KITIMTIM CHA UCHAGUZI MKUU UJAO

Kampeni zaanza kwa mikiki

lWanafunzi wa Jangwani wachenguka, kunengua na kuhama madarasa

lMsafara wa Mrema wasimama kuupisha wa Mkapa

lLipumba amuomba kura Makame

lCheyo azomewa, aambiwa atachemsha

Peter Dominic na GetruderMadembwe

BAADA ya kukubaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupokea fomu, vyama sita vya siasa vimekabidhi fomu kwa Tume hiyo na kivumbi cha kampeni za kuwanadi wagombea kinaanza leo katika viwanja mbalimbali.

Habari zilizopatikana jijini zinasema wakati mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, kitamtambulisha rasmi mgombea wake wa urais, Benjamini Mkapa na kutangaza ilani yake ya uchaguzi.

Mkapa atatambulishwa rasmi akiwa na mgombea wa Makamu wa Rais kwa tikiti ya CCM Dk. Omar Ali Juma. Kazi ya kuwatambulisha wagombea hao wa CCM, itafanya na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi. Mkuatano huo wa uzinduzi pia utahudhuriwa na mgombea urais wa Zanzibar , Aamani Abedi Karume.

Shughuli hiyo rasmi ya kuzindua kampeni hizo itafanyika saa 6:00 mchana katika Viwanja vya Jangwani.

Mgombea wa kiti hicho kwa tikiti ya chama cha CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, pia ataunguruma na chama chake kuzindua kampeni hizo saasa 8:00 mchana eneo la Kidongo Chekundu. Viwanja vyote vipo jijini Dar-Es-Salaam.

Chama cha TLP kitafanya uzinduzi wa kampeni katika viwanja hivyo vya Kidongo -Chekundu Jumapili hii wakati chama cha siasa cha NCCR-MAGEUZI kitazindua kampeni zake katika viwanja vya Obwere huko Shirati katika Jimbo la Uchaguzi la Rorya mkoani Mara Agosti 24kikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. James Mbatia.

Jana Rais Mkapa alidamkia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kurudisha fomu yake ambapo alikuwa mgombea wa kwanza wa kiti cha urais, kurudisha fomu yake iliyopokelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame.

Shamra shamra za rais Mkapa kurudisha fomu yake zilisaidiwa na gari jipya la TOT namba TZF 7756 aina ya SCANIA lililokuwa na kikundi cha watumbuizaji wa matarumbeta.

Baada ya Rais Mkapa kuzungumza na mabalozi wa nyumba kukmikumi wa CCM katika ukumbi wa Diamon Jubilei, na msafara kufika eneo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani na sauti kubwa ya nyimbo za muziki kuingia masikoni mwao, wanafunzi waliokuwa nje ya shule katika eneo hilo, walilivamia gari hilo na wengine kupanda juu na kisha kuambatana nalo huku wakicheza hadi Makao Madogo ya chama hicho tawala yaliyopo Lumumba.

Katika hekaheka hizo majira ya saa saba hivi, msafara wa mgombea wa TLP Bw. Augustine Mrema, kuelekea Tume ya Taifa ya Uchaguzi ukitokea Manzese, uliokuwa na magari mawili, ulijikuta unasimama katika kituo cha Faya katika Barabara ya Morogoro hadi gari la kampeni la Mkapa lililokuwa nyuma lilipopita. Wakati huo, Rais Mkapa hakuwepo katika msafara huo.

Wakati vyama hivyo vikirudisha fomu zao kwa ajili ya wagombea urais, wapambe waliowasindikiza walikuwa wakiimba nyimbo na kupigana vijembe.

Mgombea urais wa chama cha UDP, Bw. John Cheyo (Mapesa) alipofika na kuteremka toka kwenye gari lake kuelekea ofisi ya Tume ya Uchaguzi majira ya saa tisa hivi alasiri, baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani waliokuwa nje ya ofisi za Tume hiyo katika jengo la "Post House", walianza kumzomea huku wakisema, "Umekataa Muungano, Utachemsha."

Baada ya fomu zake kupokelewa, Lipumba alipeana mkono na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Makame huku akimwambia, "Tunashukuru, lakini na wewe naomba kura yako."

Kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Pili wa Kidemokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, zitamalizika Oktoba 28,mwaka huu.

Juzi Rais Mkapa alikemea tabia ya kuuza na kununua shahada zakupigia kura na akasema wanaofanya hivyo, wote wanafanya kosa la jinai.

