Masista Morogoro wavamiwa na majambazi

lSista mwingine acheza 'uninja' na kuruka fensi kumuokoa mwenzao

lMjane mwenye mapacha wawili aokoa jahazi

lMmoja ajeruhiwa kwa kuwazidi ujanja majambazi

Na Josephs Sabinus

WATAWA wawili wa kike na mjane mmoja aliyekuwa na watoto wake wawili wachanga ambao ni mapacha, wamewazidi "kete" watu watatu wenye silaha kali wanaodhaniwa kuwa majambazi, walipovamia nyumba yao na kumteka Sista Mkuu wa nyumba hiyo wakimtaka awape fedha.

Akisimulia mkasa huu kwa simu kutoka mjini Morogoro Ijumaa iliyopita, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita.

Alisema majambazi watatu wakiwa na bunduki pamoja na dereva wa teksi, walivamia nyumba ya masista wa COLLEGINA, wa Familia Takatifu jimboni humo majira ya saa nne asubuhi na kumlazimisha Sista Mkuu wa Nyumba hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Theresia aingie ndani na kuwapatia fedha zote.

Askofu Mkude aliendelea kusimulia kuwa, walipoingia ndani huku wamemteka na kumtanguliza, Sista huyo alianza kuwazungusha katika vyumba kadhaa bila wao kujua kuwa alikuwa na lengo la kuwajulisha wenzake waliokuwapo kiujanja.

Alisema baada ya majambazi hao kugundua kuwa wamewafikishwa katika mlango ule unaowatoa sebuleni na kwamba sasa masista wengine waliokuwa nje na mama mmoja mjane mwenye watoto mapacha aliyekwenda kuomba msaada katika nyumba hiyo, kwa ajili ya wanawe, walizidi kughadhabika na kuanza kumshambulia huku wakiwa wamemuangusha chini baada ya kuwajibu kuwa hakuna pesa.

Aliusifia ujasiri wa mama huyo mwenye mapacha na mtawa mmoja wa kike, Askofu Mkude alisema, mtawa huyo ambaye hakumtaja jina aliyeruka uzio (fensi) wa nyumba hiyo na huku kwa kushirikiana na mjane huyo kupiga yowe licha ya majambazi hao kutishia kwa kupiga bunduki hewani.

"Kwa kweli hao masista wote Theresia, na huyo mwingine ni majasiri maana hata yule mama licha ya kuona wamepiga bunduki kutishia, bado pamoja na huyo mtawa waliendelea kupiga yowe ambazo ndizo zilileta msaada. Yule mtawa aliruka waya wa uzio huku wakipiga yowe na yule mama mwenye watoto.

Na hiyo ndiyo iliwafanya majambazi hao kukimbia baada ya kuona kelele za wananchi zinazidi kuwakaribia," alisema Mhashamu Mkude.

Hata hivyo katika tukio hilo, majambazi hao hawakufanikiwa kupora chochote na pia ingawa Sista huyo alipata maumivu kadhaa, anayoendelea kutibiwa katika Hospitali ya Mkoa huo, hakupata jeraha wala kuvunjika popote.

"Jana jioni,(Alhamisi) nilipomtembelea niliambiwa kuwa X-ray imeonesha kuwa hakuvunjika popote lakini, ana maumivu makali tumboni," alisema Askofu.

Jambazi mmoja na dereva walitiwa nguvuni na wanashikiliwa na polisi mjini hapo.

Habari zaidi za kuaminika zinasema kwa takribani siku nne za nyuma kabla ya tukio hili, makundi kadhaa ya watu yalikuwa yakionekana kuzengea zengea eneo la nyumba hiyo hali iliyowafanya masista hao kuwatilia mashaka na hivyo, kutoa taarifa katika kituo cha polisi.

Hata hivyo, habari za kuaminika toka katika vyanzo vyetu vingine vya habari zinasema, hadi wakati wa tukio, hakuna hatua zozote za makusudi zilizokuwa zimechukuliwa na polisi juu ya hofu ya masista hao.

Alipoulizwa na gazeti hili juu ya suala hili la polisi kutochukua hatua, Askofu Mkude alisema,

"Siamini kweli kama polisi hawakulifanyia kazi suala hili. Unajua ingawa walikuwa hawajawakamata, inawezekana sana kuwa walikuwa wanaandaa mitego yao. Wasingeweza kuweka doria ya waziwazi, polisi huwa hawapuuzii taarifa kama hizi."

Hata hivyo alizidi kuwahimiza wananchi kutoa haraka taarifa juu ya dalili zozote zinazoonekana kuelekea kuhatarisha usalama na amani na pia, akawataka polisi kutoa ushauri wa wazi kwa watu wanaopata hofu na kutoa taarifa kuwa wafanye nini pindi hali inapokuwa mbaya kama walivyoitabiri.

