Wazee wa jadi wa Tarime wawatia kiwewe wapiga kura

lTLP kugomea Uchaguzi kuu?,watofautiana na UDP

lWasema CCM inawafundisha rushwa, inatumia sungusungu kuwatisha wananchi

lCCM wakiri ukabila umetawala mkoa kuliko udini

Na Josephs Sabinus, Tarime

WAKATI wananchi wa tarafa ya Ingwe Wilayani hapa wanadaiwa kugubikwa na kiwewe baada ya kilichodaiwa kuwa wamepewa ‘kiapo cha mila’ wasimchague Mbunge wa zamani wa Tarime Bw. Kisyeri Chambiri, chama cha TLP mkoani Mara kimesema huenda kikasusia Uchaguzi Mkuu ujao endapo CCM hawatakomesha rushwa, unyanyasaji na vitisho dhidi ya wapinzani na wananchi.

Wakizungumza na Kiongozi mjini hapa hivi karibuni kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa TLP Mkoa Bw. Maganya Roman Nyangi na Katibu Mwenezi wa UDP mkoa Bw. Gregory M. Nyanchini walisema kuwa vitendo vya rushwa ya waziwazi vilivyooneshwa na CCM wakati wa kura za maoni, vimeonesha kuwa Uchaguzi Mkuu ujao hautakuwa huru na haki kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Taasisi ya Kuzuia Rushwa(PCB), hawajachukua hatua.

"... Hizo kura zimekuwa kielelezo cha uchaguzi wa oktoba. TLP tunajua hiyo ni rushwa ile iliyohalalishwa kwa kanzu ya takrima. Sasa kama CCM imekuwa mfano wa rushwa, sisi wapinzani tutajifunza nini kwao? Rushwa!" alisema Nyangi na kuongeza,

"Kama rushwa itaendelea kuwa hivi huku CCM inatumia sungusungu kuwatisha wananchi eti wakichagua wapinzani kutotokea vita, tutawaachia wenyewe (CCM)".

Katibu Mwenezi wa UDP yeye alisema, "Sisi hatuwezi kususia uchaguzi".

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara Kapteni John Balongo alikanusha madai hayo, "...ukabila ndio nashangaa umekithiri mno kuliko hata udini... Sasa wanasema tunatumia sungusungu kuwanyanyasa, katika lipi wakati hivi sasa tunafanya shughuli za kichama? Hiyo si kweli".

Kura za maoni wilayani hapa zimetawaliwa na mizengwe na kusababisha wajumbe wa kata ya Tarime mjini kugoma kurudia uchaguzi mwanzoni mwa juma baada ya kufatia matokeo ya udiwani yaliyomshindisha Bw. Msafiri Sesani kufutwa ikiwa ni kata moja wapo kati ya nne zilizofutiwa matokeo yake mkoani Mara.

Kata hizo ni Ling’wani na Kisangule katika wilaya ya Serengeti na kata za mkoma na tarime Mjini katika wilaya ya Tarime.

Baada ya kushindikana mara mbili zaidi kata za Muriba na Nyamwaga, Jumatano iliyopita wajumbe wa CCM, walitakiwa kupiga kura za ubunge katika kata hizo.Hadi tunakwenda mitamboni hakuna habari zaidi zilizopatikana.

Hata hivyo, mizengwe hiyo imewafanya wakazi wa Tarime kuwa kujawa na kiwewe na kumekuwa na vikundi mbalimbali vya watu vikijadili hali ya mila na desturi na siasa na inatokana na ukabila, mila na baadhi ya vigogo wa CCM wa Wilaya na Mkoa kuengemea upande wa mgombea mmoja wa wagombea hali ambayo inaweza kusababisha CCM wakamsimamisha mgombea asiyekubalika katika jamii na hivyo kupoteza baadhi ya viti kutokana na uzembe wa ndani kwa ndani.

Kwa mujibu wa mila za Kikurya, baadhi ya matambiko kama yanayodaiwa kufanywa na wazee hao likiwamo la kuchinja mbuzi na kondoo na kufukia sehemu za mikutano ya uchaguzi na kuacha wazi sehemu nyeti za mwili, huwa ni onyo la mwisho na endapo yamekiukwa huaminika kuwa mhusika anaweza kudhurika kijamii, kiafya na hata kisaikolojia.

Watanzania watakiwa kuukataa 'umatonya'

Na Dalphina Rubyema

Katibu Mtandaji Mstaafu wa Shirika la Misaada la Caritas-Tanzania, Bw.Clement Rweramira, amesema umefika wakati kwa Watanzania kuacha kutegemea misaada kutoka nje ya nchi na badala yake, Waanzishe miradi ya kujitegemea.