LICHA YA MADAI YA KUNYANYASWA CUF, LIPUMBA ASEMA:

Kususia Uchaguzi ni kumwacha nguruwe ale mazao

lAsema utakufa kwa njaa ukidhani unamkomoa

l"Tume haiwezi kusitisha uchaguzi kwa ajili ya CUF’

Na Neema Dawson

MGOMBEA wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema chama chake hakiwezi kususia uchaguzi hata kama kitanyanyaswa kwa kuwa kufanya hivyo, ni sawa na kumsusia nguruwe aendelee kula mihogo ukidhani unamkomoa kumbe unajikomoa mwenyewe.

Lipupumba ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha CUF, alisema muda mfupi baada ya kuzungumza na waandishi wa habari jkatika ukumbi wa Idara ya habri (MAELEZO) jijini Dar-Es-Salaam, katikati ya juma gazeti hili lilipotaka kujua hatua ambazo CUF itachukua kufuatia madai ambayo yamekuwa yakitolewa na wanachama wa chama hicho kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwandendei haki na inawanyanyasa wapinzani

"Hatuwezi kususia uchaguzimambo yatakuwa magumu ingawa tunapata matatizo na misukosuko katika kipindi hiki cha uandikishaji, na tunajua hata katika kampeni na uchaguzi. Tunajua kufanya hivyo, tutakuwa sawa na kumuona nguruwe ameingia katika shamba lako la mihogo badala ya kumfukuza, ukasusia kumfukuza.

Matokeo yake, atakula amalize shamba zima na atakaye athirika na njaa ni mwenye shamba na si nguruwe," alisema.

Lipumba alisema kususia uchaguzi hakusaidii kitu kwa kuwa hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kubadiliwala kusitisha uchaguzi.

"Endapo tutasusia uchaguzi sidhani kama Tume ya Uchaguzi inaweza kusitisha zoezi hilo kwa sababau eti CUF wamegoma isipokuwa, uchaguzi utafanyika na watakao athirika, ni wanaCUF na si Tume wala mtu mwingine," alisema.

Alisema serikali imeongeza majeshi katika Visiwa vya Zanzibar wakiwamo Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wenye silaha vikiwamo vifaru na akamtaka Rais Mkapa kusitisha zoezi hilo kwani linatia hofu kwa wakazi wa visiwa hivyo.

Alisema zaidi ya Watu 126 wakiwemo mawakala wa wanachama wa CUF wamekamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu wanapoteseka bila sababu.

Alisema hizo ni mbinu za makusudi za kukidhoofisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 29, mwaka huu utaowachagua madiwani, rais na wabunge kwa mara ya pili katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa.

Wanahabari waambiwa wasiendeshwe na nguvu za uchumi

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Vyombo vya habari nchini vimeshauriwa kuhakikisha kuwa haviongozwi na nguvu za uchumi na maslahi binafsi bali vifanye kazi yake kwa utakatifu na uadilifu.

Mwenyekiti wa Idara ya Habari wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Askofu Anthony Banzi alitoa ushauri huo wakati akifungua warsha ya siku nne juu ya upashanaji habari katika ukumbi wa Hoteli ya Panori mjini hapa hivi karibuni.

Katika warsha hiyo ya kitaifa ya Kanisa Katoliki iliyowashirikisha wawakilishi wa idara za habari za majimbo kumi ya kanisa Katoliki Kanda ya Mashariki, Mhashamu Banzi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, alisema licha ya ukweli kwamba vyombo vya habari hutoa elimu, burudani na habari kwa urahisi katika jamii, si busara kusambaza kila jambo hata linalobomoa jamii kwa kuwa hata uhuru wa kujieleza una mipaka yake ukiwamo wajibu wa kuheshimu hadhi na uhuru halali wa wengine eti pengine kwa kisingizio cha uchumi.

"...Ni kazi yenye athari kubwa sana kwa mawazo ya umma. Haiwezi kuongozwa na nguvu za uchumi, faida binafsi au vikundi, bali inaongozwa na wazo la kazi takatifu", alisema na kuongeza kuwa, vyombo vya habari vimekabidhiwa jukumu la kuhabarisha jamii kwa faida ya wote hasa wanyonge, watoto maskini, wagonjwa na wanaobaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila, jinsia na udini.

Alisema fani ya upashanaji habari ina maadili yake ambayo hayana budi kuzingatiwa.

Aliyataja baadhi ya maadili hayo kuwa ni pamoja na kujenga jamii ya watu wenye misingi ya mshikamano, haki na upendo, kueneza ukweli juu ya uhai wa mtu na utimilifu wake katika Mungu.

"Kristo ni shahidi mwaminifu, umtazame na kumuiga yeye. Kanisa na wanahabari washirikiane kutumikia familia ya binadamu na Mungu kwa jumla," alisema.