NCCR yasema haijali sura ya mbunge bali sera

Na Neema Dawson

WAKATI gazeti hili likitaka kujua sababu ya wanachama kadhaa wakiwamo wabunge Chama cha NCCR-MAGEUZI kukihama na kujiunga na vingine kikiwamo TLP, chama hicho kimesema hakijali wingi wala sura ya mtu wakiwamo wabunge bali, sera za chama chenyewe.

Katika mahojiano hayo na KIONGOZI, yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kweke, Afisa Uchaguzi wa NCCR_MAGEUZI, Bw.Joseph Mang’ana alisema chama chake hakitishiki na wabunge wanaokihama na kukimbilia vyama vingine kuwa anajua hawafanyi hivyo kwa nia njema, bali wanatafuta wanapoweza kujipatia maslahi binafsi.

"Wabunge wanaochaguliwa katika majimbo mbalimbali wanadhani wananchi wanawaangalia kwa sura bila kujua kuwa hao hao wananchi wanaowachagua,wanatakiwa wapendezwe na sera pamoja na itikadi za vyama vyao," alisema.

Aliwatahadharisha wabunge hao kabla ya kuihama NCCR hawana budi kuangalia sera za chama wanakohamia na wasifikirie kuwa kwenda huko wataweza kupata ubunge kama ilivyotokea katika uchaguzi wa mwaka 1995 kwani sera za huko ni tofauti.

"Mfano mzuri ni tukio hivi karibuni la aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Siha Mkoani Kilimanjaro, Makidara Mosi (NCCR Mageuzi) sasa, amehama na kujiunga na TLP kwa akimfuata Lyatonga kwa kudhani atapata tena Ubunge kwa chama hicho bila kujua kuwa sera za NCCR ni nzuri na TLP hawana sera yeyote.

Kama atagombea tena Ubunge kwenye jimbo la Siha kwa tiketi ya TLP, ajue hawezi kuupata tena kwa kuwa wananchi wa Siha wanaelewa fika sera za NCCR na ndio maana walimchagua kipindi cha nyuma," alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa kitendo alichokifanya mbunge wa jimbo hilo la Siha, kinaweza kikakipa nafasi Chama cha Mapinduzi (CCM)kupata kiti hicho kwa urahisi kwani ni jambo la wazi kwamba NCCR na TLP watagawana kura.

"Kitendo cha Makidara kuihama NCCR Mageuzi ni kukitengenezea mapito Chama cha Mapinduzi. Ameamua kuifanyia CCM biashara ili ichukue kiti cha ubunge katika jimbo hilo. Tutagawana wapiga kura wa NCCR na TLP na hapo upo uwezekano mkubwa wa CCM kupata ushindi dhidi ya vyama vya upinzani ambavyo vinakosa msimamo na kuhamahama "alisema.

Hivi karibuni wabunge kadhaa wa NCCR-Mageuzi walivihama vyama vyao na kukimbilia TLP.

Wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Siha, Bw.Makidara Mosi, Mbunge wa Moshi Vijijini, Bw.Gerald Ngotolainyo na Mbunge wa Mwibara mkoani Mara, Bw. Mutamwega Mughaywa.

Watembea kilomita 221 wakila kipande cha mkate na maji

lWachangia milioni 20/=

Na Padre Regnard Bhare, Bagamoyo

ZAIDI ya shilingi milioni 20, zimechangwa na wahisani wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya ukarabati wa makumbusho yanayoelezea mwanzo ukristo yaliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Akitoa tathmini ya mpango mkubwa wa ukarabati wa mision hiyo ya kwanza Afrika Mashariki, Paroko wa Parokia ya Bagamoyo, Padre Valentine Bayo, alisema michango hiyo imetokana na wafadhili wa ndani na nje ya nchi wakiwamo wafadhili wa kutoka Ujerumani na wananchi mbalimbali walioshiriki Matembezi ya Hija ya Miaka 2000 ya Ukristo yaliyoandaliwa na Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu yanayomalizika Jumamosi hii.

Hija na mchango huo ni kwa ajili ya makumbusho ya mwanzo wa Ukristo Tanzania katika parokia ya Bagamoyo iliyopo Jimbo Katoliki la Morogoro.

Habari zilizopatikana toka kwa waandalizi wa matembezi hayo katikati ya juma zinasema, washiriki wa matembezi hayo wamelazimika kutembea kilomita 36 kwa siku wakiimba na kusali huku wakila vipande vya mikate kwa maji ya matunda na kulala katika mazingira magumu.

Habari zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kuwa zaidi ya washiriki 130 wameshiriki kutembea mwendo wa kilomita 221, kutoka Mhonda Morogoro hadi Bagamoyo ambapo kila mshiriki amechanga kiasi kisichopungua shilingi 50,00/=.

Paroko huyo alisema katika taarifa yake kuwa fedha hizo zitatumika kwa kukarabati jengo la Makumbusho, makaburi ya Wamisionari wa Kwanza wa Shirika hilo la Roho Mtakatifu, Pango la Bikira Maria wa Lourde na ujenzi wa nyumba ya shule ya sekondari ya marian ya parokia ya bagamoyo.