Bw. Rweramira aliyasema hayo jijini katikati ya juma wakati akizungumza na mwandishi wa habari juu ya hali ya uchumi nchini.

Bw.Rwelamila ambaye ametumikia CARITAS Tanzania, lililopo chini ya Kanisa Katoliki, kwa miaka 27, alisema Tanzania bado ni nchi tegemezi sana kwa mataifa ya nje hususani ya Ulaya, Asia na Amerika na kwamba wakati sasa umefika wa kuhamasisha Watanzania juu ya kujitegemea.

"Tusiwe ombaomba, tujue hakuna mahali pa kwenda kuomba sasa, huko katika nchi za Magharibi hakuna mjomba wala shangazi" alisema.

Aliongeza kuwa bila kukimbilia nje, watu wenye uwezo ndani ya nchi hii 'wajione Caritas' kwa wenzao kuwasaidia ambao hawana uwezo na kufanya hivi kutailetea sifa kubwa Tanzania kwani sasa Kiulimwengu itaonekana ni nchi inayojitegemea.

"Changamoto iwe ni kuanzia chini, wale wenye uwezo wawasaidie wasiokuwa nacho na suala hili lifanyike bila kujali dini na kabila," alisema.

Vile vile Katibu huyo mstaafu ameitaka jamii kujitathmini yenyewe juu ya matatizo iliyonayo na baada ya hapo ikimbilie Caritas kwa ajili ya kusaidiwa kitu chochote kilichopo badala ya Caritas yenyewe kufanya tathmini.

"Unajua jamii ikijitathmini na kwenda Caritas itapata msaada hata kama ni wa ushauri tu, siyo lazima uwe msaada wa vitu,siyo Caritas yenyewe ndiyo ifanye tathmini kuona kwamba sehemu fulani kuna tatizo fulani" alisema.

Mbali na kutoa changamoto hiyo, Katibu Mtendaji huyo Mstaafu wa Caritas, ametoa shukrani za dhati kwa nchi Wafadhili wa Caritas ambazo zimekuwa zikitoa michango yake ya hali na mali.

Alitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Ujerumani, Uingereza, Australia, Ufaransa, Korea ya Kusini bila kusahau Caritas Internationalis-Roma, ambayo imekuwa ni kiunganishi kikuu cha uhusiano huu mzuri wa nchi hizi.

"Caritas za nchi hizi zinafanya kazi nzuri sana kwetu, mfano mzuri ni wakati wa mvua za El-Nino hapo mwaka 1996,Caritas Ujerumani ilisadia sana karibia 3/4 ya misaada tuliyopata kutoka nje 3/4 ya misaada hiyo ilitoka Caritas Ujeruma"alisema Bw.Rwelamila.

Vile vile ameshukuru ushirikiano mzuri uliokuwepo wakati wa uongozi wake baina ya shirika hilo na uongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo alisema Wenyeviti na Makatibu wakuu wote waliopita wamekuwa wakionyesha ushirikiano mkubwa sana.

"Kwa kweli TEC inalichukulia Shirika la Caritas kama chombo chao cha maendeleo,imekuwa ikionyesha ushirikano mzuri sana na naomba ushirikiano huo uendelee"alisema.

Aliwataja Makatibu Wakuu wa TEC ambao alifanya nao kazi kwa vipindi tofauti kuwa ni Padre Robart Rweyemamu (marehemu),Padre Augustine Ndiokoya,Padre Peter Lemba (marehemu),Wilibroad Siraha (Mbunge) na Padre Method Kilaini (Askofu).

Bw.Rwelamila ndiye Katibu Mtendaji wa kwanza wa Caritas Tanzania tangu shirika hilo lianzishwe nchini mwaka 1973 na ni mwaka huo huo aliposhika wadhifa huo hadi kufikia umri wa kustaafu Juni 16 mwaka huu ,kazi aliyoifanya kwa muda wa miaka 27 kwa awamu tisa tofauti kila awamu ikiwa ni miaka mitatu mitatu.

Hivi sasa nafasi yake inashikiriwa na Bw.Peter Maduki ambaye awali alikuwa ni Katibu Mtendaji Msaidizi wa Caritas Tanzania.

Katika uongozi wake,Bw.Rwelamila amefanya kazi yake kwa uaminifu,utii na upendo wa hali ya juu na bila shaka hii ni moja ya sababu iliyomfanya ashike wadhifa huo kwa muda mrefu bila kuenguliwa.Wakati wa uongozi wake alikuwa na ushirikiano mzuri na Mashirika mengine Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na kwa hivi sasa baada ya kustaafu kazi ya Ukatibu Mtendaji wa Caritas,pamoja na kuiangalia familia yake kwa karibu lakini vile vile amejiunga na Shirika lisilo la Kiserikali la Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) ambapo ni mwanabodi na Mdhamini wa shirika hilo.