Mhashamu Banzi alivihimiza vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vinavyoharibu utamaduni na maadili ya mwanadamu yanayotimiza mapenzi ya Mungu duniani na hata mbinguni.

Alisema vyombo vingi vya habari vimekuwa vinatumiwa katika kampeni za kueneza ushawishi wa habari zinazochochea maasi badala ya kutumika kutangaza habari za Mungu.

Alitoa mfano wa nchi za Magharibi kuwa zimekuwa mstari wa mbele kwa kufuata tamaduni zinazomdhalilisha mwanamke na kushawishi mambo mengi ya kushirikiana kwa manufaa ya wakubwa.

"Wengi wanatumia vyombo vya habari kueneza ulevi na uzinzi kwa kusambaza kondomu, kushawishi wasichana wafanye kafara kutoa mimba huku wakidai kuwa kufanya hivyo si dhambi," alisema.

Ujumbe wa Siku ya Upashanaji Habari Duniani mwaka huu, ulikuwa ni kumtangaza Kristo katika Vyombo vya Habari mwanzoni mwa milenia mpya na maadhimisho hayo kitaifa yalifanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony, jimboni Tanga.

Kwa kawaida, maadhimisho ya siku hiyo kitaifa hufanyika Jumapili ya Kwanza ya Mwezi Agosti kila mwaka.

Katika ibada ya Siku ya upashanaji habari iliyoendeshwa na Msaidizi wa Askofu, Mheshimiwa Padre Casmir Magwiza, kwa niaba ya Askofu Banzi, Padre Magwiza alisema upashanaji wa habari una msingi na chimbuko katika upendo wa Mungu kwa vile huwatumia manabii, mababu, maono, na njia mbalimbali hatimaye njia ya Mwanawe ili ajitambulishe mwenyewe kwa mapenzi yake.

Alisema ingawa vyombo vya habari vinasaidia kupata taarifa za furaha, upo uwezekano wa vyombo hivyo vikapasha habari za uchungu ingawa alisema kwa hulka yake vyombo vya habari si vibaya.

"Mahusiano na vyombo vya habari yalivyo wema au ubaya haupo katika chombo bali upo ndani ya mtumiaji wa chombo. Vitakuwa mwenzi bora kama mtumiaji wake amejengeka katika dhamira safi. Vitakuwa mwenzi mbaya iwapo mtumiaji atapitisha humo maovu yake," alisema.

Alishauri watumiaji wafundishwa ukweli juu ya Mungu na huruma yake kwa kupinga ubinafsi na kutangaza haki za binadamu tangu kutungwa kwa mimba hadi kukua kwake.

CORAT AFRICA yawashauri viongozi wasing'ang'anie madaraka

Na Getruder Madembwe

MTAALAM wa mambo ya fedha kutoka shirika la CORAT AFRICA la Nairobi nchini Kenya, Bi. Valentine Gitoho, amewashauri viongozi wa sekta mbalimbali kukubali kirahisi kuachia nafasi zao za uongozi pindi muda wao unapokwisha badala ya kung’ng’ania kuwapo madarakani kinyume na taratibu.

Aliyasema hayo katikati ya juma lililopita, wakati akitoa mada katika semina ya wahasibu 22, mashirika 20 ya Kanisa Katoliki kutoka katika kanda tano za RWSAT ambazo ni Mashariki, Magharibi, Kaskazini Kusini na Kanda ya Ziwa.

Bi. Gitoho alisema kuwa kuachiana nafasi za uongozi ni vizuri kwani viongozi wote wanachaguliwa kutokana na neema ya Mungu.

"Haitakiwi kung’ang’ania madaraka kwani huwa sio vizuri na mtu yeyote ambaye hataki kubadilishana na wenzake anakuwa na kila kujipendelea (selfish) na wala Mungu au jamii haipendezwi na tabia hiyo" alisema.

Aliwataka wahasibu hao kushirikiana ili kuleta mafanikio katika utendaji wao wa kazi na kuelimisha watu walioko karibu nao juu ya masuala muhimu katika maisha yakiwamo uongozi.

Alisema mashirika hayana budi kujifanyia shughuli mbalimbali za maendeleo ili badala ya kutegemea kila kitu kutoka kwa wafadhili.

Awali, Katibu Mkuu wa RWSAT ,Sista Fides Mahunja ameliambia KIONGOZI kuwa, lengo la warsha hiyo ya wiki mbili, ni kuwapa wahasibu hao mafunzo na mbinu mbalimbali juu ya utunzaji wa kumbukumbu na pesa.

Alisema hawanabudi kuwa wakamilifu kwani wao ni sehemu muhimu na ni viongozi wakuu wa mashirika.