Habari zimesema matembezi hayo ya Hija ya Miaka 2000 (Spiritan 2000 Millenium Walk) yakliyoongozwa na Mkuuwa Shirika hilo Kanda ya Afrika Mashariki, Padre Gerard Mnamunga

Matembezi hayo yalipitia barabara iliyopitwa na wamisionari wa kwanza, yamepita pia katika barabara ya iliyokuwa maarufu kwa biashara ya watumwa.

Yana lengo la kuwaenzi wamisionari hao wa kwanza nchini walioanzisha Ukristo mwaka 1868 ambapo pamoja na mambo mengine waliyoyafanya pia waliishawishi serikali ya kikoloni ya wakati ule kupiga marufuku biashara ya watumwa.

Kumbukumbu za mwanzo za Wakristo, zinakariri kusimamia kwa maelfu ya watumwa waliowekwa huru na kuanzishwa vijiji huru na wamisionari wa shirika hilo na kufunzwa namna ya kujitegemeza katika shule maaluum za ufundi stadi walizoanzisha.

Kumbukumbu hizo pia zinaeleza kuwa miongoni mwa shughuli muhimu zilizofanywa na watumwa hao huru kwa utaalamu waliofundishwa na mapadre hao zilikuwa kujenga makanisa kadhaa makubwa likiwamo la Mtakatifu Yosefu la jijini Dar-Es-Salaam, Mandela la mkoani Pwani, Mhonda la Morogoro na Kanisa la Bagamoyo.

Matembezi hayo yanafikia kilele chake Jumamosi hii katika hatua ya mwisho na yatapokelewa na Mhashamu Telesphor Mkude, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro katika viwanja vya kanisa la Bagamoyo kwa maadhimisho maalumu.

Ukristo, Uislamu ni binamu - Mhubiri

lSheikh atumia Quran kueleza sababu ya wanaume kurithi kuliko wanawake

Dalphina Rubyema na Jenifer Aloyce, DSJ

UNDUGU uliopo baina ya Ukristo na Uislamu umefananishwa na mtu na binamu yake na hivyo kusisitizwa kutogombana baina ya wafuasi wa dini hizi mbili.

Mhubiri mmoja kutoka Norway, Dk.Bjornar Hemista alizifafanisha dini hizo katikati ya juma wakati wa mkutano maalum wa kudumisha amani baina ya Uislamu na Ukristo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya New Africa jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia juu ya masomo ya Quran na katika hilo amegundua kuwa Ukristo na Uislamu ni vitu vilivyo karibu sana hivyo haoni ni kwa nini wafuasi wake wakose uelewano na kugombana kufuatia tofauti zao.

"Nimesoma Quran, nimeona kwamba Waislamu ni binamu zetu sisi Wakristo hivyo, hakuna sababu ya kugongana katika imani, tudumishe amani na upendo kwani sote ni kitu kimoja mbele za Mungu.

Wakati huo huo: Katika mkutano huo wa siku moja uliowahusisha viongozi wa madhehebu mbali mbali ya dini, Msemaji wa Sheikh Mkuu nchini, Sheikh Suleman Gorogosi, alisema jamii haina budi kuachana na dhana kuwa Waislamu wanawanyanyasa wanawake wa dini hiyo.

Sheikh Gorogosi alisema wanaodhani hivyo wanakosea kwa kuwa hawajui vema.

Akizungumza katika mkutano huo, Sheikh Gorogosi alisema katika Quran Tukufu, imeandikwa kuwa endapo baba wa familia atafariki, na kuacha watoto wawili; wa kike na wa kiume, lazima mtoto wa kiume apate mafungu mawili ya mali iliyoachwa wakati mtoto wa kike anatakiwa apate fungu moja tu.

Aliongeza kuwa mama wa watoto atapaswa apate sehemu moja ya nane ya mali hiyo.

Sheikh Gorogosi aliendelea kufafanua kuwa endapo baba atakufa bila kuacha watoto, basi mke huyo atapata sehemu moja ya nne, ya mali iliyoachwa na kama marehemu ameacha wake wawili basi kila mwanamke anatakiwa apate sehemu moja ya sita ya mali.

"Sisi siyo kwamba tunakaa tu, na kuamua juu ya mahari, yamendikwa katika Quran Tukufu ya Mtume M.S.W. watu wasijisemee wenyewe, waje tuwaeleze; kinachotakiwa ni kuelimishana katika dini zetu," alisema Sheikh Gorogosi.

Aliwataka watu kufuta imani kuwa kitendo cha wafuasi wa dini kutooana na Wakristo siyo kwamba ni unyanyasaji bali ni moja ya mashariti ya dini hiyo.

Alisema waamini wadini hizi mbili huenda wakajiona wako tofauti ama kuonekana wananyanyasana kutokana na dini moja kutoelwawa taratibu za dini nyingine likiwemo suala hili la ndoa.