"Nitaendelea kutoa mchango wangu katika kazi zote za maendeleo ya jamii kwa watu wote popote pale nitakapo hitajika kufanya hivyo,na nitafanya hivyo bila kujali dini,rangi,kabila ,itikadi ,cheo na umri wa mtu"alisema Bw.Rwelamira.

Karibu Textiles wavamia Msalaba wa Hija Dar

Na Leocardia Moswery

KIWANDA cha nguo cha Karibu Textile (KTM)kilichopo Mbagala jijini Dar-Es-Salaam, kimevamia eneo la Kanisa Katoliki lenye kituo cha hija cha Msalabani Misheni huko Mbagala na kuanzisha ujenzi wa stoo.

Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Parokia ya Mbagala katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam Bw. Emil Hagamu, alisema kuwa ingawa Manispaa ya Temeke imetoa hati ya kuzuia kuendelea na ujenzi (Stop Order), bado bado mmiliki wa kiwanda hicho ambaye ni raia wa Pakstani, anaendelea na ujenzi katika eneo hilo takatifu.

Hagamu ambaye ni mmoja wa wana Kamati wa Ujenzi ya Kituo hicho cha Hija, alisema kuwa, "...Cha kushangaza ni pale mwenye kiwanda huyu ambae ni Mpakistani anapoendelea kujenga na tayari ameshasimamisha jengo, huku Manispaa wanadai walishampa Stop Order."

Akilalamikia hatua hiyo ya uvamizi katika eneo hilo, hagamu alisema awali eneo hilo lilikuwa la wanakanisa wa shirika la Benedictine Fathers ambapo wananchi wapatao 10, awali walijenga katika eneo hilo kinyume cha sheria na kwamba ndipo Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kupitia barua yake yenye Kumbukumbu Na. LD/163470/50 ya Septemba 1, 1998, aliiagiza Tume ya jiji kushughulikia mgogoro huo.

Sehemu ya barua ya Tume ya Jiji la Dar-Es-Salaam, yenye Kumbukumbu Na. DCC/LD/43759/78 ya Oktoba 29, 1998, kwa Waziri huyo iliyoandikwa na R.S.Ndunguru kwa niaba ya Mkurugenzi,(Nakala tunayo) inasomeka hivi,

"...Suala la watu waliovamia eneo la Benedictine Fathers mbagala, limefanyiwa kazi kwa muda mrefu na wananchi wanaohusika na uvamizi huo walitakiwa kuondoka na wamepewa notisi.

... wananchi hao walishapewa viwanja vya kuhamia na bado vipo wazi.

...Benedictine Fathers walilipa jiji jumla ya Tsh.4,396, 856/= ili zilipwe kwa wananchi hao wahusika. Wananchi hao bado hawajachukua fedha hizo kwa visingizio mbalimbali kama vile kudai kuwa fedha hizo ni kidogo na kutaka kujengewa nyumba."

Bw. Hagamu alisema alishangazwa kuona nyumba moja iliyotiwa ‘X’ na jiji imebomolewa na tayari mwenye kiwanda anajenga.

Anasema alipofika Tume ya Manispaa ya Temeke kuwaarifu aliambatana na maafisa wake wanne na Mhandisi wa Manispaa alitoa stop oda yenye kumbukumbu na. TMC/ME/STO/127 ya Agosti 7, mwaka huu, kwa Mkurugenzi KTM, plot 106-109 katika mtaa wa Mzinga kata ya Mbagala.

Barua hiyo iliutaka uongozi wa kiwanda ufike mara moja katika ofisi za manispaa Agosti 9, mwaka huu lakini.

Hata hivyo, inaonekana Mkurugenzi huyo hakufika na aliendelea na ujenzi huo.

Gazeti hili lilipotaka kuonana na Mkurugenzi wa Kiwanda cha KTM, Bw. A. Jetta Jumatano iliyopita, liliambiwa likiwa getini kuwa haiwezekani kumuona kwa madai kuwa ana kazi nyingi.

Hata hivyo, KIONGOZI lilipoonana na Afisa Uhusiano wa KTM, Bw. Justine Mnyogoro, alikataa

kusema chochote kwa madai kuwa si msemaji na kusisitiza kuwa haitawezekana kwa mwandishi kuonana na Mkurugenzi.