"Wahasibu hawana budi kuwa waaminifu katika utendaji wao wa kazi kwani wakuu wa mashirika, wanawategemea sana," alisema Sista Mahunja.

Alisema wahasibu hawana budi kuonesha ama kutoa ripoti sahihi kwa wakati muafaka kuonesha ni jinsi gani fedha na mapato mengine ya mashirika, yametumika.

Aliwataka pia wakubali mabadiliko katika utunzaji wa kumbukumbu za fedha. Alisema, kwa mfano, kama zamani walikuwa wakihifadhi kumbukumbu hizo kwa kuziandika vitabuni, sasa wanaweza kutumia kinakilishi (kompyuta).

Akifungua semina hiyo, Kaimu Katibu wa Idara ya Fedha wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Bw. Manase Kally, aliwataka wahasibu hao wafanye kazi zao kwa kujidhatiti kwani kitengo cha kudhibiti fedha kinazidi kukua siku hadi siku katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Aliwataka kuyaendeleza na kuyafanyia kazi wanayojifunza kwani wao ni watendaji muhimu katika Kanisa.

Semina hiyo ya wiki mbili inaendelea katika Kituo cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar-Es-Salaam na mafunzo yanatolewa na wataalum kutoka CORATAFRICA.

Wakurugenzi wa habari wapigwa msasa

Padre Chrysantus Ndaga na Padre Andrew Luanda, Tanga

WAKURUGENZI wa Habari wa majimbo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Mashariki, "wamepigwa msasa" juu ya mbinu bora na za kisasa za upashanaji habari katika kumtangaza Kristo mwanzoni mwa milenia mpya.

Katika warsha iliyoandaliwa na Idara ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), washiriki walifundishwa mbinu mbalimbali za ukusanyaji na usambazaji wa habari ambapo pia washiriki walifanya mazoezi ya vitendo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano wa TEC, Padre Raphael Kilumanga, aliwahimiza wanahabari wa majimbo mbalimbali ya Kanisa, kutokalia habari za majimbo yao na badala yake, wazitangaze kupitia magazeti ya KIONGOZI na MWENGE.

Alisema kwa kufanya hivyo, Wakristo na wanajamii mbalimbali watapata fursa ya kujua mambo yanayofanyika ndani ya Kanisa ili kujifunza na kuendeleza mazuri yote yanayohimzwa katika kuifanya kazi ya Mungu.

Padre Kilumanga aliwaomba washiriki wa semina hiyo ya kitaifa iliyofanyika katika Jimbo Katoliki la Tanga, kuhahakikisha kuwa, walengwa wanapata ujumbe uliokusudiwa kwa kuwafikishia na kusaidia usambazaji wa gazeti haya ambayo yanasambazwa kwa mtandao wa makanisa yote nchini, na huku KIONGOZI likiwa katika mtandao wa kompyuta duniani.

Washiriki waliliomba kanisa kuandaa semina za namna hiyo mara kwa mara ili kuboresha zaidi utendaji wa wanahabari ndani ya Kanisa.

Washiriki hao waliopata nafasi ya kutembelea mapango ya Amboni(Amboni Caves) yaliyoko umbali wa kilomita 5 hivi kutoka mjini Tanga kuelekea Mombasa, walijionea pia utajiri mkubwa wa maliasili iliyoko Tanga na katika mazungumzo kwa nyakati tofauti na gazeti hili, walishauri mapango hayo yaendelezwe zaidi kwa manufaa ya taifa.

 

Warsha hiyo iliyofanyika Agosti 9 hadi 13, mwaka huu, ilihitimishwa na sherehe za Siku ya Upashanaji Habari Duniani zilizofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony, lililopo Chumbageni jimboni Tanga.

Kanisa laipongeza serikali

Na Lazaro Blassius, Tanga

KANISA Katoliki nchini limeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa ushirikiano inayoonesha kuzisaidia taasisi za kidini kutangaza imani zao kupitia vyombo vya habari vya taifa yaani Radio na Televisheni.

Pongezi hizo zimetolewa na Mratibu wa vipindi vya dini Radioni wa Idara ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu T.E.C, Padre Paul Haule alipokuwa akitoa taarifa ya idara yake kwenye semina ya wanahabari wa Kanisa Katoliki, wa majimbo ya Kanda ya Mashariki iliyofanyika katika Hoteli ya Panori mjini Tanga hivi karibuni.

Padre Haule alisema Radio ya Taifa (RTD), hutangaza vipindi viwili vya dini kila siku asubuhi na usiku na vipindi vitano kwa siku za Jumapili.