Alisema ndoa na talaka katika Uislamu ni moja ya ibada hivyo, ni lazima wahusika wote wawe ni wa dhehebu moja.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini,(UMPT),Askofu Silvester Gamanywa, aliuambia mkutano huo kuwa kwa vile Taifa hili ni la Wakristo na Waislamu, ni lazima yawepo mahusiano mazuri bila kuweka tafsiri ya kisiasa.

"Ni lazima yawepo mahusiano mazuri baina yetu bila kuongeza ama kupunguza msimamo wa imani zetu, ukaribu huu uweze kutuelimisha kila upande kuelewa upande mwingine," alisema.

Kauli hiyo ya Askofu Gamanywa pia iliungwa mkono na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli, Dayosisi ya mashariki na Pwani, Elinaza Sendoro na Sheikh wa Msikiti wa Munyamani jijini, Sheikh Mohamed idd Mohamed na Sheikh Issa Othman.

Mwanasheria ashauri kuepuka ndoa za chapu chapu

Na Neema Dawason

MWANASHERIA kutoka katika Kituo cha msaada wa Sheria kwa wanawake Bi. Monika Muhoja amewashauri viongozi wa dini kuziepuka ndoa zinazofungwa chapuchapu kuwa zinakuwa na matatizo na migogoro hapo baadaye.

Mwanasheria huyo aliyasema hayo katika semina ya viongozi wa umoja wa wanawake wa Kianglikana (UMAKI) wa Dayosisi ya Dar es Salaam uliofanyika katika kanisa la Kiangliakana la Mtakatifu Albino juu ya umuhimu wa mwanamke katika maisha ya kila siku ambayo ilifunguliwa na Askofu Basil Sambano.

Alisema kuwa kumekuwa na migogoro mingi katika ndoa za kikristo ambazo imeonekana kuwa ndoa hizo zinafungwa kwa kujirudiarudia hali ambayo viongozi wa dini wanatakiwa kuwa makini wakati wa uandikishaji wa ndoa na ufungishaji.

"Nikiwa katika kituo cha sheria kwa wanawake nimepata malalamiko mengi ya wakristo kuhusiana na ndoa nyingi zinazofungwa kutoka mikoa kadhaa na wanapofika hapa jijini hufunga ndoa kwa baadaye" hata hivyo Askofu Basil Sambano alisema kuwa wanawake wanatakiwa kuwalea watoto wao katika malezi bora kwani watoto wengi wanangamia kwa malezi bora kwani watoto wengi wanaangamia kwa ukimwi na madawa ya kulevya kwani kama kanisa limekuwa kikikazia watu washike amri ya kutokuzini ili waepukane na ugonjwa wa ukimwi, kwani jamii ya sasa inaogopa ugonjwa wa Ukimwi kuliko dhambi.

Viongozi wa dini, serikali watakiwa kukemea rushwa

Na Elizabeth Steven

VIONGOZI wa dini , serikali na jamii kwa jumla wameelezwa kama watu wanaotakiwa kuwa mstari wa mbele ili kukemea na kukomesha kabisa vitendo vya rushwa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma Wakatoliki nchini (CPT), Jimbo kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Bw. Fabian Mganwa aliyasema hayo wakati akifungua semina ya siku moja ya vijana wa parokia ya Makuburi juu ya umuhimu wa kufanya kazi katika maisha ya binadamu.

Alisema kwa kuwa rushwa si kwamba ipo katika Tanzania pekee, bali ipo dunia nzima, basi jamii nzima wakiwamo vijana, viongozi wadini, siasa na jamii kwa ujumla hawana budi kuungana kuipiga vita kwa kuwa ni uovu zaidi hata ya uvivu na ulevi.

Bw. Mganwa alisema licha ya ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais kuchunguza mianya na kupendekeza namna ya kudhibiti rushwa nchini iliyoongozwa na Jaji Yoseph Warioba, badoimekithiri sana nchini Tanzania imekuwepo duniani wakati wote wa maisha ya binadamu.

Alisema kuwa kama ilivyo katika maeneo mengi duniani, inashangaza kuona kuwa licha ya suala la kuipiga vita kuwa wimbo uliozoeleka midomoni, bado hali hiyo ya ukiukwaji wa maadili unaopoteza haki unaendelea katika jamii na kufanywa na baadhi ya watu ambao wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa.

Akitoa mfano wa athari mbaya za rushwa katika jamii ya Watanzania, alisema kutokana na kukithiri kwa rushwa haki mbalimbali hazitendeki katika utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kama ugawaji viwanja, utoaji wa leseni za biashara na udereva, uchaguzi wa watoto wa kuingia darasa la kwanza na kidato cha kwanza, upatikanaji wa tiba na ajira.

Wakati huo huo: Makamu Mwenyekiti huyo amewataka vijana wote nchini kuepuka maisha ya anasa na starehe kwa kuishi kiujanja bila kufanya kazi.

Alisema wakati umefika kwa kila kijana kupiga vita, uvivu, ulevi wa pombe, madawa ya kulevya, mirungu na akaongeza kuwa watu wanaoendekeza ulevi wa aina yeyote, huathirika wenyewe kiafya, kimwili na kisaikolojia na pia, huathiri familia zao.