"Nimekuambia Mkurugenzi hawezi kuzungumza chochote na wala hataki kusikia labda sana sana mimi sina jinsi na siwezi kukusaidia lolote," alisema Mnyongoro na kuongeza, "Labda uende Manispaa wao wanafahamu kila kitu."

KIONGOZI lilipofika katika ofisi za Manispaa, kwa Mhandisi Bw. Enock Kitalu, alikiri ofisi yake kutoa agizo la kusimamisha ujenzi huo.

"Ofisi yangu imetoa stop order na kumtaka Mkurugenzi afike hapa leo (Jumatano Agosti 9, mwaka huu) lakini, hawakufika. Sasa iweje waseme kuwa Manispaa inafahamu?"

Kaimu Mkurugenzi wa kiwanda hicho aliyetambulika kwa jina moja tu la Mabila, alimfokea mwandishi huku akikanusha kupata barua ya kuwasimamisha kuendelea na ujenzi,

"Kama mnataka twendeni kwenye kiwanja sisi hatustahili kupewa stop oda; mambo yote Tume ya inajua."

Malalamiko haya ya Kanisa Katoliki dhidi ya Kiwanda cha Karibu Textiles yamekuwa ni ya pili ambapo hivi karibuni kanisa katoliki nchini lililalamikia kiwanda hicho kwa kuchapisha vitenge vyenye nembo ya Kanisa ambavyo ni mradi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) unaolisaidia kanisa katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii zikiwamo za kiroho na kimwili.

Anayepaswa kulaumiwa ni chama si Kiongozi - DC

Na Elizabeth Steven

IMEELEZWA kuwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali zilizowekwa na kiongozi yoyote aliyekuwa madarakani kipindi cha nyuma,isiwe ni sababu ya kutompa tena kura kiongozi huyo na badala yake lawama ziwekwe kwa chama cha siasa ambacho alikuwa anawakilisha.

Kauli hiyo ilitolewa katikati ya juma na Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar-Es-Salaa ,Kapteni Ally Mpembenwe wakati akizungumza na Gazeti hili ofisi kwake.

Alisema jamii inapaswa ielewe kuwa kiongozi yeyote aliyeshindwa kutimiza ahadi alizotoa pindi alipokuwa madarakani,asitupiwe lawama na badala yake lawama hizo

ziende kwa chama alichokuwa akiwalikisha kiongozi huyo kwani ndicho kimeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa viongozi wake.

"Chama ndicho kinatakiwa kulalamikiwa na si mgombea ,jamii ielewe kwamba kutomchagua kiongozi eti tu alishindwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi ni kumuonea, anayepaswa kuzibeba lawama zote hizo ni chama chenyewe na si mtu"alisema.

Alisema kuwa ingawa baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia chama tawala kuwa hakijafanya kitu chochote lakini chama hicho kimefanya mambo mengi.

Akiyataja baadhi ya mambo ambayo chama hicho kimeweza kuendeleza ni huduma za afya , maji,barabara pamoja na Elimu .

Aidha Kapteni Mpembenwe amelisifia jimbo lake la Temeke kuwa toka uandikishaji wa kura uanze kwa ajili ya uchaguzi Mkuu ujao hali ni shwari na hajapata malalamiko yoyote kuhusu uandikishaji huo na kusema kuwa kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo watu wanavyozidi kuongezeka kujiandikisha.

"Toka zoezi la kuandikisha wapiga kura lianze kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kwakweli sikudanganyi,Jimboni kwangu hali ni shwari kabisa naomba ushwari huo uendelee hadi mwisho"alisema.

Maaskofu wazawadiwa vito vya mamilioni

Na Charles Hililla, Geita

WAUMINI wa jimbo Katoliki la Geita wamewazawadia Maaskofu watano wa Kanisa Katoliki nchini vitu mbalimbali ambavyo thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni tano.

Zawadi hizo ambazo zinajumuisha dhahabu,pesa taslimu, gari na ng’ombe vilikabidhwa Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu wakati wa kumwekea wakfu Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Geita,Mhashamu Damian Dallu.

Maaskofu waliopewa zawadi hizo ni,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Mhashamu Severine NiweMugizi,Balozi wa Vatican nchini,Askofu Mkuu Luigi Pezzuto,Askofu wa Jimbo la Shinyanga na aliye kuwa Askofu Mlezi wa Jimbo hilo la Geita,Mhashamu Aloysius Balina na Askofu Damian Dallu mwenyewe.

Katika Zawadi hizo Mhashamu Balina alipewa ng’ombe saba kama alama ya kumbukumbu na shukrani kwa kulisimamia Kichungaji Jimbo hilo kwa muda wa miaka 15 lililokaa bila kuwa na Askofu.

