KUFUATIA MAUAJI YA PADRE

Kenya yalisakama Kanisa Katoliki

SERIKALI ya Kenya imejitoa kimasomaso kulishambulia kwa maneno kanisa Katoliki nchini Kenya kufuatia kifo cha padre mmoja raia wa Kimarekani yapata majuma mawili yaliyopita.

Kumetolewa taarifa na waziri mmoja serikalini ambaye ni Waziri katika Ofisi ya Rais akilishambulia vikali Kanisa Katoki kwa kutoa taarifa ya kuishutumu serikali kuhusiana na mauaji ya Padre Caiser. Alidai kuwa ikiwa maaskofu wana ushahidi wowote juu ya nani aliyehusika, basi watoe taarifa kwa maafisa wanaohusika.

Baada ya mazishi ya Padre John Antony Caiser aliyekuwa Mkuu wa Kanisa Katoliki katika eneo la Rift Valley, kulitolewa shutuma dhidi ya Waziri mmoja katika Serikali ya Kenya kwamba anahusika na kifo hicho japokuwa alikana tuhuma hizo kama ilivyotarajiwa

Kwa mujibu wa mahojiano kwa njia ya simu toka Nairobi baina ya mwandishi mmoja wa Gazeti la Nation la nchini Kenya, Onesmo Kironzo na Radio ya Ujerumani, upelelezi baina ya Shirika la Upelelzi la Marekani (FBI) na Polisi nchini Kenya unaendelea.

Kuna habari kuwa ingawa vigezo vilivyomhusisha Waziri huyo wa serikali na mauaji ya padre huyo Mmarekani vilitosha kumfanya mtuhumiwa kuwekwa ndani kwa upelelezi, bado hajahojiwa wala kuwekwa ndani na badala yake, anaendelea na kazi zake kama kawaida.

Kabla ya kifo chake, Padre Caiser alikuwa mtetezi sugu wa haki za binadamu na alikuwa pia akiwatetea waliofukuzwa makwao katika mkoa wa Rift Valley lakini, alipata maadui wengi serikalini na watu wengi wanashuku kwamba kifo cha Padre Caiser kinahusiana na uhasama wake na baadhi ya wakuu serikalini.

Serikali ya Kenya imekuwa ikiwataka makasisi na mashehe wasijihusishe na masuala ya kisiasa na kifo cha Padre Caiser, kinasemekana kwamba huenda kilitokana na kutetea kwake wasichana ambao wanabakwa na viongozi kama huyo Waziri aliyehusishwa na kifo hicho ambapo utetezi huo ni dhidi ya vitendo vibaya wanavyofanyiwa waamini wa kanisa lake.

Pia, kuhusu suala la kubadilisha katiba, serikali imeshikilia kwamba kanisa halina chochote kwa shughuli hiyo. Lakini viongozi wa kanisa wanasema wana wajibu wa kutetea waamini ambao ni wananchi halisi wa kenya.

"Hakika hali hiyo ilidhihirishia wengi kuwa huyu padre alikuwa na uhasama na vigogo wa serikalini kwa sababu hawakutuma risala yoyote wala kuhudhuria maombi ya mazishi yake. Hivyo kuonesha wazi kwamba serikali inashutumiwa kwamba pengine ilihusika kwa njia moja ama nyingine," alisema Bw. Kironzo.

Msumbiji yaanza mikakati ya kuboresha uchumi

MAPUTO, Msumbiji

NCHI ya Msumbiji, imeanza kupitia mipango ya kuboresha uchumi na huduma za jamii baada ya janga la mafuriko lililoikumba nchi hiyo mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, baada ya kukamilika, mapitio hayo yatapelekwa bungeni kujadiliwa zaidi na kutolewa maamuzi.

Imefahamika kuwa mwezi Mei mwaka huu, nchi hiyo ya Msumbiji ilikusanya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 480 kutokana na msaada wa mataifa mbalimbali duniani ikiwa ni sehemu ya mpango wa kujenga upya maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko hayo.

Mafuriko hayo yaliyotokea kati ya mwezi Februari na Machi, yaliharibu vibaya maeneo ya Kusini mwa nchi hiyo na inakadiriwa kuwa watu wapatao 700, walipoteza maisha.

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa waenda Eritrea, Ethiopia

ADDIS-ABABA, Ethipoia

MSEMAJI mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema waangalizi wanne kati ya saba wa Umoja wa Mataifa, wamekwisha wasili Eritrea na watatu wamewasili Ethiopia ambapo watakamilisha mafunzo ya siku nne kabla ya kwenda kwenye operesheni katika eneo lisilokuwa na majeshi.

Umoja wa Mataifa umekubali mpango wa kupeleka waangalizi wa kijeshi zaidi ya 100 kusimamia usitishaji wa mapigano kati ya Eritrea na Ethiopia

Msichana ahukumiwa viboko 180 kwa kuwa na mimba

lAtachapwa siku 40 kabla ya kujifungua

ABUJA, Nigeria

MAHAKAMA moja ya Kiislamu nchini Nigeria imemhukumu adhabu ya viboko msichana mmoja mwenye mimba baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ngono kabla ya kuolewa na kuwasingizia mimba wanaume watatu.

Imemhukumu msichana huyo adhabu ya viboko 180 ambapo viboko 100 ni kutokana na kujihusisha na mapenzi na hatimaye kupata mimba kabla ya ndoa na viboko 80, kwa kuwatuhumu wanaume watatu wasio na hatia kuhusika na mimba yake.

Msichana huyo alihukumiwa adhabu hiyo Alhamisi iliyopita baada ya kupata mimba na kuwasingizia wanaume watatu kwamba alitembea nao bila kutoa ushahidi.

Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, alisema msichana huyo Bariya Ibrahim Magazu(17), atachapwa viboko hivyo hadharani.

Habari zilizopatikana zilisema polisi walimripoti msichana huyo katika Mahakama hiyo ya Kiislamu iliyoko Kaskazini mwa Nigeria katika Jimbo la Zamfara baada ya kumgundua msichana huyo kuwa ana mimba ya miezi kadhaa.

Zamfara lilikuwa ndilo Jimbo la kwanza kutangaza matumizi Sheria ya Kiislamu ijulikanayo kama Sharia ,Januari Mwaka huu. Majimbo manane yamekwisha tangaza matumizi ya Sharia tangu Nigeria irejee kwenye utawala wa kiraia.

Sharia inawataka wakazi wote wa jimbo inapotumika, kufuata sheria za Kiislamu wawe ni Waislamu au la, na inasisitiza sala, mfungo wa Ramadhani, wanawake kutoonekana hadharani na kujitanda baibui.

Kwa mujibu wa habari hizo, msichana huyo ambaye kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake, atapewa adhabu ya kuchapwa viboko katika kipindi cha siku arobaini kabla ya kujifungua.

Adhabu zinazotolewa kwa mujibu wa Sharia, ni kuchapwa viboko, kupigwa mawe hadi kufa na kufutilia mbali anayeivunja Sharia.