"Sheria inasema kuwa mfanyakazi ni mtu yeyote aliyeingia mkataba wa kazi ili kufanya kazi iliyo halali kwa malipo halali ya kazi," alisema.

Alizidi kufafanua kuwa, kinyume cha kufanya kazi halali, ni kufanya kazi zisizo halali kama ujambazi, unyang’anyi ukahaba, ulaji rushwa na mengine alivyosema vinahatarisha maisha na ni haramu kwa kuwa vinamfanya mtu kujipatia kipato kisicho halali na kuwa anayedhulumu watu wengine.

Bw. Mganwa aliongeza kuwa, katika nchi yeyote, mwenye haki ya kula chakula na huduma nyingine bure; bila kufanyakazi ni watoto wadogo, walemavu, wagonjwa na wazee ambao jamii inapaswa kuwatunza kwa namna yoyote.

Akitaja makundi mawili ya kazi ambayo ni kazi za kujiajiri na kuajiliwa Bw. Mganwa alisema kazi ya kujiajiri kazi hasa ya kilimo inaajiri watu wengi nchini kuliko kazi nyingine za ufugaji, uvuvi, ufundi na biashara mbalimbali’

Hata hivyo alisistiza kazi zote hizo kufanyika kwa kuwa ni za manufaa kwa jamii.

Naye mjumbe binafsi Lesso na Katibu Nestori K. mlacha amewaeleza vijana kuwa bega kwa bega na wao kuahikisha wanapata ajira.

Semina hiyo iliyotolewa na CPT katika semina ya vijana Parokia ya Makuburi itaendelea juma hili lijalo ambapo itawahirikisha akina mama wote wa parokia hiyo

Masista wapongezwa kwa utumishi bora

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Pius Rutechura, amewapongeza masista wake wawili kwa utumishi wao bora na kuwataka watawa wengine kuiga mfano wao.

Padre Rutechura alitoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kuwaaga masista hao, Digna Ntewele (OSB) wa shirika la Imiliwaha Njombe na Sista na Illuminata Nathanael wa (COLU) baada ya kulitumikia baraza hilo kwa kipindi kirefu.

Hafla hiyo ilifanyika katikati ya juma katika ukumbi mdogo wa mikutanio wa TEC, uliopo ndani ya baraza hilo eneo la Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza kwa ufupi juu ya utumishi wa Sista Digna, Padre Rutechura alisema, amelitumikia Baraza la Maaskofu kwa kipindi kirefu cha miaka 11 kwa uaminifu na moyo wa uadilifu na kujituma kama mmoja wa wafanyakazi wa Idara ya Fedha, katika kitengo cha Uhasibu.

Alisema amekuwa mtumishi mwaminifu katika kitengo chake cha usimamizi wa fedha ingawa mara kwa mara alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya kiafya.Pia Katibu Mkuu huyo alimuelezea Sista Illuminata kama mtumishi mwaminifu na akaisifu kazi yake njema aliyoifanya kwa kipindi cha miaka miwili akiwa mtunza stoo katika magodauni ya Kanisa hilo yaliyo Buma.

Katika hafla hiyo, masista hao waliupongeza ushirikiano mzuri walioupata toka kwa wafanyakazi wa TEC.

Nafasi ya Sista Digna inachukuliwa na Sista Ditmara Mgaya , wa Shirika la Mtakatifu Benedikti (OSB) wakati nafasi ya Sista Illuminata inachukuliwa na Sista Beata Kingazi (COLU).

Masista Digna na Illuminata wanarudi katika mashirika yao kuendelea na majukumu mengine.

"Ninashukuru kwa ushirikiano na misaada mliyonipa licha ya kufanya kazi huku nikiwa nasumbuliwa na maradhi. Na naombeni radhi kwa wote niliowakosea, " alisema Sista Digna.

Naye Sista Illuminata, aliusifu ushirikiano aliopewa wakati akitumikia Kanisa katika magodauni ya Buma

Wakati huo huo: katika hafla hiyo fupi iliyofanyika Julai 26, mwaka huu, wafanyakazi mbalimbali wa TEC, wamempongeza mfanyakazi mwenzao Deogratias Makoye kwa kufuzu kozi yake ya uhasibu hivi karibuni.

Mashirika matatu ya usafirishaji yauzwa

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imetoa kibali cha kuuzwa mashirika matatu ya usafirishaji mikoani (RETCOS) kwa jumla ya shilingi milioni 36.

Wawekezaji katika mashirika hayo ni makampuni ya humu nchini ambayo wanahisa, vyama vya ushirika, wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka mashirika, wilaya na halmashauri.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Mfumo wa Mashirika ya Umma(PSRC)Bw. John C. Rubambe, imeyataja makampuni hayo kuwa ni Kampuni ya Uchukuzi Mtwara (KAUMU) ambayo imenunuliwa na KAUMU 2000 Limited ambayo inamilikiwa kwa pamoja na halmashauri za Wilaya na miji ya Masasi, Newala, Lindi, Mtwara, Wilaya ya Tandahimba, Kampuni ya Kilimo na Mfuko wa Pembejeo ya Mtwara(MBAITF)na wafanyakazi wa KAUMU.