Maaskofu wanne waliobaki wote kwa pamoja walipewa zawadi ya dhahabu yenye thamani ya shilingi 800,000 kwa ajili ya kutengeneza pete za kiaskofu na kumbukumbu ya ujio wao jimboni humo ambapo vile vile walipewa sh.215,000 taslimu kwaajili ya matengenezo ya pete hizo kwa sonara.

Mhashamu Aloysius Balina pia alimpa Askofu Dallu zawadi ya gari la kisasa aina ya Nissan Patrol.

Mashirika yaombwa kutafuta mbinu za kuwasaidia vijana

Na Leocardia Moswery

ILI kuepusha vijana wasijiingize katika vitendo vya uharifu ambayo vinaweza kuwasababishia ugonjwa wa Ukimwi,Mashirika mbalimbali yakiwemo ya kidini ,yameombwa kutafuta mbinu za kuwapatia ajira vijana hao.

ombi hilo ulitolewa hivi karibuni Afisa Kilimo Mseto na pia Mshauri wa vijana Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga,Bw.David Temu wakati akizungumza na Gazeti hili jijini.

Katika mazungumzao hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za Kanisa la Anglikana Dinari ya Temeke,Bw.David alisema Mashirika mbalimbali na jamii nzima havina budi kuangalia kundi la vijana kwa kuwapa miradi mbalimbali ya kujiajiri wenyewe.

"Tuwavute vijana wetu na kuwapa miradi ambayo itawawezesha kujiajiri wenyewe ili na kuwafanya wawe "busy"katika shughuli zao jambo ambalo litawafanya washindwe kupata nafasi ya kujiingiza katika vitendo viovu vikiwemo vya uashereti unao sababisha ugonjwa hatari wa ukimwi"alisema Bw.David.

Afisa Kilimo Mseto huyo alisema kwa kuonyesha mfano,yeye tayari amekwisha anzisha bustani ya Mboga za majani na matunda na pia tayari zipo hekari tatu za viazi vitamu ambayo vimepandwa katika eneo la Matumbalo Gairo katika wilaya ya Kilosa na vinatarajiwa kuvunwa mwezi huu wa Agosti".

Alisema bustani hizi ni kwa ajili ya kuwainua wanakwaya wa kwaya ya Tunguli ambao anafanya nao kazi kwa karibu.

Bwana Temu aliendelea kusema kuwa kwaya ya Tunguli ni vijana wanaojituma na hawachagui aina ama mazingira ya kazi."Wakati mwingine wanakwaya hawa hufanya vibarua vya kulima mashamba ya watu huku wakivuna mazao mbalimbali kutafuta pesa na hapo hapo wanakuwa mstari wa mbele kulitangaza neno la Mungu kwaya nyingine ambazo hazipo tayari kujituma"alisema.

Dawa ya Ukimwi ni kutokomeza umasiki-Mbeki

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki amesema kuwa jitihada za kutokomeza Ukimwi haziwezi kufanikiwa kama hazitakwenda sambamba na kutokomeza umaskini ambao ni chimbuko ugonjwa huo.

Rais Mbeki aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 13 wa Kimataifa kuhusu Ukimwi uliofanyika Darban Afrika ya Kusini, mkutano ulihudhuriwa na watua zaidi ya 14,000 toka Mabara yote ya Ulimwenguni.

Kwa mujibu wa mmoja wa washiriki wa Mkutano huo kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Dk. Arban Hokororo aliliambia Kiongozi kuwa Rais Mbeki alisema kuwa tatizo la umasikini likipatiwa ufumbuzi hapo hapo hata ukimwi utapungua.

Dk. Hokororo ambaye ni Katibu wa Idara ya Afya katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) alisema kuwa katika mkutano huo,Mashirika ya kidini yalisisitiza vijana kubadili tabia ya uasherati kwani vijana wakipata ugonjwa huo nchi zao zitaathirika.

"Katika Mkutano huo Mashirika ya Kidini yalisisitiza vijana wabadili tabia ya uasherati kwani kasi ya maambukizo ya Ukimwi kwa vijana yataathiri nchi zetu" alisema Dk. Hokororo na kuongeza kuwa ‘pia suala la kusaidia vikundi vya vijana liwe katika mazingira mazuri yaani kuwapatia elimu hasa kwa wasichana".

Vile vile alisema kuwa katika mkutano huo ilijadiliwa kuwa vita dhidi ya utumiaji wa madawa ya kulevya, sigara na pombe viendelezwe na huduma kwa waathirika wa Ukimwi zianzie katika jumuiya.

Pia jambo la kuhudumia yatima lilisitizwa kuwa wapewe misaada itakayo wawezesha kujitegemea.