Alisema vipindi hivyo hurusha hewani kwa ushiriakiano baina ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), na Jumuiya ya Makanisa (CCT).

Kuhusu Televisheni ya Taifa (TVT), Padre Haule alisema, imetoa muda wa nusu saa kila Jumapili na hivyo akatoa wito kwa wanakanisa kujitokeza kuandaa vipindi vya dini ikiwa ni pamoja na makundi ya kwaya za majimbo mbalimbali.

Akizungumzia gharama za matangazo yanayorushwa moja kwa moja na RTD wakati wa sherehe na sikukuu za Kanisa, Padre Haule, alisema, Radio hiyo ya Taifa hutoa punguzo maalum kwa ajili ya matangazo ya nje kwa sikukuu zaKikristo kama ya Krismas na sherehe za madhehebu ya Kiislamu kama Id-El-Fitri.

Katika semina hiyo iliyofanyika Agosti 9 hadi 13, mwaka huu, wakurugenzi wa habari na waandishi wa majimbo ya Dar-Es-Salaam, Zanzibar, Dodoma, Mahenge, Moshi, Same na Tanga, walijifunza mbinu za kukusanya habari kwa ajili ya magazeti na majarida, redio, TV na vichokoo ili kupeleka Habari za Wokovu kwa wengine mwanzoni mwa milenia mpya.

Pengo ahimiza kuzingatia kanisa la ndani kuliko majengo

Na leocardia Moswery

"TUNAPOBADILISHA mambo yote lazima tubadilike, Kristo ni yule yule na huo ndio ujumbe tuliopewa Kristo Jana, Leo na Daima. Ni jambo muhimu kwetu katika mwaka wa Jubilei," amesema Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Akiongoza ibada ya uzinduzi wa sherehe za ujenzi wa kanisa jipya katika parokia ya Sinza katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, hivi karibuni, Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa jimbo hilo la Kikatoliki aliwapongeza waamini kwa moyo wao wa kujitolea kufanya kazi hiyo ya Kimungu lakini, akawashauri waamini hao wasibweteke kwa ukubwa na uzuri wa jengo bali wajue kuwa, kitu cha msingi ni imani na matendo yao.

"Kitu cha msingi si kuabudu jengo bali kinachotakiwa ni mioyo yetu kwa maana kujenga Kanisa kubwa si ufahari; na wala Mungu hatambui ukubwa wa jengo, bali wewe na moyo wako na jinsi gani unavyojitolea," alisema Mwadhama.

Katika ibada hiyo ailiyohudhuriwa pia na Mkuu wa Shirika la Mungu Mwokozi(SDS), Padre James Wayker akiwakilishwa na Br. Boguslar Koza kutoka Masasi-Migongo, Mapadre, na masista wa Dekana ya Kunduchi pamoja na wahisani waalikwa,Kardinali Pengo aliwaambia waamini wa eneo hilo walichukulie kanisa hilo la nje kama ishara bora ya kuchochea kanisa bora la ndani ya mioyo.

Paroko wa parokia hiyo, Padre Africanus Lokilo(SDS), alisema kanisa hilo linatarajiwa kugharimu shilingi milioni 300,000,000/= na litajengwa kwa awamu nne.

Paroko huyo alisema kanisa linalotumika hivi sasa ni dogo mno hali ambayo huwapelekea waamini wengine kusali wakiwa wamesimama nje na wengine kwenda kusali katika maeneo mengine.

Parokia ya Sinza ilizinduliwa Desemba 21, 1997 ikiwa na waamini 5500 kitu na sasa inaongeko kubwa la waamini.

Ujenzi wa kanisa hilo umetokana na mchango wa hali na mali wa waamini ambao paroko huyo amewasifia kwa moyo wao wa dhati katika kuifanya kazi ya Mungu.

Kwa kushirikiana na Mkuu wa Shirika Br. Koza, Padre Sawio, Paroko Lukilo pamoja na wahisani, Kardinali aliweka jiwe la msingi katika eneo kanisa jipya.

Tumieni mtazamo wa kisasa kuwalea vijana-Ushauri

Na Jenifer Aloyce, DSJ

Mratibu wa Shirika la Mataifa la Kudhibiti Madawa ya kulevya ulimwenguni Dk. Fiddelis Owenya, amesema matatizo ya vijana hayana budi kuangaliwa kwa mtazamo wa kisasa na sio uliopita.

Dk. Owenya aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika semina ya vijana iliyofanyika katika ukumbi wa Don Bosco, Upanga jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema ili kuepukana na mabadiliko ya tabia kwa vijana, wazazi hawana budi kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kuwaelimisha kwa uwazi na usahihi, mabadiliko ya mwili katika kipindi cha ujana.