Bw. Rubambe alisema bei iliyoidhinishwa kwa ununuzi wa KAUMU ni shilingi milioni 101/=.

Taarifa hiyo imesema kuwa Kampuni ya Uchukuzi Morogoro (MOROTCO) imemvutia mnunuzi wake kwa jina la Morogoro Roadways Limited. Kampuni hiyo inamilikiwa na halmashauri za Wilaya na miji ya Morogoro, Ulanga, Kilosa na Wilaya ya Kilombero, TCCIA, wawekezaji binafsi na wafanyakazi wa MOROTECO.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya shirika hilo ni shilingi milioni 140/=

Mnunuzi wa kampuni ya Uchukuzi ya Mbeya(MBEYA RETCO) ni Kumbe Limited inayomilikiwa halmashauri za wilya na miji ya Rungwe, Mbozi, Mbeya, Mbarali, Kyela, Wilaya ya Ileje, vyama vya ushirika vya Mbozi, Rungwe, Isayala, Mbeya na Ileje.

Bw. Rubambe amewataja wengine kuwa ni wawekezaji binafsi wa waajiriwa wa MBEYA RETCO. Bei iliyoidhinishwa kwa ununuzi wa Kampuni hiyo ni shilingi milioni 120/= za Tanzania.

Makampuni mengine ya uchukuzi mikoani yako katika hatua mbalimbali za kubinafsishwa.

Mila potofu huchangia vifo vya watoto- Wizara

Na Neema Dawson

IMEELEZWA kuwa vifo vya watoto ambavyo vimekuwa vikitokea mara kwa mara nchini, kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikichangiwa na elimu duni na imani potofu.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mradi wa Chanjo wa Taifa kutoka Wizara ya Afya Dk.Caroline Akim wakati wa semina juu ya mbinu za kutokomeza ugonjwa wa polio iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Msimbazi uliopo jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema wazazi wengi wamekuwa wagumu kuwapeleka watoto wao hospitali pindi wanapoonyesha dalili za kuumwa na badala yake huwakimbiza kwa waganga wa kienyeji na waganga kwa kutaka pesa hukubali kutoa tiba japaokuwa wanafahamu fika kwamba ugonjwa huo ni wa kutibiwa hospitali hali ambayo husababisha kifo kwa muhusika.

Dk.Caroline alisema katika kuondoa tatizo hilo taasisi za kidini kuwahimiza waamini wake kuishi kwa kutegemea njia zinazostahili kwa huduma ya afya zao wenyewe na watoto wao.

Katika semina hiyo ambayo ilikuwa ni moja ya maandalizi ya kuelekea katika kampeni za chanjo ya kutokomeza magonjwa ya polio, surua, pamoja na uhimizaji wa vitamin A, Dk.Caroline alisema kuwa sasa umefika wakati wa wazazi na walezi wa watoto kuacha kukataa kabisa kudanganywa kwamba chanjo inaleta ulemavu kwa mtoto.

Kampeini za chanzo hizo zinazotarajia kufanyika Agosti 12 -13 mwaka huu kwa awamu ya kwanza na na awamu ya lipi kufanyika Septemba, zitatolewa bure katika Wilaya zote 52 za Tanzania bara na Visiwani.

Vyombo vya habari vyatakiwa kuelimisha jamii juu ya surua

Na Waandishi Wetu

ILI kuutokomeza ugonjwa hatari wa surua,vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuelimisha jamii juu ugonjwa huu ambao huambukizwa kwa njia ya hewa na ukosefu wa vitamini A.

Akitoa mada juu ya uhamasishaji wa jamii na jukumu la waandishi wa habari katika kupambana na surua iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa kituo cha Msimbazi jijini,mtuoa mada kutoka kituo cha kinga kilichopo chini ya wizara ya Afya, Bibi Magreth Fimbo alisema vyombo vya habari vina kila sababu ya kuuelimisha umma juu ya chanjo ya ugonjwa huo wa surua.

"Waandishi wana kila sababu ya kuelimisha jamii kuhusu chanjo inayotolewa bure kama kinga kwa ajili ya watoto wenye umri wa miezi 9 hadi miaka 5" alisema Bibi Fimbo.

Semina hiyo iliandaliwa na wizara ya Afya na kufadhiliwa na shirika la kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) imelenga kuendesha kampeni dhidi ya ugonjwa wa Surua, Polio na ukosefu wa Vitamin A .

