Mlalahoi aingia Ikulu kimiujiza

lAjipakulia chakula, kujiburudisha kwa vinywaji

lKisha, alala usingizi mororo katika kitanda cha Rais

CAPE TOWN, Afrika Kusini

MSEMAJI mmoja wa Serikali ya Afrika Kusini, amethibitisha kwamba mtu mmoja asiyetambulishwa jina, aliingia ndani ya nyumba ya Cape Townya Rais wa Afrika ya Kusini, Bw. Thabo Mbeki.

Kwa mujibu wa radio ya Sauti ya Amerika, Alhamisi Usiku, Msemaji huyo Casmil Carrim, aliiambia radio hiyo kuwa, mwishoni mwa juma lililopita, mtuhumiwa huyo alivunja dirisha la nyumba hiyo ya Rais, akaingia ndani na kisha kujistarehesha.

Amesema, kisha mtuhumiwa alijipakulia chakula akala na baadaye, akajiburudisha kwa vinywaji vya Rais Mbeki.

Habari zinasema baadaye, mtuhumiwa alilala usingizi mororo katika kitanda cha Rais.

Carrim hakumtaja mtuhumiwa huyo lakini, amesema polisi nchini humo walimkamata siku ya Jumatatu alipogunduliwa na mpishi wa Rais.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alikuwa NewYork Marekani, akihudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Maadhimisho ya Milenia Mpya. Kwa kawaida Rais Mbeki, huishi katika mji Mkuu wa Utawala nchini humo, Pritoria.

Padre ahojiwa juu ya mauaji ya padre mwenzake

lAtakiwa kuisaidia polisi ya Kenya, Marekani

NAIROBI, Kenya

KATIKA hatua za awali za uchunguzi wa kifo cha Padre Anthony Caisari, Polisi nchini Kenya kwa kushirikiana na wapelelezi wa Kimarekani, wamemhoji Padre Francis Mwangi, aliyekuwa akiishi na kufanya kazi pamoja na marehemu.

Marehemu Padre Anthony aliyekuwa akidaiwa kuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali ya Kenya, alikutwa ameuawa kwa kupigwa risasi huko Naivasha umbali wa takribani kilomita 80, toka jiji la Nairobi.

Jeshi la Polisi nchini Kenya, limeahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wapelelezi wa Kimarekani ili kupata ukweli halisi juu ya mauaji ya Padre huyo Mkatoliki.

Padre Francis Mwangi, pia ameombwa kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kuwa alimuona Marehemu kwa mara ya mwisho kabla ya kifo chake cha risasi. Marehemu alikuwa Padre wa Kanisa Katoliki akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa raia wa Marekani na alifanya kazi nchini Kenya kwa miaka 36.

Bill Clinton, Fidel Castro wapeana mikono

NEWYORK, Marekani

MARAIS Bill Clinton wa Marekani na Fidel Castro wa Cuba, wamesalimiana kwa kushikana mikono na kuzungumza kidogo pembezoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaowajumuisha viongozi wa mataifa mbalimbali mjini NewYork.

Maafisa wa Marekani waliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi hao walikutana kwa bahati nasibu tu, baada ya chakula cha mchana, kilichoandaliwa wajumbe Jumatano iliyopita.

Hatua hii inaaminika kuwa mara ya kwanza kwa Rais huyo wa Cuba(Fidel Castro), kuzungumza ana kwa ana na Rais wa Marekani aliyepo madarakani katika muda wa miongo minne.

Cuba na Marekani hazijawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 1961.

Hakuna habari zilizopatikana kuhusu yaliyozungumzwa na viongozi hao.

Ikulu ya Marekani ambayo awali ilikanusha hali hiyo, imekiri kuwa ilitokea.

Huko nyuma katika mikutano ya Umoja wa Mataifa, maafisa wa ulinzi wa Marekani na Cuba, wamekuwa wakihakikisha kuwa Bw. Clinton na Castro, hawakutani uso kwa uso.

Wakati huo huo: Bw. Fidel Castro, amesema mataifa tajiri duniani, ndiyo yanayoshikilia nguvu za uchumi, siasa na teknolojia huku sera zao zikizifanya nchi maskini duniani, kuwa maskini na kuendelea kunyonywa zaidi.

Katika hotuba yake, kiongozi huyo wa Cuba, ameukosoa zaidi mkutano huo unaowajumuisha viongozi 150 toka mataifa mbalimbali duniani.

Alisema juu ya suala hilo, hajasikia lolote kuhusu mageuzi katika Umoja wa Mataifa.

Yapo mapendekezo ya upanuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini, wanadiplomasia wanasema, haiwezekani kwa vile wanachama wake watano wa kudumu wa Baraza hilo, huenda wasikubali kuachia haki yao ya upigaji wa kura ya Veto.

Rais Castro, amesema, alichokieleza kuwa mpango wa utaratibu wa uchumi na siasa ambao hukidhi matakwa ya wengi lazima ukaribishwe.

Kiongozi huyo wa Cuba anayejulikana kwa hotuba ndefu, pia aliingiza utani kabla ya kuanza kuzungumza.

Aliweka kitambaa cheupe kwenye taa ambacho huashiria kuwa uzungumzaji kwa muda wa dakika tano, unaelekea kumalizika.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa vicheko na wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa lakini, Bw. Castro, alizungumza kwa muda wa dakika saba tu, ambao ni mfupi kuliko wengine wote waliozungumza katika mkutano huo.