini wapatao 500 wa Kikundi cha Movement for the Ten Commandments of God nchini Uganda, waliteketea na moto ndani ya Kanisa lao lililopo katika kijiji cha Kanungu.

Hata hivyo, baada ya mauaji hayo polisi nchini humo ilifanikiwa kupata maiti nyingine zilizo kuwa ndani ya kaburi moja lililopo nyumbani kwa kiongozi wa kikundi hicho Bw. Dominic Kataribabo, ambaye ni Kasisi wa zamani wa Kanisa Katoliki la Rugazi, kusini magharibi mwa Uganda.

Idadi ya maiti waliokutwa kwenye kaburi hilo ilikuwa ni watoto 26 na mjamzito mmoja ambapo katikati ya wiki hii walikuta tena maiti sita katika kaburi moja nyumbani kwa kasisi huyo wa zamani, likiwa na maiti 81.

Wiki moja iliyopita maiti nyingine 153 zilifukuliwa nyumbani kwa kiongozi mwingine wa kikundi hicho.

Kufuatia maiti hizo idadi ya watu waliokufa kutokana na mkasa huo kuwa zaidi ya 700.

Rupia awaponda wanaosomesha watoto nje

Getruder Madembwe na Elizabeth Steven

MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, Balozi Paul Rupia, amewataka baadhi ya wazazi kuacha tabia ya kuwapeleka watoto kusoma nje ya nchi kutokana na kuipuuza elimu itolewayo nchini wakati ni ya kiwango cha kutosha.

Balozi Rupia, aliyasema hayo hivi karibuni katika hafla ya kuchangia mfuko wa kujenga shule ya msingi ya ST.THERESE OF LISIEUX KINDARGARTEN eneo la Ukonga jijini Dar-Es-Salaam.

Jumla ya Shilingi 11,422,000 ikiwa pamoja na ahadi zilipatikana katika mchango huo ambapo wazazi wa watoto wa shule hiyo walitoa Sh.50,000 kila mmoja ambayo na kupata jumla ya sh.6,650,000.Ili jengo hilo kukamilika, jumla ya sh 150,000,000 zinahitajika.

Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ambalo ndilo mmiliki wa shule hiyo lenye makao makuu katika Jimbo Katoliki la Bukoba mkoani Kagera, lilichangia shilingi Milioni 2.

Katika hafla hiyo, Balozi Rupia aliyekuwa mgeni alisema, wazazi wengi wametawaliwa na dhana potofu kuwa elimu ya nje ndiyo inayofaa zaidi kuliko hapa nchini bila kuzingatia kiwango cha ubora wa elimu yenyewe.

"Wazazi wengi huwapeleka watoto wao nje wakidhani kuwa elimu inayotolewa nje inafaa zaidi na hiyo siyo kweli kabisa kwani hata hapa Tanzania kuna elimu ya kutosha,"

Alisema na kuongeza, "Ni heri hayo mamilioni ambayo mnayatumia kuyapeleka nje mkayaacha hapa hapa Tanzania ili kuweza kujenga shule zetu na kuimarisha pale zinapopungukiwa."

Akizungumzia elimu katika wilaya yake ya Ilala, alisema bado ipo nyuma kwa kuwa kuna shule chache za msingi na hata hizo wamezirithi.

Aliwapongeza masista wa shirika hilo lenye makao yake makuu mkoani Kagera kwa kuanzisha shule hiyo ya msingi.

Awali katika risala yake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Sista Perpetua Muhana alisema, shule hiyo ilianza kwa madarasa ya watoto wa shule ya awali, Januari7,1999 chini ya usimamamizi wa Mama Mkuu, Hyasinta Misingo.

 

CARITAS Tanzania yaanzisha mfuko kusaidia maafa ya Msumbiji

Na Dalphina Rubyema

SHIRIKA la misaada ya kimataifa la Kanisa Katoliki (CARITAS- TANZANIA), limeanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kusaidia walioathirika na mafuriko nchini Msumbiji. Kwa mujibu wa taarifa ya mwenyekiti wa Shirika hilo nchini Askofu Agapiti Ndorobo,mfuko huu utapokea michango toka majimboni na kwa watu binafsi.

Katika taarifa yake Mhashamu Ndorobo amesema Kanisa Katoliki duniani kote limetoa wito kwa dunia nzima kuwapa misaada waathirika wa Msumbiji katika kipindi kigumu walichonacho sasa kufuatia mvua kubwa iliyoanza hivi karibuni na kusababisha maafa ya mafuriko.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo habari kutoka Msumbiji zinasema ingawa misaada ya kibinadamu itahitajika kwa kipindi cha miezi sita ijayo bado misaada inayopatikana sasa haijafikia walau kiwango cha chini cha mahitaji muhimu kama madawa, chakula na mavazi.

Mvua kubwa iliyoanza kunyesha nchini Msumbiji imesabibisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na mafuriko yaliyosababisha maelfu ya wananchi kupoteza mali zao na nyumba na hivyo kulazimika kuishi milimani na juu ya miti.

Misaada ya haraka ya kibinadamu toka kwa wenye mapenzi na moyo mwema inahitajika haraka.

Taarifa hiyo ya Mhashamu Ndorobo imesema michango hiyo haina budi kupelekewa moja kwa moja katika Idara ya Fedha ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na nakala ya makabidhiano hayo ipatiwe Katibu Mtendaji wa Caritas Tanzania kwa utaratibu.

WAKATI HUO HUO: Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Msumbiji kufuatia maafa ya mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.

Katika salamu zake kwa niaba ya baraza zima la TEC na Kanisa zima Katoliki nchini, Kardinali Pengo amesema Wakatoliki nchini wamepokea kwa masikitiko taarifa za maafa hayo kwa wananchi wa Msumbiji.

"Tunaungana na Kanisa Katoliki la Msumbiji katika maombolezo ya vifo vya watu hao," inasema sehemu ya rambirambi hizo.

Msitende dhambi kwa kukata tamaa - Ushauri

Na Elizabeth Steven

WAUMINI wa madhehebu mbalimbali nchini wametakiwa kuwa na moyo wa upendo, unyenyekevu, huruma, uvumilivu na ujasiri wa imani ili kutenda mema badala ya kukata tamaa na hivyo kuenenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Wakizungumza kwa pamoja na gazeti hili jijini hivi karibuni, Wainjilisti Joseph Giyo wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T), na Ajuaye R. Ubwe wa K.K.K.T Usharika wa Tabata, walisema vitendo vya uharifu kwa baadhi ya waliokuwa waumini wazuri wa dini mbalimbali vinatokana na kukata tamaa ya kimaisha na kiroho na hivyo kuamua kufanya kinyume na mapenzi ya Mungu ikiwa ni pamoja na kukosa upendo, unyenyekevu, huruma na uvumilivu.

Walisema, waumini hao hawapaswi kukata tamaa bali tuongeza maombi yanayoambatana na imani na matendo safi hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma.

"Tupo katika Kwaresma, hivyo sasa inatupasa zaidi kutenda ya kumpendeza Mungu. Lazima sasa tuwe na upendo na uvumilivu na imani tele," alisema Ajuaye.