Mkutano huo ulifungwa na Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela.

Watakiwa kusali kwa bidii ili wawe watawa

lParokia ya Kigurunyembe yapata padre wa Pili mzalendo

Na Seraph Kuandika, Morogoro

VIJANA Wakatoliki, nchini wametakiwa kusali kwa bidiii ili waweze kuitikia miito ya kuwa Watawa kwa ajili ya kumtumikia Mwenyezi Mungu.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Balozi wa Vatican nchini, Mhashamu Askofu Mkuu Luigi Pezzuto, alipokuwa akizungumza na waamini Katoliki wa parokia ya Chalinze mkoa wa Pwani wakati wa ziara yake ya kulitembelea jimbo Katoliki la Morogoro.

Alisema kuna haja vijana wakawa mstari wa mbele kujitolea kumtumikia Mungu na kulieneza neno lake na akawataka wazazi kutoa msukumo kwa watoto wao wajenge tabia ya kusali mara kwa mara.

Akisisitiza zaidi juu ya hilo,Askofu Mkuu Luigi Pezzuto alitoa mfano kuwa yeye binafsi, Maaskofu, Mapadre na Masista wanaomtumikia Mungu na jamii kwa ujumla hivi sasa walikuwa pia watoto wadogo lakini wito wao wa kuwa watawa umetokana na kuisikia sauti ya Mungu na kuitikia mwito wake.

"Ningefurahi sana baadae nikikutana na Askofu wenu aniambie kuwa sasa katika parokia kuna Masista na mapadre wengi", alisema askofu Mkuu Pezzuto.

Aidha akizungumzia juu ya kuanzishwa kwa kituo cha Radio Ukweli kinachomilikiwa na jimbo Katoliki Morogoro ambacho alikikabariki yeye mwenyewe,alisema, chombo hicho cha habari na mawasiliano kitakuwa nguzo kuu ya kuwaunganisha waamini wote wa jimbo la Morogoro na wajione wako karibu.

Alisema kudumu na maendeleo ya kituo hicho kilichoanza matangazo yake rasmi Agosti 5 mwaka huu baada ya kupatiwa kibali na Tume ya Utangazaji, yatatokana na mchango wa hali na mali kutoka kwa wananchi wenyewe wa jimbo la Morogoro na maeneo mengine.

Naye Sr. Dafroza Msemwa anaripoti kuwa Parokia Katoliki ya Kigurunyembe jimboni humo ,katika mwaka huu wa jubilei kuu imejipatia Padre wa pili Mzalendo tangu ilipoanzishwa miaka 100 iliyopita.

Parokia ya Kigurunyembe ni parokia ya pili kuanzishwa tangu Ukristu ulipoingia hapa nchini, eneo la Bagamoyo. Parokia ya kwanza ni parokia ya Muhonda iliyoko Turiani Morogoro vijijini.

Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza laanzisha kituo cha kulea watoto wa mitaani

lParokia yajenga shule kuwasaidia vijana walioshindwa kujiendeleza

Na Getrude Madembwe, Mwanza

JIMBO Kuu Katoliki la Mwanza limeanzisha kituo cha kulelea watoto wa mitaani kinachojulikana kama "Upendo daima" ambacho kipo chini ya Idara ya kichungaji jimboni humo.

Kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto ambao hawana makazi maalum na watapatiwa huduma ya elimu katika shule za awali na Msingi.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Paroko wa Parokia ya Bugando jimboni humo ,Padre Bonifasi Mabula alisema kituo hicho kinawalea watoto wote wenye jinsia tofauti na wa madhehebu mbalimbali.

"Tunao watoto wa jinsia tofauti ambao tunawapeleka katika shule za msingi na awali na hii inategemea na umri wa mtoto"alisema Padre Mabula.

Aliongeza " Utakuta mtoto mwingine ana umri mkubwa lakini hajui kusoma na kuandika,hivyo tunawapeleka shuleni na wala hatuwabagui kwakusema eti huyu ni Mlutheri au Muanglikana wote tunawajali".

Alisema watoto hao wanaporudi kutoka shuleni wakati wa jioni hufundishwa masomo ya Kiingereza na Hisabati na watu ambao hujitolea kuwafundisha bure.

Paroko huyo aliendelea kusema kuwa mbali na kuwapeleka shule watoto hao, pia huwapa ushauri wa karudi nyumbani pindi wanapomaliza masomo yao ushauri ambao alisema umesaidia kwa kiasi kikubwa kwa watoto hao kukubali kurudi nyumbani.

Alisema watoto hao hutokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Mara na Mwanza yenyewe kwani kudanganywa na watu kuwa Mwanza mjini kuna ajira na kumbe sivyo.