Askofu Ngonyani ahimiza umuhimu wa hija kwa Watanzania

Na Peter Dominic

KIONGOZI wa msafara wa mahujaji 16 waliokwenda hija nchini Islael, amewahimiza Wakristo hususani Wakatoliki kujitokeza kutumia nafasi za kwenda hija zinazopatikana ili kuimarika zaidi katika imani na kushuhudia mambo mengi na miujiza iliyotendwa na watakatifu mbalimbali akiwamo Yesu kama wanavyofanya watu wa mataifa mengine.

Kiongozi huyo Askofu Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi,aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi muda mfupi baada ya kurejea nchini kutoka Israel alipokwenda akiwa kiongozi wa msafara wa jumla ya mahujaji 16 wakiwemo mapadre, Masista na Walei toka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini.

Alisema Watanzania bado hawajatambua vema umuhimu wa kushiriki hijia katika maeneo matakatifu na akatoa wito kujitokeza kwa wingi inapotokea nafasi kama hiyo.

Alisema mara nyingi mahujaji kutoka Tanzania huonekana wachache ikilinganishwa na nchi nyingine.

"Hija katika Tanzania haijapata mwamko,jirani zetu wa Uganda walijitokeza mahujaji 100 wakati sisi tulikuwa kumi na sita. Utaona kuwa hiki ni kiwango kidogo," alisema Askofu.

Hata hivyo, Mhashamu Ngonyani alisema kuwa, hali hiyo pia inachangiwa na hali duni ya Watanzania ingawa pia alisistiza uhamasishaji wa hali ya juu katika suala hili.

"Ingawa hali yetu kiuchumi ni mbaya tusiifanye kuwa kisingizio cha kushindwa kuimarisha imani zetu katika Kristo," alisema.

Aliongeza kuwa, "Viongozi wa makanisa hapa nchini tujitahidi kuwahamasisha waamini wetu juu ya suala la kuhiji ambalo ni misingi ya kuimarisha zaidi imani ya Ukristo wetu.

Ukienda hija unakuwa umejipatia nafasi ya kupaona mahali ambapo watakatifu waliishi na kutenda miujiza akiwamo Yesu Kristo mwenyewe".

Askofu Ngonyani alisema safari hiyo imefana sana kulingana na mapokeo waliyoyapata hata baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Israel na Mji Mtakatifu wa Yerusalem.

"Safari yetu imeoanishwa na hali halisi kama tunavyosoma katika Biblia. Tumeguswa katika imani; ni tendo la pekee tumevutwa kuishi Ukristo wetu, alisema na kuongeza, "Hija ni tendo takatifu linaloweza kumuongezea mtu imani maana tunawashuhudia mambo yote yaliyofanywa na Kristo".

Msafara huo wa mahujaji uliondoka nchini Julai 16 mwaka huu kwenda Islael na kurejea nchini Julai 27 mwaka huu.

Mchungaji ashangazwa na wanaotukana viongozi wa dini kwa posta

Na Neema Dawson

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiangiliaka la Mtakatifu Albano ameshangazwa na utaratibu unaotumiwa na waumini kwa kuwatukana na kuwakashifu viongozi wa dini kwa kutumia njia za posta navyombo vya habari kutokana na chuki zao binafsi.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Williamu Kambanga katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Alban ambapo alisema na kusisitiza kuwa wakristo kote nchini wanatakiwa kuwaheshimu viongozi wa dini na si kuziheshimu tu nyumba za kufanyia ibada ambapo mahubiri yake aliyasisitiza katika kitabu cha Mathayo Mtakatifu 10:34.

"Wakristo wanatakiwa kufahamu kuwa dhambi inaharibu ushirika kati ya binadamu na Mungu na kuondoa imani walizonazo baadhi yao kuwa kushirikiana na kristo ni katika sakramenti tu bila kujua kuwa kushiriki katika mateso aliyoyapata na kuyapitia ni njia bora ya kuwaongezea baraka na amani katika maisha yao" alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa katika uchungaji wao wametumwa kutenda kazi ya bwana kama yesu alivyotumwa kuja kuwakomboa wanadamu na kila mtu anatumia karama yake aliyopewa na mwenyezi Mungu.

"Kuna waumini ambao wanakuwa na chuki zao binafsi hali ambayo kuwashutumu na kuwatukana viongozi wa dini kwa kutumia vyombo vya habari na kuandika barua kwa njia ya posta na kupeleka migongano ya hapa na pale ambayo inaweza kuleta machafuko kwa viongozi wa kanisa na migawanyiko".

Aidha alisema kuwa kuna baadhi ya waumini ambao wameyageuza makanisa kama sehemu ya Matukano hali ambayo wanatakiwa kutuma kamati mbalimbali za kanisa ambazo wanaweza kuwapelekea matatizo waliyonayo na kupata msaada mkubwa zaidi ambao unaweza kuwasaidia kuliko kutumia njia hizo wanazozitumia ambapo alisema hazifai na hazimpendezi Mungu.