Alisema wazazi wengi wamejenga tabia mbaya ya kuacha jukumu la malezi ya watoto wao kwa wafanyakazi na watumishi wa nyumbani hali aliyosema inachangia watoto wao kukua bila kujua mambo mengi ya msingi juu yao yakiwamo maadili ya kijamii.

Dk. Owenya alitahadharisha kuwa tabia hiyo pia husababisha watoto kuiga tabia za wafanyakazi wao wa ndani ambazo ni mbaya kwa kuwa wengi wao hawakulelewa katika misingi ya maadili bora.

"Ukimwambia kijana wako acha tu bila kumweleza matatizo yake, ni lazima naye atajiuliza, kwanini nimeambiwa niache. Kwa hiyo, atataka ajaribu ili aone matokeo yake. Mfano, Adamu na Eva waliambiwa wasile tunda lakini, wakajiuliza kwanini? Na ndipo walipokula lile tunda na matokeo yake yakaonekana," alisema.

Vijana washauriwa

Neema Dawson na Jenifer Aloyce

VIJANA wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwajibika ili kulikomboa Taifa badala ya kujiweka nyuma kwa kuwa ndio tegemeo la taifa.

Katibu Mkuu wa Haki na Amani Bw. Joseph Ibreck,Viwawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam aliyasema hayo wakati akitoa katika kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA), juu ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Kongamano hilo la kitaifa lilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Msimbazi jijini Dar-Es-Salaam na kuwahusisha vijana kutoka katika majimbo 11 ya Kanisa Katoliki nchini

Kongamano hilo la Vijana Kitaifa lilizungumzia suala la haki na amani na kuwaeleza vijana kuwa wao ni nguzo imara ya kuleta na kudumisha haki na amani kwa kuwa utamaduni wa haki za binadamu ni wa asili.

Alisema ubabe, vita na uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu, ni kutokana na tabia mbovu za mtu mmoja mmoja au kundi la watu zikiwamo Serikali.

Aliwataka vijana kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura na akawaasa kuwachunguza, kuhudhuria mikitano ya kampeni na kuwahoji wagombea bila kuridhika tu, na majina.

Aliwaalaumu viongozi ambao wamekuwa wakiwatumia Watanzania kama ngazi na madaraja ya kujipatia mali kwa manufaa binafsi na akasema vijana hawana budi kuwaogopa na kutowakubali wagombea wenye sera zisizotekelezeka.

Alisema ni utumwa wa mwili na mawazo kupiga kura kwa kushinikizwa na watu na watu,aidha kwa ushauri, au kwa misingi ya dini naukabila na hata kwa kudanganywa kwa zawadi haramu.

Kongamano hilo lililofunguliwa na Padre Monsinyori Deogratius Mbiku, aliyewaasa vijana kuwa, katika maisha hakuna amani ya kweli na kudumu bila haki.

Alisema haki siku zote inatangulia kwanza ikifuatiwa na amani.

Padre Mbiku pia alihimiza kutafuta amani kwa mbinu sahihi na akasisitiza kuwa kukimbia matatizo ni sawa na jipu lililofichika ndani ya mwili linaloweza kuangamiza uhai na badala yake ni vema kutumia busara kukabiliana nayo.

Wakati huo huo:Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Haki na Amani, Bw. Paulo sangu, katika kongamano hilo alisema, haki ni lazima itimizwe kwa watu wote na kwamba sheria haipaswi kuwalinda wenye uwezo pekee bali, hata wanyonge wanaoonewa, wajane, yatima, wakimbizi na wenye madeni.

Sumaye asema nchi haitavumilia anayechezea amani

Na Waandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Fredrick Sumaye amesema kwa kuwa jukumu la Serikali ni kulinda uhai na usalama wa raia na mali zao, serikali haitaruhusu wala kuwavumilia watakaotaka kutumia zoezi la Uchaguzi Mkuu ujao, kukidhi matakwa yao ya kisiasa kwa njia ya vurugu.

Alisema wakati akizungumza katika sherehe za kuwekwa wakfu Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Mbulu katikati ya jumalililopita.

Alisema Tanzania imejiwekea taratibu za kuendesha mambo yake na hiyo imeiwezesha nchi kuonekana na kuheshimiwa kama kisiwa cha amanibarani Afrika

Waziri Mkuu alisema hakuna atakayeruhusiwa kuvuruga amani ya nchi kwa kutumia kisingizio na vuguvugula Uchaguzi Mkuu ujao utakaowachagua madiwani, wabunge na Rais, Oktoba 29, mwaka huu.