"Watu huwadanganya kuwa Mwanza mjini kuna kazi hivyo wao huja lakini wakifika huku huwa ni tofauti kwani utakuta wengine hawajui kusoma wala kuandika hivyo huishia kuwa watoto wa mitaani" alisema Padri Mabula.

Naye Jenifer Aloyce, DSJ anaripoti kuwa; WAAMINI wa Parokia ya Makuburi iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam wamejenga Shule kwa ajili ya kuwasaidia vijana walioshindwa kujiendeleza kutokana na matatizo mbalimbali yakiwemo ya ufukara.

Akizungumza na Gazeti hili ofisini kwake mwanzoni mwa juma,Paroko wa Parokia hiyo Padre Gerardo Derksen alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo inayojulikana kama "Elimu ya Maisha"umefanywa kutokana na michango ya waamini wa Parokia hiyo. "Tumeamua kujenga shule hii inayo chukuwa vijana kuanzia umri wa miaka 14-25 ,walioshindwa kusoma kutokana na matatizo mbalimbali kama vifo vya wazazi, ufukara"alisema Padre Gerardo.

Alisema shule hiyo tayari imekwisha funguliwa na ina Wanafunzi wapatao 40 ikiwa ni mchanganyiko wa wasichana na wavulana kutoka madhehebu yote ya kidini.

Katika shule hiyo vijana watajifunza mambo mbalimbali kama vile kusoma na kuandika, kuhesabu, mafundisho ya bustani, kilimo, elimu ya ndani yaani kulea watoto pamoja na jinsi ya kutunza mifugo.

Paroko huyo alisema kuwa ili kuwapa muda vijana hao wa kuendelea kufanya kazi kwa waajiri wao,watakuwa wanaingia darasani mara tatu kwa wiki ambapo katika siku hizi watatukuwa na jumla ya vipindi tisa.

"Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa muda wa kufanya kazi,wasije wakafukuzwa na mabosi wao maana wengine ni "Mahouse girl na Mahouseboy" hivyo siku tatu kwa wiki siyo mbaya"alisema Padre Gerardo.

Hata hivyo Paroko huyo hakuweza kutaja pesa kamili iliyotumika kujenga shule hiyo ambapo alisema ni pesa nyingi sana zimetumika.

KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE NA UDIWANI

TLP Temeke kutangaza wagombea Agosti 14

Na. Peter Dominic

WAGOMBEA wa kiti cha ubunge na udiwani kwa tiketi Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Jimbo la Temeke wanatarajiwa kutangazwa Agosti 14 mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa TLP jimboni humo Bw. Kwaller Amri wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye ofisi zake zilizopo mtaa wa Kitomondo jimboni humo.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki, Bw.Amri alisema kuwa kutangazwa kwa majina hayo kutakuja baada ya kikao maalum cha viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho kumalizika.

Alisema kikako hicho kitakachofanyika Agosti 14, mwaka huu, ndicho kitakachopendekeza mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama chao.

Wakati TLP kikijiandaa kuwatangaza wake tayari chama tawala CCM kimempitisha Bw. Manji katika kura za maoni kugombea ubunge jimboni humo na wakati huo huo, kuna tetesi kwamba CUF kitamsimamisha aliyekuwa mgombea Ubunge kwa tikiti ya NCCR mwaka 1995 Bw. Tambwe Hiza ambaye atagombea Ubunge jimboni humo.

Hata hivyo Bw. Amri aliwahakikishia wanachama wake kwamba TLP ni chama kinachokubalika kwa kiwango kikubwa jimboni humo akasema hata hivyo hawana wasiwasi na huyo aliyeshinda kura za maoni kwa tiketi ya CCM na kuongeza kuwa wana uhakika wa kushinda.

Katibu huyo aliendelea kusema kuwa chama chake kinajivunia sera nzuri ambazo wananchi wanaziunga mkono na kina mtandao wa kutosha jimboni humo kwa vile tayari kina kata 11 na kila tawi moja kina wanachama 500.

Alisema chama chake kinatarajia kupata upinzani mdogo wa vyama viwili vya CUF na CCM na akasema vyama vingine hawana wasiwasi navyo kwa vile ni vichanga.

Awali katika uchaguzi wa rais na wabunge wa mwaka 1995 chama kilichokuwa na nguvu na kuleta upinzani mkubwa kwa chama tawala kilikuwa NCCR na kilifanikiwa kuchukua kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati huo Bw. Augostine Lyatonga Mrema alishinda.