Kampuni yadaiwa kuingia mitini milioni 1/= ya vibarua

Na Dalphina Rubyema,Kigoma

KAMPUNI ya ujenzi inayojulikana kama Setelite Constructions Company Ltd ya mkoani Dodoma, inadaiwa kukimbia na zaidi ya sh.milioni moja za malipo ya vibarua wake.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mkoani Kigoma, vibarua hao wapatao 34, walidai kuwa palipo hayo ni ya siku 14 walizoifanyia kazi ya ukarabati wa jengo la Reli mkoani Kigoma.

Vibarua hao walidai kila mmoja wao alitakiwa kulipwa kati ya sh.1500 na 3500 kwa siku.

Walisema baada ya Makao Makuu ya Mamamlaka ya Reli nchini(TRC), kutangaza zabuni ya ukarabati huo, kampuni hiyo ya Setelite ilishinda na kumua kuwaajiri vibarua mbalimbali mkoani Kigoma ambao wangesaidia katika kazi hiyo.

Wanasema walipatana na msimamizi wa kampuni waliyemtaja kwa jina Biazo, kuwa wangekuwa wanapewa malipo yao kila siku baada ya kazi na zoezi hilo lilitekelezwa kwa siku mbili za mwanzo.

Baadaye, wanasema waliambiwa hawezi kutembea na pesa kila siku hivyo wakaafikiana kulipwa kila Jumamosi.

Walidai katika utaratibu huo mpya ilitakiwa wapewe hela yao Juni 6 mwaka huu lakini hawakufanyiwa hivyo na hakuna sababu yoyote ya maana waliyoipata na tukio kama hilo lilitokea wiki iliyofuata ambayo ni Juni 22."Tulivyoona huyu jamaa anendelea kukaa kimya, ilibidi tumuulize hatima yetu akajibu anawasiliana na wakuu wake ili wamtumie hela pesa.

Sasa tukazidi kukaa kimya bila kutujulisha amepata jibu gani," alisema mmoja wa vijana hao Bw.Daud Kalumba.

Walisema kutokana na ukimya huo, Juni 27 mwaka huu, vijana hao walitoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa ambapo Mkuu wa Kituo(OCS) aliingilia kati suala hilo na msimamizi huyo ambaye ni mhandisi wa ujenzi akatoa malipo hayo.

Walindelea kuwa baada ya kulipa pesa yao waliendelea na kazi kama kawaida lakini hazikupa siku nyingi msimamizi wao huyo aliondoka kwenda Biharamlo mkoani Kagera ambapo na huko wanatenda nyingine ya kutengeneza barabara na hapo Kigoma alimwacha msimamizi mwingine aliyetajwa kwa jina la Sued Masoud.

Wakadai walifanya kazi kwa wiki mbili mfululizo bila malipo na walipomuuliza msimamizi wao huyo kila mara aliwapa jibu kuwa mabosi hawajatuma fedha."Tulimwambia huyo Masoud kwamba kama hataki kutulipa hela yetu sisi tutagoma na kweli Julai 17 mwaka huu tulianza rasmi mgomo ili tumpe muda awasiliane na wakuu wake watuambia siku maalum ya kutulipa, "alisema kijana mwingine Benard Venance.

Vijana hao ambao walikuwa wamejikusanya nje ya jengo hilo linalofanyiwa ukarabati waliongeza kuwa, walipoona ukimya umezidi, waliamua kurudi tena polisi katika Kituo cha Reli ambacho kipo ndani ya jengo hilo linalofanyiwa ukarabati na huko OCS aliwaahidi kulishughulikia suala hilo.

KIONGOZI lilipo muuliza juu ya malalamiko hayo, Bw. Suedi Masoud alikiri kuwa ni kweli wanadai pesa yao ya wiki mbili.

"Malipo yao yanatofautiana kwani kuna wengine wanaodai sh.3,500/= kwa siku na kuna wengine sh.1500 kwa siku. Inategemea nafasi ya mtu na nimejitahidi kuwasiliana na mabosi wangu lakini kila mara wananiambia hali ya pesa haijawa nzuri hivyo nawashauri hata hawa wenzangu tuzidi kuvuta subira," alisema.

Naye OCS wa Kituo cha Reli alikiri kupokea malalamiko hayo na kusema tayari amekwisha wasiliana na Bw. Biazo na ameahidi kuwa pesa hiyo itatumwa.

"Nilimpigia simu huko Bialamlo aliko aliniambia pesa itatumwa endapo itapatikana kwani kwa sasa hana pesa na hata hao TRC bado hawajampa hata senti, nimemwambia afanye haraka iwezekanavyo na kama akileta mchezo nitatoa taarifa polisi huko alipo akamatwe."

Aliongeza kuwa madai kuwa TRC haijaamlipa hayana msingi maana kwamba hata yeye asiwalipe vibarua, "Mkandarasi atashikaje tenda bila pesa yake ya mfukoni, kwa kweli anasumbua," alisema OCS huyo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa kituo cha Polisi ya Reli alipiga simu kwa mhandisi huyo mbele ya mwandishi wa habari hizi lakini, hakumkuta na badala yake simu hiyo ilipokelewa na mhudumu wa hoteli alikofia.