"Nawaasa Watanzania wawe macho na baadhi ya Watanzania wenzetu wachache ambao wanajaribu kwa vitendo vyao, kusababisha vurugu hususani Dar-Es-Salaam na " kule Tanzania Visiwani.

Aliwataka wananchi wenye sifa kamili kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wasipoteze haki yao ya kupiga kura na wawasikilize wagombea wote wa nafasi mbalimbali yaani za udiwani, ubunge na Urais kwa kuwapima kama wanatimiza vigezo vya kuweza kupewa ridhaa ya kuwa viongozi wa nchi.

Alisema kura ni siri ya mtu mmoja na hivyo, hakuna sababu yoyote ya kugombea au kuleta vurugu.

Wakati huo huo: Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’Ichi, amewataka vijana bila kujali dini, kabila wala itikadi zao za kisiasa, kuipiga vita mienendo yote potofu inayoweza kuhatarisha uhai wa jamii hasa kwao vijana katika kipindi hiki ambacho ugonjwa wa ukimwi unazidi kuwa tishio la dunia.

Aliyasema hayo siku hiyo ya kuwekwa wakfu kwa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Mbulu, wakati akisoma risala kwa mgeni rasmi Waziri Mkuu Sumaye aliyemwalikisha Rais Mkapa katika sherehe hizo Agosti 15, mwka huu.

"Ipo mienendo potofu inayohatarisha uhai hasa kwa vijana katika zama hizi za ukimwi. Ninawaomba msifanye mzaha na janga hili wala msiruhusu mtu yeyote awarubuni na kuwatumbukiza katika janga hili," alisema Mhashamu Ruwa’Ichi.

Amewataka wanajamii kuukataa utamaduni wa kifo na kuzingatia utamaduni wa uhai, na akasema vijana hawana budi kujiheshimu wao wenyewe kwa kujitawala na kuepuka maadili potofu.

Askofu Rua’ichi ameitaka jamii kujitokeza kwa wingi bila kusita katika zoezi la uandikishaji kura katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea uchaguzi Mkuu.

"Kama raia wa nchi, tuko katika harakati za Uchaguzi Mkuu. Uchaguzi wa kisiasa ni haki inayokuwezesha kushiriki katika kuliongoza taifa letu kwa kuamua ni nani atuwakilishe katika majukumu ya kupanga na kuratibu mambo".

Alisema kuwa jamii haina budi kulipa kipaumbele jambo hilo kwani si jambo la lelemama wala kudanganyana na ni jambo zito na kila Mkristo, raia mwenye umri wa kupiga kura hana budi ajiandikishe na apige kura yake bila kutishwa wala kuponzwa na yeyote.

Pamoja na kuwekwa wakfu kanisa hilo, waamini wametakiwa kukamilisha mambo ambayo yanayohitajika kama sakafu, kusafisha kuta nje na kupiga plasta au rangi na kukamilisha uwekaji wa milango na madirisha ya kudumu na vyoo, viti,u pandaji wa miti na visima.

Makatekista Mahenge waunda Umoja

Na Mwandishi Wetu, Mahenge

MAKATEKISTA wa Jimbo Katoliki la Mahenge wameunda umoja wao katika sherehe za Jubilei ya Makatekista zilifanyika jimboni hapo

Kwa mujibu wa habari tulizozipata kutoka jimboni mahenge hivi karibuni, umoja huo ambao unajulikana kama umoja wa Makatekista Mahenge(UMAMA), umeanzishwa ili kuwaunganisha Makatekista wa jimbo hilo.

Mkutano huo ulimchagua Julius Njiku kushika nafasi ya uenyekiti wakati Euphemia Mbasa, amechaguliwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa umoja huo wa makatekista.

Mwingine aliyepata uongozi katika umoja huo ni Mtunga ambaye amekabidhiwa ukatibu wakati kitengo cha uhasibu kimekabidhiwa kwa Thobias Nguguvale.

Katika mkutano uliowachagua viongozi hao, pia ulianzishwa mfuko wa umoja huo ambapo Askofu wa Jimbo hilo katoliki la mahenge, Mhashamu Agapiti Ndorobo, aliuchangia Sh. 50,000 ikiwa ni kianzio cha mfuko wa umoja huo.

Makatekista hao wameahidi kuuchangia mfuko sh 5,000 kwa mwaka kwa kila mwanachama.

Umoja huo ulianzishwa Juni 3, mwaka huu huko jimboni Mahenge.