Baadhi ya wakazi wa jimbo hilo waliokuwa wanachama wa chama hicho cha NCCR ambao Gazeti hili lilitaka kupata maoni yao juu ya Chama hicho kilichowahi kuwa na nguvu kuliko vyama vingine vya upinzani jimboni humo, wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao walisema chama hicho(NCCR) kina wakati mgumu kwa vile wanachama wengi hususan jimboni humo tayari wamejiunga na chama cha TLP na wengine kubaki hawana msimamo ‘Uhai wa chama hicho unafutika’ alisema mmoja wao.

Wafanyabiashara 80 Mara Kortini kwa kushindwa kulipa 2000/=

Na Josephs Sabinus, Tarime

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime katika mkoa wa Mara, imewafikisha katika Mahakama ya Mwanzo ya Tarime, wafanyabiashara 80 kwa kushindwa kulipa ushuru wa vibanda vya halmashauri hiyo kwa miaka miwili mfululizo.

Ilielezwa na upande wa mashitaka ukiongozwa na Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Bw. Nashon Rutasha, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Tarime, Zacharia Makubi Julai 31, mwaka huu kuwa, wafanya biashara hao wameshindwa kulipa ushuru wa vibanda vya Halmashauri hiyo wa shilingi 2000/= kwa mwezi kila mmoja kwa miaka miwili mfululizo na hivyo kuikosesha halmashauri hiyo kipato chake kutokana na vibanda hivyo.

Washitakiwa katika kesi hiyo ambao wengine wamekwisha somewa shitaka lao na wengine bado, wakiwa wanaendelea kusomewa shitaka lao kwa nyakati tofauti, wamegawanywa kwa mahakimu wengine wawili wa mahakama hiyo na wale ambao shauri lao linasikilizwa na Hakimu huyo Mfawidhi Zacharia Makubi, kesi yao itaendelea Jumatatu hii ya Agosti 14, 2000.

Kuchakaa kwa Majengo ni matokeo ya Serikali kukalia siasa

Na Neema Dawson

IMEELEZWA kuwa kuchakaa na kuharibika kwa majengo mengi hapa nchini kunatokana na Serikali kuelekeza nguvu zake nyingi katika masuala ya kisiasa na kusahau kabisa shughuli za kukarabati majengo.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajiri wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiliaji Majenzi, Bw. Beda Amuri wakati akizungumza na Waandishi wa habari jijiji Dar-Es-Salaam.

Bw.Amuri alisema kuwa ingawa majengo mengi yalibuniwa vizuri lakini kutokana na serikali kutoyafuatilia, mengi yameharibika na kupoteza muonekano wake kama yalivyokuwa awali baada ya kujengwa.

"Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mabaya na kutokana na serikali kutumia muda wake mwingi katika mambo ya siasa bila kutilia mkazo majengo yaliyopo kwa kuyafanyia ukarabati," Alisema Bw. Beda.

Aliongeza kuwa akiwa mmoja wa wabunifu soko la Kariakoo mwaka 1975 hadi 1980 soko hilo lilipokuwa chini ya uangalizi wao pindi walipoikabidhi serikali hali ya soko hilo imeanza kubadilika na inakatisha tamaa.

Kutokana na hali hiyo soko hilo limekuwa na hali mbaya na imefikia hatua baadhi ya wafanyabiashara wachache kujiamria kujenga vibanda katika sehemu za madirisha ya soko hilo hivyo kuziba hewa safi kuingia ndani na ile chafu kutoka nje hali inayosababisha hewa kuwa nzito sokoni hapo.

Mwenyekiti huyo wa alitoa tahadhali kwa waajiri kuacha kuwapa kazi ya ubunifu wa majengo watu ambao hawakusajiliwa na bodi hiyo ya usajili na hairuhusiwi kumuajiri mtu bila kuwa na kibali maalum kutoka katika bodi hiyo.

Alisema ingawa kumekuwa na malalamiko kuwa Bodi hiyo inawapa zabuni nyingi watu wa nje kuliko wa hapa nchini, hali hiyo ni matokeo ya utendaji wa watu wa nchi za nje kuwa mwepesi na mzuri kutokana na vitendea kazi vingi na bora walivyonavyo.

Aliongeza kuwa hadi sasa katika usajili wa Ubunifu wa Majengo, Watanzania waliosajioliwa ni 121 ambapo 31 ni wageni na katika wakadiriaji Majenzi Watanzania ni 36 wamesajiliwa na bodi hiyo na wageni ni 13.

Alisema Makampuni ya Ubunifu wa Majengo yaliyosajiliwa ni 51 ya Watanzania na 6 ni yale ya kigeni na yale ya wakadiriaji majenzi makampuni 15 ya Watanzania yalisajiliwa na kampuni moja la kigeni.