Tofautisheni hija, utalii-Askofu

Na Sr. Costansia Mbenna,Morogoro

JAMAA imetakiwa kutofautisha hija na utalii na pia kujua kuwa imani ya mtu lazima iambatane na matendo yake kwani kintume na hivyo, ni bure.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Mhashamu Telesphor Mkude, aliyasema hayo wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Bagamoyo katika kijiji cha Kaole katika Mkoani Pwani.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakionekana na hata kusisitiza imani zao lakini matendo yao ni kinyume na imani halia aliyoisema, haisaidii kitu.

Mkuu huyo wa kanisa jimboni humo alisema kuwa ni lazima jamii ijue na kutofautisha hija na utalii.

Alisema, "Hija ni tendo linalomlenga kufanya kazi za Mwenyezi Mungu kimwili na kiroho wakati utalii ni matembezi ya kawaida tu yenye lengo la kujifurahisha kibinadamu."

Akizungumza na Wakristo wa Parokia hiyo pamoja na mahujaji waliotoka Muhonda jimboni Morogoro hadi Bagamoyo kwa miguu, wakiwamo Watanzania 56, Askofu alisema kwamba lazima sasa tuutoe Ukristo bora na tuurudishe tena Pwani, pale penye chimbuko la Ukristo na kuimarisha imani ya Kikristo.

Aliyekuwa kiongozi wa mahujaji katika matembezi hayo ya Hija ya miaka 2000 ya Ukristo, ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu Kanda ya Afrika Mashariki, Padre Gerald Mnamunga alisema,

"Maisha ya Mkristo kila siku ni hija na hasa kwa kipindi hiki tunapoadhimisha miaka 2000 iliyopita ya Jubilei Kuu ya kuzaliwa Bwana Wetu Yesu Kristu, ni lazima kuwakumbuka kwanza Wamisionari walioleta Ukristo na kuimarisha imani yetu na pia, kuamsha wito wa umisionari katika Bara na Pwani ya Afrika ya Mashariki."

Wakati huo huo: Askofu Banzi ametoa Sakramenti za Kipaimara, Ndoa, Ekaristi na kubariki ndoa 10 za Wakristo wenye Jubilei ya Ndoa.

Aliwataka vijana na Wakristo wengine wote kudumu katika imani yao ya Kikristo na kuwa askari hodari wa Jeshi la Kristo na kuimarisha Ukristo hasa sehemu za Pwani kama Bagamoyo, Tanga na Pwani yote.

Aliyaomba mashirika ya dini yawe mstari wa mbele katika kuendeleza na kukuza maadili katika elimu, afya na utume na akawahimiza raia wote wa Kitanzania wenye umri kuanzia miaka 18 kumchagua kiongozi bora atakaye iongoza vema Tanzania.

Soko Kuu hatarini kukumbwa na magonjwa

Na Josephs Sabinus, Tarime

WATUMIAJI wa Soko Kuu la Wilaya ya Tarime mkoani hapa, wako hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na soko hilo kukosa choo kwa muda mrefu hali inayosababisha vibanda ambavyo havijaanza kutumika kibiashara, kugeuzwa choo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa juma zima mjini hapa, umebaini kuwa choo kimoja cha shimo kilichokuwapo upande wa nyuma wa soko jirani na Kanisa Katoliki parokia ya Tarime, kimejaa na kuchakaa mno na kufanya vinyesi kurundikana ovyo mpaka nje hali inayotia kero ya harufu na kuhatarisha afya.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya vibanda ambavyo havijaanza kutumika jirani na maeneo yanayouza matunda, mchele na ugolo, vikiwa vimejaa vinyesi na mkojo na kumshuhudia mkazi mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja, akiwa anajisaidia haja kubwa katika moja ya vibanda hivyo majira ya saa saba mchana Agosti 8, mwaka huu.

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Soko Bw. Julius Muhere, alikiri kuwapo kwa hali hiyo na akasema tayari ofisi yake ilikwishawajulisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Afisa wa Afya wa Wilaya na kwamba sasa juhudi za kuondoa tatizo hilo zinaendelea.

"Hiyo ni kweli. Choo kimoja kilichokuwapo kimejaa. Nimepeleka barua kwa Mkurugenzi na Afisa wa Afya wa. Wilaya kwa ajili ya ufumbuzi huo. Naona wanalishughulikia sana," alisema.Hata hivyo, Mkuu huyo wa Soko Bw. Muhere, aliwataka wananchi kuwa wastaarabu kwa kuzingatia kanuni za usafi wakati huu ambao ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo, unashughulikiwa.

Endapo ufumbuzi wa haraka hautapatikana, ipo hatari ya wakazi wa wilaya ya Tarime kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na uchafu kama vile kipindupindu, kuharisha na mengine.

Juhudi za gazeti hili kumpata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa kwa kuwa lilipofika ofisini kwake siku mbili mfululizo, hakupatikana.